359
Alikuwa mtu mzima aliyepta miaka sitini na ushee kama si sabini, mwenye nywele fupi zilizoanza kujaa mvi na ndevu nyingi zenye mvi zilizokizunguka kidevu chake, na nyuma yake alifuatwa na yule msichana aliyenipokea, safari hii akiwa amejifunga kanga. Nilimtazama yule mzee huku moyo wangu ukipiga kite kwa nguvu maana sikutegemea jambo hilo.
Wakapiga hatua kikakamavu kuja pale kwenye sofa nilipokuwa nimeketi. Nilichofanya ni kutulia tu kama ambaye sikuwa na wasiwasi wowote huku nikiwatazama kwa umakini.
“Samahani sana, Jason, kwa kukuweka,” yule mzee aliniambia pindi alipokuwa akiketi jirani na lile sofa nililoketi, na wakati huo yule msichana akibaki wima. Wote walikuwa wakinitazama kwa umakini.
“Naitwa Othman Mwambe,” yule mzee alijitambulisha kwangu huku akinipatia mkono. Kisha akaelekeza kidole chake cha shahada kwa yule msichana aliyenipokea. “Huyu ni binti yangu, mtoto wangu wa mwisho kati ya watoto wawili, yeye anaitwa Rahma Mwambe… Luteni Mwambe.”
“Nashukuru kuwafahamu. Nimeitikia wito wenu,” nilisema huku nikiwatazama usoni kwa zamu nikijaribu kuyasoma mawazo yao kuona kama walikuwa watu mwema au la.
Kabla hajaongea alichoniitia aliyapeleka macho yake kutazama dirishani huku masikio yake yakisimama kama aliyekuwa akisikilizia sauti kisha akaniuliza, “Una uhakika umekuja peke yako?”
“Ndiyo…” nilimjibu kwa kujiamini.
“Unapaswa kuwa mkweli kwenye hili maana hapa unatakiwa kuja mwenyewe. Ni wewe pekee ninayekuamini kwa sasa kwa kuwa nimekuwa nikivutiwa na harakati zako,” yule mzee alisema huku akinitazama kwa umakini sana kana kwamba alikuwa mwalimu wa usafi aliyekuwa akimkagua mwanafunzi. “Sitaki mtu yeyote aanze kunifuata fuata. Nina familia inanihitaji, na maisha yangu napenda yakiwa yangu binafsi.”
Nilimtazama kwa umakini kisha nikamuuliza, “Ulijuaje kuwa nilikuwa nimefikia Naf Beach Hotel na ninatumia jina bandia la Halfan Jongo?”
“Nimekuwa kwenye idara ya ujasusi kwa miaka arobaini…” yule mzee alinijibu kwa kujiamini kisha akaendelea, “…sikia, unaweza ukawa hunijui kwa kuwa huna muda mrefu kwenye Idara ya Usalama wa Taifa, ila mimi ni mtu ambaye nimetumikia taifa hili kwa miongo minne katika nafasi mbalimbali hadi kuwa Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, na nime-
recruit maofisa wengi wa kijasusi wakiwemo mkurugenzi mkuu wa TISS, David Mshana na mkuu wako wa kikosi, Kanali Othman Mjaka… lakini huenda hayo yasiwe muhimu sana kwako bali lililo kuu ni kwamba mimi ni swahiba mkuu wa Rais, Dk. Albert Masinde, ambaye wewe unamtafuta.”
Nilimtazama yule mzee kwa namna ambayo ilikosa tafsiri sahihi. Nilihisi kusikia habari zake sehemu ingawa sikuwahi kufikiria kama siku moja ningekutana naye. Hata hivyo sikusema neno, nilibaki kimya nikimtumbulia macho mzee yule.
“
By the way, nilisahau kukuuliza… sijui utatumia kinywaji gani?” yule mzee aliniuliza huku akinikazia macho.
“Juisi ya aina yoyote itanifaa zaidi,” nilimwamba yule mzee maana nilihisi ingesaidia kupungua njaa niliyokuwa nayo. Na hapo yule mzee akageuka kumtazama Rahma na kumpa ishara.
Rahma akaliendea lile jokofu lililokuwa kwenye pembe ya sebule na kulifungua, akatoa jagi kubwa lililojaa sharubati ya mchanganyiko wa embe na pasheni na kurudi akiwa na bilauri mbili kubwa ambazo aliziweka mezani na kumimina sharubati kwenye zile bilauri, bilauri moja akampatia baba yake na nyingine akanipa.
“Karibu sana,” Rahma alisema.
“Ahsante,” nilimshukuru kisha nikapiga mafunda mawili ya nguvu na kuiweka bilauri ile mezani na hapo tukabaki tukitazamana kwa kitambo kifupi kabla yule mzee hajavunja ukimya.
“Sasa nafikiri tunaweza kuongea… kama nilivyokwambia mimi ni swahiba mkubwa wa Rais Masinde, sasa kinachoniuma mno ni kwamba nahisi nahusika na utekwaji wa Rais, maana kama ningelichukua hatua mapema huenda haya yasingetokea… Najuta sana kwa hilo,” yule mzee alisema kwa uchungu kisha akanyamaza kidogo.
Nilimtupia jicho Rahma kisha nikayarudisha macho yangu kumtazama yule mzee, bado sikuongea. Niliendelea kumpa nafasi yule mzee aendelee kujieleza pasipo kuingilia, maana ni yeye aliyeniita pale kunieleza jambo.
“Wiki mbili kabla ya Rais hajaanza ziara ya kuja huku Mtwara ofisa mmoja wa
Secret Service anayeitwa William Shamte alinifuata katika hoteli niliyofikia siku nilipokwenda Dodoma. Siku hiyo ilikuwa nionane na Rais lakini alikuwa ametingwa sana na majukumu. Shamte aliniachia ujumbe kwenye katarasi na kuondoka mara moja,” yule mzee alisema huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa kipande kidogo cha karatasi ngumu nyeupe, akanikabidhi.
Niliusoma ujumbe ule ambao uliandikwa kwa kalamu ya wino mwekundu;
‘Kuna tishio kiotani, tafadhali msaidie ndege wetu’ ambao ulimaanisha kuwa kumwomba mzee huyo amsaidie Rais kwani alikuwa yupo kwenye matatizo.
Nilishusha pumzi na kuinua uso wangu kumtazama mzee Mwambe, yeye akaendelea kuongea. “Namna kijana huyo alivyonipata na kunifikishia ujumbe ule ilinifanya nishindwe kumuuliza Rais nilipokutana naye kesho yake, ingawa nilitamani sana kumuuliza ili kujua alikuwa na shida gani. Kama unavyojua, alikuwa na walinzi wake na pia si rahisi kuwasiliana na Rais, mara nyingi ilikuwa hadi yeye anitafute, na mara ya mwisho kuongea naye ilikuwa ni juzi jioni alipofika hapa Mtwara kuanza ziara yake ya siku tatu. Alikuja hapa kunisalimia. Na baadaye jioni ofisa yule yule wa
Secret Service, akaja kwa siri na kunifikishia ujumbe mwingine.”
Mzee Mwambe aliweka kituo halafu akatoa tena karatasi nyingine toka kwenye mfuko. Karatasi ile ilikuwa na ujumbe ambao alikuwa ameuandika mwenyewe kwa mwandiko wake akinakiri taarifa alizopewa na Shamte.
‘Sasa kiota kinawaka moto, ndege tunduni yupo hatarini, ni wewe pekee anayeweza kukuamini, tafadhali msaidie dhidi ya Tiger na Chameleon...” ujumbe ulisomeka hivyo.
Tafsiri yake ilikuwa ni ile ile ya kumwomba mzee Othman Mwambe kumsaidia Rais kwani sasa alikuwa hatarini zaidi dhidi ya watu waliojiita Tiger na Chameleon.
“Nilipomuuliza Tiger na Chameleon ni akina nani, akaniambia anamfahamu Chameleon kuwa ni mkuu wa kikosi cha siri cha ulinzi wa Rais (
Secret Service), Yusuf Assad Taifa, lakini hamfahamu Tiger ila aliamini kuwa ana nafasi ya juu ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)…” yule mzee alisema, kisha akaongeza.
“Aliamini kuwa kama si mkuu wa majeshi, Jenerali Adam Kalembo basi ni Mnadhimu wa Jeshi, Luteni Jenerali Gozbert Bundala, ambaye kabla hajapanda cheo na kufikia nafasi hiyo alikuwa Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, nafasi ambayo mimi nilimwachia baada ya kustaafu.”
Kisha yule mzee aliniambia kuwa usiku wa siku iliyofuata baada ya kuletewa ule ujumbe na Shamte yakatokea yaliyotokea huku ofisa huyo aliyemletea ujumbe ule akiuawa.
“Dah!” ndiyo neno pekee nililomudu kulitamka kwa wakati huo. Kisha niliinyakua bilauri ya sharubati pale mezani na kuvuta funda moja kubwa lililosababisha sharubati yote iishe kwenye bilauri kisha nikairudisha mezani huku nikimtazama Rahma.
Endelea...