SEHEMU YA 118
Wakiwa pale sebleni Sara na kaka zake, basi kaka yake akasema kuwa mchumba wake amefika kwahiyo akaenda kumpokea kwahiyo Sara na kaka yake mwingine wakabaki wenyewe wanamsubiri huyo wifi kwa Sara na shemeji kwa Kulwa. Ila Sara alimuuliza kaka yake,
“Vipi unamjua huyo mchumba wa Doto?”
“Hata simjui kabisa, Doto msiri sana hajawahi kunionyesha hata mara moja huyo msichana wake”
“Wewe je umeshawahi kumuonyesha wa kwako?”
“Hapana, mimi mwenyewe sijawahi kumuonyesha hata mara moja ila nimepanga siku nimtambulishe hapa nyumbani. Hata leo nilitamani aje pia ila kaniambia amepata udhuru”
“Sawa”
“Na wewe wako? Najua ni Ommy ila sijamuona siku zote hizi”
“Achana na huyo mtu, kwanza ananiumiza kichwa tu. Yani mapenzi yameniumiza kweli mimi, kumbe Ommy alikuwa ananisaliti, kunionyesha kote upendo kule kumbe amepata kasichana kengine ananisaliti nako. Siku niliyogundua niliumia sana”
“Kwahiyo Ommy yuko wapi?”
“Achana nae bhana, atajijua mwenyewe alipo”
“Mmh dada jamani, unajua mtu akikusaliti unatakiwa kuwa mpole kwanza, ujue ni kwanini amekusaliti sio kuweka hasira mbele”
Sara alianza kukohoa na kumuomba kaka yake huyu akamchukulie maji ya kunywa,
“Mmmh maneno yangu yamekufanya upaliwe, basi pole. Ngoja nikakuchukulie hayo maji”
Basi Kulwa akainuka na kwenda kumchukulia maji ya kunywa Sara, ila muda huu huu Doto nae alikuja na kuingia ndani kisha akamwambia dadake asimame kumkaribisha mgeni maana ameshafika,
“Mmmh kama tunamkaribisha raisi jamani! Kumbe utamu wa mtu”
“Acha maneno yako Sara bhana”
Basi akamkaribisha Yule msichana ndani, ila Sara alipoangusha macho yake kwa Yule msichana alishtuka sana kwani alikuwa ni Mishi, alijikuta akimuuliza kaka yake kwa umakini huku akifikicha fikicha macho,
“Kaka, mwanamke mwenyewe ndio huyo?”
“Ndio, kwani vipi mzuri eeh!”
Sara alifikicha tena macho yake, ila kabla hajasema chochote Kulwa nae alikuwa ametoka jikoni akiwa na glasi ya maji ila alipomuona shemeji yake huyo, alihamaki na kumuita kwa mshangao,
“Mishi!!!”
Mishi aliangalia kwa aibu sana, na hakuongea lolote zaidi ya kufungua mlango wan je na kuondoka kuelekea getini, alifika getini na kutoka ila alivyotoka tu alijishangaa akijikuta tena yupo pale pale sebleni halafu mara Salome nae alitoka kwenye ile sebule nyingine akicheka, na kuwakuta pale sebleni huku Mishi akiwa anashangaa shangaa, kisha Salome akasema,
“Sasa Mishi unashangaa shangaa nini? Unaona kama maajabu eeh! Wakati unatenda vitu vya namna hii hukujua kama ni maajabu ya namna hii yangetokea mbele yako? Unataka kukimbia uende wapi na ukimbie kwasababu ya nini? Kaa hapo ujieleze, ni kwanini umechanganya ndugu hawa”
Doto alikuwa na hamaki tu na kujikuta akimuuliza Kulwa,
“Kwani huyu msichana unamfahamu?”
“Nio huyu nilisemaga mchumba wangu mwenyewe, leo nilitaka anitembelee pia akasema ana kazi kumbe ananichanganya na pacha mwenzangu!”
Sara nae akadakia na kutoa dukuduku lake la moyoni,
“Yote tisa, kumi ni kuwa huyu dada ndio kidudu mtu aliyekuwa anatembea na Ommy hadi moyo umeniuma sababu yake”
Wote wakashangaa kuwa Mishi amewachanganya kiasi kile, Doto akajikuta akimwambia,
“Yani kukuhudumia kote kule Mishi bado ulikuwa unanichanganya na ndugu yangu!”
Mishi alikuwa kimya kabisa kwani aibu aliyoipata leo hakuitegemea kabisa, Salome nae akaongea,
“Yani sio kwamba wewe Doto ulikuwa ukimuhudumia peke yako, ni hivi huyu binti wote mmeshiriki kumuhudumia. Kulwa pia umemuhudumia sana huyu binti, halafu hata Sara umemuhudia sana maana hela zote ulizokuwa unampa Ommy alikuwa anapeleka kwa huyu binti. Haya sasa nirudi kwako wewe fundi wa kuumiza mioyo ya watu, hivi hukuwahi kuwaza kuwa mambo unayoyafanya ipo siku utaumbuka? Hivi ni bahati za watu wangapi umezifunika wewe mmoja? Yani wewe utembee na Kulwa, wewe utembee na Doto na wewe utembee na mwanaume wa dada yao, kwahiyo umechanganya familia vilivyo”
“Nisameheni sikujua kama ni ndugu”
MIshi alipiga magoti, na kumfanya Salome acheke sana na kusema,
“Kwahiyo kama si ndugu ni sawa kuwafanyia hivyo? Mwanzoni nilijua ni Ommy anakudanganya kumbe ni wewe unaewadanganya wenzio, hivi ungefanyiwa wewe hivi ungejisikiaje?”
“Nisamehe jamani, nisameheni”
Sara alikuwa na hasira sana na huyu Mishi, hata wale mapacha nao walikuwa na hasira nao vilivyo wakatamani wote wamvamie na wampige ila Salome aliwakataza na kwenda kumkinga Mishi ili wasimpige.
“Tafadhalini jamani msimpige wala msimuumize, mwacheni jamani nataka huyu atembee na laana yangu”
Doto alikuwa na hasira sana, ila Salome alimzuia kabisa kumpiga mishi yani alijikuta akiganda tu bila kumpiga. Salome alifungua mlango na kumruhusu Mishi aondoke ila akamwambia,
“Kumbuka utatembea na laana yangu siku zote, leo utafurahi sana kuwa umewachanganya ndugu lakini hujafanywa lolote ila utatembea na laana yangu siku zote. Laiti kama ningekuwa wewe nisingeondoka leo ila ningekesha nikiomba msamaha”
Mishi hakutaka kusikiliza sana kwani alitoka muda huo huo na hakutaka tena kubakia kwenye nyumba hiyo kwani alijiona kama anamkosi kwa siku hiyo.
Kwakweli si Sara wala wale mapacha waliofurahishwa na kitendo kile kwani kila mmoja alienda njia yake mule ndani akiwa na mawazo yake, haswa Doto alihisi kudhalilishwa sana na Yule mwanamke, kwahiyo sebleni alibaki Salome peke yake.