Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

narudi buzwagi.jpeg

63

Mshtuko Mkubwa!


Saa 12:30 jioni…

REHEMA alikuwa amesimama mbele ya vioo virefu vya kujitazama vilivyokuwa kwenye meza ya vipodozi mle chumbani. Alikuwa amevaa vazi la Jampsuit la rangi ya maruni lililomkaa vyema, viatu vya ngozi vya rangi ya maruni miguuni vyenye visigino virefu na hereni za madini ghali ya tanzanite na green tourmaline zilizomfanya azidi kuonekana mrembo.

Muda huo alikuwa ameshika mkufu mdogo wa dhahabu wenye kung’aa tayari kwa kuuvaa. Mkufu ule nilimnunulia kama zawadi siku nilipomvisha pete ya uchumba. Alipoinyoosha mikono yake kwa lengo la kuuvaa mkufu huo, niliwahi nikaishika mikono yake laini na kuuchukua mkufu ule kisha nikamvalisha.

“Huwezi kupata taabu wakati mimi nipo,” nilimwambia kwa sauti ya chini iliyojaa mahaba kisha nikambusu.

Thank you, my love,” Rehema alinishukuru huku akinigeukia na kunikumbatia kimahaba.

Kwa upande wangu nilikuwa katika mwonekano wa kileo zaidi nikiwa nimevaa fulana nyepesi ya samawati niliyokuwa nimeichomekea vizuri kiunoni, juu yake nilivaa shati la kitambaa cha denimu la rangi ya bluu la mikono mirefu na suruali ya rangi ya bluu ya kitambaa cha denimu. Miguuni nilivaa buti ngumu za ngozi za rangi ya samawati, saa ya mkononi aina ya Quartz na kofia ya kitambaa cha denimu aina ya kapelo ya rangi ya bluu.

Kabla hatujatoka Rehema alichukua saa yake ndogo ghali na nzuri ya kike aina ya Cartier La Dona na kuivaa mkononi, na kuning’iniza begani mkoba wake mzuri mwekundu wa ngozi… kisha akanishika mkono tukaongozana kuelekea nje ambako tuliikuta teksi ikiwa inatusubiri.

“Ulivyopendeza utadhani malaika uliyeshushwa duniani kimakosa!” nilimtania Rehema wakati tukitoka nje. Rehema kama kawaida yake aliangua kicheko hafifu.

“Lakini malaika hawavai viatu vya mchuchumio,” Rehema alisema na sote tukacheka.

Dereva wa teksi ambaye muda wote alikuwa ametulia ndani ya gari lake aligeuza shingo yake kutuangalia na alipotuona alipigwa na butwaa asiamini macho yake kwa jinsi tulivyokuwa tumeendana na kupendeza isivyo kawaida.

Nilifungua mlango wa nyuma wa ile teksi na kumruhusu Rehema aingie ndani ya teksi kisha nilizunguka upande wa pili, nikaingia. Na hapo Rehema akamtaka dereva atupeleke Migombani Club iliyopo nje kidogo ya mji wa Ushirombo katika eneo tulivu la Migombani, kando ya barabara kuu inayoelekea Kahama.

Dereva aliiondoa teksi yake bila kusema neno na kuingia barabarani, baada ya muda mfupi tukatokea katika barabara kuu ya lami ya kuelekea Kahama, dereva akakata kona kuingia kushoto akiifuata barabara hiyo.

Niliangalia nje kupitia ukuta msafi wa kioo cha gari nikaona nyumba na vitu vikipita mbele ya macho yangu kwa kasi wakati ile teksi ikiwa inakwenda. Mara mawazo yakaanza kupita kichwani kwangu huku maongezi yangu na Rehema mchana wa siku ile yalisikika akilini kwangu.

“Najua ndoa hupangwa na Mungu, na si wote waliooana walitaka kuoana na hao waliooana nao, hata, si wote! Naomba uwe mkweli kwangu ili usizidi kuumiza moyo wangu… nimepewa miezi sita kuamua…” Niliyakumbuka vyema maneno hayo na kunifanya niwe katika wakati mgumu zaidi.

Nilitambua fika kuwa sikuwa mkweli kwa Rehema japo niliamini yeye alikuwa akinionesha mapenzi ya kweli na tulikuwa na nyakati za raha sana, ki ukweli mimi ndiye niliyekuwa nikiumiza moyo wake.

Suala la kwamba nilikuwa namtumia Rehema na kisha akichakaa niachane naye lilikuwa na ukweli fulani ndiyo maana wazee wake walitoa masharti niliyotakiwa kuyatimiza ndani ya miezi sita na sikujua ningeyatimiza vipi! Hali hiyo ilinipa wakati mgumu sana na nilianza kuogopa sana kwani dalili za kumpoteza Rehema zilianza kuonekana, kwa sababu sikujua udhati wa moyo wangu.

Nikaisikia sauti fulani ndani yangu ikiniuliza kama ni kweli sikutaka kumpoteza Rehema au nilikuwa naendeshwa na tamaa ya ngono tu?

Haikunipa shida kutambua kuwa Rehema alinipenda sana na hakuwa na hila yoyote dhidi yangu, na hata kama maneno aliyoniambia kuwa alipewa masharti ya miezi sita kutimiza takwa la wazee wake yasingekuwa na ukweli wowote, bado niliamini kuwa Rehema alinipenda sana kuliko kitu chochote. Niliona kuwa sasa ulikuwa ni wakati wangu wa kumwonesha mapenzi ya dhati na kuacha unafiki, sikupaswa kufanya kitu kingine isipokuwa kumpenda kwa dhati na nitimize ahadi ya ndoa niliyompa.

Rehema aliyarudisha tena mawazo yangu mle ndani ya teksi pale alipovunja ukimya kwa kuniambia kuwa tulikuwa tumefika, hii ilikuwa ni baada ya ile teksi kusimama mbele ya eneo la maegesho ya magari la Migombani Club. Kwa sekunde kadhaa niliyatembeza macho yangu kwa utulivu nikiyatazama mandhari ya ile club kwa umakini na tukio lile likaifanya akili yangu ishikwe na mduwao hafifu. Nikafungua mlango wangu na kushuka kisha nikazunguka upande wa pili, nikamfungulia Rehema.

Migombani Club ilikuwa club ya kisasa kabisa yenye vionjo vya daraja la juu kabisa kama ilivyo kwa club zingine za kisasa katika majiji makubwa. Rehema aliniambia kuwa club hiyo ilikuwa na kumbi kubwa za starehe ikiwemo ukumbi wa starehe wenye jukwaa zuri la kufanyia matamasha ya muziki na mikutano mbalimbali.

Pia ndani kulikuwa na huduma ya Wi-Fi (Wireless Fidelity), huduma ya mtandao wa intaneti kwa mtu yeyote mwenye kifaa kinachoweza kunasa taarifa za kimtandao wa intaneti kama simu za kisasa za mkononi au tarakilishi.

Pale nje ya club kulikuwa na magari kadhaa ya watu wenye vipato vya kueleweka waliofika kuifurahia ’week end’ yao yaliyokuwa yameegeshwa kwenye maegesho ya magari ya club ile. Tulipiga hatua taratibu kuingia kwenye lango kuu la club huku tukitembea kwa madaha.

Watu wachache waliokuwa wamesimama pale nje ya club wakiwa na mazungumzo yao waliacha maongezi yao na kugeuka kidogo kutuangalia kwa mshangao wakati tukikatiza katika viwanja vile vya maegesho kuelekea ndani. Kwa kweli tulikuwa tumependeza sana na kila jicho lilitamani kutuangalia muda wote. Tuliufikia mlango wa mbele wa ile Club tukiwa hatuwatilii maanani wale watu na badala yake tuliendelea na hamsini zetu.

Rehema akausukuma taratibu ule mlango, tukajitoma ndani na kutokezea kwenye ukumbi ya Baa, na hapo tukajikuta tukikabiliana tena na macho ya watu waliokuwa wameketi mle ndani wakiendelea na starehe zao. Watu wale haraka waligeuza shingo zao kututazama, kila mmoja kwa namna yake. Muda huo sauti ya muziki laini ilikuwa ikisikika taratibu mle ndani na hivyo kuzikonga vizuri nyoyo za watu wote waliokuwa mle ndani.

Ule ukumbi wa baa ulikuwa mkubwa kiasi wenye uwezo wa kuchukua watu wasiopungua mia moja kwa wakati mmoja bila bugudha yoyote huku ukiwa na meza nyingi fupi na pana zilizozungukwa na viti vizuri vya plastiki. Katika baadhi ya meza zile watu walikuwa wameketi kwa utulivu huku wakijipatia vinywaji. Runinga tatu bapa zilizokuwa zimetundikwa ukutani mle ukumbini zilikuwa zimejikita katika kurusha matangazo ya mpira wa miguu.

Watu waliendelea kutuangalia kwa umakini lakini hatukuwajali. Tulimaliza kukatisha katikati ya ukumbi ule na tulipokuwa mbioni kuifikia kaunta ya vinywaji upande wa kushoto Rehema akaniongoza kuufuata mlango mkubwa uliokuwa wazi lakini uliofunikwa kwa pazia zuri na jepesi, upande wetu wa kulia.

Hatimaye tulitokezea kwenye ukumbi mwingine mkubwa na wa kisasa wenye jukwaa zuri la kufanyia matamasha uliokuwa na madirisha makubwa ya vioo yaliyofunikwa na mapazia safi marefu yaliyosogezwa kando kidogo kuruhusu mwanga mdogo wa jua lililokuwa linazama kupenya kwa urahisi mle ndani.

Utulivu wa mandhari ya mle ndani ulikuwa wa hali ya juu sana uliomezwa na sauti ya muziki laini wa kubembeleza. Sauti ile tamu ya muziki laini kutoka kwa bendi moja ndogo iliyokuwa ikitumbuiza ukumbini ilirushwa kutoka katika spika zilizokuwa zimefungwa kwenye kona za dari ndani ya ukumbi ule.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

64

Kulikuwa na wahudumu wa kike warembo kweli kweli waliokuwa wakihudumia wateja waliokuwa mle ndani wameketi kwenye meza nzuri za mninga na viti vifupi vyenye foronya laini. Niliyatembeza haraka macho yangu mle ndani nikagundua kuwa idadi ya watu wengi waliokuwa mle ndani walikuwa ni watu wazito, wake kwa waume wenye vipato vikubwa au viongozi wa kiserikali na kwenye taasisi au mashirika.

Upande wa kulia wa ule ukumbi kulikuwa na mlango na dirisha dogo la jikoni na wapishi waliweza kuonekana kwa urahisi wakiwa katika mavazi yao ya kazi.

Mara tu tulipoingia mle ndani watu wote waligeuza vichwa vyao kutuangalia, wachache waliachana na sisi na kuendelea na hamsini zao lakini wengi waliendelea kutuangalia katika namna ya kutuhusudu kwa jinsi tulivyokuwa tumependeza. Wapo pia waliotuangalia kwa macho ya wivu. Nilifarijika mno kwa kitendo cha watu kutuonea wivu, japokuwa nilikuwa sipendi kuangaliwa na kugeuka kivutio, lakini siku hiyo nilijiona ni mwanaume mwenye thamani kubwa.

Nilitupa macho yangu haraka haraka kuyazungusha mle ndani, nikagundua kuwa karibia watu wote, wake kwa waume, waliendelea kutukodolea macho wakati tukiwapita kutafuta meza. Wengine walikuwa wananong’onezana, na sikuelewa ni kwa nini ilitokea vile, labda ni namna tulivyokuwa tumeendana na kupendeza.

Rehema aliniminya mkono na hapo tukazidi kuzitupa hatua zetu kwa utulivu tukitafuta sehemu nzuri ya kuketi. Ghafla bila kutegemea niliona kitu ambacho kiliushtua sana moyo wangu, kitu ambacho sikutegemea kabisa kukutana nacho katika mji wa Ushirombo, kikiwa katika ukumbi ule wa Migombani Club, na kwa muda ule!

Katika meza moja nilimwona Amanda, mwanadada mrembo mwenye umbo la namba nane ambaye alikuwa amevaa gauni la rangi ya pinki la kukata mikono lililolichora vyema umbo lake la namba nane na kuishia sentimita chache juu ya magoti yake huku mpasuo mfupi wa gauni hilo ukiliacha nusu wazi paja lake. Juu ya lile gauni alikuwa amevaa kitopu chepesi chekundu na miguuni alivaa skuna nyekundu zilizokuwa na visigino virefu.

Amanda alikuwa amekaa na mwanamume mmoja mtanashati ambaye sura yake ilikuwa ngeni kabisa machoni kwangu. Yule mwanamume alikuwa amevaa suti nzuri ya kijivu na viatu vyeusi vya ngozi.

Akiwa na umri wa miaka 25, Amanda alikuwa ameingia kwenye orodha ya warembo niliotoka nao kimapenzi na niliowapa ahadi ya kuwaoa. Kabla ya kuingia katika uhusiano huo, Amanda alikuwa mchumba wa mtu na niliweza kuichanganya akili yake kwa kiasi kikubwa na kusababisha uchumba huo uvunjike miezi miwili tu kabla hawajafunga ndoa.

Amanda aliamini kabisa kuwa ningeweza kumuoa, na kwa kuwa wakati huo Rehema alikuwa ameshahamia Ushirombo, basi nilikuwa na muda mwingi wa kufurahia penzi katika ulimwengu wa huba nikiwa na Amanda, akipika na kupakua.

Nilikutana na Amanda kwa mara ya kwanza nikiwa safarini, ndani ya basi la Makenga wakati nikielekea kwenye usaili wa kazi katika mgodi wa dhahabu wa Buzwagi kama ilivyoelezwa katika ule mkasa ambao uliandikiwa hadithi ya ‘Safari ya Buzwagi’.

Siku hiyo Amanda alikuwa anatokea Itobo kumwona mchumba wake aliyekuwa anaumwa. Kisha ukaribu wangu na Amanda ulikuja kukolezwa na rafiki yangu mkubwa tangu tukiwa Shule ya Sekondari ya Mzumbe, Swedi Mabushi, aliyekuwa mume wa dada wa Amanda.

Sasa mle ukumbini macho yangu na ya Amanda yaligongana na nikauona mshtuko wa wazi uliompata Amanda. Nadhani hata yeye hakutegemea kuniona sehemu ile na kwa muda ule, tena nikiwa na mwanamke mwingine japo alikuwa anamfahamu.

Amanda aliinamisha uso wake chini kuyakwepa macho yangu na kumfanya yule mwanamume aliyekaa naye kumshtukia baada ya kumwona alivyobadilika ghafla. Yule mwanamume aligeuza shingo yake kuangalia upande tuliokuwepo, aliponiona nikaona amani ikimtoweka ghafla. Sikujua kama alikuwa akinifahamu au lah.

Sikuwajali, nikaushika vizuri mkono Rehema na tukaendelea mbele. Hata hivyo, moyoni nilikuwa nimepatwa na mshtuko mkubwa kwani sikuwa nimetarajia kukutana na Amanda sehemu ile. Siku mbili tu zilizokuwa zimepita nilikuwa na Amanda nyumbani kwangu na nilimwambia kuwa ningekuwa na safari ya kwenda Tabora kuwasalimia wazee na ningerejea Kahama baada ya wiki moja.

Hivyo mshtuko ulionipata uliiondoa kabisa amani moyoni mwangu, hasa nilipoanza kujiuliza yule mwanamume aliyekuwa na Amanda alikuwa nani, na kwa nini Amanda hakuwa ameniambia kama angekuwa na safari ya kuja Ushirombo! Hii ilikuwa na maana kuwa alikuwa ameifanya safari hiyo kuwa siri ingawa sasa ilikuwa bayana!

Sikuwa na namna nyingine ya kufanya isipokuwa kujikausha kwani sikutaka kuiharibu furaha ya Rehema, msichana aliyeweza kuvumilia kila aina ya vitimbi toka kwangu, tangu tulipokuwa tunasoma. Mara Rehema akaiona meza moja tupu iliyokuwa imejitenga kwenye kona ya ukumbi ule na kunionesha. Na muda mfupi uliofuata tulikuwa tumeifikia meza ile, tukaketi na wakati huo Rehema aliwaona akina dada fulani wawili warembo waliokuwa wameketi na mwanamume mmoja katika meza ya tatu kutoka meza yetu.

Rehema aliinuka akanibusu mdomoni na kuniomba ruhusa ya kwenda kuwasalimia rafiki zake aliokuwa akifanya nao kazi kisha akawafuata, wakati wakisalimiana nilimwona akiwaonesha kwa kidole pale nilipokuwa nimeketi, na wote waligeuza shingo zao kuniangalia kisha wakaachia tabasamu la bashasha huku wakinipungia mkono kunisalimia na wengine walibetua vichwa vyao kukubaliana na jambo fulani ambalo Rehema aliwaambia.

Nikiwa nimeketi kwenye ile meza nilisogeza pazia la dirisha lililokuwa jirani nami na kuangalia nje, nikaweza kuyaona mandhari tulivu ya kuvutia nje ya ukumbi ule. Kulikuwa na nyasi nzuri za rangi ya kijani kibichi zilizopakana na maua ya rangi tofauti ya kuvutia. Nyasi zile zilikuwa zimepandwa kuzunguka bwawa moja la kuogelea na kando yake kulikuwa na viti vya kupumzikia vyenye miavuli mizuri ya kujikinga na mvua au miale ya jua.

Muda ule niliweza kuona watu wachache, wake kwa waume, waliokuwa wameketi kwenye vile viti wakiburudika na hakuna aliyekuwa akiogelea. Wengi walionekana kuzama katika maongezi ya faragha huku wakipata moja moto moja baridi. Kando ya bwawa lile kulikuwa na bustani nzuri ya miti yenye viti visivyohamishika katika mandhari tulivu.

Mara mawazo yangu yalihama toka kwa wale watu na kuanza kumuwaza Amanda. Kwa kweli sikutegemea kabisa kumwona pale Ushirombo akiwa na mwanamume mwingine. Nilitamani nimfuate nikamuulize na endapo angeshindwa kunipa majibu mazuri ningemtandika makofi pale pale mbele ya yule mwanamume. Japo sikuwa na mpango wa kumuoa lakini kila nilipozikumbuka nyakati nzuri za kimahaba nilizokuwa naye kwenye ulimwengu wa huba ilinifanya nitamani kummiliki peke yangu tu, kusiwepo na mwanamume mwingine.

Niliikumbuka siku ya kwanza ‘kutoka’ naye, nilimpeleka katika hoteli iliyotulia sana ya Pine Ridge, tulichukua chumba kikubwa chenye nafasi ya kutosha kilichokuwa na kitanda kikubwa cha mbao cha futi sita kwa sita chenye godoro la foronya laini lililofunikwa kwa shuka safi za rangi ya samawati, kwa siku tano tulikaa hapo tukijivinjari kwenye sayari ya huba…

My love, mbona hujaagiza chochote?” Rehema aliniuliza na kuyarudisha mawazo yangu mle ndani ya ukumbi baada ya kurudi toka katika ile meza ya rafiki zake.

“Nilikuwa nakusubiri ili tuagize kwa pamoja,” nilimwambia Rehema huku nikiachia tabasamu.

“Samahani kulikuwa na mambo fulani nilikuwa nawakumbusha kidogo wafanyakazi wenzangu, tupo ofisi moja japo idara zetu ni tofauti,” Rehema aliniambia huku akinibusu mdomoni kisha akaketi kwenye kiti.

“Nimewaona. Ni warembo hasa,” nilitania huku nikiangua kicheko hafifu lakini Rehema hakucheka na badala yake alikunja sura yake na kubetua midomo yake.

“Usithubutu tena kusema maneno hayo mbele yangu. Unajua kabisa nina wivu… sitaki nikuone ukiongea na mwanamke yeyote ukiwa hapa Ushirombo kwa sababu sitaruhusu jambo kama hilo litokee…” Rehema alisema huku uso wake ukiwa hauoneshi mzaha kabisa.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

65

Niliikunjia mikono yangu kifuani katika namna ya kuomba msamaha, nikamwona Rehema akiachia tabasamu. Wakati huo huo nikamwona mhudumu wa kike wa Migombani Club, msichana mrembo asiyezidi miaka 20, akifika na kusimama mbele ya ile meza yetu huku tabasamu la kibiashara likivinjari usoni pake. Nilipoyainua macho yangu kumtazama mhudumu yule kwa sekunde kadhaa macho yangu yakajikuta yakipumbazwa na uzuri wake.

Alikuwa msichana mzuri ambaye pia alikuwa amejiongezea urembo, japokuwa alikuwa amevaa sare za kazi lakini bado uzuri wake haukujificha kabisa. Macho yake yalikuwa makubwa na meupe yaliyozungukwa na kope ndefu na nyeusi, pua yake ilikuwa ndogo na mdomo wa kike ulikuwa na kingo nyembamba, na alikuwa na vishimo vidogo mashavuni vilivyochomoza haraka kila alipotabasamu.

Kifua chake kilikuwa cha wastani kilichobeba matiti ya wastani yenye chuchu imara zilizokuwa zikiisumbua blauzi yake ya rangi ya samawati aliyovaa, na chini alivaa sketi nyeusi fupi iliyoishia juu kidogo ya magoti na ilinasa kwenye kiuno chake chembamba huku nyuma akiwa na mzigo mkubwa wa makalio. Miguuni alivaa raba nzuri za kike za rangi nyeusi.

Nilijikuta nikiachia tabasamu pana baada ya kumsaili kwa macho na kuridhishwa na uzuri wake uliofanikiwa kuuteka moyo wangu kiasi cha kunifanya nisahau kuwa nilikuwa nimeketi na Rehema, ambaye muda wote alikuwa akiniangalia kwa umakini.

“Sijui ungependa tuagize nini?” sauti ya Rehema ilinizindua tena na kuyarudisha mawazo yangu kwenye kile kilichotupeleka pale. Nilipomwangalia Rehema nikagundua kuwa alikuwa ananiangalia kwa umakini sana, nikayakwepa macho yake na kuangalia nje ya ukumbi, kwenye bwawa la kuogelea, nikijifanya kama niliyekuwa nafikiria.

“Mmh… nadhani chochote unachopenda mpenzi, maana unajua mimi si mzuri katika uchaguzi wa vyakula,” hatimaye nilisema baada ya sekunde kadhaa za kufikiria huku nikiendelea kuangalia nje.

Rehema aliichukua kadi ngumu yenye orodha ya vyakula iliyokuwa juu ya ile meza akaipitia kwa utulivu kabla ya kuinua macho yake kumwangalia yule mhudumu. “Naomba tuletee kuku mzima wa kurosti kwa vitunguu saumu pamoja na chips,” Rehema alimwambia yule mhudumu.

“Na upande wa vinywaji?” yule mhudumu alimuuliza Rehema kwa sauti nyororo ya kumtoa nyoka pangoni huku akinitupia jicho la wizi.

“Tuletee passion juice na chupa kubwa ya maji,” Rehema alijibu na hapo nikamwona yule mhudumu akiitikia kwa kutikisa kichwa chake huku akitabasamu na wakati alipokuwa akijiandaa kuondoka eneo lile nikajifanya kumuuliza kitu, lengo langu likiwa ni kutaka kuisikia tena sauti yake nyororo.

“Sijui chakula kitachukua muda gani?” niliuliza huku nikiyatuliza macho yangu usoni kwake kwa tabasamu.

“Wala hakichelewi,” yule mhudumu alijibu huku akiendelea kutabasamu kisha akageuka na kuanza taratibu kuondoka eneo lile.

Alipokuwa akitembea mtikisiko maridhawa wa mzigo wa makalio yake ulianza kunitia msisimko. Rehema aliyahamisha macho yake toka kwa yule mhudumu na kuyahamishia kwangu, aliyatuliza usoni kwangu kujaribu kuyasoma mawazo yangu na hivyo kunifanya nishindwe kumwangalia yule mhudumu aliyeanza kuiteka akili yangu na kunipumbaza.

“Jason Sizya!” Rehema aliniita kwa jina langu kamili na kunifanya nishtuke, nilijua ana jambo.

“Unasemaje la azizi,” niliitika huku nikijitahidi kuachia tabasamu.

“Nimeshakwambia sitaki nikuone ukiongea na mwanamke yeyote ukiwa na mimi… utanisamehe kama ninakukwaza maana wewe ni mtanashati sana. Naogopa nisije nikaibiwa,” Rehema alisema na kuachia kicheko. Kwa jinsi alivyokuwa akiongea ungeweza kudhani labda alikuwa amelewa lakini hivyo ndivyo alivyo.

Kwa kawaida Rehema alikuwa mcheshi sana, mchangamfu na mwenye utani mwingi. Hata hivyo maneno yale hayakuwa ya utani na nilijua kuwa alimaanisha kile alichokuwa akikisema. Kuna wakati nilianza kujishangaa, iweje nihangaike na wasichana ambao wengi wao hawakuwa na staha kabisa wakati Rehema, msichana aliyejiheshimu, mstaarabu, mwenye kujali watu, mcheshi na mkarimu alikuwa akinipenda sana! Sifa zote hizi ndizo ziliwafanya ndugu zangu wampende sana Rehema.

Okay, sitaongea na mwanamke yeyote mbele yako lakini na wewe ukiwa na mimi usiongee na mwanamume yeyote. Tumeelewana?” nilimwambia Rehema kwa utani huku nikimtulizia macho usoni.

“Tumeelewana!” Rehema alijibu huku akiangua kicheko hafifu. Watu waliokuwa wameketi kwenye meza za karibu walikuwa wakituangalia kwa wivu jinsi tulivyokuwa tukifurahia uwepo wetu pale.

“Yaani mwanamume yeyote akiikaribia meza hii leo ninamrudisha alikotoka kwa makofi,” nilimwambia Rehema kwa utani na hapo tukaangua kicheko.

“Mmh, hivi umeshawahi kupigana katika maisha yako?” Rehema aliniuliza huku akiwa bado anacheka.

“Mara nyingi tu! Kwani umesahau kasheshe zangu tulipokuwa Morogoro?” nilijibu huku nikicheka.

“Aa wapi! Ulikuwa mpole kama nini ingawa ulikuwa kicheche! Sura yako yenyewe tu ni ya upole na haioneshi kama ni mtu wa vurugu!” Rehema alisema huku akiendelea kucheka.

Tuliendelea kuongea na kucheka tukiifurahia siku hadi nilipomwona yule dada mhudumu akirudi pale tulipoketi huku mikononi akiwa amebeba sinia kubwa lenye chakula tulichoagiza huku lile tabasamu lake la kibiashara usoni likikataa kabisa kwenda likizo. Alipofika pale mezani akainama kwa utulivu akilitua lile sinia juu ya ile meza mbele yetu, na kitendo kile cha kuinama kidogo mbele yangu kikanifanya niyaone matiti yake yenye mvuto wa kipekee.

Yule dada mhudumu alipogundua kuwa nilikuwa nikiyatazama matiti yake kwa matamanio aliachia tabasamu dogo la aibu huku akiyakwepesha macho yake pembeni yasikutane na yangu kisha akaitengeneza vizuri blauzi yake. Nilimtupia jicho Rehema nikamwona akiwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wangu, nikanywea…

Rehema aliachia mguno kwa sauti ya chini huku akitingisha kichwa chake, nikajikausha. Yule mhudumu aliondoka, akatuacha tukianza kula taratibu chakula tulicholetewa huku tukizungumza mawili matatu, ingawa muda huo muongeaji mkubwa alikuwa Rehema. Wakati tukila mawazo yangu yakahamia kwa Amanda, mara kwa mara niliyazungusha macho yangu kumtazama Amanda kwa jicho la wizi, nikagundua kuwa hata yeye alikuwa akinitazama kwa jicho la wizi na uso wake ulikuwa umesawajika sana.

Nilihisi kuwa Amanda alitamani tukio lile liwe ndoto kwani hakuwa ametegemea kabisa uwepo wangu pale. Nami kichwani kwangu nilikuwa nasumbuliwa na maswali kibao, kikubwa kilichokuwa kinanisumbua wakati huo ilikuwa ni kuhusu yule mwanamume aliyekaa na Amanda, nilijiuliza alikuwa nani? Walianza lini kukutana na kwa nini Amanda hakuwahi kuniambia kuwa alikuwa anakuja Ushirombo?

Muda wote tulipokuwa tunakula chakula nilikuwa kimya, na niliamini kuwa Rehema alikuwa ameigundua hali yangu na muda mwingi alijitahidi sana kunichangamsha kwa kunipigisha stori hizi na zile huku akicheka, baada ya kugundua nilikuwa nimepoteza uchangamfu.

Jason are you ok?” kuna muda Rehema aliniuliza kama nilikuwa sawa baada ya kushindwa kuvumilia.

Yes, I’m okay, my love,” nilimjibu Rehema kuwa nipo sawa huku nikiachia tabasamu.

Rehema aliniangalia kwa makini na kushusha pumzi za ndani kwa ndani kisha akanyanyua juu mabega yake na kubetua midomo kisha akaendelea kula kimya kimya.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

66

“Kama hakuna tatizo mbona huongei? Naona umenywea ghafla au eneo hili linakuboa?” Rehema aliniuliza tena huku akiniangalia kwa umakini.

“Wala hapajaniboa, na-enjoy chakula kitamu ingawa hawakufikii, mpenzi wangu,” nilijibu Rehema huku nikiachia tabasamu.

“Haya bwana,” Rehema aliongea kwa sauti tulivu iliyobeba uchovu. Lakini sikuona tashwishwi yoyote usoni kwake.

Muda huo nilijifanya kuzungusha macho yangu kuyatazama mandhari ya ukumbi ule lakini lengo langu lilikuwa kumwangalia Amanda. Katika uchunguzi wangu macho yangu yalianza kutua kwenye ile meza ya jirani iliyokuwa na wale akina dada wawili warembo na mwanamume mmoja, rafiki zake Rehema.

Hapo hayakukaa sana, niliyapeleka moja kwa moja kwenye meza aliyoketi Amanda na mwanamume wake, nikamwona akiinamisha kichwa chake chini kama aliyeona kitu kwenye miguu yake, aliangalia chini kwa kitambo kisha aliinua uso wake taratibu kwa madaha kana kwamba alikuwa anaigiza filamu, mara macho yetu yakakutana. Kwa nukta kadhaa macho yetu yalitulia yakitizamana kisha Amanda aliyahamisha macho yake na kutazama kando.

Muda huo huo nikamwona akiyashusha macho yake kuitazama simu yake ya mkononi ambayo ilikuwa inatoa mwanga na hapo nikatambua kuwa ilikuwa inaita. Aliitazama ile simu kwa kitambo akionekana kama aliyekuwa akijishauri jambo, akabana taya zake na kumnong’oneza jambo yule mwanamume aliyekuwa naye kisha akainuka na kusogea kando, sehemu isiyo na kelele za muziki na kuipokea kisha akaipeleka moja kwa moja sikioni.

Alionekana kuwa mtulivu sana alipokuwa akiongea na simu na muda wote alikuwa ananitupia jicho la wizi. Baada ya mazungumzo ya takriban dakika tatu huku sura yake ikibadilika kisha alikata simu na kuonekana akishusha pumzi kisha akarudi pale kwenye meza.

Nilihisi kuwepo jambo maana nilimwona akiongea jambo na yule mwanamume aliyekaa naye kisha akachukua chupa ya bia iliyokuwa juu ya meza na kuimiminia bia yote iliyokuwemo katika bilauri huku akinitupia jicho la wizi, kisha alinyanyua na kuigida bia yote na kuikita ile bilauri juu ya meza. Kisha alitupia tena jicho la wizi akionekana mwenye wasiwasi kabla hajanyanyua mkono wake kuitazama saa yake ya mkononi.

Niliendelea kumchora tu nikajisahau kuwa Rehema alikuwa ameketi pembeni yangu na alikuwa akiniangalia kwa umakini kila nilichokifanya. Amanda alinong’ona tena jambo kwa yule mwanamume aliyekuwa naye na kunyanyuka huku akinitupia jicho la wizi. Macho yetu yakagongana. Amanda akajifanya kutazama tazama huku na kule mle ukumbini kama aliyekuwa akitafuta kitu kisha nikamwona akiondoka haraka eneo lile, akaelekea kwenye vyumba vya maliwato.

Sikutaka kusubiri maana nilikuwa nahisi kuchanganyikiwa kadiri muda ulivyosonga, nikamwomba Rehema anielekeze vilipo vyumba vya maliwato, bila ajizi akanielekeza. Nilisimama nikaelekea huko na nilipomtupia jicho la wizi yule mwanamume aliyekuwa ameketi na Amanda nikagundua kuwa alikuwa akiniangalia kwa mashaka, lakini sikumjali. Nilisonga na hatimaye nikajikuta nipo mahala ambako kulikuwa na ukumbi mpana uliokuwa na picha mbili za kuchorwa zilielekeza vyoo vya wanawake upande wa kushoto na vyoo vya wanaume upande wa kulia.

Nikasimama katika eneo ambalo ningeweza kumwona kila aliyetoka katika vyoo vya wanawake nikiwa na nia ya kumsubiri Amanda ili nimbane hadi anieleze ukweli kuhusu yule mwanamume aliyekuwa naye na kwa nini alikuja Ushirombo bila kuniambia.

Mara nikamwona Amanda akitokea kwenye vyumba vya maliwato ya wanawake na aliponiona alishtuka sana akataka kurudi chooni lakini akasita, jasho lilikuwa linamtiririka na alikuwa na wasiwasi mwingi. Alijongea taratibu mahala nilipokuwa nimesimama huku akilazimisha tabasamu, alijifanya kutokuwa na shaka yoyote. Niliendelea kumwangalia kwa umakini nikiwa nimekunja uso wangu.

Aliponifikia tu nikamkamata kwa nguvu na kumvutia kwenye vyoo vya wanaume, na hapo tukajikuta tumetokea kwenye ukumbi mpana na msafi wa vyoo uliokuwa na masinki kadhaa ya kunawia mikono na kando kulikuwa na sehemu za kujisaidia haja ndogo. Niliyazungusha haraka macho yangu kutazama eneo lile huku nikiwa makini, sikumwona mtu yeyote zaidi yetu, nikaiona milango kadhaa ya vyumba vya maliwato. Sikusubiri, nikamshika mkono Amanda na kumpeleka kwenye chumba kimojawapo pasipo mtu mwingine kutuona.

Ni kama mwili wa Amanda ulikuwa umeingiwa na ganzi, hakuweza kunigomea wala kuzungumza chochote bali alifuata kila nilichomtaka kufanya na muda wote alikuwa ananiangalia kwa wasiwasi mkubwa huku jasho likimtoka. Tulipoingia mle chooni nikambana kwenye ukuta huku nikimkabili. Tukabaki tumetazamana.

Macho yake legevu yalinitazama kwa wasiwasi kama mtu ambaye alikuwa akijutia kosa fulani alilolifanya. Hisia zangu zilianza kuwa taabani na macho yangu yakaanza kufanya ziara ya kushtukiza kifuani pake na hapo kupitia kivazi chake nikaziona chuchu zake laini zilivyosimama kwa utulivu juu ya milima miwili kama zilizokuwa zikinidhihaki.

Macho yangu yakatambaa kuuangalia mwili wake na yalishuka hadi kiunoni na hapo nikaiona nyonga yake laini yenye mifupa miteke iliyopakana na mzigo imara wa makalio yaliyotuama vema. Wakati nikiwa katika hali ile ya mduwao mara nikakumbuka kuwa nilimfuata kule chooni kwa ajili ya kumuhoji na si kufanya mapenzi.

“Unafanya nini hapa Ushirombo?” nilimuuliza kwa hasira huku nikimkazia macho.

“Na wewe unafanya nini, kwani hapa ndo Tabora?” Amanda akaniuliza huku akikunja sura yake.

“Kwa hiyo tunashindana, siyo? Mimi nikifanya hivi na wewe unafanya vile?” nilimuuliza kwa hamaki huku nikimkazia macho, akabaki kimya akiwa ameinamisha uso wake. “Nitakutandika makofi sasa hivi.”

Amanda alibaki kimya akiniangalia kwa woga, alikuwa anapumua kwa shida na niliweza kuona jinsi mapigo ya moyo wake yalivyokuwa yakienda kasi isivyo kawaida.

“Niambie, yule mwanamume ni nani?” nilimuuliza kwa hasira lakini Amanda akaendela kubaki kimya huku akionekana kupumua kwa shida.

“Nakuuliza, yule mwanamume ni nani?” nililirudia tena swali langu.

“Naomba unisamehe mpenzi wangu,” Amanda alinisihi kwa sauti ya kunong’ona.

“Nikusamehe kwa lipi, naomba kwanza uniambie yule ni nani?” niliuliza kwa ukali huku nikimminya kwa nguvu pale ukutani. Amanda akaanza kutetemeka kwa hofu.

“Yule nii… nii… Jason naomba unisamehe, tutazungumza…” Amanda alitaka kusema lakini akaonekana kusita sana na kuinamisha uso wake chini. Alishindwa kuvumilia na sasa machozi yalikuwa yanamtoka.

Nilimtazama nikaona asingeweza kunijibu, na sikuwa na muda wa kuendelea kubembelezana kwani sikutaka kabisa Rehema ashtukie jambo lile baada ya kuona nimechukua muda mrefu kule chooni. Niliinua mkono wa kulia nikataka kumzaba kofi usoni, nikamwona akijikunja kwa hofu huku akitoa yowe hafifu la woga.

“Nakuuliza kwa mara ya mwisho, yule ni…” kabla sijamaliza Amanda alianza kulia na haraka akaipitisha mikono yake nyuma ya shingo yangu na kunikumbatia kwa nguvu kitendo kilichofanya chuchu za matiti yake kukitekenya kifua changu, nikahisi joto kali la mwili wake likitambaa kwa kasi mwilini kwangu na kufanya nijisikie faraja ya aina yake.

Ingawa nilikuwa nimekasirika sana lakini mbele ya Amanda nilijikuta nimekuwa kama mbwa muoga mbele ya chatu mwenye njaa kali. Bila kujua, kwa kiganja changu taratibu nikaanza kumfuta machozi lakini aliuondoa mkono wangu machoni mwake kisha akanisogezea mdomo wake kisha akaanza kuniporomoshea mabusu mfululizo mdomoni na hapo ndimi zetu zikakutana.

Kabla sijajua nini nifanye nikajikuta nikiishiwa nguvu na hapo tukaanza kubadilishana ndimi na kuufanya mwili wangu kusisimka kwa raha. Nilichoweza kusikia baada ya pale ilikuwa ni sauti nyepesi ya pumzi yake iliyokuwa ikipenya kwa fujo kwenye matundu ya pua yake. Nilitaka kuleta pingamizi lakini sikufanikiwa kwani sikuwa na ujasiri wa kupingana na hisia zangu.

Mikono yangu ikaanza kutambaa taratibu kwenye mwili wa Amanda huku kila mmoja akionekana kuwa na hamu na mwenzake japo mazingira hayakuruhusu. Nikaanza kulipandisha gauni lake juu haraka nikiwa nimedhamiria kumaliza mchezo humo humo chooni.

Mara nikahisi mlango mkubwa wa kuingilia maliwato ukifunguliwa na kisha nyayo za mtu au watu ziliingia na kusimama, kumbe hata Amanda alikuwa amezisikia lakini akazipuuzia. Mikono yangu ikaendelea kutambaa, kwa tahadhari, katika mwili wa Amanda na kumfanya azidi kulegea. Mara nikahisi kuwa zile nyayo za mtu zikija hadi pale kwenye mlango wa choo tulichokuwemo.

Kabla sijajua nifanye nini nikahisi mtu huyo akigusa kitasa cha mlango wa choo tulichopo na kukinyonga huku akiusukuma mlango kwa pupa, ukafunguka na hapo tukakatisha zoezi letu baada ya kumwona mwanamume akisimama pale mlangoni.

Niligeuka haraka kumwangalia kwa umakini nikiwa nimekasirishwa sana na kitendo chake cha kuvamia starehe za watu wengine lakini nilipomwona nikajikuta nikinywea. Alikuwa ni yule mwanamume aliyekuwa na Amanda, na alisimama akituangalia katika hali ya kutoamini kile alichokiona.

Amanda alishtuka sana, alimwangalia mara moja kisha akayarudisha macho yake kwangu kabla hajainamisha uso wake chini akionekana kutetemeka huku akiliweka vizuri gauni lake. Mapigo ya moyo wangu yakaanza kunienda mbio, si kwa sababu ya kumwogopa yule mwanamume ila kwa sababu ya ukweli kwamba kama yule mwanamume angeleta matata habari zingemfikia Rehema, na sikupenda kumuudhi.

“Amanda!” yule mwanamume alimaka kwa mshangao. “Nooo! Nooo…” alipiga kelele na taratibu nikamwona akilegea kabla hajaanguka na kupiga kichwa chake sakafuni, akapoteza fahamu. Amanda akachanganyikiwa.

Nami nilipatwa mshtuko mkubwa sana. Hata hivyo, akili yangu ilikuwa inafanya kazi haraka haraka sana.

“Sikia Amanda, nataka kesho urudi Kahama na mambo yote tutakwenda kuyamaliza huko, mchana nikukute umeshafika, sawa?” nilimwambia Amanda, akabetua kichwa chake kukubali na hapo nikatoka nje haraka nikimwacha ametaharuki asijue la kufanya.

Nilimkuta Rehema akiwa ameketi kitini kwa utulivu kama nilivyomwacha, niliketi kando yake huku nikilazimisha tabasamu ingawa uso wangu haukuweza kuficha wasiwasi niliokuwa nao, sikujua nini kingefuata baada ya yule mwanamume kuzinduka. Rehema alikuwa ananiangalia kwa umakini lakini aliendelea kuwa mtulivu sana. Sikujua alikuwa ananiwazia nini.

“Tuondoke, nimeshachoka kukaa hapa,” nilimwambia Rehema huku nikizungusha kichwa changu kuangalia upande ule wa kuelekea maliwato.

“Vipi, kuna tatizo lolote?” Rehema aliniuliza kwa sauti tulivu huku akiendelea kuniangalia kwa umakini sana.

“Hakuna tatizo, nimechoka tu kukaa hapa, nahitaji tukapumzike. Au kuna ubaya?” nilimuuliza huku nikiendelea kutabasamu. Hata hivyo moyoni nilikuwa na wasiwasi mkubwa nikiogopa kuumbuka.

Okay, as you wish!” Rehema alisema na kumwita mhudumu kisha akalipia kile chakula na vinywaji. Tukainuka na kutoka nje huku akimpigia simu dereva wa teksi iliyotuleta akimtaka atufuate.

* * *

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

67

Usinipigie Tena Simu.


Saa 2:50 usiku…

TULIINGIA ndani, nilitembea kwa kujivuta vuta hadi kwenye mojawapo ya sofa, nikajipweteka juu ya sofa huku nikipiga miayo ya uchovu. Rehema alinifuata akaketi kando yangu huku akiniangalia kwa utulivu. Nilikuwa nimedhamiria kuondoka siku iliyofuata kurudi Kahama na nilishayapanga maneno ya kumweleza Rehema ili asiweze kunishtukia. Nikakohoa kidogo kusafisha koo langu kabla sijamkabili.

“Rehema,” niliita kwa sauti tulivu huku nikimwangalia usoni.

“Abee!” Rehema aliitika kwa heshima huku akiniangalia machoni.

“Kesho narudi Buzwagi mara moja,” nilimwambia Rehema nikitegemea kuwa angeshtuka sana lakini sikumwona akishtuka, na badala yake aliachia tabasamu laini.

“Kuna nini Buzwagi?” Rehema aliniuliza kwa sauti tulivu na uso wake haukuwa na tashwishwi yoyote.

“Nataka nikaongee na Eddy kuhusu suala letu na ikiwezekana niende Tabora kwa wazee nikawafahamishe ili waharakishe mchakato wa suala la kupeleka posa kwenu,” nilisema huku nikijiweka vizuri pale kwenye sofa.

Okay!” Rehema aliongea kwa utulivu, lakini bado sikuona tashwishwi yoyote usoni kwake. “Kwa hiyo unarudi Buzwagi kwa ajili ya hili hili suala letu au unaondoka kwa sababu ya Amanda?”

Rehema aliniuliza huku akinitazama kwa umakini usoni, nilijikuta nikishtuka sana na uso wangu ulionesha maumivu makubwa baada ya kusikia Rehema akilitaja jina la Amanda.

“Amanda! Ndiyo nani?” nilijifanya sielewi chochote kuhusu Amanda.

“Kwa hiyo leo humjui Amanda?” Rehema alisema kwa msisitizo huku akiniangalia machoni. “Mwanamke mwenye mwili wa namba nane uliyemrubuni hadi akamkacha mchumba wake, yaani shemeji wa Swedi Mabushi!”

Dah! Mwili wangu wote uliingiwa ganzi kama niliyekuwa nimepigwa na ugonjwa mbaya wa kiharusi, nilifungua mdomo wangu kutaka kusema neno lakini maneno yakawa hayatoki. Nikabaki mdomo wazi huku nikijiuliza Rehema alimjuaje Amanda!

“Unashangaa nini au unadhani sielewi nini kinaendelea kati yako na Amanda?” Rehema aliongea huku akiachia tabasamu usoni kwake.

“Naona umekwisha jazwa maneno ya uzushi, mpenzi wangu…” nilijaribu kujitetea lakini Rehema akanikatisha kwa kuangua kicheko cha dharau.

“Labda niseme hivi… ninaelewa kila kitu kuhusu wewe na Amanda, nililijua hilo tangu siku tulipokutana safarini wakati mkienda kufanya usaili wa kazi katika mgodi wa dhahabu wa Buzwagi. Ninaelewa kuwa ulivunja uchumba wake kwa kuwa ulimwahidi kumuoa, ninaelewa kuwa alikuwa analala nyumbani kwako baada ya mimi kuhamia huku Ushirombo…” Rehema aliongea kwa tuo kwa sauti tulivu akijitahidi kuzuia hasira.

“Ninaelewa kuwa kule chooni Migombani Club hukuwa umekwenda kujisaidia bali ulimfuata Amanda, na ninaelewa kuwa yule mwanamume wake aliwafuata kule chooni baada ya kupatwa na wasiwasi na akawafumania. Kama ni uongo bisha!” Rehema alisema na kuachia kicheko hafifu, hakikuwa kicheko cha furaha wala dharau bali kilibeba hasira kali kuliko hata sumu ya nyoka.

Nilibaki kimya nikiwa sijui niseme nini, kwani Rehema alionesha kuyajua mengi kuhusu mimi na Amanda.

“Ila kuna kitu bado hukijui…” Rehema aliongeza baada ya kuniona nipo kimya. “Amanda na huyo mwanaume hawajaanza leo, mwanamume huyo kafa kaoza kwa Amanda, na sasa yupo mbioni kutuma washenga waende kwa wazazi wake wakatoe mahari ili aoe… anaitwa Michael Bundala, mfanyabiashara mkubwa hapa Ushirombo, anamiliki maduka makubwa ya nguo na spea za magari katika miji ya Ushirombo, Kahama na Geita.”

“Aisee!” nilijikuta nikiropoka kwa mshangao kama punguani.

Nilianza kuhisi joto kali sana likitambaa mwilini mwangu baada ya kusikia maneno yale. Kwa kweli sikujua kama Amanda alikuwa amevuka kiwango, nikavua shati langu na kuliweka kando, kisha nikabakiwa na fulana nyepesi ya ndani. Rehema alikuwa ameninasa sawa sawa mahali ambapo nisingeweza kujinasua, nilibaki nimetahayari kama mtoto aliyekutwa akiopoa nyama jikoni.

Nilishangaa sana, Rehema aliyafahamu vipi mambo yote aliyokuwa akinieleza! Kilichonitisha zaidi ni kwamba sikuelewa alianza kuyafahamu mambo hayo tangu lini na kwa nini hakuwahi kuniambia na badala yake alibaki kimya na siri yake moyoni! Nilitamani kumuuliza mambo mengi ya kumhusu Amanda na yule bwana lakini niliogopa, maana sikutaka kuendelea kumkwaza Rehema.

“Najua una maswali mengi kichwani kwako, na unajiuliza nimeyajuaje yote haya. Fahamu tu kuwa, ninajua kila kitu unachokifanya hata kama nipo mbali na wewe,” Rehema aliyakatisha mawazo yangu. Muda wote alikuwa anatabasamu ila tabasamu lake lilikuwa limeficha kitu, lilificha hasira aliyokuwa nayo na kunifanya nianze kumwogopa.

“Nayajua mengi kwa kuwa wewe ndiye maisha yangu. Wewe ndiye uliyeyashika maisha yangu na nimekukabidhi funguo za moyo wangu ili uwe mfariji na furaha yangu,” Rehema alisema kwa sauti tulivu. Sikuona tena sababu ya kuendelea kukataa.

“Ni kweli nilikuwa na uhusiano na Amanda lakini nimeamua kuukatisha baada ya maongezi yetu leo mchana. Ni kweli nilimfuata chooni lakini lengo langu lilikuwa kumweleza ukweli kuwa siwezi kuendelea kukusaliti maana moyo wangu ulikuwa unanisuta…” nilimwambia Rehema lakini bado sikuiona tashwishwi yoyote usoni kwake, alikuwa ametulia tuli akiniangalia kwa umakini.

“Naomba uniamini mpenzi, ninakwenda Buzwagi kwa ajili ya kushughulikia suala letu na wala si vinginevyo,” nilijitetea huku nikihisi hatia imenikaba kooni. Rehema aliendelea kukaa kimya huku akiniangalia kwa umakini.

Please…” nilisema na bila kujua machozi yakaanza kunidondoka. Hapo Rehema akaonekana kuingiwa na huruma.

It’s okay!” Rehema alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani na taratibu akaanza kurudi katika hali yake ya kawaida ya ucheshi na uchangamfu mkubwa.

“Sasa…” niliamua kubadilisha maongezi lakini nikakatishwa na sauti ya simu yangu ya mkononi iliyoanza kuita kwa fujo.

Niliichukua ile simu na kuangalia kwa makini ili kuona ni nani aliyekuwa akinipigia muda huo na nilichokutana nacho kikaufanya moyo wangu upige kite kwa nguvu, kijasho chembamba kikaanza kunitoka mwilini. Nilishindwa kupokea simu nikabaki kuikodolea macho kana kwamba lilikuwa bomu la kutegeshwa lililobakisha sekunde moja tu lilipuke.

Kwenye kioo cha simu lilionekana jina la Amanda, hii ilimaanisha kuwa Amanda alikuwa anapiga simu muda huo. Nikajiuliza kulikuwa na tatizo gani maana nilimwacha kule chooni akiwa na yule bwana wake aliyekuwa amepoteza fahamu! Sasa kwa nini anipigie simu muda huo wa usiku?

Koo langu lilikauka ghafla kwa hofu huku mapigo ya moyo wangu yakienda mbio isivyo kawaida. Nilimtupia jicho Rehema nikagundua kuwa alikuwa ananitazama kwa jicho la wizi na macho yake hayakuhama kwangu, badala yake yalikuwa makini kufuatilia kwa karibu kila tukio nililokuwa nalifanya.

“Pokea tu simu na uongee na mtu wako, wala usiwe na wasiwasi na mimi,” Rehema aliniambia kwa utulivu pasipo kuonesha chuki yoyote. Kwa kweli badala ya kumshangaa nilianza kumwogopa sana. Nilitamani kuikata ile simu lakini nikasita.

“Helloo!” nilisema kwa sauti tulivu mara baada ya kupokea na kuiweka ile simu kwenye sikio langu. Asalalee! Nusura moyo unipasuke kwa mshtuko mkubwa nilioupata baada ya kuisikia sauti nzito ya kiume.

“Mwanaharamu mkubwa wewe, mpenda wake za watu na ole wako tukutane utanitambua. Kumbe ndiyo mchezo wako huo wa kudandia wanawake wa watu!” yule mwanamume aliongea haraka haraka kwa hasira.

Nilibaki nimeduwaa kwa sekunde kadhaa nisijue nini cha kusema. Nilitamani kumtukana lakini nilijizuia baada ya kugundua kuwa Rehema alikuwa ameketi pembeni yangu akisikiliza kila neno lililotamkwa na yule mwanamume, nikajikuta nikiachia tabasamu huku nikimeza mate ya uchungu.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

68

“Mbona sikuelewi! Wewe ni nani na unasemaje? Nadhani utakuwa umekosea namba…” nilisema kwa utulivu.

“Unanijua fika na wala sijakosea namba, we juha! Wewe si ndo unaitwa Jason? Jason Sizya…”

“Ndiyo, ni mimi,” nilimjibu yule mwanamume huku mapigo ya moyo wangu yakinienda kwa kasi sana.

“Wewe si ndiyo nimekufumania na mchumba wangu kule chooni Migombani Club? Kwa nini unamfuata na kumtishia maisha wakati ameshakwambia kwamba hakutaki? Unachokitafuta hasa ni nini?” yule mwanamume aliendelea kufoka kwa hasira.

“Ndivyo alivyokwambia kuwa namfuata na kumtishia maisha?” nilimuuliza yule mwanamume huku nikihisi joto kali sana likizidi kutambaa mwilini mwangu kutokana na hasira iliyoanza kuibuka. Rehema alitingisha kichwa chake kwa masikitiko kisha akainuka na kuelekea chumbani akiniacha peke yangu pale sebuleni.

“Sasa sikiliza wewe mjinga…” yule mwanamume aliongea kwa hasira na jeuri.

Uvumilivu ulianza kunishinda kutokana na jeuri yake iliyosababishwa na vihela vyake, nilihamaki baada ya kuona akizidi kunitukana wakati mimi nilikuwa nikimjibu kistaarabu. Lakini nikajionya kuwa nisimjibu vibaya na niendelea kumvumilia ili nisikie alichotaka kusema.

“Nakwambia hivi, huyu ni mke wangu mtarajiwa na mimi ndiyo mumewe mtarajiwa. Mimi ndiye ninayemgharamia kwa kila kitu. Unamwona anapendeza ni kwa sababu yangu, kwa hiyo achana kabisa na mke wangu vinginevyo nitakufanyia kitu kibaya sana ambacho hutakuja kukisahau katika maisha yako,” yule mwanamume alifoka.

“Naomba tusianze kutishana!” nilisema kwa sauti tulivu ingawa nilitamani kumpa makavu lakini nikajizuia kwa sababu niliamini kuwa Rehema alikuwa amebana sehemu ananisikiliza.

“Sikiliza we mjinga, sikutishi ila nakwambia ukweli, yaani kukwambia uachane na mke wangu unataka kuniletea kibesi! Naona bado hujanielewa, sasa Amanda huyu hapa hebu ongea naye akwambie habari zangu,” nilimsikia yule mtu akimpa simu Amanda na kumlazimisha kuongea.

“Hebu ongea na huyu mbwa mwenzako na umweleze ukweli mimi ni nani kwako, pia mkanye akome kuanzia leo kukufuatilia la sivyo nitamfanyia kitu kibaya sana ambacho hatakuja kukisahau maishani kwake,” yule mtu aliongea maneno niliyoyasikia kwa mbali.

Mara nikaisikia sauti tamu na nyororo iliyozoea kuniburudisha kila mara na kunifanya nijione kama niko peponi, sauti ambayo niliamini ni moja ya sauti nzuri kuliko zote duniani, sauti ya Amanda. Alikuwa akilia kilio cha kwikwi.

“Jason, samahani sana. Naomba usiendelee kunifuata kwani sitaki kumuudhi mume wangu,” Amanda aliongea huku akilia kilio cha kwikwi, nikajua yule mwanamume alikuwa amempiga. “Nakuomba sana Jason, usinitafute na wala usinipigie tena simu…” Amanda alisema kwa uchungu, kisha simu ikakatwa.

Moyo wangu ulikuwa umepoteza kabisa utulivu katika kiwango cha hali ya juu na damu ilikuwa inakimbia kwa kasi kwenye mishipa yangu ya damu. Nilishindwa nifanyeje na kubaki nikiikodolea macho ile simu kama vile nilikuwa nimeshika guruneti la kutupa kwa mkono huku akili yangu taratibu ikizama kwenye tafakuri ya kuanza kuwaza kuhusu uhusiano wangu na Amanda. Sikupenda mwisho wake uwe vile.

Niliendelea kuketi pale sebuleni kwa muda mrefu sana huku akili yangu ikishindwa kufanya kazi sawa sawa, kila nilipotaka kuwaza nini nifanye akili yangu ilishindwa kuamua. Baada ya mahangaiko ya muda mrefu nikashusha pumzi ndefu na kuinuka, kisha nikaelekea kule chumbani kwa Rehema.

Nilimkuta Rehema akiwa ameshalala na kujifunika shuka. Taratibu nikaivua suruali yangu na ile fulana na kubakiwa na boksa kisha nikajitupa kitandani na kujiingiza kwenye shuka nikiungana na Rehema. Rehema alifungua macho yake akaniangalia kwa upole pasipo kusema neno. Mwili wangu ulikuwa umeingiwa na ganzi na baridi kali ilikuwa inanitambaa mwilini. Kwa ushawishi wa baridi lile, nilijikuta nikihitaji joto la Rehema zaidi ya shuka lililokuwa juu ya mwili wangu.

Nilimsogelea Rehema, lakini kwa tahadhari, huku nikiupima upepo. Rehema hakujivunga, akanikumbatia na kuanza kunipa joto. Nikaona kuwa ile ilikuwa ndiyo nafasi yangu ya dhahabu ya kusawazisha makosa yangu niliyokuwa nimeyafanya. Nilimvuta upande wangu na kumkumbatia sawa sawa. Rehema alikuwa akitetemeka kwa hisia kali za huba. Muda mfupi baadaye tulikuwa tumemezwa na ulimwengu wa huba.

Tulikuwa kwenye ulimwengu mzito wa huba na dunia ilikuwa kama kisiwa cha raha kwa ajili yetu. Niliyasahau masaibu yote yaliyonikuta nikazama kwenye ulimwengu wa huba, tena katika tendo lile ambalo tulipomaliza ngwe moja tulijiona kama tuliozaliwa upya. Hatukuishiwa na hamu, tukarudia tena bila kukata kiu yetu. Mwisho tulichoka hoi bin taabani, tukalala.

Hata hivyo, baada tu ya kumaliza zile ngwe mbili mawazo yangu juu ya kile kilichotokea kati yangu na Amanda yakaibuka upya. Usiku huo ulikuwa mrefu sana kwangu kuliko kawaida na usingizi ulikuwa adimu. Pamoja na kugaagaa pale kitandani nikiutafuta usingizi lakini sikuweza kuupata. Nilijikuta nikimfikiria sana Amanda, nilijiuliza hivi kweli aliweza kunifanyia ghiliba za kutoka na mwanamume mwingine kwa kipindi chote hicho, pasipo kujua?

Hata hivyo, kwa uzuri aliojaaliwa Amanda na umbo lake la kuvutia isingekuwa ajabu kufuatwa na wanaume au kujihusisha katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani mwenye fedha lakini sikutegemea kama hali ingekuwa kama ilivyotokea siku hiyo.

Niliiangalia saa yangu nikagundua kuwa ilikuwa imeshatimia saa 10:15 alfajiri, na wakati huo usingizi kwangu ulikuwa sawa na kisiwa cha mbali ambacho nisingeweza kukifikia kwa urahisi. Rehema alikuwa ametopea usingizini huku kichwa chake akiwa amekilaza kifuani kwangu. Mguu wake mmoja ulikuwa katikati ya mapaja yangu huku mkono wake mmoja ameuzungusha shingoni kwangu na kwa mbali niliweza kusikia sauti hafifu ya mkoromo wake wa uchovu.

Penzi zito la Rehema lilikuwa limeamsha kitu fulani moyoni mwangu na kunifanya nianze kujilaumu kwa usaliti wote niliokuwa nikimfanyia. Kwa mara ya kwanza nilihisi moyo wangu ukiniuma sana kwa matendo yangu machafu yaliyosababisha kuumiza moyo wa Rehema. Nilihisi machozi yalikuwa yakinitoka na kuulowesha mto niliolalia.

Sikujua kuwa uchungu ulionijaa moyoni ndiyo uliyasukuma machozi yangu yaliyokuja kutanda kwenye goroli za macho kabla ya kutiririka kama maji ya Mto Ruvu. Nilimtazama Rehema aliyekuwa ametopea kwenye usingizi huku akipumua kwa mbali. Sikujua nifanye nini ili nisimkwaze tena. Ukweli sikuwa na neno mujarabu la kusema.

Nilihisi kuwa akili yangu ilikuwa bado haifanyi kazi sawa sawa, ilikwisha vurugwa na taarifa niliyoipata toka kwa Amanda. Moyo wangu uliwaka moto, kichwa changu kiliwaka moto, na tumbo langu liliwaka moto, na hapo likawa balaa juu ya balaa mwilini mwangu! Ukweli hakuna binadamu mwenye moyo wa chuma, wote tuna mioyo ya nyama iliyoko upande wa kushoto vifuani mwetu.

Nilianza kujiuliza, vipi kuhusu ile safari niliyoipanga ya kurudi Buzwagi ili nikamkabili Amanda ingekuwaje? Je, nilipaswa kuondoka au niahirishe? Na hata ningeondoka ningekwenda kufanya nini wakati niliamini kabisa kuwa yule mwanamume asingeweza kumruhusu Amanda kuondoka, na kama angelazimisha huenda angempa kipigo ambacho asingeweza kukisahau maishani kwake.

Kwa kuisikia sauti ya yule mwanamume kwenye simu niliamini kuwa alikuwa ana jeuri ya fedha, alijivunia fedha zake ndiyo maana alikuwa ananifokea kama mtoto mdogo. Nikapanga niahirishe safari yangu na nibaki Ushirombo na Rehema wangu ambaye ndiye alikuwa mfariji wangu pekee, mwanamke pekee niliyeamini kuwa alinipenda kwa dhati na kunivumilia kwa kila hali. Lakini kulikuwa na tatizo, ningemwambiaje Rehema kuwa nimeahirisha safari? Angeniuliza kwa nini nimebadili mawazo na ningekosa jibu!

Niliazimia kupanga maneno mazuri ya kumwambia ili aniamini kuwa sijaahirisha safari kwa sababu ya sakata langu na Amanda. Lakini bado akili yangu haikuweza kufanya kazi sawa sawa…

* * *

Endelea kufuatilia...
 
Muendelezo ungefanyika hapa na haka kamvua walah skukuu ingekua njema mno mkuu@Bishop Hiluka
 
narudi buzwagi.jpeg

69

Mgomo Baridi.


Saa 1:20 asubuhi…

“Jason, amka twende kanisani,” sauti laini ya kubembeleza ya Rehema ilinizindua toka usingizini.

“Mmh!” niliguna huku nikijigeuza upande wa pili na kulivuta zaidi shuka.

“Jiandae twende kanisani, tumechelewa,” Rehema aliongea kwa sauti laini ya kulalamika.

Nilishtuka na kumwangalia Rehema kwa umakini kisha nikayazungusha macho yangu mle chumbani huku nikishangaa, sikuweza kufahamu ni wakati gani lepe hafifu la usingizi lilikuwa limefanikiwa kuziteka fikra zangu pale kitandani wakati nilipokuwa naendelea kuwaza hili na lile juu ya safari yangu ile ya kurudi Buzwagi.

“Amka ukaoge, tumechelewa bwana,” Rehema alizidi kuniambia kwa sauti ya kubembeleza.

Nilimtazama Rehema aliyekuwa amesimama mbele yangu akiwa amevaa gauni zuri, alikuwa amependeza zaidi katika muonekano wa vazi la kitenge cha wax lililoshonwa kwa ustadi mkubwa na kuushika vema mwili wake. Alikuwa amesimama akiniangalia kwa makini.

Kwa sekunde kadhaa macho yangu yalitua kwenye uso wake mtulivu uliopambwa na tabasamu laini kisha yakaanza kutambaa taratibu kwenye mwili wake mzuri na kufika kwenye kifua chake kilichobeba matiti mazuri mfano wa embe dodo yaliyoachiana nafasi ya kutosha. Matiti yale yalisimama kana kwamba yalikuwa yananidhihaki.

Macho hayakuridhika, yakaendelea kutambaa hadi kwenye tumbo lake dogo la ubapa ambalo lilionesha wazi kuwa halijawahi kabisa kubeba kiumbe chochote, kisha macho yakaenda kutuwama kwa muda katika eneo la katikati lililorembwa, na hapo yakakutana kwenye kiuno kilichobonyea na kuacha fursa ya nyonga kuchanua zilivyotaka. Nyonga zilizofinyangwa barabara. Kisha nikayahamisha macho toka kwenye nyonga hadi katikati ya mapaja yake.

Hamu ya mapenzi ikanijaa juu ya Rehema. Macho yangu yalikataa kabisa kuamini taswira ya mrembo iliyokuwa imejengeka vizuri machoni mwangu ikiwa imepambwa na tabasamu jepesi la matumaini nililoliona usoni kwake alikuwa ni Rehema. Yaani pamoja na makwazo yote niliyomfanyia bado aliweza kusimama mbele yangu na wakati wote huo alikuwa akinitazama kwa tabasamu huku akiniacha niustaajabie uzuri wake kwa mara nyingine tena. Yeye mwenyewe alijifahamu kuwa ni mzuri sana.

“Unatazama nini?” Rehema aliniuliza kwa sauti tulivu.

“Nilikuwa nauajabia ufundi wa Mungu, hakika wewe ni mzuri,” nilijikuta naropoka pasipo kujua. Rehema akaachia tabasamu.

“Amka basi ukaoge, tunazidi kuchelewa. Isitoshe leo una safari,” Rehema alinikumbusha tena.

Nilishusha pumzi huku nikipiga miayo mfululizo kutokana na uchovu wa kukosa usingizi, nilitamani nimwambie sikuwa tayari kwenda kanisani lakini nikasita. Kwa kweli sikukumbuka mara ya mwisho kwenda kanisani ilikuwa lini!

Niliinuka na kuketi pale kitandani, nikataka kumwambia ukweli kuwa hata ile safari ya Kahama niliamua kuiahirisha kwa sababu kilichokuwa kinanipeleka huko kimeshavurugika, lakini nikasita, kwa kuwa nilikuwa sijapanga maneno mazuri ya kumweleza ili kumridhisha. Kwa uvivu nikaamka na kuelekea bafuni kuoga.

Nilipoufikia mlango wa bafu niligeuka kumwangalia Rehema kwa macho yaliyojaa ubembe wa huba. Nilihisi moyo wangu ukinienda mbio kama saa mbovu! Rehema alikuwa mrembo kabisa, alikuwa mrembo kuliko neno lenyewe.

Kwa namna alivyokuwa amesimama akiniangalia kwa tabasamu la upole nilijikuta nikisitasita kuingia bafuni, nilionekana dhahiri kutaka kuungama dhambi zangu kwake na kumweleza ukweli kuwa siku zote nilikuwa namwongopea, na kwamba baada ya tukio la usiku niliazimia kuachana na mambo yote machafu ili kutimiza agano letu la kuoana. Pia nilitaka kumwambia ukweli wa safari yangu ya kurudi Buzwagi na kwamba niliamua kuahirisha. Hata hivyo isingekuwa rahisi kujieleza. Kwa hakika nilikuwa na wakati mgumu kwel ikweli.

“Mwenzetu vipi? Mbona umeganda hapo mlangoni?” Rehema aliniuliza baada ya kuona sikuwa na dalili za kutaka kuingia bafuni.

“Naingia mama, kwani kuna ubaya gani kumwangalia mpenzi wangu?” nilimwambia huku nikitabasamu.

“Hakuna ubaya wowote, lakini muda hauturuhusu. Jinsi unavyojivuta vuta ndivyo tunavyozidi kuchelewa, kumbuka pia utachelewa mabasi halafu unilaumu,” Rehema alisema na kupiga hatua taratibu, akatoka mle chumbani.

Niliingia bafuni na dakika chache baadaye nilitoka nikiwa nimechangamka kweli kweli. Kweli maji ni dawa nzuri ya uchovu. Sasa nilijisikia safi kabisa.

Dakika kumi na tano baadaye nilikuwa nimeshajiandaa na kutoka, nilikuwa nimevaa suti nzuri ya kijivu na tai ya buluu. Nikamkuta Rehema ameketi sebuleni akinisubiri, mkononi alikuwa ameshika Biblia na kitabu cha Tumwabudu Mungu.

Tukatoka na kuelekea kanisani, kanisa ambalo halikuwa mbali sana kutoka pale nyumbani kwa Rehema. Tukiwa njiani Rehema alinieleza kuhusu wasiwasi wake.

“Jason, hata sijui kwa nini nina hisia mbaya sana leo tangu kulipopambazuka? Nahisi kama kuna jambo baya litatokea!” Rehema aliniambia huku akinitazama kwa wasiwasi.

“Litatokea wapi na kwa nani?” nilimuuliza huku nikimkazia macho.

“Hata sijui, lakini hisia zangu zinaniambia hivyo, kwamba kuna jambo baya linaweza kutokea leo, hata sijui nifanyeje!” Rehema alisema kwa huzuni huku akilengwa lengwa na machozi.

“Wasiwasi wako tu, wala usizipe nafasi hisia za aina hiyo maana hiyo ni mbinu za shetani kuwatia hofu watu. Hakuna chochote kibaya kitakachotokea,” nilimtia moyo Rehema huku nikimshika mkono kwa mahaba. Kama mtu angenisikia angedhani nilikuwa mtu wa imani au pengine mtumishi wa Mungu, kumbe sivyo!

Rehema alitaka kuongea lakini akasita na kushusha pumzi za ndani kwa ndani, muda huo tulikuwa tumetokea mbele ya jengo la kanisa. Lilikuwa Kanisa la Kiluteri na nje ya kanisa lile kulikuwa na magari machache ambayo nilipoyachunguza vizuri nikagundua kuwa moja lilikuwa mali ya kanisa lile kutokana na maelezo yaliyokuwa yameandikwa ubavuni, na yalikuwa yameegeshwa katika sehemu maalumu ya kuegesha magari mbele ya kanisa.

Ilikuwa imetuchukua dakika kumi na mbili kufika hapo kanisani, tukakuta watu tayari ibada ikiendelea na watu wamejaa ndani, tukapokewa na mama moja wa makamo aliyevalia joho fupi jeupe lililokuwa na alama ya msalaba mgongoni na kifuani, akatupokea huku akionesha tabasamu usoni mwake.

Ukubwa wa lile kanisa ungeweza kumeza watu mia mbili na hamsini hadi mia tatu bila usumbufu wowote. Nilipochunguza upande wa kushoto wa lile kanisa nikaona kuwa lilikuwa limepakana na ofisi za watumishi wa kanisa pamoja na jengo la watoto maarufu kama Sunday School. Upande wa kulia wa kanisa lile lilipakana na nyumba nzuri ya mchungaji. Sikuweza kuona chochote upande wa nyuma ingawa mandhari yake yalikuwa yamepambwa na miti ya kupandwa.

“Karibuni wapendwa katika Bwana,” sauti yule mama mhudumu wa kanisa ilinizindua, nikamtazama na kumwona akiachia tabasamu.

“Ahsante mama,” Rehema alijibu huku naye akiachia tabasamu, wakati wote huo mimi nilikuwa kimya sizungumzi chochote.

“Nafasi huku nyuma zimejaa twendeni nikawaoneshe nafasi huko mbele,” yule mama mhudumu wa kanisa alitwambia huku akituongoza kuelekea sehemu ya mbele.

Tukaanza kukatiza katikati ya kanisa huku pembeni kukiwa na viti vingi vilivyojaa watu. Hatua zangu madhubuti wakati tukikatiza katikati ya waumini walioketi kwa utulivu mle kanisani zikatengeneza kishindo hafifu na hapo nyuso za waumini zikageuka na kututazama, na namna walivyokuwa wakitutazama nikawa najihisi aibu, nilianza kujihisi kama shetani aliyeingia kanisani kutubu dhambi zake.

Kadri tulivyozidi kwenda mbele ndivyo tulivyozidi kuvuta macho ya watu kutuangalia, sikupenda kuvuta macho ya watu wala kuonekana kivutio hivyo mara moja nikapunguza mwendo nikitembea taratibu huku nikiyatembeza macho yangu huku na kule kuzitazama nyuso za watu wa mle ndani na vile vile nikitafuta sehemu nzuri ya kukaa maana sikupenda kukaa mbele karibu na madhabahu.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

70

Hata hivyo, eneo lote lilikuwa limejaa waumini na hivyo tukajikuta tunaikaribia madhabahu ya kanisa. Yule mama mhudumu wa kanisa akatuonesha viti vilivyokuwa mbele kabisa karibu na madhabau, tukaketi huku Rehema akifumba macho yake na kuanza kuomba kimya kimya.

Wakati nikiketi niliwaona baadhi ya watu wakinitazama kwa umakini kidogo kisha wakayarudisha macho yao kutazama mbele kwa mchungaji aliyekuwa akitoa matangazo mafupi, ingawa wapo baadhi ya watu waliendelea kunitazama bila haya yoyote. Sikukumbuka mara ya mwisho kuingia kanisani ilikuwa lini ingawa tathmini yangu ilinionesha kuwa huenda katika kanisa lile kulikuwa na ibada moja tu kutokana na wingi wa waumini.

Niliyazungusha macho yangu haraka haraka kuyaangalia mandhari ya kanisa, nikagundua kuwa lilikuwa kanisa lenye paa refu na imara. Ukutani kulikuwa na madirisha makubwa marefu ya vioo. Kila baada ya madirisha mawili kulikuwa na nguzo kubwa ndefu zilizotoka chini hadi juu kushikilia paa la kanisa lile.

Nilipotupa macho yangu madhabahuni nikamwona mchungaji aliyevalia kanzu ndefu nyeupe na mabegani kwake kulikuwa na kitambaa kipana cha kijani chenye michoro ya misalaba midogo midogo kilichokuwa kinaizunguka shingo yake na kuning’inia mbele hadi eneo la magoti. Pembeni ya mchungaji alisimama mwanamama mmoja ambaye pia alikuwa amevaa kanzu ndefu nyeupe bila kitambaa cha kuning’inia.

Kisha macho yangu yakatulia kutazama mishumaa miwili mikubwa iliyowekwa kwenye vikombe maalumu vya shaba vilivyokuwa juu ya meza kubwa na pana mbele ya madhabahu. Nilipochunguza vizuri mle ndani ya kanisa nikagundua kuwa idadi ya wanawake ilikuwa kubwa sana ukilinganisha na idadi ya wanaume.

Mchungaji akamaliza kutoa matangazo na kisha ukafika wakati wa mahubiri na mchungaji akamkaribisha yule mwanamama ambaye alisimama katika eneo ambalo wahubiri husimama wakihubiri. Muda huo kikundi cha sifa walikuwa wanaimba wimbo wa kusifu na baada ya kumaliza wimbo huo tukaanza kuomba, kisha yule mhubiri akaanza kuhubiri mada iliyoufanya moyo wangu kukosa raha kabisa ya kukaa ndani ya kanisa huku mara kwa mara macho yangu yaligongana na mhubiri huyo.

“Wapendwa katika Bwana, andiko katika waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho, sura ya 6 na mstari wa 18 linasema: Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe…” alianza kusema yule mhubiri.

“Wapendwa, uasherati na uzinzi ni dhambi za mwili ambazo zinamchafua sana mtu na kukataliwa na MUNGU, kiroho mtu huyu asipotubu kikamilifu dhambi hizi zinachafua mwili na kumfanya Roho wa Mungu amkimbie mtu huyo. Na dhambi hizi zinaua kiroho na kimwili… Mwisho wa maisha ya mwasherati na mzinzi ni mauti. Halelluya…” alisema yule mhubiri.

“Ameen!” Watu wote akiwemo Rehema waliitikia ila mimi nilikaa kimya huku nikijaribu kuyatafakari yale maneno.

“Uzinzi huharibu ndoa, hubaribu familia, na huharibu maisha ya mtu, lakini pia huharibu roho kwa njia inayosababisha kifo cha kimwili na kiroho. Mungu anatamani kwamba tuwe bila hatia na tutumie miili yetu kama zana za matumizi na utukufu wake. Niseme ukweli, na Roho wa Mungu ananishuhudia hapa; kuna watu wapo hapa wana mapepo ya ngono. Hawapendi kupitwa na kila mwanamke mzuri anayekatiza mbele yao…” yule mhubiri alinyamaza kidogo na kumeza mate huku akinitupia jicho, jambo lililoanza kunitia wasiwasi.

“Utakuta mtu ana mke mzuri tu tena aliyetulia lakini yeye anahangaika na makahaba mtaani hadi unajiuliza huyu anakosa nini kwa mkewe? Wengine wanaishi katika uchumba kwa miaka na miaka na hawataki kufunga ndoa. Hilo ni pepo ndugu yangu na leo tutalitoa kwa uwezo wa Jina la Yesu Kristo, halelluya!”

“Ameen!” waumini waliitikia kwa nguvu zaidi. Rehema akanitupia jicho la wizi, jicho lililobeba ujumbe mkubwa sana juu yangu.

“Hizo ni roho chafu zilizomo ndani ya mtu ambazo huwafuatilia sana vijana wa Mungu, ambao Mungu anahitaji kuwatumia kama watumishi wake, halelluya!” yule mhubiri alizungumza kwa sauti kali na kuwafanya watu kishangilia kwa nguvu zaidi, hasa wanawake.

“Ameen!” waumini wakaitikia tena kwa nguvu, isipokuwa mimi.

“Nisikilize ndugu, huu ndiyo wakati wako wa kutubu. Acha uasherati, unajidanganya eti unakula ujana! Nani kakwambia ujana unaliwa? Hakuna mtu aliyewahi kupewa taji kwa sababu ya uasherati… huu ndiyo muda wako wa kutubu maana maisha haya ni mafupi sana. Tubu mpendwa. Kama vile mtu mwingine yeyote, wazinzi na makahaba pia wanayo nafasi ya kupokea wokovu na uzima wa milele kutoka kwa Mungu, wanayo nafasi ya kutakaswa kwa uovu wao wote na kupewa maisha mapya! Hujachelewa, tubu leo na ugeuke kutoka kwa maisha yako ya dhambi na kumgeukia Mungu aliye hai, ambaye neema yake na huruma hazina kipimo,” yule mhubiri alisema kwa sauti kali, na mara kwa mara nilihisi kama alikuwa amenikazia macho kana kwamba alikuwa anaisoma roho yangu kupitia katika macho yangu.

Nikahisi alikuwa ananisema mimi, mapigo ya moyo wangu yakaanza kwenda kasi sana na jasho likaanza kunitoka japo nilipokuwa nimekaa juu yake kulikuwa na feni kubwa lililokuwa linazunguka kwa kasi. Rehema alinitupia jicho kwa umakini. Sikuona tena kama nilistahili kuendelea kukaa mle kanisani na hivyo nikawa natafuta namna ya kutoka kanisani humo.

Mara simu yangu ikaanza kuita. Ilinishtua sana maana sikuwa nimeizima au kuiondoa sauti. Mlio wa simu yangu ukawafanya watu waliokuwa karibu yangu kunitazama kwa mshangao huku wengine wakionekana kuchukizwa kwani nilikuwa wanaondolea umakini katika kusikiliza mahubiri.

Hata hivyo, ikawa nafuu kubwa sana kwangu kwani niliiona hiyo ndiyo fursa ya kutoka mle kanisani. Nikanyanyuka haraka huku nikiiziba spika ili kupunguza ukubwa wa sauti na wakati huo nikipiga hatua za haraka haraka kutoka nje ya kanisa, kwa mwendo niliokuwa nao nikafanikiwa kutoka nje haraka huku nikimsikia yule mhubiri kupitia vipaza sauti mchungaji akizungumza, “Jamani wapendwa, tukumbukeni kuzima simu zetu tunapokuwa ndani ya nyumba ya Mungu, au tuziondoe sauti ili tusije tukawakwaza wengine…”

Sikuwa na haja ya kusikiliza angezungumza nini baadaye, nikapokea ile simu ambayo sikujua ilikuwa ya nani maana namba yake ilikuwa ngeni. Baadaye nikagundua kuwa mpigaji alikuwa amekosea namba. Hata hivyo sikurudi tena kanisani, nikaelekea kwenye kioski kimoja kilichokuwa jirani na kanisa na kuagiza soda, nikawa nakunywa taratibu huku nikisoma meseji mbalimbali kwenye makundi ya WhatsApp.

Kwa mbali nikawa namsikia yule mhubiri akiendele kuongea mambo mengi ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa yananilenga moja kwa moja. Baada ya saa moja na nusu ndiyo nikaanza kuwaona watu wakitoka kanisani, nikayakaza macho yangu kumwangalia Rehema na nilipomwona nikapunga mkono wangu juu kumwonesha niliposimama. Rehema alikuja hadi pale kwenye kioski huku akiniangalia kwa namna ambayo sikuweza kuelewa tafsiri yake.

* * *

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

71

Saa 5:20 asubuhi…

Tulikuwa tumemaliza kupata kifungua kinywa na Rehema aliondoa vyombo na kwenda kuvisuuza jikoni. Aliporejea nikamweleza kuwa nilikuwa tayari kwa safari. Rehema akaniomba nifunge macho ili tufanye maombi kabla sijaondoka, akanishika mikono yangu na kuanza kuomba akinikabidhi mikononi mwa Mungu na kunifunika kwa damu ya Yesu ili nisipatwe na jambo baya njiani hadi nifike safari yangu.

Nilishangaa sana maana siku hiyo Rehema alionekana mwenye huzuni. Nikakumbuka kuwa aliniambia alikuwa na hisia kuwa huenda jambo baya lingetokea. Alipomaliza maombi akachukuwa begi langu dogo la mgongoni na hapo tukatoka nje ya nyumba ile na kufunga mlango. Nilishaazimia kuondoka ili nisije nikamkwaza Rehema baada ya kugundua kuwa sikuwa mkweli kuhusu suala la kwenda kuongea na Eddy.

Muda ule hali ya hewa pale Ushirombo ilikuwa imepoa zaidi, manyunyu hafifu ya mvua yalikuwa yanaanguka kutoka angani kulikotanda wingu jepesi la mvua. Wakati tukiwa pale nje ya nyumba ya Rehema nikashangaa kuiona teksi ikija na kusimama mbele yetu. Kumbe wakati tulipokuwa tunapata mlo pale mezani Rehema tayari alikuwa amewasiliana na dereva wa teksi.

Yule dereva alishusha kioo cha dirisha lake, akatusalimia kwa bashasha huku akitaniana na Rehema. Alikuwa ni yule dereva aliyekuwa ametupeleka Migombani Club siku iliyotangulia. Kwa mwonekano tu alikuwa mtu mzima aliyekadiriwa kuwa na umri usiopungua miaka arobaini na tano. Alikuwa mrefu na mwembamba mwenye sura ya ucheshi na alikuwa amevaa shati la buluu na jaketi jeusi, suruali ya kijivu na raba miguuni.

Niliagana na Rehema, nikafungua mlango wa mbele upande wa abiria na kupanda, lakini kabla ile teksi haijaondoka Rehema akanifuata na kukiingiza kichwa chake ndani ya gari na kunibusu mdomoni huku uso wake ukiwa na huzuni.

“Mbona kama una huzuni, au niahirishe safari?” nilimuuliza Rehema huku nikimwangalia machoni.

“Hapana, ila ninakuomba tu uwe makini huko uendako, hata sijui kwa nini ninapatwa na hisia mbaya!” Rehema alisema kwa huzuni.

Nilimtazama Rehema kwa umakini kisha nikashusha pumzi za ndani kwa ndani. hali aliyokuwa nayo Rehema ikaanza kunitia wasiwasi lakini nikajipa moyo kuwa hizo zilikuwa hisia tu, wala hakuna jambo baya ambalo lingetokea kati yetu.

“Usijali, nitakuwa makini,” nilisema na kuachia tabasamu, kisha nikaongeza, “Ninakupenda sana mpenzi wangu.”

“Ninakupenda pia, kuwa makini,” Rehema alisema na kushusha pumzi ndefu kama aliyetoka kukimbia mbio ndefu.

“Usijali,” nilisema huku nikiusogeza uso wake karibu yangu na kumpiga busu mdomoni, kisha nikairuhusu ile teksi kuondoka.

Tukaanza kuondoka taratibu huku yule dereva wa teksi akanisemesha kwa lugha ya Kisumbwa, nikababaika kidogo katika kujibu maana japo nilielewa alichokizungumza lakini tatizo lilikuwa katika kukiongea Kisumbwa. Niliweza zaidi kuongea Kinyamwezi. Yule dereva alipoona nikibabaika kidogo aliamua kubadili lugha na kunisemesha kwa Kiswahili.

“Kwema lakini?” yule dereva wa teksi aliniuliza huku akinitupia jicho.

“Kwema, kaka. Sijui wewe?” nilimjibu huku nikijiweka sawa.

“Mimi sijambo. Kwani wewe si mtu wa huku Ushirombo?” yule dereva wa teksi aliniuliza kwa mshangao.

“Mimi si Msumbwa, mimi ni Mnyamwezi wa Tabora,” niliongea kwa utulivu huku nikimtazama kwa umakini.

“Oh! Kumbe wewe ni Mnyamwezi wa Tabora? Hata hivyo Kisumbwa kimetokana na Kinyamwezi. Karibu sana Ushirombo. Mimi naitwa Maduki, ni Msumbwa orijino na al-watan hapa Ushirombo. Hakuna asiyenifahamu hata ukimuuliza mtoto mdogo atakuleta hadi nyumbani kwangu,” alisema yule dereva wa teksi kwa tambo nyingi huku akigeuza shingo yake kuniangalia na kuachia kicheko hafifu. Sikusema kitu bali niliachia tabasamu.

“Nimezoeana kiasi na bosi Rehema ila sikuwahi kumwona shemeji yangu. Kumbe wewe ndiyo shemeji yetu!” yule dereva wa teksi alisema katika namna ya kuendeleza maongezi.

Yeah, ila bado sijamuoa rasmi, huenda tukafunga ndoa hivi karibuni,” nilimwambia kwa utulivu.

Maelezo yangu yakamfanya yule dereva ageuze shingo yake kuniangalia usoni kwa umakini.

“Mmeendana kweli kweli na sikushangaa jana nilipokuona. Una bahati sana kumpata mwanamke kama Rehema, mwanamke ametulia sana na kila mwanaume hapa Ushirombo anatamani kuwa naye lakini ndo hivyo tena!” yule dereva alisema huku akiangua tena kicheko hafifu.

“Kwa hiyo, kwa sasa unaishi wapi?” yule dereva aliniuliza baada ya kile kicheko.

“Naishi Kahama,” nilimjibu kwa utulivu.

“Ooh! Nilisahau kama Rehema aliwahi kuniambia kuwa mchumba wake anakaa Kahama! Unafanya kazi katika mgodi wa Buzwagi, siyo?” yule dereva aliniuliza.

“Ndiyo, nipo Buzwagi,” nilimjibu yule dereva.

Nikamwona akiachia tabasamu. Alionekana kuwa mcheshi sana na alijua kutengeneza mazingira yaliyomfanya abiria wake kuwa rafiki yake wa karibu.

Mwendo mfupi baadaye tukawa tumefika mbele ya eneo la stendi ya mabasi. Bila kupoteza muda nikachukua waleti yangu kutoka mfukoni na kutoa noti moja ya shilingi elfu tano kumpa yule dereva lakini akatingisha kichwa chake taratibu.

“Rehema alishalipia kila kitu,” yule dereva wa teksi aliniambia.

“Hakuna kilichoharibika, chukua tu itakusaidia kwenye mambo yako, ila usimwambie Rehema kama nimekupa fedha,” nilimwambia yule dereva kumtoa wasiwasi.

Yule dereva alinitazama kwa umakini huku uso wake ukitengeneza tabasamu la kirafiki na wakati huo huo akiichukua ile noti na kuibusu kisha akaitia kwenye pochi yake.

“Nashukuru sana, bosi wangu. Nakutakia safari njema na uwasalimie sana huko Buzwagi,” yule dereva aliniambia huku akinyoosha mkono wake kunipa. Sura yake ilipambwa na tabasamu.

“Ahsante, Mungu akipenda tutaonana siku chache zijazo,” nilimwambia huku nikishuka toka ndani ya ile teksi kisha aliiondoa teksi yake taratibu huku akinipungia mkono, tabasamu lake la kibiashara lilizidi kuchanua usoni kwake.

Niligeuka kuitazama ile teksi namna ilivyokuwa ikitokomea barabarani, jua lilikuwa limeanza kuingia kwenye mawingu na hali ya hewa kwa wakati ule ilikuwa ya baridi. Pilika pilika za watu zilikuwa zimeshamiri nyakati hizo za asubuhi na hivyo kuufanya mji wa Ushirombo kuchangamka kiasi.

Kulikuwa na wachuuzi kadhaa wa biashara ndogo ndogo. Niliwaona wapiga debe wawili watatu wa eneo lile la stendi ya mabasi walionipokea kwa bashasha zote, hata hivyo, hali niliyoikuta katika stendi ile ilinitia wasiwasi kidogo.

Nilishuhudia abiria wengi waliokuwa wamezagaa katika eneo la stendi ile huku mizigo ikiwa imejazana katika vibanda vya ofisi za usafirishaji kwa namna ya kuashiria kuwa huduma za usafiri zilikuwa zimesitishwa kwa muda, ingawaje wapiga debe wa eneo lile la stendi walikuwa wakiendelea kupiga debe kuwaambia abiria kama mimi tuliokuwa tukiendelea kufika eneo lile kuwa tusiwe na hofu kwani tutapata tu usafiri.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

72

Hatimaye nikaamua kuwauliza abiria wenzangu niliowakuta katika eneo lile la stendi kuhusu kilichokuwa kikiendelea pale, na baada ya kudadisi nikagundua kuwa safari za mabasi, si Ushirombo peke yake bali nchi nzima, zilikuwa zimesitishwa kwa muda usiojulikana kutokana na mgomo wa madereva wa mabasi kwa nchi nzima.

Abiria mmoja mtu mzima alinieleza kwamba madereva wote wa mabasi nchi nzima walikuwa wanasubiri tamko kutoka kwa viongozi wa chama cha madereva ambao walikuwa kwenye mazungumzo na serikali yaliyokuwa yanaendelea muda ule jijini Dar es Salaam, na baada ya kuafikiana lingetolewa tamko ndipo safari zingeanza tena kama kawaida.

Kwa kweli hali ile ilinifanya nitake kurudi nyumbani kwa Rehema kwa kuwa nilikuwa nimepata sababu ya kuahirisha safari. Nilisimama pale nikijishauri nini cha kufanya na hatimaye nilijikuta nikiwa katika mvutano wa ndani kwa ndani, sauti moja ikinitaka nirejee nyumbani kwa Rehema na sauti nyingine ikipinga kabisa wazo la kurejea huko.

Nilivuta pumzi ndefu za ndani kwa ndani kisha nikazishusha taratibu, nikaona busara ilikuwa ni kutembeatembea kidogo eneo lile ili kujaribu kutafuta namna yoyote ya kuondoka pale, iwe ni kurudi nyumbani kwa Rehema au kuendelea na safari yangu. Taratibu nikaanza kupiga hatua zangu nikiifuata barabara ile iliyoelekea Kahama kana kwamba nilikuwa nimeamua kwenda kwa miguu.

Nilitembea taratibu, kichwa changu nilikuwa nimekiinamisha na macho yangu yakiangalia chini kana kwamba nilikuwa natafuta kitu muhimu kwenye ardhi. Wakati natembea taratibu nikiwa katikati ya barabara nilikuwa nikigeuza shingo yangu mara kwa mara kutazama nyuma yangu, nikaliona gari dogo aina ya Toyota RAV4 lililokuwa likija kwa mwendo wa kasi.

Nilijikuta napata wazo la kusimama katikati ya barabara na kuanza kupunga juu mikono yangu yote miwili kumtaka dereva asimame. Sauti fulani ndani yangu ilikuwa ikinisisitiza kuendelea kupunga mikono yangu juu nikiwa pale katikati ya barabara.

Dereva wa lile gari hakuonesha dalili zozote za kutaka kusimama, aliwasha taa za mbele za gari lake kuniashiria niondoke katikati ya barabara, lakini nilikaidi na kuendela kusimama palepale huku nikizidi kupunga mikono yangu yote miwili juu kwa nguvu kumtaka dereva wa gari asimame.

Hatimaye yule dereva aliyeonekana kuwa na umri kama wangu alikanyaga breki kwa nguvu na gari lake likasota na kuyumba kwenye ile barabara ya lami huku akijaribu kunikwepa. Kisha lile gari lilisimama huku yule dereva akisonya kwa hasira na kupiga ngumi katikati ya usukani wa gari lake kwa hasira, muda ule lile gari lilikuwa limesimama hatua chache tu mbele yangu.

Dereva wa lile gari alikuwa kijana wa umri wangu mwenye asili ya Kiarabu, japokuwa alikuwa ameketi lakini niliweza kubaini kuwa alikuwa mrefu na mwenye umbo kubwa, alikuwa amevaa kofia aina ya kapelo na miwani myeusi ya jua.

Alishusha kioo cha dirisha na kuniangalia kwa makini huku akionekana kukerwa sana na kitendo changu cha kumlazimisha kusimama wakati hakuwa na mpango wa kusimama. Bila kujali namna alivyokuwa akiniangalia au kuniwazia, nilimsogelea na kusimama kando ya kioo cha dirisha lake huku nikijaribu kutengeneza tabasamu la kirafiki katika kujaribu kumfanya anisikilize na kulipa uzito ombi langu.

Wakati namsogelea yule dereva alibaki kimya akiendelea kuniangalia kwa makini huku akiwa amekunja sura yake kiasi cha kutengeneza matuta madogo madogo usoni kwake. Nilipokaribia pale dirishani kwake nikamshuhudia akiachia tabasamu pana la urafiki.

Hey nigga! Unafanya nini huku Ushirombo?” yule dereva alimaka kwa furaha huku akinitupia swali mara tu niliposimama usawa na dirisha lake.

“Ni wewe Jason au naota?” yule dereva aliongea kwa furaha huku akishusha pumza ndefu bila hata kunipa muda wa kujibu maswali yake.

Nilimtazama kwa makini nikijaribu kukumbuka kama niliwahi kumwona sehemu yoyote, lakini sikuweza kukumbuka, ingawa sura yake haikuwa ngeni kabisa machoni kwangu. Nikajiambia kuwa huenda alikuwa mmoja wa watu niliowahi kukutana nao mgodini Buzwagi. Yule dereva aligundua hilo, akaipandisha juu miwani yake aliyokuwa amevaa na kunikazia macho huku akinitazama kwa makini bila kupepesa macho.

Mara tu alipovua miwani yake nilijikuta nikiruka kwa furaha, nilikuwa nimemtambua vyema. Kumbe alikuwa ni ‘school mate’ wangu kule Mzumbe. Aliitwa Selemani Abeid, na tulikuwa marafiki wakubwa sana, mimi, yeye pamoja na Swedi Mabushi wakati tukisoma darasa moja mimi pale Shule ya Sekondari ya Mzumbe, na baada ya kumaliza tuliendelea kuwasiliana wakati nikiwa Afrika Kusini na yeye alibaki palepale Mzumbe.

Wakati tunasoma Selemani Abeid alikuwa anaishi na wazazi wake eneo la Boma Road, Morogoro. Baba yake, Abeid Rashid alikuwa daktari katika Hospitali ya Mkoa. Yeye alikuwa amejiunga na Chuo Kikuu cha Mzumbe kabla hajaamua kujishughulisha na biashara ya magari. Mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa ni pale nilipokuwa nasafiri kwenda Afrika Kusini.

Sasa alikuwa mbele yangu akiniangalia kwa tabasamu. Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani huku nikimwangalia kwa mshangao. “Dah, ama kweli milima haikutani!”

“Umeona eh!” Selemani aliniambia huku akishusha pumzi.

“Umenenepa sana, ndiyo maana nilikusahau!” nilimwambia Selemani huku nikimtazama kwa makini.

“Hata wewe umenawili sana,” Selemani aliniambia huku akiendelea kuniangalia kwa umakini. “Mbona uko hapa?”

“Nilikuja kumwona mtu fulani, na sasa naelekea Kahama, bahati mbaya nimekwama hapa kwa sababu ya mgomo wa madereva wa mabasi nchi nzima,” nilimwambia Selemani.

“Daah… Pole sana ndugu yangu, bahati mbaya mimi naishia Masumbwe. Lakini kama hutojali, naweza kukusogeza hadi hapo Masumbwe najua ukifika hapo huwezi kukosa namna ya kufika Kahama,” aliniambia Selemani huku akiniashiria nizunguke upande wa pili niingie kwenye gari.

Sikujivunga, nilizunguka upande wa pili wa lile gari nikafungua mlango wa nyuma wa abiria na kupanda ndani ya gari. Ndani ya gari lile kulikuwa na watu wengine watatu, mwanadada mmoja mrembo wa Kiarabu ambaye sikuweza kumtambua, alivaa hijabu iliyomwonesha sura tu na alikuwa ameketi kwenye siti ya mbele kushoto kwa dereva, na kwa mwonekano wa haraka tu ungeweza kubaini kuwa ki umri hakuwa amezidi miaka ishirini na tano.

Kwenye siti mbili za nyuma kulikuwa na kijana mdogo wa kiume ambaye nilipomtazama mara moja tu niliweza kuhisi kuwa alikuwa mtoto wa Selemani kwa kuwa walifanana sana. Alikuwa na umri wa kukadiria wa miaka mitano hivi na alikuwa ameketi kando ya mwanadada mwingine mrembo wa Kiarabu ambaye pia alivaa hijabu iliyomwonesha sura tu, nilipomuona tu nikamtambua mara moja kuwa alikuwa ni dada wa Selemani, aliyeitwa Jamila Abedi.

Jamila alikuwa mdogo kwa Selemani kwa miaka tisa, nilikuwa namwona wakati ule nilipokuwa namsindikiza Selemani nyumbani kwao katika siku za mapumziko ya shule, wakati huo Jamila alikuwa anasoma shule ya msingi. Japo sasa alikuwa na miaka 21 lakini sura yake haikuwa imebadilika na niliweza kumtambua kirahisi hata kama alikuwa amevaa hijabu.

Wakati naingia na kuketi kule nyuma, Jamila alikuwa akinitazama kwa tabasamu la bashasha, akaniamkia kwa bashasha zote huku akionekana kubabaika kidogo na utanashati wangu. Nisisitize tu kuwa nilikuwa miongoni mwa vijana wachache sana waliokuwa na mvuto wa hali ya juu kwa wasichana warembo wa sampuli ile ya Jamila.

Nami niliitikia ile salamu yake kwa bashasha na kumuuliza habari za siku nyingi lakini Jamila alinijibu kwa kifupi huku akionesha kuwa na woga fulani hivi usoni kwake, mara kwa mara alikuwa akimtupia jicho la wizi Selemani, jicho lililokuwa limebeba hofu fulani.

Baada ya kusalimiana na Jamila niligeuza shingo yangu kumtazama yule mwanadada mwingine aliyekuwa ameketi kule mbele kushoto kwa dereva, nikamsalimia pia kwa bashasha ili isionekane kuwa nilikuwa nabagua. Wakati wote huo nikiwasalimia wale wasichana Selemani alikuwa kimya akinitazama kwa makini.

Nilipomaliza salamu Selemani akanitambulisha kwa yule mwanadada aliyekuwa ameketi kwenye ile siti ya abiria ya mbele kushoto kwake kuwa alikuwa ni mke wake, Ada Abdulaziz, na yule mtoto aliyekuwa ameketi kule kwenye siti ya nyuma alikuwa mtoto wao na alikuwa amempa jina la baba yake, Abeid.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

73

Alipomaliza utambulisho ule akaniuliza kama na mimi nilikuwa nina mke na watoto. Swali lile likanifanya nitabasamu kidogo huku nikimtupia jicho la wizi Jamila ambaye wakati wote huo alikuwa anatabasamu tu huku akiviminyaminya vidole vya mikono yake kama mtoto aliyekuwa anadeka.

Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani kisha nikamjibu Selemani kuwa nilikuwa bado sijaoa na wala sikuwa na mchumba. Jamila akaonesha mshangao mkubwa uliochanganyika na furaha na kuniuliza swali kuwa iliwezekanaje kwa mwanaume mzuri kama mimi kusema kuwa nilikuwa sijaoa na sikuwa na mchumba?

Nilimjibu kuwa nilikuwa bado natafuta mwenza wangu kwa kuwa niliamini kuwa mke mwema hupatikana kwa subira na muda ukifika hakuna kitu ambacho kingenizuia kuoa. Nilisema na kuangua kicheko hafifu.

Wakati nilipokuwa nikiongea maneno yale niligundua jambo moja, ilionekana wazi kuwa swali la Jamila halikuwa limemfurahisha kabisa Selemani, kwani aligeuka na kumkata jicho lililoashiria kuchukizwa. Kwa swali lile ilionekana kana kwamba Jamila alikuwa amefanya dhambi fulani kubwa ambayo ilimshangaza hata shetani.

Nilibaki kimya na muda uleule Selemani aliliondoa gari na safari ya kuelekea Masumbwe ikaanza. Kuanzia hapo hakukuwa na stori tena, tulisafiri tukiwa kimya kabisa kwa kitambo kirefu hadi pale nilipoamua kuanzisha maongezi kwa kumuuliza Selemani ni wapi walikokuwa wakitoka.

“Tunatoka Biharamulo kwenye shughuli ya harusi ya mdogo wake waifu, tulienda majuzi na ndoa ilikuwa jana,” Selemani aliniambia.

Okay… na Masumbwe ni kwa nani?” nilimsaili Selemani katika namna ya kutaka kuwachangamsha baada ya kuhisi hali fulani ya ukimya ndani ya lile gari.

“Nyumbani. Unajua baada ya mzee kustaafu aliamua kurudi nyumbani Masumbwe, na mimi baadaye niliamua kuhamishia makazi yangu huku baada ya mzee kufariki dunia,” Selemani alisema na kunifanya nishangae kidogo.

Nikakumbuka kuwa wakati tunasoma alikuwa akitwambia kuwa nyumbani kwao ni Masumbwe.

Ooh, okay! Nilisikia habari za msiba wa mzee. Poleni sana. Bahati mbaya tangu nitoke South Africa hatujakutana,” nilimwambia Selemani. “Kuna siku moja tu, nadhani ilikuwa mwaka juzi, nilikutana na kaka yako Feisal nikiwa katika mishemishe zangu Kahama, akaniambia kuwa ulikuwa Oman,” nikaongeza.

“Ni kweli, huwa naenda huko nakaa miezi kadhaa halafu narudi. Si unajua tena unapokuwa na mke hutakiwi kuwa mbali kipindi kirefu, unaweza kushangaa siku unarudi unakuta mkeo ameolewa…” Selemani alisema kwa mzaha huku akigeuza shingo yake kumtazama mkewe na kutufanya wote tucheke. “Halafu nilisikia kuwa unafanya kazi Buzwagi, sema sijapata muda wa kukutafuta. Imekuwa bahati leo tumekutana.”

Tuliendelea kupiga stori lakini muda wote wa mazungumzo yetu Jamila alikuwa mkimya sana na sasa alikuwa ameegemeza vizuri kichwa chake kwenye siti huku akinitupia jicho la wizi mara kwa mara. Nilivyomchunguza niligundua kuwa alikuwa akitamani sana kuchangia maongezi lakini ni wazi alikuwa akimwogopa sana kaka yake.

Kutokana na hali ile hisia fulani hivi ndani yangu zikaanza kunipata na kunifanya nihisi hali isiyokuwa ya kawaida kukaa karibu na Jamila, ingawa hiyo haikuwa mara yangu ya kwanza kukaa karibu na Jamila, kwani tulipokuwa tunasoma Mzumbe, Selemani aliwahi kuniomba nimwelekeze Jamila hesabu kwa kuwa nilikuwa bingwa wa hesabu darasani.

Na kipindi chote hicho nilikuwa nikimchukulia kama mdogo wetu na yeye aliniona kama kaka yake, sawa na alivyokuwa akimchukulia Selemani, na sikuwahi hata siku moja kufikiria kama ningeweza kuanzisha uhusiano wowote wa kimapenzi na binti yule.

Hivyo nilianza kujiuliza kwa nini Jamila alikuwa akiniangalia kwa jicho la aina ile tena kwa wizi kana kwamba alikuwa ameniona kwa mara ya kwanza! Hata hivyo, sikutaka kumnyima nafasi ile ya kuniangalia, hivyo mara kwa mara nikawa nikizuga kuangalia nje ya gari lile kupitia kioo kisafi cha dirisha.

Niligundua kuwa jicho la Jamila lilipokuwa likiniangalia kwa namna moja au nyingine lilikuwa linazidi kuamsha hisia zangu na kuyaruhusu mawazo mengi kuanza kupitia kichwani kwangu, nilianza kujiuliza maswali mengi pasipo kupata majibu: kwanza kwa nini alishangaa sana na kuonesha furaha pale aliposikia kuwa nilikuwa sijaoa na wala sikuwa na mchumba?

Je, swali lake kuwa iliwezekanaje kwa mwanaume mzuri kama mimi kusema kuwa sijaoa na sina mchumba liliashiria nini kwa mtazamo wake, kwamba sikupaswa kusema vile au ilikuwa ni dhambi kwangu kutokuwa na mke wala mchumba?

Maswali hayo na mengine mengi yalizidi kupita kichwani kwangu, hata hivyo, sikutaka kuyapa sana nafasi maana sikujua Jamila alikuwa anawaza nini juu yangu. Huenda aliniona kama kijana mhuni asiyeweza kuishi na mwanamke au pengine nilikuwa mtu fulani asiye na mbele wala nyuma!

“Vipi maisha ya Masumbwe, unajihusisha na shughuli gani hasa?” nilimuuliza Selemani baada ya kitambo kirefu cha ukimya ndani ya lile gari.

“Biashara tu ndugu yangu, nina miradi kadhaa…” alisema na kusita, mara nikamsikia akiguna. Nilipomtazama kwa makini nikamwona akiwa ameshtuka sana huku akikodoa macho yake kutazama kwenye dashibodi ya gari.

Nami nikayapeleka macho yangu kutazama pale kwenye dashibodi ya lile gari na kuona taa ndogo ya njano ikiwaka na mshale wa mafuta ukienda kombo, na hapo nikajua kuwa mafuta kwenye lile gari yalikuwa yakielekea kuisha.

“Dah, nilisahau kabisa kuongeza mafuta tulipofika pale Ushirombo, naona wakati wowote yatakata. Sijui kama yatafanikiwa kutufikisha pale Kabila ili tujaze mafuta mengine,” Selemani alisema kwa wasiwasi huku akigeuza shingo yake kumtazama mke wake ingawa sauti yake ilikuwa tulivu.

Hata hivyo, aliendelea kuwa makini sana kuudhibiti vizuri usukani wa lile gari kwenye kipande kifupi korofi cha barabara ile iliyopitiwa na magari mengi makubwa yanayoenda nchi za Rwanda, Burundi na Uganda.

“Kwani mafuta yameisha kabisa!” Ada aligutuka na kumtazama Selemani kwa wasiwasi.

“Hayajaisha kabisa, ila kwa sasa tunatembelea mafuta ya akiba,” Selemani alisema huku akiongeza kasi ya gari.

“Naamini Mungu atatusaidia yataweza kutufikisha Kabila,” safari hii Ada aliongea kwa hisia fulani iliyoonesha kukata tamaa. Hata hivyo, Selemani hakutia neno lolote bali alikuwa makini zaidi akiyakaza macho yake barabarani.

Baada ya kitambo kirefu cha safari tukakivuka kile kipande kifupi korofi cha barabara na hapo Selemani alikanyaga pedeli ya mafuta na gari likaongeza mwendo likipita katikati ya msitu, na tulipokwenda mbele zaidi kama kilomita tano hivi tukaanza kukiona kituo cha kujazia mafuta cha Kabila kikiwa mbele yetu upande wa kulia kwetu.

Sasa sikuwa na mashaka kuwa kituo kile cha kujazia mafuta ndiyo kile alichokuwa amekizungumzia Selemani hapo awali. Muda mfupi uliofuata akachepuka na kuingia upande wa kulia na kwenda kuegesha gari kwenye upande wenye pampu ya kujazia mafuta ya petroli chini ya paa kubwa la kituo kile cha Kabila.

Pale kwenye kituo cha kujazia mafuta cha Kabila kulikuwa na magari mawili, gari moja lilikuwa aina ya Noah na jingine lilikuwa ni roli la mafuta lililokuwa limeegeshwa kando ya kile kituo cha kujazia mafuta. Mbali na magari yale mawili hapakuwa na dalili ya gari jingine lolote eneo lile. Kulikuwa na wafanyakazi watatu niliowaona katika eneo lile, kati yao wawili walikuwa wa kike na mmoja wa kiume wakiwa wamevaa sare maalumu za kituo kile cha Kabila.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

74

Selemani aliliegesha gari lake mbele ya msichana mmoja aliyekuwa amesimama kwenye pampu moja na bila kupoteza muda aliinama na kubonyeza kitufe fulani cha kufungua mfuniko wa tenki la mafuta.

Kisha bila kuchelewa alitoa pochi yake mfukoni na kuifungua, akahesabu na kutoa noti tano za shilingi elfu kumi kumi na kufungua mlango wa gari yake, akashuka. Aliposhuka alisimama jirani na yule mfanyakazi wa kike wa kile kituo cha kujazia mafuta na kumpa zile noti.

Zoezi la kujaza mafuta likafanyika kwa muda mfupi tu, kisha muda huohuo nikamwona mkewe Selemani, Ada, akishuka kutoka kwenye gari na kuonekana akinong’ona jambo kwa Selemani. Baada ya kujaziwa mafuta Selemani aliufunga ule mfuniko wa tenki la mafuta kisha yeye na Ada wakachepuka kidogo kwenda kwenye vyoo vya kile kituo cha Kabila, nikahisi kuwa walikwenda kushusha haja ndogo.

Niligeuza shingo yangu kumtazama Jamila ambaye muda wote alikuwa kimya kabisa kainamisha uso wake chini huku aking’ong’ona kucha zake za vidole vya mkono wa kulia, alionekana kuwa mbali sana kimawazo.

Sikutaka kujivunga, nikaona kuwa ule ndiyo ulikuwa wakati mzuri wa kuongea naye ili kujua kilichokuwa kikiendelea kati yake na kaka yake, maana ilionekana kama hakuwa huru mbele ya Selemani. Hivyo nikaamua kuutumia mwanya ule ambao Selemani na Ada walikuwa wamekwenda kujisaidia kumuuliza maswali Jamila.

“Jamila, una tatizo gani?” nilimuuliza Jamila huku nikimtazama kwa makini usoni.

“Hakuna!” Jamila alinijibu huku akiwa haniangalii machoni.

“Hujaniambia, vipi umeolewa?” nilimuuliza Jamila swali ambalo lilimfanya anitupie jicho na kuachia tabasamu dogo huku akiviminyaminya vidole vya mikono yake. Kisha nilimuona akishusha pumzi za ndani kwa ndani na kubaki kimya kwa kitambo kidogo kama aliyekuwa akifikiria au akitunga jibu la kunipa, baada ya hapo akanitazama moja kwa moja machoni huku akiendelea kunionesha tabasamu lake maridhawa.

“Sijaolewa ila familia tayari imeshanitafutia mchumba,” Jamila alisema kwa sauti tulivu huku akitupa macho yake kutazama kule kwenye vyoo vya kile kituo cha kujazia mafuta cha Kabila.

“Umetafutiwa mchumba na familia? Hadi karne hii bado yapo mambo ya kutafutiana wachumba!” niliuliza huku nikionesha kushangazwa sana na maelezo yake.

“Kwa hiyo, mchumba wako yuko wapi?” nilimuuliza Jamila kwa shauku huku nikiendelea kumkazia macho kwa mshangao. Jamila aliminya midomo yake huku akishusha pumzi ndefu.

“Yuko Oman, mimi sijawahi kumwona ila kaka Selemani na Mama wanamfahamu,” Jamila alinijibu huku akionekana kutofurahia maongezi yale na ilionesha wazi kuwa ama alikuwa hampendi huyo mchumba au hakupenda kuulizwa kuhusu mchumba huyo.

“Ni ajabu sana!” nilitamka huku nikishindwa kujizuia kushangaa.

Japokuwa Jamila hakuonesha kuyafurahia maongezi yale lakini nilikuwa na shauku ya kutaka kujua mengi zaidi kutoka kwake, ingawa nilishindwa kuyauliza kwa sababu nilihisi donge fulani hivi lilikuwa likianza kunikaba kooni.

“Kwa hiyo, ndoa lini?” nilimuuliza tena bila kujali kama angenijibu au la.

“Alikuwa ananisubiri nimalize kwanza chuo ndipo mchakato wa harusi uanze,” alisema huku akiinamisha uso wake kutazama chini.

“Kwani bado unasoma?” nilizidi kumuuliza maswali.

“Nimemaliza mwaka huu, nilikuwa nachukua Diploma ya Clinical Medicine,” Jamila alisema huku akiminya midomo yake na kuachia tabasamu laini lililozidi kunichanganya.

Okay! Kumbe wewe ni daktari! Nina uhakika mtafunga ndoa hivi karibuni!” nilimwambia Jamila huku moyoni nikihisi wivu jambo lililoanza kunishangaza. Tangu lini nikaona wivu juu ya Jamila niliyemchukulia kama dada yangu, mdogo wangu!

“Kama Mungu akipenda,” Jamila aliongea kwa unyonge na kushusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani kisha akageuka tena kutazama kule kwenye vyoo vya kile kituo cha kujazia mafuta.

Kitendo cha Jamila kutazama kule kwenye vyoo vya kile kituo cha kujazia mafuta kikanifanya nami kugeuza shingo yangu kutazama upande ule kisha nikamtazama Jamila kwa udadisi zaidi.

“Nina uhakika huyo mwanamume ana bahati sana kokote aliko, kumpata mke mrembo kama wewe, halafu daktari!” nilichombeza kwa utani huku nikiachia kicheko hafifu. Jamila alibaki kimya akiwa anaangalia chini kwa aibu.

“Ingekuwa ni mimi, wala nisingechelewa kabisa, tungefunga ndoa mara tu ulipomaliza chuo,” niliongea kwa utani huku nikiendelea kucheka kicheko hafifu.

Kauli hiyo ilimfanya Jamila anikate jicho ambalo sikuweza kuelewa lilikuwa na maana gani, alitaka kusema neno lakini akasita na kushusha pumzi ndefu kisha akainamisha tena uso wake chini akionekana kuwaza mbali.

Nilimtazama kwa makini nikajikuta napata uhakika kwamba hakuwa akiyafurahia kabisa maongezi yale, sikujua ni kwa nini alionesha hali ile ya kutoyafurahia mazungumzo yale ilhali mwanzoni tulipokuwa tukija nilimwona akitamani sana kuchangia mazungumzo!

Maswali mengi yalianza kuzunguka kichwani kwangu lakini nilifikia uamuzi wa kukaa kimya ili nisije nikamkwaza zaidi. Nilipotupa macho yangu kule kwenye vyoo vya kile kituo cha kujazia mafuta nikawaona Selemani na Ada wakirudi taratibu kwenye gari. Jamila alinitazama kwa makini na kushusha tena pumzi zake ndani kwa ndani, akatoa haraka simu yake kutoka kwenye mkoba wake mdogo na kunipa akiniomba niandikie namba yangu ya simu.

Niliipokea ile simu na kuandika haraka namba yangu kisha nikamrudishia, nikamwona akiipiga ile namba palepale na simu yangu ilipoita aliachia tabasamu na kukata simu. Kisha aliirudisha simu yake kwenye mkoba na kuegemeza kichwa chake kwenye siti kama mwanzo, akafumba macho yake akijifanya kuwa amepitiwa na usingizi.

Niliitazama kwa makini ile namba ya simu ya Jamila iliyoonekana kwenye kioo cha simu yangu na kuihifadhi kwenye sehemu maalumu ya kuhifadhia majina ndani ya simu huku nikishusha pumzi za ndani kwa ndani, kisha nikairudisha simu yangu kwenye mfuko wa suruali.

Selemani na mkewe Ada wakafika na kuingia kwenye gari, wakanitaka radhi kwa kuchelewa kidogo na hapo safari yetu ikaanza tena tukiondoka eneo lile na kuingia barabarani.

Tulikwenda kitambo fulani cha safari nikaanza kuuona mji wa Masumbwe kwa mbali wenye nyumba nyingi. Nyumba hizo baadhi zikiwa ni za kisasa na nyingine kuukuu kama za vijijini na baada ya muda tukaanza kukatisha katikati ya makazi ya watu katika barabara ile. Tuliendelea kukatisha katikati ya yale makazi ya watu katika mji ule mdogo kisha tukaingia eneo ambalo wenyeji walipaita mjini, muda huo ilikuwa tayari imetimia saa nane mchana.

Selemani aliniacha katika stendi ya mabasi ya Masumbwe na kunitakia safari njema endapo ningebahatika kupata usafiri. Nilimshukuru sana Selemani na kuwatakia wote safari njema ya kule walikokuwa wakielekea, pia nilimtaka anifikishie salamu zangu kwa Mama na wanafamilia wengine.

Mara tu nilipokanyaga miguu yangu katika stendi ya mabasi ya Masumbwe nilishtuka kukuta hata pale Masumbwe abiria waliokuwa wanasubiri usafiri wa kuelekea maeneo mbalimbali walikuwa wengi sana na walionekana kukata tamaa.

Nilisimama pale nikiwa sijui nifanye nini, nilianza kuchunguza eneo lile kuona kama kungekuwepo uwezekano wa kutafuta njia mbadala ya kuweza kunifikisha Kahama lakini sikuona chochote zaidi ya bodaboda zilizokuwa zikizunguka eneo lile.

Nilitaka nikodi bodaboda ili inipeleke Kahama lakini haraka sana nikalipinga wazo hilo, kwani niliwahi kushuhudia jamaa zangu watatu kwa nyakati tofauti wakifa kwa ajali ya bodaboda, sababu ikiwa ni kutaka kuwahi waendako. Nikapiga moyo konde nikiamini kuwa ingetokea gari binafsi iliyoelekea Kahama na kutuchukua.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

75

Nilisimama pale kituoni kwa takriban dakika arobaini nikijaribu kubahatisha kama ningeweza kupata usafiri lakini kadiri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo hali ilivyozidi kutananisha.

Nikaamua kuzungukazunguka eneo lile huku matumaini ya kupata usafiri wa kuelekea Kahama yakiwa yameanza kutoweka kabisa, hii ilikuwa ni baada ya wapiga debe kunieleza kuwa viongozi wa madereva walishindwa kuafikiana na serikali kuhusu madai yao katika kikao chao kilichokuwa kikifanyika jijini Dar es Salaam.

Kwa hali hiyo, ilimaanisha kuwa safari zote za nchi nzima kwa kutumia mabasi zingeendelea kusitishwa hadi wafikie mwafaka na serikali kuhusu madai yao. Taarifa zile zilipowafikia abiria pale kituo cha mabasi Masumbwe zikaibua zogo la aina yake, hasa kwa abiria ambao walikuwa wamekata tiketi, walianza kudai warudishiwe nauli zao.

Kwa kweli nilikata tamaa sana hasa kwa kuchukulia kuwa nilikuwa tayari nimepoteza muda wangu mwingi eneo lile, na hasa nilipoanza kuwaza kuwa kutokana na hali ile nisingeweza tena kupata nafasi ya kuendelea na safari ya Kahama, na badala yake nikaanza kufikiria kurudi Ushirombo.

Nilifikiria kutafuta mgahawa wowote uliokuwa jirani na eneo lile ili nipate japo chakula au kinywaji wakati nikitafakari nini cha kufanya. Nilitoa simu yangu na kutafuta namba ya Eddy nikamjulisha kuwa nilikuwa natoka Ushirombo kwa Rehema na kwamba mgomo wa madereva wa mabasi ulikuwa umenisababisha nikwame Masumbwe wakati nikiwa narudi Kahama.

Kisha nilimpigia Rehema kumjulisha kuhusu hali ile, alinionea huruma lakini hakuwa na namna ya kunisaidia. Hata hivyo alinishauri kuwa endapo ingefika jioni bado sijapata usafiri angetafuta namna ya kunifanya nirudi Ushirombo hata kwa kumtuma yule dereva wa teksi anifuate. Tukakubaliana.

Nilipokata simu nilimsogelea mtu mmoja aliyeonekana kuwa mwenyeji wa eneo lile na kumuuliza kama ningeweza kupata chakula kizuri, bila kusita akanionesha mgahawa mmoja ulioitwa ‘Victoria’, ambao ulikuwa jirani na kituo kimoja cha kujazia mafuta, pale Masumbwe.

Nilianza safari ya kuelekea katika ule mgahawa wa Victoria ambao haukuwa mbali sana na eneo lile nililokuwa nimesimama, nilipofika nilitafuta sehemu nzuri nikaketi, na mara mhudumu mmoja mcheshi alinifuata huku akiachia tabasamu bashasha la makaribisho.

Alikuwa msichana mrembo na mtanashati, msichana wa Kisumbwa aliyekuwa amevaa sare maalumu za mgahawa ule akionekana kuyazingatia vizuri maadili ya kazi yake kwa kutabasamu mbele ya wateja waliowasili pale kwenye mgahawa.

“Karibu kaka, sijui ungependa chakula gani?” aliniuliza yule mhudumu kwa sauti tulivu na nyororo ya kumtoa nyoka pangoni iliyonifanya nishikwe na mdawao kwa sekunde kadhaa kana kwamba nilikuwa sijui nile au ninywe nini. Yule mhudumu alinitazama kwa makini huku akitabasamu, na baada ya kitambo kifupi nikavunja ukimya huku nami nikitabasamu.

“Niletee ugali wa dona na samaki sato, na usisahau maziwa mtindi,” nilimwagiza huku nikimchunguza vizuri. Yule mhudumu aliitikia kwa kubetua kichwa chake huku akiendelea kutabasamu na wakati alipokuwa akitaka kuondoka kutoka eneo lile nikamtupia swali.

“Sijui kitachukua muda gani?”

“Sasa hivi, kwa kuwa kipo tayari,” aliniambia yule mhudumu huku tabasamu bashasha usoni kwake likiwa halitaki kwenda likizo.

Okay, basi nifanyie chapchap, nataka nibahatishe magari ya kunifikisha Kahama,” nilimwambia yule mhudumu huku nikimkonyeza na kumfanya azidi kutabasamu.

Aligeuka na kuondoka haraka kutoka eneo lile na wakati akitembea nilimsindikiza kwa macho hadi pale alipotokomea kabisa jikoni, kisha nikaanza kufikiria namna ya kujinasua kutoka katika janga lile la kukosa usafiri. Nilifikiria sana kama nilitakiwa niendelee na safari yangu au nitegee hadi jioni ili nirudi Ushirombo lakini sikuweza kabisa kupata jibu.

Nilifikiria kumuuliza yule mhudumu kama alikuwa ameolewa, na kama hajaolewa nimwage sera zangu na kutafuta nyumba nzuri ya kulala wageni pale Masumbwe ili tuumalize usiku pamoja, lakini nilijikuta nikilifuta kabisa wazo lile, maana nilishakata shauri la kubadili tabia yangu ili nisiendelee kumkwaza Rehema ambaye alidai anajua kila nilichokuwa nikikifanya, hata kama yupo mbali nami.

Wakati nikitafakari hayo mara nikakumbuka kuwa sikuwa nimechukua namba ya simu ya Selemani, ningeweza kumpigia simu na kumwambia aniazime gari moja la kunifikisha Kahama, maana niliamini kuwa nyumbani alikuwa na magari mengine.

Hata hivyo, kwa muda ule nisingeweza tena kumpata maana sikujua aliishi sehemu gani pale Masumbwe, ingawa nilikuwa na namba ya simu ya Jamila lakini nisingeweza kumpigia simu. Nilimfahamu vyema Selemani, na kama angegundua kuwa nilichukua namba ya simu ya Jamila basi huo ungekuwa mwisho wa urafiki wetu, kwani alimlinda sana dada yake.

“Karibu chakula, kaka,” sauti ya yule mhudumu wa mgahawa aliyekuwa amesimama akinitazama kwa makini baada ya kuniletea chakula ilinizindua kutoka kwenye mawazo yangu. Nilimtazama usoni yule mhudumu huku nikiachia tabasamu jambo lililomfanya naye atabasamu kidogo kwa aibu huku akiyakwepesha macho yake pembeni yasikutane na yangu.

Wakati huo huo alichukua birika la maji na beseni dogo kisha akaanza kuninawisha mikono yangu huku akikwepa kuniangalia usoni. Alipomaliza kuninawisha aliondoka haraka kutoka eneo lile akiniacha napata mlo wangu taratibu, huku kichwani nikiendelea kufikiria juu ya safari yangu ya Kahama. Ki ukweli sasa nilikuwa nimedhamiria kuendelea na safari ya Kahama na hatimaye Buzwagi kwa namna yoyote ile, ije mvua au lile jua. Niliona kuwa ni bora nitimize ahadi ya kuongea na Eddy kuhusu suala la kumuoa Rehema.

Nilipomaliza kula kile chakula, ambacho ki ukweli kilikuwa kitamu sana, nikamwona yule dada mhudumu akija pale mezani mara moja kuondoa vile vyombo na kusafisha ile meza huku lile tabasamu lake la kibiashara usoni likionekana kukataa kabisa kwenda likizo.

Alipokuwa akisafisha ile meza kabla hajaondoa vyombo, nilimwagiza aniletee chupa kubwa ya lita moja na nusu ya maji ya vuguvugu. Alibetua kichwa chake kukubali na kuondoka haraka kisha akaniletea yale maji, nikaanza kunywa taratibu huku nikiendelea kutafakari jinsi ambavyo ilikuwa muhimu kwangu kufika Kahama siku hiyo.

Niliketi hapo kwa muda mrefu nikiwaza mambo mengi, picha ya maisha yangu ilikuwa ikinijia akilini, sasa niliamua kuachana na wasichana wote ili nianze maisha mapya ya ndoa nikiwa na Rehema.

* * *

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

76

Taharuki.


Saa 11:30 jioni…

Mawazo mengi yalikuwa yamepita kichwani kwangu na nilipokuja kushtuka muda mrefu ulikuwa umepita nikiwa bado nimeketi palepale kwenye mgahawa, hivyo nikaanza kuhisi kuwa nilikuwa nimetumia muda mwingi sana kukaa ndani ya mgahawa ule.

Nilizungusha macho yangu kutazama huku na kule na kugundua kuwa wahudumu wa ule mgahawa walikuwa wakiniangalia kwa umakini sana, huku wakionekana kuongea kwa sauti ya chini. Kwa hali ile nilidhani kuwa huenda wale wahudumu wa ule mgahawa walikuwa wakinishangaa sana kwa kuona kuwa wateja wengine walikuja wakahudumiwa na kuondoka lakini mimi niliendelea kukaa palepale nikionekana kuwaza mbali.

Sikuwa na uhakika kama wakati nilipokuwa mbali kimawazo huenda walinishuhudia nikiongea peke yangu, maana hali ya mtu kuongea peke yake humpata anapokuwa katika hali ya mawazo mengi. Mara nikakumbuka kuwa nilikuwa sijalipa fedha ya chakula nilichokula, hivyo nilimwita yule mhudumu aliyenihudumia, nikamlipa fedha ya ule mlo niliokula.

Niliporudishiwa chenji yangu nikachukua begi langu na kutoka nje ya ule mgahawa, nikatembea taratibu kurudi katika eneo la stendi ya mabasi huku wale wahudumu wa mgahawa wakinisindikiza kwa macho yaliyojaa mshangao.

Nilipofika pale stendi nilipowaacha abiria wengine nikaangaza macho yangu huku na kule na haraka nikagundua kuwa abiria wengi waliokuwa katika eneo lile wakisubiri usafiri hawakuwepo tena, ila wapiga debe wachache waliokuwa wakizungukazunguka tu eneo lile pasipo kazi maalumu ya kufanya.

Hali ile ikanifanya niingiwe na wasiwasi zaidi kuwa huenda usafiri wa dharura ulikuwa umepatikana wakati mimi nilipokuwa nimekaa ndani ya ule mgahawa nikiwa natafakari. Nilimfuata kijana mmoja ambaye mwanzoni nilimkuta akipiga debe katika ile stendi nikamuuliza kama kulikuwa na usafiri wowote ulioondoka kuelekea Kahama katika kipindi kile ambacho mimi sikuwepo pale stendi.

Yule mpiga debe aliniambia kuwa kulitokea gari moja la kibinafsi lililochukua abiria wachache tu, lakini mgomo wa mabasi uliendelea kwani agizo lililokuwa limetolewa na viongozi wa madereva wa magari ya abiria nchini Tanzania kuwa usafiri ulikuwa umesitishwa kabisa kwa safari zote nchini kwa siku hiyo.

Wakati yule mpiga debe akinieleza nilikuwa nayatembeza macho yangu taratibu kulikagua eneo lile huku nikiziangalia nyuso za watu wachache waliokuwa bado wapo maeneo yale. Katika uchunguzi wangu dhidi ya watu wale wachache waliokuwepo eneo lile mara macho yangu yakavutiwa kumwangalia msichana mmoja aliyekuwa amesimama peke yake mbali kidogo na eneo lile akiwa ameshika kiuno.

Nilipomwangalia kwa makini yule msichana nilimwona ni kama na yeye alikuwa amekatishwa tamaa sana na tamko lile la kusitishwa kwa usafiri. Nikajaribu kuyasoma mawazo yake lakini sikuweza kufahamu mara moja alikuwa akiwaza nini muda ule.

Alikuwa msichana mrefu na mweupe wa asili, si ule weupe wa mkorogo bali ule wa asili wenye ung’avu wa kuteleza. Umri wake ulikuwa hauzidi miaka 25, alikuwa mwembamba lakini akiwa na umbile lililovutia mno na mwenye haiba nzuri ya kuvutia.

Kwa yeyote awaye mwanaume rijali hapana shaka kama angemwona msichana yule asingeacha kukiri kuwa alikuwa ni moto wa kuotea mbali, kwani kwa mlingano wa macho tu, msichana yule alitoa tafsiri ya kuwa na ule uzuri usiomithilika ambao ungeweza kumfanya hata bubu aongee.

Alikuwa amevaa suruali ya dengrizi ya rangi ya bluu bahari iliyokuwa inambana na ilikuwa imechanwa mbele katika maeneo ya mapaja yake na kuifanya miguu mizuri iliyotazamika kuonekana vizuri.

Juu alikuwa amevaa fulana nzito ya rangi la samawati iliyoyafanya matiti yake yenye ukubwa wa wastani yaliyochongoka mbele na yaliyoonekana kuwa na hasira ya kutoboa fulana hiyo yaonekanae vizuri, na juu ya fulana hiyo alivaa shati zito la rangi ya bluu la kitambaa cha kadeti, na hakuwa amefunga vifungo.

Miguuni alikuwa amevaa buti ngumu za kike zilizokuwa zimemtoa bomba zaidi na kumfanya apendeze sana kwa mapigo ya msichana wa kileo. Mgongoni alikuwa amebeba begi dogo na mkononi alikuwa ameshika pochi nzuri nyeusi ya kike.

Kwa mwonekano wa haraka tu niliweza kutambua kuwa wazazi wake walikuwa ni watu wenye uwezo mkubwa kifedha, maana mavazi yake yalikuwa ya gharama kubwa ingawa kwa mtazamo wa haraka ungeweza kudhani ni ya kawaida.

Pia niliweza kung’amua kuwa alikuwa amevaa mkufu uliotengenezwa kwa vito vya thamani kama vile dhahabu na kadhalika ingawa alikuwa ameuficha ndani ya fulana na shati lake. Vitu vyote hivyo kwa pamoja na asili ya urembo wake vilimtoa katika sura ya mrembo matata aliyekuwa amekolea sana!

Kwa nukta chache nilihisi kama moyo wangu ulisahahu mapigo yake, na mara yalipoanza tena nilijikuta nikivuta pumzi ndefu za ndani kwa ndani, kisha nikazishusha taratibu.

Sikujua kwa nini nilipatwa na mshtuko kiasi kile baada ya kumwona yule msichana, lakini nilichokifahamu kwa wakati ule ni kitu kimoja tu, kwamba nilivutiwa sana kumtazama huku nikiwa na uhakika kabisa kuwa alikuwa hafahamu chochote kuwa nilikuwa nikimwangalia kwa kificho. Hali ile ikanifanya niendelee na udadisi wangu. Mara nikamwona akiinua mkono wake kutazama saa yake ya mkononi kisha akakunja sura yake akionekana kushtuka sana.

Nilipoichunguza vizuri, japo alikuwa amesimama mbali kidogo nami, niligundua kuwa ilikuwa ni saa ghali sana ya kike aina ya Swatch Skinmesh, ambayo bei yake si haba. Kisha nikamwona akifungua pochi yake na kutoa simu yake ya mkononi kutoka kwenye ile pochi, akaanza kutafuta namba fulani ili apige, mara nikajikuta nikianza kupiga hatua kumfuata pale alipokuwa amesimama.

Wakati naanza kumfuata nikamwona akisogea kando zaidi na kwenda kusimama kwenye kibanda kimoja kilichokuwa eneo lile, kisha akawa anaongea na simu huku akionekana kukata tamaa. Nilihisi kuwa maelezo ya wale wapiga debe pale stendi yalimfanya aondoe kabisa matumaini ya kupata usafiri.

Niliweza kusogea karibu zaidi huku uso wangu ukianza kutengeneza tabasamu la kirafiki. Msichana yule akawahi kugeuka na kuniangalia na hapo macho yuetu yakakutana, nikamsalimia kwa kupunga mkono huku uso wangu ukitengeneza tabasamu la kirafiki. Msichana yule aliniangalia kwa mshangao kidogo kuanzia chini hadi juu kana kwamba alikuwa akijaribu kukumbuka kama aliwahi kuniona mahala.

Hata hivyo, hakunijibu bali alisogea mbali zaidi na mimi huku akiendelea kuongea na simu kwa muda mrefu sana akionekana kulalamika, na mara kadhaa aligeuza shingo yake kunitupia jicho la wizi. Wakati akiendelea na maongezi yake kwenye simu nikagundua kuwa idadi ya watu ilikuwa ikiendelea kupungua taratibu huku dalili za kusafiri zikizidi kufifia.

Hivyo, akili yangu ikaanza kuchangamka nikianza kufikiria nini nifanye. Nikiwa katika kuwaza kama nimpigie simu Rehema kumwambia kuwa nilitaka nirudi Ushirombo mara nikamwona yule msichana akiondoka pale alipokuwa amesimama na kumfuata kijana mmoja aliyekuwa amesimama kando ya eneo lile akiangaza macho yake huku na kule kama aliyekuwa akitafuta kitu.

Nilimwona yule msichana akizungumza na yule kijana na baada muda mfupi wa maongezi yao nikamwona yule kijana akigeuka kutuangalia mimi na watu wengine wachache tuliokuwepo katika eneo lile kisha akatuonesha ishara ya kuuliza kama tulikuwa tayari kusafiri kwenda Kahama. Nilijisogeza haraka pale walipokuwa wamesimama na kupitia maongezi yao nikaelewa kuwa kulikuwa na usafiri wa mtu binafsi wa kuelekea Kahama.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

77

Hivyo yule kijana alikuwa mhusika mmojawapo wa gari lile ambalo kwa mujibu wa maelezo yake ni kuwa, gari hilo lilikuwa limeegeshwa nyuma ya kituo cha kujazia mafuta kilichokuwa jirani na eneo lile. Alituambia kuwa walikuwa wameliegesha gari lao kule nyuma ya kituo cha kujazia mafuta kwa kuhofia kufanyiwa fujo na madereva wa magari ya abiria endapo wangeliegesha pale stendi na kutafuta abiria.

Sikuwa na wasiwasi wowote na yule kijana kwani katika hali na mazingira kama yale usafiri wa magendo wa namna ile ulikuwa ni jambo la kawaida kufanyika katika stendi yoyote ile, hususan pale inapotokea shida ya usafiri. Nikamuuliza yule kijana nauli ingekuwa shilingi ngapi kutoka Masumbwe hadi Kahama, akanieleza kuwa alikuwa akitoza shilingi elfu kumi kwa kila abiria.

Sikuona kwa nini nijivunge, hata kama ingekuwa shilingi elfu ishirini ningesafiri tu, niligeuka kuwaangalia wale abiria wengine, hususan yule msichana nikitaka kufahamu wao walikuwa wakilichukuliaje suala lile. Wote walionekana wako tayari kusafiri kwa gharama yoyote.

Tuliongozana na yule kijana hadi kule nyuma ya kile kituo cha kujazia mafuta ambako walikuwa wameliegesha gari lao. Wakati tukitembea kuelekea kule nyuma ya kile kituo cha kujazia mafuta mara kwa mara yule msichana alikuwa akinitazama katika namna ambayo sikuweza kuielewa. Baada ya mwendo mfupi wa safari yetu hatimaye tukawa tumekifikia kituo kile cha kujazia mafuta.

Tulipolikaribia vizuri eneo lile mara nikaliona gari moja aina ya Toyota Land Cruiser Prado lenye muundo wa kizamani la rangi ya samawati likiwa limeegeshwa kando ya kituo kile cha kujazia mafuta. Japo lile gari ingawa lilikuwa la muundo wa kizamani lakini lilionekana kuwa bado imara na lenye uwezo mzuri wa kumudu safari.

Mle ndani tulikuta kuna watu watano wameketi kwa utulivu. Mbele kulikuwa na dereva wa lile gari, mwanaume wa makamo aliyekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 40 hadi 45, alikuwa mrefu na mweupe. Macho yake yalikuwa makali na alikuwa amevaa baragashia nyeupe ya kufumwa. Alikuwa ameketi nyuma ya usukani akionekana kuendelea kusubiri abiria na siti ya abiria upande wa kushoto wa dereva ilikuwa tupu.

Ile sehemu ya katikati kulikuwa tayari kuna watu wanne waliokaa kwa kubanana, wote vijana ambao kwa mtazamo wa haraka tu hawakuzidi miaka therathini. Kati yao mmoja alikuwa ni mwanadada mfupi mnene. Niliwasalimia wale abiria kiungwana na wote wakaitikia kwa pamoja. Yule kijana aliyetuleta alitufungulia mlango wa nyuma ambako ndiko kulikokuwa na siti tupu.

Mimi sikujali, badala yake nilijitoma ndani ya lile gari na kuketi kwenye siti za nyuma za kutazamana. Wale abiria wengine pia wakapanda na hivyo kukawa na nafasi moja tu iliyokuwa imebakia. Muda huohuo simu yangu ikaanza kuita na nilipoitazama kwa makini nikaliona jina la Rehema kwenye kioo. Nilipokea nikamfahamisha kuwa nimeshapata usafiri na nilikuwa njiani kuelekea Kahama.

Nikakata simu huku nikimwangalia yule msichana ambaye alikuwa amefungua ule mlango wa mbele kwenye siti ya abiria upande wa kushoto wa dereva lakini yule kijana aliyetuleta alimtaka akae nyuma kwa kuwa siti ile ilikuwa tayari ina mwenyewe. Yule msichana alisimama pale akionekana kukata tamaa huku akiwa hataki kukaa kule nyuma, aliminya midomo yake huku akishusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani.

Yule kijana akasikika akimweleza kuwa hakuna usafiri mwingine, hivyo kama angebaki ingekuwa ni shauri lake mwenyewe. Nilimwona yule msichana akinyanyua mabega yake juu na kuyashusha kisha alibetua midomo yake huku akionekana kubadili msimamo wake pale alipoona hakuna namna nyingine ya kumwezesha kusafiri.

Alikuja kule nyuma ya lile gari na kuingia kisha akaketi mbele yangu upande wa pili kwenye siti iliyokuwa mkabala na mimi, na kutokana na muundo wa siti za lile gari, mtindo ule wa ukaaji ukatufanya tujikute tukitazamana.

Muda ule ule nikamwona mwanamume mmoja wa makamo aliyekuwa amevaa suti maridadi akija haraka eneo lile akitokea kwenye ule mgahawa wa Victoria huku akiwa amebeba mkoba mzuri mweusi wa gharama katika mkono wake wa kulia na mkono wake wa kushoto alikuwa ameshika chupa kubwa ya lita moja na nusu ya maji safi.

Alipofika kwenye lile gari alishika kitasa cha mlango ule wa mbele wa ile gari, akavuta na kufungua kisha aliingia na kuketi kwenye ile siti ya abiria upande wa kushoto wa dereva. Muda uleule nikaliona gari moja aina ya Land Cruiser Pick-up likipita pale na kusimama mbele yetu, kwenye kile kituo cha kujazia mafuta.

Ndani ya lile gari kulikuwa na wanaume watatu, dereva na mtu mmoja walikuwa wameketi mbele na mtu mwingine alikuwa amesimama kule nyuma ya lile gari. Wote walikuwa warefu na wenye miili imara iliyojengeka. Nilijikuta nikivutiwa sana kuwaangalia wale watu ingawa sikujua kwa nini nilijikuta nikivutiwa sana kuwaangalia.

Mara nikamwona yule mtu aliyekuwa amesimama kule nyuma ya lile gari akishuka haraka kisha akatazama huku na kule na kuharakisha kuvuka barabara na kuja moja kwa moja upande tuliokuwepo.

Wakati akivuka kuja upande tuliokuwepo nikawaona wanaume wawili wakitoka ndani ya ule mgahawa wa Victoria na kupanda kwenye lile Land Cruiser Pick-up lililomshusha yule mtu, na hapo lile gari likaondoka na kuingia barabara iliyoelekea Kahama.

Wakati huo yule kijana aliyekuwa ametuleta kwenye lile gari alizunguka kwenda kwenye mlango wa dereva, nikamwona yule dereva akijipapasa mifukoni, na kama aliyegutuka akatugeukia, lakini kabla hajasema chochote yule jamaa aliyeshuka kwenye lile gari Land Cruiser Pick-up akasogea mlangoni kwa dereva.

Alipokuwa pale nikashtushwa sana na macho yake makubwa yaliyoonesha uchovu lakini yalikuwa ni aina fulani ya yale macho yaliyoashiria shari. Alikuwa na uso mrefu uliokuwa umetulia, alikuwa amevaa kofia aina ya kapelo na miwani midogo myeusi ya jua aliyokuwa ameipandisha juu ya uso wake.

Aliposimama pale mlangoni kwa dereva akawa anachungulia mle ndani kiaina kama aliyekuwa anamtafuta mtu fulani ndani ya lile gari tulilopanda, kwani alipochungulia alikuwa akitutazama usoni kiaina. Dereva akamtazama kwa makini.

“Vipi kuna mtu unamtafuta?” dereva wa lile gari alimuuliza yule jamaa.

“Hapana, nataka kujua kama mnaelekea Kahama!” yule mtu alimwambia yule dereva huku akiendelea kututupia jicho la wizi.

“Ndiyo, tunaelekea Kahama lakini tayari gari limeshapendeza, si unaona mwenyewe,” yule dereva alimwambia yule mtu huku akiendelea kumtazama kwa macho ya udadisi.

Yule jamaa alishusha pumzi na kulizunguka gari akiendelea kutuangalia kwa makini, kisha akaondoka zake. Muda wote nilikuwa namtazama kwa umakini na sura yake ikanitia mashaka. Sikujua kwa nini nilikumbwa na hisia mbaya juu yake, na hapo nikamkumbuka Rehema. Hata hivyo, niliamua kuzipuuza hisia zangu na kuanza kuifikiria safari yangu ya kurudi Buzwagi.

Mara yule dereva wa gari tulilopanda akageuka tena nyuma na kuanza kudai nauli, alitutazama kwa utulivu huku akitengeneza tabasamu jepesi usoni mwake. Bila kupoteza muda kila mmoja alitoa fedha na kumpa, nami bila kuchelewa nikachukua pochi yangu kutoka mfukoni na nilipoifungua nikahesabu noti zenye thamani ya nauli iliyohitajika na kumpa yule dereva kama malipo ya nauli yangu.

Yule dereva alizipokea zile fedha na kuanza kuzihesabu taratibu huku ukimya ndani ya lile gari ukitawala. Kisha alichukua noti ya shilingi elfu tano kutoka kwenye zile fedha na kumpa yule kijana aliyetuleta. Akawasha gari lake tayari kwa safari ya kuelekea Kahama. Niliitazama saa yangu nikagundua kuwa ilikuwa imeshatimu saa 12:45 jioni.

Yule dereva aliliondoa lile gari kwa mbwembwe huku akiwa makini kutazama barabarani na kuingia kwenye barabara ya Kahama na mbele kidogo tukalipita lile gari aina ya Land Cruiser Pick-up likiwa limeegeshwa kando ya barabara huku nyuma yake kukiwa na alama ya pembe tatu inayoakisi mwanga kama ishara ya kutambulisha kuwa gari lile lilikuwa limepata hitilafu.

Itaendelea...
 
narudi buzwagi.jpeg

78

Nje ya lile gari kulikuwa na wale wanaume wawili walioonekana wameinamia kwenye boneti la gari lililokuwa limefunguliwa wakiwa wanalitengeneza. Nikaangalia huku na kule lakini sikuweza kuwaona wale wanaume wengine wawili waliopandia pale kwenye kituo cha kujazia mafuta. Tulipowapita nikawaona wakiinua sura zao na kugeuka kulitazama gari letu kwa makini sana kana kwamba kuna kitu kilikuwa kinawashangaza.

Sasa nikaanza kujiwa na hisia mbaya na njia nzima nikawa ninayafikiria maneno ya Rehema kuwa alihisi kuna jambo baya lingetokea, na hivyo njia nzima nikawa nipo makini sana. Wakati huo gari lilikuwa linakata upepo na safari ikaendelea huku dereva akiwa makini zaidi kutazama barabarani.

Miale hafifu ya jua la machweo ilikuwa mbioni kutoweka angani na kiza kilikuwa mbioni kuchukua nafasi yake. Dereva aliendesha kwa kasi akiifuata barabara ile ya Kahama huku taratibu tukianza kuuacha mji wa Masumbwe nyuma yetu.

Nilikuwa nimezama katikati ya tafakuri nzito nikifikiria jinsi nitakavyoongea na Eddy hadi aniamini na baadaye tuongee na wazee ili waone namna ya kutuma washenga nyumbani kwa wazazi wa Rehema.

Muda mfupi baadaye tukawa tumeuacha kabisa mji wa Masumbwe nyuma yetu, na sasa sauti pekee iliyokuwa ikisikika mle ndani ya gari ilikuwa ni sauti ya muungurumo wa injini ya lile gari.

Lile gari lilikuwa likienda mwendo wa kasi ingawa yule dereva alionekana kuwa makini sana huku akionekana pia kuizoea vizuri ile barabara, na wakati safari ikiwa inaendelea nikaanza kumchunguza yule msichana mrembo nikitafuta namna ya kumzoea.

Nilimwona akiwa ameelemewa sana na usingizi, nilidhani kwa sababu ya uchovu, na muda huo giza hafifu lilikuwa limeanza kutanda angani, hata hivyo, dereva wa lile gari aliwasha taa kubwa za mbele na mwanga mkali wa taa zile ulijitahidi kulifukuza giza lile lililokuwa limetanda mbele yetu huku tukizidi kutokomea mbele zaidi.

Hakuna aliyekuwa akiongea muda huo na hivyo mle ndani ya gari kulitawaliwa na kiasi kikubwa cha ukimya wa namna yake. Nilimtazama yule msichana mrembo, sikuona tashwishwi yoyote katika sura yake kama ilivyokuwa kwa abiria wengine ndani ya lile gari, na kila mmoja alionekana kuchoka sana. Uso wa yule mrembo ulikuwa umepoteza kabisa nuru na utulivu, kwa namna nyingine nilimwona akiitupia jicho saa yake ya mkononi mara kwa mara na kusonya na mara akaonekana kuzama kwenye fikra fulani.

Mwendo wetu ulikuwa si wa kubabaisha tukikatiza katikati ya pori na baada ya mwendo mfupi wa safari yetu mbele kidogo tukaanza kuvuka makazi ya watu katika kijiji fulani, njia panda ya Kanegere, na hapo nikawaona watu watatu wakilisimamisha gari letu, hata hivyo dereva hakusimama. Tuliendelea kukatisha katikati ya msitu mnene wenye giza zito huku manyunyu hafifu ya mvua yakianza kudondoka hali iliyofanya barabara ile izidi kutisha wakati ule wa usiku.

Tulipishana na magari mawili matatu wakati tukikatiza katikati ya lile pori la Kanegere, muda wote dereva alikuwa yuko makini sana huku akiendesha kwa mwendo kasi lakini wenye tahadhari za aina zote. Kisha tukaanza kukatisha katikati yam situ mnene huku safari ikionekana kuwa ndefu sana lakini yule dereva wetu alikuwa makini mno akiendelea kuendesha kwa mwendo kasi na hakuna aliyekuwa akimsemesha mwenzake muda wote wa safari yetu.

Huku tukizidi kuuvuka msitu mnene, vichaka na kona kadhaa za ile barabara, niliwatazama tena wale abiria wenzangu ndani ya gari na kuwaona wote wakiwa hoi kwa usingizi kutokana na uchovu wa kutwa nzima. Ni mimi na dereva tu ambao hatukuwa tumesinzia, na katika ukimya ule, nilijikuta nikianza kuwaza namna ambavyo ningeweza kutimiza ahadi niliyompa Rehema na hatimaye tuwe mume na mke.

Wakati nikiendelea kuwaza, tukawa tunavuka mpaka uliotengenisha mikoa ya Shinyanga na Geita, kisha tukaanza kuvuka makazi ya watu katika Kijiji cha Tumaini kilichokuwa kando ya barabara kwa upande mmoja na upande mwingine pori, na kwa wakati ule wa usiku nyumba za makazi ya watu zilionekana kama vichaka kwani wakazi wake wengi walikuwa wamekwisha ingia majumbani.

Muda huo nilianza kuhisi kuzidiwa na uchovu wa kutwa nzima, nikainamisha kichwa changu na kuanza kusinzia, lakini nilishtuka baada ya hisia mbaya kunijia tena akilini mwangu huku maneno ya Rehema yakijirudia akilini mwangu, na hapo haraka nikainua kichwa changu na kuyapeleka macho yangu kuangalia nyuma tulikokuwa tunatoka.

Mara nikaiona miale mirefu ya mwanga mkali wa taa za gari moja lililokuwa linakuja nyuma yetu kwa mwendo wa kasi zaidi. Macho yangu yalivutiwa kulitazama lile gari namna lilivyokuwa likija kwa kasi na kutukaribia nyuma yetu, huku akili yangu ikianza kutafakari juu ya gari lile kwa jinsi lilivyokuwa likizidi kutusogelea.

Baada ya muda mfupi lile gari likawa limetufikia na sasa lilikuwa nyuma yetu, takriban mita ishirini hivi kutoka lilipokuwa gari letu. Mara likaanza kutupita kwa kasi ya ajabu. Tukio lile likamfanya dereva wetu apunguze mwendo wa gari na kuliruhusu lile gari lipite kwa uhuru na kuendelea na safari yake.

Wakati likitupita nikapata wasaa mzuri wa kulichunguza na hapo nikagundua kuwa lilikuwa ni lile gari Land Cruiser Pick-up tulilolipita kando ya barabara pale Masumbwe likiwa limeharibika. Niliweza hata kuzikumbuka namba zake za usajili. Hisia mbaya zaidi zikanijia na kunifanya nianze kusali kimoyo moyo nikimwomba Mungu atuepushie balaa lolote.

Mara tu baada ya lile Land Cruiser Pick-up kutupita, nikaliona likipunguza mwendo ghafla na kwenda kutuzuia kwa mbele. Kitendo kile cha kupunguza mwendo ghafla mbele yetu huku likituzuia kikamfanya dereva wa gari letu kukanyaga breki za ghafla huku akijitahidi kwa kila namna kulikwepa lile gari huku ufundi wake katika udereva ukionekana kugonga mwamba.

Kutokana na mwendo wake alionekana kushindwa kuhimili na hivyo gari letu liliyumba na kuserereka huku magurudumu yakilalamika kwenye ile barabara ya lami. Hata hivyo, alikuwa amekwisha chelewa, akaligonga lile gari kwa nyuma na kusababisha taa za mbele za gari letu kuvunjika baada ya kugonga kwenye ngao ngumu ya nyuma ya lile Land Cruiser Pick-up lililokuwa limesimama mbele yetu.

Muda ule ule nikawaona watu watatu waliokuwa nyuma ya lile gari Land Cruiser Pick-up wakiruka kutoka kwenye lile gari huku wakiwa wameshika vyema bunduki za kivita aina ya SMG na kuzielekeza kwenye gari letu.

Sasa nilikuwa na uhakika kabisa kuwa zile hisia mbaya zilizokuwa zikinijia zilikuwa sahihi, na tukio lile likanidhihirishia kuwa hatukuwa salama, kwani tulikuwa tukielekea kukabiliana na utekaji kutoka kwa wale watu. Wakati nikitafakari kuhusu jambo hilo nilijikuta nikishikwa na hofu kubwa na taharuki isiyoelezeka.

Sikuwa na shaka na wala sikuhitaji mtu yeyote kunieleza kuwa mambo hayakuwa shwari tena, hivyo nilipaswa kufanya uamuzi wa haraka kabla sijashuhudia jambo baya likitokea mbele ya macho yangu, ambalo lingeacha taswira isiyoelezeka ndani ya akili yangu, kama ningebahatisha kubaki hai.

Kabla sijajua nifanye nini nikamwona dereva wetu aliyekuwa amepagawa baada ya kuhisi jambo baya lilikuwa mbioni kutokea, akifanya jambo lisilotarajiwa, kwani aliingiza gia ya kurudi nyuma na hapo hapo kukanyaga pedeli ya mafuta na kulifanya gari letu lianze kurudi nyuma kwa mwendo wa kasi ya ajabu.

Hata hivyo, hatukuweza kwenda umbali mrefu zaidi kwani muda ule ule sote tulishtushwa na mlio mkali wa risasi zilizopasua kioo cha mbele cha gari na kulifanya liende likiyumbayumba barabara nzima.

Katika taharuki ile gari lile likaanza kuserereka likielekea kando ya barabara na kuanza kuingia vichakani kwa mwendo uleule wa kasi huku likiyumba na kisha kwenda kugota kwenye mti mkubwa uliokuwa takriban mita hamsini nje kabisa ya ile barabara. Kitendo cha lile gari letu kugota pale kwenye ule mti mkubwa kikanifanya nigonge kichwa changu na kusikia maumivu makali yaliyosambaa hadi mgongoni.

Itaendelea...
 
Back
Top Bottom