Na Mwandishi wetu
23rd February 2010
Jumla ya Sh.Milioni 20 zimetolewa na mdau mmoja kwa ajili ya maandalizi ya timu za Simba na African Lyon zitakazopambana kesho katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Uhuru.
Kwa mujibu wa habari zilizoifikia Nipashe, kati ya fedha hizo, Sh. Milioni 10 wamepewa Simba na kiasi kama hicho wamepewa African Lyon kutoka kwa mdau huyo ambaye ni mtu wa karibu na klabu zote mbili.
Chanzo chetu kiliendelea kusema kwamba lengo la kutoa fedha hizo ni kila upande kufanya maandalizi sahihi ya mechi hiyo bila kuwa na kisingizio ukata.
"Si unajua Lyon imekabidhiwa kwa wadau wa Simba, sasa zimetolewa fedha hizo ili kila upande ufanye maandalizi mazuri na vijana waweze kuonyesha kandanda," kilisema chanzo hicho.
Katika hatua nyingine, kocha msaidizi wa African Lyon, Suleiman Matola, amesema kuwa timu yake imepania kuendeleza ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi.
Matola alisema kwamba wamejipanga kufanya mapinduzi katika mzunguko wa pili na lengo ni kuendelea kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.
"Tutaifunga Simba, vijana wamejipanga na wanajua cha kufanya, sisi ndio wana- mapinduzi," alitamba nahodha huyo wa zamani wa Simba.
African Lyon iliyokuwa mkiani, imeibuka katika mzunguko huu wa lala-salama na sasa hivi imefikisha pointi 18 ikiwaacha Prisons na Toto African wakiendelea kupumulia 'mashine'.
African Lyon iliyoanza Ligi Kuu kwa kutoka sare ya 1-1 na Yanga msimu huu, iko chini ya kocha mkuu Boniface Mkwasa, na sasa inasimamiwa na wadau wa Simba akiwemo, Kassim Dewji ambao wamepewa jukumu la kuiratibu timu hiyo kuinusuru isiteremke daraja.
Simba na Lyon zilipokutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza Oktoba 9 mwaka jana, wana Msimbazi walishinda 1-0.