Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #721
297
Hata hivyo, ilionekana pia kundi hili lililokuwa na watu ndani ya Serikali ya Msumbiji waliotumika kutaka kuvuruga uhusiano mzuri uliokuwepo kati ya Tanzania na Msumbiji, uhusiano ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na mwasisi wa chama cha kupigania uhuru wa Msumbiji, ‘FRELIMO’, Eduardo Chivamba Mondlane tokea mwaka 1962, kisha uhusiano huo ukatiliwa nguvu na Rais wa kwanza wa Msumbiji, Samora Machel.
Kwa taarifa hizi Idara ya Usalama la Taifa iliamua kuweka utaratibu na kugawana malengo ya kushughulikia. Ili kurahisisha mizunguko ya mjini na ufuatiliaji wa ‘leads’ nyingi kwa wakati mmoja, wakuu walikubaliana kukipanua zaidi kikosi kazi na kukigawanya katika makundi mengine madogo madogo ya utendaji.
Kila kundi lilikuwa na maofisa kumi na mbili waliotoka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID), Kikosi cha Siri cha Ulinzi (SS) na Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (MI).
Kisha kila kundi lilipaswa kupewa magari maalumu mawili hadi matatu ambayo serikali ilikuwa mbioni kuyakodi, kwa msaada wa nchi marafiki, kutoka mawakala mbalimbali jijini Dar es Salaam, yakiwa na namba za kiraia. Baada ya mgawanyo wa vikundi kukamilika, maofisa walipaswa kugawana majukumu kulingana na mkakati wa utendaji.
Hata hivyo mgawanyo huu usingeliathiri kundi letu la ‘Nge’ lililokuwa na jukumu la kufuatilia mawasiliano yote yaliyofanywa na watuhumiwa, kuanzia mawasiliano ya simu za mkononi, barua pepe na hata account zao kwenye mitandao ya kijamii. Kwa jinsi tukio lilivyofanyika, tulikuwa na kila sababu ya kuamini kwamba wahusika walikuwa na mtandao mkubwa, uliohusisha washiriki na wafadhili walioko nje ya nchi, na walikuwa na mawasiliano ya kila aina.
Kwa kuwa sikuwa nimeshiriki kwa ukaribu zaidi kwenye shughuli za kundi langu la ‘Nge’ kutokana na jukumu zito nililopewa, Tunu alinifahamisha kuhusu hatua kubwa iliyokuwa imepigwa na kundi letu katika kufuatilia kwa umakini kumbukumbu zote za simu zilizopigwa ndani na nje ya nchi katika kipindi cha miezi mitatu iliyokuwa imepita na jumbe mbalimbali zilizotumwa kwa njia ya simu na intaneti.
Tunu pia alinionesha taarifa ya awali aliyokuwa ameipata ya kundi la pili lililojulikana kama “Spider” (Buibui) ambalo maofisa wake walitakiwa kufanya uchunguzi wa haraka wa eneo la tukio kabla halijavurugwa, na kupata maelezo ya mashahidi kabla hawajatoweka na kuiwasilisha taarifa hiyo kwenye task force. Kiukweli kundi hili lilikuwa limepiga hatua kubwa katika uchunguzi wao. Walijigawa katika makundi mawili, moja lilifuatilia majeruhi waliolazwa katika hospitali za Muhimbili, Mwananyamala na Agakhan kwa ajili ya matibabu.
Waliwahoji, wakachukua maelezo yao kwa kufuata taratibu za kisheria na kuwatambua wale waliokuwa na taarifa muhimu ambazo zingeweza kusaidia katika upelelezi. Kwa vile wengi wa majeruhi hao walikuwa wameshatambuliwa, na taarifa zao kuchukuliwa muda mfupi baada ya mlipuko kazi ya kuwapata ilikuwa rahisi.
Wengi wa watu hao hawakuwa na maelezo mengi kwani walishitukizwa na mlipuko kiasi kwamba hawakujua ni kitu gani hasa kilichotokea. Hata hivyo baadhi yao waliweza kueleza kwa ufasaha hali ilivyokuwa. Mmojawapo wa watu waliokuwa na kumbukumbu nzuri ya tukio hilo ni mzee Julius Mhilu, mwandishi mkongwe wa riwaya na mwongozaji wa filamu aliyekuwa katika harakati za kugombea daladala la kueleka Tabata.
Katika maelezo yake mzee Mhilu aliwaeleza maofisa wa kikosi kazi kwamba, wakati akigombea daladala la Tabata lililokuwa jirani la jengo la Alpha Mall, ghafla aliona mwanga mkali kama wa radi ambao ulifuatiwa na muungurumo mkubwa ulioambatana na vumbi, vipande vya vioo na vitu vinginevyo vilivyorushwa kwa nguvu.
Vitu hivyo vilimpiga na kumchana sehemu ya kifua chake na mikono aliyokuwa ameitumia kujiziba uso wake. Kwa sekunde kadhaa aliduwaa asijue la kufanya na alipopata fahamu alijiona akiwa chini, damu imetapakaa kila mahali. Alipoangalia vizuri alimwona kila mtu aliyekuwa eneo lile akivuja damu.
Kikosi kazi pia kilimhoji Adam Chande, mmiliki wa duka la nguo (Kidoti Boutique) ambaye alieleza kuwa wakati wa tukio, yeye pamoja na mkewe Halima walikuwa wanafika katika eneo hilo.
Wakati anakunja kona ili kuingia mtaa ambao jengo la Alpha Mall lilikuwepo, akiwa umbali wa mita kama thetathini hivi, ghafla ulitokea muungurumo mkubwa uliopasua vioo vya gari lake na kuvisambaza ndani ya gari. Alipotazama kwa umakini mbele yake kuona nini kilichotokea, alishituka kuona damu ikimminika.
Alipomtazama mkewe akamwona akiwa amepatwa na mshtuko mkubwa na kupoteza fahamu na alikuwa amejeruhiwa eneo la usoni na kifuani. Kwa sekunde kadhaa aliendelea kusikia mfululizo wa miungurumo mingine midogo dogo iliyofanana na milio ya bunduki. Baadaye alitambua kuwa milipuko hiyo ilisababishwa na kupasuka kwa matairi ya magari yaliyokuwa yakiungua kwenye maegesho ya magari nje ya jengo lile. Kwa vile majeraha aliyopata hayakuwa mabaya sana, Adam Chande aliweza kuwasaidia wengine waliojeruhiwa.
Mtu mwingine aliitwa Sarah Hillary, ambaye alikuwa mhudumu mgahawa wa kisasa wa Nuru Café uliokuwa kwenye ghorofa ya pili ya jengo lile. Sarah alikieleza kikosi kazi kuwa kupona kwake ulikuwa muujiza mkubwa kwani mlipuko wa bomu ulimfanya apoteze fahamu kabisa na alipozinduka alijikuta akiwa amefunikwa na kifusi, huku mwili wake ukiwa umelowa kitu kinachofanana na Mafuta.
Sekunde chache baadaye alipata fahamu vizuri na kutambua kuwa yale hayakuwa mafuta bali ilikuwa damu iliyochanganyika na vumbi la kifusi. Wakati akihangaika kujiinua ndipo watoa msaada walipofika na kuondoa kifusi kilichokuwa kimemfunika yeye na wenzake.
Akiwa anapelekwa kwenye gari la wagonjwa, Sarah aliona vipande vya nyama na viungo vya watu vilivyosambaa kila mahali hali iliyomfanya asite kukanyaga eneo hilo na alipoangaza zaidi alimwona bosi wake, meneja wa mgahawa huo akiwa ameungua mwili mzima.
Mtu mwingine aliyehojiwa na kikosi kazi aliitwa Halima Mlacha, mmoja wa wanasheria wa kampuni ya Kitomari Advocates iliyokuwa na ofisi zake ndani ya jengo la Alpha Mall. Halima alieleza kuwa dakika takriban kumi kabla ya mlipuko alitoka kwenda kununua chakula kwenye mgahawa mmoja uliokuwa katika jengo la Makumbusho Plaza baada ya kugundua kuwa alikuwa hajala.
Mara tu baada ya kununua chakula hicho, Halima alianza kurudi kwenye lile jengo taratibu lakini kabla hajaenda zaidi akasikia mlipuko mkubwa uliotingisha kila mahali. Kwa sekunde kadhaa alijikuta amebutwaa asijue kilichotokea; lakini ghafla akaona moto mkubwa ukiwaka kwenye jengo la Alpha Mall. Alishitushwa sana kuona jengo likiporomoka na magari yakiungua moto huku na damu nyingi ikitapakaa na viungo vya binadamu vikiwa vimesambaa kila mahali.
Maelezo yalikuwa mengi kwani kikosi kazi hiki pia kiliwahoji mamia ya watu wengine waliokuwepo katika eneo la tukio. Watu walioonekana kuwa na taarifa za maana waliorodheshwa na kupangiwa siku ya mahojiano. Kwa vile wengi wa watu hao bado walikuwa katika hali mbaya ki afya, yaani kimwili na kisaikolojia, hivyo iliamuliwa kuwa mahojiano ya pili yakafanyikie kwenye makazi yao au mahali pengine ambapo wangejisikia huru kuzungumza kwa uhuru, bila hofu.
Endelea...