WAKATI hoja ya serikali tatu iliyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba Mpya ikiwagawa Watanzania, mwanazuoni Profesa Issa Shivji, naye amepinga muundo huo kwa hoja kwamba ni mwanzo wa safari ya kuvunja Muungano. Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akitangaza azma ya kungatuka katika nafasi yake ya uenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, alisema anaamini uwapo wa dola mbili ni njia pekee itakayoendeleza Muungano wa Tanzania.
Akiichambua kwa undani Rasimu ya Katiba Mpya, alisema Muungano hauhitaji idadi ya serikali tatu, bali ni uboreshaji wa mazingira ya demokrasia kwa wananchi.
Kwa udhani wangu baada ya kuichambua rasimu hii, naona ndani ya Tume ya Katiba kulikuwa na mvutano mkubwa hivyo kutuzalishia rasimu ya maelezo na sio mapatano ya mwafaka.
Siku zote maelezo ya makubaliano huzalisha jambo dhaifu na hili ndilo limezalishwa na Tume ya Jaji Warioba, alisema Profesa Shivji.
Aidha, aliifananisha Rasimu ya Katiba Mpya na ganda lisilokuwa na tunda huku akiweka wazi upungufu kwa baadhi ya vipengele vilivyopo katika Rasimu hiyo.
Katika hatua ya muundo wa muungano wa serikali tatu, alielezea wasiwasi wake kuhusu mambo mbalimbali yatakayoleta utata na baadaye kuuvunja Muungano.
Alisema kutokana na baadhi ya vipengele nyeti kushindwa kuweka wazi lengo la kubana serikali washirika yakiwamo mambo ya ukomo wa mamlaka ya uhusiano wa Serikali ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Akielezea kwa undani kipengele hicho, alisema kwa mfumo wa serikali tatu kama ulivyoainishwa ni lazima ionyeshe mipaka baina ya nchi washirika.
Alisema ikifika hatua ya kuwekeana mipaka baina ya nchi na nchi basi moja kwa moja kutazaa mgogoro mwingine mkubwa kwa nchi washirika ambao ni vigumu kusuruhishwa na Serikali ya Muungano.
Sasa leo kuwapo serikali tatu, kama ilivyoainishwa katika rasimu ambapo Jamhuri ya Muungano itakuwa na umiliki wa mipaka yote ya nchi kavu, serikali washirika nikimaanisha Tanzania Bara na Zanzibar nao lazima wajiwekee mipaka, hapo kwa uzoefu wa mataifa yaliyowahi kuvunja serikali za mashirikisho suala la mipaka ni moja ya sababu zilizosambaratisha kwa hiyo hata katika mfumo huu tutegemee hili.
Jamani athari ya kuvunjika kwa muungano ni kubwa zaidi kuliko mnavyofikiria, nadhani leo hii yanayotokea kati ya Sudani na Sudani Kusini mnayaona au jinsi Urusi ilivyogawanyika ambapo hadi leo kuna mapigano yasiyokuwa na ukomo, alisema Profesa Shivji.
Kwa hisani ya Mtanzania.