Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

View attachment 2385020
320

“Vipi, kuna tatizo?” nilimuuliza Sharifa huku nikimtazama kwa umakini usoni.

“Hapana, nilikuwa naangalia saa,” Sharifa aliniambia huku akinyanyua bilauri yake ya mvinyo na kupiga funda kubwa. Nikashangaa iweje atazame saa kwenye simu wakati alikuwa amevaa saa ya mkononi! Hata hivyo nikapuuzia.

Muda huo huo simu yake ya mkononi ikaanza kuita, akaitazama kwa kitambo akionekana kama aliyekuwa akijishauri iwapo aipokee au aipotezee, kisha akabana taya zake na kuikata. Halafu akainua mkono wake wa kushoto kutazama saa yake ya mkononi na kukunja sura yake. Nikashangaa zaidi.

Kisha alichukua chupa ya Dodoma Wine na kumimina mvinyo katika bilauri yake japokuwa bilauri hiyo ilikuwa bado ina mvinyo nusu, alikuwa akimimina huku akiwa hatazami kwenye bilauri na alionekana kuwaza mbali. Bilauri ile ilijaa na mvinyo ukaanza kumwagika juu ya meza Sharifa akiwa hana habari. Nikamshtua, wakati huo mvinyo ulishaanza kulowesha kwenye suruali yake, akashtuka na kuruka huku akinitazama kwa aibu.

Kwa kuwa mvinyo ulimwagika na kuanza kusambaa juu ya meza Sharifa aliondoa haraka mkoba na simu yake toka juu ya meza huku akisonya, kisha huku akinitazama kwa jicho la wizi, akaondoka haraka kuelekea maliwato.

Hisia tofauti zilianza kuumbika kichwani mwangu, moyo wangu nao ulipiga kite kwa nguvu, hata hivyo niliendelea kutulia kwenye kiti changu nikimalizia chakula. Jambo moja nilikuwa na uhakika nalo, kuwa Sharifa alikuwa amemwaga ule mvinyo makusudi, kwa kuwa wakati ile bilauri ikiwa imejaa aliitupia jicho kisha akayahamisha macho yake akijifanya kutazama kando na kuendelea kumimina hadi nilipomshtua. Na hata mshtuko wake ulikuwa wa kuigiza.

Nilihisi kuwepo kwa hila fulani na hapo nikatamani kumfuatilia kule maliwato ili nijue nini kilikuwa kinaendelea lakini sikuweza kufanya hivyo. Nilipoyatupa macho yangu juu ya ile meza nikakiona kikaratasi kilichokunjwa vizuri, ambacho awali sikuweza kukiona kwa kuwa kilikuwa chini ya mkoba, nikashawishika kukichukua na kukifungua. Na hapo nikajikuta nikipigwa na butwaa. Karatasi ile ilikuwa na ujumbe ulioandikwa:

Jason Sizya, nakushauri uachane na upelelezi huu uliojiingiza na ufunge mdomo wako, la ukikaidi nakuhakikishia kwamba hatatuchukua siku moja kwa familia yako kuwa mikononi mwetu, tutawakata kiungo kimoja kimoja na watakufa taratibu lakini kwa maumivu makubwa. Hatukutishi ila tunakushauri zingatia ushauri huu na familia yako haitaguswa.

Kama kuna kitu ambacho sikukipenda maishani mwangu basi ni suala la kutishiwa maisha yangu au familia yangu. Sasa nilijikuta nikisisimkwa mwili wangu na damu ikaanza kunichemka na kukimbia kwenye mishipa yangu ya damu, vinyweleo mwilini na nywele kichwani zilinisisimka kwa hasira huku mapigo ya moyo yakianza kwenda mbio!

Sikusubiri, nikaikunja ile karatasi na kuinuka, nikaelekea kwenye maliwato ya wanawake alikokuwa ameelekea Sharifa, lakini nikiwa na tahadhari zote kichwani. Nilipofika nikasimama kwa muda pale katika mlango wa kuingilia huku nikisikiliza kwa makini, baada ya kuhakikisha hali ni shwari nikaingia nikiwa na nia moja tu, kumbana Sharifa anieleze ukweli.

Nilipoingia nikajikuta nimetokea kwenye ukumbi mpana na msafi wa maliwato uliokuwa na masinki kadhaa ya kunawia mikono. Nikayazungusha macho yangu kutazama eneo lile na kuiona milango kadhaa ya vyoo. Nikaanza kutembea kwa tahadhari nikiwa makini kutafuta ni choo kipi alichokuwa ameingia Sharifa. Wanawake wawili waliingia mle ndani na waliponiona wakashtuka, nikawapa ishara kuwa wasiwe na wasiwasi, nikaendelea kumtafuta Sharifa. Hata hivyo hakuwemo mle vyooni.

Nilipochunguza vizuri nikagundua kioo cha dirisha moja kilikuwa kimeondolewa na Sharifa alikwisha toweka. Sikutaka kusubiri, nikatoka mbio na kuelekea ukumbini kisha nikaufuata mlango mkubwa wa kutokea nje nikiwa sitaki kumpoteza Sharifa.

Kule nje manyunyu yalikuwa yamekata lakini kulikuwa na wingu zito lililoashiria kuwa mvua kubwa ilikuwa mbioni kunyesha. Bado hakukuwa na dalili za uwepo wa Sharifa, nikaamua kutoka kabisa katika eneo lile na kuvuka barabara kisha nikaelekea upande wa pili uliotazamana na ile Club, ambako kulikuwa na kijiwe cha madereva wa teksi waliokuwa wakisubiria abiria. Baadhi ya madereva hao walianza kunichangamkia, sikuwajali.

Nikaangaza macho yangu huku na huko lakini hakukuwa na dalili yoyote ya Sharifa. Kwa mwendo wa miguu, nikaanza kuondoka eneo lile nikiifuata Barabara ya Mwinjuma, sikutaka kuchukua teksi eneo lile kwa kuogopa kujiingiza kwenye hatari. Sikuwa nikimwamini mtu.

Wakati nikiwa natembea taratibu kando ya barabara, nyuma yangu kulikuwa na watu wawili waliokuwa wakija upande ule ule niliokuwepo na walikuwa wametokea katika Club ile ile. Niliporudisha uso wangu mbele nikamwona mtu mmoja akija upande niliokuwepo, sikuonesha kugwaya, nikapeleka mkono wangu kiunoni na kuipapasa bastola yangu na hapo mwili ukanisisimka, nikaendelea kutembea kwa mwendo ule ule.

Nilipofika katikati, wa nyuma na wa mbele wakiwa umbali sawa, nikasimama na kuinama nikijifanya kufunga vizuri kamba za viatu vyangu na wakati huo nikisubiri nione watu hao wangechukua hatua gani. Nilisubiri kuona kama wangesita basi ningeng’amua kuwa walikuwa watu wabaya kwangu lakini kama si watu wabaya wangepita na hamsini zao.

Yule aliyekuwa akija mbele yangu aliendelea na hamsini zake lakini wale watu wawili waliokuwa wakija nyuma yangu walisita kidogo, wakawa kama wanaojiuliza jambo huku mmoja akijifanya kutoa simu yake na kuanza kuongea, kwa vitendo hivyo nikajua wazi kuwa nilikuwa nawindwa. Nilichoamua ni kugeuza na kuanza kurudi kule kwa wale watu wawili, na hapo nikawaona wakiingiwa na woga fulani, nikaongeza mwendo kuwaendea.

Haraka sana nikamwona mmoja wao akipeleka mkono wake kiunoni huku akiniamuru nisimame. Nikakaidi amri yake na kuanza kuwapita kwa mwendo ule ule. Nilipowapita kwa hatua mbili tu wakageuka na mmoja wao tayari alishatoa bastola na kuanza kuielekeza kwangu. Jambo hilo nililitegemea tangu mwanzo nikageuka haraka kwa teke maridadi la karate na kuupiga mkono wake wenye bastola, ikamtoka na kuanguka chini.

Akiwa bado hajakaa sawa nikampiga konde moja lililotua shavuni, akaenda chini. Yule wa pili akarusha ngumi nikaudaka mkono wake na kuuzungusha haraka, halafu nikauvunja. Akapiga yowe kali la uchungu huku macho yakimtoka pima kama mjusi kabanwa na mlango. Kabla hajakaa sawa nikaachia ngumi kali kwenye shingo na kuvunja taya lake, akaanguka chini akiwa hana fahamu.

Yule wa kwanza alikuwa ameshainuka, akanijia na kurusha mapigo matatu ya haraka haraka, nikayaona na kuyakwepa, na kwa haraka akanipiga teke kali la tumboni, nikahisi kichefuchefu cha ghafla huku maumivu makali yasiyo na mfano yakisambaa mwilini.

Kabla sijakaa sawa akanitandika teke la nguvu kwenye korodani. Maumivu niliyoyasikia hapo yalifanya nigande kama sanamu. Alipoleta ngumi ya usoni nikajibetua nyuma na kusimama. Mapigo mengine mawili ya karate yaliponijia shingoni nikayakinga katika namna ya kuyapunguza nguvu kisha kwa nguvu zangu zote nikapeleka ngumi moja matata na kuuvunja mwamba wa pua ya yule mtu, akapepesuka na kupoteza mhimili.

Sikusubiri atulie, nikamuwahi kwa mapigo mengine mawili lakini yule mtu alikuwa makini sana, akayapangua mapigo yale kama mchezo na kunikwepa. Nguvu nyingi nilizowekeza kwenye mapigo yale na kumkosa zikanifanya nipepesuke kama mlevi. Yule mtu akaruka teke la kuzunguka na kunishindilia teke mgongoni nikaanguka chini bila kupenda huku maumivu makali yakisambaa mgongoni mwangu. Hakika yule mtu alikuwa mpambanaji matata mwenye mwili ulioshiba.

Pigo jingine la teke lilipokuja nikawahi kuliona na kuinama chini kidogo kulikwepa na hapo pigo lile likakata upepo bila mafanikio. Nikajipinda na kumchota mtama wa nguvu, akapaa hewani huku akiweweseka, nikamsubiri atue ili nimwadhibu lakini yule mtu alikuwa mjanja na kutua chini kama paka kwa miguu yake miwili na mkono mmoja chini huku akinitazama kwa hasira.

Kisha akanyanyuka tayari kwa mpambano, kabla hajaamua afanye nini nikainua mguu wangu wa kulia kama niliyetaka kumpiga teke akakinga mikono yake, nikazunguka kwa kasi ya ajabu na kuachia teke mzunguko la mguu wa kushoto lililotua kifuani kwake, akaanguka chini, na hapo mapigo matatu makini yakavunja mbavu zake na kumfanya apige yowe kali la maumivu huku damu ikianza kumtoka mdomoni.

Muda huo watu walishaanza kujaa eneo lile, sikutaka kuendelea kupoteza muda kwa kuhofia wenzao wangefika na mambo kuwa magumu zaidi, hivyo nikaondoka haraka na kuvuka barabara kisha nikaingia kwenye kichochoro fulani, nikapotelea kizani.

* * *

Harakati za Jason Sizya bado zinaendelea, na sasa mambo yanazidi kunoga, endelea kufuatilia hadi mwisho...
Pamoja Sana bishop
 
Harakati za Jason Sizya sehemu ya TAHARUKI haitabiriki kabisa, kongole mkuu Bishop. Umesuka visa na matukio katika upeo wa juu sanaa.....hakika ndio maana ya taharuki nasi tupo katika taharuki kuliko Jason Sizya mwenyewe.
 
taharuki..jpg

321

Saa 6:15 usiku…

Baada ya kushushwa na teksi katika Mtaa wa Isevya nikaanza kutembea taratibu kuelekea Mtaa wa Kibasira ambako nyumba niliyokuwa nikiishi ilikuwepo. Muda wote akili yangu ilikuwa bado inamfikiria mwanadada Sharifa Mbwana. Huyu mwanamke ni nani hasa? Aliwezaje kujua kuwa nilikuwepo pale Nuru Club muda huo? Na alifikaje pale kwenye meza yangu pasipo kugundua na badala yake nikashtukia tu tayari ameshakaa?

Wakati nikitembea huku nawaza nikajikuta nimetokeza katika Mtaa wa Kibasira, na kwa mbali nikaliona gari moja likiwa limesimama kwenye mti mkubwa wa kivuli, mbele ya nyumba yangu. Shaka ikanipata.

Hata hivyo sikuwa na uhakika kama gari lile lilikuwa limesimama mbele ya nyumba yangu kwa kuwa mtaa ule ulikuwa mrefu kiasi kwamba hata kama ni mchana isingekuwa rahisi kuona nyumba za mwanzo au hata za mwisho wa mtaa huo, achilia mbali mida hii ya usiku wenye giza nene, giza totoro. Giza ambalo lilimudu kufifisha mwanga wa umeme uliothubutu kutoka katika baadhi ya majumba ya ghorofa ya mtaa huu, na kufanya mwanga huo wa umeme kuonekana kama vibatari.

Nikasimama kwanza huku nikijaribu kulichambua gari hilo. Kwa kuwa mtaa huu ulikuwa na giza nikaamua kusogea kidogo ili nipate kuliona vizuri. Na hapo nikagundua kuwa lilikuwa gari aina ya Lexus la rangi ya fedha na lilisimama mbele ya nyumba yangu.

Macho yangu yakawa makini kutazama eneo lile liliposimama gari hilo, na mara nikamwona mwanamke mmoja akitokea ndani ya geti kubwa jeusi la nyumba yangu, akapanda ndani ya gari hilo upesi. Utembeaji wake na mavazi yake yakanifanya nimtambue mara moja. Alikuwa ni Daniella. Nikashtuka sana. Ina maana hawa watu wameamua kunifuata hadi nyumbani? Nikajiuliza.

Nikiwa bado sijajua nifanye nini nikamwona mwanamume mmoja mrefu akiwa amesimama kando ya gari. Alikuwa amevaa suruali nyeusi ya dengrizi, kofia kubwa ya pama iliyofunika uso wake na koti refu jeusi. Sikujua mwanamume huyo alitokea wapi! Nilishtukia tu kumwona akiwa anaegemeza mikono yake dirishani mwa gari na alionekana kuongea jambo na mtu au watu waliokuwemo ndani ya lile gari.

Kisha alitazama huku na kule, akapanda kwenye gari hilo na muda huo huo gari lile likaondoka kwa mwendo wa kasi. Nililisindikiza gari lile kwa macho mpaka lilipopotelea mtaani kisha nikatoka pale mafichoni na kuelekea nyumbani kwangu, lakini nikiwa nina tahadhari zote.

Nilipofika usawa wa geti la nyumba yangu nikafanya kama ninayepita kuendelea mbele nikiwa na nia ya kupima upepo ili nibaini kama kulikuwa na usalama eneo lile, na hapo nikamsikia mlinzi wa nyumba yangu, kutoka kampuni ya ulinzi ya Gadi Security, akikohoa kabla ya kufuatisha kwa mluzi wimbo wa mwanamuziki wa kizazi kipya, Marioo, wa ‘Bia Tamu’.

Nikashusha pumzi na kulisogelea geti kisha nikabonyeza kengele ya getini, yule mlinzi ambaye aliitwa Kibwana Majaliwa akachungulia kwenye kidirisha kidogo cha getini na kuniona, akashusha pumzi na kufungua geti ili kuniruhusu kuingia ndani ya uzio mpana wa nyumbani kwangu. Nilipoingia akalifunga lile geti huku akinisalimia kwa bashasha, nikamwitikia na kabla sijamuuliza chochote kuhusu wale watu waliokuja pale nyumbani usiku huo Kibwana akaanza kusema huku akitweta, “Samahani sana, mista Sizya…”

“Bila samahani, Kibwana, unasemaje?” nilimjibu huku nikiwa makini mno.

“Dah… kuna jambo tu nataka nikwambie mkuu, yaani nilisahau kabisa kukwambia… Jana jioni kiasi cha saa kumi na moja na nusu hivi, alikuja bwana mmoja akasema anahitaji sana kuonana na wewe lakini hataki ijulikane kama ameonana na wewe,” Kibwana alisema na kunifanya niwe makini zaidi kumsikiliza huku nikiuhisi moyo wangu ukipiga tiktaka ndani ya kifua changu, lakini nilijitahidi kuwa msikivu.

“Leo tena mchana akaja na kuniuliza kama nilikwambia, nikamwambia nilisahau. Sasa amekuja tena usiku huu na wametoka hapa muda si mrefu, safari hii akiwa na mdada fulani hivi mzuuuri,” Kibwana alisema huku akitoa macho ya matamanio na kumeza mate ya uchu.

Ingawa sasa moyo wangu ulikuwa anaenda mchaka-mchaka ndani ya kifua changu lakini hiyo haikunizuia kuachia tabasamu kwa sababu namna Kibwana alivyokuwa akimwelezea Daniella nilifahamu kabisa kuwa yeye pia alikuwa ‘mgonjwa’ sana kwa wanawake. Hata hivyo sikufahamu mwanamume aliyeambatana na Daniella kuja nyumbani kwangu alikuwa nani.

“Yukoje huyo mtu? Na mbona hujamwelekeza aje ofisini kwangu?” nilimuuliza Kibwana kwa shauku.

“Dah… sasa hapo ndo ninapomshangaa yule mtu, alisema anapajua ofisini kwako lakini hawezi kuja huko eti kuna nyoka, na wala hawezi kukupigia simu… na hata alipokuja hapa mara zote alikuwa amevaa miwani myeusi ya jua na kofia kubwa ya pama iliyoficha uso wake… Ajabu hata usiku huu alipokuja tena alikuwa amevaa miwani myeusi ya jua na alikuwa kama ana wasiwasi hivi!” Kibwana alisema.

“Hakutaja jina lake au sehemu anayotokea?” nilimuuliza tena Kibwana huku maswali mengi yakianza kupita kichwani mwangu. Nilijiuliza angekuwa nani na kwa nini hakutaka kuja ofisini kwangu na badala yake aje nyumbani? Tena katika muda ambao alijua fika kuwa siwezi kuwepo nyumbani? Halafu… ni nyoka yupi aliyemwogopa pale ofisini kwangu?

“Hapana… hakunipa nafasi ya kumuuliza maswali,” Kibwana alisema na kushusha pumzi. Kabla hajaendelea nikawahi kumtupia swali lingine.

“Wala hajaacha ujumbe wowote?” nilimuuliza na hapo nikamwona akijipapasa kwenye mifuko ya gwanda lake la kazi na kutoa kipande cha karatasi kilichokinjwa vizuri.

“Ameniachia karatasi hii…” Kibwana alisema huku akinipa karatasi ile. kisha akaongeza, “Amesisitiza sana ikufikie wewe tu na si mtu mwingine. Na kwamba ili niwe salama ni lazima mtu yeyote zaidi yako asijue kwamba nimepewa ujumbe nikufikishie kwani hataki niingie kwenye matatizo.”

Nilimtazama Kibwana kwa sekunde kadhaa, nikauona uso wake ukiwa na mashaka makubwa. Nikaifungua ile karatasi na kukuta maandishi yaliyokuwa na ujumbe mfupi:

“Mstari mwekundu unaelea kwenye kina kirefu, ni paku… pute ni popo kwenye nanga…”

Ulikuwa ujumbe mfupi lakini wenye maana kubwa. Nilishtuka sana kwa ujumbe ule kwa kuwa niliitambua lugha ile, ilikuwa lugha ya kijasusi kisha nilimtupia jicho Kibwana, nikamwona akinitazama kwa wasiwasi mkubwa na shauku ya kutaka kujua nini kilikuwa kimeandikwa kwenye ile karatasi.

Niliielewa lugha iliyotumika kwenye ujumbe huo: “Mstari mwekundu” ilimaanisha hatari kubwa iliyoonekana na “kina kirefu” ilimaanisha siri kubwa ya wenye nguvu ambayo haikupaswa kabisa kufahamika.

Endelea...
 
taharuki..jpg

322

“Paku” katika lugha ile ya kijasusi ilimaanisha moja, na “pute” ni mbili… neno “popo” lilimaanisha msaliti ofisini, na “nanga” ni kazi. Hivyo nilielewa kuwa mwandishi wa ujumbe ule alimaanisha kuwa kulikuwa na hatari kubwa baada ya kugundua siri ya wakubwa, hilo ni jambo moja aliloliona… na hatari ya pili ilikuwepo ofisini ambako kulikuwa na msaliti, na kwamba hatari zote zilinikabili na nilitakiwa kuzifanyia kazi.

Chini kabisa ya ile karatasi kulikuwa na maneno fulani yaliyoandikwa: “G2603H70=RM” Hapa ilikuwa ni maelezo yenye herufi na namba tu bila ufafanuzi wake.

Nilitambua kuwa hizi zilikuwa ‘codes’ (mafumbo) na ziliandikwa kwa ugumu hasa na zilihitaji umakini sana au wataalamu wa code ili kuzifungua. Nilizitazama zile codes kwa kitambo fulani nikijaribu kuzifungua lakini nikagundua kuwa nisingeweza kwani muda huo akili yangu haikuwa imetulia. Na hivyo niliishia kutumbua macho tu pasipo kuambua chochote.

Dah! Nilihisi hofu ikinitambaa mwilini mwangu, mitupo ya mapigo ya moyo wangu ikaongezeka mara dufu na nywele zikanisimama kichwani kwa tahadhari. Mara moja nikayapeleka macho yangu kumtazama Kibwana na macho yetu yalipokutana niliweza kuiona hofu iliyokuwa imejengeka usoni mwake.

“Ooh! Nimeshamtambua, huyu ni mmoja kati ya jamaa niliosoma nao chuoni, ana matatizo makubwa sana, kadhulumiwa mali zake na mtu mmoja mkubwa serikalini na anahitaji msaada wangu…” nilimwambia Kibwana huku nikiachia tabasamu katika namna ya kumzuga. “Nadhani natakiwa kumtafuta usiku huu huu niongee naye ili kuona namna ya kumsaidia, unajua nina marafiki wengi watu wa usalama na ninaamini watamsaidia.”

Niliposema hivyo nikauona uso Kibwana ukisajili mshangao tu. Kibwana hakuwa akijua lolote kuhusu kazi yangu ya ushushushu, zaidi alijua kuwa nilikuwa mwandishi wa habari. Hata hivyo sikumpa muda wa kufikiri wala kuongea zaidi.

“Ahsante sana Kibwana kwa taarifa hii. Ngoja niangalie mazingira ili nimfuatilie, na kama akija tena tukapishana mweleze kuwa ujumbe wake nimeupata na ninaufanyia kazi, sawa?” nilimwambia Kibwana.

“Bila shaka, mzee,” Kibwana alijibu akiniita mzee. Alipenda kuniita mzee japo alinizidi umri.

Sikusubiri, nikaondoka haraka kuelekea ndani kwangu huku nikimwachia Kibwana noti ya shilingi elfu tano, nikaona akifurahi sana na kuahidi kuwa pindi yule jamaa akitokea tena angempa taarifa na kisha angenipigia simu kuniambia.

Nilianza kutembea haraka kuelekea ndani huku nikiyatupa macho yangu kuangalia huku na huko. Kichwani mawazo yalianza kunitawala. Nilifungua mlango wa nyumba yangu na kuingia ndani kisha nikapanda ngazi haraka haraka kueleka juu ghorofani kilipokuwa chumba changu. Sasa kichwani mwangu kulikuwa kuna mgongano wa mawazo. Niliazimia jambo moja tu, niwatafute akina Luteni Lister na Pamela usiku huo ili tuongee kuhusu jambo lile.

_____

Saa 8:20 usiku…

Muda huu ulitukuta tukiwa nyumbani kwa Luteni Lister eneo la Oysterbay. Timu nzima ya watu watatu ilikuwa imekamilika, tulikuwa tumeketi kwenye bustani iliyokuwa ndani ya uzio mpana wa nyumba ya Lister. Tukiwa tumeketi kwa utulivu, bilauri za pombe kali zilikuwa mkononi na taratibu tulikunywa huku tukijadiliana kile kilichotukusanyisha pale usiku huo.

Kwa mbali, muziki laini toka kwenye redio kubwa iliyokuwa sebuleni ulisikika kwa sauti ambayo haikutufanya tushindwe kusikilizana. Wakati huu jiko kubwa la kuoka nyama lilikuwa limekokwa moto huku Luteni Lister akiwa bize kuweka weka mafuta ili nyama iwe tamu, nzuri na laini.

“Wandugu, kabla Jason hujatueleza nini kilichotokea ngoja kwanza niwajuze juu ya kile ambacho Ikulu imetuomba tukitupie jicho. Tunajua kuwa hata kama tusingeombwa tayari jambo hili lipo katika hati ya maagizo tuliyopewa na DGIS ila kwa sasa ni agizo kutoka kwa mheshimiwa Rais, hatuna budi kulitilia mkazo…” Luteni Lister alisema nasi tukatikisa vichwa.

“Mheshimiwa Rais amesifia sana akisema tumefanya kazi nzuri mno, hasa amekusifu wewe Jason, anataka kukutana na wewe siku moja kwani sifa zako amezisikia, kwanza ilikuwa toka kwa Rais wa Kenya na sasa toka kwa mkurugenzi mkuu wa Idara!” Luteni Lister alisema, “lakini kazi ndiyo kwanzaa inaanza, mheshimiwa Rais amesema anataka aone watu wote waliopo kwenye orodha ya mgawo wa fedha, pasipo kujali nyadhifa zao, wanakamatwa kwa ushahidi madhubuti na kufikishwa mahakamani.”

“Kasema hivyo?” niliuliza kilevi levi.

“Ndiyo! Tena kasisitiza sana, kwa kuwa kesho ndiyo siku ya kumzika waziri wetu Ummi Mrutu, anataka kuona hatua zikichukuliwa kabla ya kuondoka kuelekea jijini Dodoma,” Luteni Lister alinijibu.

“Ooh, kumbe kesho ndiyo mazishi ya waziri! Atazikwa wapi?” niliuliza.

“Hapa hapa Dar es Salaam, kwenye makaburi ya Kinondoni,” Lister alisema.

“Basi sawa. Na suala aliloagiza Rais ni wajibu wetu daima kuweka rehani maisha yetu, kama atakavyo atawaona watu hawa wakiwa nyuma ya nondo hivi karibuni,” nilisema kwa kujiamini.

Muda wote Pamela alikuwa kimya kabisa, hakutaka kuongea wala kujibu swali. Kisha nami niliwaeleza jinsi nilivyohangaika kumtafuta Sajenti Mambo kila mahali bila mafanikio kabala sijakutana na Sharifa na yote yaliyotokea pale Nuru Club, hadi nilivyokuta ujumbe nyumbani kwangu.

Baada ya hapo nikawapa ile karatasi yenye ujumbe wa kijasusi niliyoikuta nyumbani. Tuliutazama ule ujumbe na kila mmoja wetu aliweza kuutafsiri ule ujumbe lakini shida ilikuwa kwenye lile fumbo! “G2603H70=RM”. Hapa kila mtu alijikuta akitweta kidogo.

“Kama mnavyoona hapo, huyo jamaa ametumia code ngumu kuandika na binafsi nimeshindwa kuambua hata neno moja…” niliwambia.

Baada ya kusugua bongo zetu kwa muda tukijaribu kuzifungua zile codes “G2603H70=RM”, hatimaye tulikubaliana watumiwe wataalamu wa masuala ya codes ili watusaidie kuzifungua na tupate jibu kabla ya saa sita mchana. Usiku ule ule Luteni Lister aliwasiliana na mkurugenzi mkuu wa Idara, mzee Rajabu Kaunda na kumwomba atusaidie kuwapatia wataalamu wa codes ili watufungulie, halafu Luteni Lister akamtumia zile codes kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi.

Baada ya hapo tukaendelea kunywa na kula nyama choma tukijipongeza japo kazi ilikuwa bado mbichi kabisa.

“Dah, kama mambo yenyewe ndo hivi kila siku nitakuwa natia timu hapa maana Luteni umejua kutuwekea mavitu si ya kitoto,” nilitania wakati nikitafuna pande la nyama choma.

“Ndo hivyo, tule tunywe maana kazi yenyewe hii tufanyayo haina guarantee, wadogo wangu…” Luteni Lister alisema.

“Hiyo ni kweli kabisa,” Pamela alidakia huku akijimiminia pombe kwenye bilauri yake na kugida.

Ilikuwa ni kawaida kwa Luteni Lister kuhifadhi nyama nyingi kwenye jokofu kwa ajili ya kula na kwa wageni waliomfikia nyumbani kwake. Hakupenda kwenda kwenye mabaa na kwenye mikusanyiko ya watu bali alipendelea kutulia nyumbani akiwa na marafiki wakila na kunywa. Hadi umri huo hakuwa ameoa ingawa alikuwa na watoto wawili wa kike kutoka kwa mama tofauti.

Endelea...
 
taharuki..jpg

323

Tukiwa pale nyumbani kwa Lister, suala la vinywaji vikali halikuwa la kutusumbua vichwa, tulikuwa na uwezo wa kunywa mpaka jioni na pale tulipotaka pombe zitutoke kichwani basi zingetutoka, tulijua ni kitu gani tungefanya ambacho kingetufaya turudi haraka katika hali yetu ya kawaida.

Ukiwa usiku mwingi na upepo mwanana ukitupepea toka baharini, kama mwanamume rijali nilijikuta nikishindwa kabisa kuvumilia kumtazama Pamela, nikawa natamani kumsogelea kisha nimkumbatie na kumbusu. Sikuwa tena na uwezo wa kustahimili. Tayari nilikuwa nimemaliza chupa nzima ya whisky na sasa akili yangu ilinituma kufanya jambo.

Japokuwa kazi ndo kwanza ilikuwa imeanza, ilikuwa bado mbichi, na Pamela alikuwa jasusi aliyezoea mikikimikiki kiasi cha kutokuwa na hisia za ngono, lakini akili yangu iliniambia si kila wakati ni wakati wa hatari. Si kweli kuwa kila chui huvaa ngozi ya kondoo! Pamela alikuwa msichana wa kawaida kabisa na pia alikuwa na matamanio kama wasichana wengine.

“Mbona hunywi?” Pamela alinizindua toka kwenye mawazo ya ngono yaliyoanza kuniteka.

“Dah, kinywaji kama hiki na upweke hakipandi kabisa. Ingekuwa tupo wawili tu hapa, na hayo macho yako mazuri yakiendelea kuniloga, ningekuwa tayari nimeshaku… ah, au basi!” nilisema kwa utani.

Kauli hiyo ilimfanya Pamela aangue kicheko kisha akapiga funda la pombe. “Nina nini miye hata uchanganyikiwe kiasi hicho!”

“Hujui una nini!” nilimuuliza huku nikijisogeza karibu yake, kauli ambayo ilimfanya Pamela azidi kucheka. Shingo yake ndefu aliilaza upande kidogo, macho yake kiasi yakilainika huku vidole vikiitua glasi ya pombe na kuanza kutekenyana.

Nikapitisha mkono wangu kwenye kiuno chake. Pamela akatulia huku akinitazama usoni kwa mshangao. Ilikuwa picha ya kusisimua, picha ya kuvutia, picha ambayo, kwa muda ilizifanya fikra zangu zichukue likizo na nafasi yake kuchukuliwa na hisia za ajabu, hisia za kimaumbile zilizonifanya niwaze kumtoa nguo moja moja kisha nimkumbatie akiwa kama alivyozaliwa! Dah, nilianza kujishangaa kwani haikuwa akili yangu bali akili ya pombe!

“Ni nini unawaza wewe?” Pamela aliniuliza huku akinitazama kwa macho yaliyorembua. Kabla sijamjibu, kwanza nilimtupia jicho Luteni Lister na kumwona amejiegemeza kwenye kiti na macho ameyafumba, huenda alikuwa amepitiwa na usingizi au alikuwa ametopea kwenye lindi la mawazo yaliyomfanya kimwili awepo pale lakini kimawazo awe mbali. Nikashusha pumzi ndefu.

“Kuna kitu kinanitatiza hapa,” nilisema nikiwa namtazama Pamela kwa macho yaliyojaa ubembe wa huba.

“Najua… ila pumzisha kichwa sasa. Au nikupatie ndimu ukate kilevi?” Pamela aliniuliza.

“Kwa nini nikate kilevi?” nilimuuliza kwa mshangao.

“Maana naona unaanza kuingiwa ana mawazo ya… au basi!” alisema kwa utani na kuangua kicheko.

“Unaonaje tukajipa mapumziko kidogo na kuburudisha mioyo yetu baada ya kazi hii?” nilimuuliza Pamela huku nikiendelea kumtazama kwa matamanio. “Naona kazi hii imekuwa ngumu kuliko nilivyotarajia, na hatujui itatupeleka mpaka wapi!”

Pamela aliachia tabasamu kisha akauliza, “Niambie wewe unafikiria nini?”

“Unajua napenda sana maeneo yaliyotulia sana kama sehemu za ufukweni hivi,” nilisema kisha nikatabasamu na kunywa pombe. “Ninapokuwa huko akili yangu hutulia kabisa kwa kuwa upepo ule hufukuza matatizo yangu kichwani.”

Pamela alinitumbulia macho kwa kitambo kidogo, kimya, kama aliyekuwa anatafakari jambo ambalo hakulielewa.

“Vipi, Pamela?” nikamuuliza. “Ni nini unawaza? Au haujapenda wazo langu?”

‘Hapana,” Pamela alijibu akitazama chini kwa muda kisha alitazama bilauri yake ya pombe halafu akayahamishia macho yake kwangu na macho yake yakagongana na ya kwangu. na hapo nikagundua kuwa siku zote nilipokutana naye sikuwa nikimchanganyia macho kwani sikuwa kugundua kama alikuwa na macho yake laini yanayobembeleza, macho ambayo si kwamba yalikuwa yanabembeleza tu, bali pia yalikuwa yanashawishi na kushurutisha. Wakati tukitazama, mara Pamela akacheka.

“Nini kimekufurahisha hivyo?” nilimuuliza nikiwa nimekunja ndita na kutabasamu kwa wakati mmoja.

“Jason, nimegundua kuwa mbali na uwezo mkubwa wa kishushushu ulio nao sikuwa najua kama uko charming na una vituko namna hii!” Pamela alisema.

“Vituko?” nilimuuliza kwa mshangao.

“Hujioni ulivyo! Napenda sana jinsi ulivyo maana wajua kufikiria haraka nini cha kufanya. Nadhani hiyo ni talanta uliyobarikiwa na Mungu mbali na mafunzo,” Pamela alisema kisha akagida pombe yote iliyokuwemo kwenye bilauri yake. “Nakubaliana na wewe, ni kweli tunahitaji mapumziko kidogo na kuburudisha mioyo yetu.”

Kwa kuwa pombe ilikuwa imenikolea na ilinishawishi kufanya jambo, maneno ya Pamela kwangu ilikuwa ndiyo ruhusu ya kufanya jambo langu, hivyo nikashusha pumzi ndefu kisha nikamkumbatia kwa nguvu na kumbusu mdomoni huku mkono wangu mmoja ukikiminya kiuno chake, kisha nikamsogeza karibu yangu na kukamtazama machoni.

“Jason, kwani nini shida?” Pamela aliniuliza akinitazama machoni. Alikuwa amelegeza macho yake na kinywa.

“Unataka kujua shida yangu?” nilimuuliza huku nikiendelea kumtazama machoni.

“Ndiyo. Shida yako nini?” Pamela alisema huku akitabasamu kwa mbali.

“Nikikwambia utakubali au…?” nilimuuliza na kumkonyeza kilevi huku nikiendelea kukiminya minya kiuno chake chenye mifupa miteke.

“Itategemea,” Pamela alisema na kuachia kicheko hafifu. Muda huo alikuwa anapumua kwa nguvu.

“Unaonaje tukiumalizia usiku huu kwa kupongezana kwa hatua nzuri tuliyofikia?” nilimuuliza huku nikimkazia macho. Na hapo nikamwona akiyakwepa macho yangu na kutazama kando akiwa kimya kidogo.

“Niwe mkweli tu, ningependa iwe hivyo lakini sitaki kumsaliti mkeo…” Pamela alisema kwa sauti ya chini huku akionekana kupumua kwa shida kidogo, “Namheshimu Rehema, sitaki kugombana naye na pia najua ukionja asali utataka kuchonga mzinga kabisa jambo ambalo sitaki litokee.”

Niliachia tabasamu kabla ya tabasamu hilo halijaunda kicheko kidogo, kisha nikamminya tena kiunoni kabla sijamvuta na kumbusu shingoni, halafu kwenye shavu kabla ya mdomo wangu kuhamia kwenye mdomo wake.

“Basi fanya hivi… nipe mara moja tu halafu uniambie koma! Nitakuelewa,” nilimnong’oneza sikioni. Sauti yangu ikaonekana kuusisimua sana mwili wake. Niligundua kuwa chuchu zake zilikuwa zimesimama na kuwa ngumu.

“Mh! Yana ukweli hayo? Maana nyie wanaume mkitaka jambo lenu…” Pamela alisema kwa sauti ya chini ya mahaba halafu akaiachia sentensi yake hewani pasipo kuimalizia. Mwili wake ulikuwa unatetemeka kwa ashki na alikuwa ananitazama machoni kisha akaachia tabasamu kwa mbali. Halafu akageuka kumtazama Luteni Lister, aliporidhika akanikonyeza na kuinuka akaelekea maliwato huku akigeuka kunitazama kwa macho ya mahaba yaliyokuwa yakinialika.

Nikataka kuinuka ili nimfuate, na hapo nikamwona Luteni Lister akiyafumbua macho yake na kunitazama huku akitabasamu. Tabasamu lake lilikuwa pana na kisha alikunja na kutikisa ngumi, “Safi sana!” Alinong’ona. “Nakwaminia jembe langu! Kaza hivyo hivyo mpaka kieleweke.”

Nikashangaa sana. Kumbe muda wote Luteni Lister alikuwa akiyasikia maongezi yetu wakati tukiongea!

“Sasa sikiliza… usilaze damu sasa, nyanyuka umfuate huko huko ukamalize mchezo,” Luteni Lister alinisisitiza kwa sauti ya chini huku akigeuka kutazama kule alikokuwa ameelekea Pamela.

Sikutaka kujivunga, nikanyanyuka na kupiga hatua za haraka kuelekea kule bafuni. Huku nyuma nikamsikia Luteni Lister akisema, “Nakukubali sana, mwanangu!”

* * *

Harakati za Jason Sizya bado zinaendelea, kwa kuwa wamechukua mapumziko kidogo nasi tuchukue mapumziko vile vile😀... tukirudi tena mambo yatakuwa byee!😀
 
nafikiri baada ya husen tuwa na riwaya zake bora za taharuki kwa mara ya kwanza nakutana na mtu mwenye uwezo mkubwa wa riwaya za taharuki.big up bishop
 
[emoji23][emoji23][emoji23][emoji23][emoji23]haya sasa vicheche wamekutana,ptuuuu jason malaya jaman
 
Back
Top Bottom