Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Mei 20, 2026 kulitokea tukio linalodhaniwa kuwa la utekaji wa David Djumbe ambaye ni msaidizi wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa, Djumbe alifanikiwa kuwatoroka watekaji waliojitambulisha kuwa ni maofisa wa polisi.
Akisimulia tukio hilo, David Djumbe amesema lilitokea majira ya saa nne kasoro, wakati yeye na rafiki yake wakirejea nyumbani katika Kijiji cha Vikawe wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
Yeye ndiye alikuwa akiendesha gari la rafiki yake na ndipo vamiwa na gari aina ya Toyota Prpbox lililokuja kwa kasi na kuwapita upande wa kulia (overtake) na kuwazibia njia kwa mbele (block), huku gari lingine likiwazibia kwa nyuma.
Watu wapatao watano au sita walishuka kwenye magari hayo na kufungua milango yao na walinza kwa kumtoa rafiki yake upande wa pili kwa nguvu na kumbeba na ndipo yeye alipotambua kuwa hao ni watekaji na hivyo alipiga kelele.
Rafiki asimulia
Akizungumzia tukio hilo, rafiki yake aliyejitambulisha Allan Macha amesema jana jioni (Mei 20) alipogiwa simu na Djumbe akimwomba ampitie warudi nyumbani.
“Wakati jana nipo ofini karibu ninatoka maeneo ya mjini, Djumbe alinipigia simu, akanieleza kwamba niko gereji gari yangu inatengenezwa, hivyo akaniambia kama unatoka mjini nnaomba unichukue turudi nyumbani.
“Ilikuwa saa 2 usiku, kwa hiyo nikampitia nikamchukua, ila nikamwambia yeye aendeshe kwasababu mimi kiundo kinaniuma. Akakubali kuendesha,” amesema.
Ameendelea kusimulia: “Aliendesha mpaka tumekaribia kufika nyumbani karibu mita 20 hivi, nikaiona gari nyuma na pikipiki mbili zinakuja kwa kasi kubwa.
“Nikamwambia awapishe wapite, ile kuwapisha jamaa akatuzuia na gari (aina ya Toyota Probox). Hapo tumeshapita Bunju tumepita Mingoi, tumeingia barabara ya Kimele kuelekea nyumbani maana sisi tunaishi, Kijiji Vikawe Kata ya Pangani Wilaya ya Kibaha,” amesema.
View: https://www.youtube.com/watch?v=ZJwKHot4i0k
Anaendelea, “Walivyotuzuia mara ya pili na ya tatu kukawa na uwazi mahali, wakatuzuia tena, wakashuka watu sita kwenye gari yao, wakaanza kutuambia wao ni polisi, ila walikuwa na nguo za kiraia, ni mmoja tu niliona amevaa nguo kama za askari wale wanaovaa nguo za kijani.
Soma Pia:
- Msaidizi wa Lissu apatikana baada ya kudaiwa kutekwa akiwa na pingu mkononi pamoja na majeraha
- David Djumbe (Msaidizi wa Lissu) adaiwa kutekwa
“Kile kitendo cha kutukamata kilikuwa cha kimafia kabisa. Wakawa wanasema leta pingu, huku wakifyatua risasi hewani.
“Baadaye wakaondoka na David Djumbe, wakaondona na gari lao na gari langu, wakiwa wanaendesha wao.
“Waliendelea kufyatua risasi hata walipofika Boko Magengeni, ili kuwatimua madereva wa bodaboda waliokuwa wakiwafuata.
Mwisho wakaingia kwenye ule msitu wa Usalama wa Taifa pale Mbweni. Baada ya matukio yale nikarudi kwenda kuripoti tukio hilo kituo cha polisi Mbweni.
“Baadaye niliporudi hadi Mapinga, ndiyo nikapata taarifa kutoka kwa RCO (Ofisa Upelelezi Mkoa) wa Pwani, akisema gari langu limetelekezwa Mbweni na ametoa maelekezo kwamba lipelekwe kituo cha Polisi Mbeni.
“Kweli polisi waliofika hapa ofisi za CHADEMA wamesema gari langu lipo kituo cha Polisi Mbweni. Kwa hiyo mimi nikitoka hapa nakwenda kituo cha Polisi Oysterbay na baadaye nitakwenda Mbeni nifuate gari langu,” ameeleza.
Djumbe alivyowatoroka watekaji
Kwa upande mwingine, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Amani Golugwa akiwa makao makuu ya chama hicho Mikocheni, ameeleza kuwa, katika purukushani hizo, Djumbe aliwatoroka waliomteka.
“Bodaboda walifukuzia lile gari wale jamaa wakaona mambo yanaharibika, wakashuka kwenye gari wakawa wanapiga risasi. Inasemekana bodaboda walikuwa wengi kama 50 hivi.
“Wakiwa msituni huko, wakawa wanaendelea kupiga risasi, sasa katika zile purukushani, jamaa akafungua mlango wa gari akakimbilia huko porini akiwa na pingu,” amesema Golugwa.
Hata hivyo, amesema Djumbe alifanikiwa kurudi nyumbani kwake akiwa na pingu na asubuhi ya leo ameelekea kituo cha Polisi Oysterbay kuripoti.
“Amekwenda na viongozi wa chama na mawakili watakaomsaidia. Lakini tunaamini hana hatia na kwa kuwa zile pingu ni ngumu, inabidi zifunguliwe,” amesema.
Polisi wafika Makao Makuu ya CHADEMA
Golugwa amesema, wakati wanajiandaa kwa mkutano na waandishi wa habari, gari la polisi lilifika na baadhi ya maofisa waliingia ofisini na alizungumza nao.
“Polisi walipofika walisema wamekuja kumchukua Djumbe kwa sababu ametoroka na ni mtuhumiwa na pia amefungwa pingu na kama amepigwa akatibiwe.
“Sisi tumemwambia kwamba, kama polisi walikuwa wanamtafuta katika hali ya kawaida, kwa nini wamemchukua na gari wamelitelekeza? Kwa nini hilo liwe exhibit?
“Maswali yangu yakawa hivi, mmejuaje kwamba amefungwa pingu? Pili, ametoroka alikuwa kwenye mikono ya nani? Tatu ni mtuhumiwa anatuhumiwa nini? Nani amewaambia kama anatuhumiwa?”
“Nikawaambia aliyepo hapa ni mtu aliyekuwa naye na baadaye nikawaambia kwamba Djumbe ameshapatikana wakamfungue pingu,” ameeleza.
Kwanini Djumbe akamatwe?
Kwa mujibu wa Golugwa, Djumbe hana rekodi ya uhalifu na wala hajawahi kuambiwa kuwa anatafutwa kwa uhalifu.
“Hana tuhuma yoyote, ila waliomkamata ndio watuambie. Ndiyo maana nimewaambia wakamfungue.
“Huo ni utekaji kwa maneno waliyomwambia wenyewe, kwamba wewe unajifanya una kiherehere, ninyi ndio mnajifanya mnamtetea Lissu,” amesema.
Golugwa amekanusha madai kwamba Djumbe ndiye alitoa taarifa za Lissu kuugua tumbo akiwa gerezani.
“Pale wanaoruhusiwa kwenda ni familia ya Lissu tu, yaani ndugu wa damu, ambao ni Vincent, Lucy ambaye ni dada yake wa Songea na Ikoti.
“Watu wengine hawaruhusiwi, hata mawakili wake hawaruhusiwi kwenda, ndiyo maana kuna kesi imefunguliwa.”
Msimamo wa CHADEMA
“Sisi msimamo wetu ni kwamba hilo ni tukio la utekaji lililoshindikana. Pili, ni keke yetu ambayo haitakoma kwa mamlaka za usalama, kwamba hakuna seriousness kwenye usalama wa watu, tunachukuliana kawaida sana.
“Tatu, tumelilaani jambo hilo na tumempa taarifa Afande (Faustine) Mafwele ambaye nimeongea naye kwamba tumepata taarifa kwamba amepatikana hivyo wakamfungue pingu.”
Taarifa ya Polisi