Tukubali tukatae, kisiasa na kwa upana wake hata kwenye masuala ya usalama, Tanzania bado ipo katika mfumo wa kijamaa. Ndiyo maana unasikia kelele zisizoisha za Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi. Ni kwa sababu kimsingi, nchi ina mfumo tofauti na ule ambao watu wanaaminishwa unaendesha maisha yao ya kila siku.
Viongozi wamekuwa mabepari wa kutupwa wanaonuka kila aina ya rushwa na ufisadi ila bado wanasimama mbele ya mic na kuongelea habari za "watwana". Nilichogundua wote wameacha kutumia neno "walala hoi".
Baada ya tukio la kulipuka kwa kituo cha nyuklia cha Chernobyl kule Urusi, ilikuwa ngumu sana kuwajibisha wahusika waliosababisha maafa yale. Watendaji wa serikali wakatupiana mpira, lengo likiwa kulinda sura ya mfumo wa kikomunisti wa Urusi ambao watawala walitumia nguvu na miaka mingi kuaminisha wananchi wao na dunia kwa ujumla kuwa ni mfumo usio na mapungufu wala makosa. Warusi wakaunda Tume, uchunguzi wa kila aina ulifanyika ila waliona ni lazima mfumo ulindwe kwa gharama zote hata kwa kuficha ukweli.
Kwa miaka mingi, Tanzania tumekuwa katika hali hiyo. Kila matatizo ya kimfumo, ni heri atafutwe wa kuangushiwa jumba bovu ila mfumo "takatifu" wa CCM ubaki salama.
Hata katika hili la MO29, Tume zitaundwa, uchunguzi utafanyika na tafiti za kila namna, ila ukweli unapotishia uhai wa mfumo, wako radhi ukweli huo uwekwe kando na mfumo upone.