Follow along with the video below to see how to install our site as a web app on your home screen.
Note: This feature may not be available in some browsers.
Kabisa. Ila wapo zaidi yakeMkuu Elton Tonny, asante kwa simulizi yenye mafunzo na burudani ndani yake. 😄
Huyu Efraim Donald naona na yeye alijiona ni mungu kwenye dunia yake 😂😂😂
Shukran!CHANGE
Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA AROBAINI NA SITA
★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Mwanaume ndiyo alikuwa amefika! Ikiwa Efraim Donald alidhani kwamba angeweza kukaa sehemu hiyo ya mbali kwa kujiachia na asipatikane kwa Draxton, basi sasa ndiyo alikuwa ametambua kwamba alikosea sana. Kuzima simu na kuzitupa na hata kuwaleta wanawake hawa sehemu hiyo kusingemzuia Draxton kuwafuata, kwa sababu hakuna kitu kilichokuwa na uvutano mkubwa sana kwa Draxton kutoka kwa Namouih kama harufu yake. Yaani hata kama wangekwenda nje ya jiji, Draxton angempata tu mwanamke huyo kwa kufatilia harufu yake.
Alipotoka pale nyumbani kwa Blandina, mwanaume huyu alikwenda mpaka kwenye nyumba ya Efraim Donald na kuingia kule ndani, na ndiyo alikuta mauaji ya yule mlinzi wa pale; Alfani. Akatumia uwezo wake vizuri na kuitafuta harufu ya Namouih mpaka alipofanikiwa kuifikia sehemu hiyo ambayo Efraim alikuwa amemfungia. Yaani kutokea pale nyumbani kwake Efraim Donald, Draxton hakutumia gari lake tena bali miguu tu, akikimbia na kutembea kwa zaidi ya masaa mawili. Alipokuwa ameifikia nyumba hiyo ambayo Efraim aliwashikilia wanawake hao, alikutana na wale wanaume wengine wawili waliotoka kumdhibiti, naye akawavunja-vunja viungo vyao na kuwaacha wanakimbizana na uhai ardhini, na ndipo akawa ameingia ndani ya nyumba hiyo kwa kishindo kikubwa.
Baada ya kuwapiga wanaume wale pamoja na Efraim Donald, Draxton akashuka chini bila kukawia na kukiokota kisu, kisha akajichana kuanzia sehemu ya kati ya mkono wake wa kushoto mpaka usawa wa kiganja chake, halafu akauweka mkono huo usawa wa tumbo la Sasha na kuiinua shingo ya mtoto juu kidogo kumwelekea usoni, akikitoa kitambaa kilichouziba mdomo wa binti kwa kutumia meno. Efraim Donald akajivuta taratibu akiwa amehisi maumivu mwilini kutokana na kuupiga chini kwa nguvu, naye akaangalia sehemu hiyo aliyokuwepo adui yake mkuu na kuona kwamba kisado chenye damu ya Sasha kilikuwa kimeangukia pembeni, na damu yote ya binti ilimwagika kabisa. Aliingiwa na hasira kali sana, naye akaanza kusema maneno yake ya kuzimu-kuzimu ili mwili wake uingiwe na nguvu za giza.
Draxton alihakikisha analinywesha tumbo la Sasha damu yake nyingi sana, na binti bado alikuwa anahangaika mno hasa kwenye kuisaka pumzi yake. Wale wanaume wawili wa Efraim wakajinyanyua pia na kuanza kumfata, mmoja akiwa amefanikiwa kuvuta sululu iliyokuwa ukutani, kisha wakamkaribia na kumrukia kwa nguvu. Draxton tayari alikuwa amewaona walipomkaribia, naye akakiweka kichwa cha Sasha chini na kugeuka ili awadhibiti. Alikuwa amegeuka tu na kuukamata mkono wa mwanaume mmoja na kuuvunja, naye akaigeuza nguvu ya yule aliyeshika sululu impige mwenziye kifuani mpaka kukipasua, kisha akaikamata shingo yake na kuinyonga kwa nguvu. Akawasukuma wanaume hao pembeni na kukiokota kisu tena, halafu akamfata Zakia na kuzikata kamba zilizomfunga. Alikuwa anafanya mambo mengi kwa uharaka mno, naye akampa Zakia hicho kisu na kumwambia akamfungue Namouih upesi, na Zakia akamfata binti yake.
Hisia za Draxton tayari zilikuwa zimetahadharika kwamba kuna hatari iliyokuwa nyuma yake, naye akageuka na kukuta Efraim Donald akiwa ameshasimama huku akimwangalia kwa njia ya kikatili. Macho yake sasa yalikuwa mekundu yenye kutisha sana, na hata wakati Zakia alipoanza kuzikata gundi zile zilizofunika mwili wa Namouih aliweza kuyaona macho hayo na kutoa ishara ya msalaba kwa hofu. Namouih pia aliyatazama macho ya Efraim kwa woga, akiwa ameshaelewa kwamba nguvu za giza zilikuwa zimemwingia mwanaume huyo, naye Draxton akamtazama kwa ujasiri. Bado alikuwa na mwonekano wa kawaida tu huku nywele zake zikiwa ndefu vilevile.
"Umejileta kwenye kifo chako mwenyewe. Nitakuua kwa njia mbaya sana," Efraim akasema hivyo kwa sauti nzito yenye kutisha sana.
"Nimeshakufa mara nyingi... kwa njia nyingi. Ngoja tuone kama ya kwako itanifanya nisinyanyuke tena," Draxton akasema bila hofu.
"Unacheza na sisi wewe mwanadamu?" sauti nzito sana ya Efraim akamuuliza.
"La. Ni wewe ndiyo umecheza na mimi," Draxton akasema kwa ujasiri.
Efraim Donald akatoka kwa kasi pale aliposimama na kumpamia Draxton kwa nguvu sana, lakini Draxton alikuwa ameiwahi nguvu ya mwanaume huyo na kumgeuzia yeye upande wa pili hivyo wote wakaelekea ukutani na kuugonga kwa kishindo kilichofanya sehemu hiyo itikisike. Efraim akanyanyuka na kumwahi Draxton, akamkandamiza ukutani hapo kwa nguvu sana, na Draxton akawa anashindwa kujitoa maana nguvu za Efraim zilikuwa nyingi kupitiliza. Tayari Namouih alikuwa amefunguliwa na mama yake, kisha wote wakaenda pale ambapo Sasha alikuwa amelala huku bado mwili wa Namouih ukiwa na maumivu. Binti alikuwa amefumba macho sasa, lakini Namouih alitambua kuwa bado uhai ulikuwemo ndani yake. Akamwambia Zakia amsaidie ili wambebe binti na kumtoa nje upesi, na kwa hofu ya kilichokuwa kinaendelea baina ya Efraim na Draxton, Zakia akabaki kuzubaa tu.
Muda huo huo Efraim akawa amemvuta Draxton kwa nguvu na kumrusha hewani, na mwili wa mwanaume huyo ukaenda kudondokea pale ambapo kulikuwa na kiti alichoketishwa Namouih na chote kikavunjika. Zakia akawa amedondoka chini huku akimwangalia Efraim kwa hofu kubwa, na mwanaume huyo akaanza kumfata mama ya mke wake akiwa na lengo la kwenda kummaliza. Zakia alimwangalia kwa hofu sana, naye Namouih akasogea pale mama yake alipokuwa na kumkinga ili Efraim asimuumize, na ndipo Efraim Donald akasikia sauti ya muungurumo wa chini kutoka pale alipoangukia Draxton. Akatazama hapo na kumwona Draxton akisimama, huku sasa ngozi ya mwili wake ikiwa nyeupe na macho yake kugeuka na kuwa ya blue, naye Efraim akatabasamu.
Draxton akatoka hapo alipokuwa na kumfata Efraim kwa kasi sana, kisha wawili hawa wakaanza kupigana kwa njia zenye kutiana maumivu mengi. Makucha ya Draxton yalimuumiza sana Efraim, na hata mapigo ya Efraim kwa Draxton yalimtia maumivu mnyama huyo kutokana na Efraim kuwa ya nguvu zisizo za kawaida. Namouih akaitumia nafasi hiyo kumsihi mama yake wamwondoe Sasha sehemu hiyo haraka, naye Zakia akajitahidi kuondoa bumbuazi lake na kwenda kumbeba binti yake pamoja na Namouih. Alishangaa kiasi baada kukuta tumbo la Sasha likiwa limejiunga tena, kana kwamba halikuwa limekatwa kwa kisu kabisa, naye akamtazama Namouih kimaswali na binti yake akasema angeelezea baadaye.
Wakambeba Sasha na kuanza kuondoka naye, huku Namouih akiona wazi namna ambavyo Draxton alikuwa anamshinda nguvu Efraim kwa mapigo yake ya hasira, na ndipo Efraim Donald akawa ameangushwa chini na kuwaona wanawake hao wakiondoka. Kufikia hapo Mnyama-Draxton alikuwa amempatia kipondo bila kujali ana jini wala nini, na ndipo Efraim akaamua kuongeza nguvu yake ili aondokane na kero ya mwanaume huyo. Akaanza kuongea maneno mengine ya kishetani huku akitokwa na damu nyingi mwilini mwake, na yalikuwa ni maneno ya kumruhusu roho huyo mwovu aliyeishi ndani yake auvae kabisa mwili huo. Akaanza kujipinda-pinda kwa nguvu huku mwili wake ukianza kukua sana, naye akawa anatoa sauti za kukwaruza sana.
Mnyama-Draxton akaendelea kumwangalia kwa tahadhari kuu, akiona namna ambavyo mwili huo ulirefuka sana, ngozi ikigeuka na kuwa kama imechanika-chanika na nyeusi sana, na mikono na miguu yake Efraim ikirefusha makucha yake kwa kiwango cha hali ya juu. Kichwa chake kikachukua umbo la kichwa cha nyoka mkubwa, naye akaanza kukipeleka huku na huku kama vile anamwinda Draxton, na ulimi wake mrefu katikati ya meno mengi makali na marefu ukitoka mara kwa mara kama nyoka afanyavyo. Alitisha! Umbo hili la sehemu ya roho ya jini aliyeishi ndani yake lilikuwa hususani kwa matumizi ya kunywa damu za kafara za wasichana aliowatoa, lakini sasa Efraim Donald alikuwa ameamua kulitoa ili limfundishe Draxton adabu na kuwaua wanawake wale bila kukonyeza; hasa Sasha, ambaye bado alikuwa na umuhimu wake hapo.
Wakati huu tayari Namouih na Zakia walikuwa wamemtoa Sasha ndani ya jengo hilo na kuanza kumpeleka upande ambao gari la Efraim lilikuwa limeegeshwa, mwanamke huyu akiombea wakute funguo mule ndani ili waweze kumwahisha Sasha hospitali, na ndipo Zakia akawa ameukwaa mguu wake kwenye jiwe gumu chini baada ya kuzubaa kuitazama miili ya wale wanaume wengine wawili waliokuwa wameshakufa hapo nje, na hilo likasababisha wadondoke kwa pamoja. Zakia alikuwa ameutegua mguu wake vibaya, naye akawa anatoa miguno ya maumivu, hivyo Namouih akamsogelea na kuanza kujitahidi kumtuliza. Ni wakati huo ndipo mvua ikaanza kunyesha.
Kule ndani, Draxton alikuwa na kibarua haswa. Alijitahidi kupigana na kiumbe kile kwa njia zake zote lakini ilikuwa kugonga mwamba tu. Jini la Efraim Donald lilikuwa na nguvu sana, na kwa sekunde hizo chache lilikuwa ni kama linausoma tu mchezo wa mwana-mnyama huyo, kisha likamkamata na kuanza kukikandamiza kichwa chake kwa pande zake za pembeni, kama linataka kukipasua. Draxton alijitahidi sana kumtandika na kumkwarua kwa makucha yake, lakini akamalizwa nguvu baada ya kiumbe huyo kukipasua kichwa chake kama puto lililojazwa maji! Alimbakiza akiwa na kiwiliwili tu kutokea shingoni, na mikono ya Draxton ikalegea kabisa kuonyesha alikuwa mbali na uhai; kwa mtazamo wa haraka!
Efraim aliyepagawa na jini akaurusha mwili wa Draxton pembeni, kisha upesi akaanza kuelekea nje akiwa anajivuta-vuta utadhani ameumia vile. Huko nje mvua iliendelea kunyesha, na Namouih alikuwa anajitahidi kumsihi mama yake ajikaze ili wasaidizane kumtoa mtoto hapo lakini Zakia akawa anasema asingeweza. Ndipo Namouih akasikia sauti nzito ya Efraim ikiita jina lake, naye akaingiwa na hofu baada ya kutazama huko na kuona jitu lile likija upande wake. Alichoka! Hakuwahi kutazamia angekuja kuona kitu kilichotisha namna hiyo, na kwa kuangalia hali ya mama na mdogo wake alielewa hakukuwa na njia ya kukiepuka kifo kutoka kwa kiumbe hicho hatari. Hivi ni nani aliyemshinikiza mpaka akaingia kwenye ndoa na mwanaume huyo ambaye hakufaa hata kidogo kuitwa mtu?
Zakia akageuka na kuona zari lililokuwa linakuja, naye akapiga kelele kwa kuogopa sana na kujitahidi kunyanyuka baada ya nguvu mpya kumwingia. Namouih akamfata Sasha pale chini na kujitahidi kumwinua, kisha akambeba mikononi mwake akiwa anashindwa kumweka vizuri sana mikononi kutokana na uzito na utelezi, lakini akaanza kujikongoja pamoja naye ili walifikie gari. Ilikuwa ni kidogo tu walifikie gari hilo na hapo hapo jitu lile likatua juu yake na kulikandamiza gari hilo mpaka likabonyea na kupasuka-pasuka vioo, na wanawake hao wakadondoka huku wakilia kwa hofu.
Jitu hilo likawageukia na kuanza kuwafata, wanawake wakijirudi nyuma, na lilipofika usawa wa mwili wa Sasha, likasimama na kuuangalia. Namouih akaingiwa na hofu zaidi ya kutotaka kuona mdogo wake anaumizwa, naye akasogea hapo ambapo mwili wa Sasha ulikuwa na kuulalia. Alikuwa tayari kujitoa afe badala ya mdogo wake, ikiwa hilo lingemaanisha chochote, na jambo hilo lilimgusa sana Zakia kiasi kwamba hata yeye akajisogeza hapo na kulala kwa kuwakumbatia binti zake. Kama huu ndiyo uliokuwa mwisho, basi wangeufikia kwa pamoja. Efraim Donald akiwa amejawa na roho mbaya sana ya jini hilo, akawa anawaangalia tu kama mtu anayetathmini chakula chake kitamu kabla ya kuanza makamuzi, kisha akaachia sauti ya kukwaruza kama nyoka na kunyanyua limkono lake lenye makucha marefu mno ili akishushe kifo hapo chini, na ndipo wanawake hawa wakasikia sauti nzito ya vishindo na upepo mkali ukiwapuliza walipokuwa chini hapo.
Namouih alikuwa wa kwanza kunyanyua macho yake juu na kuona jitu lile likiwa limerushwa mbali nao kiasi, na kitu kama ngome au nguzo nzito ya simenti ya kushikilia nyumba ikiwa imeangukia pembeni ya jitu hilo kuashiria kwamba lilikuwa limepondwa nayo, naye akageuka nyuma na kutazama kwenye ile nyumba. Juu kabisa ya ghorofa, aliweza kuona umbo la kitu kikubwa chenye mwili, lakini kwa sababu ya ukungu wa mvua hakuweza kukiona kwa usahihi, na ndipo kitu hicho kikajifyatua kutoka huko na kuja kutua mbele yake na mama yake kwa kishindo kikubwa sana! Lilikuwa umbo la mnyama mkubwa sana, na taratibu likaanza kusimama vizuri zaidi, miguu ikiwa minne na mikubwa sana, manyoya mengi meupe yaliyolazwa kwa maji ya mvua iliyokuwa ikinyesha, na muungurumo wa chini uliosikika kutoka kwa kiumbe hicho. Jitu lile lililouvaa mwili wa Efraim Donald likasimama na kumwangalia vizuri zaidi mnyama huyo mbele yake, na mnyama huyo mwenye kufanana na mbwa mwitu mkubwa sana akapiga hatua chache mbele na kutoa sauti nzito ya kuunguruma!
Ilikuwa ni kama vile anampa kitisho Efraim mwenye jini, au challenge, na tayari Namouih alielewa kwamba huyo alikuwa ni Draxton wa badiliko la mwisho. Zakia alihisi ni kama miguu yake yote imeishiwa nguvu, yaani kila kitu alichokuwa anaona kilimwogopesha kupita maelezo. Jitu la Efraim Donald likaingiwa na hasira zaidi, nalo likaanza kumfata mnyama huyo. Huyo mnyama hakuwa Draxton tena, alikuwa kiumbe mwingine kabisa. Akatoka kwa kasi pia na kumfata Efraim kwa hasira, na pambano la viumbe wawili wenye kuogopesha sana likaanza. Walipigana kwa uzito sana, hakuna huruma hata kidogo, na ilikuwa inamshangaza kiumbe wa Efraim kwamba alimtia majeraha makubwa sana Mnyama-Draxton ila bado alikuwa akiendelea kumsumbua sana. Yaani hata angemchoma kwa makucha yake marefu mpaka kuyatokeza upande mwingine wa mwili lakini sehemu hiyo ingejirudishia upya tena kwa njia fulani kama inajiponya.
Namouih na Zakia walibaki kuangalia mambo hayo kana kwamba walikuwa wapenzi watazamaji wa kipindi maalumu cha mapigano. Viumbe vile vilipigana haswa na kuelekea sehemu za mbele zaidi za eneo hilo mpaka kutokomea kutoka kwenye macho ya wanawake hao.
Efraim Donald, akiwa amepagawa na jini lake, alihisi kuchoka sana, na hii ilikuwa ni ajabu kwa kuwa hakudhani kuna kiumbe ambacho kingeweza kushindana na nguvu aliyokuwa nayo kwa kiwango hiki alichokiona kwa Draxton. Ikafika hatua akawa ameangushwa kwa nguvu sana usawa wa mti mkubwa na kukaribia kuuvunja, na mnyama wa Draxton akawa amemkaribia zaidi huku akimwangalia kikatili. Efraim alikuwa ameshaishiwa nguvu, naye akabaki kupumua kwa uzito tu akiwa amekubali sasa kwamba kulikuwa na nguvu zaidi ya zile alizoziona kuwa kubwa zaidi, na ingawa hakujua ya Draxton ilitokana na nini, alijua sasa kwamba kiumbe huyo alistahili kupewa heshima.
Akiwa bado ndani ya umbo lake baya la kutisha, kichwa chake kikaanza kurudia hali ya kawaida na kuwa kichwa cha mwanadamu, kisha akasema, "Ulikuwa sahihi kumtabiria mwargentina... kwa hiyo nadhani tokea mwanzo ushindi ulikuwa ni wako. Maliza ulichokianza... lakini usisahau kwamba bado kuna vitu vitakuja tu.... mwanadamu."
Hayo yalikuwa maneno yaliyobeba onyo fulani zito, katika maana ambayo aliijua yeye mwenyewe. Mnyama wa Draxton akaunguruma kwa sauti ya chini, akionekana kukwanguka sehemu za usoni, kisha akapanua kinywa chake na kuikamata sehemu ya kati ya shingo ya jitu la Efraim na kuinyofoa yote! Huo ndiyo ukawa mwisho wa maisha batili ya mwanaume huyo!
Mvua iliendelea kushuka, na wakati huu haikuwa kubwa kama namna ambavyo ilikuwa imeanza. Namouih na Zakia bado walikuwa wamekaa chini pale karibu na mwili wa Sasha, wakihisi baridi mwilini. Walikuwa wameshindwa hata kunyanyuka na kubaki wameshikana viganja vyao tu kama vile wanasubiri hatma yao ya mwisho ndani ya mkasa huo, na ndipo kutokea kule kwenye miti wakaanza kumwona mnyama huyo mkubwa akitembea kuuelekea upande wao taratibu huku akiunguruma kwa sauti ya chini. Zakia alikikaza zaidi kiganja cha binti yake huku akiwa ameingiwa na hofu kubwa zaidi, akielewa huo ndiyo ulikuwa mwisho wao, lakini Namouih akawa anamwangalia mnyama huyo kwa hisia sana. Alielewa kurudi kwa mnyama wa Draxton kulimaanisha kwamba alikuwa amemmaliza Efraim, naye akaanza kutokwa na machozi ambayo hayangeweza kuonekana mvuani hapo.
Akakiachia kiganja cha mama yake na kuanza kujitahidi kunyanyuka, huku Zakia akimtazama kwa wasiwasi, kisha mwanamke huyo akaanza kutembea kimaumivu kuelekea upande ambao mnyama huyo alikuwa anatokea. Zakia aliingiwa na taharuki zaidi, akihisi ni kama binti yake alikuwa anakwenda kujihalalishia mwisho wake mapema, lakini Namouih alikuwa anakwenda kwa mnyama huyo akiamini jambo lingine tofauti kabisa ndani ya moyo wake. Ni jambo ambalo alikuwa ameshalitafakari kwa kina tokea alipomwona mnyama huyo kwa mara ya kwanza kabisa, na aliamini hilo ndiyo sababu iliyofanya asimuumize usiku huo alipomlazimu Draxton abadilike.
Alipokuja kuamka siku iliyofuata na kumuuliza Draxton kwa nini mnyama wake hakumdhuru ingawa alisema inakuwa si yeye akibadilika, mwanzoni mwanaume huyo hakuwa na jibu, lakini baadaye akaweka wazi kuwa upande wake wa pili ulivutiwa na Namouih kwa sababu ulimpenda kwa njia kama ile ya mama yake mzazi. Jambo hili lilipelekea Namouih kuamini kwamba mnyama huyo hangemdhuru kabisa, kwa kuwa hata usiku ule mnyama huyo angeweza kumdhuru lakini hakufanya hivyo, tena inawezekana alilala pembeni kabisa ya mwanamke huyu alipopoteza fahamu; ikimaanisha alikuwa anamlinda. Hata na wakati huu, alikuwa amemlinda kutokana na ukatili wa mume wake, kwa hiyo alitaka kuonyesha kwamba hakumwogopa kwa sababu ya kuwa mnyama, bali alimthamini kwa namna yoyote ile aliyokuwa.
Namouih akawa amefika karibu na mnyama huyo kisha kusimama, na kiumbe huyo mkubwa akawa amezisitisha hatua zake mbele ya mwanamke huyo huku akimwangalia kwa njia ya ukali wa kinyama. Namouih hakuogopa, bali alikuwa ametawaliwa na hisia nyingi sana za shukrani kuwahi kukutana na mtu, au mnyama kama huyo kwenye maisha yake. Mnyama huyu mkubwa akatoa muungurumo wa chini huku akionyesha meno yake makali. Namouih akatabasamu kwa hisia tu, halafu akanyanyua kiganja chake na kukigusisha chini kwenye manyoya ya kinywa kipana cha mnyama huyo, akijihisi kama yuko ndani ya tamthilia fulani yenye matukio yasiyokuwa halisi hata kidogo, na yeye akiwa ndiyo mhusika mkuu. Zakia alikuwa anatazama jambo hilo kwa umakini sana, naye akaona jinsi ambavyo mnyama huyo mkali mwenye kutisha alikuwa amegeuka kuwa kama mnyama wa kufugwa mbele za binti yake. Kweli akatambua maisha ya Namouih yalikuwa na mambo mengi sana!
Namouih akaendelea kuyachezea manyoya yenye utelezi ya kiumbe huyo, na mnyama mwenyewe akashusha kichwa chake kumwelekea Namouih na kukiweka juu ya paji la uso la mwanamke huyo! Ilikuwa ni wakati uliomsisimua sana Namouih. Alifumba macho yake huku sasa akikishika kichwa cha mnyama wake kwa mikono yake yote, akiendelea kuyachezea manyoya yake kwa upendo. Ilionekana kama vile mambo mengi sana yaliyotokea yalipatwa na suluhu au tamati ya haraka na rahisi sana, lakini siyo jinsi mambo yalivyokuwa. Walikuwa wamepitia mambo mengi pamoja, na ilimfariji sana Namouih kujua kwamba alipendwa sana hata na upande huo mkali wa mwanaume aliyekuwa ndani yake.
Akafumbua macho yake na kugeukia pale mama yake alipokuwa amekaa, naye akampa tabasamu la faraja kumhakikishia kwamba sasa mambo yalikuwa sawa.....
★★★★
Sasha anafumbua macho yake taratibu na kujikuta amelazwa kwenye kitanda ndani ya chumba asichokitambua. Anashtuka kiasi na kujigusa tumboni, akiwa amekumbuka kitendo ambacho Efraim Donald alikuwa amemfanyia mara ya mwisho kabisa alipokuwa na ufahamu wake. Lakini hahisi maumivu ya aina yoyote tumboni, naye anapojitazama kwa umakini anatambua kwamba sehemu aliyopo ni hospitali kutokana na mkono wake kuwekewa mrija maalumu wa kuingiza virutubishi fulani mwilini. Anapoangalia upande wake wa kushoto, anamwona mama yake, Zakia, akiwa amelala kwenye sofa humo humo ndani ya chumba, naye Sasha anaanza kujiuliza ilikuwa vipi mpaka wakafika sehemu hiyo iihali wangetakiwa kuwa wamekufa.
Binti akiwa bado anajishangaa, mlango wa kuingilia ndani humo ukafunguka, na hapo akamwona dada yake mrembo akiingia taratibu. Sasha alihisi furaha tele moyoni kumwona Namouih akiwa mzima, naye akaanza kupumua kwa njia iliyoonyesha msisimko mwingi. Namouih alikuwa ndiyo ameingia tu bila kutambua kwamba tayari mdogo wake alikuwa ameamka, akiwa amebeba mifuko yenye vifaa fulani, na ndipo akatazama hapo kitandani na kuona Sasha yuko macho. Aliiachia mifuko hiyo na kuweka viganja vyake mdomoni kwa kuhisi furaha sana, naye akatembea upesi kuelekea kitanda na kumfikia mdogo wake, kisha akakikumbatia kichwa chake huku akicheka na kulia kwa wakati huo huo.
Zakia akawa ameamka pia na kukuta binti zake wakiwa wameshikana kwa upendo, naye akaingiwa na furaha na kunyanyuka ili akajiunge nao hapo. Wanawake hawa watatu wakakumbatiana pamoja, huku Sasha akilia sana, naye Namouih akamwachia na kuanza kumfuta machozi kwa upendo.
"Shh... usilie mdogo wangu... kila kitu kiko sawa..." Namouih akasema kwa kubembeleza.
Sasha alikuwa hsamini kama kweli bado yuko hai.
"Sasha... unajisikiaje mama? Mwili... unahisi chochote kile?" Zakia akamuuliza kwa kujali.
Sasha akamwangalia mama yake na kusema, "Nasikia njaa."
Namouih na Zakia wakacheka kidogo, na mama yake akasema angekwenda nje kuchukua chakula kitamu kwa ajili yake. Hii ilikuwa ni asubuhi, na Zakia alijua kwamba binti yake huyo alipenda sana supu ya nyama ya ng'ombe, kwa hiyo kwenye manunuzi hicho ndiyo kingekuwa cha kwanza. Akatoka ndani hapo na kuwaacha binti zake wakiwa wameshikana viganja.
"Leo siku gani?" Sasha akamuuliza dada yake.
"Jumatano," Namouih akamjibu huku anazilaza-laza nywele za mdogo wake.
"Nimelala kwa muda mrefu?"
"Wiki tu," Namouih akasema.
"Dada... nini kilitokea? Nakumbuka.... alinikata tumboni...."
"Sasha nakuomba usikumbukie hayo tena, umenisikia? Kuanzia sasa iwe kama hayakuwahi tokea... sahau kabisa, kwa sababu yameisha," Namouih akamwambia.
"Ilikuwaje?" Sasha akauliza.
"Sasha tafadhali..."
"Niambie tu dada. Nini kilitokea? Mume wako yuko wapi?" Sasha akasisitiza.
Namouih akashusha pumzi na kutazama chini, kisha akasema, "Efraim amekufa."
Sasha akabaki kumtazama tu usoni.
"Hayupo tena. Hatatusumbua tena. Na ndiyo maana nakusihi usahau yote kuhusu huyo mwanaume," Namouih akasema kwa upole.
"Nani alimuua?" Sasha akauliza.
"Max... namaanisha... Draxton," Namouih akamwambia.
Sasha akaangalia pembeni, akionekana kutatizika sana akilini.
"Ni mambo mengi yametokea mdogo wangu... lakini kwa sasa yamepita kabisa. Usiogope chochote tena, sawa? Mimi na mama bado tuko pamoja nawe, na hatutaachana hata hali ziweje, umenisikia? Achana kabisa na mawazo ya hayo mambo. Kuanzia sasa tuangalie kile kilicho mbele ya safari zetu... ndiyo kinachojalisha zaidi, umeelewa?" Namouih akasema kwa upole.
Sasha akatikisa kichwa kuonyesha kwamba ameelewa. "Wamenifanyaje hawa waganga? Yaani... sisikii maumivu tumboni wakati nili.... au wamenifanyia upasuaji?" binti akauliza.
"Hapana. Ni Draxton ndiyo alikusaidia kabla hatujaja hospitali. Hapa walichokuwa wakifanya ni kukuongezea damu na kukutunza... sasa hivi uko sawa," Namouih akasema.
"Draxton alifanya nini mpaka utumbo wangu ukaunganika?" Sasha akauliza.
"Ni... ni vitu vingi, nitakuja kukuelezea. Usiwe na hofu," Namouih akamtuliza.
Sasha akamwangalia dada yake kwa hisia, kisha akasema, "Dada... naomba sana unisamehe. Nimekukosea sana."
"Hapana Sasha, haujanikosea..."
"Nimekukosea dada. Hata kama nilikuwa chini ya mkazo, sikupaswa kusema... au kufanya niliyofanya. Ninahisi aibu sana dada kwa kukutendea vibaya namna ile naomba sana unisamehe..." Sasha akaongea kwa huzuni.
Namouih akamwonea huruma sana, naye akaanza kumfuta machozi huku akisema, "Msamaha wangu hautajalisha ikiwa nami pia sitakuomba unisamehe. Nimefanya makosa pia, na nilikutendea kwa njia mbaya Sasha. Nakuomba pia unisamehe... na mimi ndiyo nitakusamehe."
Sasha akacheka kwa hisia huku bado akidondosha machozi, naye akavikaza viganja vya dada yake akijihisi vizuri sana moyoni. "Asante sana dada... kwa yote. Efraim alikuwa ameivuruga akili yangu, yaani haikuwa mimi kabisa. Nakuahidi dada nitakuwa mpya kuanzia sasa. Nitafanya yote ili kuipa familia yetu furaha... nakuahidi hilo."
Namouih akatabasamu na kuendelea kuzichezea nywele za mdogo wake kwa upendo.
Ni wakati huo ndipo mlango ukafunguliwa na dada hao wawili wakatazama huko kumwona Draxton anaingia. Namouih akaachia tabasamu kwa hisia, naye Sasha akawa anamwangalia kwa umakini. Namouih akamwangalia mdogo wake na kuona alikuwa anamtazama Draxton kwa hofu kiasi, na ilieleweka wazi hiyo ilikuwa kwa nini. Draxton akaanza kuelekea sehemu waliyopo wanawake hawa, akiwa na mwonekano wake wa kawaida kabisa, naye akasimama nyuma yake Namouih huku akimtazama Sasha kwa njia ya kirafiki.
"Naona umeamka," Draxton akasema kwa sauti yake tulivu.
"Tena muda siyo mrefu," Namouih akasema.
"Unahisije mwilini?" Draxton akamuuliza binti.
"Vizuri tu," Sasha akajibu.
"Ni jambo jema. Mama?" Draxton akamuuliza Namouih.
"Amemfatia mtoto supu," Namouih akamjibu.
"Okay. Nafurahi kuona umeamka Sasha. Pole kwa yote uliyopitia," Draxton akasema.
"Asante. Kaka Draxton..." Sasha akasema.
"Naam Sasha..." Draxton akaitika.
"Nataka kukuomba samahani kwa mambo yote niliyofanya...." Sasha akasema huku machozi yakimtoka.
"Sasha..." Namouih akamsemesha kwa kubembeleza.
"Nisamehe sana kaka, akili yangu haikuwa sawa kabisa, yaani... nakuomba unisamehe sana..." Sasha akasema kwa hisia.
"Usijali Sasha, naelewa. Haina haja ya kuniomba samahani maana hata mimi nilikukosea sana..." Draxton akasema kwa upole.
"Ulinikosea? Kivipi?" Sasha akauliza.
"Nisingechelewa kuwafikia hiyo siku, haya yote yasingetokea. Nilikuwa nimepanga nifike pale, nikufungue, halafu tufanye collabo tumpe yule bwege kipondo si cha nchi hii..." Draxton akasema.
Sasha akacheka kidogo, na Namouih akatabasamu kwa hisia.
"Ila sasa kila kitu kitakuwa sawa. Uko sawa, na mambo yaliyopita hayatakusumbua tena. Ukija kutoka hapa, jinyanyue tu na kusonga mbele kwa kuwa mtu bora unayeweza kuwa," Draxton akaongea kwa upole.
Sasha akatikisa kichwa kukubali, na Namouih akawa anayafuta machozi yake.
Draxton akaweka kiganja chake begani kwa Namouih, naye Namouih akakishika kwa wororo. "Daktari anasemaje?" mwanaume akamuuliza.
"Bado hajaingia... halafu nilikuwa nimeshasahau, natakiwa kuongea naye maana huyu ameshaamka. Ngoja mama aje twende wote, eh?" Namouih akasema.
"Sawa," Draxton akakubali.
"Si nitatoka mapema tu?" Sasha akauliza.
"Tutasikiliza swagger za doctor, ndiyo tutajua," Namouih akamjibu.
"Ukitoka unataka kufanya mambo gani?" Draxton akamuuliza binti.
"Mengi. Sijihisi kuumwa sana ila... nafikiri shule ndo' cha kwanza. Nimewamiss marafiki zangu," Sasha akasema.
Draxton na Namouih wakatabasamu, naye Namouih akasema, "Kuna rafiki yako anaitwa... Sabna nadhani...."
"Sabrina..." Sasha akasema huku anatabasamu.
"Ndiyo, Sabrina. Huwa anapiga simu kila siku kukujulia hali. Atafurahi akijua umeamka," Namouih akasema.
Sasha akaonekana kuwa na amani zaidi sasa, na ni jambo lililomfariji mno dada yake. Zakia akawa amerejea hapo pamoja na mwanadada fulani aliyebeba vyombo kadhaa vilivyofunikwa, naye akamwona Draxton na kusalimiana naye vizuri. Mwanadada yule alikuwa ameleta chakula kwa ajili ya Sasha, naye Zakia akaanza kusaidiana naye ili aweze kuanza kumlisha binti yake kwa upendo. Namouih akasema sasa kwamba angekwenda kuonana na daktari, naye akamuaga mdogo wake kwa kumbusu kichwani, kisha akatoka hapo pamoja na Draxton na kusimama pembeni ya mlango wa chumba hicho kumsubiri aufunge. Kilikuwa ni chumba cha kulaza mgonjwa binafsi ndani ya hospitali kubwa jijini hapo.
Draxton alipoanza kumwongoza Namouih, mwanamke huyu akamshika mkono kama kumzuia kwanza, nao wakatazamana machoni, kisha akamsogelea na kuuliza, "Sa'hivi maaskari wamefikia wapi?"
"Wamechunguza mambo mengi... wameshangazwa na yule kiumbe kama ilivyo ila... imekuwa ni ishu ya ajabu tu kwenye vyombo vya habari bila kueleweka imekuwaje hivyo. Natumaini hawatawafikia nyie maana mambo mliyopitia ni mengi mno kuanza kuzinguliwa na maaskari tena," Draxton akasema.
"Nasikia waliichunguza miili ya wale wanaume wengine ila fingerprint walizokuta ni za mnyama na si mwanadamu... kwa hiyo angalau kwako wewe hakutakuwa na jambo la kukusumbua," Namouih akasema.
"Ni wiki tu imepita, inabidi tusubiri kuona itakavyokuwa," Draxton akasema.
"Nikikaa kutafakari hiyo siku sometimes... najiuliza ingekuwa vipi kama usingekuja kutusaidia..." Namouih akasema kwa hisia.
"Ilikuwa lazima nije. Maisha yenu nyote yalikuwa hatarini... na ya mtoto wetu pia," Draxton akamwambia huku akimtazama tumboni.
Namouih akajishika tumboni taratibu, kisha akauliza, "Blandina?"
Draxton akamtazama machoni kwa ufupi, naye akatikisa kichwa kuonyesha kwamba hajui.
"Hata mimi nimejaribu kumtafuta ila hapatikani. Nimempoteza rafiki yangu Max," Namouih akasema kwa hisia.
"Hapana, haujampoteza. Anaumia tu Namouih. Na inaeleweka kwa nini. Mpe muda. Na usiache kumtafuta. Ipo siku tu utampata, na mtakuwa wote tena," Draxton akamwambia.
"Unaamini kabisa kwamba ipo siku atakuja kunisamehe?" Namouih akauliza.
Draxton akatikisa kichwa chake kukubali.
Namouih akaangalia chini kwa huzuni, kisha akashusha pumzi. Akamwangalia tena Draxton na kuona ameweka umakini wake kwenye jambo fulani, naye akauliza, "Vipi?"
Draxton akamtazama na kusema, "Unakumbuka nilichokwambia kuhusu yule mwanaume niliyekutana naye ule usiku nimepotea?"
"Yule anayeitwa Mark?" Namouih akauliza.
"Ndiyo. Amefika hapa."
"Wapi... yuko wapi?"
"Huyo hapo," Draxton akasema na kutazama nyuma yake Namouih.
Namouih akageuka na kumwona mwanaume fulani mzungu, akiwa amevaa kwa njia ile ile kama tu mara ya kwanza ambayo Draxton alikuwa amekutana naye. Tayari Draxton alikuwa amemsimulia Namouih kuhusiana na Mark, akimwambia kwamba mwanaume huyo alikuwa na majibu yote ya maisha yake ya nyuma, na kwamba kwa sasa kulikuwa na kisa kingine alichokuja nacho kilichohitaji msaada wake. Walikuwa wameachana kwa makubaliano kwamba Draxton angemtafuta baadaye kwa sababu alihitaji kushughulika na masuala mengine ya maisha yake kwanza kabla hajajiingiza kwenye hayo mapya kama siyo ya zamani tu, na huu ndiyo wakati ambao mwanaume huyo alikuwa amerejea ili kuyaweka wazi.
Kurasa za hadithi ya maisha ya wawili hawa hazikuwa zimemalizika, kwa kuwa sasa zingeanza kufunguliwa zingine zaidi ambazo zingeleta badiliko kubwa kabisa ndani ya maisha ya Draxton kwa njia ambayo ingeathiri maisha ya mwanamke aliyechagua kumpenda, Namouih.
★★★★★★★★★★
MWISHO
★★★★★★★★★★
CHANGE: Spinoff ya DRAXTON Itakuja Hivi Karibuni.
Written by Elton Tonny.
Am back my friendAmani iwe nawe mkuu Elton Tonny . Umetusahau sisi wadau wako aisee sisi wengine ni wapenzi wa simulizi zenye spiritual power ndani yake. Tafadhali fanya jambo
daaah! Jf bwana ni kiwanda cha arosto, sawa tunasubiri mateso kwa hamuDRAXTON
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Siri, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
(R-rated 18+)
Ni mwendelezo wa story kali sana ya CHANGE utakaotupeleka katika nyanja za juu zaidi ndani ya kisa cha maisha halisi ya mhusika aitwaye Draxton. Itaanza kuruka hapa Jumamosi na Jumapili kwa utaratibu huo huo kama kawaida ya mwandishi Elton Tonny. Itakuwa ni hadithi nzuri sana inayozama zaidi kwenye maisha ya Draxton na badiliko lake mpaka jinsi yalivyoyaathiri maisha ya watu kama Namouih na Blandina. Karibuni sana. Hii si nakala ya kukosa!
DRAXTON... COMING SOON
WhatsApp +255 678 017 280View attachment 2756213
Bro niko tight sanaaaDRAXTON
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Siri, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
(R-rated 18+)
Ni mwendelezo wa story kali sana ya CHANGE utakaotupeleka katika nyanja za juu zaidi ndani ya kisa cha maisha halisi ya mhusika aitwaye Draxton. Itaanza kuruka hapa Jumamosi na Jumapili kwa utaratibu huo huo kama kawaida ya mwandishi Elton Tonny. Itakuwa ni hadithi nzuri sana inayozama zaidi kwenye maisha ya Draxton na badiliko lake mpaka jinsi yalivyoyaathiri maisha ya watu kama Namouih na Blandina. Karibuni sana. Hii si nakala ya kukosa!
DRAXTON... COMING SOON
WhatsApp +255 678 017 280View attachment 2756213
Naam! Asante kwa kuja mkuu wadau wako tupo tunasubiriDRAXTON
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Siri, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
(R-rated 18+)
Ni mwendelezo wa story kali sana ya CHANGE utakaotupeleka katika nyanja za juu zaidi ndani ya kisa cha maisha halisi ya mhusika aitwaye Draxton. Itaanza kuruka hapa Jumamosi na Jumapili kwa utaratibu huo huo kama kawaida ya mwandishi Elton Tonny. Itakuwa ni hadithi nzuri sana inayozama zaidi kwenye maisha ya Draxton na badiliko lake mpaka jinsi yalivyoyaathiri maisha ya watu kama Namouih na Blandina. Karibuni sana. Hii si nakala ya kukosa!
DRAXTON... COMING SOON
WhatsApp +255 678 017 280View attachment 2756213
Usijali Kaka. Pole kwa changamotoBro niko tight sanaaa