Mrithi wa Maximo kuwa bei poa
Pamoja na kiwango cha juu cha ujuzi na uzoefu, kocha atakayekuwa na gharama nafuu za malipo ndiye atarithi nafasi ya mwalimu Marcio Maximo kwenye timu ya taifa, Taifa Stars, shirikisho la soka, TFF, limesema.
Katibu mkuu wa shirikisho la soka Frederick Mwakalebela alisema mbali na kuangalia wasifu wa makocha wote watakaotuma maombi ya kuajiriwa, pia TFF itazingatia wenye gharama nafuu za malipo.
``Makocha wanatofautiana kwa mishahara mikubwa, hivyo tutaangalia pale tunapoweza,`` alisema Mwakalebela ambaye alibainisha inapoweza TFF ni mshahara ambao ``sio mkubwa sana au mdogo sana.``
Mbali na mshahara usio mkubwa sana au mdogo sana, kocha mpya wa Taifa Stars baada ya kukamilika kwa mkataba wa Maximo Julai mwakani atalipiwa pango la nyumba na gari dogo la kutembelea.
Maximo analipwa na serikali dola 10,000 za Marekani (sawa na shilingi milioni 11.6) kwa mwezi, kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.
Serikali imeshaeleza kusudio la kuacha kulipa mshahara wa kocha wa Stars na kujikita katika kusaidia kunyanyua michezo midogo kama riadha.
Utafutaji wa mwalimu mpya wa timu ya taifa utakuwa chini ya Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, alisema Mwakalebela.
``Inabidi huu mchakato uanze mapema, kwani sio hadi Maximo anamaliza ndio tunaanza kuhaha ndio maana tunasema benchi la ufundi litakapotangaza nafasi hiyo ya kazi itakuwa haraka.``
Tayari kocha mkuu wa timu za vijana za taifa Marcus Tinoco kutoka Brazili pia kama Maximo, ametangaza nia yake ya kumrithi mwalimu huyo.
Hatahivyo upo uwezekano mdogo wa Tinoco kupata nafasi hiyo kutokana na kutokuwa na uzoefu wa kutosha kimataifa na ukweli kuwa Mbrazili aliyemtangulia ameshindwa kufikia malengo ya TFF na serikali katika miaka mitatu atakayofundisha.
SOURCE:
Lete Raha