289
Hakustahili kufa…
Saa 8:30 mchana…
NILIPOMALIZA kuyasoma maelezo niliyokuwa nimeyaandika kwenye notebook yangu kuhusu kile nilichojadili na mkuu wangu wa kazi asubuhi ya siku hii, akili yangu ikaonekana kupata afya njema na hisia zangu za kikazi zikafufuka upya na kunifanya nijihisi kuwa sasa nilikuwa nimeianza rasmi kazi yangu ya kufuatilia suala la ugaidi uliosababisha mlipuko wa bomu katika jengo la Alpha Mall. Mlipuko ambao ulimwacha Waziri Ummi Mrutu na watu wengine 32 wakiwa wamepoteza maisha yao huku wengine 95 wakijeruhiwa.
Muda huu wataalamu walikuwa mbioni kukakimilisha uchunguzi wao wa vinasaba (
DNA) ili kuwatambua watu waliouawa katika shambulio hilo la kigaidi na pia kuthibitisha uwepo wa mtuhumiwa au watuhumiwa katika eneo husika kwa kuchunguza viungo vya watu hao ili kupambanua akina nani walikuwa waathirika, na nani walikuwa na viashiria vya kuwa wabebaji wa bomu.
Kazi ya uchunguzi huu ilitarajiwa kukamilika siku iliyofuata na baada ya hapo miili ya marehemu hao ingekabidhiwa kwa ndugu ili mipango ya mazishi yao ifanyike!
Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani na kuchukua magazeti yaliyokuwa juu ya meza yangu ili kuona kile kilichokuwa kimeandikwa kwenye magazeti hayo. Mezani kwangu kulikuwa na jumla ya magazeti manne ya
HabariLeo,
Rindima,
Mwanahabari na
Nijuze.
Magazeti haya yaliandika na kudodosa hili na lile juu ya ugaidi huu uliosababisha kifo cha Waziri Ummi Mrutu ambaye jina lake halisi aliitwa Ummi Imani Uledi, kwani jina la Mrutu lilikuwa la mumewe na ndilo alilolitumia katika shughuli zake za kiofisi. Mumewe aliitwa Rashid Mrutu, jina kubwa katika jamii.
Katika habari zote nilizozisoma kwenye magazaeti haya, lililokuwa wazi katika maandishi yote ni utata juu ya nani waliofanya ugaidi huu hadi kusababisha kifo cha Waziri Ummi. Wingu zito lilitanda juu ya kifo cha Waziri Ummi kutokana na swali zito lililokuwa likisumbua vichwa; bomu hilo lilimkusudia yeye au magaidi hao walitaka kutuma ujumbe fulani kwa serikali?
Gazeti la
Rindima lilikwenda mbele zaidi katika habari yao ambayo iliandikwa pia kama maoni ikibebwa na kichwa cha habari; “
Waziri Ummi hakustahili kufa kifo hiki!”
Habari hii iliandikwa;
Ni Ummi Mrutu ni waziri aliyesifika sana kwa kupambana na mafisadi, wauza mihadarati, wahujumu na wote wenye nia ya kuihujumu Tanzania. Tunaamini kuwa kazi aliyotumwa na Mungu hapa duniani alikuwa hajaimaliza ila wanadamu wameamua kuyakatisha maisha yake… hakika hakustahili kufa kifo hiki! Tunaiomba serikali izidishe uchunguzi ulio makini na wa haraka ili kujua kitu gani hasa kilicho nyuma ya tukio hili lililosababisha mshumaa huu uliokuwa nuru kwa Watanzania wanyonge kuzimika ghafla…
Gazeti la
HabariLeo lilizifuatilia habari za kifo cha waziri huyo kwa mtindo wake. Liliwasiliana na Ikulu hususan Ofisi ya Rais kutaka kujua Rais alikuwa anajisikiaje kumpoteza jemadari wake ambaye kulikuwa na tetesi kuwa ndiye aliyekuwa akiandaliwa kuwa Rais ajaye wa Tanzania baada ya yeye kuondoka madarakani.
Hakuna aliyejua!
Pengine jambo pekee ambalo uchunguzi wa gazeti la HabariLeo ulifanikiwa kupata ni pale walipofanikiwa kuzungumza na kaka wa marehemu, Dk. Kassim Uledi, ambaye alisema kuwa Waziri Ummi na mumewe, Rashid Mrutu, hawakuwa wakiishi pamoja baada ya kutengana takriban mwaka mmoja uliokuwa umepita na kisha Rashid Mrutu kuhamishia makazi yake Jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini! Kwa nini walitengana na kwa nini Rashid Mrutu alihamia Afrika Kusini?
Hakuna aliyejua!
Picha ya Rashid Mrutu ilitoka sambamba na ya mkewe Waziri Ummi katika habari hizi. Ilikuwa ni picha waliyopiga pamoja katika mojawapo ya siku zao za furaha. Walikuwa wakiitazama kamera na kwa kuangaliza nyuso zao tu niliweza kubaini kuwa mapenzi yalikuwa wazi kabisa katika macho ya wenzi hawa.
Kwa kusoma habari hii nikakumbuka nilipokwenda msibani mara ya kwanza asubuhi ya Jumapili, nilisikia kuhusu jambo hili na hivyo kumtafuta Dk. Kassim Uledi, nikamkuta akiwa ameketi chini ya kivuli kikubwa cha mti, mbele ya nyumba ya marehemu. Alikuwa amekaa kwenye kochi dogo la sofa lililomfanya nusu awe amekaa, nusu amelala. Mara kwa mara alifumba macho yake kama mtu aliyekuwa akificha machozi, jambo lililoyafanya macho yake yawe mekundu kuliko ilivyokuwa kawaida yake.
Kilichonisukuma kwenda msibani siku hiyo ni ile hisia kwamba muuaji mara nyingi huwa na tabia ya kuhudhuria msiba na hata kudiriki kwenda kumzika mtu aliyemuua.
Nilipofika hapo nililisogelea kundi dogo la watu waliokuwa wameketi na Dk. Kassim Uledi pale chini ya mti wa kivuli na kuomba kuzungumza faragha na kaka huyo wa marehemu. Dk. Uledi alisimama na kuniongoza upande wa pili wa bustani kulikokuwa na viti vilivyochongwa vizuri toka katika magogo ya miti. Tukaketi kwa kutazamana.
Dk. Uledi, mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikuwa mtu mzima mwenye umri wa miaka 55. Alikuwa mrefu na mnene kiasi, mweupe na mwenye sura ya mviringo iliyoonesha utulivu na macho yake yalikuwa makini sana kama ya kachero mbobezi. Japokuwa uso wake ulikuwa umesawajika lakini kwa kawaida alikuwa mcheshi sana.
“Enhe, sijui unasemaje?” Dk. Uledi alinisaili huku akinitazama machoni. Uso wake ulikuwa umesawajika kidogo.
“Mimi ni mwandishi wa habari, naitwa…” nilianza kujitambulisha lakini Dk. Uledi akanikata kauli.
“Nakufahamu sana… unaitwa Jason Sizya, sivyo? Mwandishi mahiri wa habari za uchunguzi,” Dk. Uledi alisema huku akishusha pumzi.
“Ni kweli…” nilisema kwa sauti tulivu, kisha kwa sauti iliyobeba majonzi nikaongeza, “nilimfahamu sana marehemu kupitia nafasi yake na niliondokea kuwa mshabiki wake mkubwa. Kwa kweli kifo chake ni pengo kubwa sana, si tu kwa familia yake bali kwa taifa. Poleni sana…”
“Dah! Ahsante sana… kwa kweli maisha ya dada’angu yamekatishwa ghafla,” Dk. Uledi alijibu huku chozi likimdondoka na kuteleza juu ya shavu lake kabla hajalifuta kwa kiwiko cha mkono wake.
“Ndiyo dunia,” nilisema kwa utulivu. “Sote njia yetu ni hiyo hiyo.”
“Ni kweli,” Dk. Uledi aliunga mkono. “Kwa hiyo ulihitaji nini toka kwangu, ndugu Sizya?”
“Kama mwanahabari ninayeandika habari za uchunguzi, kuna mawili matatu ninayohitaji kufahamu kutoka kwako,” nilimwambia Dk. Uledi.
“Kama yepi?” Dk. Uledi aliniuliza huku akinitazama kwa tuo.
“Ni ya kawaida tu… kwa mfano, ningependa kujua hisia zako kuhusu vifo mfululizo vya wapendwa wako vilivyotokea ndani ya mwezi mmoja tu. Alianza mpwao, mtoto pekee wa dada yako aliyekufa kifo cha kutatanisha, na sasa mama yake ameuawa. Unadhani vifo hivi vinaweza kuwa vimesababishwa na mtu au kundi lile lile, na kwa sababu gani?”
“Dah! ukweli nimechanganyikiwa sana kiasi kwamba nahisi kama akili yangu haifanyi kazi sawa sawa. Laiti ningewajua waliosababisha vifo hivi ningewaua kwa mikono yangu kwanza na kuwapeleka polisi baadaye,” Dk. Uledi alijibu.
Endelea...