Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #741
306
“Nadhani ungeniacha tu niende zangu kwa amani,” nilimwambia ACP Mwamba kwa sauti tulivu huku nikitaka kuondoka lakini akanizuia kwa kunielekezea bastola.
“Huendi kokote,” ACP Mwamba aliniambia huku akinitazama kwa kuminya macho kisha akanitaka nimkabidhi ile bahasha niliyokuwa nimeishika mkononi.
“Kwa nini nikukabidhi? Ni nani aliyekutuma au labda wewe unahusika vipi na nyaraka hizi?” nilimuuliza ACP Mwamba huku nikiwa makini sana na kila hatua aliyotaka kuipiga dhidi yangu.
“Naona haunifahamu vizuri wewe… Sipendi kuchezewa na waandishi uchwara,” ACP Mwamba alisema kwa hasira huku akiendelea kunisisitizia nimkabidhi ile bahasha. Na sasa alinitishia kuwa endapo nisingefanya alichokitaka ndani ya dakika moja angenionesha cha mtema kuni.
Nikacheka. “Unadhani unaweza ukanifanya kitu?” nilimuuliza kisha nikaongeza, “Ni mara ngapi umejaribu kunidhuru ukashindwa?”
Nikamwona tena ACP Mwamba akitaka kusema neno lakini akasita na kubinjua midomo yake.
“Au unadhani sifahamu mipango yako? Usidhani mimi ni mjinga sema nangoja tu muda wangu ufike,” nilisema kwa sauti makini nikiwa napeleka mkono wangu wa kulia kiunoni kwa kificho na kuigusa bastola yangu.
ACP Mwamba aliguna kidharau. “Wakati gani huo, Mr. Sizya? Unadhani unaweza ukapigana na ukuta?” Kisha akacheka. “Kwanza sina muda wa kujibishana na mtu kama wewe. Nipe hiyo bahasha au niichukue kwa nguvu?”
Nikaiweka ile bahasha juu ya meza pasipo kusema neno, kisha nikainua uso wangu kumtazama kwa dharau, sasa macho yangu yaliashiria vita.
ACP Mwamba akatabasamu kwa dharau. “Nilikuwa naingoja sana hii nafasi. Leo nitakufundisha adabu ili siku nyingine uwe na heshima kwa wakubwa wako.” Alisema na kuirudisha bastola yake kiunoni.
Nikajua kuwa alitaka mapigano ya ana kwa ana. Nikakunja ngumi na kusimama sawia kwa ajili ya mpambano huku nikimtazama kwa macho ya kina nikimkagua kuanzia juu mpaka chini kisha nikasema na moyo wangu, “Ngoja nimwoneshe, kumbe hanijui huyu.”
ACP Mwamba alikunja ngumi, akatanua miguu yake kupata balansi kabla hajanivamia kwa mapigo ya haraka haraka akirusha ngumi kama tano kwa wepesi mno na kwa hasira! Hakika alikuwa mwepesi mno kwenye kufanya uamuzi na kujifyatua. Alionekana kuwa na haja ya kunipa kichapo kuliko ambavyo nilikuwa na haja ya kumchapa yeye.
Ila pamoja na wepesi wake wa kufanya uamuzi niligundua kuwa alikuwa anatumia nguvu nyingi kushambulia lakini alikuwa mdhaifu kwenye kujikinga. Muda wote nilikuwa nazuia mashambulizi yake na sikuona haja ya kummaliza mapema. Sikudhani kama alistahili kumalizwa mapema.
Sasa nilimwona akinitazama kwa namna ya kunishangaa sana, macho yake yalianza kuonesha wasiwasi kwani alikuwa amepiga ngumi nyingi zisizo na idadi pasipo kufanikiwa hata moja! Na wala mimi nilikuwa sijaanza kumshambulia.
Nikamwona akibadilisha mtindo na sasa akawa ananishambulia kwa mateke zaidi na ngumi za kushtukiza. Hapa sasa akafanikiwa kunitwanga ngumi moja ya shavuni iliyonipepesua. Nikajikuta nikitema damu na kujipangusa na mgongo wa kiganja.
Ngumi ile ilinifanya nighafirike mno. Na hapo nikajikuta nikianza kumshambulia mithili ya nyuki waliotibuliwa kwenye mzinga wao! Sasa ilikuwa kazi yake kuzipangua ngumi zangu na mateke. Kwa kasi ya umeme, kabla hajafikisha ngumi juu ya mwili wangu, mimi nikawa nimeshamchapa ngumi kadhaa na mateke matatu yaliyompeleka sakafuni mara mbili!
ACP alikuwa mwepesi mno ila mimi nilikuwa mithili ya umeme na nilikuwa nikimsoma na kuzitambua nyendo zake kabla hajaamua hata kuzitekeleza. Alinitazama kwa ghadhabu kisha akajikakamua kunyanyuka aendelee na pambano. Kwa wepesi mno akanikimbilia lakini nilishajiandaa, kabla hajafanya shambulizi lolote alishtukia nimemfyeka miguu yake na yupo hewani kimo cha ndama! Na kabla hajakaa sawa nikamshindilia teke la tumbo lililomtupa sakafuni na kumfanya acheue damu!
Alitulia pale kwa muda chini, huenda alikuwa hajielewi kwa maumivu makali aliyoyapata. Halafu akanitazama kwa mshangao na kujikongoja kusimama kwa tabu, akanijongea kwa kasi kama nyati aliyejeruhiwa. Akakutana na teke la mzunguko lililombwaga kifudifudi. Kisha nikamkwida ukosi na kumwinua. Nikamzungusha na kumnyuka ngumi tatu za mfululizo.
ACP Mwamba akapepesuka na kukung’uta kichwa chake kuondosha ulevi uliomzonga. Kisha nikamwona akijizatiti na kujikumbuka yeye ni nani. Akakurupuka tena na kurusha ngumi, akarusha teke. Vyote viliambulia patupu. Akajirekebisha na kujaribu kujiweka sawa. Akarusha ngumi, akarusha teke na kujikuta anakata tena hewa na kuzidi kujichosha.
Sasa akaona haya ni maji marefu, akatoa bastola yake haraka na kuielekeza kwangu lakini nikawahi kuupiga teke mkono wake ulioshika bastola, ikamtoka na kuanguka mbali. Kisha nikajizungusha na kumfumua teke la juu kwa juu. ACP Mwamba akapepesuka. Nikamfumua teke la usoni. Akadondoka kama gunia.
Alipoinuka tu nikainua mguu wa kulia kama niliyetaka kumpiga teke na mguu huo, akafanya kosa kukinga mikono yake ili kuzuia teke langu, na hapo nikazunguka na kuinua mguu wa kushoto, nikampiga teke mauti lililokata mawasiliano kwenye uti wa mgongo. Akapiga yowe huku akiangua chini na kutulia, hakuweza kuusogeza mwili wake zaidi ya macho tu ndiyo yalikuwa yanazunguka kutazama huku na kule.
Hali ile ikamfanya ACP Mwamba aanze kulia na kuniomba nimwinue kwani alikuwa hawezi hata kusogea. Sikutaka kukutwa tena mle ndani, hivyo kila nilichokifanya nilikifanya kwa haraka na muda mfupi uliofuata nikawa nimemaliza kufanya upekuzi makini katika kile chumba cha mwisho ambacho kilikuwa ofisi binafsi ya SSP Kambi, hata hivyo sikupata kitu chochote kingine muhimu katika uchunguzi wangu.
Sikuona sababu ya kuendelea kupoteza muda wangu zaidi mle ndani, hivyo haraka nikatoka kwenye ile nyumba nikimwacha ACP Mwamba pale sakafuni akiendelea kulia kwa uchungu. Muda mfupi uliofuata nilikuwa nimeshafika nilipoegesha gari langu. Kabla sijaondoka nikampigia simu Tunu na kumweleza kile kilichotokea nyumbani kwa SSP Kambi halafu nikajipakia kwenye gari na kuondoka huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu. Usiku bado ulikuwa mwingi.
* * *
Tukutane tena wakati mwingine katika harakati hizi za Jason Sizya...