Simulizi: Harakati za Jason Sizya

Simulizi: Harakati za Jason Sizya

utata.JPG

355

Anahitaji msaada…




Saa 3:00 usiku…

DANIELLA aliliegesha gari katika viunga vya majengo ya VETA Mtwara, nikateremka na kuanza kupiga hatua zangu taratibu kando kando ya Barabara ya Chuno nikielekea katika hoteli tuliyofikia, Naf Beach Hotel. Macho yangu yalikuwa makini kuangaza kila pembe kuona kama palikuwa na yeyote mwenye shauku nami.

Tulikubaliana kutofika pamoja pale hotelini kwa sababu ya usalama wetu maana ilishaonekana wazi kuwa uwepo wetu katika Mji wa Mtwara ulikuwa unajulikana na adui zetu, na walionekana kuwa wana mtandao mpana sana uliowafanya kupata taarifa za kila hatua tuliyopiga, jambo lililotufanya kuzidisha tahadhari.

Hadi muda huo, japokuwa tulikuwa hatujamaliza hata saa ishirini na nne katika harakazi zetu, lakini nilikuwa na hisia kuwa hatukuwa tumepiga hatua nzuri katika harakati hizo za kuutafuta ukweli kuhusu kutoweka kwa Rais Masinde.

Wasiwasi wangu ulikuwa kwamba habari za kutoweka Rais Masinde zisije zikavifikia vyombo vya habari kabla hatujampata, na hivyo kutusababishia fedheha kubwa kama nchi na taasisi kwa kuonekana taasisi za ulinzi na usalama hazina uwezo wa kumlinda Rais na taifa kwa ujumla.

Kilichokuwa kikiniumiza kichwa ni kuwa, katika maeneo yote tuliyopita na watu wote tulioongea nao au kuwahoji tulikuwa tumeambulia majibu ambayo hayakuwa yametuongoza kwenye kulifumbua fumbo tata la kutoweka kwa Rais Masinde, na badala yake fumbo lilizidi kuwa gumu. Zaidi ya kusikia majina mawili ya Chameleon na Tiger hakuna jambo la maana tulilopata. Hata hayo majina yenyewe yaliendelea kuwa fumbo tata.

Wakati nilipokuwa nikimhoji yule mateka nyumbani kwa Daktari Chitemo, Daniella yeye alimpeleka mke wa Samson Dadi kwenye mojawapo wa nyumba salama na kisha alikwenda kuonana na mke wa Rais, Mama Juliana Masinde, kwa ajili ya kupata maelezo ambayo yangesaidia kulifumbua fumbo tata lakini hakuambua chochote cha maana.

Aliambiwa kuwa Mama Masinde hayupo kwenye ‘mood’ ya kuongea na mtu yeyote tangu mumewe alipotekwa, na alikuwa mtu wa kulia na kujitenga tu jambo lililowafanya walinzi wake na daktari waone kuwa isingekuwa busara kumruhusu Daniella kuongea naye. Hata pale Daniella aliposisitiza umuhimu wa kumwona mama huyo kwani hicho ndicho kilichomleta Mtwara toka Dar es Salaam, alijibiwa kuwa Mama Masinde hakuwa radhi kuonana, achilia mbali kuongea, na yeyote.

Daktari wa mama huyo alisisitiza kuwa asingeweza kumlazimisha mke wa Rais kuongea na mtu kwa sababu alikuwa depressed, yaani alikuwa amefadhaishwa sana na tukio lililomtokea mumewe na kumfanya aonekane kama aliyechanganyikiwa, na walidhani kuwa ni muda pekee ndiyo ungeweza kumtuliza…

Hata hivyo Daniella hakukata tamaa, alimwachia yule daktari namba zake za simu akimwomba kuwasiliana naye pindi hali ya mama huyo ikitulia.

Kwa hali hii, njaa ilikuwa inaniuma kama kidonda huku nikisikia mikoromo tumboni mwangu. Pia hali niliyokuwa nayo nilidhani nilihitaji kuoga, maana mbali na njaa kali iliyosababisha tumbo langu liungurume, nilikuwa mchovu sana.

Hatimaye nikawa nimefika mbele ya ile hoteli ya Naf na kuanza kukatisha katikati ya eneo la maegesho ya magari kuelekea mbele ya hoteli. Katika viunga vile vya maegesho ya magari kulikuwa na magari matatu madogo yaliyoegeshwa.

Wakati nikitembea nilihakikisha kuwa hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia nyendo zangu eneo lile. Nilikuwa nikiyachunguza magari na watu wote katika eneo lile ili kubaini kama kulikuwa na mtu yeyote aliyeonekana kunizingatia.

Nilipofika mbele ya jengo la ile hoteli nikausukuma mlango mkubwa wa kioo na kutokomea ndani huku nikitokea eneo la mapokezi nilipowakuta watu watatu wakiwa wameketi kwenye makochi ya sofa, walikuwa makini kufuatilia taarifa zilizokuwa zikirushwa kwenye runinga pana ya bapa iliyokuwa imetundikwa ukutani pale mapokezi.

Wakati naingia kituo kimoja cha runinga kilikuwa kinarusha taarifa ya matukio ya kigaidi iliyotokea Tanzania katika miji ya Dodoma na Mtwara. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, SACP Deus Kashani alikuwa anatoa mtaarifa kwa waandishi wa habari kuhusu shambulio la kigaidi lililotokea katika Hospitali ya Ligula na madhara yaliyotokea eneo lile, akibainisha kuwa watu watano walikufa na wengine saba kujeruhiwa. Pia aliwaeleza waandishi wa habari kuhusu kuahirishwa kwa ziara ya Rais Masinde mkoani Mtwara kutokana na sababu ambazo hakutaka kuziweka wazi.

Nilianza kusikia minong’ono kutoka wale watu waliokuwa wakifuatilia taarifa ile pale hotelini, walidai kuwa hakukuwa na sababu nyingine iliyomfanya Rais kuahirisha ziara yake zaidi ya ukosefu wa usalama.

Nilitambua kwa nini ilikuwa muhimu itangazwe kuwa ziara ya Rais ilikuwa imesitishwa, kwani wakazi wa Mtwara walishaanza kuingiwa na wasiwasi wakitaka kujua Rais wao alikuwa wapi! Kiongozi ni kiongozi, kutoa taarifa kuwa alitekwa kungeweza kusababisha taharuki nchini na hata vurugu, kwa sababu alikuwa na wafuasi wengi.

Baada ya taarifa ya tukio lile la Mtwara sasa ikawa zamu ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, SACP Yasin Mzee, ambaye alitoa taarifa juu ya shambulio la kigaidi lililotokea Capital Social Club Jijini Dodoma.

Katika taarifa yake alidai ripoti ya awali ya kiuchunguzi ilionesha kwamba ukumbi ule wa kisasa wa burudani wa Capital uliokadiriwa ulikuwa na watu zaidi ya 500 ulilipuliwa baada ya kutokea shambulio kati ya makundi mawili ambayo yalisababisha tukio la kutupiana risasi na hatimaye silaha nzito za kivita kama vile mabomu kutumika.

SACP Yasin Mzee alisema mapigano hayo yaliyosababisha milipuko miwili mikubwa ambayo Jeshi la Polisi lilikuwa bado linaifanyia uchunguzi ili kubaini kama ni mabomu, yalisababisha vifo vya watu 52 na wengine zaidi ya 150 walijeruhiwa, 42 kati yao walikuwa na hali mbaya sana.

Majeruhi walikuwa wamelazwa katika hospitali za Benjamin Mkapa na ile ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, na waliokuwa katika hali mbaya sana walikuwa wamepelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Dah! Taarifa ile ilinifanya nihisi mwili wangu ukisisimka, moja kwa moja mawazo yangu yalienda kwa Almasi, Sofia na Amanda. Nilitamani sana kujua walikuwa na hali gani!

Hata hivyo mawazo yangu yalikatishwa na taarifa iliyofuata ambapo SACP Yasin Mzee alisema kuwa mojawapo wa majeruhi wa kadhia hiyo ambao walikuwa wamelazwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa walikuwa ni Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Almasi Dilunga, na mkewe Sofia, huku dada wa Sofia aliyefahamika kwa jina la Amanda akisalimika.

Pia taarifa zilimkariri mkurugenzi huyo wa Jiji la Dodoma, Almasi Dilunga, ambaye alikuwa akizungumza kwa tabu ndani ya wodi ya VIP katika Hospitali ya Benjamin Mkapa alikolazwa yeye na mkewe kutokana na majeraha waliyoyapata, akimshukuru Mungu kusalimika kwenye kadhia ile ila alikuwa na masikitiko makubwa kwa kuwa alihisi rafiki ambaye pia alikuwa mwandishi maarufu wa habari za kiuchunguzi, Jason Sizya huenda alikuwa mmoja wa watu waliopoteza maisha kwenye tukio hilo.

Endelea...
 
utata.JPG

356

Taarifa ile ikanifanya niyazungushe macho yangu kuwatazama watu wote waliokuwepo pale mapokezi, nikianzia kwa mhudumu wa kike aliyekuwa amesimama kwenye kaunta ya mapokezi akiwa katika sare nadhifu za kazi. Nilikuwa nikimwona kwa mara ya kwanza na kubaini kuwa alikuwa msichana mrefu na mwembamba mwenye miwani mikubwa ya kumsaidia kuona.

Kisha niligeuza shingo yangu nyuma na kuyatembeza macho yangu taratibu kuchunguza kama kulikuwa na sura yoyote ya kuitilia shaka. Kwa kufanya vile nikamwona mwanamume mmoja kati ya wale watatu walioketi kwa utulivu kwenye sofa, alikuwa na mwili alioshiba akiwa ameketi mwishoni kabisa mwa sofa akiwa amevaa shati jeusi la mikono mirefu lenye miraba myeupe na suruali ya dengrizi, na kofia aina ya pama aliyoishusha kidogo usoni na kuziba sehemu ya juu ya uso wake.

Nilijikuta nikivutiwa kumtazama yule mwanamume kwa umakini lakini sikuweza kumtambua.

Mwanamume yule alikuwa ametulia tuli kwenye kochi akiwa ameshika gazeti la Kiingereza la Daily News akionekana kujisomea kimya kimya lakini macho yangu ya kishushushu yalibaini kuwa hakuwa akilisoma lile gazeti bali macho yake yalikuwa makini sana kuchunguza nyendo zangu. Hapo hapo kengele ya hatari ikalia kichwani kwangu.

Nikiwa naanza kumezwa na dunia ya mawazo, yule mhudumu akanishtua kwa kunikaribisha kwa sauti nyororo ya kike. Ilionesha kuwa wakati naingia akili yake ilikuwa imemezwa kufuatilia ile taarifa ya matukio ya kigaidi kwenye runinga na sasa ndiyo kwanza aligundua uwepo wangu pale mapokezi.

Nikawahi kumsalimia huku usoni nikitengeneza tabasamu la kikazi na kisha nikajitambulisha jina na kuomba funguo za chumba. Yule mhudumu alichukua funguo na kunipatia, nikapokea kisha nikaanza kuvuta hatua zangu kueleka kwenye ngazi za kuelekea juu kwenye ghorofa ya kwanza kilipokuwepo chumba chetu, hata hivyo akili yangu ilikuwa kwa yule mwanamume mwenye gazeti la Daily News.

Wakati nikizikwea ngazi za kuelekea juu nilitoa simu yangu na kuwasiliana na Daniella, nilimweleza kuhusu wasiwasi wangu juu ya mtu yule mwenye gazeti la Daily News na kumtaka ashughulike naye wakati nikielekea kule chumbani kuona kama kulikuwa na chochote cha kutiliwa shaka. Hata hivyo roho yangu ilikuwa imefarijika kidogo baada ya kupata taarifa kuwa Almasi, Sofia na Amanda walikuwa wazima.

Nilipoingia tu chumbani jicho langu la kijasusi lilizunguka haraka chumba chote na sikuchelewa kugundua kuwa kulikuwa na upekuzi wa siri uliofanyika. Hii ilimaanisha kuwa adui zetu walishajua makazi yetu, niliwaza.

Ili kuhakikisha kama kulikuwa na chochote kilichotegwa mle chumbani, kwa hatua za taratibu nilikipita kitanda cha Daniella na kisha kitanda changu, nikaenda mpaka usawa wa dirisha, na kwa kufanya vile wakati nakipita kijimeza kidogo kilichokuwa katikati ya vitanda, ambacho juu yake kulikuwa na taa ndogo kwa ajili ya kusomea, saa yangu ya mkononi ikaanza kunifinya na kutoa mlio fulani wa tahadhari.

Saa yangu ilikuwa imefungwa mfumo maalumu wa utambuzi wa TracerMark na hivyo kitendo kile cha saa kunifinya na kutoa mlio wa tahadhari kilimaanisha mambo hayakuwa salama ndani ya chumba kile.

Nikarudi hadi pale kwenye meza na kusimama kisha nikaiinua ile taa na kuichunguza kwa makini, na hapo nikagundua kuwa kulikuwa na kidubwasha kidogo sana kilichokuwa kimebandikwa pembeni, nilipokiona tu nikakitambua kuwa kilikuwa na kazi ya kunasa sauti na kutuma mahala fulani.

Nilikuwa mtaalamu mbobezi wa teknolojia ya habari na mawasiliano hivyo nilikitambua kifaa hicho kuwa kilikuwa na uwezo mdogo wa kurusha mawimbi hayo kwa umbali usiozidi mita 200 za mraba. Jambo hili lilimaanisha kuwa adui zetu hawakuwa mbali na eneo lile. Nilikwenda dirishani nikajaribu kuzungusha macho yangu nikijaribu kubaini ni nyumba ipi ingeweza kuwa kituo chao cha mawasiliano.

Japo nilikuwa makini lakini mwili wangu ulikuwa na uchovu mkubwa na kijiusingizi kilikuwa kikininyemelea kwa mbali, lakini mara kwa mara nilikuwa nikipambana na hali hiyo.

Uchovu wa mwili na akili ulizidi kunitesa tangu nilipoingia chumbani mle, nikatamani kuelekea bafuni ili nijimwagie kwanza maji. Zaidi ya yote njaa nayo ilizidi kunitesa. Nikiwa bado nimesimama pale dirishani mlango wa chumba changu ukagongwa.

“Nani?” niliuliza huku nikitoka pale dirishani lakini sikujibiwa, na badala yake mlango ukafunguliwa na kusukumwa kwa ndani.

Nilishtuka sana na kuruka nyuma ya mlango huku nikiupeleka mkono wangu kiunoni kuikwapua bastola yangu lakini nikasita baada ya kumwona yule msichana mhudumu wa mapokezi akiingia chumbani na kusimama huku akishangaa, maana hakujua nilikuwa wapi!

“Unasemaje?” nilimuuliza yule mhudumu huku nikiwa makini zaidi na nyendo zake.

“Kuna ujumbe wako nilipewa,” yule mhudumu alisema akinitazama kwa wasiwasi.

“Ulipewa saa ngapi?” nilimuuliza huku nikimkazia macho.

“Nilipoingia tu, ilikuwa kama saa moja na nusu,” yule mhudumu alisema huku akikunja sura yake katika namna ya kujaribu kuvuta kumbukumbu.

“Sasa kwa nini usingenipa nilipokuwa pale mapokezi hadi uulete huku chumbani? Na imekuwaje unaingia tu wala husubiri kufunguliwa mlango?” nilimuuliza huku nikihisi hasira ikinikaba kooni.

Yule mhudumu hakunijibu. Alinitazama na macho yake kama ya paka kisha akaifuata ile meza ndogo katikati ya vitanda na kuweka kikaratasi kilichokunjwa vizuri juu ya meza ile na kisha akaenda zake.

“Dah huyu mhudumu ana matatizo ya akili, si bure!” nililalama huku nikikifuata kile kikaratasi na kukiokota toka pale juu ya meza. Nilikitazama kwa umakini, kilikuwa kimeandikwa jina langu bandia nililoandikisha pale hotelini la Halfan Jongo, na namba ya chumba.

Nikapatwa na shauku ya kukifungua ili kujua ujumbe huo ulitoka wapi, na nilipokikunjua ili kukisoma nikakutana na ujumbe mfupi, “Tafadhali nitafute. Uwe peke yako…” Kisha chini yake kulikuwa na namba za simu na anwani ya eneo fulani lililopo ufukweni mwa bahari.

Nilitaka kumwita yule mhudumu nimuulize kuhusu huo ujumbe ila nikagundua kuwa alikwisha tokomea mbali na eneo lile. Nikafikiri kidogo kisha nikaitazama tena ile karatasi na kuzinakiri zile namba za simu na ile anwani akilini kwangu, halafu nikaichana ile karatasi na vipande vyake nikaenda kuvitia kwenye sinki la chooni na ku-flash maji.

Nilipomaliza nikatoka chumbani na kuufunga mlango halafu nikaelekea mapokezi. Nilipofika pale mapokezi niliyatembeza macho yangu taratibu kuchunguza kama kulikuwa na ongezeko la mtu mwingine eneo lile la mapokezi. Sikumwona mtu yeyote aliyeongezeka isipokuwa niligundua kuwa watu walipungua. Yule mwanamume aliyekuwa ameshika gazeti la Daily News hakuwepo.

“Nani kakupa ile karatasi?” nilimuuliza yule mhudumu kwa sauti ya chini huku nikigeuza tena shingo yangu na kuyatembeza macho yangu taratibu kuzichunguza zile sura zilizokuwepo eneo lile kuona kama kulikuwa na yeyote aliyefuatilia maongezi yetu. Sikumwona.

Wote walikuwa wanafuatilia kipindi kilichokuwa kikirushwa kwenye ile runinga pana iliyokuwa imetundikwa ukutani. Na hivyo nikayarudisha tena macho yangu kumtazama yule mfanyakazi wa hoteli.

Endelea...
 
utata.JPG

357

“Kuna dada mmoja alikuja hapa akaniomba nikupe ujumbe huo ukiwa peke yako na mtu mwingine yeyote asifahamu kama nimekupa ujumbe huo,” yule mfanyakazi wa mapokezi aliniambia. Uso wake haukuwa na tashwishwi yoyote.

“Yukoje?” nilimuuliza tena huku akili yangu ikihangaika kubashiri angeweza kuwa nani.

“Ni mrefu kiasi na mweupe kiasi, alikuwa amevaa suruali nyeusi ya jeans na blauzi nyeupe, usoni alivaa miwani mikubwa myeusi iliyofunika macho yake,” yule mfanyakazi wa mapokezi alimwelezea huyo dada.

Akili yangu ikaanza kusumbuka nikijiuliza angeweza kuwa nani! Nilijaribu kuwaza na mara nikajikuta nikimkumbuka Pamela Mkosamali. Nilihisi angeweza kuwa Pamela na kwa kuwa wanawake hawapendani ndiyo maana alinitaka niende nikaonane naye nikiwa peke yangu bila Daniella… hata hivyo, nililiondoa haraka wazo kuwa Pamela ndiye aliyeleta ule ujumbe kwa kujua kuwa sikuwa nimemjulisha kama nilifikia hoteli ile ya Naf Beach, achilia mbali jina bandia la Halfan Jongo.

Sasa, kama si Pamela, angeweza kuwa mwanamke gani aliyefahamu uwepo wangu pale Mtwara na kwenye hoteli ile? Na alitaka kukutana na mimi ili aniambie nini? Maswali mengi yalianza kupita haraka haraka akilini kwangu na kuzidi kunitatiza.

Nilimtazama tena yule mfanyakazi wa mapokezi na kushusha pumzi kisha nikamshukuru kwa ujumbe ule, halafu nikanyanyua mkono wangu kuitazama saa yangu ya mkononi na nilipojiridhisha na mwenendo wa majira yake nikapiga hatua kuelekea nje ya hoteli ile huku nikitoa simu yangu na kumtumia ujumbe mfupi Daniella kumuuliza alikuwa wapi!

Dakika iliyofuata ujumbe kutoka kwa Daniella ukaingia kwenye simu yangu, Daniella alinitaarifu kuwa alikuwa amemfuatilia yule mwanamume niliyekuwa nimemtilia shaka, na kwamba alikuwa anajiandaa kuingia kwenye nyumba fulani hivyo angenijulisha kile ambacho kingetukia huko. Nami nikamjulisha nilivyobaini kuwa upekuzi ulikuwa umefanywa kule chumbani na kifaa cha kunasa mawasiliano kilikuwa kimetegeshwa.

Baada ya hapo niliziandika kwenye simu yangu zile namba za simu nilizozikariri kichwani toka kwenye ile karatasi niliyoletewa na mfanyakazi wa mapokezi na kisha nikazipiga. Simu ikaita mara moja tu na kupokelewa. Na kabla sijasema chochote, sauti tamu ya kike ikaniuliza, “Jason Sizya?” Ilikuwa sauti nyororo ila ndani yake ilikuwa na msisitizo.

“Ndiyo, ni mimi… Wewe ni nani?” niliitikia huku nikiuliza kwa wasiwasi, maana sikujua ni mwanamke gani aliyenitambua kwa jina langu halisi.

“Fanya hima ufike eneo uliloelekezwa kwenye ujumbe,” sauti ile ilinikatisha na kabla sijasema neno simu ikakatwa. Hapo nikabakia na maswali. Ni mwanamke gani huyu mwenye kuniamuru kiasi hiki?

Nilitaka kumpigia tena simu lakini nikasita na kuirudisha simu yangu mfukoni huku nikiwaza. Nafsini mwangu sikutaka kwenda huko. Lakini pia nilijiuliza kwa nini nisiende? Upande mmoja wa nafsi yangu uliniambia kuwa huo ulikuwa mtego lakini upande mwingine uliniambia ningebainishaje kuwa ni mtego au si mtego pasipo kwenda?

Hata hivyo swali kuu lililonijia akilini mwangu ni kuwa; mwanamke yule alikuwa nani na alijuaje kuwa mimi ni Jason Sizya na nilikuwepo katika hoteli ile ya Naf Beach nikitumia jina bandia la Halfan Jongo?

Wakati nikiwa bado nipo njia panda nikitafakari iwapo niende au nisiende mara ujumbe mfupi ukaingia kwenye simu yangu, ujumbe huo ulisomeka; “Nina jambo muhimu la kukwambia kuhusu Rais Masinde!” Nilipotazama vizuri namba ya simu iliyonitumia ujumbe huo nikagundua kuwa ilikuwa ni ile ile niliyotoka kuwasiliana nayo muda mfupi uliokuwa umepita.

Sikutaka kuendelea kujiuliza maswali, nilichoamua ni kwenda huko nilikoitwa na kama ulikuwa ni mtego ningejua huko huko. Nikaanza kutafuta usafiri wa kunifikisha huko na baada ya dakika kama tatu hivi nilikuwa ndani ya teksi nikielekea huko kulikoelekezwa kwenye anwani. Kimahesabu sehemu hiyo haikuwa mbali sana toka pale hotelini, ni kama kilomita moja na nusu hivi toka pale Naf Beach Hotel.

Nikiwa barabarani, akili yangu ilianza kusumbuka kuhusu usalama wangu na hapo nikajikuta nikipata msukumo wa kutaka kumshirikisha Daniella kuhusu jambo hilo. Nikatoa simu yangu na kuandika ujumbe kumtaarifu aje kwenye eneo kama ilivyoelekezwa kwenye ile karatasi na sababu. Daniella alinijibu kuwa angefika eneo lile mara baada ya kumalizana na watu aliowafuatilia.

Japokuwa ujumbe niliopatiwa ulinitaka niende peke yangu lakini nilifanya kumjulisha Daniella kwa sababu ya usalama wangu na uzito wa jambo tulilokuwa tukilifuatilia pale Mtwara. Endapo basi ingelitokea tatizo lolote lile kwangu, uwepo wa mtu ambaye angeweza kutoa taarifa nyuma yangu lilikuwa jambo muhimu.

Sikuwa mwoga wa kifo hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa kifo ni ada ya kila binadamu. Lakini sikuwa tayari kufa kabla ya kupata majibu ya fumbo lile lenye utata. Sikuwa tayari kufa kabla ya kutekeleza jukumu langu muhimu ambalo lilihusiana na kutimiza wajibu wangu kwa taifa langu kama nilivyoapa baada ya mafunzo yangu ya ujasusi… Ni baada ya hapo tu ndipo ningekuwa radhi kumwachia adui roho yangu!

Dakika kadhaa baadaye nilikuwa nimefika eneo nililohitaji kufika na kuteremka toka kwenye teksi huku nikiyazungusha macho yangu, na hapo nikagundua kuwa eneo lile lilikuwa la ufukweni mwa Bahari ya Hindi na lilijengwa nyumba za kisasa zilizozingatia ujenzi wa anwani za makazi.

Kisha macho yangu yalitazama moja kwa moja kwenye nyumba husika ambayo niliitambua mara moja kutokana na namba iliyoandikwa kwenye geti. Ilikuwa ni nyumba kubwa nzuri iliyozungushiwa uzio wa ukuta mrefu usiomruhusu mtu kuona ndani na geti jekundu mbele yake ingawa geti hilo lilionekana kuchakaa kidogo. Pia nyumba ilikuwa imezungukwa na miti mizuri ya kivuli.

Kabla sijaelekea kwenye nyumba ile, niliyazungusha macho yangu kulikagua eneo lote kwa macho ya wepesi. Katika nyakati zile za usiku wa kuelekea saa nne hakukuwa na watu barabarani wala waliokuwa nje ya nyumba, hali ilikuwa ya utulivu mno. Tulivu uliotisha kidogo.

Nilipojiridhisha na usalama wangu, nikapiga hatua kuelekea kwenye geti la mbele na kubonyeza kitufe cha kengele huku nikitazama nyuma yangu ng’ambo ya ile barabara kama kulikuwa na mtu yeyote aliyekuwa akifuatilia nyendo zangu.

Baada ya kubonyeza kitufe cha kengele kwenye geti lile mara kadhaa bila kujibiwa sikuona sababu ya kuendelea kubonyeza kengele ile kwa kuhisi kuwa nilikuwa nikipoteza muda wangu hivyo nikawa njia panda nikitakafari iwapo niondoke zangu au nitumie njia nilizozijua kuingia mle ndani.

Kilichonisukuma kutaka kuingia mle ndani ni suala la kutaka kujua sababu iliyomfanya aliyeniletea ujumbe kuitaja nyumba ile. Niliamini kuwa ndani ya ile nyumba kulikuwa na majibu ya fumbo tata lililotuleta Mtwara. Nikiwa bado sijaamua kipi cha kufanya mara nikahisi kusikia sauti ya hatua za mtu akilikaribia geti lile kwa ndani, nikaupeleka mkono wangu kiunoni na kujiandaa kukabiliana na tukio lolote la kushtukiza ambalo lingejaribu kuhatarisha usalama wangu.

Endelea...
 
utata.JPG

358

Mara nikasikia kitasa cha mlango mdogo uliokuwa pembeni ya lile geti kubwa jekundu kikizungushwa kisha muda huo huo mlango ule ulifunguliwa, na hapo mwanadada mmoja mrefu kiasi mwenye wajihi kama nilivyoelezwa na yule mhudumu wa mapokezi pale Naf Beach Hotel akajitokeza. Uso wake ulikuwa wa duara na ulipambwa na tabasamu.

Nikajikuta nikishikwa na butwaa baada ya kumwona msichana mzuri akiwa amesimama hatua moja mbele yangu huku amevaa kaptura fupi sana ya bluu ya kitambaa cha dengrizi iliyoyaacha wazi mapaja yake yaliyonona na blauzi nyepesi nyeupe iliyoshindwa kukificha kifua chake chenye matiti ya ukubwa wa wastani yenye chuchu nyeusi zilizosimama kama mkuki wa Kimasai na kishimo kidogo cha kitovu kwenye tumbo lake dogo.

Msichana yule alikuwa na nywele zake ndefu alikuwa amezibana kwa nyuma, shingoni alining’iniza kidani cha kifuu kilichochongwa katika umbo la ramani ya Afrika, na miguuni alivaa makobazi ya ngozi ya kike yenye mikanda.

Yule mwanadada aliyazungusha kwanza macho yake katika namna ya kulikagua eneo lote kisha akanitazama usoni na kuuliza, “Jason Sizya?”

“Ndiyo, ni mimi,” nilimjibu huku nikimtazama kwa umakini usoni.

“Karibu ndani,” yule mwanadada alisema huku akinipisha.

Kabla ya kuingia ndani niligeuka kutazama tena nyuma yangu nilipojiridhisha kuwa hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akinifuatilia nikaingia ndani huku taratibu nikiurudishia vizuri ule mlango nyuma yangu. Mara tu nilipoingia mle ndani nikajikuta nimetokea kwenye uzio mpana wa ile nyumba. Nilisimama nikachunguza vizuri mazingira ya eneo la nyumba ile.

Yalikuwa mandhari ya kupendeza na ile nyumba ilikuwa kubwa ya kisasa yenye madirisha makubwa ya vioo na baraza kubwa mbele yake. Upande wa kushoto kulikuwa na banda la wazi la kuegeshea magari na kulikuwa na gari moja tu aina ya Toyota Lexus RX la rangi nyeupe. Ndani ya uzio huo kulikuwa na miti mitatu mikubwa, miti miwili ilikuwa mbele ya nyumba na mti mwingine ulikuwa ubavuni mwa nyumba ile, upande wa kushoto.

Kisha yule mwanadada aliniongoza kuelekea ndani. Hata hivyo bado nilikuwa na mshangao mkubwa nikijiuliza ni aina gani ya mwanamke anayeweza kumfungulia mlango mgeni asiyemjua huku akiwa amevaa kivazi cha aina ile?

Yule msichana alikuwa akitembea taratibu bila wasiwasi wowote, nilimfuata nyuma huku nikiyatazama mapaja yake yaliyonona na makalio yake makubwa kiasi ambayo yalitetema wakati akitembea hali iliyoyafanya mapigo ya moyo wangu yaanze kwenda mbio. Nilipiga moyo konde na kuzifukuza hisia mbaya zilizoanza kujengeka kichwani mwangu.

Nikiwa naendelea kumtazama kwa nyuma nilizitupa hatua zangu taratibu na kwa tahadhari nikimfuata msichana yule mbele yangu na tulipofika kwenye mlango mkubwa wa kuingilia ndani nikapiga piga miguu yangu kwenye zulia dogo lililokuwa pale nje mlangoni ili kukung’uta vumbi kwenye viatu vyangu kisha nikaingia ndani pasipo kuvivua nikimfuata yule mwanadada.

Nilipoingia mle ndani nikagundua kuwa pale ilikuwa ni sehemu ya jikoni, tukasonga mbele na kuuvuka ukumbi wa kulia chakula wa nyumba ile uliokuwa upande wa kulia halafu tukaifuata korido fupi mbele yetu. Katikati ya korido ile upande wa kushoto kulikuwa na mlango, tulipoingia ndani ya mlango ule tukawa tumetokezea kwenye sebule pana.

Ilikuwa sebule ya kisasa yenye samani za kuvutia kama makochi makubwa mazuri ya sofa, sakafu nzuri, runinga ya kisasa, redio kubwa ya kisasa, jokofu kubwa la vinywaji lililokuwa kwenye kona ukutani pamoja na kabati pana la vyombo vilivyopangwa kwa unadhifu mkubwa.

Madirisha mapana ya sebule ile yalikuwa yamefunikwa kwa mapazia mepesi na hivyo kufanya upepo murua wa baharini upenye kwa urahisi na kutuama pale sebuleni. Nikajikuta nikitulia kidogo huku nikiyatembeza macho yangu kuitazama ile sebule kubwa yenye samani zote muhimu na za kisasa.

Yule mwanadada aliniangalia kwa umakini kisha akaniashiria niketi kwenye sofa. “Karibu uketi, Jason,” alisema.

“Ahsante,” nilimjibu huku nikichagua kochi moja na kuketi.

“Samahani naomba usubiri kidogo,” yule msichana aliniambia na kabla hata sijamjibu akaondoka na kuufuata mlango mmoja wa kioo, akaufungua na kuingia akipotelea huko ndani.

Wakati akiondoka nilibaki nikimsindikiza kwa macho na hapo nikaziona tena sehemu zake za nyuma zilivyotikisika taratibu kwa kadiri alivyokuwa akizitupa hatua zake kutembea. Na alipopotea machoni kwangu nikayarudisha mawazo na akili yangu ndani ya sebule ile na wakati huo niliweza kuzisikia hatua za msichana yule zilivyokuwa zikiyoyoma.

Nilibaki nikiwa mtulivu huku nikijiuliza sababu ya wito ule kutoka kwa msichana ambaye sikuwa na kumbukumbu kama nilishawahi kumwona mahali popote, hata hivyo, hiyo haikunizuia kufanya udadisi pale sebuleni huku nikiendelea kumsubiri mwenyeji wangu. Nilipanga kuwa ningetumia muda wa nusu saa tu kuongea na mwenyeji wangu na baada ya hapo ningeondoka kurudi kule hotelini ili nikajimwagie maji na kutafuta chakula, maana njaa ilizidi kunitesa.

Nilipoitazama saa yangu ya mkononi nikagundua kuwa ilikuwa imeshatimia saa tatu na dakika arobaini na tano, dakika kumi na tano tangu nilipowasiliana na Daniella na kumtaka aje katika nyumba hiyo, nikashangaa kuwa hadi muda huo hakuwa amewasiliana nami kunieleza kama angekuja au nini kilikuwa kikiendelea huko alikokuwa.

Sikukaa kizembe, nilianza kuyatembeza macho yangu mle ndani kuyatazama mandhari ya ile sebule kwa jicho la kishushushu. Wakati nikiendelea na uchunguzi ule mara nikawa nimekiona kitu kimoja kilichonishtua na kunigusa zaidi moyoni.

Pembeni ya kabati la vyombo, jirani na ule mlango alioingia yule msichana kulikuwa na jozi moja ya viatu vya kiume. Nilivitazama viatu vile toka pale nilipoketi na kuhakikisha kuwa vilikuwa vya mwanamume hali iliyomaanisha kuwa mle ndani hakuwa yule msichana peke yake ila kulikuwa na mwanaume aliyekuwa anaishi na msichana yule.

Kisha nikaendelea kuyatembeza macho yangu kuchunguza iwapo kulikuwa na kamera yoyote ya ulinzi, nikaziona kamera mbili za kificho zilizofungwa kwa namna ambayo kama si mtaalamu wa teknolojia basi huwezi kutambua, kamera moja ilikuwa mfano wa balbu ya umeme ikiwa imetundikwa sehemu fulani kwenye ile dari na nyingine ilikuwa mfano wa swichi ya umeme iliyowekwa ukutani.

Na hapo nikagundua kuwa kamera zile zilikuwa zinachukua picha pale sebuleni na kutuma taarifa kwenye chumba fulani, na kwamba kila nilichokuwa nakifanya pale sebuleni kilikuwa kinaonekana na yule mwenyeji wangu.

Hali hiyo ikanifanya nizidi kuchukua tahadhari huku nikianza tena kuwaza kuhusu wito ule. Je, yule msichana ni nani na alikuwa na habari gani kuhusu Rais Masinde? Nilijiuliza.

Nikiwa bado natafakari mara nikasikia sauti ya hatua za mtu, Hapana… hatua za watu, zikisogea, nikageuka kutazama upande ule na hapo nikauona ule mlango ukifunguka kisha mwanamume mmoja mrefu aliyevaa shati zuri la kitenge lililodariziwa vizuri shingoni kwa nyuzi za dhahabu na suruali nyeusi ya kodrai, miguuni akiwa amevaa makobazi ya ngozi na machoni amevaa miwani ya kumsaidia kuona huku bakora yake ya heshima ikiwa mkononi, akajitokeza.

Endelea...
 
utata.JPG

359

Alikuwa mtu mzima aliyepta miaka sitini na ushee kama si sabini, mwenye nywele fupi zilizoanza kujaa mvi na ndevu nyingi zenye mvi zilizokizunguka kidevu chake, na nyuma yake alifuatwa na yule msichana aliyenipokea, safari hii akiwa amejifunga kanga. Nilimtazama yule mzee huku moyo wangu ukipiga kite kwa nguvu maana sikutegemea jambo hilo.

Wakapiga hatua kikakamavu kuja pale kwenye sofa nilipokuwa nimeketi. Nilichofanya ni kutulia tu kama ambaye sikuwa na wasiwasi wowote huku nikiwatazama kwa umakini.

“Samahani sana, Jason, kwa kukuweka,” yule mzee aliniambia pindi alipokuwa akiketi jirani na lile sofa nililoketi, na wakati huo yule msichana akibaki wima. Wote walikuwa wakinitazama kwa umakini.

“Naitwa Othman Mwambe,” yule mzee alijitambulisha kwangu huku akinipatia mkono. Kisha akaelekeza kidole chake cha shahada kwa yule msichana aliyenipokea. “Huyu ni binti yangu, mtoto wangu wa mwisho kati ya watoto wawili, yeye anaitwa Rahma Mwambe… Luteni Mwambe.”

“Nashukuru kuwafahamu. Nimeitikia wito wenu,” nilisema huku nikiwatazama usoni kwa zamu nikijaribu kuyasoma mawazo yao kuona kama walikuwa watu mwema au la.

Kabla hajaongea alichoniitia aliyapeleka macho yake kutazama dirishani huku masikio yake yakisimama kama aliyekuwa akisikilizia sauti kisha akaniuliza, “Una uhakika umekuja peke yako?”

“Ndiyo…” nilimjibu kwa kujiamini.

“Unapaswa kuwa mkweli kwenye hili maana hapa unatakiwa kuja mwenyewe. Ni wewe pekee ninayekuamini kwa sasa kwa kuwa nimekuwa nikivutiwa na harakati zako,” yule mzee alisema huku akinitazama kwa umakini sana kana kwamba alikuwa mwalimu wa usafi aliyekuwa akimkagua mwanafunzi. “Sitaki mtu yeyote aanze kunifuata fuata. Nina familia inanihitaji, na maisha yangu napenda yakiwa yangu binafsi.”

Nilimtazama kwa umakini kisha nikamuuliza, “Ulijuaje kuwa nilikuwa nimefikia Naf Beach Hotel na ninatumia jina bandia la Halfan Jongo?”

“Nimekuwa kwenye idara ya ujasusi kwa miaka arobaini…” yule mzee alinijibu kwa kujiamini kisha akaendelea, “…sikia, unaweza ukawa hunijui kwa kuwa huna muda mrefu kwenye Idara ya Usalama wa Taifa, ila mimi ni mtu ambaye nimetumikia taifa hili kwa miongo minne katika nafasi mbalimbali hadi kuwa Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, na nime-recruit maofisa wengi wa kijasusi wakiwemo mkurugenzi mkuu wa TISS, David Mshana na mkuu wako wa kikosi, Kanali Othman Mjaka… lakini huenda hayo yasiwe muhimu sana kwako bali lililo kuu ni kwamba mimi ni swahiba mkuu wa Rais, Dk. Albert Masinde, ambaye wewe unamtafuta.”

Nilimtazama yule mzee kwa namna ambayo ilikosa tafsiri sahihi. Nilihisi kusikia habari zake sehemu ingawa sikuwahi kufikiria kama siku moja ningekutana naye. Hata hivyo sikusema neno, nilibaki kimya nikimtumbulia macho mzee yule.

By the way, nilisahau kukuuliza… sijui utatumia kinywaji gani?” yule mzee aliniuliza huku akinikazia macho.

“Juisi ya aina yoyote itanifaa zaidi,” nilimwamba yule mzee maana nilihisi ingesaidia kupungua njaa niliyokuwa nayo. Na hapo yule mzee akageuka kumtazama Rahma na kumpa ishara.

Rahma akaliendea lile jokofu lililokuwa kwenye pembe ya sebule na kulifungua, akatoa jagi kubwa lililojaa sharubati ya mchanganyiko wa embe na pasheni na kurudi akiwa na bilauri mbili kubwa ambazo aliziweka mezani na kumimina sharubati kwenye zile bilauri, bilauri moja akampatia baba yake na nyingine akanipa.

“Karibu sana,” Rahma alisema.

“Ahsante,” nilimshukuru kisha nikapiga mafunda mawili ya nguvu na kuiweka bilauri ile mezani na hapo tukabaki tukitazamana kwa kitambo kifupi kabla yule mzee hajavunja ukimya.

“Sasa nafikiri tunaweza kuongea… kama nilivyokwambia mimi ni swahiba mkubwa wa Rais Masinde, sasa kinachoniuma mno ni kwamba nahisi nahusika na utekwaji wa Rais, maana kama ningelichukua hatua mapema huenda haya yasingetokea… Najuta sana kwa hilo,” yule mzee alisema kwa uchungu kisha akanyamaza kidogo.

Nilimtupia jicho Rahma kisha nikayarudisha macho yangu kumtazama yule mzee, bado sikuongea. Niliendelea kumpa nafasi yule mzee aendelee kujieleza pasipo kuingilia, maana ni yeye aliyeniita pale kunieleza jambo.

“Wiki mbili kabla ya Rais hajaanza ziara ya kuja huku Mtwara ofisa mmoja wa Secret Service anayeitwa William Shamte alinifuata katika hoteli niliyofikia siku nilipokwenda Dodoma. Siku hiyo ilikuwa nionane na Rais lakini alikuwa ametingwa sana na majukumu. Shamte aliniachia ujumbe kwenye katarasi na kuondoka mara moja,” yule mzee alisema huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa kipande kidogo cha karatasi ngumu nyeupe, akanikabidhi.

Niliusoma ujumbe ule ambao uliandikwa kwa kalamu ya wino mwekundu; ‘Kuna tishio kiotani, tafadhali msaidie ndege wetu’ ambao ulimaanisha kuwa kumwomba mzee huyo amsaidie Rais kwani alikuwa yupo kwenye matatizo.

Nilishusha pumzi na kuinua uso wangu kumtazama mzee Mwambe, yeye akaendelea kuongea. “Namna kijana huyo alivyonipata na kunifikishia ujumbe ule ilinifanya nishindwe kumuuliza Rais nilipokutana naye kesho yake, ingawa nilitamani sana kumuuliza ili kujua alikuwa na shida gani. Kama unavyojua, alikuwa na walinzi wake na pia si rahisi kuwasiliana na Rais, mara nyingi ilikuwa hadi yeye anitafute, na mara ya mwisho kuongea naye ilikuwa ni juzi jioni alipofika hapa Mtwara kuanza ziara yake ya siku tatu. Alikuja hapa kunisalimia. Na baadaye jioni ofisa yule yule wa Secret Service, akaja kwa siri na kunifikishia ujumbe mwingine.”

Mzee Mwambe aliweka kituo halafu akatoa tena karatasi nyingine toka kwenye mfuko. Karatasi ile ilikuwa na ujumbe ambao alikuwa ameuandika mwenyewe kwa mwandiko wake akinakiri taarifa alizopewa na Shamte.

‘Sasa kiota kinawaka moto, ndege tunduni yupo hatarini, ni wewe pekee anayeweza kukuamini, tafadhali msaidie dhidi ya Tiger na Chameleon...” ujumbe ulisomeka hivyo.

Tafsiri yake ilikuwa ni ile ile ya kumwomba mzee Othman Mwambe kumsaidia Rais kwani sasa alikuwa hatarini zaidi dhidi ya watu waliojiita Tiger na Chameleon.

“Nilipomuuliza Tiger na Chameleon ni akina nani, akaniambia anamfahamu Chameleon kuwa ni mkuu wa kikosi cha siri cha ulinzi wa Rais (Secret Service), Yusuf Assad Taifa, lakini hamfahamu Tiger ila aliamini kuwa ana nafasi ya juu ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)…” yule mzee alisema, kisha akaongeza.

“Aliamini kuwa kama si mkuu wa majeshi, Jenerali Adam Kalembo basi ni Mnadhimu wa Jeshi, Luteni Jenerali Gozbert Bundala, ambaye kabla hajapanda cheo na kufikia nafasi hiyo alikuwa Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, nafasi ambayo mimi nilimwachia baada ya kustaafu.”

Kisha yule mzee aliniambia kuwa usiku wa siku iliyofuata baada ya kuletewa ule ujumbe na Shamte yakatokea yaliyotokea huku ofisa huyo aliyemletea ujumbe ule akiuawa.

“Dah!” ndiyo neno pekee nililomudu kulitamka kwa wakati huo. Kisha niliinyakua bilauri ya sharubati pale mezani na kuvuta funda moja kubwa lililosababisha sharubati yote iishe kwenye bilauri kisha nikairudisha mezani huku nikimtazama Rahma.

Endelea...
 
utata.JPG

360

Kitendo cha kumtazama kilimfanya Rahma asogee pale mezani, akanyanyua jagi la sharubati na kumimina tena sharubati akiijaza bilauri yangu. Mzee Mwambe akaendelea kuongea.

“Sasa, kwa hali hii sitaki kabisa kuharibu maisha yangu endapo itagundulika kuwa nafahamu kwa kiasi kuhusu sakata hili. Hata wewe nimekutafuta kwa sababu nimefuatilia operesheni zako mbili, ile uliyofanya kule Mombasa na nyingine iliyohusiana na mauaji ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Ummi Mrutu, na hivyo nimejikuta nikikuamini sana… naomba msaidie mheshimiwa Rais, kwa vyovyote anahitaji msaada huko aliko!”

“Unajua ni wapi anaweza kuwa amepelekwa?” nilimuuliza yule mzee huku nikimtazama kwa umakini usoni.

“Sijui! Ndiyo maana nikafanya utaratibu wa kukutafuta nikiamini kuwa taarifa zangu zitakusaidia kumpata…” yule mzee alisema kisha akaongeza, “pia tambua kuwa mimi na wewe hatujawahi kuonana wala kuzungumza chochote, hii ni kwa usalama wangu na wa familia yangu. Ukishaondoa mguu wako humu ndani sahau kama tulishawahi kuonana.”

“Vipi kama nikihitaji taarifa nyingine toka kwako?” nilimuuliza yule mzee.

“Sina taarifa zaidi ya hizo… ila ikitokea nikizipata basi nitakutafuta kwa njia ile ile kama nilivyofanya leo,” aliniambia kisha akainuka na kunipa mkono wa kuagana.

Nami nikainuka, tukapeana mikono halafu nikanyanyua bilauri yangu ya sharubati na kuinywa sharubati yote kisha nikairudisha ile bilauri juu ya meza na kutoka nikisindikizwa na Rahma hadi getini, na tulipofika getini Rahma alifungua geti dogo na kuchungulia nje kuhakikisha usalama kisha tukapeana mikono kuagana.

Nilitoka nje ya nyumba ile huku nikiliacha geti la ile nyumba likifungwa nyuma yangu, kisha nilitembea nikiifuata barabara ya mtaa ule huku macho yangu yakiwa makini kutazama huku na huko.

Kichwani nilikuwa nimepanga kwenda kutafuta taarifa za watu wawili; Mkuu wa Majeshi Jenerali Adam Kalembo na Mnadhimu wa Jeshi, Luteni Jenerali Gozbert Bundala. Nilikuwa natafakari namna ya kuzifanyia kazi zile taarifa nilizopewa na mzee Othman Mwambe, mara simu yangu ikaanza kuita, nilipotazama nikaliona jina la Daniella, alikuwa akinipigia.

Nilipokea na kumwelekeza mahali nilipokuwa. Na ndani ya dakika mbili akawa amefika katika eneo lile, nikapanda garini na hapo safari ikaanza huku nikiwa makini kuchunguza endapo kulikuwa na gari lililotufungia mkia nyuma yetu. Hata hivyo sikuona gari lolote la kulitilia mashaka. Sasa nikaanza kumweleza Daniella yote niliyoyapata kwa mzee Othman Mwambe.

Daniella alishusha pumzi na kuniambia kuwa alimfahamu mzee Othman Mwambe kwa kuwa alikuwa mkuu wake wakati akiongoza Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania japokuwa hawakuwa na ukaribu. Kisha alianza kunieleza kile kilichotokea kwenye harakati zake za kumfuatilia yule mtu niliyemtilia shaka kule hotelini.

Daniella aliniambia kuwa yule mtu alikuwa na mwenzake na hivyo aliwafuatilia na kuwaona wakiufuata Mtaa wa Duara kuelekea nyuma ya hoteli ile ya Naf, kisha waliingia kwenye nyumba moja iliyokuwa nyuma ya hoteli ile ya Naf. Walikuwa wanatembea kwa mguu na hivyo alipofika usawa wa ile nyumba waliyoingia wale watu yeye alipitiliza akiipita ile nyumba kama aliyekuwa anakwenda kutokea Barabara ya Njombe, wakati huo alikuwa akijipa utulivu katika akili yake.

Baada ya kuipita nyumba ile akakunja kushoto kama aliyekuwa akielekea katika Hoteli ya Victoria na kuiacha nyumba ile ikiwa nyuma yake, lakini hakuingia hotelini akageuza na kuanza kuambaa ambaa na vivuli vya miti iliyopandwa kando ya barabara kisha kwa wepesi usioufikiria akadandia ukuta wa nyumba moja ya jirani na kudondokea ndani ya uzio wa nyumba hiyo bila kutoa kishindo.

Halikuwa lengo lake kuingia kwenye nyumba ile ila aliingia pale maana ukuta wa nyumba zile ulikuwa umeungana, kwa hiyo ili aingie katika nyumba aliyoikusudia ilimbidi apitie ukuta ule, na ndivyo alivyofanya.

Akiwa ndani ya uzio wa nyumba ile mara ujumbe mfupi wa maandishi ukaingia kwenye simu yake na alipoutazama akagundua ulikuwa unatoka kwangu, akatulia kidogo na kuusoma halafu akaujibu. Ulikuwa ni ule ujumbe wa kumtaka anifuate kule nyumbani kwa mzee Othman Mwambe.

Aliujibu ujumbe ule kisha ukaingia ujumbe mwingine ambao pia aliujibu na kuizima simu yake. Kisha alitazama kushoto na kulia, hakuona wenyeji wa nyumba ile hapo akapiga hatua kadhaa na kuutathimini ukuta ule akauparamia na kudondokea kwenye uzio mpana wa nyumba aliyoikusudia ila hakujua kama kulikuwa na macho ya mtu yalikuwa yakitazama kila hatua aliyopiga.

Kumbe mmoja wa wale watu wawili waliofika hapo alikuwa amejificha sehemu akizifuatilia harakati za Daniella akiwa hatua kadhaa kutoka eneo husika kwa ajili ya kuhakikisha nyumba inakuwa salama.

Alikuwa ametulia mahali akamwona Daniella wakati akitafuta namna kuingia mle ndani na kumtilia shaka kulingana na utembeaji wake, ilikuwa ni rahisi kwake kutilia shaka nyendo kwa sababu hakuwa mgeni na watu wa aina hiyo, na hivyo Daniella aliporuka ukuta macho ya mtu yule hayakumwacha, na hapo kwa haraka aliwahi ndani kwenda kuwajulisha wenzake wawili waliokuwa ndani habari za kuvamiwa, kisha wakajipanga kumpokea mgeni wao.

Baada ya Daniella kuingia ndani ya uzio wa nyumba ile alianza kunyata haraka na kukifikia kichaka kilichotengenezwa na maua yaliyopandwa kwenye mandhari ya nyumba ile, hapo akatulia kidogo na kutazama mlango wa kuingilia ndani ya nyumba ile.

Hali ilikuwa ya ukimya uliopitiliza kana kwamba hakukuwa na mtu mle ndani ilimfaya ajipa tahadhari kuwa tayari watu wake walishajua kuwa wamepata mgeni, akanyata tena kwa kutumia vidole vya miguu yake na kuikaribia baraza ya nyumba ile, akajipa tena utulivu akatazama mlangoni akauona upo nusu wazi lakini taa za ndani zikiwa zimezimwa, akajua ulikuwa mtego, naye akapanga kuutegua.

Alipotazama kando akakiona kigogo kidogo kilichokuwa pembeni ya maua akakifuata na kukishika vizuri kisha akachomoa bastola yake iliyofungwa kuwambo cha kuzuia sauti na kuilenga taa kubwa iliyokuwa inatoa mwangaza pale nje, halafu akatulia.

Sasa eneo lile lilibaki giza. Daniella akasogea hadi jirani na mlango kisha akakirusha kile kigogo kwenda mlangoni, punde ukasikika mshindo mkubwa wakati kile kigogo kikitua mle ndani halafu zikasikika sauti za risasi zilizovurumishwa kutokea ndani.

Risasi zilipokoma tu na taa za ndani kuwashwa Daniella akateleza na kama nyoka na kudondokea ndani kwenye sebule pana huku watu watatu wakiwa wamesimama na bastola mkononi wakiwa wanashangaa kuona gogo la mti limelala mbele yao. Kabla hawajajua nini kinatokea watu wawili wakajikuta wakidondoka chini kama magunia huku uhai ukiwa unawatoroka.

Mwanamume mmoja, yule aliyekuwa pale mapokezi ya Naf Beach Hotel akiwa ameshika gazeti la Daily News alikuwa ameushtukia mchezo muda mrefu wakati Daniella alipoteleza kuingia ndani kwa kasi, yeye hakuwa mjinga na hivyo aliruka pembeni haraka na kuwashuhudia wenzie wakidondoka chini. Na alipotaka kunyanyuka afanye shambulizi kwa adui yake alikutana na mtutu wa bunduki ukimtazama.

Endelea...
 
utata.JPG

361

Daniella akiwa amekunja sura yake alimwamuru yule mwanamume atupe mbele silaha yake chini, naye akatii huku akiamini kuwa hakuwa na ujanja kwani alikuwa kapatikana. Lakini alishangaa kumwona Daniella akiisogelea ile bastola na kuipiga teke, ikaenda mbali kisha yeye akairudisha bastola yake kiunoni.

Yule mwanamume akaona kama aliyedharauliwa na mwanamke. Akainuka na kukunja ngumi akisimama sawia kwa ajili ya mpambano.

Daniella alimtazama mwanaume yule kwa macho ya kina. Akamkagua kuanzia juu mpaka chini kisha akasema na moyo wake kuwa, laiti angejua yeye ni nani asingefanya ujinga kama ule, ujinga ambao ulikuwa unakwenda kumgharimu. Akakunja ngumi, akatanua miguu kupata balansi. Basi haraka yule mwanamume akamvamia Daniella. Akarusha ngumi tano kwa wepesi mno na kwa hasira! Zote zikakata upepo.

Kinyume na mwonekano wa mwili wake ulivyokuwa mkubwa, yule mwanamume alikuwa mwepesi kwenye kufanya maamuzi na kujifyatua. Alikuwa ana haja ya kummaliza Daniella kuliko Daniella alivyokuwa na haja ya kummaliza yeye. Alikuwa anatumia nguvu nyingi kushambulia lakini alikuwa mdhaifu kwenye kujikinga. Daniella alilitambua hilo. Lakini bado hakuwa na haja ya kummaliza yule mwanamume. Hakudhani kama mwanaume huyo alistahili kufa kwa haraka… Hakustahili kabisa!

Daniella aliamini kuwa mwanaume huyo alipaswa kufa baada ya kuutapika ukweli wote alioujua. Tena baada ya kupata mateso makali ambayo yangemfanya mwenyewe akitamani kifo akikiona ndiyo ahueni yake.

Shit!” yule mwanamume alilaani baada ya kuona kila pigo alilopiga liliambulia patupu. Alikuwa amepiga ngumi nyingi mno zisizo na idadi pasipo kufanikiwa hata moja! Na wala Daniella hakuwa akimshambulia.

Yule mwanamume alibadilisha mtindo, akawa anamshambulia Daniella kwa mateke zaidi na ngumi za kushtukiza. Kidogo akafanikiwa kumtwanga Daniella ngumi moja ya kifuani iliyomfanya apepesuke.

Sasa akawa ameamsha wazimu wa mbwa maana Daniella alianza kumshambulia mwanamume yule mithili ya nyuki waliotibuliwa kwenye mzinga wao. Yule mwanamume alikuwa na kazi ya kupangua ngumi na mateke yaliyomjia kwa kasi ya ajabu. Yule mwanamume alikuwa mwepesi lakini Daniella alikuwa mithili ya umeme. Alikuwa anatambua nyendo za mwanamume yule kabla hajaamua hata kuzitekeleza.

Yule mwanamume alimtazama Daniella kwa ghadhabu kisha akajikakamua kunyanyuka aendelee na pambano. Akataka kufanya shambulizi la kushtukiza lakini kabla hajafanya shambulizi lolote, akastaajabu Daniella amemfyeka miguu yake na yupo hewani kimo cha ndama. Na kabla hajatua chini akashindiliwa teke la tumbo lililombwaga sakafuni kama gunia na kumfanya acheue chakula alichokula!

Yule mwanamume aliinua uso wake kumtazama Daniella kwa mshangao mkubwa akiwa haamini kama mwanamke mrembo kama yule alikuwa akimwadhibu kama mtoto mdogo, kisha akacheka mwenyewe akiwa pale chini, si kama alicheka kwa dharau bali alicheka kwa sababu hakupata kumwona mtu, tena mwanamke mrembo, akifanya mashambulizi kwa wepesi wa kiasi kile, na kwa ufanisi mkubwa!

Jambo ambalo huenda yule mwanamume hakulijua ni kuwa, licha ya kuwa Daniella alikuwa mwanamke mrembo lakini hakuwa mtu wa kawaida. Alikuwa ni komando na jasusi mwenye mbinu za hali ya juu, aliyefuzu katika kila idara.

“Umeshinda, dada, nakubali umenipiga… sasa nipo tayari kutekeleza lolote utakaloniamuru,” yule mwanamume alisema kwa Kiswahili chenye lafudhi iliyomtambulisha kuwa hakuwa Mtanzania. Alisema huku akijikongoja kunyanyuka kwa tabu pale sakafuni.

Daniella alimtazama yule mwanamume bila kusema neno. Alikuwa makini na kila hatua aliyopita yule mwanamume akiamini kuwa huo ulikuwa mtego tu, maana yule mwanamume asingeweza kusalimu amri kirahisi namna ile.

Mara yule mwanamume aliposimama sawa sawa akamjongea Daniella kwa kasi ya ajabu apate kurusha tena turufu yake, huenda aliamini ingekuwa turufu ya mwisho, ya kumaliza mchezo. Lakini katika namna ambayo bila shaka hakuielewa ilitokeaje, alistaajabu kujikuta yupo chini! Hakuweza kuusogeza mwili wake!

“We mwanamke!” yule mwanamume aliita kwa hofu. “Umenifanya nini? Umenifanya nini we mwanamke?”

Daniella alimtazama tu pasipo kusema kitu. Macho yake yalikuwa yamebadilika kabisa! Yalikuwa mekundu na yalitoa cheche… yalikuwa kama yanayosema, “Go to hell!

“Nisaidie tafadhali, siwezi kuinuka!” yule mwanamume aliomba kisha akaanza kulia kwa uchungu.

Daniella alikuwa amemvunja mgongo yule mwanamume na sasa alimtaka Daniella amsaidie kuinuka. Alimwambia kuwa alikuwa tayari kumwambia kila kitu kwani kwa hali aliyokuwa nayo hata asingesema alichokijua ilikuwa kazi bure.

Daniella akaacha hatua zake zimfikie mwanamume yule pale chini, alipomfikia akasimama na kumtazama kwa umakini. “Okay, unaweza kuniambia ukweli wote unaoujua sasa nami nitakusaidia.”

“Najua mnamtafuta Rais, nafahamu wapi wamemficha…” yule mwanamume alisema kwa tabu. “Ila sijui kama mtafanikiwa kumkomboa maana Tiger na Chameleon wamejizatiti sana… These people are powerful and monsters.”

“Unawafahamu Tiger na Chameleon?” Daniella alimuuliza yule mwanamume.

“Ndiyo, nawafahamu sana…” yule mwanamume alisema na kuongeza, “Chameleon ni yule mkuu wa kikosi cha ulinzi wa Rais… Yusuf Taifa… Na Tiger ni…” hakuweza kumaliza kauli yake, risasi zikarindima toka sehemu fulani na kuutawanya ubongo wake.

Daniella aliruka na kutua upande mwingine wa sebule huku akiikwapua bastola yake toka kiuoni na kuiweka sawa tayari kwa mapambano lakini wakati akiijaribu bahati yake akashangaa kuona risasi nyingine zikizipasua taa zilizokuwa zikiwaka subuleni pale. Sebule yote ikawa giza.

Daniella akiwa anapambana na giza akasikia mdondoko wa kitu kama paka, wakati akijitahidi kukodoa macho yake kwenye lile giza la gafla lililotanda pale sebuleni, kwa mbali aliweza kuona kama kivuli cha mtu akinyata na kusogea mahali kulipokuwa na dirisha kisha akaruka na kulikumba dirisha la kioo, akatokomea kusikojulikana.

Daniella aliliona tukio lile, akajiuliza mtu yule ni nani na alifuata nini mle ndani maana kama alikuwa na haja ya kummaliza au kupambana naye kwa nini akimbie? Na hapo akakumbuka kuwa wakati akipambana na yule mwanamume pale sakafuni ni kama aliona kitu fulani mfano wa kivuli cha mtu kimefichama mahali ila hakukitilia maanani sana.

Akajikuta akitoa tusi zito la nguoni na kunyanyuka baada ya kuhisi usalama wa eneo lile ulikuwa mdogo, akazifanyia upekuzi wa haraka haraka zile maiti na hakuzikuta na vitu vya maana zaidi ya bastola na vitambulivyo vilivyoonesha walikuwa maofisa wa jeshi> hata hivyo kwenye maiti ya yule mwanamume aliyepambana naye mwisho, aligundua kuwa yeye alikuwa komando, Kapteni Edwardo Munambo.

Jina lile la Edwardo Munambo lilimfanya Daniella ahisi kuwa mtu yule hakuwa Mtanzania bali alikuwa mwanajeshi kutoka nchi jirani ya Msumbiji.

Baada ya upekuzi wake usio na tija aliamua kuondoka lakini nafsi yake ikamwambia amfanyie upekuzi zaidi yule komando Kapteni Edwardo Munambo na kwenye mfuko mdogo wa suruali yake ya dengrizi akaiona bahasha ndogo ya kaki iliyokunjwa na kuwekwa vizuri.

Bila ya kupoteza muda Daniella aliichukua ile bahasha na kuitia mfukoni. Akaondoka zake akiwa na lengo la kuwahi kule nilikomwambia anifuate.

Dah, nilishusha pumzi baada ya kusikia habari zile, sasa nikawa na hamu ya kutaka kujua ni nini kilichokuwa ndani ya ile bahasha ya kaki.

* * *

Usichoke, endelea kufuatilia hadi mwisho...
 
Haha! Msikonde wakuu, umeme ukija tu natupia fasta. Hapa nilipo kuna shida ya umeme, siku mbili tumeshinda bila umeme, na ukija dakika mbili tu wanakata tena. Nilidhani matatizo haya ni huko mkoa tu nilikokuwa kumbe hata Dar![emoji849]...
Umeme ni janga la taifa! Kwahiyo haujarudi tu huko boss 🤦
 
Back
Top Bottom