Maximo Akiri Vipigo Vya Taifa Stars
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo Friday, November 13, 2009 5:36 PM
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo amekiri kwa kusema kuwa ,matokeo mbaya waliyoyapata katika mechi tatu za kirafiki za kimataifa katika nchi za Misri na Yemen yatachochea moyo wa kujituma kwa wachezaji wake.Maximo alisema watakuwa na hamu ya kufanya vema kwa timu ya Tanzania Bara itakayoshiriki michuano ya Chalenji itakayofanyika Kenya kuanzia mwishoni mwa mwezi huu.
Gazeti moja la kila siku limeandika kuwa, Maximo alitarajia kupata matokeo mazuri katika michezo mitatu waliyocheza, lakini hali imekuwa tofauti kabisa kutokana na sababu tofauti ikiwemo kuzidiwa na hali mbaya ya hewa nchini Yemeni.
Stars ilifungwa na Misri 5-1, ikatoka sare ya 1-1 na Yemen katika mchezo wa kwanza na kupoteza mchezo wa pili baada ya kufungwa 2-1.
"Misri ni timu ya kiwango cha juu mno na ukitaka kucheza nayo lazima ujiandae, nilikubali kucheza mchezo huu kwa sababu tulikuwa tumewaomba muda mrefu kucheza nao bila mafaniko, niliona hii ilikuwa ni fursa nzuri kupima kikosi changu licha ya kufanya mazeozi siku mbili tu, lakini huu ndiyo mpira, tumejifunza mengi.
"Yemen ni timu ya kiwango cha chini ukilinganisha na Taifa Stars, tulijitahidi kuwabana katika michezo yote miwili na kumiliki mpira kwa asilimia kubwa, lakini nafasi tuilizotengeneza hatukuzitumia kupachika magoli, lazima tuichukue hali hii kama changamoto tunapokwenda kwenye Chalenji hakuna njia," alitanabaisha Maximo.
Kocha Maximo ambaye amekuwa akiinoa Stars kwa miezi 39 sasa amesema jambo lingine ambalo anaona ni la manufaa katika ziara hii ni kuwa ameweza kuwatumia wachezaji wake wote 19 aliokuwa nao safarini na hivyo kuweza kupima uwezo na maendeleo ya kila mchezaji kwani kila mmoja amepata nafasi ya kucheza walau mchezo mmoja.
"Matokeo si mazuri, lakini kuna mambo mengi ya manufaa, nataka kutumia siku tisa tutazokuwa kambini kurekebisha kasoro hizi kabla ya kwenda Nairobi," alifafanua.
Mbrazil huyo alisema makosa yaliyojitokeza katika safu ya kiungo na ushambuliaji yanahitaji ufumbuzi wa haraka.
"Lazima tumiliki mpira na kupunguza mianya sehemu ya kiungo huku tukiwabana vilivyo wapinzani wetu muda wote na baada ya hapo tulenge lango mara nyingi zaidi ili tupate magoli ya kutosha, nitajihidi kuyaweka sawa yote hayo na sina shaka tutafanikiwa."
Mashindano ya Chalenji yamepangwa kuanza Novemba 28 na kumalizika Desemba 13 mwaka huu na yatachezwa katika miji ya Nairobi na Mumias.
Tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo miaka 35 iliyopita Tanzania Bara imetwaa ubingwa mara mbili tu mwaka 1974 ilipokuwa mwenyeji na mwaka 1994 ilipofanyika Kenya.
Katika miaka ya 1975, 1980,1981, 1992 na 2002 Tanzania Bara ilifungwa katika michezo ya fainali na Uganda, mara mbili, Kenya, mara mbili na Sudan mara moja.