Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

taharuki..jpg

306

“Nadhani ungeniacha tu niende zangu kwa amani,” nilimwambia ACP Mwamba kwa sauti tulivu huku nikitaka kuondoka lakini akanizuia kwa kunielekezea bastola.

“Huendi kokote,” ACP Mwamba aliniambia huku akinitazama kwa kuminya macho kisha akanitaka nimkabidhi ile bahasha niliyokuwa nimeishika mkononi.

“Kwa nini nikukabidhi? Ni nani aliyekutuma au labda wewe unahusika vipi na nyaraka hizi?” nilimuuliza ACP Mwamba huku nikiwa makini sana na kila hatua aliyotaka kuipiga dhidi yangu.

“Naona haunifahamu vizuri wewe… Sipendi kuchezewa na waandishi uchwara,” ACP Mwamba alisema kwa hasira huku akiendelea kunisisitizia nimkabidhi ile bahasha. Na sasa alinitishia kuwa endapo nisingefanya alichokitaka ndani ya dakika moja angenionesha cha mtema kuni.

Nikacheka. “Unadhani unaweza ukanifanya kitu?” nilimuuliza kisha nikaongeza, “Ni mara ngapi umejaribu kunidhuru ukashindwa?”

Nikamwona tena ACP Mwamba akitaka kusema neno lakini akasita na kubinjua midomo yake.

“Au unadhani sifahamu mipango yako? Usidhani mimi ni mjinga sema nangoja tu muda wangu ufike,” nilisema kwa sauti makini nikiwa napeleka mkono wangu wa kulia kiunoni kwa kificho na kuigusa bastola yangu.

ACP Mwamba aliguna kidharau. “Wakati gani huo, Mr. Sizya? Unadhani unaweza ukapigana na ukuta?” Kisha akacheka. “Kwanza sina muda wa kujibishana na mtu kama wewe. Nipe hiyo bahasha au niichukue kwa nguvu?”

Nikaiweka ile bahasha juu ya meza pasipo kusema neno, kisha nikainua uso wangu kumtazama kwa dharau, sasa macho yangu yaliashiria vita.

ACP Mwamba akatabasamu kwa dharau. “Nilikuwa naingoja sana hii nafasi. Leo nitakufundisha adabu ili siku nyingine uwe na heshima kwa wakubwa wako.” Alisema na kuirudisha bastola yake kiunoni.

Nikajua kuwa alitaka mapigano ya ana kwa ana. Nikakunja ngumi na kusimama sawia kwa ajili ya mpambano huku nikimtazama kwa macho ya kina nikimkagua kuanzia juu mpaka chini kisha nikasema na moyo wangu, “Ngoja nimwoneshe, kumbe hanijui huyu.”

ACP Mwamba alikunja ngumi, akatanua miguu yake kupata balansi kabla hajanivamia kwa mapigo ya haraka haraka akirusha ngumi kama tano kwa wepesi mno na kwa hasira! Hakika alikuwa mwepesi mno kwenye kufanya uamuzi na kujifyatua. Alionekana kuwa na haja ya kunipa kichapo kuliko ambavyo nilikuwa na haja ya kumchapa yeye.

Ila pamoja na wepesi wake wa kufanya uamuzi niligundua kuwa alikuwa anatumia nguvu nyingi kushambulia lakini alikuwa mdhaifu kwenye kujikinga. Muda wote nilikuwa nazuia mashambulizi yake na sikuona haja ya kummaliza mapema. Sikudhani kama alistahili kumalizwa mapema.

Sasa nilimwona akinitazama kwa namna ya kunishangaa sana, macho yake yalianza kuonesha wasiwasi kwani alikuwa amepiga ngumi nyingi zisizo na idadi pasipo kufanikiwa hata moja! Na wala mimi nilikuwa sijaanza kumshambulia.

Nikamwona akibadilisha mtindo na sasa akawa ananishambulia kwa mateke zaidi na ngumi za kushtukiza. Hapa sasa akafanikiwa kunitwanga ngumi moja ya shavuni iliyonipepesua. Nikajikuta nikitema damu na kujipangusa na mgongo wa kiganja.

Ngumi ile ilinifanya nighafirike mno. Na hapo nikajikuta nikianza kumshambulia mithili ya nyuki waliotibuliwa kwenye mzinga wao! Sasa ilikuwa kazi yake kuzipangua ngumi zangu na mateke. Kwa kasi ya umeme, kabla hajafikisha ngumi juu ya mwili wangu, mimi nikawa nimeshamchapa ngumi kadhaa na mateke matatu yaliyompeleka sakafuni mara mbili!

ACP alikuwa mwepesi mno ila mimi nilikuwa mithili ya umeme na nilikuwa nikimsoma na kuzitambua nyendo zake kabla hajaamua hata kuzitekeleza. Alinitazama kwa ghadhabu kisha akajikakamua kunyanyuka aendelee na pambano. Kwa wepesi mno akanikimbilia lakini nilishajiandaa, kabla hajafanya shambulizi lolote alishtukia nimemfyeka miguu yake na yupo hewani kimo cha ndama! Na kabla hajakaa sawa nikamshindilia teke la tumbo lililomtupa sakafuni na kumfanya acheue damu!

Alitulia pale kwa muda chini, huenda alikuwa hajielewi kwa maumivu makali aliyoyapata. Halafu akanitazama kwa mshangao na kujikongoja kusimama kwa tabu, akanijongea kwa kasi kama nyati aliyejeruhiwa. Akakutana na teke la mzunguko lililombwaga kifudifudi. Kisha nikamkwida ukosi na kumwinua. Nikamzungusha na kumnyuka ngumi tatu za mfululizo.

ACP Mwamba akapepesuka na kukung’uta kichwa chake kuondosha ulevi uliomzonga. Kisha nikamwona akijizatiti na kujikumbuka yeye ni nani. Akakurupuka tena na kurusha ngumi, akarusha teke. Vyote viliambulia patupu. Akajirekebisha na kujaribu kujiweka sawa. Akarusha ngumi, akarusha teke na kujikuta anakata tena hewa na kuzidi kujichosha.

Sasa akaona haya ni maji marefu, akatoa bastola yake haraka na kuielekeza kwangu lakini nikawahi kuupiga teke mkono wake ulioshika bastola, ikamtoka na kuanguka mbali. Kisha nikajizungusha na kumfumua teke la juu kwa juu. ACP Mwamba akapepesuka. Nikamfumua teke la usoni. Akadondoka kama gunia.

Alipoinuka tu nikainua mguu wa kulia kama niliyetaka kumpiga teke na mguu huo, akafanya kosa kukinga mikono yake ili kuzuia teke langu, na hapo nikazunguka na kuinua mguu wa kushoto, nikampiga teke mauti lililokata mawasiliano kwenye uti wa mgongo. Akapiga yowe huku akiangua chini na kutulia, hakuweza kuusogeza mwili wake zaidi ya macho tu ndiyo yalikuwa yanazunguka kutazama huku na kule.

Hali ile ikamfanya ACP Mwamba aanze kulia na kuniomba nimwinue kwani alikuwa hawezi hata kusogea. Sikutaka kukutwa tena mle ndani, hivyo kila nilichokifanya nilikifanya kwa haraka na muda mfupi uliofuata nikawa nimemaliza kufanya upekuzi makini katika kile chumba cha mwisho ambacho kilikuwa ofisi binafsi ya SSP Kambi, hata hivyo sikupata kitu chochote kingine muhimu katika uchunguzi wangu.

Sikuona sababu ya kuendelea kupoteza muda wangu zaidi mle ndani, hivyo haraka nikatoka kwenye ile nyumba nikimwacha ACP Mwamba pale sakafuni akiendelea kulia kwa uchungu. Muda mfupi uliofuata nilikuwa nimeshafika nilipoegesha gari langu. Kabla sijaondoka nikampigia simu Tunu na kumweleza kile kilichotokea nyumbani kwa SSP Kambi halafu nikajipakia kwenye gari na kuondoka huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu. Usiku bado ulikuwa mwingi.

* * *

Tukutane tena wakati mwingine katika harakati hizi za Jason Sizya...
 
View attachment 2375675

Hongera sana Mkuu.
 
Dah! Humu kumepoa sana kana kwamba watu mmeamua kunisusia [emoji17], ni watu wachache sana wanaotia moyo... nafikiria nikiimaliza season hii ya Taharuki niachane na harakati hizi za Jason Sizya, ingawa bado kuna season kibao huko mbele...
Mwaga nguki Bishop tunafuatilia kimya kimya...piga matukio marefu...
 
taharuki..jpg

307

Saa 9: 50 usiku...

Kwa mbali zilisikia sauti za majogoo waliokuwa wakishindana kuwika kwenye mabanda kuashiria kuwa siku mpya ilikuwa imeanza, na ndani ya chumba changu sauti ya muziki laini ilikuwa inasikika toka kwenye spika ndogo za tarakilishi yangu ya kazi. Mazingira yalikuwa yametulia mno kiasi kwamba ungeweza kusikia vizuri sauti tamu ya mwanamama Judy Boucher akiimba kibao chake matata cha Each and Everyday.

Ilikuwa inaelekea kuwa saa kumi ya alfajiri nikiwa bado sijaambua japo lepe la usingizi, muda huu nilikuwa nimeketi juu ya sofa chumbani kwangu, nikiwa kifua wazi na bukta nyepesi ya kulalia. Mbele ya sofa hilo la kuketi watu wawili kulikuwa na meza ndogo ya kioo, na juu ya meza hiyo kulikuwa na chupa kubwa ya whisky, kando yake kulikuwa na tarakilishi mpakato na ile bahasha yenye barua ya maelekezo kwa meneja wa Alpha Commercial Bank, Mr. Andrew Adonis, pamoja na hundi niliyoitoa nyumbani kwa SSP Kambi.

Baada ya harakati zangu za mchana kutwa na kile kilichotokea baadaye usiku kwenye lile jaribio la mauaji dhidi yangu, nilidhani kuwa nilihitaji kunywa pombe kali ili kupata utulivu wa moyo na akili yangu hasa katika kipindi hiki ambacho familia yangu, kwa maana ya mke wangu Rehema, mtoto wetu na mfanyakazi wa ndani, wakiwa Tabora kwa wazee.

Muda wote picha za jaribio lile la mauaji dhidi yangu kutoka kwa wanausalama kule Soko la TX Kinondoni na baadaye uvamizi wa ACP Mwamba nyumbani kwa SSP Kambi huko Mbezi Beach, zilizunguka akilini kwangu utadhani nilikuwa natazama filamu.

Baada ya kutoka Mbezi Beach na kurejea nyumbani kwangu usiku huo sikutaka kulala, nilipanga kutafuta taarifa zote muhimu kwenye programu yangu maalumu ya TracerMark kuhusiana na kile nilichokuwa nikikichunguza, hususan wale wanausalama watatu walionishambulia pamoja na ACP Mwamba.

Hata hivyo, huenda ni kutokana na uchovu mwingi, nilijikuta nikishindwa kufanya lolote na badala yake nikabaki kunywa tu mvinyo. Na baada ya kunywa mafunda kadhaa ya mvinyo nikidhani ingenisaidia kuichangamsha akili yangu, ndiyo ikasababisha kichwa kishindwe kuendeleza na kazi, ndipo nikajimwaga kwenye sofa!

Kwa yale yaliyotokea, ilikuwa wazi kuwa kulikuwa na mpango haramu ambao sikuufahamu, dhidi yangu au pengine dhidi ya haki, kutoka kwa wanausalama mafisadi wasiozingatia maadili yao ya kazi, wanausalama ambao waliniona kuwa tishio kwa mambo yao.

Maswali mengi yalipita akilini kwangu; nilijiuliza kwa nini wanausalama hao walianza kuniwinda ili waniangamize? Ni nani aliyewatuma kunimaliza, na kwa sababu gani? Je, ACP Mwamba alijuaje kuwa nilikuwa nyumbani kwa SSP Kambi nikifanya upekuzi au alikuja na mambo yake lakini ndo hivyo tukakutana? Na kwa nini alikuwa akiing’ang’ania bahasha niliyoichukua mle ndani ya nyumba ya SSP Kambi?

Nilihisi kwamba ACP Mwamba alikuwa anajua kilichokuwa ndani ya ile bahasha na alikuwa anataka kuficha jambo. Kitendo chake cha kufika pale usiku na kisha kuingia mle ndani ya nyumba ya SSP Kambi kwa siri vilinithibitishia hayo. Lakini nikathibitisha zaidi kuwa ni kweli ACP Mwamba hakuwa polisi safi maana kama angekuwa msafi kwa nini alikuja peke yake, tena kwa siri?

Kama alikuwa kwenye majukumu ya kikazi basi angeongozana na askari wengine kama ilivyokuwa kawaida. Hii ilinionesha kuwa alikuwa anahusika na genge la matukio ya uhalifu jijini, ambalo baadhi ya wanausalama walihusika nalo.

Hadi muda huo sikuwa na uhakika na hali ya ACP Mwamba, na sikujua kama polisi wenzake walishamwona na kumpeleka hospitali, maana nilimwacha akiwa na hali mbaya sana. Alikuwa nusu mfu.

Hata hivyo, maswali yalizidi kupita kichwani kwangu nikijiuliza; je, kama polisi wakimwona halafu akaamua kunigeuzia kibao kwa kusema kuwa ni mimi niliyemfuata nyumbani kwa SSP Kambi na kumvamia nikimzuia kutimiza majukumu yake! Je, ningekuwa na utetezi upi, hasa ikizingatiwa kuwa wengi walimwamini sana ACP Mwamba kuwa alikuwa askari mpambanaji na kiboko ya wahalifu? Ila… ni majukumu yapi hayo aliyokuwa akiyatimiza muda huo nyumbani kwa SSP Kambi? Upelelezi wa jaribio la mauaji dhidi yangu? Nilijiuliza…

Hata hivyo, vyovyote vile iwavyo, sikuwa na hofu kabisa kwani niliamini penye ukweli uongo hujitenga. Kwani mimi nilikuwa na sababu za kufika nyumbani kwa SSP Kambi na mkuu wangu wa kazi alikuwa anajua, nilikwenda huko nikiamini kuwa nilikuwa na haki kwa sababu nilihusishwa kwenye jaribio la mauaji na marehemu Yusuf Kambi.

Sikudhani kama ilikuwa vibaya kufuatilia sababu iliyomfanya SSP Kambi na wenzake kujaribu kuniua. Kitendo cha kufuatiliwa barabarani usiku na gari halafu ukashambuliwa kwa risasi katika jaribio la kukuua si jambo la kawaida, hasa ikizingataiwa kuwa mimi pia nilikuwa ofisa wa Usalama wa Taifa!

Lakini… ngoja kwanza! Hapa lilikuwepo jambo lililoanza kunisumbua akili yangu. Nilijiuliza ikiwa kulikuwepo uhusiano wowote kati ya jaribio lile la mauaji dhidi yangu na kile nilichokuwa nikikichunguza, yaani mlipuko wa bomu kwenye jengo la Alpha Mall! Na kama vitu hivi vilihusiana, je, hao waliotaka kuniangamiza walijuaje kuwa nilikuwa ninazo taarifa muhimu kuhusu mlipuko huo? Nani aliwaambia? Hadi muda huo nilikuwa na uhakika kuwa ni Tunu peke yake aliyekuwa anajua kuhusu jambo hilo.

Japokuwa kanuni za kijasusi zilinionya kutomwamini mtu yeyote katika harakati zangu, hata marehemu, lakini niliamini kabisa kuwa Tunu asingeweza kuniuza, kwa bei yoyote ile! Yeye ndiye aliyekuwa mkuu wangu wa kazi na ndiye aliyenituma kuifanya kazi ile. Basi ni nani mwingine aliyekuwa anajua kuhusu jambo hilo? Sauti fulani ikaninongoneza ndani yangu kuwa huenda Kamishina Koba alifahamu.

Hapana!

Lakini… mbona kama… alikuwa na wasiwasi hivi na alitamani sana kujua kama nilikuwa na fununu zozote kuhusiana na mlipuko ule wa kigaidi kwenye jengo la Alpha Mall? Kwa nini awe na wasiwasi na mimi kiasi kile? Ni nani aliyemdokeza? Hata hivyo niliamini kuwa Kamishina Koba alikuwa askari mwadilifu aliyekuwa akizingatia maadili ya kazi yake, hata askari wa chini yake walimsifu kwa hilo. Ndiyo maana niliamini uwa hata kama angekuwa anajua kuwa nilikuwa na ushahidi mzito kuhusiana na mlipuko ule asingeweza kuwa katika kundi moja na watu kama SSP Kambi na ACP Mwamba.

Sasa akili yangu ilianza kushindwa kufanya kazi sawa sawa na kichwa changu kilizunguka. Nilianza kupata wasiwasi, sikujua ni nani hasa niliyekuwa namchunguza, au nini nilichokuwa nakitafuta! Je, nilitakiwa kujikita zaidi kwenye kuchunguza watu waliolipua jengo la Alpha Mall au nilitakiwa nianzishe uchunguzi kuhusu jaribio la mauaji dhidi yangu? Hisia zangu ziliniambia kuwa yote mawili yalikuwa muhimu sana, hivyo nilipaswa kufanya uchunguzi wa matukio yote sambamba maana muda ulikuwa mchache na mambo yalikuwa mengi.

Kwa kuwa akili ilikuwa imechoka niliamua kupumzika japo kwa saa mbili zilizobakia kabla sijaanza tena harakati za kufuatilia kila nilichokitilia shaka ambacho kingeweza kuniletea majibu. Sasa jambo lingine lilikuwa limeongezeka, hundi. Ili kupata majibu nilipanga kufuatilia mawasiliano ya akina SSP Kambi ya miezi mitatu nyuma ili kubaini endapo kulikuwa na chochote cha kutia shaka, huenda ningefahamu ni nani aliyekuwa amewatuma kunimaliza.

Pia ningemshirikisha Tunu kabla hajaenda kukutana na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa ili nisikie upande wake alifikiria nini, niliamini kwa kumshirikisha Tunu nisingeshindwa kupata ufumbuzi wa maswali hayo.

* * *

Endelea...
 
taharuki..jpg

308

Kikosi maalumu…

Saa 1:30 asubuhi…

SIKU iliyofuata nilifika ofisi za SPACE, Oysterbay, mapema mno kuliko kawaida. Lakini pamoja na kuwahi huko ofisini nilimkuta bosi wangu, Tunu, na maofisa wengine wote wakiwa wameshafika na wameketi kuzunguka meza ya mkutano tayari kwa SITREP. Bila kupoteza muda niliwajulia hali na kuketi katika kiti kilichokuwa wazi.

Kikao cha asubuhi hii kilikuwa moto sana na cha aina yake kwani kikosi kazi katika kundi letu la Nge kilikuwa kimefanya kazi kubwa sana ya kuchunguza mawasiliano ya simu na jumbe mbalimbali za simu na kwenye mitandao ya kijamii zilizokuwa na viashiria vya uhalifu, na kuanza kufuatilia kuwabaini watu hao. Yalikuwepo matumaini ya kuwabaini watu waliopanga jambo hilo.

Maofisa wote walikuwa na hali ya mori kubwa na walichangamka. Mimi pekee ndiye nilikuwa katika hali isiyo ya kawaida. Matukio ya siku iliyokuwa imepita yalinionesha wazi kuwa kama nisingekuwa makini hatari kubwa ilikuwa mbele yangu.

Kama kawaida, Tunu ndiye aliyefungua kikao kwa kutoa maelezo mafupi kuhusu hali ya usalama nchini. Kama ilivyokuwa kwa kikao kilichofanyika siku moja kabla ambapo masuala ya uchumi, siasa na huduma za kijamii yaliwekwa pembeni kwanza, siku hii pia agenda kuu ilikuwa suala la ugaidi.

Kwa dakika kumi na tano hivi Tunu alitusomea taarifa maalumu iliyotolewa na makao makuu kuhusu shambulio lililotokea katika jengo la Alpha Mall, taarifa ambayo tayari nilikuwa naifahamu kwa kuwa niliiona usiku wa siku iliyotangulia baada ya kwenda nyumbani kwa Tunu.

Baada ya maelezo hayo Tunu alitoa nafasi kwa maofisa kujadili taarifa hiyo kabla ya kuanza utekelezaji wake katika medani. Taarifa ilijadiliwa kwa kina na kupatiwa ufumbuzi.

Kisha ofisa mwandamizi, Nuru Kabwe, alinyoosha mkono wake juu akiomba kuzungumza jambo tofauti kidogo na hoja iliyokuwepo mezani ingawa alihisi lingekuwa na uhusiano kwa namna fulani. “Mkuu, nakushukuru sana kwa taarifa uliyotupa” Nuru Kabwe alianza baada ya kupewa nafasi ya kutaka kuongea. “Ila tungependa kupewa ukweli wa taarifa tunazozisikia kuwa jana usiku kulifanyiwa jaribio la kutaka kumuua ofisa mwenzetu lililofanywa na baadhi ya maofisa wa usalama. Hivi jambo hili halina uhusiano na hili kweli?” Nuru Kabwe alimalizia.

Hoja hiyo iliungwa mkono na maofisa wengine waliokuwa katika SITREP. Maofisa hao walionesha shauku kubwa ya kutaka kujua nini hasa kilikuwa nyuma ya jaribio lile, na hali halisi ilivyokuwa.

“Nakubaliana nanyi, Jason ana maelezo mazuri sana,” Tunu alimjibu Nuru Kabwe. “Hata hivyo taarifa yake haiwezi kuwa sehemu ya SITREP hii maana tayari ipo kwenye mamlaka nyingine, Polisi Oysterbay, ila kwa faida ya maofisa mliopo hapa, namruhusu awaeleze kwa kifupi ili nanyi mjue hali halisi ilivyokuwa.”

Kisha Tunu aliniashiria nianze kuzungumza. Niliwaeleza kwa kirefu jinsi mambo yalivyokuwa tangu nilipokuwa natoka Oysterbay nyumbani kwa Tunu, kisha nikagundua kuwa kulikuwa na gari aina ya Jeep Wrangler jeusi lililokuwa likinifuata, ili kuhakikisha kama ni kweli nilifungiwa mkia nikaanza mizunguko na kubaini kuwa hisia zangu zilikuwa sahihi ndipo niliposimama eneo la Soko la TX Kinondoni kabla mashambulizi la risasi kwenye gari langu hayajakatokea.

Nilijitahidi sana kuwapa maelezo ya kina ili kuwapa picha halisi ya mfululizo wa matukio bila kugusia mawasiliano yangu na Tunu, taarifa nilizokuwa nimeziwasilisha kwake au uchunguzi nilioufanya nyumbani kwa SSP Kambi. Mambo hayo yalishaingia katika utaratibu wa usiri sambamba hivyo sikupaswa kuyaeleza kwa maofisa wengine.

Ofisa mwingine mwandamizi Jonas Marwa pia alitaka kujua kama kulikuwa na uhusiano kati ya tukio la kushambuliwa na tukio lingine lililozua gumzo kubwa miongoni mwa wanausalama kuhusu ACP Mwamba kukutwa akiwa hajielewi na amepooza viungo kwenye nyumba ya mmoja wa watu waliotaka kuniua, SSP Kambi. Kwa kueleza hayo Jonas alituonesha picha ya ACP Mwamba kwenye simu yake akiwa amelala chini sakafuni mdomo wazi hajitambui.

Tunu aliwaomba maofisa wawe na subira kwenye mambo hayo kwani yalikuwa yanashughulikiwa na mamlaka zingine na majibu ya maswali hayo yangepatikana mapema zaidi kwa kuwa zilikuwepo hoja nyingi kuhusiana na tukio lile la ACP Mwamba ambazo hakuna aliyekuwa na majibu isipokuwa ACP Mwamba mwenyewe. Nini kilikuwa kimemkumba ndani ya nyumba ya marehemu? Alikuwa akifanya nini hapo? Yote hayo yangejulikana muda si mrefu.

Baada ya maelezo yangu na ya Tunu tuliendelea na SITREP kwa dakika zisizopungua arobaini hivi, kujadili kila suala tuliloona ni muhimu kufuatia hali tete iliyokuwepo nchini.

Wakati tukiendelea kujadiliana tukidadavua suala moja baada ya jingine, simu iliyokuwa mezani kwa Tunu ilianza kuita. Haraka Tunu alinyanyua kikonyo chake na kukipeleka sikioni. “Halow!” aliita kwa sauti kavu.

Baada ya kusikia sauti iliyokuwa upande wa pili, Tunu alituashiria tutoke ofisini kwake ili aweze kuzungumza kwa uhuru zaidi. Mara moja sote tulisimama na kutoka chumbani humo ili kumpa faragha zaidi.

Wakati tukimsubiri Tunu amalize mazungumzo yake kwenye simu, tuliketi sehemu na kuendelea na mazungumzo. Na hapo nikajikuta nikiwa mzungumzaji mkuu kwa kuwa maofisa wenzangu bado walikuwa na kiu ya kutaka kujua hali ilivyokuwa katika mapambano ya risasi kati yangu na watu waliotaka kuniua, na hali niliyokuwa nayo baada ya shambulio hilo.

Kila ofisa kwa wakati wake aliniuliza swali aliloona lingenifanya nitoe maelezo ya kina zaidi ya hatua ambazo nilidhani zingefaa kuchukuliwa. Nami bila kuvunja miiko ya usiri sambamba niliwaeleza yote niliyoona walistahili kuyajua. Kwa ujumla tukio zima lilikuwa kama filamu. Tukiwa katikati ya mazungumzo, Salha Mwapachu, katibu muhtasi wa Tunu alitufuata akionesha kuwa mwenye haraka na ujio wake ulionekana kana kwamba si wa kawaida. Tulijikuta tukinyamaza kimya ili kumsikiliza.

“Mr Sizya unaitwa na mkuu” Salha alisema kwa sauti laini huku akinikazia macho, halafu bila kuongeza neno aligeuka akarudi alikotoka.

Bila kupoteza hata sekunde niliinuka na kuelekea ofisini kwa mama Tunu nikiwa na shauku kubwa. Niliufungua mlango na kuingia, kisha nikaufunga taratibu. Tunu alikuwa bado ameshikilia kikonyo cha simu akiendelea kuongea kwa sauti ya chini. Aliponiona akaniashiria nisogee karibu na kuketi katika moja ya viti vilivyokuwa pembeni ya meza yake. Bila kusema neno nilifanya kama alivyoniagiza.

“Mkurugenzi, Jason Sizya tayari yupo hapa,” Tunu alimwambia mtu aliyekuwa upande wa pili wa simu mara tu alipoona nimeshakaa pembeni kisha alinyoosha mkono wake kunikabidhi kikonyo cha simu. Akasema, “Ongea na DGIS.”

Mwili ulinisisimka na koo langu lilinikauka ghafla huku baridi nyepesi ikinitambaa mwilini. Nilijiuliza DGIS alitaka kuzungumza nini na mimi? Pia kwa nafasi na wadhifa niliokuwa nao ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa, sikuwa miongoni mwa maofisa ambao wangeweza kupigiwa simu na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa kwa sababu yoyote ile. Chain of command ilinitenga na wakubwa hata kama ningekuwa katika operesheni nyeti kiasi gani.

Hata hivyo badala ya kuifurahia fursa ile ya kuzungumza na mkurugenzi mkuu asubuhi hiyo kwani ilinifanya niwe mtu muhimu sana ingawa sikuwa na fununu ya jambo alilotaka kunieleza, lakini nilijikuta nikitamani iwe ndoto.

Endelea...
 
taharuki..jpg

309

“Shikamoo, mkuu!” nilimsalimia DGIS kwa unyenyekevu mkubwa mara tu nilipoiweka simu katika sikio langu la kushoto.

“Marahaba, Jason, u hali gani?” DGIS aliniuliza kwa upole kama vile mzazi anayeongea na mwanawe.

“Sijambo, mkuu,” nilimjibu kwa unyenyekevu.

“Nimepata taarifa za shambulio dhidi yako pale Soko la TX Kinondoni na kile kilichotokea kati yako na ACP Mwamba, sasa hivi nimetoka kuongea na mkuu wako wa taasisi, amenieleza kuwa umefanya kazi kubwa sana juu ya kile kilichotokea kwenye jengo la Alpha Mall na unao ushahidi mzito utakaosaidia kuwapata watuhumiwa wa ugaidi. Pamoja na maelezo mazuri ya bosi wako nimeona si vibaya nikiongea nawe moja kwa moja ili uweze kuona uzito wa jambo lenyewe…” DGIS alisema na kunyamaza kidogo, huenda alitaka maneno yake yaniingie vizuri.

“Sasa, nakuhitaji hapa ofisini, kwa kuwa nina kikao na mkuu wako asubuhi hii basi si vibaya mkija wote ili nisikie moja kwa moja kutoka kwako badala ya kusikia juu juu,” DGIS aliongeza akizungumza kwa msisitizo.

“Sawa, mkuu, nitafika bila kukosa,” nilijibu kwa unyenyekevu huku nikihisi mwili wangu ukisisimka na pumzi zikinipaa. Kisha aliniomba nimpe simu Tunu ili aweze kumalizana naye.

Sikuweza kujua hasa nilijisikiaje baada ya kumaliza mazungumzo yangu na DGIS, moyo wangu ulikuwa umepoteza utulivu na kijasho chepesi kilikuwa kikinitoka sehemu mbalimbali za mwili wangu.

_____

Saa tatu na nusu asubuhi ilitukuta mimi na Tunu tukiwa ndani ya ofisi ya mzee Rajabu Kaunda, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (DGIS) katika makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Mzee Rajabu Kaunda alikuwa mwanamume mtu mzima wa umri wa miaka 59 na ushee akibakiza miezi michache tu ya kustaafu, kichwa chake kilianza kujaa mvi na alikuwa na ndevu nyingi nyeupe zilizokizunguka kidevu chake.

Tukiwa mle ofisini kwake, mkurugenzi mkuu alinitaka nimweleze kwa mapana kuhusu kila kitu kilichotokea kuanzia jaribio la kutaka kuniua hadi mkasa wa ACP Mwamba, na nyongeza ya yale ambayo nilikuwa nikiyafahamu kuhusu shambulio la bomu pale kwenye jengo la Alpha Mall.

Kwa uangalifu mkubwa nilimweleza mkurugenzi mkuu habari yote, nikianzia mwanzo kabisa nilipovutiwa kupiga picha za watu wakigombea usafiri wa daladala kwenye kituo cha daladala cha Makumbusho, nilivyomshuhudia Waziri Ummi na katibu wake wakifika kwenye jengo la Alpha Mall na kuelekea ofisini kwa Daniel Kayera, kisha yule mtu aliyefika hapo na pikipiki ya magurudumu matatu na kulazimisha kuipachika katikati ya magari ya Waziri Ummi na Daniel Kayera, hadi mlipuko ulipotokea.

Nikaendelea kumweleza hali ya uharibifu niliyoikuta pale kwenye jengo la Alpha Mall na tahadhari za kiusalama ambazo nilichukua dhidi ya kila mtu niliyemtilia shaka. Nikamweleza mkutano wangu na Kamishina Koba ndani ya gari lake na nilivyosita kumwambia kuwa nilikuwa na fununu kuhusu waliolipua bomu hilo, nilivyogundua kuwa mtu aliyetumika kutengeneza bomu hilo ni Gahizi, raia wa Rwanda, hadi ilivyotokea nikagundua kulikuwa na gari likinifuata nyuma na hatimaye kuvamiwa pale Soko la TX Kinondoni katika jaribio la kutaka kuniua kabla ya baadaye kwenda Mbezi Beach kufanya upekuzi nyumbani kwa SSP Kambi.

Muda wote mkurugenzi mkuu alikuwa kimya akinitazama kwa umakini sana, hadi namaliza maelezo yangu alikuwa bado yupo kimya kabisa, kisha nilitoa ile bahasha kubwa ya kaki ya A4 iliyokuwa na barua ya maelekezo kwa meneja wa benki ya Alpha Commercial Bank na hundi na kuviweka juu ya meza yake huku nikieleza shaka yangu kuwa kulikuwepo na genge hatari la uhalifu lililowahusisha baadhi ya maofisa wa usalama wa taifa na polisi ambao walikuwa wakilipwa fedha nyingi sana kulinda uhalifu.

Baada ya maelezo hayo mkuu wangu wa kazi, Bi Tunu Michael, alitoa zile nyaraka za taarifa nilizokuwa nimemkabidhi na kumpa mkurugenzi na kuomba niongezewe nguvu katika kukabiliana na genge hilo hatari, ambalo kwa mtazamo wake alihisi ndilo lililohusika na tukio la kigaidi pale Alpha Mall.

I see! Hii ni taarifa nzuri sana, ina details za kutosha na inanifanya nijivunie kuwa na vijana kama nyinyi katika idara yangu. In fact, hakuna yeyote ndani ya Idara au hata kwenye kikosi kazi aliyeweza kupiga hatua kwa kiwango hiki hadi sasa…” DGIS alisema na kuongeza, “Saa tano nitakuwa na kikao na wakurugenzi, nilitamani sana kulifanya jambo hili liwe mojawapo ya ajenda lakini nachelea kusema tuendelee kulifanya top secret maana huwezi kujua nani yumo ndani ya sindicate hii na nani hayumo… ila ni muhimu kumjulisha Rais.”

Mimi na Tunu tuliangaliana pasipo kusema neno, kisha nikavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku nikihisi faraja kubwa moyoni mwangu. Muda huo moyo wangu ulikuwa ukinidunda kwa kasi kutokana na mchanganyiko wa furaha na wasiwasi wa uzito wa jambo nililokuwa nikijitwika.

“Operesheni hii ni muhimu sana na ya aina yake, na kutokana na unyeti wake nadhani ni vizuri niunde task force ndogo ya maofisa watatu tu lakini walio makini sana na wenye kuaminika, na kazi yenu itaanzia kwa meneja wa Alpha Commercial Bank…” Mkurugenzi mkuu alisema na kunyamaza kidogo kana kwamba alikuwa ananipa nafasi ya kutafakari mambo aliyoyasema, kisha akaendelea.

“Kwa hiyo, Tunu, naomba kuanzia sasa huyu Jason hatakuwa chini ya Taasisi ya SPACE tena na atawajibika moja kwa moja kwa Komando Luteni Lister kama kiongozi wa task force hii ndogo itakayojumuisha watu watatu; Luteni Lister mwenyewe, Jason na Pamela Mkosamali, na watapokea maagizo kutoka kwangu, kupitia channel husika. Mpaka hapo tumeelewana?”

“Nimekuelewa, mkuu, na nashukuru sana kwa kuendelea kumwamini Jason maana naamini yeye ni hazina kubwa sana katika nchi yetu,” Tunu alijibu na kumfanya mkurugenzi mkuu anitazame na kubetua kichwa chake kukubali.

“Na baada ya mazungumzo haya Jason atakabidhi kazi zote za taasisi ulizompa ili uweze kuwapangia maofisa wengine kwa kuwa yeye atashughulika na suala hili hadi tuujue mwisho wa haya,” mkurugenzi mkuu alihitimisha.

Kisha alimpigia simu katibu muhtasi wake ambaye aliingia mara moja mle ofisini akiwa ameshikilia faili moja lenye rangi nyekundu. Akaliweka mezani.

“Wapigie simu Luteni Lister na Pamela Mkosamali, waambie wafike hapa ofisini kwangu haraka kuna kazi maalumu ya kufanya,” mkurugenzi mkuu alimwambia katibu wake muhtasi.

“Sawa, mkuu,” Dada huyo alijibu kwa unyenyekevu na kutoka.

Baada ya maelezo hayo mkurugenzi mkuu aliniruhusu kuondoka ofisini hapo na kwenda kusubiri kwenye ofisi ya katibu wake muhtasi wakati akiendelea na kikao na Tunu kabla ya kwenda kwenye kikao cha wakurugenzi ambacho Tunu pia alikuwa mjumbe. Nilikwenda ofisini kwa katibu muhtasi wa mkurugenzi mkuu ili kuwasubiri Luteni Lister na Pamela.

* * *

Saa 6:00 mchana…

Nilizikwea ngazi za jengo la Makumbusho Plaza haraka haraka na kuelekea kwenye ofisi yangu katika kampuni ya Capital Media Inc. wakati nikiukaribia mlango wa ofisini kwangu nikaona mlango huo ukifunguliwa a na Winnie akatoka ndani ya chumba hicho. Aliponiona akashtuka sana japokuwa alijitahidi kuuficha mshtuko wake na kulazimisha tabasamu.

Alikuwa amevaa sketi fupi ya bluu yenye miraba myeupe iliyoishia sentimita chache juu ya magoti yake na yenye mpasuo mfupi ulioliacha nusu wazi paja lake, blauzi nyekundu ya mikono mirefu na viatu vyekundu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio. Na kama kawaida alikuwa amevalia miwani yenye fremu kubwa nyeusi na nywele zake ndefu nyeusi zikiwa zimefungwa kwa nyuma.

“Habari, boss!” Winnie aliwahi kunisalimia huku akilazimisha tabasamu.

“Njema, habari za kwako!” nilijibu salamu yake huku nikishusha pumzi ndefu.

“Nzuri, nilijaribu sana kukutafuta kwa simu jana jioni lakini haukuwa unapokea, Kamishina Koba alikuja hapa,” Winnie aliniambia huku uso wake ukiwa bado umepambwa na tabasamu.

“Anasemaje?” nilimuuliza huku nikimtazama machoni katika namna ya kumsoma.

“Hakuniambia alikuwa anataka nini, alisema angekutafuta mwenyewe baadaye. Sijui kama alikupigia?” Winnie alisema huku akiminya macho yake kwa mbwembwe kana kwamba alikuwa ananikonyeza.

“Alinipigia…” nilimwambia kisha nilimuuliza nikiwa bado namtazama machoni. “Vipi kuna kipya hapa?”

Uso wangu haukuwa na chembe ya masikhara. Sikutaka kupoteza muda kwa kazi nilizokuwa nazo, kwani Luteni Lister na Pamela walikuwa wananisubiri kwenye gari kule chini ya jengo ili tuelekee Alpha Commercial Bank kuonana na meneja wa benki hiyo, Mr. Andrew Adonis.

Winnie aliguna. “Hakuna. Nilidhani labda wewe umekuja na jipya!” alisema na kuachia kicheko hafifu. Nikatikisa kichwa changu na kutazama dari huku akili yangu ikihangaika. Winnie akaanza kuondoka lakini nikamuwahi.

“Winnie!” niliita kwa sauti tulivu pasipo kuyaondooa macho yangu kwenye dari.

“Abee!” Winnie aliitika huku akinitazama kwa wasiwasi.

“Kuna kitu unakijua halafu unanificha,” nilimwambia huku nikiyaondoa macho yangu kwenye dari na kumtazama usoni. Winnie alionekana kushtuka kidogo.

“Kitu gani, boss?” Winnie aliuliza huku akinyanyua mabega yake juu na kuyashusha.

“Sijajua lakini naamini wewe unakijua. Ni kipi hicho?” nilimuuliza nikiwa nimemkazia macho.

“Mbona hakuna kitu ninachokijua ambacho ninakuficha! Kwani kitu hicho kinahusiana na nini?” Winnie alisema na kushusha pumzi.

“Una uhakika kuwa hujui chochote?” nilimuuliza, sura na sauti yangu havikuonesha mzaha.

“Ndiyo. Nina uhakika,” Winnie alisema huku akikunja sura yake.

“Unajua. Na lazima uniambie nini kinakusumbua hivi ambacho hutaki nijue?” nilimuuliza Winnie nikiwa nimeshika kiuno changu. Hasira zilianza kunijaa kifuani.

“Kitu gani, boss? Kwa nini unawaza hivyo?” Winnie aliniuliza huku akinitazama kwa mshangao.

“Kwa nini unanifuatilia sana kutaka kujua kinachoendelea? Hivi unamtumikia nani?” nilizidi kumsaili Winnie.

“Nakufuat… he! Boss, ki vipi?” Winnie aliuliza akionekana kushtuka sana.

“Winnie, hebu tuache kufanyana watoto. Kuna jambo linaendelea huko ambalo wewe unanificha na unaepuka sana nisilijue. Ni bora ukaniambia mapema…” nilisema kwa sauti kavu iliyoonesha wazi kuwa nilikuwa nimekasirika.

Winnie alinitazama kwa kitambo akiwa kimya kisha akaanza kupiga hatua kuondoka. “Naona leo boss umeamua kunituhumu kwa jambo ambalo wala silifahamu. Samahani naomba niende nikaendelee na kazi.”

Nilitikisa kichwa changu kwa huzuni maana nilimwonea huruma. Hakika hakujua kuwa alikuwa anacheza na hatari! “Nitakapogundua, wewe na hao unaowatumikia mtakuwa mmechelewa sana,” nilimwambia wakati akifungua mlango wa chumba cha ofisi ya kitengo cha graphics.

Winnie alinitazama tu pasipo kusema neno huku sura imesawajika, akaingia ndani ya chumba cha graphics. Nikaingia ofisini kwangu na kusimama katikati ya chumba hicho nikiikagua ofisi yangu kwa macho tu na kugundua kuwa ilikuwa imefanyiwa upekuzi makini sana, upekuzi ambao kwa mtu asiye na taaluma ya ujasusi asingeweza kubaini.

Dakika tano baadaye nilitoka mle ofisini na kuziendea ngazi, nikashuka haraka kuelekea chini na baada ya hapo nikajipakia ndani ya gari tayari kwa safari ya kuelekea Alpha Commercial Bank.

* * *

Harakati za Jason Sizya bado zinaendelea, usichoke kufuatilia...
 
Asante mkuu, huyu wini na koba nna waswas nao sana ila i miss rehema n am curious abt zainab
 
Du mkuu uko vizuri, kazi umeipanga vyema visa na matukio viko vizuri.straight forward umeitumia ipasanyo .umeshift kutoka love mpaka ujasusi. Pongezi Sana bishop.kila season ina vionjo vyake. Nilikuwa nasoma kimyakimya ila imenibidi nikometi leo
 
Ni vizuri ku comment maana comments zenu zinatuongezea mzuka na kutuonesha kuwa kumbe kuna watu wanasoma hadithi zetu, wanavutiwa au kukerwa na vitu fulani...
 
Back
Top Bottom