Simulizi: Ajira Toka Kuzimu

Simulizi: Ajira Toka Kuzimu

SEHEMU YA 26


"Asalaam Aleykum" sauti yenye ukarimu ya kijana Hassan Tembo ilimjulia hali Rehema.
"Aaleykum-salaam" Alijibu kwa nidhamu ya hali ya juu kwa lafudhi nzuri ya kiswahili iliyochanganyikana na upemba na uarabu kwa mbali. Sauti hiyo ikampa ladha Fulani Tembo, akatoa tabasamu hafifu.
“Khaifa….” Tembo akaupima ujuzi wa Rehema kama alikuwa kweli ameiva kidini ama alikuwa anarashia rashia. Rehema akashindwa kujibu, Tembo akajipa majibu yake kichwani.
Robert alimtanguliza Tembo akaifikia sofa nyekundu iliyoanza kupoteza ubora wake wa awali. Laiti kama kingekuwa kipindi cha nyuma basi huenda sofa hii ingekuwa ya kuitazama mara mbili. Huenda aliinunua kwa mtu ambaye alikuwa ameanza kuichoka au alikuwa katika kununua sofa nyingine akaamua kuiuza hii.
"Roby mambo?!"
"Poa ndugu za siku kadhaa, hatuonani" Rehema hakujibu badala yake akacheka kwa kujilazimisha. Sura yake ilitangaza dhiki ya hali ya juu.
“Naona upo na mtu mkubwa sana kama shehe vile, kaka umependeza sio siri” Rehema alimsifia Hassan kupitia mazungunmzo yake na Robert.
“Huyu Mufti kabisa mbona…” Roby alikolezea kikatoka kicheko kidogo kutoka kwa Rehema, safari hii aliufumbua mdomo wake, Tembo akauona mwanya. Moyo ukamdunda sana kana kwamba ameona kitu cha kutisha ama kushangaza sana.
"Kaka unatumia kinywaji gani?" Rehema alimuhoji Tembo huku akiwa wima wima, akajibiwa kwa kichwa. Tembo hakuhitaji kinywaji.
“Jamani kaka, hata maji tu…”
Anazuga huyu hana pesa wala nini! Tembo aliwaza kisha akausimamia msimamo wake ili asije kumwaibisha Rehema.
"Mimi niletee maji yanatosha" Robert aliomba. Rehema akatoka nje, Tembo hakuona dalili ya pesa katka mikono ya Rehema.
Akaduwaa!
"Oya kaka, mzigo wenyewe ndo huo hapo sasa,..ona!" Robert alimnong'oneza Tembo. Tembo hakujibu kitu zaidi ya kuitazama subwoofer iliyoketi kipweke katika stuli ndogo yenye mguu mmoja mbovu. Ilikuwa inavutia sana, lakini kwa Tembo ilivutia zaidi, sio kuwa hakuwa na uwezo wa kununua mpya tena yenye ubora kupita ile bali aliiona kama vile ni chambo ya kumnasa Rehema. Tayari Hassan Tembo alikuwa amevutiwa na mwanya wa Rehema pamoja na ile mitikisiko aliyoishuhudia ikipenyeza kutoka katika kanga moja nyepesi.
Kabla Tembo hajajibu lolote, aliingia msichana mwingine bila kugonga mlango. Bila shaka yalikuwa ni mazoea yake kufanya hivyo!!
Au huenda alijisahau!! Nani anajua?
"Rehema yuko wapi?" Aliuliza kibabe huku akiwa amekunja ndita. Hakuna aliyemjibu bila shaka wote walikuwa wamekereka na kitendo hicho cha kuingia bila hodi pale ndani halafu mbaya zaidi hata salamu pekee hakukumbuka pia!!!
 
SEHEMU YA 27


Yule binti hakuonyesha kukerwa na jambo hilo la wawili hawa kukaa kimya badala yake aliendelea kubwatuka.
“Aisee akija mwambieni Hawa kaibuka hapa…mkimwambia atajua nilifata nini…” alimaliza kutia mkwara huo akatokomea zake huku akiipa tabu ardhi kwa vishindo alivyokuwa akikanyaga. Tembo alimtazama Robert akagundua kuwa hakuwa akimtazama akahamisha macho kwenye simu yake. Kichwani akajiongeza kuwa yule Hawa alikuwa anamdai Rehema.
“Maisha ya chuo bwana!!!!!” alijisemea Tembo huku akibetua midomo yake kisha akajikuna kichwa chake kisichokuwa na nywele.
Bila kuzungumza lolote na Robert mara Rehema akaingia ndani. Alikuwa amemletea maji kopo dogo kupita yote yanayotengenezwa na kiwanda cha tajiri maarufu ambaye sura yake haifahamiki kwa watu wengi hapa nchini, Maji ya uhai. Na bei yake ilikuwa ya chini sana kupita yote, ondoa yale maji ya ‘Kandoro’ ambayo huuzwa bei chee zaidi.
“Mh!! Huku kwetu aisee maji makubwa hamna nimezunguka mpaka basi!!!” Rehema alijisemesha bila kujiamini. Robert na Tembo wote wakajilazimisha kucheka.
Anazuga tena maskini!!! Tembo aliwaza huku akiibia kumtazama Rehema, aliyekuwa amekaa mkao Fulani wa kuinama. Macho ya Tembo yakatua katika kifua chenye rangi ya dhahabu mpauko, kifua hicho kikiwa kimebeba matiti mekundu, hakuwa amevaa ‘kinyanyua matiti’ bila shaka yalikuwa yamesimama peke yake!!!!
Wacha wee!!
Kikohozi kikamkaba Tembo, ila akafanikiwa kukikabili!!! Hakukohoa.
Kama vile Rehema aliendelea kufanya mambo hayo makusudi. Sasa alikuwa amekaa vibaya. Paja lenye rangi kama ya kifua chake likachungulia nje. Ule mfanano wa rangi ulithibitisha kuwa alikuwa na ngozi ya asili hakuwa akijichubua. Akili ya Tembo haikuwa pale na wala hakumsikia Robert alivyomnong’oneza mpaka alivyorudia tena!!!!
“Kwa hiyo inakuwaje bosi!!!”
“Aaaah!!! Hebu ngoja nifike kwanza ofisini feri kuna ishu imetokea ‘then’ ntakupigia tuje kumaliza biashara” alijibu Hassan Tembo huku akiwa nusu amekaa nusu amesimama.
“Basi poa utanishtua!!!” alijibu Robert. Wakasimama wakamuaga Rehema mtoto wa Hussein, wakatokomea garini.
Walipofika garini, Tembo akaingiza mkono wake katika suruali na kurekebisha ustaarabu ulioanza kuvurugika.
Rehema aliwasindikiza kwa macho yaleyale yaliyotangaza dhiki. Laiti kama wangeweza kumsoma vizuri macho yale yalisema, “Jamani maji yenyewe pia nimekopa nilitegemea mtanipatia pesa nilipe…..na Hawa naye aaah!!”
Bahati mbaya kwake!!!!
Rehema aliufunga mlango akakimbilia kitanda chake akajirusha na kuanza kumlaani Tembo kwa kupewa taarifa kisha kuondoka bila kumaliza biashara. Wazo la kutafuta mteja mwingine likamuingia. Akaitwaa simu yake, akajaribu kupiga, yule mwanamke anayekera kwa lazima akamjibu kuwa ‘Huna kiwango cha kutosha katika simu yako tafadhali ongeza salio…….” Rehema akaikata simu na kufura kwa ghadhabu.
Njaa nayo ilikuwa inamtafuna!!!!
**REHEMA katika balaa la chuo….. Tembo analitambua balaa hilo na tayari amevutiwa….
**JE ni wakati wa Rehema kumsahau Rahim na kuingia katika ajira ya Tembo???
USIKOSE KESHO!!!
 
SEHEMU YA 28


*****
Hodi ya kwanza ilikuwa na heri na ilileta tabasamu kidogo japo ilimalizikia kwenye machungu, alichokitarajia hakukipata kwa wakati. Mlango ukagongwa tena Rehema akaenda kuufungua safari hii hakuulizia chochote.
Moyo ukampasuka Rehema, alikuwa ni Hawa. Wiki mbili zimepita akiwa anachengachenga kumlipa pesa yake sasa yupo mbele yake, sura yake ikiwa imetawaliwa na shari tupu..
“Sihitaji maelezo aisee nipatie pesa yangu nadaiwa huko…yaani nilikupa kiistaarabu kunirudishia ndo tunasumbuana hivyo???” alikoroma Hawa huku akiwa ametega mkono kusubiri chochote na sio maelezo, mkono mmoja kiunoni mwingine ukiwa umetega ukingoja pesa. Rehema akakosa la kuzungumza, akajilazimisha kutabasamu. Hawa hakuwa pale kimzaha alimaanisha.
Hawa akazidi kupayuka, neno ‘nivumilie’ hakutaka kulisikia kabisa. Rehema aibu zikamtawala na kuanza kujilaani kwa starehe alizofanya kwa pupa hadi kufikia hatua ya kumaliza pesa zote.
Wakati sakata hili likiendelea mara akaongezeka mdada mwingine huyu alikuwa rafiki yake na Hawa, wote wakaanza kumsimanga Rehema. Rehema akahisi anaonewa na hana mtetezi.
Machozi yakamlengalenga huku moyo ukiwalaani Tembo na mwenzake kwa kushindwa kumpa pesa awapatie Sub woofer.
Laiti wangempa basi angeikwepa aibu hii kwa kulipa deni.
Wakati akimlaumu Mungu kwa kumpa adhabu hii ya aibu mara akatokea mtu mwingine huyu sasa alikuwa upande wa Rehema. Hakuwa akimfahamu yeyote pale bali Rehema. Huyu naye hakugonga hodi kwani mlango ulikuwa wazi!!!!!
“Karibu …….” Rehema alijitutumua akasema, kisha akawakonyeza akina Hawa ili wasiendelee kumdai kwa sekunde kadhaa ili yule mtu aliyeingia asijue lolote.
.
“Oya!!!! Hebu mwambie bwanako atulipe chetu tusepe!!!!” Hawa akarusha kombora. Kombora hili likamshinda nguvu Rehema, likapokelewa na Munyama Mkubwa, Mnyama asiyeunguruma lakini akitembea anatikisa pori. Tembo!!!!!!
Hassan Tembo kijana asiyekuwa na mbwembwe nyingi lakini anaamini kuwa hakuna kamba nzuri na imara zaidi ya pesa. Tembo akajikoholesha kidogo kisha akamsogelea Rehema, akamdaka kiuno.
“Baby!! Hebu kaa nitamalizana nao!!!” Tembo akatupa chombezo. Ikawakera akina Hawa.
 
SEHEMU YA 29


Lilikuwa lengo lake!!!
“Mnadai nini labda samahani!!!! Na mnaonaje mkiongea sauti za chini kidogo, maana si mimi hata wewe umewahi kukopa. Utajisikiaje ukidaiwa kwa shari kiasi hiki?” maneno yake na kujiamini vikawakata mzuka waliokuwa wamepandisha.
“Sikia shem nilimwazima Rehema elfu hamsini yangu….hadi leo ananizingua mwezi umepita sasa, hata ungekuwa wewe ungetoa wapi uvumilivu?”
“Aaaah!! Samahani sana na poleni, ni mimi wa kulaumiwa sio Rehema naombeni mnisamehe, nilichukua pesa hiyo nikaitumia kama nauli kwenda visiwani ndo nimerejea na alikuwa hataki kuzungumza na mimi najua zilikuwa ni hasira..” Hassan Tembo akazungumza maneno ambayo hata yeye hajui aliyatolea wapi, Rehema akabaki kuduwaa.
“Mamii…..nisamehe mie…” sauti ya upole ya Tembo ikapenya katika masikio ya Rehema, ikasafiri mpaka moyoni, ikamwambia Tembo anakupigania…..Machozi yakaanza kumtoka, Hawa akawa wa kwanza kumbembeleza. Baadaye Tembo akachukua jukumu, akampakata Rehema!!!!
Wivu ukapenya na kuwasurubu akina Hawa. Mara mikono ya Tembo ikapenya na kukumbatia tumbo dogo la Rehema, bila kujua wapo katika mchezo wa kuigiza Rehema naye akajibu mapigo, akaanza kupapasa kifua cha Tembo. Tembo akacheka kimya kimya kisha akajitoa katika mikono ya Rehema akasogelea kochi alilokuwa amekaa awali. Akaitwaa ‘pochi’ yake. Hapo ndipo Rehema akatambua kwa nini Tembo amerejea, kumbe alikuwa amesahau pochi yake.
Pochi ikafunguliwa kwa kujiamini, noti ambazo hazijapita katika mikono ya watu wengi zikatolewa bila kuhesabiwa kwa umakini. Hawa akakabidhiwa akazihesabu. Zilikuwa zimezidi mara tatu. Yaani laki moja na nusu.
“Baby…si ananidai elfu hamsini tu!!!” Rehema akajikuta anamwita Tembo baby…
Ajabu!!
“Usijali na ya usumbufu!!!” alijibu Hassan Tembo kwa sauti ya gharama, sauti nzito lakini ya kuvutia.
Rehema alionekana kutopendezwa na uamuzi huo wa Tembo, labda alidhani kuwa Tembo hana pesa nyingine tena zaidi ya hizo alizotoa. Mawazo yake hayakuwa sahihi hata kidogo. Tembo alikuwa kifaa kingine!!!!!
“Mh!! Baby mbona kama hujaridhika vile mpenzi wangu!!!”
“Hamna nimeridhika…”
“Kama umeridhika kweli sogea hapa…” Rehema akasogea.
“Mbele ya rafiki zako naomba unichumu..” Tembo akamwambia Rehema huku akiwa amemtazama usoni.
Rehema akaingiwa kigugumizi, waliopo mbele yake wanajua kuwa Tembo ni mpenzi wake tena wa siku nyingi, kama hiyo haitoshi amemsaidia kulipa deni kubwa kama lile tena kwa kiwango mara tatu. sasa Tembo anataka apewe busu tena hadharani. Kama akikataa kumbusu basi ana kinyongo moyoni, jambo ambalo hakuwa tayari litokee, na kama akikubali basi amemsaliti mpenzi wake masikini wa jijini Mwanza. Rahim!!!!!
 
SEHEMU YA 30


Macho ya Tembo yakatazamana na Rehema. Rehema akajaribu kukwepesha alipoyarudisha bado alikuwa anatazamwa. Hawa na mwenzake huku wivu ukiwashambulia walikuwa watazamaji. Ile pesa iliwafanya wawe mabwege, walibaki kama matahira bila kujua yale hayawahusu.
Sura ya Tembo ikauvaa upole wa Rahim wa Mwanza, kanzu aliyovaa pia ikamkumbusha Rehema uvaaji wa Rahim siku kama hiyo ya ijumaa. Japo Rahim hakuwa nadhifu kama Tembo lakini waliendana. Tembo hakuwa mrefu lakini kwa kuwa walikuwa wamekaa hilo halikuleta shida. Kosa kubwa alilofanya Rehema ni kufumba macho.
Ikajengeka taswira ya Rahim wa kweli. Akafungua midomo yake yenye njaa, Tembo akasikia maneno yakimwambia karibu. Akamvagaa Rehema, kwa dakika moja ndimi zao zikawa katika mpambano wa kufurahisha. Hawa na mwezake wakawa watazamaji, huku roho zikiwauma.
Walipomaliza Rehema akakimbilia kitandani. Hawa na mwenzake wakaaga.
Akiwa kitandani Rehema akawa anajipa matumaini kuwa ‘hata hivyo ni busu tu!! Kwani nini??’…..
Laiti kama angejua kuwa lile halikuwa busu la kawaida kama linalotoka kwa mpenzi wake wa Mwanza basi angesita kulipokea.Lakini ndio tayari alikuwa amelipokea………………………………..
amelipokea………………………………..
“Mimi natoka Rehema…..naitwa Hassan Tembo, marafiki zangu huniita Munyama Mukubwa…….” Alijitambulisha Tembo. Rehema akashukuru bila kugeuza shingo yake kumtazama Tembo.
“Sasa kuna hii hapa….” Alizungumza Tembo huku akifungua wallet yake maksudi ikapiga kelele…Rehema akasikia akageuka upesi upesi. Tembo akamtazama kwa ncha za macho, Rehema wa Hussein akushtukia tego hilo, Tembo akatumia nafasi hiyo kufanya shambulizi, noti zaidi ya kumi zenye rangi nyekundu na harufu ya kipekee zilipita katika viganja vyake kisha zikatua mezani katika mfumo wa kusambaa.
“…….Utaangalia basi chakula kidogo!!” alimalizia kauli yake Tembo kisha akatokomea bila kuaga mara nyingine. Rehema mapigo ya moyo yalikuwa juu sana.
Shambulizi alilofanya Tembo ni wasichana wachache sana wanaweza kupindua!!! Wachache sana!!
Pesa ya chakula!!!!! Alijiuliza, kama hii ni ya chakula je ya matumizi ya wiki itakuwaje sasa. Tamaa ikamkonyeza kidogo!!!
Rehema kwa kunyata kama vile akitembea upesi upesi zile pesa zitapeperuka alisogea na kuzifikia zile pesa, akataka kuzigusa akasita. Akauendea mlango na kuufunga vyema na kitasa. Akayashusha mapazia halafu akawasha taa, chumba kikawa kama usiku. Hali hiyo ikamfanya Rehema ajione kama vile yu ndotoni!!!
Hakika yale yalikuwa mauzauza. Siku iliyoonekana mbaya kupita zote sasa ilikuwa imegeuka ya kupendeza. Rehema akazikusanya zile noti, zote zilikuwa na rangi nyekundu kasoro noti moja tu ndo ilikuwa haieleweki eleweki. Alipoitazama vyema akagundua kuwa ilikuwa ndogo kuliko zote. Akaisogeza kwenye upeo wa macho yake, akaisoma kidogo akagundua ilikuwa ni ‘Business card’ hakuitilia maanani akaiweka katika moja ya viti vilivyokuwa pale ndani.
Laki moja na elfu ishirini!!!!!
Pesa hii ilikizunguka kichwa cha Rehema. Tayari alijisahaulisha shida iliyokuwa inamkabili na pia alikuwa hana wakati wa kuwaza juu aibu ambayo almanusura imkumbe na kisha kupata msaada wa aina yake kutoka kwa mtu wa aina yake. Kibaya zaidi Rehema akamsahau mtu huyo kuwa ni Hassan na alihitaji kupewa walau neno moja kuu ‘Asante’….Rehema hakuwa ametoa shukrani.
Sasa alikuwa katika ki-bar cha jirani akipata bia mbili tatu ambazo alikuwa akizinywa kwa fujo sana kwani ni siku nyingi alikuwa hajazigida. Mara akaagiza huduma kutoka jikoni. Aliyekuwa mbele yake ni muhudumu wa vinywaji. Kwa kumjali mteja wake huyu akaamua kumuita muhudumu wa jikoni, “Hassan…we Hassan!!!!” muhudumu akaita kwa sauti ya juu kidogo. Akili ya Rehema ikashtuka akakumbuka hizo pesa alizokuwa anatumia zilitoka kwa kijana aliyeitwa Hassan hakukumbuka jina la pili. Hapo hapo akakumbuka pia kuwa alikuwa hajatoa shukrani kwa yote aliyofanyiwa na Hassan. Sasa akalikumbuka na lile busu motomoto. Akakunja sura kama vile mtu aliyepatwa na kichefuchefu cha ghafla.
“Ngoja nimpigie simu..yaani namwambia asante halafu nakata simu hakuna la ziada hapa!!!” alijisemea Rehema kisha akaitoa simu yake. Akabaki anajishangaa kumpigia mtu simu wakati hana namba yake. Akataka kuifuata ‘Business card’ ya Hassan lakini ile harufu nzuri ya kuku wa kuchoma ikamshawishi kubaki. Tabia Fulani ya ulafi ikawa inamtawala na kile kimuhemuhe cha kuwa na pesa za ghafla mfukoni kikawa kinampelekesha.
 
SEHEMU YA 31


Akiwa anairejesha simu yake mara ikaingia simu, alikuwa ni Robert kumbukumbu zikamjia kuwa Robert alihitaji kununua vifaa kadhaa kutoka kwake tena kwa bei poa sana. Rehema akaitazama ile simu kisha bila kuipokea akapiga mafunda mfululizo ya bia iliyokuwa mbele yake katika mfumo wa tarumbeta huku akijisahau kuwa ndani ya glasi pia alikuwa amemimina kiasi cha pombe yake. Robert aliyekuwa Lulu masaa machache yaliyopita akakosa maana tena, ile subwoofer iliyokuwa iuzwe kwa bei poa sasa haikufikiriwa kuuza. Rehema alikuwa katika starehe zake, starehe alizozilaani wakati akiwa na matatizo chungu nzima. Akaipokea simu!!!
“Roby kakangu nitakupigia nipo diskasheni” Rehema alijieleza upesi upesi kisha akakata simu. Robert akapiga tena, Rehema akaanza kuhisi kero. Akaacha kuipokea.
Ilipokatika ikaita tena safari hii aliichukua kwa jazba, akaipokea bila kuangalia mpigaji alikuwa nani.
“Jamani Ro…….”, kabla hajaendelea akakatishwa na sauti nyingine, haikuwa ya Robert.
“Mambo vipi…..”, ilikuwa sauti ngeni sana masikioni mwake. Akaitoa simu sikioni na kuitazama, ilikuwa namba mpya.
“Nani mwenzangu, samahani lakini simu yangu ilijiblock, nikawa nimerinyuu laini…..”
“Usijali usijali naitwa Tembo….”
“Temboooo….Tembo yupi??” Rehema aliuliza huku akiichukua bia yake na kuisogeza karibu na mdomo tayari kwa shambulizi.
“Hassan…..”
“Oooh!!! Jamani Kaka Hassan mambo vipi za mida”
“Poa vipi upo wapui??”
“Nipo kwangu hapa nimejipumzisha tu!!!”
“Poa napita baadaye kidogo” alisema Tembo kwa kujiamini. Rehema alitamani kukataa na nafsini mwake hakupenda Tembo arejee nyumbani kwake usiku huo. Lakini mdogo ulishindwa kutamka hadi pale Hassan alipokata simu.
laiti kama binti huyu angeijua nia ya Tembo, mapema kabisa angeukwepa mtego huu….
Lakini hakujua lolote!!!
***UMASIKINI UMEMPONZA REHEMA….ANAJIKUTA ANAKUWA MTUMWA BILA KUJUA.
***BUSU ALILOPEWA LINA MADHARA GANI…..
 
SEHEMU YA 32


Hapa akija asitegemee mtelemko, eti visenti alivyonipa nd’o atanipa kirahisi.. mimi namba nyingine aisee.
“Naitwa Tembo, rafiki zangu wananiita Munyama mkubwa nyooo…” Rehema akazungumza huku akibana pua yake.
Hatua kwa hatua akarejea nyumbani kwake kwenda kumngoja Hassan Tembo.
******
Hakuwa tena katika vazi la kanzu ila sasa alikuwa katika vazi la fulana na suruali ngumu aina ya cardet. Machoni alikuwa na miwani nyeusi, kiatu chake kilitangaza bei kwa ubora wake. Marashi makali yasiyokera yalikitawala chumba cha Rehema. Mbele yake alikuwepo Hassan Tembo. Ilikuwa tayari saa nne kasoro dakika kadhaa usiku. Ilikuwa mara ya kwanza kwa mwanaume kuwa katika chumba cha Rehema hadi muda huo wa usiku, Rehema alitamani kumwambia Tembo aondoke mdomo ukawa mzito.
Rehema hakuwa na uoga wa kuzungumza pale alipojisikia kuzungumza lakini sasa mbele ya huyu Tembo akawa na mdomo mzito.
“Rehema naweza kuungana nawe hapo kitandani….” Hassan kwa kujiamini na bila kumtazama machoni Rehema alimwambia. Rehema akashtushwa na kauli hiyo, akatamani kukataa mdomo ukawa mzito sana. Nafsi ilipinga vikali ombi hilo lakini mdomo haukusema lolote.
“no..no nooo…” akili ilisema lakini mdomo haukutoa sauti yoyote ile. Ulikuwa mzito.
Sasa Hassan alisimama kwa madaha, hatua kwa hatua akakifikia kitanda akaketi pembeni ya Rehema.
“Vipi mbona kama hujiamini au kuna mtu anakuja baadaye” Rehema akajichekesha lakini haikusaidia kuificha hofu yake.
“Najiamini.. najiamini sana na haunifanyi chochote nakuapia..” akili ilisema lakini mdomo ukawa mzito kutoa maneno haya… hivyo Tembo hakusikia lolote.
“Rehema…” Tembo aliita…..Rehema akaitika kwa kutikisa kichwa, “Asante kwa busu lako la muda ule” Tembo aliongea kwa sauti ya chini. Rehema akawa msikilizaji. Maneno ya Tembo ya kukumbushia busu alilopewa mchanaq yalimkera na kuona kama anadhalilishwa lakini hakuwa na la kufanya.
 
SEHEMU YA 33



Akiwa bado hajajua nia ya Tembo ni nini mara aliusikia mkono wa Tembo ukimgusa begani, kisha ukahama kutoka bega hili ukaenda lile, Rehema akawa ameganda kama gogo. Hakuwa na ujasiri tena.
“Sitaki.. sitaki niache.. nasema niache!!” bado mdomo haukutoa sauti, haya ni maneno aliyoyawaza akilini na hayakumfikia Tembo.
Maskini Rehema hakujua lile busu limemletea madhara gani, madhara ya kuisikia akili ikisema lakini mdomo kushindwa kufunguka. Sasa tatizo hili likayazua haya.
Rehema hakuwa na kiguo chake cha juu, akawa kama zezeta, hakuelewa kama alikuwa anaota ama ni kweli yanatokea. Muda si mrefu wakawa katika mapenzi mazito. Bado Rehema akawa anajiuliza ni kweli yanatokea???
Hakuweza kuzungumza, alifuata vile Tembo alivyotaka. Akili ilikataa kabisa, lakini ajabu mdomo haukutoa ushirikian kusema hapana….
Hakuna neno la ‘ninakupenda’ lililotamkwa na Hassan Tembo hadi walipomaliza na kusinzia wakiwa wamekumbatiana. Boxer ya Tembo ilikuwa imechanganyikana na skin taiti ya Rehema na kichupi, gauni lilikuwa uvunguni huku suruali ikiwa sakafuni, hakuna aliyekuwa na nguo ya ziada.
Suala la kuwa na mdomo mzito lilikuwa moja lakini likazuka jingie. Tembo alikuwa na ujuzi maradufu zaidi ya Rahim, mpenzi wa Rehema aliyeko Mwanza. Kutokana na maisha magumu aliyoishi Rahim, pia hata uwezo wake chumbani ulikuwa chini.
Rehema alikuwa hajawahi kujaribu ladha nyingine lakini leo hii alikuwa katika ulimwengu wa Hassan Tembo, kijana machachari aliyemgalagaza Beatrice kwa mtego wa Chipsi kuku, Clara wa Mwanza kwa kumzuga na hadithi za kubuni, Tembo aliyemkanyagakanyaga Lucy Kezi bila kujali amemzidi miaka kibao, Tembo yule yule aliyegeuza bahari kuwa uwanja wa malavidavi akamchinja binti wa watu huko. Sasa Tembo alikuwa anashughulika kwa Rehema. Rehema akapagawa!!!!! Tembo mwenye afya njema alikuwa ametenda kile alichokikosa kwa Rahim Mwanza.
 
SEHEMU YA 34


Alfajiri Tembo alikuwa ndani ya gari yake akirejea nyumbani kwake. Alikuwa ametimiza wajibu wake. Wajibu asiojua kwa nini anautimiza
Rehema alibaki peke yake akijilaani kwa kumsaliti Rahim wake, lakini mdomo wake haukuzungumza kitu. Huku akiamini pia hiyo ilikuwa bahati mbaya, mlolongo ukaanza, siku hii akiwa na mwanafunzi mwenzake wa kiume wakiwa nyumbani kwake, ikaanza kama utani yule kijana akamtaka Rehema, huku akiamini kuwa Rehema ana msimamo sana alifanya kama kubahatisha tu.
Maajabu!!!! Rehema hakupinga wala hakukubali. Raymond akajaribu kumsogelea, Rehema hakupinga wala hakukubali, mara akaanza kumpapasa. Bado Rehema hakupinga wala hakukubali.
“Vipi nifunge mlango??” Rehema hakujibu. Ray akajiongeza ukiona kimya ujue kakubali. Mlango ukafungwa.
Sasa tayari alikuwa kama alivyozaliwa akiwa mfano wa zezeta. Raymond akachangamkia dili.
“Baby….nitumie mpira au upo safe” Rehema alikuwa hajitambui wakati swali hilo linaulizwa. Raymond akajipa jibu ‘yupo safe huyu’ akafakamia na kuukamia mchezo. Kwani mimba kitu gani bwana?
Baada ya hapo kila mtu akawa anamtazama mwenzake. Mwisho Rehema aliaga na kuondoka.
Alipofika nyumbani kwake akaanza kujutia, lakini mdomo haukusema lolote. Ajabu kweli!!
Mvulana ni mvulana tu….Rayumond akafuata mkondo wa tabia za wanaume wengine. Akawatangazia wenzake alivyopata tunda kwa wepesi. Walimsifia huku wengine wakijiapiza kimoyomoyo kuwa watajaribu.
Kweli waliokuwa na nia ya dhati wakajaribu. Maajabu tena!!!! Wakafanikiwa.
Rehema aliyekuwa na msimamo mkali sasa hajui kusema ‘NO’. kila aliyejaribu akawa anapata. Baada ya kuridhika na majaribio sasa akapewa jina rasmi la ‘MAMA HURUMA’ na wale wasiokuwa na haya wakawa wanamwita ‘CHA WOTE!!!’. Masikini lile busu kutoka kwa Hassan Tembo likamkata kabisa msimamo wake. Busu kutoka kuzimu!!!!!
Wanaume wakapangana kwa foleni bila kujijua ni wangapi wanapita katika njia moja wajanja walitumia kinga na walio wajinga hawakutumia kinga. Ajira hii ikawatumbukiza katika mkondo wa kushindana kwa kila namna kuusaka UKIMWI. Tembo alishatimiza kazi yake na kuwaachia wafuasi wake!!!!
Uzuri ama ubaya wa Tembo, akionja mara moja harudi nyuma tena….
*****
 
SEHEMU YA 35

Taarifa za juu juu zilimfikia Hassan Tembo akiwa katika mawindo yake kwenye saluni moja ya kike. Akiwa anajidai hasikii lolote linalozungumzwa huku akiwa bize na simu yake na mwanamama mfanyakazi wa pale akiendelea kuzitengeneza nywele za Tembo kama alivyotaka yeye. Stori iliyokuwepo ni kuhusu mcheza shoo maarufu jijini ambaye inasemekana alifikisha lawama kwa shoga zake kuwa mpenzi wake yuko bize sana na anashindwa kumpa vyema pendo analolihitaji yeye. Wanawake wale waliendelea kupiga stori. Tembo akawa anaburudika maana walitaja hadi mahali anapokaa yule mwanadada.

Kwa kuwa alikuwa anajulikana basi Tembo alimfahamu kwa wepesi sana. Ile stori ikamkolea akaanza kukijengea picha kile kiuno cha mwanadada yule akiwa stejini anavyozungusha, laiti kama angeanza kuwika kabla ya Ray C huenda lile jina la kiuno bila mfupa angepewa yeye.
Hassan Tembo akaanza kutamani kuijua kwa vitendo ladha ya kiuno bila mfupa. Pia akakumbuka sifa wanazopewa wacheza shoo kuwa wana habari kubwa chumbani. Tembo Hassan akamweka katika mahesabu yake Mamamia Mango!!!!
Ni huyu ndo alimuhitaji, ni huyu alikuwa na kiuno kisichokuwa na mfupa. Lini na nitampata vipi??? Tembo alijiuliza!!!!!
Hakuwa na jibu la haraka haraka. Alihitaji muda wa kufikiri!!!!
Lakini wakati wa kufikiri akashangaa yeye na akili zake. Baada ya muda mrefu wa kurukaruka na wasichana leo hii anawaza juu ya ladha ya msichana? Kulikoni!!
Huyo Mamamia na kiuno chake asichokijua ndo anakiwaza ama?
Alistaajabu lakini akajiapiza kuwa kwa hali na mali lazima amsake Mamamia!!
Laiti kama angeijua safari anayoiwaza ilivyo.. ni heri asingelisikia lile jina tena!!!
***TEMBO ametembelea na kuacha alama na ajira za kutisha katika mitandao ya kijamii, vyuo vikuu na sasa ameingia mtaani kujaribu kuwaajiri watu wenye umaarufu…….
****JE? TEMBO atampata MAMAMIA MANGO?????
 
SEHEMU YA 36
****
Mamamia Mango kama jina lake lilivyokuwa maarufu jijini Dar es salaam na pande nyingine ndani ya nchi . Alizaliwa miaka ishirini na sita iliyopita na kupatiwa jina la Lulu kutoka kwa wazazi wake, alikuwa na thamani ya lulu kweli kama wazazi wake walivyompa jina hilo. Akiwa na miaka kumi tu, tayari ule urembo wake wa asili ukachomoza machoni pa watu. Hakujijua kama ni mrembo hadi baadhi ya watu walipoanza kumwita mrembo. Kitotototo aliamini kuwa ni utani. Mama yake mzazi akaona kuwa mwanaye alikuwa na thamani kupita hiyo lulu yenyewe, taratibu akaanza kumwita mtoto wa mama, baadaye bwana mmoja aliyejifanya mjuaji sana akamtonya mama yake Lulu kuwa mtoto wa mama kwa ki italiano anaitwa mamamia, mama Lulu akapuuza lakini yule bwana mara moja akaanza kumwita Lulu: mamamia, jina hili likaanza kunoga hatimaye Lulu likasahaulika akawa anaitwa Mamamia. Yeye binafsi alilipenda.
Kasoro moja tu, Mamamia hakuwa mwelevu darasani hivyo alijikuta mara kwa mara akifeli masomo yake. Hali duni ya wazazi wake ikamsukumia katika kucheza ngoma za kiasili, kiuno chake kilizimudu haswa ngoma hizo. Baadaye kiuno kile kikahitaji mambo ya kisasa zaidi. Bendi ya Twanga pepeta ya jijini Dar es salaam ilipohitaji madensa wapya ilifanya shindano dogo katika ukumbi maarufu na wa muda mrefu wa Mango Garden maeneo ya Kinondoni.
Mamamia alikuwa mmoja kati ya washiriki katika mashindano haya. Hakuwa na kipingamizi chochote alishinda kwa kura nyingi sana. Akawa Mamamia wa Mango Garden, baadaye akafupishwa kuwa Mamamia Mango, likavuma sana hatimaye likawa jina lake. Wale waliomjulia ukubwani wakisikia unamuita Lulu wanadhani umekosea. Jina hilo lilisahaulika kabisa!!
Mamamia akaweka heshima mbele. Alikuwa mgumu sana kuukabidhi moyo wake kwa mwanaume lakini hatimaye akanasa kwa mtengenezaji wa muziki, aliyeitwa Romeo, urembo wa Mamamia haukuwa tiba tosha kwa Romeo aliyezoea kujibadilishia wanawake kila anapowachoka. Mamamia alivumilia kwa kila hali alimpenda Romeo kwa jinsi alivyoweza. Hakuitaka orodha ya wanaume wengi katika maisha yake ya usichana.
Ni hapa mnyama mwenye nguvu za ajabu. Hassan Tembo alikuwa amepatamani. Swali likabakia anaingia vipi??
****
Ukumbi wa Mango Garden uliopo maeneo ya Kinondoni jijini Dar es salaam ulikuwa umesheheni watu kadha wa kadha waliofika pale kwa nia ya kujipatia vinywaji na kutazama burudani kutoka kwa wakali wa muziki wa dansi.
Katika meza ndogo iliyotosheleza watu wawili alikuwepo kijana ambaye alifika mapema kuliko wateja wengine, meza yake ilikuwa imebeba chupa tupu tatu za bia aina ya ‘castle lite’…… hapakuwa na dalili ya kumsubiri mtu. Alikuwa ameridhika sana na kuwa peke yake.
Majira ya saa nne usiku umati ulikuwa mkubwa na kila mtu alikuwa katika pilika pilika zake huku na kule. Bendi ya Twanga pepeta ilikuwa imejikita katika kutoa burudani. Sasa macho ya kijana huyu yalikuwa yapo makini kabisa yakilitazama jukwaa, kuna kitu alihitaji kukiona lakini hakukiona. Akahama kutoka alipokuwa akasogea karibu zaidi, bado hakuonekana kuridhika. Baadaye akawa kama aliyekata tamaa lakini kelele za ghafla kutoka kwa wateja waliofika pale zilimgutusha akageuka nyuma. Macho yake yakampa jibu la kwamba hizo kelele zimesababishwa na nini. Mbele yake kilionekana kiwiliwili kikijiviringisha huku na kule katika namna ya kipekee, kiwiliwili kile kilikuwa kimejigeuzia nyuma na kuwaachia wateja wajionee mgongo na makalio yanavyotikisika kiufundi. Na hicho ndio kikubwa wateja walipendelea. Huyu alikuwa ni Mamamia Mango akijishughulisha jukwaani. Tembo akatahamaki, alikuwa hajawahi kuonana na Mamamia ana kwa ana. Moyo ukapiga kwa mshindo mkubwa. Akakaa kwenye kiti. Akajitokeza mteja mmoja kwenda kumtuza Mamamia, Tembo naye akaunga tela. Alipofika pale nia yake ilikuwa kumtumbukizia Mamamia pesa kwenye matiti yake ili aweze kumpakaza miujiza yake.
 
SEHEMU YA 37


Alipomfikia Mamamia ilikuwa ni aibu ya mwezi, hakuwa na pesa hata kidogo. Kumbe katika kushangaa wajanja wa mjini walikwishajichukulia vilivyo vyao. Tembo akapatwa na mshituko.
Walinzi wakawahi wakamtoa walijua ni mlevi!!!!
Taharuki iliyomkumba Tembo ikamfanya atoweke eneo lile akafika nje na kupiga simu kwa rafiki zake waweze kumpatia pesa, bahati nzuri walikuwa na pesa lakini pesa hizi zilikuwa katika mfumo wa Tigo pesa na Mpesa. Haraka haraka wakamtumia, sasa sita hii Mpesa na Tigo pesa wapi na wapi??? Tembo ambaye hakuja na gari siku hiyo kwa simanzi kubwa akaondoka kwa miguu kurejea nyumbani. Mbagala!!!
Kila hatua aliyotembea alijikuta akihamishia hasira zaidi kwa Mamamia kama ni yeye aliyemtuma kuja hapo Mango Gardern.
Kinondoni Studio, Mkwajuni, Morocco hoteli, Magomeni, Kigogo, Msimbazi, Ilala, Veta, Keko, Taifa, Uhasibu, Sabasaba, Kwa Azizi Ally, Mtongani, Mission, Sabasaba ya pili, Kipati hapa ndo akapata lifti ya kumalizia safari yake.
Alifika hoi sana. Hakupata hata muda wa kuingia bafuni akajitupa kitandani akalala.
Hasira ikiwa imemtawala
Kesho yake alizinduka majira ya saa sita mchana. Karaha ya siku iliyofuata ilikuwa haijaisha. Mamamia Mango, jina hilo likakiteka kichwa chake. Akaingia bafuni kuoga. Alipotoka akawasha gari lake, safari ya kwenda Kinondoni!!!!!
Hakuwa na uhakika ni wapi hasa anaelekea na ni nini hasa atamwambia Mamamia lakini alichoamini kuwa lazima aonane na Mamamia.
Hapakuwa na foleni sana hivyo alifika kwa wakati ambao aliufurahia. Saa kumi alasiri mida ambayo wapenzi wengi hupenda kukutana. Ilikuwa ni siku ya mapumziko.
Tembo akaanza kuichora ramani ya wapi nyumbani kwa Mamamia. Alipoona haichoreki akaamua kuulizia, haikumchukua watu watatu kuweza kuliona geti la nyumba iliyosemekana kuwa ni makazi ya Mamamia.
“Naenda kumwambia nini sasa???” alijiuliza Tembo. Kwa mara ya kwanza akajihisi uoga kumvaa msichana.
Akastaajabu!!
Akapiga moyo konde akaisogeza gari taratibu akapiga honi getini. Baada ya muda akatoka ndani msichana, kiumbile alirandana na Mamamia lakini tatizo moja tu hakuwa na kiuno kisichokuwa na mfupa.
“Samahani kaka….unamuhitaji nani??” aliuliza Yule dada baada ya kumjulia hali Tembo.
“Mamamia….sijui yupo”
“Una ahadi naye??” aliulizwa.
Aaaah!!! Washaanza uzungu wao!!!! Tembo Hassan alilalamika kimoyomoyo.
“Hapana kwa kweli ila nahitaji sana kumwona!!!! Mimi ni shabiki wake namba moja” alijibu Tembo.
“Mh!! Hebu ngoja nimuulize…nimwambie nani??”
“Hassani!!”
Yule binti akaitwaa simu yake akabonyeza namba kadhaa.
“Dada kuna mgeni wako anaitwa Hassani”
“……..Hapana….haya….” alimaliza mazungumzo.
“Msubiri anakuja….”
Tembo akakubali kwa kutikisa kichwa Yule binti akaingia ndani kisha akalifunga geti akimwacha Hassan nje. Kitendo hicho kikamkera Hassan akahisi amedhalilishwa.
Alisubiri dakika kumi mara zikawa ishirini na hatimaye nusu saa….hasira zikaanza kujiunda kooni. Akachukizwa na dharau hiyo. Akataka kupiga honi tena, akajikuta katika kusita akaacha. Akashuka kutoka ndani ya gari yake. Akaliendea geti ili aweze kuingia ndani na kuulizia kulikoni.
Ile anataka kugonga hodi akakatishwa na geti kufunguliwa, alikuwa ni yule yule aliyelifunga awali.
 
SEHEMU YA 38


“Amesema samahani anakuja sasa hivi” alimaliza kutoa taarifa na kufunga tena geti. Hakumkaribisha Tembo ndani. Tembo akajiuliza kulikoni, hakupata majibu. Kitendo cha Mamamia kutuma maombi ya samahani kidogo kikamfariji Tembo. Akarejea ndani ya gari akaketi, akauacha mlango wazi akazima kiyoyozi.
Hatimaye geti kubwa lilifunguliwa. Tembo akadhani ilikuwa ni zamu yake kukaribishwa na kuliingiza gari lake ndani. Akazama garini akajiweka sawa kwa ajili ya kuendesha, tofauti na mawazo yake mara akasikia honi, ilikuwa inatoka gari nyingine. Gari mfano wa mpya, aina ya Grand Vitara.
“Kama ni ya kwake amenipiga bao la kwanza!!!” Tembo alijisemea. Na baada ya muda akalipata jibu la uhakika. Kioo kiliposhushwa kikachomoza kichwa cha mwanadada ambaye hakuwa Yule anayekata viuno mbele ya umati, huyu alikuwa Mamamia mwingine.
Tembo akataharuki. Kisha akajaribu kujiweka sawa. Mamamia akamwita Tembo, kwa ishara ya vidole viwili, Tembo akatii. Akasogea hadi karibu na gari aliyokuwa anaendesha Mamamia.
“Nisamehe kwa kukuweka sana…..”
“Aaaah!! Usijali dadangu”
“Naitwa Lulu….niseme Mamamia huenda ndio utanielewa vyema, sijui mwenzangu”
“Hassan….Munya…..aaah!! niite Hassan” Tembo akaogopa kuweka mbwembwe, nidhamu ya uoga mbele ya Mamamia ikawa inamshambulia bila kutarajia.
“Ehe!! Nambie…” Mamamia akamwachia uwanja Tembo ajieleze.
“Nilikuwa na maongezi na wewe”
“Ndo hapa sasa nipo zungumza…” alijibu Mamamia. Bila kushuka garini.
“Mamamia nahitaji kuzungumza kirefu na wewe.” Alijiumauma Tembo.
“Hebu sema kwa kifupi halafu kama yana maana nitakuambia unieleze kwa kirefu.” Mamamia akajibu huku akiiweka miwani yake vyema machoni pake.
“Aaaah!! Mamamia bana….haya…..”, alijichekesha kimtindo kisha akaendelea. “Mamamia ni masuala Fulani kuhusu mahusiano”
“We ni mwandishi wa habari????” Mamamia hakushtushwa na kauli ya Tembo juu ya mahusiano. Badala yake akazua mengine.
“Hapana sio mwandishi kwani vipi….”
“Nilijua unaandaa makala kuhusu mahusiano….” Mamamia akatoa kijembe. Kikamkera Tembo akajichekesha huku akiumia moyoni.
“Na pia kama ungekuwa mwandishi huu mzigo wa mahusiano wangekuwa wamekuonea, mbona we kadogo hivyo?” Mamamia alizungumza hayo huku chembechembe za dharau zikichomoza.
Kadogo!!!!!!! Amenidharau @Q#$4%....Tembo akamtukania Mamamia mama yake kimya kimya.
“Ehe!! Au sijaelewa mahusiano kivipi??”
“Nahitaji kuzungumza na wewe Mamamia…ni maongezi kuhusu mimi na wewe”
“Na hapa tuko mimi na wewe, Hassan!!!” Alisisitiza.
Tembo akakosa la kujitetea, akaamua kuachana na mada hiyo.
“Basi tutaonana siku nyingine Mamamia…ila nakupenda”
“Asante karibu home!!!” neno la mwisho halikusikika vizuri, gari ilikuwa mita kadhaa ikiondoka.
Tembo akatazama kushoto na kulia kuangalia kama kuna mtu alikuwa anawatazama. Aibu kama zingekuwa zinapimwa kwa mzani, hii ya leo ilikuwa haipimiki, isitoshe Tembo alikuwa anajiamini sana. Kushindwa huku kukamfadhaisha.
 
SEHEMU YA 39



Tembo akiwa katika bumbuwazi, mara geti likafunguliwa.
Akashtuka!!!! Kutazama akatoka yule binti ambaye ndiye alimkaribisha.
“Ahh!! Kaka umeonana naye eeeh!!”
“Yeah!! Nimeonana naye alikuwa na haraka huyo, lakini tumeelewana” alidanganya Tembo.
“Mh!! Yukogo bize huyo we acha tu!!!” aliongezea yule mwanadada.
“Haya mi ngoja niondoke tutaonana siku nyingine.”
“Thamahani kaka, unapitia njia ipi…”
“Vipi na wewe unatoka, naweza kukusindikiza sina haraka”
“Naelekea Mlimani City hapo….magari ya kwenda Ubungo taabu kweli”
“Kama umeshajiandaa twende zetu”
“Mi nipo tayari”
Tembo akashuka garini akamfungulia mlango yule binti, akaingia kwa madaha akakaa siti ya mbele.
Kinguo chake kilichokuwa kimevuka magoti kidogo kikavuka zaidi na kuacha mapaja yake meupe kwa nje.
Tembo akachungulia kidogo!!!
Safari ikaanza.
“Mimi nilikwambia naitwa Hassan, na wewe je?”
“Mimi??” aliuliza kama vile ndani ya gari wapo sita.
“Naitwa Brenda Brendson shothti dhangu wananiita BreBre…”
“Kwa hiyo mi nikiita yote nakosea…”
“Aje?”
“Brenda BreBre” Tembo akatamka kiufasaha, jina lile likampendeza Brenda na yeye akalitamka huku akiliwekea nakshi za kimjini mjini, “Brenda BreBre” kisha akacheka kizungu huku akijiziba mdomo, Tembo akawa makini kwenye kioo cha ndani akimtazama.
“Hathani jamani nimelipenda hilo jina!” Brenda akamwambia Hassan. Tembo akasikia kitu akaanza kujiuliza ni nini hicho, mara akatanabai kuwa ni KITHEMBE!!!!!
Brenda alikuwa na kithembe, badala ya kusema Hassan maskini Brenda anaita Hathani. Hali hiyo haikumkera Tembo akafurahia na kujikuta akianza kumsahau Mamamia. Mwili ukamsisimika, akaanza kufikiria kumtoa Brenda kafara ya Mamamia, yaani ajichinjie Brenda kupunguza machungu ya kuaibishwa na Mamamia.
Halmashauri ya kichwa chake ikapitisha uamuzi huo.
**Kwa mara ya kwanza Munyama anagonga mwamba kwa mwanadada….. Mamamia wa Mango….
Ili kujipooza machungu anataka kuhamishia makali kwa Brenda….
Je itawezekana…
 
Back
Top Bottom