374
Yule mzee alimtazama Daniella kwa utulivu pasipo kusema neno. Sasa Daniella akaanza kutoa utambulisho mfupi. Na hapo nikafahamu kuwa yule mzee aliitwa Askofu Jerome Masinde, kaka wa mama yake Daniella, na alikuwa Askofu Mkuu wa
Living Paradise Ministries.
Nilishtushwa kidogo na jina la mwisho la askofu yule, ‘Masinde’, kwa kuwa lilifanana na jina la mwisho la Rais Albert Masinde, ambaye ndiye sababu ya sisi kuwepo pale Mtwara.
Halafu Daniella alinitambulisha kwa yule askofu, katika namna ya kunipamba zaidi, na kwamba tulikuwa tumefika pale kwake usiku huo kutafuta hifadhi baada ya kushambuliwa. Hata hivyo, Daniella hakuwa amegusia suala la kutoweka kwa Rais Masinde.
Maelezo ya Daniella yalikuwa yamenyooka na hivyo wakati akimalizia kutoa utambulisho Askofu Masinde aliinuka na kunipa mkono japokuwa niliona mashaka kidogo katika uso wake.
“Na wewe ni mpelelezi?” hatimaye Askofu Masinde aliniuliza huku akinitazama usoni.
“Ndiyo! Mimi ni mpelelezi” niliongea kwa utulivu.
“Nilikufahamu tangu nilipokuona kwa mara ya kwanza. Mara nyingi nimekuwa nakutana na wapelelezi na baadhi yao wakitaka kunipeleleza juu ya huduma yangu,” Askofu Masinde aliongea kwa utulivu huku akigeuka kumtazama Daniella.
“Kwa hiyo, mko hapa kwa ajili ya upelelezi juu ya kitu gani hasa?” Askofu Masinde alimuuliza Daniella huku akimtazama kwa umakini.
Mimi na Daniella tulitazamana, hisia zangu ziliniambia kuwa tulipaswa kumwamini yule mzee na kumweleza ukweli kwani huenda angekuwa na msaada mkubwa kwetu hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa mtumishi wa Mungu. Kwenye kazi za kishushushu wakati mwingine unapaswa kujiumbua (kusema ukweli wa kazi yako) ili upate taarifa muhimu unazozitaka. Hivyo nikaamua kumgusia juu ya kutekwa kwa Rais Masinde.
Mara tu nilipoongea juu ya kutekwa kwa Rais Askofu Masinde alinitazama kwa mshangao. “Albert ametekwa…!” aliongea kwa utulivu huku akitafakari.
“Ndiyo, na Idara ya Usalama wa Taifa haifahamu Rais alipo. Siku ya kwanza tu ya ziara yake hapa Mtwara akatekwa na kupelekwa kusikojulikana,” niliongea kwa utulivu.
Askofu Masinde hakusema neno, alikunja sura yake na kutazama dirishani kana kwamba alihisi uwepo wa mtu aliyekuwa akisikiliza maongezi yetu. Nilipomtazama vizuri nikatambua kuwa fikra zake hazikuwa pale bali zilikuwa kilomita nyingi nje ya chumba kile. Kisha kilipita kitambo fulani cha ukimya.
“Ulikuwa unafahamu kuhusu jambo hili?” nilijikuta nikisukumwa nafsini mwangu kumtupia swali lile Askofu Masinde huku nikimtazama usoni kwa makini. Swali langu likamfanya alegeze kidogo uso wake na kutabasamu kisha akakohoa kidogo kusafisha koo lake na hatimaye kuvunja ukimya.
“Ndiyo nafahamu,” Askofu Masinde alijibu na kutufanya mimi na Daniella tushikwe na mduwao wa aina yake na kwa sekunde kadhaa tukamtazama katika namna ya kutoamini maneno yale.
Loh! Hatimaye nilishusha pumzi taratibu na kuulegeza uso wangu huku nikiliruhusu tabasamu jepesi kuchomoza usoni mwangu kisha nikaketi vizuri kwenye kiti changu.
“Albert ni rafiki yangu mkubwa…” Askofu Masinde aliongea kwa utulivu. “Na alikuwa akifika hapa kunisalimia kila mara akija Mtwara.”
“Nataka kufahamu ni mazingira gani yaliyokufanya utambue kuwa Rais ametekwa?” nilimtupia swali lingine Askofu Masinde, swali lile lilimfanya aupishe utulivu kidogo huku akionekana kufikiri jambo kisha akaniambia.
“Ilikuwa kama saa saba za usiku niliposhtushwa kutoka usingizini na mlio wa simu yangu maalumu iliyokuwa mezani chumbani kwangu…” Askofu Masinde alisema huku akionekana kuzidi kuvuta kumbukumbu.
Hata hivyo nilimkatisha. “Simu hiyo ilitoka kwa nani?”
“Ilikuwa ni simu ya Albert, kutoka kwenye namba yake maalumu ambayo hakuwa akiitumia ovyo bali kwa watu maalumu sana na kwa shughuli maalumu, na mzungumzaji alikuwa ni Albert mwenyewe,” Askofu Masinde alisema na kuweka kituo.
Maelezo yale yalikuwa yameanza kunivuta hivyo nilimtazama Daniella, ambaye muda wote alikuwa mtulivu akimtazama mjomba wake kwa shauku kama mwewe aliyeona kifaranga cha kuku, kisha nikaiegemeza vizuri mikono yangu pale juu mezani huku nikimtazama yule mzee kwa umakini.
“Una hakika kuwa sauti ya mzungumzaji kwenye hiyo simu uliyopokea ilikuwa ni ya Rais Masinde mwenyewe?” nilimuuliza Askofu Masinde katika namna ya kutaka kupata uhakika.
“Nina uhakika kabisa kwani sauti ya Albert naifahamu vizuri sana kama ninavyoifahamu mistari ya kiganja changu,” Askofu Masinde alisema huku akichombeza utani.
“Mara baada ya kuipokea hiyo simu Rais alikueleza nini?” hatimaye Daniella aliuliza kwa mara ya kwanza.
“Sauti yake ilikuwa imetawaliwa na kitetemeshi cha hofu na mashaka wakati aliponieleza kuwa maisha yake yalikuwa hatarini, kwani makazi yake yalikuwa yamevamiwa na watu wasiojulikana, hivyo alinitaka kumsaidia na kumwombea kwa Mungu aepushiwe na mabaya,” Askofu Masinde alisema na hapo maelezo yake yakawa yameamsha hisia tofauti nafsini mwangu, sasa niliamua kuuruhusu utulivu kichwani mwangu huku nikitafakari kwa kina juu ya maelezo yale.
Hatimaye nikamuuliza, “Halafu nini kilifuata baada ya hapo?’’
“Nilimdadisi kwa kumuuliza kuwa ni kipi kilichokuwa kimemfanya ahisi kuwa alikuwa amefanyiwa uvamizi, akanieleza kuwa nyumba yake ilikuwa imezingirwa na wavamizi hao wasiojulikana na nje kulikuwa na majibizano ya risasi kati ya walinzi wake na wavamizi hao,” Askofu Masinde alisema na kuweka kituo kisha alitutazama kwa zamu kama mtu afikiriaye jambo.
“Wakati akikupigia simu alikuwa wapi?” hatimaye niliuliza Askofu Masinde kwa shauku baada ya kuhisi kuwa ukimya ulikuwa mbioni kushika hatamu mle ndani.
“Muda huo alikuwa amekimbilia chooni…” Askofu Masinde alisema.
“Baada ya hapo alikueleza nini?” Daniella aliwahi kumuuliza Askofu Masinde.
Askofu Masinde alimtazama Daniella kwa utulivu kisha akasema, “Hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya mwisho kuisikia sauti ya Albert, kwani wakati nilipokuwa nikijiandaa kutia neno ghafla sauti yake ilitoweka hewani na simu yake ilikatwa kabisa na sikuweza kusikia chochote. Nilipoipiga ikawa haipatikani,” Askofu Masinde alisema kwa huzuni. “Hofu ikanishika, sikupata tena usingizi na badala yake nikaamka kutoka kitandani na kuanza kuomba nikimlilia Mungu amwepushie mabaya yote.”
Nilipomtazama Askofu Masinde usoni nikagundua kuwa uso wake ulikuwa umejawa sana na simanzi na hapo nikajua kuwa alikuwa amehuzunishwa sana na tukio lile la kutekwa kwa Rais.
“Kuanzia siku hiyo nimeshindwa kabisa kupata usingizi, na sasa nipo kwenye maombi maalumu na mfungo usio na kikomo kuomba rehema za Mungu ili amwepushe Rais wetu wa mabaya yoyote,” hatimaye Askofu Masinde alisema tena na kushusha pumzi.
“Kuna mtu mwingine yeyote uliyemweleza habari hizi za kutekwa kwa Rais?” nilimuuliza tena Askofu Masinde.
“Hapana! Ila mke wangu alipatwa na shaka lakini nikalazimika kumweleza uongo kuwa Rais alipata dharura na hivyo aliamua kukatisha ziara yake na kuondoka haraka usiku huo,” Askofu Masinde alisema.
Endelea...