Nadhani pia hiyo ulioita "Political Succession" iko kila mahali. Niongezee: "The Culture of Succession Politics." Tunaiona huko Marekani nao wana aina yake inaendelea hata sasa; sisi hapa tunayo ya kwetu ambayo sawa kabisa kuiita ni nzuri kama ulivyofanya. Naamini hata hapa Tanzania viongozi wanaomaliza muda wao hupenda mtu fulani angerithi kiti cha Urais. Shida ni kwamba yeye peke yake hawezi kumweka katika kinyangiro kinachohusika. Mwalimu inasemekana alikuwa na chaguo lake; Mzee Mkapa naye alikuwa na lake na hata Ndugu yetu Kikwete naye alikuwa na chaguo lake. Ni mfumo wetu ndio unaofanya kuwa ngumu sana kwa kiongozi aliyepo kumpitisha yule anayempenda amrithi.
Kenya kwa upande wao mtu huupata Urais kwa mafungamano ya wapiga Kura ama kikanda ama kimakabila. Utasikia juu ya kura za GEMA (Gikuyu, Embu, Meru Association); ama za Miji Kenda yaani makabila yale 9 ya Pwani ama za Masai na Wakamba namna hiyo. Mapatano hufanyika toka mwanzo: "Mtuunge Mkono nasi tutawaunga mkono baada ya miaka 10 ama 8", namna hiyo.
Kwa hiyo makabila kama Kalenjin yalifungmana na Gikuyu na huenda GEMA yote na Kenyatta akapita na Ruto akijua wazi Unaibu Rais ni wake. Musalia alipomwacha Raila kipindi kilichopita alihamisha kura nyingi sana za WaLuhya na kuzipeleka kwingine. Kwa hiyo Kiongozi anayetaka Urais kule hutafuta mfungamano wa Kikabila, na hapo makubaliano ya muda mrefu hufanyika.
Kumekuwepo kutoridhika katika utaratibu huu kama pale Wajaluo walipojiunga na Kibaki kipindi kile na Raila akisikika akisema "Kibaki Tosha"; akitegemea kwamba Mzee akimaliza ni zamu ya Raila na Wajaluo. Bahati mbaya haikuwa hivyo.
Kwa hiyo ni utamaduni wa makundi ya kikabila kufungamana kutafuta kiongozi. Sijui uchaguzi ujao huko jirani watapanga mikakati ipi ya mafungamano ya kikanda, kimkoa na Kikabila kupata mrithi wa kiongozi aliyepo. Je Jubillee watakubali kuwachia W. Ruto kiti hicho yaani kuwaachia Wakalenjin? Mmoja aliandika akasema Kibaki alikuwa tayari kufikiria kumwandalia mazingira mazuri Raila achukue lakini wazee wa Kikuyu walimfuata na kumpa somo juu ya nia yake hiyo. Akaghairi.
Tusubiri tuone ikiwa ni sasa ama kipindi kijacho kile kingine ikiwa Mhe atamwachia Mkalenjin kama vile baba yake Mzee Kenyata alivyofanya hapo zamani akimkabidhi Mhe. Moi hatamu za nchi yao.