Simba bingwa michuano ya vijana
TIMU ya vijana chini ya miaka 20 ya Simba jana ilitwaa ubingwa wa ligi ya timu hizo ‘Uhai Cup' baada ya kuichapa Azam kwa mikwaju ya penati 6-5 katika fainali iliyochezwa kwenye uwanja wa Karume, Ilala. Katika mchezo huo mkali timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana na kulazimu kuongezwa dakika 30 ambazo hata hivyo ziliisha kwa timu hizo kutoka sare tena ndipo sheria ya changamoto ya mikwaju ya penalti ilipochukua nafasi yake.
Simba walifunga penalti zao zote kupitia kwa wachezaji wao Abdallah Selemani, Ramadhani Singano, Jamal Mwambeleko, Edward Christopher, Haruna Athumani na Wiliam Lugani. Wakati penalti za Azam ziliwekwa kimiani na Mgaya Jaffar, Calvin Idd, Ibrahim Juma,Tumaini Venance na Mussa Kanyagha huku mchezaji Yaluku alikosa kwa upande wa Azam na kuipa Simba ubingwa wake wa kwanza tokea mashindano hayo yaanze karibu miaka mitatu iliyopita.
Simba iliingia fainali za mashindano hayo baada ya kuzifunga timu za JKT Oljoro mabao 5-2 katika mchezo wa robo fainali na baadaye kuwafunga Toto Africans ya Mwanza mabao 4-1 katika mchezo wa nusu fainali. Kwa ushindi huo, Simba imepata Sh milioni 1.5 kutoka kwa wadhamini wa michuano hiyo S.S. Bakhesa, na Azam iliyoshika nafasi ya pili imepata Sh milioni moja.
Kocha mkuu wa mabingwa hao, Selemani Matola aliteuliwa kuwa kocha bora wa mashindano hayo ambapo alipata Sh 500,000 huku mshambuliaji hatari wa timu hiyo Ramadhani Singano akipata nafasi ya mchezaji bora na kupata Sh 400,000.