DYLAN
Story by Elton Tonny
Familia, Kazi, Urafiki, Mapenzi, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Visasi, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
(R-rated 18+)
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA AROBAINI NA TATU
★★★★★★★★★★★★★★★★★
"No... no... no.... Camila... no!" Gilbert akawa anaongea huku akilia.
Mwili wa Camila ulianguka chini baada ya risasi hizo kumpiga kifuani. Damu nyingi zilianza kumtoka na kusambaa kwenye nguo yake nyeupe iliyokuwa kwa ajili ya bibi harusi. Tena, Beatrice akawa ameua mtu asiyekuwa na hatia; kama kujifurahisha tu. Midomo ya Dylan ilianza kutetemeka sana akimwangalia shangazi yake kipenzi chini hapo, ambaye hakuwa na uhai tena. Grace alikuwa akilia sana huku mikono yake ikitetemeka kwa hofu kubwa, naye Jaquelin akawa analia pia huku akiiita jina la wifi yake.
Beatrice akapuliza tundu la bastola yake, kisha akasema, "Huyo hakuwa na faida yoyote kwangu. Angalau sasa wamebaki watakaoburudisha zaidi au siyo?"
Wanaume wake wakaanza kucheka.
Gilbert alilia sana. Dylan alishindwa hata kutoa sauti ya kilio na kubaki anadondosha tu machozi huku anautazama mwili wa Camila.
"Okay tuendelee. Mmmm... sijui nani afate sasa hivi. Jaquelin... Grace... kijacho... ohohohoh... kweli nikimuua Grace na kijacho anaenda... kwa hiyooo... nimpasue tumbo, nimtoe kijacho, halafu tupige selfie aliyokuwa anaitaka Dylan, then nimuue mama mbele ya kijacho... au huko nitakuwa nimepita mbali sana? Possibilities nyingi yaani dah..." Beatrice akaongea kwa dharau huku watu wake wakicheka kwa sifa.
"Beatrice... mdogo wangu alikukosea nini? Kwa nini umeamua kuwa mnyama kiasi hiki? Kama kuna mtu unataka kuua niue mimi! Kwa nini unawaumiza wengine..." Gilbert akaongea kwa huzuni.
"Don't be a p***y Gilbert! Nafikiri... itafaa sa'hivi tukipiga kura labda, au mnaonaje? Nitaanza na wewe Gilbert. Ungependa nani afate kati ya mkeo, au mpenzi wa mwanao? Mmm?"
Dah! Huyu mwanamke alichosha. Dylan akafumba macho kwa nguvu na kuanza kuivuta mikono yake kwa nguvu sana ili akate kamba. Zilikuwa ngumu mno kiasi kwamba mpaka akaichubua mikono yake akijaribu tu kuzikata, lakini akashindwa. Akapiga kelele za hasira huku analia kwa uchungu.
"Oooh... jomonii... usilie mtoto. Huo ni mwanzo tu," Beatrice akasema kikejeli.
"Boss..." Seba akamwita Beatrice.
"Usijali Seb, mapolisi hawawezi kuja sasa hivi hata kama wangesikia huo mlio. Hapa tutacheza mpaka chakunaku," akasema Beatrice.
"Ahahah... ahahahah...."
Wote waliokuwa hapo walianza kumshangaa Dylan, kwa sababu alikuwa anacheka.
"Well, well, well... naona show imeanza kukuingia vyema dogo," Beatrice akamwambia.
"Ahah... siyo kihivyo. Nilikuwa tu... nawaza... haya yote unayoyafanya, hivi David atataka tena kuwa na mama kama wewe?" Dylan akamuuliza.
Swali lake lilimfanya Beatrice akerwe kiasi.
"Nini?" Beatrice akauliza.
"Ahahah... fanya ufanyavyo... lakini ipo siku dogo atajua uliwaua dada yake na baba yake... na hawa watu wengine wote. Na hiyo siku ukiwa naye nimeshaiona yeye pia atafata... tena nafikiri kwa akili yako kama ya bata mzinga utachukua oven umwingize humo aive then awe ndiyo supper! Ukifika huo mlo usisahau kunialika..." Dylan akamwambia.
Wazazi wake, Grace, na hata wale wanaume walikuwa wakijiuliza alikuwa na tatizo gani. Walishindwa kumwelewa kwa sababu wakati huu ambao Beatrice alikuwa akijitahidi kumvunja moyo, yeye ni kama alizidi kuwa imara. Beatrice akamtathini kwa sekunde kadhaa. Aliwaza kijana huyu kuna kitu alikuwa anafanya zaidi ya kile ambacho alionekana anafanya. Mwanamke huyu alikuwa mwerevu sana kutambua kwamba kuna sababu iliyomfanya Dylan atende hivyo.
"Unajua... toka tulivyoanza kuongea... umekuwa ukijaribu tu ku.... unanipotezea muda!" Beatrice akasema baada ya kutambua hilo.
Dylan akawa anamwangalia kwa mkazo kutokea chini pale.
"Kwa nini unafanya hivyo?" Beatrice akamuuliza.
"Beatrice... tafadhali nakuomba umwachie Grace... anahitaji huduma...."
"Kaa kimya Gilbert! Wewe... niambie unapanga nini? Umejifungia bomu hapo? Au unawasubiri mapolisi? Niambie kwa nini unajifanya mjanja sana..." Beatrice akamwambia Dylan.
Alipoona Dylan amekaa kimya tu, akainyoosha bastola yake kuelekea kichwa cha Grace!
"Beatrice!" Gilbert na Jaquelin wakasema kwa hofu.
Dylan akawa anapumua kwa hofu pia.
"Sihitaji kura tena. Unafata sweetheart," Beatrice akamwambia Grace.
"No... don't..." Dylan akamwomba.
"Fine. Niue. Niue tu! Itakupa faida gani? Kwamba umeongeza namba za vifo kwenye ledger yako iliyojaa umwagaji damu? Go ahead... shoot me!" Grace akamwambia kwa hasira.
Kwake yeye ilikuwa imefikia "too much!" Beatrice akaikoki bastola yake akionyesha utayari wa kumtandika Grace risasi. Dylan, Gilbert na Jaquelin walikuwa wakiomba kwa sauti za juu kwamba Beatrice asifyatue risasi, na papo hapo mlio mkubwa wa risasi ukasikika!
Wote walishtuka sana, kwa sababu risasi hiyo ilikuwa imeipiga bastola ya Beatrice na kufanya aidondoshe pembeni. Yeye pamoja na wanaume wake pia walishangaa sana na kuangalia upande wa kuingilia jengoni humo, nao wakaweza kuwaona wanaume wanne wakiwa wanaingia; watatu wakiwaelekezea bastola na mwingine akiwa bila bastola. Dylan aliingiwa na matumaini baada ya kumtambua mwanaume huyo ambaye hakubeba bastola kuwa ni Bosco.
Beatrice aliduwaa! Akabaki kuwaangalia wanaume hao waliokuwa na miili mikubwa na wenye sura zisizotaka mchezo kabisa.
"Wekeni vyuma vyote chini! Mikono kichwani!" mmoja wao akawaamrisha wanaume wa Beatrice.
Wale wawili waliokuwa wamesimama pembezoni mwa Gilbert na Dylan wakaweka mikono yao vichwani kwa njia ya kujisalimisha, na wawili waliokuwa usawa wa Grace na mwili wa Camila wakafanya hivyo hivyo pia; ikionyesha hawakuwa na bunduki. Lakini yule aliyemshikilia Jaquelin akaendelea kumng'ang'ania na kutoa vitisho kwamba angemuua ikiwa wangeendelea kuwaonyeshea bastola namna hiyo, kwa hiyo eti wazishushe.
Baunsa huyu aliyekuwa ametoa amri kwa wanaume wa Beatrice akamwelekezea bastola jamaa huyo kwa makini sana na kufyatua risasi iliyompata kupitia shavu usoni! Wote walishtuka sana, kwa sababu alionyesha shabaha ya hali ya juu mno. Ni Beatrice na Seba peke yao ndiyo waliokuwa na bastola, hivyo Seba akaitoa yake taratibu huku akipiga mahesabu ya kufanya ujanja fulani.
"Tupa chini... usijifanye mjanja!" baunsa huyo akamwambia Seba.
Hakuwa na jinsi tena ila kutii kwa sababu bastola zote zilielekezwa kwake. Akairusha pembeni mwa jengo, na hapo hapo Bosco akamkimbilia Dylan ili kwenda kumfungulia kamba haraka. Wanaume wale walioingia na Bosco wakawaamrisha wanaume wa Beatrice walale chini upesi. Wote wakatii na kulalia matumbo yao huku mikono wakiwa wameiweka vichwani, wakimwacha Beatrice amesimama tu. Wanaume wawili waliokuwa pamoja na Bosco wakawafuata Grace na Jaquelin ili kuwafungulia kamba na wao pia, huku yule baunsa mmoja akimwelekezea Beatrice bastola. Jaquelin akamfata Grace na kumshika vizuri akimuuliza kama alihisi maumivu sehemu.
"Dylan pole sana bro... tumekutafuta sana... nilimtafuta Queen akakutrack lakini baadae tukakupoteza... nafikiri hawa walitupa simu yako kwo' Queen akatugawa ili tukutafute sehemu za karibu..." Bosco akawa anamwambia Dylan baada ya kumfungulia kamba na kuanza kumfungua Gilbert pia.
Dylan akasimama. Alikuwa anamtazama mtu mmoja tu... Beatrice. Beatrice alimwangalia Dylan kwa hofu sana, kwa sababu mwanaume alikuwa anamtazama kwa njia ya hasira nyingi mno. Hangeweza kumwacha salama mwanamke huyo aliyethubutu kumuua shangazi yake kipenzi na kutishia kumuua mtu aliyempenda sana, yaani Grace, hivyo alikuwa anawaza kumshika ili amfunze somo ambalo hangesahau.
Ile Dylan alipoanza kumfata Beatrice, akashtuka baada ya kuona kama mtu fulani anakuja taratibu nyuma ya yule mwanaume baunsa aliyekuwa amemwelekezea bastola Beatrice kutokea kule aliposimama. Lakini hakuweza kutoa onyo mapema kutokana na kumshangaa kiasi. Mviziaji huyo akamkaba mwanaume yule na kumwekea bastola kichwani, na kisha akaipiga pembeni sana bastola aliyoishika mwanaume huyo. Baada ya wote kumtazama kwa makini wakatambua ilikuwa ni Jafari.
"Nyie wawili tupeni bunduki zenu, la sivyo nampasua huyu kichwa!" Jafari akawaamrisha wale wenzake na baunsa huyo.
"Jafari... unafanya nini?" Grace akauliza kwa mshangao.
Kila mtu alishangaa sana.
"Mmenisikia? Zitupeni!" Jafari akafoka.
Wale wanaume wawili hawakutupa silaha zao, bali wakamnyooshea Jafari kwa ujasiri kabisa. Dylan akawa anamtazama Jafari kwa njia ya kawaida tu. Beatrice akatabasamu kiasi na kumwangalia Dylan kwa kiburi.
"Jafari... nini una..." Gilbert akasema.
"Ni yeye ndiye aliyetupiga vichwa wakati tuko nyumbani baba. Na yeye ni puppet wa huyu mwanamke!" Dylan akasema.
"Unbelievable!" Grace akasema kwa kushangaa sana.
"Sihitaji kuwaelezea chochote. Nyie wawili shusheni bastola zenu la sivyo nitamuua huyu! Nina mafunzo..." Jafari akanena.
"Kweli Jafari na yote tuliyofanya pamoja unaamua kunisaliti? Amekununua kwa shilingi ngapi huyu mwanamke?" Grace akamuuliza.
"Haikuhusu..." Jafari akamjibu.
Beatrice alikuwa anampa ishara mwanaume wake mmoja alielala chini kwamba aichukue bastola ile aliyoidondosha chini baada ya kuwa imepigwa na risasi muda ule. Ilikuwa imedondokea karibu na usawa wake, hivyo jamaa akawa anapiga hesabu za kuichukua upesi ili aitumie.
"Hainihusu? Kwa nini? Eeh? Sema Jafari! Ni nini ambacho hauja.... aah.... aaaah!"
Grace akiwa hajamaliza kuongea akaanza kutoa vilio hivyo. Wote walipomtazama, waliweza kuona kama maji yakitiririka kutokea katikati ya miguu yake na kumwagikia chini. Akalegea sana na kumfanya Jaquelin ampe egamio huku naye akihofia usalama wa Grace.
"Grace..." Dylan akaita kwa wasiwasi.
"Maii yamepasuka! Mtoto anakuja!" Jaquelin akaonya.
"Grace... Jafari... nahitaji... Grace..." Dylan akaanza kubabaika.
Hiki ndiyo kikengeusha fikira alichokihitaji mwanaume yule wa Beatrice pale chini. Akajiviringisha haraka na kuichukua bastola ile, kisha akamfyatua risasi ya ubavuni mwanaume mmoja kati ya wale wawili waliokuwa wameelekeza bunduki kwa Jafari. Jaquelin akapiga kelele huku akiwa bado amemshikilia Grace ambaye alikuwa akilia kwa kuhisi uchungu. Dylan na Beatrice wakainama chini, na wakati mwanaume yule alipotaka kumfyatua risasi yule mwanaume wa pili aliyekuja na Bosco, Gilbert akamwahi na kumrukia mkono ulioshika bastola na kufanya ipige risasi kwenye paja la mwanaume huyo, hivyo bastola ya mwanaume huyo ikadondokea pembeni. Bosco akamfata Gilbert pia ili amsaidie kumdhibiti mwanaume huyo.
Mwanaume ambaye alikuwa amekabwa na Jafari akajitoa kwa nguvu mikononi mwake na kuanza kupigana naye, lakini Jafari akamzidi ujanja na kumfyatua risasi ya kifua na kufanya adondoke chini. Ile Jafari anatazama juu akakutana na teke la tiki-taka kutoka kwa Dylan, ambaye aliwahi upande wake haraka sana. Jafari akaweweseka na kurudi nyuma, kisha akataka kumwelekezea Dylan bastola ili ampige na yeye risasi lakini kwa mtindo wa sarakasi Dylan akawa amemrukia na kuutandika mkono huo kwa teke; hivyo bastola ya Jafari ikadondokea pembeni.
Wakati Gilbert na Bosco walipofanikiwa kumdhibiti mwanaume yule pale chini, Gilbert akampatia bastola ile Bosco na kumwambia amchunge ili yeye akatoe msaada kwa Grace, lakini ni hapa hapa ndipo Beatrice alikuwa ameshaiwahi bastola ile iliyodondoka ya yule mwanaume aliyepigwa risasi pajani. Dylan sasa alikuwa anamchangamkia Jafari kwa kumtandika ngumi zisizo za kitoto kutokana na hasira kali aliyokuwa nayo kumwelekea kwa sababu ya usaliti wake. Lakini Jaquelin akamwita kwa sauti ya juu kumkumbusha kwamba Grace alihitaji sana msaada, hivyo Dylan akaona aachane na Jafari kwa kuwa alikuwa ameshadebweda balaa.
Ni wakati amegeuka ili amfate Grace upesi, pale alipoona mkono wa Beatrice ulioshika bastola ukiwa umemwelekea baby mama wake. Akatoa macho na kuanza kukimbia haraka ili akamzibe, lakini akawa amechelewa. Beatrice alifyatua risasi kumwelekea Grace, akiwa amelilenga tumbo lake kabisa! Mshtuko ulikuwa ni mkubwa kwa Dylan baada ya kusikia mlio huo wa risasi kiasi kwamba hata hakuona mambo vizuri, lakini baada ya Beatrice kuwa amefyatua hiyo risasi papo hapo sauti za juu za milio ya risasi zikazidi kusikika tena. Risasi kumi na mbili!
Hakuna aliyeelewa kilichoendelea mpaka wote walipomtazama Beatrice na kukuta akiwa ametobolewa-tobolewa mwilini kwa risasi nyingi, na mwili wake ukadondokea chini kwa kishindo baada ya kula risasi kumi na mbili *****! Dylan, Bosco, Jafari, na wanaume wale waliobaki pale chini wote walitazama kutokea upande wa kuingilia kwenye jumba hilo, na hapo wakaweza kumwona, si mwingine, ila Queen mwenyewe! Alikuwa ameelekeza bastola upande ule alipodondokea Beatrice, na wote wakatambua kwamba ilikuwa ni yeye ndiye aliyemtandika risasi hizo zote.
Dylan aliangalia upande wa mama yake na Grace, na hapo akaweza kuona kama mtu fulani akiwa amewakumbatia Jaquelin na Grace. Kwa haraka akatambua kwamba ilikuwa ni Gilbert, baba yake, naye Dylan akanyanyuka na kwenda hapo upesi. Gilbert alikuwa na tundu la risasi nyuma ya mgongo wake, na hii ikamwambia Dylan kwamba wakati Beatrice alipofyatua risasi ile kumwelekea Grace, baba yake alijiweka hapo ili impige yeye badala. Alihuzunika sana.
Grace bado alikuwa anaugulia maumivu ya uchungu mwingi sana uliokuja kabla ya wakati mwafaka, naye Jaquelin alikuwa akilia sana kwa sababu mume wake alikuwa hoi na risasi mgongoni. Dylan akashindwa afanye nini. Ajigawe vipi? Wanaume kadhaa wakaingia, wakiwa ni watu wa Queen, nao wakawafuata pale na kuanza kutoa msaada, huku wengine wakiwadhibiti wale wanaume wa Beatrice. Bosco akasaidiana nao ili wambebe Grace na kumwahisha kwenye gari apelekwe hospitali upesi.
Jaquelin akabaki chini hapo akiwa amemshikilia Gilbert, ambaye sasa hakuwa hai tena. Alikuwa akilia kwa uchungu mwingi sana, naye akawa anamwambia Dylan aende hospitali tu kwa sababu Grace angehitaji awepo kule. Dylan akanyanyuka na kusimama, akiwa ameghafilika sana, na hapo Queen akaja nyuma yake na kumshika begani.
"Queen..." Dylan akashindwa kuongea zaidi.
"Its okay. Go. Nitakuwa pamoja nao," akamwambia Dylan.
Dylan akaanza kuondoka upesi kuwahi kwenye gari lile walilompeleka Grace, na baada ya kufika akaketi karibu yake, nalo likaondolewa hapo ili kuwahi hospitali. Jaquelin akabaki tu anamlilia mume wake kwa huzuni, akihisi kama vile mambo haya yote ni ndoto. Queen akapiga simu polisi na kuwaambia kuhusiana na tukio hilo hapo. Akahakikisha Jafari na wale wanaume wengine wamefungwa vizuri sana hapo, naye akachuchumaa karibu na Jaquelin na kumtazama kwa makini.
"Najua huu ni wakati mgumu kwako, lakini mapolisi wakifika...."
"Usijali.... hhhh... najua la kufanya..." Jaquelin akamkatisha Queen huku akiwa bado analia.
Queen akatikisa kichwa taratibu kuonyesha ameelewa. Kwa kuwa hakutaka kujionyesha kwa mapolisi ambao bila shaka wangeanza kumfatilia-fatilia, akaondoka haraka na kumwachia Jaquelin walinzi wake wawili kabla ya mapolisi kufika.
Grace alifikishwa hospitali baada ya dakika kadhaa, na kufikia wakati huu alikuwa akitokwa na damu kwa sababu ya mkazo mwingi aliopitia siku hiyo. Wakamwahisha kwenye chumba cha dharura, nao madaktari wakaingia ili kuanza kutoa msaada haraka. Bosco alikuwa pamoja na Dylan, akimtia moyo kuwa kila jambo lingekwenda sawa tu, ijapokuwa Dylan alikuwa amepasuka sana moyo. Alikuwa analia mno. Baraka, Harleen, Matilda, Camila, baba yake, na wengine wote Beatrice aliowaua kikatili ni mambo yaliyomfanya augue sana moyoni mwake, hasa kwa kuwa aliona sababu ilikuwa ni yeye. Hakutaka kumpoteza na Grace, wala mtoto. Hivyo ndiyo kati ya mambo yaliyobaki ambayo yangempa nguvu ya kusonga mbele, kwa hiyo kama angewapoteza, basi angekata tamaa ya maisha.
Baada ya muda fulani, daktari akatoka kwenye chumba kile, naye Dylan pamoja na Bosco wakamfuata huku Dylan akiuliza hali ya Grace na mtoto. Daktari akashusha pumzi, kisha akamshika Dylan begani kwake.........
★★★★★
MIAKA MINNE BAADAE.....
"Harakisha bwana, muda umeenda!" akasema Shani.
"Mama usikonde, mambo yako fresh hata kama nikikawia dakika 20 bado watakuwa hawajafika," Steven akamwambia mama yake.
"Yaani kweli nimewezaje kusahau kumnunulia Yogurt... na alishaniambia kanapenda kweli!" Shani akasema.
"Steven kimbilia haraka sasa..." Leila akamwambia mdogo wake.
Steven akatoka upesi kwenye nyumba yao na kuelekea dukani.
"Okay wali, nyama, tambi, chips, marage, njegele, kuku, soseji, juisi na...."
"Mama jamani kila kitu kiko sawa. Ni Yogurt kwa ajili ya dogo tu ndiyo imekosekana... Steven anaiwahisha... hapa kila kitu kiko safi wakifika ni kujinoma tu," Leila akamwambia mama yake.
"Sawa. Hawatachukua muda mrefu, me naenda kujiandaa," akasema Shani, na kisha kuelekea juu chumbani.
Hii ilikuwa ni siku nzuri sana kwao kwa kuwa walikuwa na wageni muhimu ambao waliwasubiri kwa hamu sana. Shani ndiye aliyeonyesha furaha kubwa kwa kuwa alitazamia kwa hamu sana wageni hao wapendwa wafike, hivyo vyakula viliandaliwa kwa kila aina ya ufundi wanaojua wanawake wazoefu kwenye mapishi. Bado walikuwa kwenye nyumba yao hii mpya iliyokuwa ya familia ya Gilbert kipindi cha nyuma, na kufikia wakati huu palikuwa pamebadilika haswa na kupendeza hata zaidi kwa mazingira yake.
Kufikia kipindi hiki, Shani alikuwa amefungua mgahawa mzuri jijini huku, naye Leila alikuwa ndiyo msimamizi mkuu wa Dy-Foods Restaurant, ule mgahawa wa Fetty. Fetty yeye aliondoka kwenda kuendelea na masomo zaidi, hivyo alikuwa ameuacha mgahawa wake chini ya uangalizi muhimu wa Leila, ambaye pia alikuwa rafiki yake sana wakati huu. Hakuubadili jina mgahawa huo kwa kuwa "Dy-Foods" ingemkumbusha sikuzote alikotoka na mtu muhimu aliyempatia fursa hiyo ya kuumiliki. Steven alikuwa mkubwa sasa, mwenye miaka 16, akiwa kidato cha nne.
Baada ya Steven kuwa amerudi na vile alivyoagizwa, wote wakakaa kwa utayari wakiwasubiri wageni wafike. Hazikupita dakika nyingi sana nao waliweza kusikia 'horn' mbili za gari nje ya geti, naye Steven akatoka upesi kwenda kulifungua. Shani na Leila walitoka mpaka usawa wa sehemu pana pale nje ya kuegeshea magari na kusimama, wakiwa wanatazama kwa hamu getini. Baada ya Steven kufungua geti, likaingia gari ndani hapo, aina ya Range Rover SV Luxury 2022, lenye rangi nyeusi, lililokuwa linangaa kama ndiyo limetoka dukani!
"Aisee! Cheki gari hiyo..." Leila akamwambia mama yake.
"Inaonekana ya gharama," akasema Shani.
"Sana."
Gari likaingia moja kwa moja mpaka sehemu ya kuegeshea, kisha Steven akafunga geti na kuanza kuelekea upande huo wa gari. Mlango wa nyuma ulianza kufunguka, kisha akashuka mwanamke ambaye walimfahamu vizuri sana. Shani na Leila wakaanza kumfata huku naye akiwaelekea na tabasamu la furaha.
"Wow... jamani Jaquelin!" Shani akasema kwa furaha.
"Shani mpenzi, za siku nyingi?" akasema Jaquelin akiwa amemfikia na kumkumbatia.
"Safi tu. Yaani jamani... karibu sana mpendwa," Shani akasema.
"Asante dear," Jaquelin akamwambia.
Leila akamsalimu Jaquelin vizuri naye akamwitikia. Ni hapa ndipo wakawaona wengine kutokea kwenye gari wakija upande wao pia, nao wakafurahi sana.
"Kaka Dylan!" Steven akaita kwa furaha.
"Steven huyo! Vipi jembe?" Dylan akamsalimu pia na kugongesha kiganja chake kwake alipomkaribia.
"Wow! Dylan... Grace jamani!" Shani akawafata na kumkumbatia Grace kwa upendo.
"Hee! Kaone na haka!" akasema Leila.
Ndiyo. Ilikuwa ni Grace na Dylan, wakiwa na mtoto wao mdogo wa kike. Leila akambeba msichana huyo na kuanza kuchezea mashavu yake makubwa. Kalikuwa kanakula pipi tu huku kakiwa hakaelewi somo! Kalikuwa kazuri sana kama mama yake. Na kalipendeza mno kwa gauni la rangi ya pink na viatu vyeupe vilivyowakawaka kila wakati ambapo kangekanyaga chini. Nywele zake zilikuwa ndefu na laini, nazo zilisukwa kwa mtindo fulani kama rasta.
Grace huyo! Alikuwa amefanikiwa kujifungua msichana huyu usiku ule ambao ulikuwa wenye kuhofisha sana aliowahi kupitia kwenye maisha yake. Sasa alikuwa mama, na mke wa Dylan. Walifunga ndoa mwaka mmoja uliopita wakati binti yao alipokuwa na miaka mitatu, nao wakaendelea na maisha mazuri yaliyojaa upendo mwingi sana na furaha. Baada ya ndoa yao walikwenda fungate (honeymoon) la muda mrefu sana pamoja na binti yao huyu nje ya nchi, kule Indonesia, nao wakaendelea kukaa huko kwa miezi mingi mpaka waliporejea nchini tena wiki moja iliyopita kufikia siku hii.
Hapa sasa ndiyo walikuwa wamekuja kuwatembelea marafiki zao wapendwa baada ya kutoonana kwa kipindi hicho chote. Grace alikuwa amevaa gauni refu la rangi ya maziwa lenye urembo wa maua maua, lililokuwa na mpasuo mrefu pia kufikia pajani, na miguuni akivaa viatu vidogo vya matembezi. Usoni alipendeza sana pia na kuonekana kama mwanadada wa umri mdogo tu, na nywele zake alikuwa amezisukia kwa "weaving" la nywele za kizungu lililofanya aonekane kama mmarekani mweusi. Pesa hizo! Dylan pia alikuwa amependezea kwa kuvaa shati nyepesi yenye maua-maua na suruali nyeusi ya jeans, pamoja na sneaker kali nyeupe.
"Jamani mashavu! Hujambo? Eeh? Amekua!" Shani akawa anamsemea mtoto.
"Nakwambia kagoma kukaa na mimi eti anamtaka mama yake tu... nimemwambia nimemgaya," Jaquelin akasema, na wote wakacheka.
"Halafu jina lake huwa linanitoka jamani. Nakumbuka ni gumu kweli..." akasema Shani.
"Siyo hata gumu, ni uzee wako tu," Steven akamwambia mama yake, na wote wakacheka.
"Katoto, eti waitwa nani? Eeh? What is your name?" Shani akawa anamuuliza mtoto.
Kenyewe kakawa kanamwangalia tu huku kanamumunya pipi.
"Ni nani kweli? Me mwenyewe limenitoka..." akasema Leila.
"Marcelyn," akajibu Grace.
"Wow! Zuri kweli," akasema Leila.
"Jamani karibuni ndani..." Shani akasema.
"Asante. Pamebadilika sana huku. Tokea mara ya mwisho nimefika..." Jaquelin akawa anasema.
Wote wakaelekea ndani huku wakiongea kwa furaha. Walifika na kuketi pamoja kwenye masofa na kuongea kwa ufupi, kisha Leila akawakaribisha mezani ili waweze kupata chakula pamoja. Muda wote Shani na wengine waliojaribu kumsemesha Marcelyn, dogo alikuwa haongei chochote ila kufanya tu michezo yake ya kitoto bila kujali muda! Wakakaa naye mezani tayari kwa ajili ya kula huku wakifurahia maongezi.
"Eti jamani... yaani mbali kote kule! Mgeenda hata pale Ushirombo kuna sehemu nzuri za kutembelea," akawa anasema Steven, na wote wakacheka.
"Ushirombo pazuri eeh?" akauliza Grace.
"Acha! Indonesia hapaoni ndani," akajibu Steven.
"Tutakuja kumpeleka Celyn apaone... ole wako sa' nikute ni msitu tu," Dylan akamwambia Steven kiutani.
"Huko Indonesia ni pazuri sana?" akauliza Leila.
"Ndiyo kuna sehemu nyingi ni nzuri sana. Kuna mahoteli na vivutio vya watalii wengi," akasema Grace.
"Kule wanaongeaga kiingereza kwani?" akauliza Shani.
"Kwa wageni wanaofika kwenye hoteli kama hizo kiingereza ni must, baada ya kuzoea hapo inategemea na mnakaa muda gani unaweza hata kujifunza lugha yao," akasema Dylan.
"Mpe Shani zile picha... mwonyeshe," Jaquelin akamwambia Grace.
Grace akachukua simu yake na kutafuta picha za sehemu waliyokaa kule Indonesia na kumpatia Shani atazame. Leila na Steven pia wakawa wanaziangalia.
"Eh! Pazuri sana!" akasema Shani.
"Ahahahah... kaone ka Meriselin hapo kanarukaruka," akasema Steven.
"We naye unaharibu jina la mtoto afu' ulikuwa unasema mama mzee kumbe we ndo' kibabu!" Leila akampa ukweli, na wote wakacheka.
"Panaitwaje? Hii hoteli yaani mliyokuwepo na eneo lake?" Shani akauliza.
"Ni villa... hoteli kubwa yaani... inaitwa Kamuela Seminyak, kule Bali," akajibu Grace.
"Bonge la jitu!" akasema Steven.
"Tuambieni mlifanya mambo gani huko..." akasema Leila kwa shauku.
"Mh! Vitu vingi sana. Tulitembelea beach nyingi za kule, kuogelea baharini, kujifunza tamaduni zao... na nyingi ni nzuri sana. Tulifanya matembezi kwa helicopter... yaani mambo mengi sana..." akawa anasema Dylan.
"Ahahahah... mara ya kwanza Celyn amepanda helicopter alimng'ang'ania baba yake mpaka kidogo amchanie shati!" Grace akakumbushia, nao wote wakacheka.
"Hadi raha. Na sisi tutaenda siku moja," akasema Steven.
"Ndiyo mtaenda tu," akasema Dylan.
"Lazima ilikuwa pesa ndefu sana kukaa muda wote huo huko..." akasema Leila.
"Ndiyo. Sema kuna extradi...."
"Mommy..." Marcelyn akamkatisha Grace.
"Yes darling?" akaitika.
"I want pizza," kakasema.
Wote wakawa wanakaangalia huku wanatabasamu.
"You want pizza? Okay. Finish this first, then we'll get some pizza, alright? (unataka pizza? sawa maliza hii kwanza, halafu tutafata pizza eti?)" Grace akamwambia.
"Okay," kakakubali na kuendelea kula soseji.
"Wacha! Amekuelewa!" Steven akasema.
"Ahahahah... ndiyo," Grace akajibu.
"Kaka Dylan, Indonesia inanihusu. Nataka nami nikirudi nisijue kiswazi hata chembe, yaani itasaidia mama asiwe ananisemesha kabisa!" Steven akatania, nao wote wakacheka.
Waliendelea kufurahia chakula, na baada ya kumaliza wakaanza kuongea mambo mengi hata zaidi.
Baadae wakubwa wakawa wameketi pamoja kwenye masofa, huku Steven akiwa na Marcelyn sehemu ya chini pembeni akicheza pamoja naye. Shani akawa anaongelea kuhusu maisha yao huku tokea Dylan na Grace walipoondoka, akigusia jinsi yeye na Jaquelin walivyokuwa mashosti haswa. Akamzungumzia na Emilia pia, ambaye sasa alikuwa chuo kikuu akisomea udaktari.
"Emilia ni smart sana kama mimi tu mama yake," Shani akawa anasema.
"Kweli," Leila akaongea kwa njia ya kejeli.
Dylan na Grace wakatabasamu.
"Muda unapita haraka sana," akasema Jaquelin.
"Yeah," Dylan akakubali.
"Vipi kuhusu David? Yule kijana yuko wapi siku hizi?" akauliza Grace.
"Nasikia yuko kule Nairobi. Aliachiwa fortune kubwa na mama yake kwa hiyo he's living the life," akasema Jaquelin.
"Atakuwa mkubwa sasa hivi," akasema Grace huku anamwangalia Dylan.
"Ndiyo, hajamwacha sana Steven," Jaquelin akasema.
Wote wakawa kimya kwa ufupi, wakimtazama Marcelyn akicheza.
"Unajua... huwa natamani sana... Baraka na Gilbert wangekuwepo kuiona hii siku," akasema Shani kwa hisia.
"Wanaiona. Wao ndiyo wanatuangalia kutoka juu," akasema Jaquelin.
"Ndiyo," akasema Grace.
"Ahah... inaonekana mama siku hizi ameanza kusoma Bible," Dylan akatania.
"Ahahahah... hakuwahi kuisoma kwani?" akauliza Shani.
"Walikuwa wananisema sana huyu na baba yake ikabidi nianze," akasema Jaquelin.
"Umeimaliza?" akauliza Shani.
"Nilisoma kama mistari miwili hivi... mpaka leo sijagusa tena..."
"Haya sasa..." akasema Dylan, nao wote wakacheka pamoja.
Dylan alikuwa amekaa karibu na Grace huku mke wake huyo akiwa amemwegamia kidogo, lakini sasa akajitengeneza vizuri na kuweka mkao uliowaambia wanawake hao kuwa alitaka kusema jambo fulani la muhimu, hivyo wakamwangalia kwa umakini.
"Kuna vitu huwa vinakuja na kwenda... kama vile muziki fulani mzuri ukiingilia kipindi fulani unakuwa bonge la buzz, lakini baada ya muda mwingine unakuja na kuufunika..." akaanza kusema.
"Ahahah... ndiyo ni kweli," akasema Leila.
"Ila kama ni kitu fulani kisichofunikwa hata kama muda mrefu utapita kadiri gani... ni upendo wa mzazi kwa mwanaye. Kuna jamaa aliwahi kusema, 'huwa hatujui kikamili upendo wa mzazi mpaka na sisi watoto tukija kuwa wazazi pia...'"
"Ndiyo... kweli kabisa..." Shani akakubali.
"Yeah... kwa hiyo ingawa hata hatutaweza kuonana tena na wazazi, au wapendwa wetu... upendo wao kwetu ni kitu ambacho hakitaweza kamwe kufutika wala kusahaulika. Baba, aunt Camila, na Baraka... wote tuko nao bado... kwa kuwa wataendelea kuishi mioyoni mwetu milele. Mambo yote yaliyotokea, mazuri na mabaya, yametufikisha sisi sote kwenye wakati huu. Kwa hiyo tunapaswa kuendelea kuishi kwa kushukuru juu ya kila zawadi Mungu alizotupatia, na kujitahidi kuonyesha upendo mwingi hata zaidi kwa wenzetu..." Dylan akaongea kwa busara.
"Uko sahihi Dylan," akasema Jaquelin.
Grace akatabasamu na kusema, "Maneno mazuri love... asante sana. Zawadi kubwa tuliyonayo ni uhai, na pia..."
"Marcelyn hahahah..." akamalizia Shani.
Wote wakatabasamu kwa furaha na kumwangalia mtoto. Yeye pia alikuwa amegeuka na kuwaangalia baada ya kusikia jina lake likitajwa na Shani, hivyo wakaanza kumsemesha. Dylan na Grace wakashikana viganja vyao kwa upendo na kumtazama binti yao huku wanatabasamu, naye Marcelyn akatabasamu pia kwa furaha.
★★★★★★★★★★★★
MWISHO
★★★★★★★★★★★★