CHANGE
Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Namouih alifika nyumbani kwake kwenye mida ya saa tatu asubuhi hiyo, naye akaelekea chumbani na kumkuta mume wake akiwa tayari kuondoka, lakini haikuwa kuondoka kwenda kazini. Alikuwa ameweka nguo chache kwenye begi dogo la mgongoni na baadhi ya vifaa muhimu vya kikazi, jambo lililomwambia Namouih kwamba mume wake alikuwa anataka kufanya safari fupi ya kikazi. Efraim Donald alimlaki Namouih kwa furaha baada ya kuwa amerudi, naye akamuuliza ikiwa mambo yalikwenda vizuri jana akiwa na rafiki yake.
Kwa kutotaka kuingiza zile habari za ugomvi uliotokea usiku, Namouih akaamua kuficha ukweli na kusema, "Ndiyo. Mambo yalikwenda vyema."
"Angalau umetuliza akili kidogo eh?" Efraim Donald akamuuliza.
Namouih akatikisa kichwa kukubali na kuangalia chini kama kuonyesha hana raha.
"Ona Namouih... najua tuna mambo mengi sana ya kuzungumzia ila kuna huu mkutano mkubwa umejitokeza... masuala yale yale ya mikataba na nini... kwa hiyo nafikiri ndani ya wiki nitakuwa nimerudi. Naomba univumilie... tutaongea vizuri sana nikirudi," Efraim akamwambia huku akiwa ameyashikilia mabega ya mke wake.
"Ni sawa Efraim. Nitasubiri," Namouih akamwambia.
"Nitakaporudi nafikiri maandalizi yatakuwa yameshakamilika... nataka hii party mwaka huu iwe spectacular... utafurahia sana honey," Efraim akasema.
"Party?" Namouih akauliza akiwa hajaelewa.
Efraim Donald akaachia tabasamu na kuuliza, "Umesahau?"
"Nini?"
"Birthday yako inakaribia Namouih," Efraim akamkumbusha.
Namouih akatazama pembeni na kuachia tabasamu hafifu, naye Efraim Donald akacheka kidogo.
"Mambo yamekuwa mengi, siyo rahisi kukumbuka yaani. Ulikuwa unafanya maandalizi ya birthday
party?" Namouih akauliza.
"Yeah. Na ninataka mwaka huu ndugu zetu wote wawepo huku," Efraim akasema.
Namouih akatabasamu huku akimwangalia kwa hisia.
"Mama, Zakia, Sasha, Nasma, na washkaji zako wote nawaleta huku... ahah... nataka yaani ifunike sherehe zingine zozote za kuzaliwa nchi nzima," Efraim akamwambia.
"Ahahah... haiwezi kuzidi sherehe zingine zote. Kuna watu wana pesa zaidi yaani siku ya kuzaliwa mtu ananunuliwa ndege," Namouih akasema.
"Aa, hayo ni akina Beyonce na Jay-Z tu ndiyo wanafanya, ushaona wapi kwa nchi yetu? Wewe subiri tu, nimekuahidi utaifurahia, utafurahia kweli," Efraim akasema.
Namouih akatikisa kichwa kukubali na kusema, "Sawa. Asante Efraim."
Efraim Donald akambusu mke wake mdomoni, na Namouih akatania kwamba hakuwa ameosha mdomo kwa hiyo busu hiyo isifike mbali. Mume wake akacheka na kumkumbatia, kisha akaanza
kuondoka na kwenda mpaka nje ili kupanda gari; alikokuwa anasubiriwa na Suleiman. Kupitia dirishani, Namouih alisimama kwenye kiubaraza kidogo kwa nje huko huko juu na kumpungia mkono wa kwa heri mume wake, kisha Efraim Donald akaingia ndani ya gari na kuondoka hapo hatimaye.
Namouih alibaki amesimama sehemu hiyo akiwaza mambo mengi. Ni ile hali fulani ya kuhisi hatia
kwamba ingawa alikuwa amemwambia mume wake jambo zito sana siku iliyotangulia, bado
mwanaume huyo alimtendea vizuri na angalau kwa wakati huu alionyesha nia ya kutaka kurekebisha mambo. Lakini bado Namouih hakuwa ameridhika mpaka suala lile lililoisumbua ndoa yao litatuliwe kwa usahihi, kwa hiyo ingawa alihisi ni kama anamsukuma mno mume wake, bado angeendelea kushikilia msimamo huo mpaka kieleweke kweli.
Akarudi tu ndani baada ya hapo na kwenda kuoga, kisha akavaa nguo nzuri sana za kikazi na kujitengeneza vizuri sana kichwani na usoni kuumeremetisha urembo wake, halafu akaamua kumpigia tu rafiki yake ili kumjulia hali. Blandina alipopokea simu, aliongea kwa shauku nyingi sana akisema yeye na Draxton walikuwa wamerudiana tena, na ingawa alihisi kwamba furaha yake ilipita kiasi mno lakini bado alijihisi vizuri sana moyoni. Aligusia pia suala la jinsi alivyoamka na kujikuta hana jeraha kichwani, naye Namouih akamwambia tu Draxton alipofika pale walipokuwa usiku wa
jana alimsaidia kwa dawa, bila kusema kwa undani ni dawa gani hiyo. Blandina akasema kwamba
wangekutana baadaye ofisini kwa kuwa alijisikia vizuri sana kufanya kazi leo.
Jinsi Blandina alivyokuwa anamwongelea mwanaume wake, kwamba amempikia, jana alimwokoa, na kumbeba mpaka chumbani, bila kusahau busu kali waliyopeana asubuhi hiyo, ilimfanya
Namouih acheke sana. Akafurahi kwa ajili ya rafiki yake na kumpa hongera, kisha wakaagana kwa
wakati huo, na mwanamke huyu akaelekea chini kupata kiamsha kinywa alichoandaliwa na Esma.
Akatumia muda mfupi kucheza na paka wake wa kufugwa, na baada ya hapo akaelekea kazini pia.
★★
Watu wengi ndani ya kampuni aliyofanyia kazi Namouih walifurahi sana kumwona tena, na wengi
walitumia muda wao kuzungumza naye wakimjulia hali na kuuliza jinsi alivyookoka kifo kwenye ile "ajali" iliyompata. Aliongea kwa ustaarabu na kuwashukuru wengi waliomtumia salamu zao, na sasa alikuwa amerudi kazini tena kuendelea kufanya kazi kwa bidii, hivyo bila kukawia akaingia ofisini kwake na kumkuta Blandina akiwa humo. Marafiki hawa wakakumbatiana kwa upendo mwingi sana, na Blandina alionekana kuwa na furaha isiyo na kifani, kwa hiyo wangezianza kazi
zao huku wanapata maongezi kuhusu mambo yaliyotokea jana usiku mpaka Blandina akajikuta
anaamkia mikononi mwa Draxton wake asubuhi hii.
Waliendelea na kazi za hapa na pale mpaka imefika mida ya saa saba mchana, ndiyo Namouih akawa amemwita Blandina na kumkumbusha kuhusu kukutanika kwao na marafiki zao wale wawili
waliokuwa wanakuja upande huu wa jiji leo kuwatembelea. Blandina alikuwa ameshasahau kabisa kuhusu hilo, naye akamwambia Namouih kwamba kwa sababu alikuwa amesahau, tayari alikuwa
ameshafanya mipango ya kukutana na Draxton mchana huo kwa hiyo alihisi asingeweza kwenda kule walikopanga kukutana na rafiki zao hao. Namouih akamwambia haikuwa na shida, kwamba waende kukutana na rafiki zao huko kwa muda huu kabla Draxton hajaja kumpitia, au angempitia wakiwa huko huko.
Wazo la pili lilionekana kuwa zuri hasa kwa sababu Blandina alitaka sana pia kuwaona mashosti zake wale, kwa hiyo akatoka na kumpigia simu Draxton ili amjulishe kwamba angekwenda sehemu fulani ya jiji, kwa hiyo ampitie akiwa huko. Draxton kama Draxton hakuwa na shida, naye akasema kuna mambo alikuwa anamalizia kisha ndiyo angempitia kwa hiyo wangeonana baadaye. Basi baada ya hayo, Blandina akamjulisha Namouih, ndiyo marafiki hawa wakaondoka pamoja kuelekea kule walikoahidiana kukutana na marafiki zao; Dantu na Marietta.
★★
Marafiki hawa wawili walikwenda pamoja kwenye eneo la kati la jiji ambako kulikuwa na hoteli fulani ya kifahari sana iliyopewa jina Zakhem. Haikuwa hoteli kwamba ni hoteli iliyopokea wageni wa kulala, bali hoteli maalumu kwa ajili ya vyakula vizuri sana na vya gharama. Ilikuwa ni kama mgahawa lakini kwa sababu ya kiwango chake kikubwa cha umaridadi iliitwa hoteli, na Namouih
pamoja na Blandina wakawa wamefika hapo na kwenda ndani kutafuta sehemu za kukaa.
Walikaribishwa vyema, nao wakapewa meza moja iliyozungukwa na viti kama masofa, kisha wakaagiza vinywaji vya juice za cream na chips fulani kavu sana zenye pilipili kali (chilli fries), nao
wakaanza kula taratibu huku wakiwasubiria marafiki zao ambao tayari walikuwa wamekwishawasiliana nao. Hatimaye Dantu na Marietta wakawa wamefika, nao wakapokelewa kwa shangwe sana kwa kuwa ni muda mrefu ulikuwa umepita bila ya wao kuonana. Waliishi mkoa tofauti na huu na walifanya kazi kwenye maduka makubwa ya vito vya gharama na masuala ya mitindo na urembo, hivyo walikuwa aina ya wanawake wenye nguvu kipesa.
Dantu alikuwa mweupe, mtu wa zenji, na ingawa alikuwa na miaka 40 lakini alionekana kuwa kama na miaka 25 kutokana na kujua kupangilia mwonekano wake kwa uzuri wa hali ya juu. Alikuwa
mwanamke mwerevu sana na ndiyo alikuwa amevalishwa pete siku za hivi karibuni na mpenzi wake wa muda mrefu mwenye pesa pia, na tayari alikuwa na mtoto mmoja wa kike pamoja na huyo huyo mchumba wake. Marietta yeye alikuwa mwanamke mzuri sana pia, mwenye miaka 35, aliyekuwa na mashauzi mengi hatari. Alipenda sana kuponda raha na alikuwa na akili nyepesi, yaani mjanja. Umbo lake lilikuwa namba nane, na urefu wake ulikaribiana na urefu wa Namouih
hasa kama angevaa viatu virefu, na alikuwa bado hajaolewa wala kuwa na mtoto.
Ujio wao ulifanya wote wachangamke na kuanza kuongelea mambo mengi sana yenye kufurahisha na hata kuhuzunisha, kama suala la kifo cha Felix, na wanawake hao pia wakaagiza vyakula na juice ili kujiunga pamoja na wenzao kwenye makamuzi. Maongezi yalipohamia kwenye maisha ya mapenzi, wote waliwazungumzia wanaume wao na namna wanavyoumiza vichwa sana lakini hakukuwa na namna ila kukomaa tu na mahusiano. Blandina alianza kumwongelea Draxton wake
pia, akimsifia kuwa mtu mzuri mno ambaye hajawahi kukutana na aina yake hata mara moja. Alikuwa anamwongelea vizuri sana kwa mashoga zake hasa kwa kuwa Marietta aliulizia mno habari zake. Blandina angesema kwamba Draxton alimfaa kabisa hata kuolewa naye, na Namouih akawa kimya tu kuelekea maongezi yaliyomhusu mwanaume yule ingawa alijua vitu vingi kumhusu.
Baada ya muda mfupi, Blandina akapigiwa simu, ikiwa ni Draxton, ambaye alimjulisha kwamba tayari alikuwa sehemu ya nje ya jengo hilo kumpitia, hivyo mrembo atoke ndani hapo. Baada ya Blandina kukubali na kukata simu, Dantu na Marietta wakaanza kumshinikiza amlete Draxton ndani hapo ili nao wamwone pia kwa sababu walitaka tu hata kusikia sauti yake. Namouih akaingilia kati na kuwaambia halingekuwa jambo zuri kumsumbua kaka wa watu, lakini wenzake wakampondea, wakisema aache ubahili wa macho kwa kuwa yeye tayari aliwahi kumwona. Wakamshawishi Blandina atunge kisingizio chochote tu cha kumwambia Draxton ili amlete ndani hapo, naye Blandina akakubali na kuondoka. Hata hivyo na yeye Blandina alitaka mashoga zake wamwone mwanaume wake mubashara ili awadolishie kwa njia fulani, kama ujuavyo mambo ya wanawake.
Akatoka mpaka nje na kuliona gari la mwanaume wake likiwa limeegeshwa usawa wa barabara,
naye akaliendea na kuingia ndani yake, akitazamwa na watu kadhaa kutokana na mwonekano wa shepu nono aliokuwa nao. Draxton alikuwa ameketi kwenye siti ya usukani huku akimwangalia kwa upendezi, naye Blandina akampa tabasamu la madoido.
"Tukazurure sasa," Draxton akamwambia.
"Ndiyo, ila kuna ishu imezuka..." Blandina akasema.
"Mm-hmm..."
"Kuna rafiki yangu mwingine... ana mzigo wangu. Anatoka huko juu anakuja kunipitishia, kwa hiyo
naomba tumsubirie kidogo," Blandina akamwambia.
"Sawa, haina shida," Draxton akamwambia kwa upole.
"Twende ndani basi, tukamsubirie..."
"Huko ulipokuwa?"
"Yeah."
"Si ni bora tu tukikaa humu?"
"Ndiyo ila, nimewaacha rafiki zangu pale. Itakuwa nzuri zaidi tukienda kukaa nao kwa ufupi."
Draxton akapandisha nyusi huku akimtazama kama anauliza 'kweli?'
"Ahahah... na ndiyo, nataka wakujue pia. Dantu kavishwa pete juzi juzi, twende hata ukampe hongera," Blandina akasema.
Draxton akavuta pumzi na kuishusha huku akisema, "Okay."
Blandina akafurahi na kumsogelea karibu zaidi, naye Draxton akambusu mara tatu mdomoni. Lipstick nyekundu ya Blandina ikabaki mdomoni mwake Draxton, naye Blandina akaifuta taratibu huku wakiangaliana kwa hisia.
"Twende."
Blandina akamwambia hivyo na kuketi vizuri kwenye siti yake. Draxton akazima gari lake na
kushuka, halafu akazungukia upande wa Blandina na kukuta anashuka pia. Akaifunga milango na wote wakaanza kuelekea kwenye hoteli ile huku wameshikana mikono. Draxton alikuwa amevalia koti gumu jeusi (leather jacket) lililokuwa juu ya T-shirt nyeupe aliyovaa kwa ndani, suruali ya jeans ya rangi nyeusi na viatu vyeusi chini. Blandina alitembea naye kwa ukaribu sana, akijivunia kuangaliwa na baadhi ya watu eneo hilo ingawa hakuonyesha hilo.
Wakafika sehemu ya ndani na kuanza kuelekea pale alipowaacha rafiki zake. Tayari rafiki zake
Blandina walikuwa wamemwona Draxton pindi alipoingia tu, nao wakawa wanasema kweli jamaa alionekana kuwa ngangali sana mbali na kuwa na sura nzuri. Namouih alikuwa anamtazama kwa
umakini, akipendezwa kwa kiasi fulani na mwonekano wa mwanaume huyo. Draxton tayari alikuwa
ametambua uwepo wa Namouih kwenye mchanganyiko wa watu hapo baada ya kuivuta harufu yake mapema, na hakuwa ametarajia kumkuta hapo pia, lakini kuvunga kwamba hawakuwa na akili
moja juu ya jambo fulani ilikuwa kitu muhimu kwa wawili hawa.
Blandina akawa amemfikisha mwanaume wake walipokuwa Dantu, Marietta, na Namouih, nao
wakasalimiana vizuri. Blandina akaketi kwenye sehemu yake na kumwachia nafasi Draxton ili naye
akae, na mwanaume akaketi. Harufu nzuri ya Draxton iliwavutia sana wanawake wote, na Marietta akaanza kumsemesha.
"Draxton... agiza chochote... me nitalipa," akasema kiutani.
Wengine wakacheka, naye Blandina akasema, "Tayari unataka kumuiba!"
"Siyo hivyo, ila we' ukichelewa lazima me nijiongeze," Marietta akamwambia.
"Umekwama baby. Drax, huyu ni Marietta na Dantu. Yule pale nafanya naye kazi hata simkumbuki jina lakini," Blandina akawatambulisha wenzake, nao wakacheka kwa namna alivyomtania Namouih.
"Nimefurahi kuwafahamu. Hongera pia Dantu kwa kuwa unaelekea kuwa jiko rasmi," Draxton akaongea.
"Ahahahah... asante. Amekwambia huyu eeh?" Dantu akauliza.
"Ndiyo," Draxton akajibu.
"Nasikia ulivunja rekodi ya Namouih ya kutopoteza kesi hata moja," akasema Marietta.
Wengine wakacheka kidogo, kisha Namouih akasema, "Yeah. Draxton ni bingwa."
Draxton akamwangalia machoni, naye Namouih akatabasamu kwa mbali na kuangalia chini.
"Mwitie mhudumu basi," Marietta akamwambia Blandina.
"Oh no, niko sawa. Tunamsubiri tu rafiki yenu, akifika tunaondoka," Draxton akasema.
Blandina akawatazama wenzake na kukodoa macho kidogo huku amejishika shingoni, njia fulani ya kuwaambia kwamba hicho ndiyo kisingizio alichokuwa amempa jamaa. Wenzake walipoelewa hilo, wakaanza kusema 'aaaah sawa' kwa kupishana, jambo lililofanya Namouih acheke kidogo.
"Vipi? Mbona unacheka?" Draxton akamuuliza.
"Aa... hamna kitu. Nilikuwa tu nimekumbuka kitu fulani... kabla hujafika tulikuwa tunazungumzia
kuhusu wasanii. So nimekumbuka tu," Namouih akaongea kwa kujihami ili abadili mawazo upesi.
"Okay sawa. Wasanii na vituko vyao eh?" Draxton akauliza.
"Yeah, ila sana sana kuhusu mafanikio. Tulikuwa tuki-discuss nani angefika mbali sana kama Mdee na Mondi walivyofanikiwa kufanya kwanza," Blandina akamwambia.
"Siyo Diamond na Vanessa Mdee peke yao, ni basi tu kwa sababu wewe unawashobokea sana,"
Marietta akamwambia.
"Nani mwingine amefika mbali kabla yao? Kisanaa tu?" Blandina akauliza.
"Wapo wengi mbona? AY, K-Lynn, Kanumba... tena Kanumba ndiyo alikuwa kubwa yao," Marietta
akasema.
"Ee... ndiyo ni kweli, Kanumba. Imagine kama angekuwepo mpaka sasa hivi. Alikuwa na kipawa kizuri sana cha kutunga story," Dantu akasema.
"Eee kweli. Nani mwingine angetop hao watatu? Eti Draxton? We' unafikiri nani?" Marietta akauliza.
Draxton akatabasamu tu.
Namouih alikuwa anamtazama kwa umakini sana.
"Haionekani kama unafatiliaga sana wasanii, eti shem? Oh, ni sawa nikikuita shem?" Marietta
akamuuliza.
Wengine wakacheka kidogo, naye Draxton akasema, "Ndiyo ni sawa, shem."
Blandina akaachia tabasamu la furaha sana.
"Najua wasanii pia Marietta, na mimi kwa upande wangu nafikiri ingekuwa ni Sharo Millionea," Draxton akamwambia.
"Oh, maskini! Umenikumbusha mbali sana," Dantu akasema kwa shauku.
Namouih akaachia tabasamu hafifu huku akimtazama Draxton, na marafiki zake wakaanza kuongelea kuhusiana na jinsi msanii huyo alivyokuwa vizuri aana.
"Alikuwa na style nzuri mno. Angekuwa mbali sana kuliko hata huyo ndomo wako!" Marietta
akamwambia Blandina.
"Thubutu! We' si ndiyo wale vibishoo vya bandia aliowaimba ndiyo maana hazipandi fresh," Blandina akasema.
"Na ndiyo maana haukuagi tu. Draxton usipoangalia atakuja kukufanya kuwa henpecked huyu,"
Marietta akasema.
"Kweli eti? Bora tu nimteme mapema kabla haijawa too late," Draxton akaongea kiutani.
"Halafu uende kwa nani?" Blandina akamuuliza.
"Marietta," Draxton akamwambia na kuwafanya wengine wacheke.
"Weee, 'ntamuua," akasema Blandina.
"Ahahahah... atanilinda Draxton. Tunazaa na watoto tunakimbia, unakuja kutukuta Haiti," Marietta
akasema.
"Koma. Drax angalia huyu asije akakupulizia unga," Blandina akasema.
Maongezi yao haya ya kuzoeana yalifanya wachangamke, naye Dantu akauliza, "Una miaka mingapi Draxton?"
Namouih akamwangalia Draxton kwa umakini, akisubiri kusikia jibu lake.
"Ishirini na tano," Draxton akasema.
"Eh! Kumbe? Unaonekana mkubwa!" Dantu akasema.
"Na ni lazima awe na mambo kubwa," Marietta akasema kiutani.
Wote wakacheka kwa pamoja, na Namouih akamsukuma Marietta kidogo begani.
"Ahahah.... Kwa hiyo Draxton, uko tayari kufanya commitment kwa Blanding'a?" Dantu akamuuliza.
Lilikuwa swali ambalo Draxton hakutarajia kabisa, naye akaangalia chini kidogo.
"Halafu nimeshakukataza kuwa unaniita hivyo," Blandina akamwambia Dantu.
"Oh, am sorry Blanding'aaa," Dantu akamtania tena.
"Blandina mali safi bwana, shem hatachelewesha. Draxton wachawi wengi, inabidi umweke huyu ndani mapema kabla hawajamroga kukuacha," Marietta akasema.
Blandina na Dantu wakacheka kidogo, naye Draxton akatabasamu pia. Namouih akamwangalia Draxton na kutambua kwamba tabasamu hilo lilikuwa la kujilazimiaha, naye akagundua kwamba maongezi hayo kuhusu ndoa yalimfanya asijihisi wepesi.
"Drax wazoee tu hawa, wanaongea mno," Blandina akamwambia.
"Yeah, Marietta ana point. We ni mali safi Blandina. Lakini bado nitakimbia naye kwenda Haiti," Draxton akatania.
Wanawake wakacheka, naye Blandina akampiga Draxton begani kidogo.
"Kuna stage tano za uhusiano. Kujuana, urafiki, kupendana, commitment, na ndoa. Mie na Blandina tupo ya tatu, na tutaruhusu muda upite ili kuona kama tunafaana vya kutosha kufika mpaka ya tano," Draxton akasema hivyo na kukiingiza kiganja chake ndani ya kiganja cha Blandina.
Dantu akatabasamu na kusema, "Unaongea vizuri sana."
"Ndiyo, kisomi zaidi. Blandi lazima aringe," Marietta akasema, nao wakacheka pamoja.
Draxton akaendelea kuonyesha ustaarabu wake mzuri, lakini Namouih akiwa ameshaona jinsi hali
hii ilivyomkosesha amani kwa kiasi fulani, akaamua kukatisha mkutano huu kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
"Blandina... mpigie basi nanii... muulize amefika wapi," Namouih akasema.
"Oh, sawa. Babe, ngoja nimpigie huyu. Nakuja," Blandina akamwambia Draxton.
Draxton akatikisa kichwa kukubali, naye Blandina akanyanyuka na kwenda pembeni kuigiza kwamba alikuwa anampigia huyo rafiki mwingine.
Dantu na Marietta wakaendelea kumsemesha Draxton, lakini Namouih akatambua kwamba
umakini wa mwanaume huyu ulikuwa kwa Blandina ingawa hakumwangalia. Si ndiyo akawa
amekumbuka kwamba jamaa anaweza kusikia mbali! Maigizo ya Blandina hayakuwa na faida yoyote kwa kuwa Draxton akamwangalia Namouih kwa ufupi na kuachia tabasamu hafifu, kisha akatazama chini tu. Namouih akaibana midomo yake na kufunika uso kwa kiganja akihisi aibu kiasi, na hakuna yeyote kati ya rafiki zake aliyegundua yaliyoendelea baina ya wawili hawa.
Namouih akawa anajizuia kutoa tabasamu la wazi, naye Draxton akaendelea tu kushiriki maongezi
na rafiki zao.
Blandina akarejea kutoka alipokuwa amesimama, naye akamwambia kwamba rafiki yake huyo amesema kwamba angechelewa sana kwa hiyo wangeweza tu kuondoka sasa. Marafiki zake walikuwa wakidhani kwamba uzushi huo mdogo ulifanikiwa kwa asilimia zote, kwa sababu waliridhika kumwona "shem" na haikuonekana kama alijua walichofanya, ila Namouih alielewa wazi kwamba Draxton alijua. Mwanaume akamwambia Blandina tu sawa, yaani haina shida, kisha
wakawaaga wengine na kuanza kuondoka hatimaye.
Marietta akawa akimsifia sana Draxton, akiwaambia rafiki zake yaani kwa mwanaume mzuri kama huyo ikiwa Blandina angezubaa basi yeye angepita naye. Namouih alitaka hata kumzuia asiongee hivyo kwa kuwa alielewa kwamba Draxton angemsikia, lakini kwa hapo ingekuwa kazi bure maana
Marietta aliendelea tu. Namouih kujua Draxton kutokuwa mtu mwenye makuu wala gubu lolote
kulimfanya atulie tu, na alizidi kupendezwa sana na jinsi mwanaume yule alivyoonyesha usawaziko na kujitahidi kushughulika na hali hii iliyokuwa tata kwake kwa njia nzuri.
★★
Muda ulisonga sana siku hii, na Namouih alikuwa ameachana na Dantu pamoja na Marietta tayari,
ambao walielekea kule walikochukua chumba cha kulipia kwa muda ambao wangekuwa jijini. Blandina na Draxton walikuwa wameachana pia baada ya kufanya mizunguko mingi pamoja, na mwanamke huyo alirudi tena kazini pamoja na Namouih ili kufunga kazi zao zingine. Namouih yeye akawahi kuondoka ikiwa imefika mida ya saa kumi na moja, na Blandina angemalizia muda
uliobaki wa saa moja kwa kuwa kazi zao zilikwisha muda wa saa kumi na mbili; yaani kwa upande wao wa kazi za kisheria.
Namouih hakuwa amekwenda kupumzika nyumbani, bali alikuwa anakwenda pale Draxton
alikopangishwa vyumba. Walikuwa wameshawasiliana kwa ujumbe na kukubaliana kukutana huko ili wazungumze kuhusiana na suala la kifo cha Felix, kwa kuwa Draxton alikuwa amepata mambo fulani katika uchunguzi mdogo aliokuwa ameufanya. Hawakutakiwa kumwambia Blandina kuhusiana na hili kwanza ili wafanye mambo kwa umakini, kwa hiyo rafiki yake hakujua kama anakwenda nyumbani kwa mpenzi wake kwa muda huo.
Akawa amefika nje ya nyumba hiyo, na kwa kupendeza, Draxton tayari alikuwa amesimama nje akionekana kuwa anamsubiri. Namouih akatabasamu tu baada ya kumwona, kisha akashuka kutoka ndani ya gari baada ya kuliegesha. Leo Namouih alikuwa amevaa nguo fulani iliyounganika kama suti ya kike iliyobana na kuishia magotini, nyeupe yenye mistari myekundu na myeusi ya drafti, iliyokuwa imeacha uwazi katikati ya matiti yake na kuyafanya yaonekane kwa juu kiasi, hivyo alikuwa anaonekana kuwa mtamu balaa! Draxton yeye sasa alikuwa amevalia tu T-shirt nyeupe yenye mikono mifupi na kaptura ya kijani, akionekana kuwa makini sana kama vile amemsubiri mwanamke huyo hapo kwa hamu, na Namouih akawa amemfikia karibu.
Draxton akajisawazisha namna alivyokuwa amesimama huku akionekana kuivuta harufu nzuri ya
mwanamke huyo, na Namouih akatabasamu na kupitisha kidole chake kwenye nywele yake
iliyokuwa imedondokea usoni na kuirudisha nyuma kwa njonjo.
"Samahani..." Draxton akasema hivyo, akimaanisha suala la yeye kushindwa kujizuia kuvuta harufu
nzuri ya mwanamke huyu.
Namouih akatabasamu kidogo na kusema, "Usijali. Nimeshazoea."
Draxton akatikisa kichwa kuonyesha uelewa, kisha akamwambia amfuate ili wakaongelee kule ndani. Sehemu hiyo ya nje ilikuwa na watu kadhaa waliowaangalia sana hasa kutokana na Namouih kuonekana kuwa wa matawi na mrembo mno, na wawili hawa wakaelekea ndani huku wazushi wakianza kusema huyo mwanamke "sugar mommy" alikuwa amepelekwa kupigwa miti huko ndani; kama kwa lugha ya waswahili. Namouih akapelekwa mpaka ndani kwake Draxton, ikiwa ndiyo mara ya kwanza kabisa kuingia hapo, na kiukweli alivutiwa na namna palivyopangiliwa vizuri. Akaketi kwenye sofa moja, kisha Draxton akamletea juice ya baridi kwenye glasi na kumwekea mezani.
"Asante," Namouih akasema huku akitabasamu.
"Karibu. Hapa ndiyo mageto," Draxton akasema.
"Ahahahah... mara ya kwanza nimekukuta hapa unakumbuka ilivyokuwa?"
"Ahahah... ulikuwa mkali kweli!"
"Mimi au wewe?"
"Ahahahah... basi wote."
Namouih akatabasamu na kunywa juice kidogo. Alipomwangalia tena Draxton, akaona akiwa kama
ameinamisha uso na kukaza macho yake kwa umakini, halafu akaachia tabasamu la chini kiasi lililofanya Namouih atambue kwamba kuna kitu fulani kilikuwa kinaendelea.
"Vipi Draxton?" Namouih akauliza.
"Naam?"
"Kwa nini una... tabasamu namna hiyo?"
"Aa... hakuna kitu wala... usi..."
"Niambie," Namouih akasema huku naye akitabasamu.
Draxton akaangalia pembeni na kutabasamu tena, kwa njia iliyoonyesha kuna jambo lilikuwa
linamfurahisha sana.
"Niambie basi... nini kinakufurahisha?"
"Ni... majirani... humo ndani. Wanatuongelea," Draxton akamwambia.
"Ahahah... kweli? Unawasikia?"
"Ndiyo."
"Wanasemaje?"
Draxton akatabasamu na kutikisa kichwa chake.
"Tell me," Namouih akamsisitizia huku akitabasamu.
"Wanaongea sana. Wanafikiri mimi na wewe tumekuja ku... you know..."
"Ahahahah... ni Rehema na Salhat eeh?"
"Unawajua?"
"Ahahah... ndiyo. Nimeshakutana nao. Nafahamu wana maneno mengi sana. Wameshawahi kuona umemleta Blandina hapa kwa hiyo lazima waongee tu..."
"Yaani!"
"Ahahahah... piga picha kama Blandina angejua nimekuja huku now, au mara ghafla aje anikute
hapa..."
"Ahah... angeshangaa ila na yeye ndiyo angetakiwa kueleza kwa nini alinidanganya kwamba rafiki yake anamletea mzigo ili tu wenzake wanione..."
Namouih alikuwa anakunywa juice wakati huu, naye akaishusha huku akicheka sana kwa kusikia kauli hiyo.
"Niligundua umetambua kwamba alikuwa anazuga tu, yaani Draxton nilihisi aibu," Namouih akamwambia.
Draxton akacheka kidogo.
"Haikukukera kabisa kwamba alikuzingua namna hiyo?" Namouih akamuuliza.
"La. Nafurahi Blandina akionyesha anajivunia kuwa na mimi. Angalau yeye hafichi mambo mazito kama ilivyo kwangu," Draxton akamwambia.
Namouih akawa anamwangalia kwa uelewa.
"Okay, tuachane na hayo. Back to Felix," Draxton akasema.
"Right."
"So, usiku huo tulikutana pub moja hivi, nilikuwa na Blandina, tukaongea kifupi sana, na... kiukweli nilitambua alitenda kwa njia fulani ya udadisi kwangu mimi ingawa sikujua alikuwa ameanza kunipeleleza. Sikuwa nimeamua kufuatilia vifo vya wasichana waliokuwa wanakufa kila mwezi kwa njia ile ile mpaka jambo hilo lilipompata Agnes. Nilipoenda pale ile siku huyo msichana ameuliwa, ilikuwa ni ili kumsaidia... lakini pia kuona kama ningepata harufu ya mhusika," Draxton akaeleza.
"Harufu?"
"Ndiyo. Uwezo wangu wa kuvuta harufu unaniruhusu kufuatilia ilikoelekea, na nilijaribu kufuatilia ya
mhusika wa mauaji ya Agnes lakini nikashindwa kufikia mwisho wake. Ilikuwa ni kama... ilipotea tu... kitu ambacho siyo cha kawaida. Mwanzoni nilidhani ningepata harufu ya mtu aliyemtoa Agnes kifungoni siku hiyo au yeyote yule regardless lakini... hiyo harufu ili-vanish tu. Ni ngumu sana kujua ni nani kwa njia hiyo tena ikija kwa Felix, na siwezi kupata njia nyingine hasa kwa kuwa mwili wake umeshazikwa," Draxton akamwambia.
"Ulijuaje kwamba harufu ya aliyemuua Felix ndiyo harufu ile ile ya muuaji wa Agnes sasa?"
"Felix alikatwa tumbo akiwa bado na nguo, tofauti na Agnes na wasichana wengine. Kwenye taratibu za kuuhifadhi mwili wake niliweza kuipata harufu hiyo kwenye nguo yake waliyoitupa tu. Nilikuwa nimejitahidi sana kufatilia hii harufu kwa uwezo wote nilionao... lakini na penyewe haikuwa na matokeo mazuri..."
"Ulifanya hayo yote lini?"
"Siku ya kuamkia.... baada ya kifo chake. Nilijaribu kila mara Namouih... nilitaka sana kujua nani alimfanyia vile lakini ikashindikana, na sikutaka wenye mamlaka wanikute nikifanya uchunguzi huo, na maswali na nini... unaelewa...."
"Ndiyo naelewa. Nilikuwa nafikiri hukuwepo msibani na Blandina kwa sababu ulijificha kumbe... inabidi nirudie kukuomba tena samahani kwa kukufanyia nilivyokufanyia siku ile msibani ulipo...."
"Namouih usiwe na hofu, hiyo imeshapita. Unatakiwa ujue kwamba kuna jambo fulani ambalo liko
tofauti kati ya hivi vifo vyote ikilinganishwa na kifo cha Felix," Draxton akamwambia.
Namouih akabaki kumtazama kwa umakini, akiweka usikivu wa hali ya juu.
"Dhumuni la kumuua Felix lilikuwa tofauti na lile kwa wasichana wengine wote kufikia Agnes.
Nimefatilia taarifa za baadhi ya wasichana hao na kugundua kwamba wote wamekufa tarehe 19 ya kila mwezi, hata na Agnes pia. Nachojaribu kusema ni kwamba, kila mara msichana anapouawa kwa njia hiyo, hana nguo, tarehe ni moja kwenye kila mwezi, lengo ni moja. Lakini Felix kafa kwa njia hiyo hiyo, ana nguo, tarehe tofauti,...."
"Lengo tofauti," Namouih akamalizia maneno ya Draxton.
"Ndiyo. Kwa nini lengo liwe tofauti? Ni kwa sababu tofauti, lakini mhusika ni yule yule. Ikiwa tutasema ni kwa sababu Felix alikuwa anapeleleza vifo hivi, hiyo hainge-make sense kwa kuwa
wanaofatilia ni wengi. Kwa nini iwe yeye? Aliyemuua Felix ni yule yule aliyemuua Agnes, lakini kwa Felix ilikuwa ni kwa sababu ya KIBINAFSI, na siyo kwa MPANGILIO kama ilivyo kwa wasichana," Draxton akaeleza.
Namouih akatazama chini na kutikisa kichwa chake kwa uelewa, kisha akasema, "Nilikuwa hata
sijatambua kwamba tarehe ni ile ile ya mwezi kila mara msichana anapouawa namna hiyo. Tarehe 19. Kwa nini tarehe 19?"
"Kwa hapa ni ngumu sana kumpata huyu mtu, maana haachi clue zozote, ni maeneo tofauti-tofauti ya mkoa, na ndiyo sababu maaskari wanashindwa kujua aliko."
"Kwa hiyo unasema kwamba tutatakiwa kusubiria mpaka tarehe 19, msichana mwingine afe, ili
tufatilie kwa ukaribu?"
"Ndiyo inavyoonekana. Wengi hawajatambua kuhusu hili, na sijui tu ni kwa nini lakini wanalichukulia kijuujuu mno. Kila mara likitokea, linakaziwa attention, kidogo tu wanasahau, repeat," Draxton akasema.
"Ni kwa sababu pia lilikuwa limefichwa kwa muda mrefu..."
"Ndiyo. Lakini anayefanya hivi atakuwa anatumia nguvu ya ziada," Draxton akaongea kwa umakini.
"Unamaanisha nini? Kama uchawi?" Namouih akauliza.
"Inawezekana. Lakini nisemeje.... uchawi ulioenda shule," Draxton akamwambia.
Namouih akainamisha uso wake kwa njia ya huzuni.
"Uko sawa?" Draxton akauliza kwa upole.
"Yeah. Ni kwamba tu... nikimfikiria mke wake Felix... Oprah... na watoto wake yaani, nakosa amani every time nikikumbuka kwamba kwa njia kubwa nilisababisha wakampoteza...."
"Usiwe unasema hivyo. Haukumuua wewe. Tu-focus tu kwenye kumpata muuaji wake ili yeye ndiyo aje kuikosa hiyo amani vizuri," Draxton akamwambia.
Namouih akamwangalia na kutikisa kichwa kukubali. "Asante sana Draxton. Unanisaidia sana,"
akamwambia.
"Ingekuwa vizuri kama taarifa za ndani zaidi tungezipata kutoka kwa maaskari, ila...."
"Tutazipata sasa?"
Draxton akatikisa kichwa kwa njia ya kusikitika.
"Ni kama usemavyo, wanachukulia haya mambo kijuujuu tu ndiyo maana sifikirii hata kama tutapata lolote," Namouih akasema.
"Hatuwezi kuwa na uhakika, only time will tell. Acha tu tuwe na subira, huenda isiwe lazima kusubiri mpaka tarehe 19 na tukapata jambo fulani," Draxton akamwambia.
Namouih akatikisa kichwa kukubali.
Wawili hao wakaendelea na maongezi ya hapa na pale kuhusiana na jambo hilo ambalo bado lilikuwa na utata mwingi sana, kwa kuwa haikujulikana kama hata wangeifikia hatamu waliyoihitaji ili maswali mengi yaweze kujibiwa na haki itendeke ipasavyo, lakini matumaini ya kupata ushindi walikuwa nayo, hivyo wangetakiwa kuendelea kusubiri kuona matokeo ya uchunguzi wao kulielekea suala hilo zito....
★★★★
Kwake Efraim Donald. Mume huyu wa mwanasheria mahiri Namouih alifanikiwa kufika kule alikokwenda baada ya kuaga kuondoka kwa ajili ya safari, akiwa ametumia ndege ya kibinafsi. Ilikuwa ni sehemu ambayo angetumia muda wake kukutana na wafanyabiashara wengine wakubwa kwa ajili ya kupanga makubaliano mapya ya kazi zao ili kuongeza ukuzi wa biashara zake. Lakini hii haikuwa sehemu yoyote tu, alikuwa ametoka ndani ya nchi na kwenda nje kabisa,
kule Nairobi, Kenya. Alichukua chumba kwenye hoteli fulani ya kifahari, kisha akawasiliana na mtu
muhimu aliyetaka kuzungumza naye kabla ya kuanza kufanya mikutano hiyo, na alikuwa ni rafiki yake wa karibu zaidi, yaani Mr. Godwin Shigela.
Godwin alifurahi sana baada ya kujua kwamba rafiki yake alikuwa huko pia, naye akamwambia wakutane mahali fulani kulikokuwa na nyumba kubwa za starehe mida ya usiku ili wajumuike na kufurahia maongezi na vinywaji. Efraim Donald alihitaji sana kuzungumza na rafiki yake huyo kwa
sababu kwa kipindi kirefu hawakuonana, na ni yeye hasa kuliko mtu mwingine yeyote ndiyo
angemwelewa vizuri sana kwa mengi aliyotaka kuzungumzia. Hivyo ilipofika mida ya kwenda huko
akachukua gari la muda ambalo alikodi kutumia kwa muda ambao angekuwa huku na kuelekea huko kukutana na rafiki yake.
Alifika na kumkuta Godwin akiwepo tayari, naye akampokea vizuri sana. Mwanaume huyo alikuwa mfupi kiasi kumfikia Efraim Donald begani, mwenye mwili mpana na mikono imara, naye alikuwa mweusi na kichwani alinyoa kipara. Wakati huu alikuwa amevalia nguo za kawaida tu; shati jeupe a mikono mifupi akichomekea ndani ya suruali ya jeans na viatu vyeusi chini. Huu ulikuwa ukumbi wa starehe, kukiwa na watu wengi walioponda raha tu kwa kucheza muziki taratibu, kunywa
vinywaji, na kujiburudisha na wanawake. Godwin akamwongoza Efraim mpaka sehemu maalumu
iliyokuwa na sofa pana jekundu lililozunguka meza nyeusi iliyokuwa na chupa nyingi za vinywaji na glasi kadhaa, naye akaketi psmoja naye hapo.
Kulikuwa na wanawake wanne sehemu hiyo, weusi, warembo, waliovalia vigauni vifupi sana na
kufanya ieleweke wazi kwamba walikuwa ni vyombo vya starehe tu hapo kwa ajili ya pesa, na wawili wakaanza kumshika-shika Efraim kwa njia ya kuamsha hisia za mahaba, lakini mwanaume huyo alionyesha kutopendezwa na jambo hilo hata kidogo. Godwin akamtathmini sana na kutambua kwamba akili ya rafiki yake ilikuwa sehemu nyingine kabisa hata alipojaribu kunwongelesha kwa shauku, hivyo akawaambia warembo hao wawapishe kwanza, nao wakatii na kuondoka.
Godwin akamsogelea Efraim karibu zaidi na kusema, "Vipi kaka? Hao manze hawajakupa entice nzuri tuite wengine?"
Efraim Donald akatabasamu kidogo na kunywa kileo chake.
"Nilikuwa natarajia uje na amsha yako hapa ila umeshaanza kunifanya nihisi usingizi," Godwin akasema.
Efraim Donald akamtazama.
"Mambo yamekaaje?" Godwin akauliza kwa umakini.
Efraim Donald akatikisa kichwa kuonyesha mkazo mwingi, kisha akasema, "Mke wangu Godwin...
mke wangu ameanza kupotea."
"Oh come on bro... umekuja all the way to Nairobi kuanza kuongelea stress za mke wako? Hebu jaribu kuvaa viatu vyangu hapa me nimekuandalia quality time nzuri halafu...."
"Siyo kihivyo, Godwin. Namouih... ameanza kuona vitu ambavyo hatakiwi kuona," Efraim akasema.
Godwin akaweka sura makini zaidi, kisha akasema, "Ina maana bado ndoto zinamsumbua? Ameanza kuona nini?"
"Vitu vingi. Mara vivuli, mara yuko mochwari, mara aone wafu, mara akutane na jitu linalokunywa damu... unaelewa nachomaanisha?"
"Donald acha masihara. Namouih ndiyo alikuwa perfect kabisa. Haiwezekani uwe umebakiza muda
mfupi tu halafu ndiyo aanze kuona haya mambo. Ina maana hata baada ya kumwondoa yule mwanaume bado haikutoa vikwazo vyake?"
"Namouih hakuwa na uhusiano huyo mwanaume Godwin... ndiyo sababu bado aliendelea kusumbuliwa na ndoto mbaya hata nilipomuua," Efraim Donald akasema.
"Kwa hiyo ulimuua kazi bure tu?"
"Nilidhani ni huyo maana nilipomfatilia nilimwona naye hiyo siku... aagh, inakera sana... ikiwa
atatambua kinachoendelea kabla ya mzunguko kukamilika sijui itakuwaje," Efraim akaongea kwa
hasira.
Godwin akamshika begani na kusema, "Calm down. Unatakiwa tu kumfatilia ili ieleweke ana-cheat na nani, halafu ummalize huyo mtu."
"Namouih hani-cheat Godwin. Yaani kila sehemu yuko msafi..."
"Hilo linawezekanaje? Angeweza vipi kuota ndoto mbaya kama hajaanza kuku-cheat?"
"Hii haihusishi ku-cheat kwa kufanya mapenzi. Godwin... kuna mtu inaonekana Namouih amempenda... lakini hata yeye mwenyewe hajajua hilo. Inakuwa ngumu kujua ni nani kwa sababu hiyo ndiyo maana nashindwa kumwondoa..."
"Hupaswi kusema neno kushindwa mbele ya meza yetu. Amka mwanaume! Ongea na roho yako
ikuonyeshe huyo mtu ili umwondoe mapema maana ukijiremba utasababisha kila kitu kiporomoke,
na huo utakuwa ni uzembe wako. Nilikwambia mapema kabisa... sasa now utafanya nini? Ikifikia hatua Namouih akauona uso wako kwenye hizo ndoto je?"
Efraim Donald akamwangalia kwa hisia kali na kusema, "Sitaruhusu hilo litokee. Nimemuua Felix lakini haijasaidia lolote, ndiyo maana natakiwa kuwa mwangalifu sana ili nisikosee next time. Namouih ameshaongea mpaka kuhusu kutaka kutoka nje ya ndoa na talaka kwa sababu simpi haki yake, na hiyo ni moja kati ya mambo yanayochangia hili tatizo. Kama amempenda mtu fulani bila yeye mwenyewe kujua hiyo inamaanisha nitapaswa kutulia kusikilizia hali, maana mzunguko hauko mbali kuisha... nimebakiza msichana mmoja tu wa kuua... yaani mpaka nahisi hasira kaka... why now? Wakati niko karibu sana? Agh..."
"Kaka, fanya ukweli. Hakikisha hilo tatizo linaondoka upesi. Najua ni jinsi gani unataka sana kumla yule mwanamke heheheh..." Godwin akasema huku akicheka.
"Yaani! Huwezi amini kaka... Namouih ni mwanamke mmoja nayeweza kusema ni mtamu sana
ingawa bado sijamuonja, ndiyo maana nataka kuhakikisha haya yanaisha kabla sijampoteza..."
"Usiwaze kumpoteza. Kila kitu kitakwenda sawa, cha muhimu ni kuendelea kutokosea mahesabu. Na usipuuzie ushauri wangu... mwombe Subiani msaada... atakusaidia kujua nani ameuteka moyo wa mke wako ili...."
"Godwin, sitakiwi kufanya hivyo. Task ya kuondoa tatizo ni yangu, nikijipeleka mbele yake nitaombwa malipo zaidi, kitu ambacho ni ngumu wakati unajua nina mzigo mkubwa kukamilisha kabla ya.... yaani... I don't know," Efraim akaongea kwa mkazo na kupiga fundo mbili za haraka.
"Kaza moyo mwanaume. Hata mimi nilipita pagumu sana, lakini si unaniona sasa hivi nilipo? Hapo ulipo kwa sasa yaani bado sana... utajiri juu yako ni mwingi mno ukikamilisha hili zoezi. Njia uliyochagua ni ngumu mno, lakini hakuna kurudi nyuma sasa. Komaa. Hakikisha hilo tatizo
linaondoka. Mwangalie mke wako kwa makini, macho yake tu yatakuonyesha ni nani anayemwangalia zaidi ili umnase," Godwin akasema.
"Sawa. Nitalifanyia kazi ipasavyo. Ila... kuna jambo fulani yaani linanipa raha sana kila nikifikiria... ni raha fulani hivi nataka niipitie kwanza kabla ya kuendelea na haya yote... inaonekana kuwa tamu mno... Subiani ataipenda sana," akasema Efraim na kuanza kutabasamu.
"Hautaniambia ni raha gani hiyo?" Godwin akauliza.
"Nitakuja kukuonyesha tu. Bonge moja la show nataka kufanya... hahahahah..." Efraim Donald akaongea huku akinywa.
Wanaume hawa wakacheka kwa pamoja na kuongeza vinywaji ili waendelee na maongezi yao.
Mambo hayo! Hapa ndiyo msemo wa usilolijua ni sawa na usiku wa giza utafaa kutumika kwa asilimia zote. Katika mzunguko mkubwa wa mambo mengi mabaya, sikuzote msababishi hutokea pale pale ambapo wengine hupaona kuwa pazuri sana, na katika kisa hiki chote, ni mwanaume huyu ndiye aliyekuwa msababishi wa hayo yote. Efraim Donald hakuwa namna alivyoonekana kwa nje tokea mwanzo alipoingia kwenye maisha ya mwanadada Namouih. Huyu alikuwa ni mtu mbaya sana mwenye kila aina ya sifa kuitwa mkatili wa hali ya juu, na alificha mambo mengi ya kikatili kwa msaada wa roho mwovu na mkubwa sana, mwenye nguvu nyingi, ambaye kwa wengi
hufahamika kama JINI SUBIANI. Ilikuwaje mpaka maisha ya mwanaume huyo mwenye nyuso mbili yakawa namna hiyo? Na lengo lake kumwelekea Namouih lilikuwa nini?
★★★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★★★
Huo ndiyo mwisho wa msimu wa kwanza wa hadithi hii ya CHANGE. Sehemu za mwendelezo wa hadithi hii kali zitaanzisha msimu wa pili. Ni story nzuri na ndefu sana. Waweza ipata nakala yote kwa gharama nafuu sana. Karibu WhatsApp au kwa E-mail yangu.
WhatsApp no: +255 678 017 280
e-mail:
eltontonny72@gmail.com