Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Rehema kirangaaaaa kichokupeleka kilosa nini?! Unajiamini nini wewe, ukiwekewa sumu ufe je mume mwenyewe sasaa mchafu muhuni fox simpendi
Hahahaaa, Mkuu Litro, mume siku hizi katulia sana hafuatilii tena habari za watoto wazuri. Yuko bize na kazi tu....
 

317

Sharifa Mbwana…




Saa 12:50 jioni…

TULIKUWA tumeketi kwa utulivu tukimtazama kwa umakini mzee Rajabu Kaunda, mkurugenzi mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Yeye alikuwa ameketi kwenye kiti chake akitutazama mmoja mmoja kwa umakini kana kwamba alikuwa mwalimu wa usafi aliyekuwa akitafuta kasoro kwenye sare za wanafunzi wake.

Mzee huyu alikuwa mpole sana na ni mara chache sana ungemsikia akipaza sauti yake aongeapo na mtu. Alipenda sana kutumia macho yake na maneno machache tu hasa akikukumbusha juu ya uwepo wako kwenye taasisi hii nyeti ya Usalama wa Taifa, ambayo ndiyo moyo wa nchi.

Siku hii ya Jumanne ilinifanya nijisikie mtu muhimu sana, japokuwa sikuwa mtu wa karibu wa mzee huyu, si tu kwa sababu ya muda mfupi wa utumishi wangu ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa, bali pia cheo na wadhifa niliokuwa nao katika Idara hii ya ujasusi vilinifanya nisiwe miongoni mwa watu ambao wangeweza kuwa na ukaribu na mkurugenzi mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa kwa sababu yoyote ile. Chain of command ilinitenga na wakubwa hata kama ningekuwa katika operesheni nyeti.

Mara zote wakuu wa operesheni hizo (kama ilivyokuwa kwa Luteni Lister) ndio waliokuwa na nafasi ya kuwa karibu au kuzungumza na wakurugenzi wa Idara kwa niaba yetu, wakati sisi tukiwa katika mapambano. Mara zote sisi watu wa medani (field) kumbukumbu zetu zilibaki katika mafaili, na katika vichwa vya wale tulioshirikiana nao katika vita. Basi!

Kabla ya siku hii, mara ya mwisho kuwa karibu au kukutana uso kwa uso na mkurugenzi mkuu mzee Kaunda ilikuwa ni kipindi kile nilipotoka kwenye mafunzo ya ujasusi nchini Misri, ni yeye aliyenipokea na kunipa pongezi kutokana na kufanya vyema kwenye mafunzo yangu ya ujasusi kiasi cha kuiletea sifa Idara ya Usalama wa Taifa. Japokuwa sikuwa mtu wa karibu wa mkurugenzi mkuu, lakini nilitambua kuwa mzee huyu alipenda sana kusema kabla ya kuwaruhusu wanausalama wakafanye kazi zao, “TISS ni moyo wa Tanzania, hivyo msifanye taifa kuwa mfu.”

Ilikuwa vigumu sana kumjua kama yupo kwenye huzuni, msongo wa mawazo ama kwenye furaha. Mara zote uso wake haukuonesha tashwishwi yoyote, kwa ujumla alikuwa mfichaji mzuri sana wa hisia. Nilijaribu sana kuwa kama yeye lakini nikaishia kushindwa hasa kila nilipokutana na wadada warembo. Haha!

Muda huu tukiwa tumeketi kwa utulivu kwenye viti tulisubiri kusikia kauli ya mzee huyu, hatukujua alikuwa anafikiria nini baada ya kutoka kuongea, kwenye simu, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia hatukujua waliongea nini. Hii ilikuwa ni baada ya kumwelezea kwa kirefu kuhusu kile kilichotokea kule Alpha Commercial Bank hadi pale mlipuko wa bomu ulipotokea na kisha Luteni Lister alimpatia vile vielelezo vyote tulivyovitoa kule Alpha Commercial Bank.

Kikao chetu kilikuwa kimechukua muda wa dakika hamsini na tano tu kabla hajainuka na kutuacha ofisini kwake ili kwenda kuongea na Rais kwenye simu. Katika kikao chetu tulikuwa tumejadili kwa mapana na marefu kuhusu orodha ya majina ya watu waliotakiwa kupokea mgawo wa fedha toka kwenye benki ile. Tulijiuliza, malipo hayo yalitokana na kazi gani? Sote tukakubaliana kuwa vyovyote iwavyo kazi hiyo haikuwa kazi halali, lazima ilikuwa kazi haramu na huenda ilihusiana na lile tukio la kigaidi pale kwenye jengo la Alpha Mall.

Na kama hivyo ndivyo ilivyokuwa basi kikosi kazi kilichoundwa na makao makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa kilipaswa kufumuliwa na kusukwa upya kwani baadhi ya waliotajwa kwenye orodha ile walikuwepo pia kwenye kikosi kazi hicho ili kuchunguza kuhusu tukio lile la kigaidi.

Kwa mzee Kaunda, mambo yalikuwa magumu mno. Yeye ndiye aliyekuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha ndani ya nchi hakuna ugaidi, uhujumu, uzandiki na mambo yote yanakuwa salama, kwani idara aliyokuwa akiiongoza ndiyo ilikuwa moyo wa taifa. Kutokana na wadhifa wake alipaswa kuwasiliana na mkuu wa nchi na kumshauri kuhusu masuala ya usalama wa taifa na hata kuitisha kikao cha dharura cha usalama.

Katika kikao hicho pia tulijadili kuhusu kitendo cha Sajenti Mambo kunipa ishara kuwa tusipande gari lililotegwa bomu wakati alikuwa anahusika kwenye sakata lile, tukakubaliana kwamba pamoja na yote bado Sajenti Mambo alibaki kuwa mtu muhimu sana kwenye upelelezi wetu na alipaswa apatikane kabla ya siku iliyofuata. Jukumu la kumtafuta liliachwa kwangu.

Na kwa kuhitimisha niliwaonesha picha ya yule dada aliyetukimbia pale Alpha Commercial Bank kisha akaondoka na gari aina ya Nissan V8 muda mfupi kabla bomu halijalipuka na kuliteketeza gari letu. Picha hiyo nilikuwa nayo kwenye simu yangu baada ya kumpiga kwa siri akiwa na SSP Kambi nyumbani kwa Waziri Ummi Mrutu. Japo kwenye picha hii alikuwa amevaa hijabu lakini hiyo haikulizuia jicho la kishushushu la Luteni Lister mara baada ya kuyaona macho ya dada huyo. Tulimwona Luteni Lister akigutuka na kuonesha kuwa alikuwa anamfahamu.

Luteni Lister alitwambia kuwa dada huyo alikuwa akiitwa Daniella Palangyo, komando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na aliaikuwa katika Idara ya Ujasusi jeshini (Millitary Intelligence).

Sasa, baada ya kutoka kuongea na Rais, mkurugenzi mkuu alibaki kimya kwa dakika kadhaa akitutazama kwa namna fulani hivi ya kutuhusudu, macho yake yalionesha wazi kuwa alikuwa akijivunia sana kuwa na vijana kama sisi kwenye Idara aliyokuwa akiiongoza. Mkononi alikuwa bado ameishika ile karatasi yenye orodha ya majina ya watu waliopaswa kupokea mgawo wao pale Alpha Commercial Bank.

Baada ya kitambo fulani alikohoa kidogo katika namna ya kusafisha koo lake kisha akanitazama na kusema, “Jason, sasa nimetambua ni kwa nini watu hawa walikuwa wanakutafuta ili wakuue, ni kwamba walikuwa wana uhakika kuwa wewe ndiye mtu tishio kwao na walikuwa wanajua kilichokuwa kinaendelea ofisini kwako!”

Alinyamaza tena, akameza funda la mate kutowesha koo lake kisha akatutazama kwa zamu akiyahamisha macho yake kutoka kwenye uso wangu na kumtazama Pamela na mwisho akamalizia kwa Luteni Lister. “Hapa tuongeapo, mheshimiwa Rais ananisubiri Ikulu, nami nisingependa kuiangusha Idara ninayoiongoza na wala sitaki kustaafu nikiwa nimeharibu rekodi yangu ya utendaji kazi… kwa hiyo kuna kazi ngumu sana ninataka kuwapa ili kuendelea kulinda heshima ya Idara, najua hamtaniangusha.”

Akili yangu ikaanza kuwaza ni kazi gani aliyotaka kutupatia? Nilikuwa makini sana katika kumsikiliza mzee huyo huku nikijaribu kuwaza nini angesema. Ndivyo tulivyofundishwa chuoni. Yakupasa kuwaza ya mbele hata kubashiri kwa mantiki pale unapoona kuna haja ya kufanya hivyo. Halikuwa kosa. Ila sikuweza kuwaza sana kwa maana nilipaswa pia kuweka akili na masikio yangu kwenye kinywa cha mkurugenzi mkuu.

Endelea...
 

418

Ndipo mkurugenzi mkuu akatukabidhi hati ya maagizo ya kazi ambayo tulitakiwa kuishughulikia. Hati za namna hiyo tuliziita ‘SIMU’ na zilikuwa zinafungwa katika mafumbo (codes). Hata hivyo, hati hii ilikuwa ni mwendelezo wa kazi tuliyokuwa tukiifanya ila kulikuwa na maagizo maalumu tuliyopaswa kuyafuata ili kufanikisha kazi yetu. Ni kazi ambayo ilikuwa ikiniumiza sana kichwa. Katika utekelezaji wa kazi hii mkurugenzi mkuu alitupatia kibali maalumu ili kukamilisha mambo fulani.

Huku akili yangu ikijikita katika kuifikiria kazi hii hatari ambayo tulipaswa kuhakikisha imekamilika ndani ya saa sabini na mbili, kwa maana ya siku tatu, bado mawazo juu ya Daniella na kitendo alichokifanya kule ndani ya jengo la Alpha Commercial Bank yalianza kuitawala akili yangu. Nilihisi kama Daniella aliamua makusudi kunisubiri mle ndani ya jengo la benki ili nimwone ndipo aondoke! Sasa akili yangu ilianza kufunguka kila nilipomfikiria Daniella, nilihisi na kitendo chake kilikuwa cha makusudi… huenda alikifanya kwa faida yangu.

Hakuishia hapo, hata alipokuwa akiondoka na lile gari aina ya Nissan V8 na kuamua kushusha kioo cha gari wakati gari lile likinipita kilikuwa kitendo cha makusudi… ili nijue kuwa alikuwa amepanda gari lile. Kwa nini alifanya vile? Je, ni yeye aliyetega lile bomu kwenye gari letu? Na kwa nini asingeondoka mara baada ya kutega bomu na badala yake akasubiri nimwone? Nilijiuliza sana pasipo kupata majibu.

Halafu, ni kama yeye na Sajenti Mambo walikuwa wana ushirika, maana hata kile kitendo cha Sajenti Mambo kunikazia macho akitaka kuvuta umakini wangu ili nijue kuwa alikuwepo eneo lile huku akiwa hataki watu wengine wagundue jambo hilo pia kilinishangaza. Sikujua alikuwa na maana gani? Je, alijua kuwa nilikuwepo pale benki muda ule na alijua kuwa gari letu lilitegwa bomu? Kama ndivyo… kulikuwa na nini basi kwa watu hawa? Na iweje akapotea baada ya mlipuko ule wa bomu?

“Kwa hiyo mmenielewa?” mkurugenzi mkuu alituuliza huku akitutazama kwa umakini usoni. Kwa kweli sikuwa najua ni maneno gani ya mwisho alikuwa ametoka kuyaongea hadi kutuuliza swali lile, kwani muda huo mawazo yangu yalikuwa mbali sana. Yalikuwa nje ya zile kuta nne za chumba cha ofisi yake.

“Tumeelewa, mkuu!” Luteni Lister na Pamela waliitikia kwa unyenyekevu huku mimi nikibaki nashangaa.

“Luteni, wewe kama kiongozi wa timu hii utaongozana na mimi kwenda Ikulu kuonana na mheshimiwa Rais. Hutakuwepo kwenye kikao chetu lakini huenda wakati wa mazungumzo yetu mheshimiwa Rais akataka kuuliza maswali au kupata maelezo ya ziada. Ili kuondoa usumbufu wa kukutafuta wakati tukiwa katikati ya kikao ni bora uwepo karibu, sawa?” mkurugenzi mkuu alimwambia Luteni Lister.

“Sawa, mkuu,” Luteni Lister alijibu kwa unyenyekevu.

Kisha mkurugenzi mkuu akaturuhusu mimi na Pamela kuondoka ofisini hapo ili kwenda kujiandaa na kazi tuliyotakiwa kuishughulikia kama alivyokuwa ameelekeza kwenye hati ya maagizo ya kazi. Kama ilivyo ada ya Watanzania tulimuaga kwa kumpa mkono, kisha tukaondoka.

* * *



Saa 4:30 usiku…

Hali ya hewa ilikuwa ya baridi kidogo na manyunyu mepesi ya mvua yalikuwa yanaanguka ardhini kutoka angani. Pamoja na manyunyu hayo bado hayakuweza kuzuia pilika pilika za wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuelekea kwenye mambo yao na wengine kurejea kwenye makazi yao baada ya shughuli za kutwa nzima za kuisaka shilingi.

Kwangu siku hii iliniishia nikiwa napita maeneo ambayo nilidhani ningempata Sajenti Mambo lakini sikuwa nimefanikiwa kumwona au hata kupata taarifa zake. Nilipotazama saa yangu ilikuwa imetimia saa nne na nusu za usiku, tumbo nalo lilikuwa linanichachafya bila huruma, na hapo nikakumbuka kuwa nilikuwa sijala siku nzima zaidi ya kunywa kahawa na sharubati tu hapa na pale.

Ndipo Nuru Club iliyopo eneo la Kinondoni ikanikaribisha baada ya uchovu wa siku ndefu ya kazi. Club hii ilikuwa na eneo kubwa na majengo yake yalitengenezwa kwa ustadi wa hali juu na ilikuwa kwa kuta safi za vioo na nje kulikuwa na bango kubwa jeupe lenye maandishi makubwa mekundu yaliyoandikwa ‘NURU CLUB’.

Pale nje kulikuwa na magari machache yaliyokuwa yameegeshwa kwenye eneo la maegesho ya magari na nilipoyachunguza vizuri magari yale haraka nikagundua kuwa mengi yalikuwa ni magari ya watu wenye vipato vya kueleweka ambao walikuwa mle ndani wakijipatia vinywaji, chakula au starehe yoyote iliyokuwa ikipatikana ndani ya Club ile.

Nilipoingia ndani nilitembea taratibu huku nikiyatembeza macho yangu kwa makini kuyapeleleza mandhari yale na kuzitazama sura zilizokuwemo mle kisha nikajichagulia meza ya peke yangu iliyokuwa kwenye kona moja, sehemu iliyoniwezesha kumwona kila aliyeingia au kutoka mle ukumbini. Utulivu wa mandhari yake ulikuwa wa hali ya juu uliomezwa na sauti ya muziki laini wa kubembeleza uliokuwa ukirushwa kutoka katika spika zilizokuwa maeneo fulani kwenye kona za ukumbi ule.

Kulikuwa na wahudumu wa kike warembo waliokuwa wakihudumia wateja waliokuwa mle ndani wameketi kwenye meza nzuri na viti vifupi vyenye foronya laini. Nilipoketi niliyatembeza tena macho yangu haraka mle ndani ili kuzikagua sura za watu waliokuwemo lakini sikuona sura yoyote ya kuitilia shaka.

Mara msichana mmoja mrembo, mhudumu wa ukumbi ule wa chakula alikuja na kusimama mbele ya ile meza niliyoketi huku tabasamu la kibiashara likivinjari usoni pake. Nilimtazama mhudumu yule kwa sekunde kadhaa huku macho yangu yakipumbazwa na uzuri wake. “Dah! Haya ni matumizi mabaya sana ya rasilimali watu,” nilijiambia.

Alikuwa msichana mzuri na mrembo sana ambaye kamwe sikuwahi kumwona msichana wa namna ile akifanya kazi kama mhudumu. Msichana huyu hakupaswa kabisa kuwa mmoja wa wahudumu, alitakiwa kuwekwa ndani na mwanamume mwenye fedha zake, ale na apumzike tu kwa ajili ya kazi moja. Japokuwa alikuwa amevaa sare za kazi lakini bado uzuri wake haukujificha kabisa.

“Karibu kaka, sijui ungependa kuagiza nini?” yule mhudumu aliniuliza kwa sauti tamu na tulivu iliyonifanya kwa sekunde kadhaa nikose neno la kuongea kutokana na kuendelea kupumbazika na uzuri wake. Baada ya kitambo kifupi hatimaye nikavunja ukimya huku nikitabasamu.

“Naomba niletee kuku wa kienyeji nusu na ugali dona bila kusahau pilipili na limao,” nilimwambia yule mhudumu huku nikimtazama moja kwa moja machoni. Nikamwona akiinamisha uso wake chini kwa aibu baada ya kuona macho yangu yakimtazama kwa namna ya kumhusudu, kisha alijifanya akiitazama saa yake ili kuzuga.

“Kuna kingine chochote ungependa…?” yule msichana mrembo mhudumu aliniuliza huku akinitazama kwa tabasamu.

“Vipo vingi nivipendavyo kwako…” nilisema huku nikiachia tabasamu, macho yangu yalikuwa makini kumtazama usoni. Macho yetu yakagongana na hapo yule msichana akahimili kunitazama kwa sekunde mbili tu, sekunde ya tatu macho yake yakaangukia chini huku akiachia tabasamu maridhawa la aibu. Na hapo pembe za midomo yake zikafinya na vishimo vidogo kwenye mashavu yake vikachomoza na kuzidi kuzisulubu hisia zangu.

Endelea...
 

319

“…lakini niletee kwanza msosi halafu hivyo vingine nitakwambia nikishashiba,” niliongeza huku tabasamu usoni kwangu likikataa kwenda likizo.

“Ondoa shaka,” yule mhudumu aliniambia kisha akageuka na kuanza kuondoka taratibu eneo lile na wakati akitembea akili yangu ikajikuta ikizidi kupumbazika na mtikisiko maridhawa wa makalio yake.

Nilijikuta nikikiri moyoni kuwa japo Jiji la Dar es Salaam lilifurika wasichana warembo kupindukia na wengi wao wakiwa wameuongeza urembo wao wa asili maradufu kwa vipodozi lukuki, lakini msichana huyo mhudumu hakuwa wa kawaida kabisa machoni mwangu. Alikuwa na ziada juu ya uzuri wake.

Ziada hiyo haikutokana na rangi ya asili ya ngozi yake, la hasha! Haikutokana na lile tabasamu lake maridhawa lililofanikiwa kuichanganya akili yangu. Hali kadhalika, ziada hiyo haikutokana na umbile lake refu na zuri lililofinyangwa kiufundi na muumba, haikutokana na yale macho yake malegevu yenye kushawishi, pua yake ndogo iliyochongoka wala meno yake mazuri meupe yaliyojipanga vizuri kinywani mwake. Hata hivyo, alikuwa na ziada! Lakini ziada hiyo ilikuwa ipi? Ni swali lililoanza kunitesa.

Niliendelea kujiuliza wakati nikimsindikiza yule msichana mhudumu kwa macho hadi pale alipoifikia kaunta ya jikoni ya ukumbi ule wa maakuli na kisha akageuza shingo yake kunitazama, macho yetu yalipogongana msichana yule aliyaondosha haraka macho yake na kutazama chini kwa aibu huku akiachia tabasamu maridhawa la aibu. Ni hapo sasa nilipobaini ile ziada iliyonivutia kwa msichana huyo. Haya!

Nilijikuta nikivutiwa sana na jambo hilo! Niliamini kuwa katika karne hii kukutana na msichana mzuri wa aina ile, tena akifanya kazi ya uhudumu kwenye Club, mwenye haya lilikuwa jambo gumu mno! Lakini msichana huyo alikuwa mmoja kati ya wasichana wachache sana duniani waliobakia na haya.

Yule msichana alitokomea kwenye ile kaunta ya jikoni ya ukumbi ule wa maakuli huku akiniacha nikijisikia faraja ya kipekee kabla ya mawazo yangu kurudishwa pale mezani baada ya kugundua kuwa sikuwa peke yangu, kulikuwa na mtu mwingine aliyekuwa ameongezeka.

Alikuwa msichana fulani mrefu mwenye asili ya Kiarabu akiwa amevaa fulana nyeusi iliyoandikwa kwa maandishi makubwa ya kubandika 'Kiss Me’ yaliyotulia juu ya kifua chake chenye matiti yenye chuchu zilizosimama kama zilizokuwa zikinidhihaki. Kichwani alivaa kofia nyeusi ya kapelo yenye nembo ya mwanamapinduzi Che Guevara ikizifunika nywele zake ndefu, na suruali ya bluu ya dengrizi.

Aliitua mkoba wake mdogo na simu yake ya kisasa aina ya Iphone 13 Pro Max na kuviweka mezani huku akinitazama kwa tabasamu.

“Nimeona si vibaya kama nitaungana nawe hapa,” yule msichana alisema huku mikono yake akiiegemeza juu ya meza. Alinitazama kama aliyekuwa akisubiri ruhusa yangu, usoni hakuonesha kuwa na wasiwasi wowote.

“Aliyekwambia meza ya baa ina mwenyewe nani? Karibu sana,” nilimjibu yule dada wa Kiarabu huku nikimtazama kwa umakini na kwa kufanya vile nikaweza kumtathmini vizuri. Mfinyanzi alikuwa ametulia kwa umakini wakati wa kumuumba yule dada hasa sura na shepu yake isipokuwa miguu! Haikunivutia, japokuwa haikuwa myembamba lakini pia haikuwa ile tunayoiita ya bia.

“Hujambo lakini?” yule msichana alinisalimia huku akiulegeza uso wake na kutabasamu.

“Mimi sijambo, sijui wewe?” niliongea kwa utulivu huku nikimtazama usoni.

“Niko poa. Nadhani si vibaya tukafahamiana, kama hutojali… mimi naitwa Sharifa Mbwana mwenyeji wa Tanga, sijui mwenzangu waitwa nani?” yule dada aliniuliza huku tabasamu maridhawa likichomoza usoni mwake na kuusuuza moyo wangu.

“Naitwa Alishanto Mbaga,” nilimwambia yule mrembo kwa kujiamini kana kwamba lile lilikuwa jina langu halisi. Akacheka sana

“Ha! Hilo ni jina au matusi?” yule mrembo aliniuliza huku akinitazama moja kwa moja machoni. Nikatabasamu.

“Kwani wewe si ulitaka kujua jina langu au uli…?” nilimuuliza lakini nikakatisha swali langu baada ya yule dada mhudumu kurudi pale mezani huku mikononi akiwa amebeba sinia kubwa la chajio, sasa alikuwa akinitazama kwa jicho la wizi huku lile tabasamu lake la kibiashara usoni likijitokeza kwa mbali.

Yule mhudumu aliinama kwa utulivu akalitua lile sinia juu ya ile meza mbele yangu na kitendo kile cha kuinama kidogo kikayafanya macho yangu yaone matiti yake. Nikasisimkwa kwani matiti yalikuwa na mvuto wa kipekee. Kwa kuwa alikuwa akinitazama kwa wizi akashtuka na kuitengeneza vizuri blauzi yake huku akiona aibu kidogo mbele yangu.

Nikamtazama usoni mrembo yule huku nikitabasamu tukio lile likamfanya atabasamu kidogo kwa aibu huku akiyakwepesha macho yake pembeni yasikutane na yangu na tabia yake ile ya heshima ikazidi kunitia mshawasha. Na hapo Sharifa akaonekana kutovumilia. Akamwambia yule dada mhudumu, “Mhudumu, halafu utuletee na chupa ya Dodoma Wine tafadhali,” kisha akanigeukia, “Au unasemaje?”

“Ahsante, mimi sinywi pombe, labda maji tu,” nilimjibu na hapo nikaanza kukishambulia chakula changu kwa kuwa nilikuwa na njaa.

Sharifa alinitazama kwa kitambo kifupi kisha akashusha pumzi halafu akatoa noti kadhaa na kumpa yule dada mhudumu akimwambia akate na chakula nilichoagiza. Dakika mbili baadaye chupa Dodoma Wine na bilauri moja vikawa vimeletwa mezani, Sharifa akajimiminia mvinyo kwenye bilauri na kuanza kunywa taratibu. Ni wakati huo nilipopata wasaa mzuri wa kumchunguza kwa jicho la wiziwizi.

Hisia zangu zikanifanya nijisikie furaha kwa kuketi pamoja na msichana kama yeye hasa nilipogundua kuwa watu wengine waliokuwa mle ndani ya ule ukumbi wa chakula walikuwa wakitutazama kwa jicho la wivu. Hakika tulipendeza sana na kuonekana kama wapenzi tulioshibana na kuendana vizuri sana. Wakati nikiendelea kupata mlo nikagundua kuwa hata Sharifa alikuwa akinitazama kwa jicho la wizi.

Alipoona nimemshtukia akainamisha uso wake kutazama ndani ya ile bilauri ya mvinyo kwa kitambo kama aliyeona kitu kisha akainua uso wake taratibu kwa madaha kana kwamba alikuwa anaigiza filamu, mara macho yetu yakakutana. Kwa takriban dakika nzima macho yetu yalitulia yakitizamana kama watu ambao tulikuwa tukisomana fikra zetu, kisha Sharifa aliyahamisha macho yake na kutazama kando.

Muda huo huo sauti ya kuashiria kuwa ujumbe mfupi wa maneno ulikuwa umeingia kwenye simu yangu ya mkononi ukasikika, nikaitoa simu mfukoni na kuitazama vizuri. Ulikuwa ujumbe kutoka kwa Luteni Lister aliyetaka kujua nipo wapi na kama nilifanikiwa kumpata Sajenti Mambo!

Nikafungua sehemu ya kutuma ujumbe na kumwandikia nikimweleza hali halisi na hatua niliyofikia kwenye harakati zangu. Wakati nikifanya vile Sharifa alikuwa akinitazama kwa kuiba iba, hata hivyo sikumtilia maanani.

Ule ujumbe wa taarifa fupi ulipoenda nikairudisha simu yangu mfukoni huku nikishusha pumzi ndefu. Kitendo cha kuiweka simu yangu mfukoni kinakifanya kugundua jambo, Sharifa alikuwa makini kufuatilia kila nilichokuwa nikikifanya kwenye simu yangu na nilipoiweka mfukoni naye akaichukua simu yake ya mkononi haraka pale mezani na kuitazama kisha akayahamishia macho yake kunitazama kidogo kabla ya kuyahamishia pembeni.

Endelea...
 

320

“Vipi, kuna tatizo?” nilimuuliza Sharifa huku nikimtazama kwa umakini usoni.

“Hapana, nilikuwa naangalia saa,” Sharifa aliniambia huku akinyanyua bilauri yake ya mvinyo na kupiga funda kubwa. Nikashangaa iweje atazame saa kwenye simu wakati alikuwa amevaa saa ya mkononi! Hata hivyo nikapuuzia.

Muda huo huo simu yake ya mkononi ikaanza kuita, akaitazama kwa kitambo akionekana kama aliyekuwa akijishauri iwapo aipokee au aipotezee, kisha akabana taya zake na kuikata. Halafu akainua mkono wake wa kushoto kutazama saa yake ya mkononi na kukunja sura yake. Nikashangaa zaidi.

Kisha alichukua chupa ya Dodoma Wine na kumimina mvinyo katika bilauri yake japokuwa bilauri hiyo ilikuwa bado ina mvinyo nusu, alikuwa akimimina huku akiwa hatazami kwenye bilauri na alionekana kuwaza mbali. Bilauri ile ilijaa na mvinyo ukaanza kumwagika juu ya meza Sharifa akiwa hana habari. Nikamshtua, wakati huo mvinyo ulishaanza kulowesha kwenye suruali yake, akashtuka na kuruka huku akinitazama kwa aibu.

Kwa kuwa mvinyo ulimwagika na kuanza kusambaa juu ya meza Sharifa aliondoa haraka mkoba na simu yake toka juu ya meza huku akisonya, kisha huku akinitazama kwa jicho la wizi, akaondoka haraka kuelekea maliwato.

Hisia tofauti zilianza kuumbika kichwani mwangu, moyo wangu nao ulipiga kite kwa nguvu, hata hivyo niliendelea kutulia kwenye kiti changu nikimalizia chakula. Jambo moja nilikuwa na uhakika nalo, kuwa Sharifa alikuwa amemwaga ule mvinyo makusudi, kwa kuwa wakati ile bilauri ikiwa imejaa aliitupia jicho kisha akayahamisha macho yake akijifanya kutazama kando na kuendelea kumimina hadi nilipomshtua. Na hata mshtuko wake ulikuwa wa kuigiza.

Nilihisi kuwepo kwa hila fulani na hapo nikatamani kumfuatilia kule maliwato ili nijue nini kilikuwa kinaendelea lakini sikuweza kufanya hivyo. Nilipoyatupa macho yangu juu ya ile meza nikakiona kikaratasi kilichokunjwa vizuri, ambacho awali sikuweza kukiona kwa kuwa kilikuwa chini ya mkoba, nikashawishika kukichukua na kukifungua. Na hapo nikajikuta nikipigwa na butwaa. Karatasi ile ilikuwa na ujumbe ulioandikwa:

Jason Sizya, nakushauri uachane na upelelezi huu uliojiingiza na ufunge mdomo wako, la ukikaidi nakuhakikishia kwamba hatatuchukua siku moja kwa familia yako kuwa mikononi mwetu, tutawakata kiungo kimoja kimoja na watakufa taratibu lakini kwa maumivu makubwa. Hatukutishi ila tunakushauri zingatia ushauri huu na familia yako haitaguswa.

Kama kuna kitu ambacho sikukipenda maishani mwangu basi ni suala la kutishiwa maisha yangu au familia yangu. Sasa nilijikuta nikisisimkwa mwili wangu na damu ikaanza kunichemka na kukimbia kwenye mishipa yangu ya damu, vinyweleo mwilini na nywele kichwani zilinisisimka kwa hasira huku mapigo ya moyo yakianza kwenda mbio!

Sikusubiri, nikaikunja ile karatasi na kuinuka, nikaelekea kwenye maliwato ya wanawake alikokuwa ameelekea Sharifa, lakini nikiwa na tahadhari zote kichwani. Nilipofika nikasimama kwa muda pale katika mlango wa kuingilia huku nikisikiliza kwa makini, baada ya kuhakikisha hali ni shwari nikaingia nikiwa na nia moja tu, kumbana Sharifa anieleze ukweli.

Nilipoingia nikajikuta nimetokea kwenye ukumbi mpana na msafi wa maliwato uliokuwa na masinki kadhaa ya kunawia mikono. Nikayazungusha macho yangu kutazama eneo lile na kuiona milango kadhaa ya vyoo. Nikaanza kutembea kwa tahadhari nikiwa makini kutafuta ni choo kipi alichokuwa ameingia Sharifa. Wanawake wawili waliingia mle ndani na waliponiona wakashtuka, nikawapa ishara kuwa wasiwe na wasiwasi, nikaendelea kumtafuta Sharifa. Hata hivyo hakuwemo mle vyooni.

Nilipochunguza vizuri nikagundua kioo cha dirisha moja kilikuwa kimeondolewa na Sharifa alikwisha toweka. Sikutaka kusubiri, nikatoka mbio na kuelekea ukumbini kisha nikaufuata mlango mkubwa wa kutokea nje nikiwa sitaki kumpoteza Sharifa.

Kule nje manyunyu yalikuwa yamekata lakini kulikuwa na wingu zito lililoashiria kuwa mvua kubwa ilikuwa mbioni kunyesha. Bado hakukuwa na dalili za uwepo wa Sharifa, nikaamua kutoka kabisa katika eneo lile na kuvuka barabara kisha nikaelekea upande wa pili uliotazamana na ile Club, ambako kulikuwa na kijiwe cha madereva wa teksi waliokuwa wakisubiria abiria. Baadhi ya madereva hao walianza kunichangamkia, sikuwajali.

Nikaangaza macho yangu huku na huko lakini hakukuwa na dalili yoyote ya Sharifa. Kwa mwendo wa miguu, nikaanza kuondoka eneo lile nikiifuata Barabara ya Mwinjuma, sikutaka kuchukua teksi eneo lile kwa kuogopa kujiingiza kwenye hatari. Sikuwa nikimwamini mtu.

Wakati nikiwa natembea taratibu kando ya barabara, nyuma yangu kulikuwa na watu wawili waliokuwa wakija upande ule ule niliokuwepo na walikuwa wametokea katika Club ile ile. Niliporudisha uso wangu mbele nikamwona mtu mmoja akija upande niliokuwepo, sikuonesha kugwaya, nikapeleka mkono wangu kiunoni na kuipapasa bastola yangu na hapo mwili ukanisisimka, nikaendelea kutembea kwa mwendo ule ule.

Nilipofika katikati, wa nyuma na wa mbele wakiwa umbali sawa, nikasimama na kuinama nikijifanya kufunga vizuri kamba za viatu vyangu na wakati huo nikisubiri nione watu hao wangechukua hatua gani. Nilisubiri kuona kama wangesita basi ningeng’amua kuwa walikuwa watu wabaya kwangu lakini kama si watu wabaya wangepita na hamsini zao.

Yule aliyekuwa akija mbele yangu aliendelea na hamsini zake lakini wale watu wawili waliokuwa wakija nyuma yangu walisita kidogo, wakawa kama wanaojiuliza jambo huku mmoja akijifanya kutoa simu yake na kuanza kuongea, kwa vitendo hivyo nikajua wazi kuwa nilikuwa nawindwa. Nilichoamua ni kugeuza na kuanza kurudi kule kwa wale watu wawili, na hapo nikawaona wakiingiwa na woga fulani, nikaongeza mwendo kuwaendea.

Haraka sana nikamwona mmoja wao akipeleka mkono wake kiunoni huku akiniamuru nisimame. Nikakaidi amri yake na kuanza kuwapita kwa mwendo ule ule. Nilipowapita kwa hatua mbili tu wakageuka na mmoja wao tayari alishatoa bastola na kuanza kuielekeza kwangu. Jambo hilo nililitegemea tangu mwanzo nikageuka haraka kwa teke maridadi la karate na kuupiga mkono wake wenye bastola, ikamtoka na kuanguka chini.

Akiwa bado hajakaa sawa nikampiga konde moja lililotua shavuni, akaenda chini. Yule wa pili akarusha ngumi nikaudaka mkono wake na kuuzungusha haraka, halafu nikauvunja. Akapiga yowe kali la uchungu huku macho yakimtoka pima kama mjusi kabanwa na mlango. Kabla hajakaa sawa nikaachia ngumi kali kwenye shingo na kuvunja taya lake, akaanguka chini akiwa hana fahamu.

Yule wa kwanza alikuwa ameshainuka, akanijia na kurusha mapigo matatu ya haraka haraka, nikayaona na kuyakwepa, na kwa haraka akanipiga teke kali la tumboni, nikahisi kichefuchefu cha ghafla huku maumivu makali yasiyo na mfano yakisambaa mwilini.

Kabla sijakaa sawa akanitandika teke la nguvu kwenye korodani. Maumivu niliyoyasikia hapo yalifanya nigande kama sanamu. Alipoleta ngumi ya usoni nikajibetua nyuma na kusimama. Mapigo mengine mawili ya karate yaliponijia shingoni nikayakinga katika namna ya kuyapunguza nguvu kisha kwa nguvu zangu zote nikapeleka ngumi moja matata na kuuvunja mwamba wa pua ya yule mtu, akapepesuka na kupoteza mhimili.

Sikusubiri atulie, nikamuwahi kwa mapigo mengine mawili lakini yule mtu alikuwa makini sana, akayapangua mapigo yale kama mchezo na kunikwepa. Nguvu nyingi nilizowekeza kwenye mapigo yale na kumkosa zikanifanya nipepesuke kama mlevi. Yule mtu akaruka teke la kuzunguka na kunishindilia teke mgongoni nikaanguka chini bila kupenda huku maumivu makali yakisambaa mgongoni mwangu. Hakika yule mtu alikuwa mpambanaji matata mwenye mwili ulioshiba.

Pigo jingine la teke lilipokuja nikawahi kuliona na kuinama chini kidogo kulikwepa na hapo pigo lile likakata upepo bila mafanikio. Nikajipinda na kumchota mtama wa nguvu, akapaa hewani huku akiweweseka, nikamsubiri atue ili nimwadhibu lakini yule mtu alikuwa mjanja na kutua chini kama paka kwa miguu yake miwili na mkono mmoja chini huku akinitazama kwa hasira.

Kisha akanyanyuka tayari kwa mpambano, kabla hajaamua afanye nini nikainua mguu wangu wa kulia kama niliyetaka kumpiga teke akakinga mikono yake, nikazunguka kwa kasi ya ajabu na kuachia teke mzunguko la mguu wa kushoto lililotua kifuani kwake, akaanguka chini, na hapo mapigo matatu makini yakavunja mbavu zake na kumfanya apige yowe kali la maumivu huku damu ikianza kumtoka mdomoni.

Muda huo watu walishaanza kujaa eneo lile, sikutaka kuendelea kupoteza muda kwa kuhofia wenzao wangefika na mambo kuwa magumu zaidi, hivyo nikaondoka haraka na kuvuka barabara kisha nikaingia kwenye kichochoro fulani, nikapotelea kizani.

* * *

Harakati za Jason Sizya bado zinaendelea, na sasa mambo yanazidi kunoga, endelea kufuatilia hadi mwisho...
 
ALISHANTO MBAGA leo kidigo apasuliwe korodani BAHARIA ANGEUMALIZA MWENDO ila bahati ilikua kwake
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…