Abdallahking
JF-Expert Member
- Mar 19, 2018
- 3,985
- 10,840
Simulizi: AJIRA TOKA KUZIMU
Mwandishi: GEORGE IRON MOSENYA
Imeletwa kwenu na: BURE SERIES
SEHEMU YA 1
Aliitazama nchi hii kwa mbali sana, aliyekuwa mkuu wake alimuonyesha kwa kutumia kidole kimoja. Ilikuwa ina rangi ya bluu hii ndio ilikuwa nchi kubwa aliyokuwa ameagizwa kumfanyia kazi yake ambayo hakuwa ameshurutishwa kuifanya bali kwa hiari yake mwenyewe. Baada ya kuelekezwa vyema katika nchi hii sasa alimuelekeza vi-nchi vingine vidogo vidogo ambavyo havikuwa na ukubwa wa kutisha. Majina yake mengi yalikuwa ya kigeni lakini yalieleweka na kukaa vyema katika kichwa cha kijana huyu aliyekuwa anaelekezwa. Alitikisa kichwa juu na chini kuashiria kuwa anaelewa somo alilokuwa anapewa.
Mkuu wake aliyefahamika kwa jina la Tuntufye Kanyenye ama kwa kifupi Tuntu alitoa tabasamu ambalo kwake lilikuwa bora lakini linatia karaha ukilitazama. Tabasamu hili lilimaanisha kuwa alikuwa na imani kubwa na kijana huyu aliyekuwa anaagizwa katika nchi hii ya bluu na nyingine ndogo ndogo.
“Nakutakia safari njema yenye mafanikio….” Tuntu alimtamkia kijana wake huku akimpapasa kichwa chake katika hali ya kubariki. Baada ya hapo akampulizia marashi fulani katika nguo zake. Halafu akamtwaa na kumnyanyua juu juu tayari kwa kumrusha katika dunia hiyo. Hofu ikaanza kumtawala kijana huyu akawa anatetemeka ujasiri aliokuwanao ukaanza kuyeyuka akawa anatweta kwa hofu lakini tayari alikuwa katika mikono hii mibaya yenye nguvu. Akiwa bado katika uoga mara alirushwa kwa nguvu zote akauacha ule ulimwengu akawa anaelekea katika ulimwengu mwingine. Alikuwa anarusha miguu huku na kule lakini aliishia kuipatia majeraha hewa ambayo ilikuwa katika kila sehemu.
Kwa takribani dakika tano nzima alikuwa hewani na sasa alikuwa anakaribia kutua katika nchi hii ya bluu. Uoga ukamzidi akajikunyata akauziba uso wake kisha akapiga kelele kubwa sana za uoga huku akijaribu kukwepa asitue eneo lile aliloliona kuwa la hatari sana.
Jasho kali lilikuwa linamtoka, alikuwa peke yake chumbani alikuwa amekaa kitako katika kitanda chake cha futi tano kwa sita. Alikuwa anatetemeka. Taa ilikuwa imezimwa akasimama aweze kwenda kuiwasha lakini akajihisi kuwa alikuwa katika kutetemeka, akarudi akaketi tena. Alikuwa ametoka kuota ndoto mbaya sana ambayo hajawahi kuiota kabla. Alijaribu kupikichapikicha macho yake ili aweze kuona kama aliyoyaota yalikuwa ndani ya chumba kile lakini hapakuwa na mfano wa kitu kama hicho pale ndani. Kwa unyonge akarejea kitandani akauchapa usingizi tena.
Palipokucha hakuwa na kumbukumbu tena kama usiku ule alikuwa ameota ndoto mbaya. Aliamka akiwa na amani tele. Alijisikia mwenye nguvu za kustaajabisha!!
Hakujua kama alikuwa ameingia katika utumwa
Utumwa wa bila kujua.
****
Hassan alikuwa anazipitia post za hapa na pale katika mtandao wa kijamii wa facebook katika namna ambayo hakuwahi kuifanya hapo kabla. Alizitazama post za mapenzi hasa hasa za wasichana, hakujalisha kama ni warembo ama la. Hakuwahi kufikiria kuwa siku moja anaweza kuwa kama alivyo.
“Beatrice Cosmas” alilisoma jina hilo na kulirudia mara kwa mara, “Saint Augustine Mwanza” akakisoma na hicho chuo alichokuwa anasoma dada huyu.
“Nipo njiani nakuja Dar yeyote aje kunipokea jamani” hatimaye akaikariri na ile post aliyoweka dada huyu mnene katika picha akiwa na mwanya na macho ya kuvutia.
Hassan aliingia katika inbox ya dada huyu akamkaribisha Dar huku akimwomba ampe nafasi ya kumpokea mara atakapofika. Beatrrice akazuga kujizungusha zungusha na kumwomba Hassan namba yake ya simu na kuahidi kumpa taarifa baada ya kufika. Hassan bila kinyongo alimpatia namba yake ya simu huku akitoa tabasamu.
Hassan aliingia katika shughuli zake huku akiwa ameanza kusahau kama alikuwa na ahadi ya kupokea simu yoyote ile mpya. Ilikuwa kama bahati ya kipekee baada ya kuwa amepokea malipo baada ya mauzo ya mzigo wake wa samaki.
Wakati anaingia katika gari lake aina ya GX 100 alikutana na mlio wa simu yake, ilikuwa namba mpya, aliitazama kisha akabonyeza kitufe cha kupiga. Simu ikaita kidogo ikapokelewa na sauti nyembamba ya kike.