Simulizi : Facebook Imeharibu Maisha Yangu

Simulizi : Facebook Imeharibu Maisha Yangu

SEHEMU YA 21

"Acha uoga bro mbona hata sisi babu yetu alikuwa chifu? kwani chifu na mbunge nani zaidi" alitania Rosemary kumwondoa hofu kaka yake.

Mapokezi waliyoyapata kutokea kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo yaliwashangaza mno waliwakuta watu wa kuwapokea na kwenda nao kwenye gari mbili walizokuja nazo,waliwafikisha hadi getini ambapo kina dada wawili kwa heshima kabisa waliwaongoza hadi sehemu maalum iliyoandaliwa kwa ajili yao,japo usoni waliuficha mshangao wao lakini moyoni uliwajaa tele.

Adam akiwa ndani ya suti nyeusi wanazotumia wanasheria katika shughuli zao na Rosemary aliyevaa suti pia walielekezwa wapi walipo wazazi wa Reshmail wakaenda kutoa salamu zao,ilikuwa ni hafla kubwa sana ndugu,jamaa na marafiki wapatao miamoja walikuwa wamealikwa na mheshimiwa huyu. Ilikuwa kama harusi kwa asiyejua lakini ulikuwa utambulisho tu.

Bwana na bibi Manyama walipendeza kwelikweli na walikuwa na kila haki ya kuitwa wakwe na Adam. Furaha ya Bi. Gaudencia ilificha chuki aliyokuwa nayo moyoni dhidi ya Adam kwa kumchukua mwanae ambaye ndio alikuwa anampa raha zote za dunia.

Hadi hafla inafikia tamati majira ya saa mbili usiku kila mtu alikuwa amepata furaha kubwa sana,wabunge na madiwani ambao ni marafiki wa karibu wa Manyama walitoa zawadi nyingi kwa wawili hawa huku babu yake Reshmail akitoa mawaidha yenye maana kubwa sana katika maisha waliyotarajia kuyaishi Reshmail na Adam siku za usoni.

Mzee Manyama kwa ombi la mwanae aliwasiliana na wazazi wa Adam kuwa muda wa mapumziko ya siku tano alizobakiza Adam amalizie katika familia yake,hapakuwa na kinyongo wala kipingamizi chochote walikubali kwa moyo mmoja na Adam akaendelea kuishi pale huku dada yake akirejea Mwanza kwa usafiri wa ndege ambao gharama zote zilikuwa juu ya mheshimiwa Manyama.

Kila alipowasiliana na wazazi wake Adam hakusita kuelezea upendo wa kipekee anaoupata kutoka familia ya Reshmail hata wao walifarijika sana.

***********************
 
SEHEMU YA 22

Ilikuwa jumapili moja tulivu sana baada ya kutoka kanisani familia yote akiwemo pia Adam,baba yake Reshmail aliongozana na mwanae kwenda mjini kwa lengo kuu la kuonana na walimu mbalimbali wa masomo ya ziada(Tution) watakaompendeza Reshmail basi waweze kumfundishia nyumbani.

Huku nyuma alibaki Adam pamoja na mkwewe (Mama Reshmail) baada ya kupata kifungua kinywa Adam alimwaga mkwewe kuwa anaenda kuzungukazunguka bustanini

"Tena nilitaka nikwambie leo unataka uondoke hata bustanini hujawahi kufika,afadhali nenda mwanangu" alijibu mama Reshmail.

Ulikuwa mpango kabambe uliosukwa na Bi. Gaudencia,kwa dhumuni kuu la kumwondolea mamlaka Adam ya kuwa na Reshmail. Kwa kuwatumia vijana kutoka katika ngome ya vigogo,ngome maalum iliyokuwa inatumiwa na watu wenye pesa zao kwa ajili ya kuwatenda vibaya watu wanaoonekana kuingilia mambo yao aidha kimapenzi au kibiashara.

Alipoaga anaenda bustanini Gaudencia alitumia fursa hiyo kupiga simu kwa wanaume hao wa shoka ambao tayari alikiwa ameelewana nao bei.

"Ndani ya dakika tano tutakuwa hapo" ndio jibu lililotolewa upande wa pili
Bila kuongezea lolote Bi.Gaudencia alikata simu yake na kutoka nje.

"Babu kwa mama Veneranda si unapajua?" alitoa swali hlo Bi. Gaudencia kwenda kwa mlinzi wao wa getini.

"Ndio si yule mama anayesuka pale mbele"

"Hapo hapo haya haraka nenda kaniangalizie kama kuna foleni kubwa" aliamrisha Bi. Gaude na mlinzi akatii amri hiyo haraka haraka akaondoka katika lindo lake akaenda kutimiza amri ya bosi wake.
Baada ya dakika takribani kumi alirejea mlinzi yule

"Yupo mmoja tu anamaliziwa" alileta taarifa hiyo kwa furaha.
 
SEHEMU YA 23


"Haya mi ninatoka nimemwacha Adam ndani amelala akiamka mwambie nimetoka kidogo" alisema mama Reshmail huku akiondoka.

"sawa bosi nitamwambia"

Masaa mawili badae alirejea akiwa amesukwa tayari nywele zake,ni muda huohuo Reshmail na baba yake walikuwa wametoka mizungukoni, walimkuta Gaudencia anatokea ndani.

"Babu Adam alivyoamka ameenda wapi? au bustanini?"Aliuliza Gaudencia na kuongezea

"Maana nimegonga chumbani kwake kimya, hebu Reshmail ingia ukamwangalie ndani mwake humo huenda amelala bado" kwa mwendo wa maringo lakini harakaharaka Reshmail alijongea ndani.

"Babu unasema Adam hajatoka?" Resh aliuliza baada ya kurejea akiwa na hofu kidogo usoni.

"Hajatoka na mimi hapa sijatoka tangu mama alipoenda kusuka na kumwacha Adam amelala" alijieleza mlinzi yule jibu lililopokelewa kwa furaha na Bi.Gaudencia.

Jambo gumu zaidi kwa ambao hawakujua janja ya mama huyu ni kwamba simu ya Adam ilikuwa haipatikani hali hiyo ilileta wasiwasi sana, walisubiri huenda atarudi hadi jioni hali ilikuwa tete ndipo mzee Manyama alipoamua kupiga simu kituo cha polisi maeneo ya jirani kwa sababu alikuwa mbunge msako ulianza usiku huohuo.

Siku tatu zilipita bila taarifa yoyote kutoka katika kituo cha polisi,Reshmail alikuwa amepooza sana kupita maelezo mara kwa mara alimpigia baba yake simu na kuuliza kulikoni lakini jibu bado lilikuwa lilelile kuwa hajapatikana.

"Mama niache tafadhali,tena niache nasema upuuzi wako siutaki tena niache!" alifoka Reshmail pale mama yake alivyomkuta amekaa sebuleni na kujaribu kumpapasa huku akimpa pole ya kupotelewa na Adam wake ghafla.
 
SEHEMU YA 24

"Mwanangu usiwe na hasira kiasi hicho polisi watafanikisha upelelezi na watamrejesha Adam akiwa mzima wa afya" alibembeleza Bi. Gaudencia lakini Reshmail hakujibu kitu akajiondokea akiwa ameuvuta mdomo wake sana.


Siku ya tano polisi waliopewa jukumu la kufanya upelelezi huo walirejea na taarifa yao huku wakiambatana na ushahidi. Zilikuwa nguo aliyokuwa amevaa Adam kwenda kanisani ikiwa na matundu sita ya risasi na ikiwa imetapakaa damu pote, suruali ilikuwa na matundu matatu ya risasi.

"Hapana hawezi kuwa Adam hata kidogo nasema hawezi kuwa yeye" alifoka Manyama huku akiwa wimawima mbele ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai jiji la Dar-es-salaam Chacha Boniphace au maarufu kama Chacha B.

"Mheshimiwa lakini huu ni upelelezi wa awali tunaendelea zaidi na zaidi tutazidi kutoa taarifa kadri tunavyopata majibu mapya" alijieleza kwa utulivu bila wasiwasi kabisa jambo ambalo kidogo lilirejesha amani ya Manyama japo hofu tayari ilishaukumba moyo wake kwamba huenda Adam ameuwawa tena kikatili.
 
SEHEMU YA 25


Ilikuwa ni shughuli pevu kwa Reshmail kuamini kile ambacho alikuwa anaelezwa na baba yake kwamba Adam anadhaniwa kuuwawa kwa risasi nane kisha mwili wake hauonekani. Bi. Gaudencia tayari alikuwa anaangua kilio kikubwa hata kabla maelezo hayajaisha ikawa kazi kwa mumewe kumbembeleza.

"Mke wangu Adam hajafa ila inadhaniwa pia upelelezi bado unaendelea jamani,ukilia hivyo unakuaribisha msiba mama watoto sawa" alibembeleza mzee Manyama huku amemkumbatia mkewe.

"Baba haiwezekani baba haiwezekani nguo za Adam zipatikane katika hali hiyo halafu mnasema hajafa,jamani Adam wangu wamemuua"

alipiga mayowe Reshmail ikamlazimu mzee Manyama kufanya kazi mara mbili jambo ambalo lilimtoa jasho mzee huyu.

"Reshmail mwanangu,tulia hiyo siyo taarifa rasmi jamani ni majibu ya awali mbona mnanifanyia hivyo au mnataka nipate presha nife?" alijieleza Manyama huku akijifuta jasho kwa kutumia shati lake.

Reshmail mbio mbio akaondoka pale sebuleni akaanza kuzipanda ngazi kuelekea chumbani kwake huku akilia,mzee Manyama nae huyo nyuma yake.

"Reshmail mwanangu,njoo malkia wangu,njoo mwanangu"

aliyazungumza hayo huku akimkimbiza kwa nyuma. Wakati huo Bi. Gaudencia tayari alikuwa amenyamaza kimya kabisa,akijaribu kupikicha macho yake.

Reshmail hakusimama hadi chumbani kwake akajifungia,baba yake alibembeleza mpaka akachoka hakupata jibu zaidi ya kilio cha kwikwi kutoka ndani.

"Baba Resh twende chumbani mume wangu,twende utakaa hapa hadi saa ngapi cha msingi tumwombe Mungu asije akajidhuru mwanetu"

Gaudencia alimnyanyua mumewe wakajikongoja kuelekea chumbani kwao,Manyama akiwa amelegea kabisa.
 
SEHEMU YA 26

Asubuhi ya siku iliyofuata naibu waziri wa ulinzi na usalama,alifika na msafara wake wa magari matano kwa mbunge Manyama kuja kutoa pole ya kutokewa tukio hilo lenye utata kwa mwenzao.

Shughuli ngumu iliyokuwa mbele yao ni jinsi gani watawaeleza wazazi wake Adam ambao hadi dakika hiyo waliamini Adam yupo salama na mwenye furaha kwa mchumba wake Reshmail,Manyama alimuomba waziri ashughulikie hilo suala na bila kupoteza muda alinyanyua simu yake ya mkononi na kutoa taarifa hiyo kwa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mwanza pamoja na mawasiliano anayoweza kumpata baba yake Adam.

Ilikuwa vigumu sana kwa baba Adam kuelewa anachoelezwa lakini kwa kadri ya uwezo wake na taaluma yake mkuu huyo alifanikiwa kumwelewesha ambapo baba yake Adam aliondoka akiwa na matumaini kwamba ipo siku Adam atapatikana.

Nyumba nzima ya kina Adam ilipooza sana dada yake Adam (Rosemary) alikuwa analia muda wote kwa uchungu hakuamini kwamba siku ile pale uwanja wa ndege alivyosindikizwa na familia nzima ya mhe.Manyama ndio ilikuwa mara ya mwisho kumwona kaka yake kipenzi(Adam).

Uongozi wa polisi uliifikisha taarifa hiyo pale chuoni ambao pia walipokea kwa simanzi kubwa.

"MAUAJI YA KUTISHA",

ndivyo mandishi meusi kabisa kwenye magazeti mbalimbali yalisomeka,hali hiyo ilithibitisha kabisa kuwa Adam hayuko hai tena.

Picha yake iliyoambatanishwa na habari hizo akiwa na mtoto wa mbunge iliteka na kuumiza mioyo ya watu wengi hasahasa vijana.

"Tumempoteza mwanasheria"

ndilo neno la pamoja walilosema wasomi wa chuo kikuu cha mtakatifu Augustino Mwanza katika misa ya pamoja kumwombea mema Adam kama yupo hai au kumtakia pumziko jema la milele kama tayari Mungu ameichukua roho yake,kila uso ulikuwa na simanzi kubwa ilikuwa kama tamthilia.

Reshmail alikuwa kama zezeta,hamwelewi mtu yeyote,roho yake ilimwambia kwamba mama yake mzazi anahusika kwa namna moja au nyingine katika tukio hili lililojaa utata.

Lakini ataanzia wapi kumweleza baba yake,atajisikiaje mzee Manyama akigundua kwamba mke na mtoto wake walikuwa katika ndoa haramu ya siri ndani ya nyumba yake.
 
SEHEMU YA 27

"Hapana sitaki kuongeza tatizo juu ya tatizo nitasubiri liwalo na liwe,kama Mungu alimpanga Adam awe wangu naapa sitaolewa na mwingine kamwe,lakini kama hakuwa halali yangu basi ataletwa mwanaume duniani kwa ajili yangu tena"

Alijipa ujasiri wa hali ya juu Reshmail huku akijipigapiga kifuani.

"Nitarejea shule na nitasoma tena kwa bidii sana,sitamwaza mwanaume yeyote tena alikuwa Adam na atabaki kuwa Adam hadi Mungu aamue tena"

aliendelea kujipa matumaini.

"Bibi yangu aliniambia maneno ya mdomo huumba halisi,na nina uhakika ninachokiongea kwa mdomo wangu Mungu ataniumbia"

Aliendelea kuongea huku machozi yakifumba macho yake na kitambaa alichokuwa anatumia kujifuta kilikuwa kimelowana tayari kwa wingi wa machozi alikuwa kama yatima vile, Resh alikuwa akifungasha baadhi ya mizigo yake tayari kwa kurejea shuleni tena,tangu tukio la Adam kupotea hakuna aliyetegemea hata siku moja Resh atawaza kurudi tena shuleni kwani waziwazi akili yake ilionekana kuathirika kwa kiasi kikubwa kwa kumpoteza Adam katika mazingira yasiyoeleweka.
 
SEHEMU YA 28


"Baba kesho narejea shule si unajua tayari shule imefunguliwa?" Reshmail alimkurupua mzazi wake huyo kutoka alipokaa kwa mshangao

"Umesema nini malkia wangu!" alihoji Manyama huku akiwa wima

"Narejea shule kesho" kwa msisitizo na tabasamu alijibu Reshmail.

Mzee Manyama hakuamini kwani alikuwa akiwaza ni namna gani atamshawishi mwanae aweze tena kurejea shuleni baada ya matatizo yote yaliyojitokeza kwa mchumba wake Adam ambaye hadi wakati huo bado mwili wake ulikuwa haujapatikana wala taarifa yoyote zaidi ya nguo zikiwa na matundu ya risasi na damu.

"asante sana mwanangu nakupenda sana" mzee Manyama aliongea kwa furaha huku akimkumbatia mwanae.

Tangu kupotea kwa Adam aliyehisiwa kuwa tayari amekufa kulipokelewa kwa hisia tofauti na wananchi huku asilimia kubwa ikiegemea upande wa imani potofu za kishirikina wakihusisha tukio hilo na utajiri alionao Mh. Manyama na uchaguzi uliokuwa mbele yake.

**** *******
 
SEHEMU YA 29



"Wamemtoa mwanangu kafara ili waongeze utajiri,nilimwambia Adam aoe msukuma mwenzake ona sasa,watoto wa siku hizi wabishi wanajifanya wanajua sana na elimu yao inawadanganya"

mama yake Adam alikuwa analaani vikali mbele ya mume wake wakiwa ndani ya nyumba yao maeneo ya Igoma kwa 'one-way'

"Usiseme hivyo mama Adam kumbuka sisi ni wakristu,tumwachie Mungu yeye ndio atajua nini cha kufanya"

Babaye Adam alimtuliza mkewe huku akimgongagonga mgongoni kwa kutumia kiganja cha mkono wake wa kuume.

Mawasiliano baina ya familia hizi mbili ya Adam jijini Mwanza na ya Reshmail jijini Dar-es-salaam yalikuwa yamekatika licha ya baba yake Adam (mzee Michael) kutangaza kuwa kutoka moyoni mwake amesamehe yote yaliyotokea na anaamini ni mipango ya Mungu.

Lakini kinyongo kilionekana dhahiri kwa matendo,upendo wa zamani haukuwepo tena jambo hilo lilimfadhaisha sana mzee Manyama kiasi cha kukondeana na kukosa umakini katika utendaji wake wa kazi jambo lililoishusha sana heshima yake kama mbunge aliyekuwa anaheshimika sana kuanzia bungeni hadi jimboni kwake,

Wapinzani walitumia fursa hiyo kumchafua hasahasa na kweli uchafu huo ukakubalika kwa wananchi kwa ujumla Manyama hakuwa na lake tena pale,wananchi walimpuuzia sana tofauti na zamani na hata hiyo miaka miwili iliyobaki wananchi waliiona kama ni mingi sana kuwa na kiongozi wa aina yake.

Kuliko fedheha yote hiyo Mh. Manyama kwa hiari yake mwenyewe alipitisha kura ya maoni ya wananchi kuhusu imani waliyonayo kwake kama mbunge wao.

Asilimia 70 ya waliopiga kura walidai hawana imani naye huku asilimia kumi na nne tu ndio wakidai bado wana imani naye na kura zilizobaki zikiharibika,rasmi Manyama akawa ametolewa bungeni na katika uchaguzi mdogo uliofanyika akachaguliwa mbunge kutoka chama cha upinzani na maisha yakaendelea huku Mh.Manyama akiendelea na biashara zake mikoani.

* **
 
SEHEMU YA 30

Adam akiwa pale bustanini alivamiwa ghafla na wanaume wawili wa shoka wakiwa na bunduki,ishara ya kidole mdomoni ilimfanya atulie tuli kisha wakamwonyesha ishara kwamba awafuate alifanya kama walivyotaka hadi kwenye gari iliyokuwa imepaki pembeni kidogo ya nyumba yao Adam alishangazwa sana na ukimya uliokuwepo hakuwepo mlinzi wala mama mkwe wake.

Safari yao ilikwenda mpaka Iringa gari iliyokuwa na vioo vyeusi 'tinted' ilimzuia Adam kujua ni wapi alipo,gari ilizimishwa ndani ya jumba kubwa sana ambapo alipelekwa kwenye chumba kikubwa tu,hofu kubwa ilimtawala hakujua kwa nini yuko pale,hakupigwa wala kupewa bughudha yoyote,hali hiyo ilzidi kumshangaza

"au ndio wachuna ngozi" alijiuliza Adam kwa hofu tele.

Hayo ndio masharti ambayo mama Reshmail alitoa kwa vijana aliowapa tenda hiyo ya kumtorosha Adam pale nyumbani. Shida yake haikuwa kumtesa Adam bali kumweka mbali na mwana (Reshmail) ambaye alikuwa amempagawisha ipasavyo katika mapenzi ya jinsia moja.

Suala la pesa halikuwa tatizo hata kidogo alichohitaji ni kutimiziwa alichotaka. Mkataba wa miaka mitano ndio alioingia na watu hawa kukaa na Adam bila kumruhusu kutoka nje ya jingo.

Bi Gaudencia aliamini kwamba kwa kutokomea Adam mbele ya uso wa Reshmail ilikuwa fursa nzuri ya kurudisha tena uhusiano wake na Reshmail ambao ulikuwa unaelekea kufa lakini kinyume chake alikuwa ameibua chuki kubwa baina yake na mwanae ?heri wote tukose kama ni hivyo? alijiapiza mama Reshmail baada ya kuona dalili za kumshawishi Reshmail hazipo tena

Alikuwa ni Reshmail mwingine kabisa mkasa uliomkumba ulimbadilisha sana na kuitanua akili yake sana,Eveline naye alisikitishwa na yaliyomkumba shoga yake akajitahhdi sana kuwa karibu naye kumpa moyo huku akijiepusha sana kufanya vitendo ambavyo vitamkumbusha Resh jinsi alivyoweza kukutana na Adam.

Ni katika kujiepusha na kumkera rafiki yake huyo kipenzi Eveline akajikuta amefuta picha za uchi na filamu za ngono katika kompyuta yake akawa si mtu wa kutoroka shule,hakuwa tena mtu wa wanaume na hatimaye akawa Eveline wa kuigwa na wanafunzi wenzake jambo hilo liliwaduwaza sana wanafunzi pale shuleni lakini ndio hivyo Eve alikuwa amekubali mabadiliko katika maisha yake.
 
SEHEMU YA 31

Juhudi zao katika masomo ziliendelea kuwaweka katika nafasi nzuri ya kufanya vizuri mtihani wao wa mwisho. Hawakuyazungumzia tena yaliyopita tena walijadili mapya na yanayowanufaisha

"Eveline wewe ni kama dada yangu nakupenda sana"

"Nakupenda pia Reshmail umebadili maisha yangu moja kwa moja nina maisha mazuri sasa" alijibu Eva kwa upole huku akimwangalia Reshmail aliyekuwa anaishusha chandarua yake aweze kulala. Ni kweli walitokea kupendana wawili hawa.

"Hivi Resh una mpango bado wa kusomea uhasibu mi lazima niwe mhasibu"

"Mh! unavyojiaminisha utadhani tumefaulu tayari" alijibu Resh.

"He! mi najua sisi kufaulu kwetu sio swali ni jibu,swali ni je tunaenda chuo gani na kusomea nini." alijiaminisha Eveline.

"ok! nilidhani nitasomea uhasibu lakini kwa heshima ya Adam nitasomea sheria" alijibu Reshmail kwa furaha.

"Mh! na upole wako huo na mambo ya kutoa hukumu wapi na wapi? mwenzio naangalia ankara" alisema Eva.

"Wala hata siendi kuhukumiana naenda kwa heshima tu" alisisitiza Reshmail.

"Mh! haya mheshimiwa hakimu napenda kujitetea kama ifuatavyo"

Eve alitania akifuatiwa na kicheko kikubwa kutoka kwa Reshmail.


Maisha yaliendelea vyema sana tu japo yalikuwa maisha ya mashaka Adam aliruhusiwa kuongea na kuuliza kila kitu kasoro swali moja tu "Kwa nini niko hapa?",ndio hakuruhusiwa kuliuliza hata kwa mbali,watu wote pale hawakuwa na ubaya nae hata kidogo,hawakumtesa,hakugombezwa wala hakufanya kazi,alipewa huduma zote za msingi,aliweza kutoka nje na kwenda bustanini lakini nje ya geti hakuruhusiwa.

Tayari aliyazoea maisha haya lakini kumbukumbu ya jinsi alivyochukuliwa ndani ya jumba la wakweze bila kupata msaada wowote ule "Nani atakuwa nyuma ya haya yote mlinzi alikuwa wapi? Mama Resh je?" alijiuliza sana bila kupata wa kumpa jibu.

"Hivi unaitwa dada nani vile?" Adam alimuuliza dada mmoja ambaye kila baada ya siku tatu alikuja kufanya usafi katika chumba chake.
 
SEHEMU YA 32

"Naitwa Beatrice Cosmas niite Bite" alijibu huku anafuta vioo kwa dirisha la chumba cha Adam.

"Una jina zuri wewe mh!"Alisanifu Adam.

"Asante wewe ni Adam eeh!" aliongezea yule binti huku akiwa ameacha shughuli yake aliyokuwa anafanya.

"Ndio mimi ni Adam! samahani nikuulize maswali machache"

"Uliza tu lakini sitakujibu sasa hivi"

"Kwa nini?"

"We uliza yote ndo nitakwambia kwa nini"

"Hivi hapa ni wapi? kwa nani? na kwa nini nipo hapa?"

"Ndio hayo matatu tu?...sawa nitakujibu kwa sharti dogo sana yaani"

"Sharti gani hilo mi nipo tayari"alitoa uhakika Adam bila hata kulijua sharti lenyewe.

"Sikia Adam sina haja ya kuzunguka zunguka nina mwaka wa pili hapa kitu kinaitwa mwanaume katika mwili wangu ni kama ndoto sasa ni wewe wa kutii kiu yangu na mimi nitajibu maswali yako" alijieleza Bite,jambo ambalio lilikuwa zito na la kumshangaza Adam.

"Mh! au ndo mtego tena kutoka kwa Reshmail? dah! ikiwa hivyo nitaaibika kweli mimi"Alijiwazia Adam kwa mashaka makubwa kabla ya kujibu.

"Basi utakuja kunijibu baadaye!" alisema Adam.

"Haya usiku na wewe jiandae" alijibu na kuaga Bite.

Hayawi hayawi mara yakawa usiku wa saa tatu,Bite tayari ndani ya chumba cha Adam ndani ya khanga moja peke yake.
 
SEHEMU YA 33

"Haya nipe nikupe hakuna longolongo hapa" alizungumza Bite.

"Subiri taratibu basi,sikiliza" alianza kujitetea Adam wakati Bite anajisogeza kitandani,Adam alikuwa amechelewa tayari joto la Bite lilipenya katika mwili wake na kumchanganya hadi kujikuta akifanya kinyume na alivyotarajia kwamba atafanikiwa kutegua mtego wa Bite badala yake alikuwa ameshafanya mapenzi na Bite.

Kwa Bite ulikuwa ushindi mkubwa sana kwani tangu aletwe hapo kuwa msaidizi wa kazi za ndani ya vyumba hakuwahi kutoka nje ya jengo hilo,sio kwamba alikuwa amefungwa hapana kila kitu kilikuwepo ndani kila siku pia alikuwa ameridhika kuwa hapo.

"Hapa ni Iringa,nimejibu swali lako la kwanza tuendelee tena nikujibu swali la pili na tatu" alisema Bite kwa shauku kubwa sana.

"Hapana Bite imetosha kwa leo sijisikii vizuri,siku nyingine basi sawa!" alidanganya Adam na Bite hakuwa mbishi akambusu Adam shavuni akajiondokea zake.

Ilimchukua takribani siku tano Bite kugundua kwamba tayari ameshika ujauzito jambo ambalo halikuruhusiwa katika jumba hilo na alipewa onyo kali wakati anaingia hapo. Kwa usalama wake na Adam alifikiria suala la kutoroka lakini haya yote aliyafanya baada ya kuongea na Adam na kumweleza hali halisi.

Ni katika wasaa huo alimweleza Adam chanzo ambacho kinaweza kuwa kimemsababishia yeye kuwepo pale

"Umemchukulia kigogo mpenzi wake,umemendea mtoto wa kizito au umemkataa kimapenzi mtu maarafu" hizo ndizo zilikuwa baadhi ya sababu alizoorodheshewa na Bite,lakini kwake yeye aliona hakuna hata moja inayomuhusu kwani wazazi wote wawili wa Reshmail walimpenda sana hakuwa tayari kuweka hisia kwamba pengine moyoni wanamchukia.

"Usijali lakini hutakaa milele humu,huwa unafika

Muda aliyekuweka humu akiridhika unatoka.

"Nitamlea mtoto,napenda watoto hata kama usipokuwa mpenzi au mume wangu nitampenda sana na nitamwita....."

"Christian akiwa mvulana au Christina akiwa msichana" alidakia Adam ambaye kwa mbali alianza kumtamani Bite kimapenzi.

* * *
 
SEHEMU YA 34


Biashara za baba yake zilikuwa zinaendelea vizuri na skendo lake lilikuwa linafifia taratibu. Hadi anamaliza kidato cha sita Reshmail mapenzi kwa wazazi wake yalikuwa palepale na japo hakutaka kumwongelea Adam jena alikuwa na picha yake waliyopiga pamoja siku moja kabla ya tukio lile la kushangaza na kuumiza.

Reshmail kwa ruhusa ya wazazi wa Eveline alienda nae mpaka kwao ambapo walikaa wote kwa siku tano kisha akarejea tena Arusha.

Urembo wa Reshmail ulipagawisha kila mwanaume na hata baba yake ilifikia kipindi akakiri kwamba kweli pale alizaa mtoto mmoja wa kipekee na kweli alikuwa wa kipekee. Mama Resh bado alikuwa na matamanio lakini kwa sasa alimwogopa sana Reshmail tofauti na miaka mingi iliyopita.

"Baba na mama wiki ijayo nataka kwenda Mwanza kwa wazazi wa Adam" Resh alitoa hoja yake wakiwa mezani wanakula.

"Wapi? Mwanza! hawatakuelewa mwanangu utakuwa kwa maksudi kabisa unafufua shari iliyopoa tayari"

Kwa busara tele na upole mzee Manyama alimweleza mwanae ambaye pia aliyapokea kwa nidhamu ya hali ya juu na kichwa chake kuyakubali kuwa yana maana kubwa ndani yake.

"Nimekuelewa baba sitaenda tena" alijibu kwa unyenyekevu sana Reshmail.


Matokeo ya kidato cha sita yalipotoka hayakuwa ya kushangaza sana kwa upande wake kwani alikuwa amevuna alichokipanda. Reshmail alikuwa amepata daraja la kwanza na ndivyo alivyotarajia,furaha yake iliongezeka baada ya kumwona katika orodha Eveline Maige rafiki yake kipenzi naye akiwa amepata daraja la kwanza huku wakitofautiana pointi kadhaa.

Akiwa anajiandaa kumpigia simu tayari simu yake iliwakawaka na kuandika "pacha" jina ambalo alikuwa amemwandika Eve katika simu yake,badala ya kuongea wote kwa pamoja wakaanza kucheka,walicheka sana hadi simu ilipokatika. Zilikuwa ni furaha kutoka moyoni,kwa nini wasifurahi wakati ndoto zao zilikuwa zinatimia?

Tanzania Commission of Universities (T.C.U) ilipotoa uchaguzi wa kwenda vyuoni Reshmail kama alivyopenda alichaguliwa chuo kikuu cha mtakatifu Augustine Mwanza kwa masomo ya sheria huku Eveline Maige akipelekwa Mzumbe chuo kikuu kwenda kuchukua masomo ya uhasibu shahada ya juu.
 
SEHEMU YA 35

"Ndugu hakimu naomba kujitetea!" Eve alimtania Resh utani wao wa shuleni siku walipokuwa wanaagana.

Walikuwa wametenganishwa hatimaye lakini mawasiliano yao yalidumu

Kama alivyojiwekea kiapo chake cha kutopenda hovyohovyo ni hivyohivyo alivyoingia pale chuoni,hakuringia uzuri wake lakini hakutaka pia usumbufu unaopitiliza kutoka kwa wanaume yaani kwa kifupi alikuwa na msimamo mkali sana,ni rafiki yake (Eve) pamoja na wazazi wake ambao wangeweza kubashiri sababu hasa inayomfanya binti huyu awe hivi na si mtu mwingine pale chuoni.

Maringo yake yalifichwa na werevu wake darasani,kwani ilikuwa ni warembo wachache sana wa aina yake waliofanya vizuri kimasomo,jambo hilo lililowavutia waalimu wengi sana na wanafunzi ambao wanapenda maendeleo kimasomo. Reshmail hakuwa mtu wa mambo mengi hakunywa pombe wala kwenda kumbi za starehe usiku starehe yake ilikuwa ni kusoma na michezo.

Mnamo mwezi wa pili michezo ya FAWASCO ilipoanza michezo hiyo inayohusisha vitivo vyote pale chuoni,kwa maksudi alichaguliwa kuwa mhamasishaji kwa wasichana wajibu alioufanya vizuri ipasavyo na kikubwa zaidi akawa pia mdhamini mkubwa sana. Moyo wake wa kujitolea uliwavutia sana wanadarasa wenzake ambao baadhi walimpenda huku wengine wakidai ana maringo, msimamo wa Reshmail ulibaki palepale.

Mwaka wa pili pale chuoni ndio ulikuwa mbaya kwake. Darasa walilolitumia mwaka wa pili wanafunzi wa kitivo cha sheria,lililojulikana kama Mombasa Raha kwa mbele lilikuwa na picha kubwa sana ya Adam ambayo ilikuwa pembeni ya ubao wa kufundishia hiyo ikimaanisha kwamba kila atakapoingia darasani lazima aione,"ADAM THE GREAT" yaliandikwa maandishi haya chini ya picha kubwa ya Adam.

Amani,ikatoweka kabisa moyoni mwake kumbukumbu mbaya za kumpoteza mpenzi wake Adam zikaanza kumrejea kwa kasi sana.Reshmail akaanza kujihisi yeye ndiye chanzo cha yote hayo,tofauti na waalimu wake hakuna mwanafunzi aliyemfahamu Adam zaidi ya kujua tu historia ya yaliyomkuta na wengi kuichukulia kama simulizi tu ya kusadikika. Reshmail alianza kuwa mtoro darasani na hata alipoingia badala ya kumwangalia na kumsikiliza mwalimu,mawazo yake yote yalivutwa na picha ya Adam yenye tabasamu pana mara zote aliamini inamuangalia yeye na kumlaumu kwa kumkatisha masomo yake kwa penzi la mtandaoni.

"Adam stop blaming me!!(Adam usinilaumu)" alipiga kelele kwa nguvu Reshmail bila kujitambua.
 
SEHEMU YA 36



Mwalimu alimshangaa na hakuelewa kilikuwa kimemsibu nini "Is she dreaming? (Anaota?)" aliuliza mwalimu Sijjo aliyekuwa anawafundisha somo la mawasiliano (Communication skills),darasa zima likacheka kwa fujo sana,lakini Reshmail alikuwa analia huku akitetemeka sana,kwa ghadhabu akasimama na kutoka nje.

Japo ulikuwa ni mwezi mmoja tu tangu waanze masomo ya mwaka wa pili lakini
tabu na mateso aliyokuwa ameyapata yalitosha kumshawishi kuwa huenda amesoma hapo kwa miaka kumi.Wazazi wake hawakuwa na la kufanya,Eveline alibaki kumwonea huruma shoga yake huyu alijaribu mara kwa mara kumpigia simu lakini haikuwa tiba ya tatizo la Reshmail.

Ni kweli Reshmail asingeweza kujilazimisha kuwa na furaha kwani ni yeye aliyemshawishi Adam awe nae kimapenzi na ni yeye huyuhuyu alimshawishi Adam aende kwao kwa ajili ya kujitambulisha na safari hiyo ikawa ya mwisho ya Adam.

"Nikiwaambia waalimu wangu watanielewaje,na hata wakinielewa itakuwaje wanafunzi wenzangu wakijua siri hii? watajenga picha gani tena kuhusu mimi, mh! niepushe na hali hi bwana,kama uliweza kuniondolea mawazo haya hadi nikamaliza kidato cha sita vyema hebu baba na sasa ondoa tena na hili jaribu zito mbele yangu na jina lako lisifiwe."

aliweka ombi fupi Reshmail katika mawazo yake hayo. Lilikuwa ni jambo gumu sana kwa Reshmail alikonda sana na punde si punde maneno ya wakosaji yakaanza tena "Mh! kumbe ndio maana anakataa wanaume kumbe anaishi kwa matumaini maskini,dada mrembo kama huyu" yalisikika maneno hayo katika vijiwe vya wanafunzi pale chuoni.

Ilikuwa ni kero kubwa kila alipokatiza vidole vilimwelekea yeye umaarufu wake wa awali kwamba ni mrembo ukaongezeka maradufu karibia chuo kizima lakini wakati huu ilikuwa ni sifa mbaya kwamba ana virusi vya UKIMWI hata yeye aliyasikia maneno hayo yalikuwa yakivuma kwa kasi,hakuwa na uwezo wa kuzuia tetesi hizo

"Wangejua kwamba mi ni bikra na wanayoyasema yote ni uongo,hata wasingenyanyua midomo yao michafu kuropoka upuuzi huo,lakini bila Adam watajuaje?" alijiuliza Reshmail akiwa chumbani mwake katika hosteli ya Ngulelo aliyokuwa amepanga chumba alichoishi peke yake. Marafiki zake taratibu wakaanza kumtenga wakiamini ameathirika,hilo halikumuumiza kichwa kwani alilitegemea sana hasa hasa dhana ya unyanyapaa kwa waathirika iliyokuwa inatawala chuoni hapo.

***
 
SEHEMU YA 37


Bite alifanikiwa kutoroka katika ngome ile kubwa aliyokuwa amehifadhiwa Adam. Kwa jinsi alivyokuwa amezoeleka pale haikumchukua muda mrefu kumshawishi mlinzi amfungulie geti atoke kidogo na ndio ikawa jumla hakwenda mbali sana na mkoa wa Iringa bali aliweka kambi yake maeneo ya Uyole Mbeya mkoa uliopo jirani na Iringa ambapo kipesa kidogo alichoondoka nacho pale ndani alifungua kibanda chake sokoni na kupanga nyumba eneo jirani la Igawilo akianzia maisha ya kulala chini hadi aliponunua godoro.

Biashara ya kuuza nyanya na mbogamboga ilimkimu sana maisha yake kwani wazo wala tegemeo lake halikuwa kununua gari,au kujenga nyumba hapana lengo lake lilikuwa uhai pekee,na shilngi elfu moja alizozipata zilikuwa zinamtosha kabisa.

Alikuwa mchangamfu na mstaarabu sana,wateja walivutika kwake kwa kasi kufaidi ukarimu wake katika biashara.Tumbo lake lilianza kukua taratibu,kina mama sokoni wakaanza kuhisi tayari Bite kapata mjanja Mbeya amemjaza mimba,lakini miezi yake ya kujifungua ndiyo ilifungua akili za waliokuwa na maswali na kugundua kwamba ile mimba alikuja nayo pale na sio kwamba aliipatia pale. Salama bin salmin Bite alijifungua mtoto wa kiume miezi tisa ilipowadia.

"Mh! baba yake atafurahi tena alimpa jina pale tu nilipomwambia nimeshika mimba" Bite kwa furaha tele aliwaambia kina mama wa pale sokoni,akiwemo jirani yake mama wawili,ni hao ndio walikuwa ndugu zake.

"Hongera Bite,sijui ndio unakuwa mama nani vile" Bite alihojiwa na mama wawili

"Mwanangu anaitwa Christian" alijibu Bite huku akibusu kichanga chake hicho ambacho kilikuwa kinarusharusha miguu na mikono yake huku na huko.

Christian alizaliwa akiwa na afya tele na hakusumbuliwa na magonjwa wakati wa ukuaji wake mwaka wa kwanza,ilikuwa furaha kubwa kwa mama yake.

**************

Miaka ilizidi kukatika wazo la Bi. Gaudencia kumtoa Adam katika jumba lile lilikuwepo kichwani mwake kwani udhaifu alioupata Reshmail pamoja na kashfa mbaya anazozipata pale chuoni zilimsononesha sana lakini ataanzia wapi kuificha aibu yake pale ambapo Adam,akasababisha uovu wa mama huyu uwekwe hadharani.

Ni jambo hilo lililomuumiza kichwa mama huyu.
 
SEHEMU YA 38

"Reshmail na baba yake watanielewaje kwa mabaya niliyowafanyia,nimeishusha heshima ya mume wangu aliyekuwa na heshima kubwa bungeni" alizidi kuwaza

Huku Iringa maeneo ya Ruaha Adam alikuwa anauanza mwaka wa tatu,akiishi kama nyumbani kwake,lakini hakuridhika hata kidogo maisha hayo ya ufungwa.

Miaka mitatu ilikuwa mingi sana "Mama na baba yangu wanahisi niko wapi? vipi kuhusu mpenzi wangu Reshmail,hapana imetosha nahitaji kutoka hapa,lakini lazima nijiulize nitatoka vipi hapa katika ngome hii" alijisisitiza Adam japo ulinzi madhubuti ulioongezwa kutokana na kutoroka kwa Bite katika mazingira ya kutatanisha pale ngomeni

***

Mwaka wa pili uliisha hivyohivyo kimateso makali yaliyojawa na kumbukumbu mbaya na isingekuwa kuhamishwa kwa darasa la sheria mwaka wa pili kwenda katika maghorofa ya Mwanjonde chuoni hapo basi Reshmail angefeli vibaya masomo yake kutokana na msongo wa mawazo.

Akiwa mwaka wa tatu afya yake ilirejea tele kwani hakuwa akiiona tena picha kubwa ya Adam machoni pake hali hiyo ya afya kurejea ilizusha msemo mpya tena,tofauti na mwanzo walivyosema ana Ukimwi,sasa walisema "Akikonda ana virusi,akinenepa ameanza kutumia dozi"

Yote hayo alituhumiwa Reshmail lakini kamwe hakuwahi kuthubutu kunyanyua mdomo wake kujibu vijembe hivyo yeye alikuwa mkimya huku akipambana na masomo hadi alipoumaliza mwaka wake wa nne vyema.

Mnamo mwezi wa kumi na moja familia yake yote ilisafiri kuelekea jijini Mwanza kusheherekea kwa pamoja mahafali ya mtoto wao,Eveline ambaye tayari alikuwa kazini baada ya kuwa amemaliza miaka yake mitatu chuoni na kufaulu vizuri pia alijumuika katika kukamilisha furaha hii ya rafiki yake mpenzi huku akiongozana na mchumba wake Benjamin Simon.

Reshmail alifurahishwa sana na ujio wa Eve kwani alizidi kudhihirisha kuwa ni kiasi gani yeye ni rafiki wa kweli.

Yalikuwa ni mahafali makubwa na ya kipekee kuliko yote yaliyowahi kutokea ambapo chuo cha Mt.Augustino kilifanya mahafali ya pamoja na matawi yake yote Tanzania,yaani Iringa,Mtwara na Tabora. Kwa ufupi yalikuwa yamefana.
 
SEHEMU YA 39

Ni katika pirikapirika na pitapita za huku na huko za sherehe hiyo ndipo Reshmail akiwa na Eveline ana kwa ana anakutana na familia ya Adam yaani baba na mama yake,aliwatambua kwa uwepo wa Rosemary yule mdogo wake Adam.

Rosemary alikuwa ndio kwanza amehitimu shahada ya elimu katika chuo kikuu cha mtakatifu Augustino tawi la mtwara hivyo yeye na familia yake pia walikuwepo katika viwanja vya Raila Odinga kusheherekea mahafali yale.

"Mchawi...mchawi!" alianza kupiga kelele mama yake Adam wakati Reshmail akisogea taratibu katika eneo walilokuwepo kwa furaha.

"Uuuwii" alipiga makelele kwa sauti ya juu jambo lililovuruga usikivu katika eneo lile na watu kuanza kumwangalia yeye kama mtu aliyechanganyikiwa, Reshmail na Eve walikuwa wameganda tu na mama Adam akizidi kupiga kelele,

Jitihada za baba yake Adam kumtuliza mkewe hazikufua dafu,mara ghafla mama Adam akakurupuka akiwa na chupa iliyokuwa na soda ambayo haijafunguliwa bado na kwa kasi akaenda kumkabili Reshmail ambaye akili yake ni kama ilikuwa imesimama na umati uliokuwa umemkazia macho kwa kitendo cha kuitwa mchawi ulimzidishia hofu na fedheha kwake, Eve alimshika mkono Reshmail na kujaribu kumvuta watoke eneo lile lakini tayari mama Adam alishawafikia na kwa nguvu kabisa akaituliza chupa ile juu ya kichwa cha Reshmail palepale akaenda chini huku damu nyingi ikimtoka kichwani.

Wanaume watatu akiwemo pia baba yake Adam walifika na kumbeba juu juu,mama Adam ambaye alionekana dhahiri kuwa bado hajaridhika na kipigo alichotoa kwa Reshmail kwani bado alikuwa anaangaza huku na huko kama palikuwa na silaha nyingine. Alikuwa kama mwendawazimu.

Wengine walimbeba Rshmail ambaye joho lake la kipekee kabisa lilikuwa limechafuliwa vibaya na vumbi la uwanja wa mpirawa miguu wa Raila Odinga ambapo ndio sherehe zilifanyika. Hali ya sintofahamu ilitawala sherehe zile kwa takribani nusu saa nzima hadi Reshmail alivyoondolewa na familia yake kuelekea hospitali na mama Adam kutiwa katika nguvu ya dola

***

Halikuwa jeraha kubwa sana nyuzi mbili zilipita katika kichwa chake kushona jeraha lile
 
SEHEMU YA 40


?kwa nini mama mkwe wako akutende hivi? eve alimuuliza Reshmail akiwa pale kitandani

?ni haki yake hata kunipiga risasi mimi ni chanzo cha maumivu haya wanayoyapata? alijibu Resh huku akilazimisha tabasamu

?kwa hio hapa amenionea huruma sana mimi ni sawasawa na muuaji tena wa kukusudia na haki yangu ni kuuawa pia? aliendelea Reshmail huku akitoa tabasamu hafifu tena

?usiseme hivyo mamii sio wewe uliyetaka iwe hivyo ni Mungu pekee? aliongea kwa upole Eve huku akivibinyabinya vidole vya Reshmail

?mama mwambie baba afatilie mama mkwe asije kulazwa selo hata kwa saa moja hana kosa lolote? Reshmail alimwambia mama yake alipoingia katika chumba cha hospitali ya Agha khan aliyokuwaelazwa kwa ajili ya matibabu maneno hayo yalimshangaza sana mama yake aliyetegemea Reshmail atakuwa na hasira ya kutendwa vile mbele ya hadhara

Nafsi ilikuwa inamsuta sana mama reshmail,moyo uliomba msamaha lakini mdomo ulikuwa mzito sana kufanya hivyo. Hali hiyo ilimkondesha sana na kumkosesha raha ndani kwa ndani unene wake wa asili uliyafunika yote hayo na hakuna aliyejua jambo zito alilobeba mama huyu.

Kweli badala ya bwana na bibi Manyama kuegemea upande wa mashtaka ili mama Adam apewe adhabu la wao waliunga mkono kwamba Reshmail alikuwa na makosa mahakama ikatupilia mbali mashtaka hayo na mama Adam akawa huru,jambo hilo badala ya kurudisha undugu liliongeza chuki na uadui

?si nilikwambia ukabisha?? Kama hawajamtoa mwanetu kafara kwanini sasa wamekubali niachiwe huru??? mama Adam alimwambia mumewe jambo ambalo wakati huu hata yeye alikubaliana nalo kuwa motto wao mkubwa wa kiume(Adam) alitendwa vibaya na familia ya reshmail .

kuamini kwa mzee Michael baba yake Adam ni sawa na familia nzima kuamini kabisa na sumu ya chuki ikamwingia kila mwanafamilia na kuwa aadui wakubwa wa familia ya mzee Manyama.
 
Back
Top Bottom