"Kwa maoni yangu, kama tungekuwa na mtazamo wa kidemokrasia tungeweza kubuni muundo ambao unakidhi matakwa ya pande zote mbili bila hatari ya kuuvunja Muungano. Mimi binafsi nimewahi kutoa pendekezo la muundo mbadala. Mara ya kwanza niliwasilisha pendekezo langu kwa Baraza la Wawakilishi [...] miezi michache iliyopita. Kwa muhtasari, nilipendekeza dola kamili mbili, la Zanzibar na la Muungano. Bunge la Muungano litakuwa na mabaraza mawili, Baraza la Wananchi na Baraza la Nchi. Wajumbe wa Baraza la Wananchi watachaguliwa moja kwa moja na wananchi wa pande zote mbili kutoka majimboni. Baraza la Nchi litakuwa dogo lenye, tuseme kama wajumbe 30, 15 kutoka Bara na 15 kutoka Zanzibar wakichaguliwa na Bunge la Zanzibar na wabunge kutoka Bara katika Baraza la Wananchi ilimradi wasiwe wajumbe wa bunge lolote lile. Na nilipendekeza orodha tatu - moja ya mambo ya muungano, nyingine ya mambo ya kushirikiana (concurrent matters) na orodha ya tatu ni juu ya mambo ya pamoja (joint interest). Kutokana na muda siwezi kufafanua; nia yangu ni kudhihirisha kwamba muundo mbadala unawezekana" - Issa Shivji (2013), Ukurasa wa 40-41, Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya: Mhadhara wa Kuaga Kigoda cha [Taaluma cha] Mwalimu [Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam]