Simulizi: Kurudi Kwa Moza

Simulizi: Kurudi Kwa Moza

SEHEMU YA 104


Wakina Sara walifikishwa na Jesca kwa mkaka ambaye anasadikika kuwa alimbeba Salome wakati ameanguka kaburini, waliweza kufika baada ya Yule Jesca kuwaunganisha na Yule ambaye alikuwa akimjua vizuri Yule dereva.
Walifika na kusalimiana kisha wakaanza maongezi ya hapa na pale na haswa ni kuulizia kuhusu Salome,
“Jamani hata mimi mwenyewe sielewi, Yule mtoto alikuwa na mama yake kwenye gari na mama yake alikuwa akilia sana, gafla nilisikia akiongea na mama yake na muda kidogo mama yake akaniambia kuwa tusiende tena hospitali bali twende nyumbani kwao. Basi nilifanya hivyo kwa kuwapeleka nyumbani kwao”
“Mmmh kwahiyo hujui alizindukaje zindukaje. Wewe si ulimbeba na uliiona hali yake?”
“Ni kweli nilimbeba na alikuwa kama mtu aliyepigwa na shoti ya umeme tena nilijua amekufa yani nilikuwa naenda nao tu hospitali ila nilikuwa najua lazima tutaambiwa kuwa amekufa. Hata mimi nilipomsikia anaongea tena akiwa mzima kabisa nilishtuka sana”
“Mmmh inabidi tukaongee na mama yake, lazima kuna kitu anakijua. Unapajua kwao?”
“Napakumbuka vizuri sana, kwa tukio kama lile lazima nikumbuke kwao ni wapi”
Basi wale kaka wa Sara wakamuomba huyu dereva awapeleke kwao na Salome ili wakaongee na mama yake kwani kuna kitu walianza kuhisi kuwa hakipo sawa na Salome na walihisi kuwa wakiongea na mama yake wataujua ukweli wa mambo yote.
Basi safari ikaanza ya kuelekea kwakina Salome, na kweli walifika ila kwa bahati mbaya ilikuwa ni kwakina Salome kwa zamani na hakuna hata mmoja pale mtaani aliyejua nyumba mpya waliohamia wakina Salome, na waliambiwa ni kitambo sana wamehama. Ikabidi waachane pale na kila mmoja kuelekea sehemu yake, ambapo wale mapacha na dada yao waliamua kurudi tu nyumbani kwani siku ya leo hakuna walichofanya zaidi ya kufatilia mambo hayo.
“Ila mnakumbuka kuwa mama alisema tusirudi mpaka atupigie simu”
“Sasa mpaka saa hizi jamani, saa mbili hii labda mama kasahau. Tumpigie tu simu sisi wenyewe”
Wakaamua kumpigia simu mama yao ila simu ya mama yao iliita bila ya kupokelewa ikabidi wakubaliane tu kurudi nyumbani.
 
SEHEMU YA 106


Rose aliingia chumbani kwake akihisi kwamba Patrick atamkuta maana alimuona akirudi ila alijiuliza kitu,
“Inawezekana akawa Patrick wa mazingaombwe Yule. Mlinzi mwenyewe hata kumsalimia namuogopa maana sina hakika kama ni yeye kweli”
Akaenda kuoga kisha akarudi, ila leo akakumbuka dawa zake ambazo huwa zinamsaiia kumtoa uoga kabisa, na mara nyingi huzitumia kama anataka kufanya tukio la tofauti ili asipatwe na uoga. Sasa kutokana na matukio ya siku hiyo na yale ya siku za karibuni akaona ni vyema kuchukua hiyo dawa yake na kuanza kuichoma, kwahiyo akachukua kiberiti na kuanza kuwasha dawa zake hizo ambapo harufu ya dawa zile ilienea nyumba nzima. Mara akasikia mlango wake ukigongwa, akainuka na kwenda kufungua, akamkuta Salome mlangoni akionyesha kujawa na hasira halafu akamwambia,
“Zima hizo dawa zako”
“Nizime ili iweje? Kwani wewe zinakusumbua nini?”
“Sizitaki zinaniumiza kichwa, nimekwambia zima”
“Wewe mtoto usinitishie maisha, kwanza umeharibu sana mfumo mzima wa maisha yangu halafu saivi unajifanya unajua kila kitu. Dawa hizi sizimi na utanitambua baada ya kumaliza kuchoma hizi dawa”
“Unasema huzimi?”
“Ndio sizimi”
“Unajiamini kabisa?”
“Najiamini ndio na sizimi, usinibabaishe”
Rose akafunga mlango wake kwa nguvu kwani aliona kamavile Salome anampigia makelele tu, kisha akarui na kuendelea kuchoma dawa zake ambazo kwa yeye zilikuwa zinmburudisha sana na alikuwa anajisikia vyema moyoni ila ile dawa ilikuwa inawaumiza sana watu aliowafungia kwenye chumba chake na ndiomana Salome hakuitaka maana aliweza kuyahisi maumivu waliyoyapata watu wale.
Rose akiwa amestarehe kabisa na dawa zake, huku amezishika akizichoma gafla alihisi kama kuna mtu amekuja na kuzizima, alipoangalia vizuri alimuona Salome. Rose akashtuka kidogo kisha alimuuliza Salome,
“Hivi wewe ni mchawi? Umeingiaje humu?”
“Dawa imeanza kukupa ujasiri eeh!”
“Nijibu umeingiaje?”
“Kama ambavyo wewe huingiaga kwenye vyumba vya watu vikiwa vimefungwa”
“Wewe ni mchawi”
“Hapana mimi si mchawi”
Gafla Rose akainuliwa na nguvu ya ajabu yani alikuwa kama yupo juu akimtazama Salome kwa chini na mara akaona kama macho ya Salome yakiwaka waka taa, kwa mara ya kwanza Rose alishikwa na uoga kiasi na kutaka kupiga kelele ila alihisi kama akizibwa mdomo na hapo hapo akapata jibu kuwa mtu pekee anayewasumbua kwenye nyumba ile si Moza bali ni Salome, yeye alihisi kuwa Moza ameshakufa ila Salome ana nguvu za kichawi ndio anawasumbua. Kitu kilichomshangaza kuhusu Salome kuwa ni mchawi wa aina gani ambaye hatambuliki na wachawi wengine. Mdomo wa Rose ulikuwa umezibwa na akaamua awe mpole, alimuomba jambo moja tu Salome,
“Niruhusu hata nikalale sebleni kwa siku ya leo”
“Kwani unaogopa? Wewe ni jasiri, unatoa wapi uoga wa namna hiyo? Kama umeweza kufuga watu na hawafurukuti kwako unawezaje kumuogopa mtu kama mimi?”
Rose alikuwa kimya tu akitetemeka kwani ukweli ni kuwa uoga ulimshika vilivyo.
“Muda wa kufanya uwanga wako unafika? Unajua matatizo ya uchawi wa kununua? Utakudhuru mwenyewe tu. Haya toka ukalale sebleni”
Akajikuta tu ameachiwa na kuanguka kisha akainuka upesi na kuanza kutoka chumbani kwake kwa uoga na kufanya haraka haraka, kufika sebleni akamkuta Salome amekaa kwenye kochi, hapo ndipo akili yake ikapoteza dira kabisa.
 
SEHEMU YA 107


Akajikuta tu ameachiwa na kuanguka kisha akainuka upesi na kuanza kutoka chumbani kwake kwa uoga na kufanya haraka haraka, kufika sebleni akamkuta Salome amekaa kwenye kochi, hapo ndipo akili yake ikapoteza dira kabisa.
Akashtuka ila Salome akacheka na kumuuliza,
“Unashtuka nini sasa?”
Rose alikuwa kimya kabisa na kushindwa kujibu kwani kadri alivyomuona Salome ndivyo uoga ulivyokuwa ukimshika, kisha Salome akamwambia tena,
“Wewe si ulikuwa unataka mimi niuwawe wewe, eti unamwambia Ashura aniwekee sumu kwenye chakula, sasa unashtuka saivi umeona mzimu au nsyuka? Si kila siku unaniona hapa, sasa unashtuka nini? Pona yako wewe ni kuachana na mambo unayoyafanya, kwanza kabisa uwafungulie wale uliowafungia”
Rose alikuwa akitetemeka tu, ila Salome aliendelea kuongea,
“Nipe ahadi utawafungua lini?”
“Nisamehe kwa hilo sitaweza kufanya, naogopa kufa”
“Kama wewe unaogopa kufa mbona unaua wenzio bila huruma? Kwani Moza alikukosea nini hadi ufurahie kifo chake?”
“Sikufurahia na wala sikutaka afe ila Moza alikuwa mbea ndio kitu ambacho sikukipenda”
“Mbea wa kuchunguza mambo yako mabaya unatyoyafanya, uliona nini kuacha baada ya kugundua ni mbea? Na hata hivyo, sababu mbea ndio utake afe? Angekuwa muongo je? Unajua tofauti ya mbea na muongo? Muongo huongea vitu vya uongo, ingawa kuna uongo wa aina mbili wa kubomoa na kujenga. Ila mbea anaongea vitu vya ukweli, tofauti ya ukweli na uongo ni moja tu, ukweli unauma ndiomana mtu mbea anaonekaga kuwa mbaya kuliko muongo. Ila siku ukikutana na mtu muongo na mnafki ndio utasema bora ya mbea.”
“Unanichanganya Salome, sipo hapa kuulizia tofauti ya mbea na muongo ila nipo hapa ili nipumzike kidogo, uwepo wako unanifanya nisiweze kupumzika”
“Toka lini wewe ukapumzika usiku? Huu si ndio muda wa kufanya mambo yako yasiyofaa? Halafu unataka mimi niende wapi nikapumzike pia?”
“Si kule chumbani kwa Moza”
“Chumba ambacho ulitaka kufanyia uchafu! Mimi niko makini kuliko wewe, niingie kwenye chumba ulichotaka kuzini na mlinzi wako!”
Kumbe Sara aliposikia mabishano sebleni alitoka, na muda huo ndio akasikia kuwa chumba cha Moza, mama yake alitaka kuzini na mlinzi wao. Alijikuta akisema kwa nguvu,
“Mama azini na mlinzi!”
Salome alijibu kanakwamba alitambua kuwa Sara angekuja na kuuliza hilo swali,
“Ndio, mama yenu alitaka kuzini na mlinzi kwenye chumba cha Moza. Muoneeni huruma mama yenu, kaeni nae chini muongee nae anapoelekea atazini hadi na maiti ili arekebishe nyumba yake. Rose nyumba imebadilika hii kama kitumbua tayari kimeingia mchanga, swala ni wewe tu kuachana na hayo unayoyafanya”
Rose aliinama chini kwani hapo ataliweza kudhihilika wazi kuwa anafanyaga mambo ya ajabu yani hata kujitetea hakuweza kabisa, alimuangalia mwanae kwa macho ya kuibia ila cha kushukia Salome alinyoosha mkono wake juu kisha Rose na Sara walijikuta wakilala pale sebleni.
 
SEHEMU YA 108



Ilikuwa ni siku nyingine, siku hii Neema alikuwepo kwenye kijiji cha mama yake na kuamua kwenda kutembelea kaburi la baba yake kisha kwenda kumsalimia aliyekuwa mama yake wa kambo, na hapo akakumbuka kuhusu Ashura na kuamua kuuliza.
“Eti mama, nilikuwa na ndugu yangu mwingine kwa baba?”
“Mmmh atoke wapi?”
“Eti alizaliwa na mama mwingine”
“Neema, baba yako alikuwa na mtoto mmoja tu ambaye ndiye wewe ila hakuwahi kuzaa tena mtoto mwingine”
Ikabidi Neema amueleze mama yake huyu jinsi alivyokutana na Ashura na jinsi alivyojitambulisha kwake kuwa ni ndugu yake, ila huyu mama alionekana kushangaa sana na kumwambia Neema,
“Sikia Neema, wewe ni mtoto wa pekee wa marehemu baba yako. Hajawahi kuwa na mtoto mwingine sehemu yoyote, alipatwa na ugonjwa wa ajabu baaa tu ya kuzaliwa wewe na hakuweza kuzalisha tena, hata mimi sijazaa nae sababu ya matatizo hayo. Sasa hizo habari za huyo ndugu yako wa kuitwa Ashura sizijui, ningekuwa simjui vizuri mume wangu sawa, ila nilimjua vizuri sana na alipenda watoto balaa kwahiyo ingekuwa huyo mtoto wake lazima ningejua. Labda huyo Ashura ni ndugu yako kwa mama yako huko ila baba yako hajawahi kuwa na mtoto mwingine zaidi yako”
Neema alishangazwa sana na ile habari na kukumbuka jinsi Ashura alivyoonyesha kumfahamu, na jinsi alivyoishi nae kama ndugu yake hadi ilifikia hatua ya kumpa hadi siri zake, alishangaa kusikia baba yake hakuwa na mtoto mwingine kwahiyo Ashura hakuwa ndugu yake ila akajiuliza kama ni kweli hakuwa ndugu yake sasa kwanini kamdanganya? Hakupata jibu ila huyu mama yake wa kambo alimsisitizia kabisa kuwa hakuwa na ndugu wa dizaini hiyo.
 
SEHEMU YA 109


Ana ndiye aliyemuamsha mama yake baada ya kumkuta anakoroma sebleni,
"Mama, mama imekuwaje tena?"
Rose aliamka ila alikuwa akishangaa shangaa tu, mara wale mapacha nao walikuja na kumuamsha Sara maana waliona mama yao akiamshwa na Ana. Walimuuliza dada yao kuwa kapatwa na nini hadi kalala sebleni, hakukumbuka kwa wakati huo, wakamsogelea na mama yao ila mama yao akawaambia wamuache na alitaka kwenda chumbani kwake ila aongozane na Ana, basi akaondoka na Ana na kuwaacha wale wengine pale sebleni.
Walibaki wakiendelea kumuuliza tu Sara kuwa ni kitu gani ila bado Sara hakuweza kuwajibu kwani hakuwa na jibu la imekuwaje kwa wakati huo, akili yake ilikuwa kama imesizi hivi kwa kiasi fulani, basi kaka zake wakamshauri kuwa akajiandae ili waondoke pamoja, nae Sara akainuka ili akafanye hivyo alivyoshauriwa na kaka zake.
alipofungua mlango wa chumbani kwake alishtuka sana kwani alimkuta Salome akiwa kitandani kwake amejilaza,
"Kheeee Salome!"
"Ndio ni mimi, mbona umeshtuka sana?"
"Sikutegemea kukukuta chumbani kwangu, umeingiaje bila ruhusa yangu!"
"Na wewe kwako kunataka ruhusa? kwani mama yenu kabla ya kufanya yote aliyoyafanya aliomba ruhusa?"
Ndio hapa Sara akajikuta akikumbuka mambo ya usiku na kujikuta akiuliza kwa makini,
"Ni kweli mama yangu alitaka kuzini na mlinzi?"
"Nadhani itakuwa vyema kama ukimuuliza mwenyewe"
Sara hakuendelea tena kuuliza chochote bali alitoka na moja kwa moja akaenda chumbani kwa mamake, na kugonga mlango ila alimkuta mama yake ndio alikuwa anatoka na Ana,
"Kheeee mama unaenda wapi?"
"Ndio salamu hiyo?"
"Hapana mama, shikamoo"
"Sina haja, Ana twende mwanangu"
Wakatoka na kumuacha Sara akiwa palepale mlangoni, ila alijaribu kuwafata nyuma ambapo aliwashuhudia tu wakiondoka bila hata kuwaaga wale mapacha waliokuwepo pale sebleni. Sara aliwasogelea kaka zake, ila na wao wakamshangaa kuwa hajajiandaa toka muda ule,
"Vipi bado hujajiandaa tu!"
"Jamani, si muda huu huu jamani!"
"Muda huu huu! Tumekusubiri hapa karibia lisaa limoja, unasema muda huu huu, kwakweli tunaondoka Sara"
"Jamani acheni masikhara, lisaa limoja limepita saa ngapi wakati ni muda huu huu!"
"Utatukuta ukija"
Na wao wakatoka na kuondoka kwahiyo wakamuacha Sara pale sebleni.
Muda kidogo Salome alitoka na kumwambia Sara,
"Ulitaka kuniacha peke yangu, hapana leo utashinda na mimi hapa"
Sara alimuangalia Salome na kuona kama mtu anayefanya mambo ya ajabu kwenye nyumba yao, ila hakumuuliza chochote zaidi ya kwenda chumbani kwake ili ajiandae na atoke hivyo hivyo.
Basi Sara akajiandaa na alipomaliza alitoka sebleni ilia toke nje na aondoke zake ila pale sebleni alikuwepo Salome ambaye alimwambia Sara,
“Si nimekwambia leo tunabaki wote!”
“Tunabaki wote kivipi? Mimi nina safari zangu bhana”
“Usiwe mbishi Sara, leo tunabaki wote humu ndani. Mimi leo siendi popote na wewe leo huendi popote. Tunabaki wote”
“Na wewe Salome aaah usinibabaishe bhana”
Sara akafungua mlango na kutoka nje, ila gafla akajikuta yupo chumbani kwake,
“Jamani si nimefungua mlango wa kutoka nje, iweje nimerudi tena chumbani?”
Hakuelewa aliona kamavile ni mchezo wa kuigiza, akatoka mule chumbani kwake na kwenda tena sebleni ambako alimkuta Salome amekaa kama kawaida na kuwaza kuwa mwanzoni laba ilikuwa ni mawazo yake ila si kweli kuwa alifungua mlango na kutoka nje, basi akajikuta akimuuliza Salome,
“Hivi tumeongea mimi na wewe muda si mrefu?”
“Ndio tumeongea, kwanini umeuliza?”
“Ulinikataza kutoka nje na ukasema tutabaki wote leo?”
“Ndio, leo tutabaki wote. Mimi siendi popote na wewe utabaki hapa na mimi”
Sara akamuangalia Salome bila ya kummaliza, kisha akaenda tena kufungua mlango wa nje na kujikuta yupo chumbani kwake tena. Akili yake sasa ikaanza kuchanganyikiwa kwani aliona kamavile ni mazingaombwe kabisa ukizingatia mambo hayo yalikuwa ni ya ajabu sana kwake, alijiuliza kuwa ule mchezo anafanyiwa na nani, kama ni Salome basi Salome ni mtu wa aina gani mwenye uwezo wa kukurudisha chumbani wakati ulikuwa ukitoka nje? Alifanya hivyo kama mara tano, na mar azote alijikuta akirudi chumbani. Uoga ukamshika na kuamua kukaa chini pale chumbani, akachukua simu yake na kumpigia mama yake.
“Mama, nipo ndani nataka kutoka ila nashindwa, eti kila nikitoka najikuta nimerudishwa chumbani”
“Mbona sikuelewi Sara, hebu nieleweshe”
“Sijui nikueleze vipi ila kutoka ndani ya nyumba siwezi”
Sara aliamua kama kumuelekeza mama yake kwenye simu ila bado ilikuwa ngumu kwa Rose kumuelewa mwanae, ikabidi Sara akate tu simu ya mama yake na kujibaza kwenye kitanda chake.
 
SEHEMU YA 110


Rose muda huu alikuwa mwenyewe akielekea kwa Yule mganga, siku ya leo alimuacha Ana aende shule kama kawaida halafu yeye ndio alienda tena kwa Yule mganga, na njiani nio alipigiwa simu na mwanae Sara akimueleza jinsi hawezi kutoka ndani ya nyumba. Hiki kitu kilimstaajabisha sana Rose ila alijisemea kuwa atamwambia na swala hilo mganga kwani bado hakukata tamaa kuwa ameshindwa kupambana na alioamini kuwa ni mzimu ndio unasumbua ingawa mganga alimuhakikishia kuwa sio mzimu.
Alifika kwa mganga na kama bahati leo hakukuta foleni kubwa kama alivyoena mara ya mwisho. Yule mganga kama kawaida alianza kwa kumuelezea yeye matatizo yake,
“Najua kuwa umekosea masharti, tatizo lako mdomo, yani huwezi kunyamaza kimya”
“Nisaidie mganga nifanyeje?”
“Sasa inatakiwa nitume kombora la kushambaratisha nyumba nzima, yani kila kilichopo ndani kombora langu litaenda kusambaratisha”
“Ndani ya nyumba yangu?”
“Ndio nyumbani kwako, natakiwa kutuma kombora yani kila kitu kinasambaratika mule nani. Nyumba inakuwa nyeupe kabisa”
“Sasa mwanangu Sara yupo ndani”
“Yeye hajatoka? Mpigie simu na umshawishi atoke”
“Ametoka kunipigia simu na amesema kuwa kila akijaribu kutoka anashindwa”
Yule mganga akaanza kuangalia kibuyu chake, kisha akatikisa kichwa na kumwambia Rose,
“Ndani kwako kuna mtu yani yeye anajua mipango yetu kabla hata hatujapanga, kwamaana hiyo amefanya makusudi mwanao asitoke ili kombora likitumwa basin a mwanao adhurike”
“Huyo mtu ni nani?”
“Namuona binti mdogo, mwenye sura ya kipole ila ana roho ya kikatili”
“Anaitwa Salome huyo mganga, sijui ni mchawi”
“Najaribu kuangalia nguvu alizonazo huyu binti nashindwa”
“Mwanzoni huyo binti niliweza kumdhibiti lakini saivi siwezi, nilikuwa najua tunasumbuliwa na Moza kumbe ni Yule Yule Salome. Je Moza yuko wapi?”
“Naona kuna nguvu za Moza zikifanya kazi kwenye nyumba yako ila alipo simuoni, sema sijajua huyu binti ana nguvu za aina gani. Nadhani ni vyema kama nitakuja kwako”
“Dah utakuwa umenisaidia sana, huyo mtoto Salome sikumpenda toka mdogo ila kila nikijaribu kumuua nashindwa”
“Basi tutafanya kitu, nitakuja nyumbani kwako”
Rose alifarijika sana kusikia kuwa huyu mganga atafika nyumbani kwake, na aliamua kumuomba kuwa waende nae siku hiyo hiyo. Alimuomba sana na hatimaye Yule mganga akakubali.
 
SEHEMU YA 111



Rose na mganga walijiandaa kisha wakaianza safari ya kwena nyumbani kwa Rose, walienda vizuri njia nzima hadi walifika getini kwa Rose na kufungua mlango na kuingiza gari ndani. Rose alimuonyesha Yule mganga alipo mlinzi wake, Yule mganga alitikisa kichwa tu.
“Basi jana alitoweka ndani huyo”
“Ni mazingaombwe tu hayo, ila usijali maana sasa kila kitu kinaenda kufika mwisho”
Basi wakashuka kwenye gari na kwenda kufungua mlango wa sebleni ili waingie nani, ila walipofungua tu walishangaa kujikuta wapo kibandani kule kule kwa mganga walipotoka.


Basi wakashuka kwenye gari na kwenda kufungua mlango wa sebleni ili waingie nani, ila walipofungua tu walishangaa kujikuta wapo kibandani kule kule kwa mganga walipotoka.
Yani kila mmoja alimuangalia mwenzie kwa mshangao, tena Rose akawa wa kwanza kumuuliza mganga,
“Mbona tumerudi tena huku huku wakati tulishafika mpaka nyumbani?”
“Hata mimi mwenyewe sielewi imekuwaje, ila ngoja nifanye dawa zangu kwanza. Naomba nisubiri nje”
Rose alitoka nje ya kibanda cha mganga huku akiangalia huku na kule, kwani mazingira ni hay ohayo na waliondoka kabisa hadi akakumbuka kuwa alimuonyesha mganga mlinzi na wakaongea halafu wameruishwa tena kule kule, kwakweli ilikuwa ngumu sana kwa Rose kuelewa.
“Kama ni uchawi basi huu ni wa viwango vingine, inamaana ni Moza au Salome! Yule mtoto atapata wapi nguvu za hivi? Anapata wapi uwezo wa kufanya makubwa haya? Ila sidhani kama ni yeye, ila na huyo Moza kwa staili hii ya kurudishwa na mganga tutaweza kupambana nae kweli? Kuna uwezekano wa kupambana na huyu kiumbe kweli?”
Alijiuliza sana huku akingoja mganga wake afanye dawa, na baada ya muda mganga alimuita tena Rose na kuanza kuongea nae,
“Unajua nguvu aliyokuwa nayo Yule binti nyumbani kwako ni kubwa mno, yani kiasi kwamba tunaweza siku nzima ya leo hadi usiku wa manane tukawa tunaenda kwako na kurudishwa hapa hapa”
“Sasa tutafanyaje?”
“Inabidi tutoe kafara”
“Kafara ipi?”
“Kafara ya damu, damu ya mtu unayempenda”
“Mmmh labda Patrick”
“Huyo ndio umpendae?”
“Ndio”
“Si kweli, mtu umpendae huwezi kukubali kwa haraka haraka hivyo atolewe kafara, huyo humpendi”
“Ya watoto wangu hapana, nimefikia hatua hii sababu yao. Nawapenda sana wanangu, tafadhari kafara isiwe ya wanangu, bora Patrick nipo tayari kumtoa”
“Upo tayari, ila kumtoa huyo mtu ni ngumu sana”
“Kwanini ni ngumu?”
“Huyo mtu analindwa sana, naona amezingirwa na ulinzi wa hali ya juu. Kumtoa kafara haiwezekani”
“Basi nimtoe mlinzi wangu”
“Hausiani na wewe huyo, bora siku ile ungekuwa umefanikisha zoezi la kulala nae ningekuruhusu kumtoa ila kwasasa haiwezekani. Inatakiwa ni mwanao tu”
“Tafadhari mganga bora tutafute mbinu nyingine, wanangu ndio maisha yangu. Tafadhari nisiwatoe kafara wanangu, nawapenda sana. Sijaweza kujiunga makundi ya wachawi wazoefu sababu ya kuogopa kutolewa wanangu, nawapenda sana”
“Unawapenda wanao ila unaishi na hatari ndani ya nyumba yako”
“Tujaribu tena kwenda mganga”
“Hata tukijaribu ni kazi bure, tutarudishwa tena hapa hapa, labda uende kwanza wewe halafu mie nije leo leo au hata kesho”
“Leo leo mganga, pale kwangu hapalaliki mganga, njoo leo leo”
“Ila ngoja nikupe onyo kabla hujaondoka”
“Onyo gani?”
“Msifanye sherehe yoyote pale kwako mpaka nije kufanya dawa, yani msifanye tukio lolote la sherehe sijui ya kuzaliwa, sijui kipaimara msifanye”
“Sinaga tabia ya kufanya sherehe nyumbani kwangu, hata birthday za wanangu huwa nikiamua basi naenda nao hotelini ila huwa hatufanyi sherehe nyumbani”
“Sawa sawa, nimekutahadhalisha kabisa kwani pale kwako hapatakiwi kusikika vigelegele vya shangwe kwa kipindi hiki mpaka nitakapofika na kufanya dawa, kuna nguvu kubwa sana pale kwenye nyumba yako”
“Nimekuelewa ila naomba ufike mapema iwezekanavyo”
“Usijali kwa hilo, ngoja tu nifanye dawa kwanza”
Bas Rose akamuachia mganga nauli ya kutosha kisha yeye akaanza safari ya kurudi nyumbani kwake kwa mara nyingine.
 
SEHEMU YA 112


Rose alifika kwake wakati usiku ulikuwa umeshaingia hadi akajishangaa kuwa ametumiaje muda hadi usiku umeingia vile, aliangalia saa yake aliona ni saa tatu ya usiku. Aliingia ndani na kukuta familia yake yote ikiwepo sebleni, halafu wakionekana kama walikuwa wanamngoja kwa shauku kwani alipoingia tu, wote wakapiga kelele,
“Surprise”
Rose akawashangaa sana kuwa ni surprise ya kitu gani, ila wote walianza kumuimba mama yao,
“Happy birthday to you, happy birthday to you, happy birthday dear mommy, happy birthday to you”
Na vigelegele vikasikika, yani Rose alichoka kabisa na kukaa chini kwani aliona wanae wakiharibu kila kitu. Alipokaa chini walidhani mama yao amevutiwa na walichokuwa wanafanya basi wakamuagiza Ana alete keki ambapo Ana alileta keki na kuanza kuimba,
“Kata keki tule……”
Ila mama yao alitahamaki sana na kusema,
“Hadi wewe Ana!”
Akaanguka chini na kuzimia kidogo, wote wakashtuka
“Jamani surprise gani hii kwa mama yetu mpaka amezimia!”
Wakaanza kumpepea, ila Salome akaenda kuchukua maji kidogo na kuja kumwagia kwahiyo Rose akazinduka na alivyozinduka tu watoto wake wakapiga kelele za shangwe kisha Sara akaanza kumwambia mama yao,
“Mama jamani usistaajabu kiasi hiko, watoto wako tunakupenda na hatujawahi kukufanyia kitu cha namna hii hata mara moja. Nashukurun leo Salome katukumbusha kitu hiki, kumbe alikuwa ananikataza kutoka sababu leo ni siku yako ya kuzaliwa. Natumai mama yetu umefurahi! Tumeandaa keki na vyakula tofauti tofauti vya kujipongeza kama familia”
“Naomba niacheni kidogo niende chumbani”
Kisha Rose akainukana kwenda chumbani kwake,watoto wake wakashangaa sana kwani mama yao hakuonyesha kufurahia lile jambo hata kidogo, na keki yao hakukata wala nini.
“Jamani, mama tumemfanyia kitu kikubwa hivi ila haonyeshi kufurahishwa nacho kabisa. Hebu Ana kaongee na mama”
Ana akaondoka na kuwaacha pale sebleni wakijadiliana kwanini mama yao hajapendezwa na kile kitu walichomfanyia, ila Salome akawapooza,
“Mnajua mambo ya kumshtukiza mtu huwa yanachanganya sana, itakuwa leo hakujipanga kabisa kuhusu sherehe labda ndiomana amestaajabu sana ila natumai kafurahia”
“Natumai pia kafurahia”
Kuhusu swala la kuandaa sherehe fupi ya kuzaliwa kwa Rose ni Salome aliipanga na wote walimsifia kwani hawakuwahi kumfanyia mama yao sherehe.
 
SEHEMU YA 113



Ana alimfata mama yake chumbani na kuanza kuzungumza nae, alimuuliza mama yake kwanini hajafurahishwa na ile surprise yao,
“Ana nilikuwa nakuamini sana, sikutegemea kama na wewe ungeweza kuingia kwenye mtego kiasi hiko jamani! Toka lini birthday yangu ikawa mwezi huu? Hivi kwanini kupena kuharibiana dawa? Nani ametoa wazo hilo?”
“Mama, mimi sijui. Kama kawaida nimerui kutoka shule na kuwakuta hapa nyumbani wamejipanga vilivyo kuwa kuna sherehe ya kuzaliwa wewe, mwanzoni nilibisha ila Sara alileta vitambulisho vyako na vilionyesha tarehe ya leo na mwezi wa leo, kwakweli hata mimi niliona ni wazo jema kukufanyia wewe sherehe ukizingatia hatujawahi kukufanyia hivyo. Siku zote huwa sishirikiani nao ila leo niliona ni jambo jema”
“Ana mwanangu, ni mtego huo unajua umeharibu dawa zangu na hivyo vigeregere vyenu! Yani mganga amenisisitiza sana kutofanya sherehe ya aina yoyote ile na kutokupiga vigeregere ila nimerudi nyumbani ndio kilichotokea”
Rose alianza kumueleza Ana kuhusu siku hiyo na jinsi walivyofika hadi hapo nyumbani na kurudishwa tena kwenye kibanda cha mganga, hadi mua huo kuamua kuja mwenyewe.
“Mama, kwamaana hiyo huyu Salome ni mchawi eeh!”
“Angekuwa mchawi tungemtambua, ni zaiddi ya mchawi halafu mganga amesema kuwa Salome ana nguvu nyingi sana, ambapo amejaribu kuziangalia ila hajaweza kuzichanganua”
“Mmmh sasa mama tutafanyaje?”
“Hata sijui maana masharti nishayaharibu tena, hapa hata sielewi nianzie wapi na niishie wapi”
“Ngoja nikatafakari mama”
Ana alitoka mule chumbani kwa mama yake na kwenda chumbani kwake kutafakari ambapo alijaribu kufanya dawa zake halafu kitu kikamuonyesha kuwa kama hawatokata ile keki waliyomuandalia mama yao basi wanaweza kidogo wakapona kwenye mtego, kwahiyo akainuka ili aende akaitupe ile keki, kufika sebleni alishangaa kuona dada yake Sara na wale mapacha walishaikata ile keki kitambo na walikuwa wanakula huku wakimuita walipomuona,
“Ana, keki tamu hiyo yani tamu sana”
“Sasa kwanini mmekata kabla mama mwenyewe hajakata? Nani katoa wazo la kuikata kabla ya muhusika kuja?”
“Salome katushauri tukate labda mama amechoka sana, ndiomana tumeamua kuikata na jinsi ilivyokuwa inatamanisha ndio kabisa yani”
Ana alisikitika sana kwani ndugu zake ndio wamekuwa rahisi kabisa kutekwa akili zao tofauti na mtu mwingine.
Akaamua kuichukua ile iliyobaki na kuibwaga chini, ila kabla haijafika chini alishangaa kuiona bado ikiwa kwenye sahani yake, kitendo hiko kilimchanganya sana ingawa ndugu zake walihisi kama Ana amewafanyia mazingaombwe hapo maana walishamjua kwa uchawi, ila hawakujua kama kitendo hiki kilimshangaza sana Ana na akajikuta akikimbilia chumbani kwa mama yake na kumueleza kuhusu dawa aliyokuwa akifanya na jinsi alivyopata ushauri wa kuhusu keki, na alichokiona sebleni.
“Mama, sasa nimeanza kuelewa kuwa ilikuwaje mkajikuta mnarudishwa kwa mganga wakati mlifika hapa nyumbani. Yani ile keki niliona kabisa nimeibwaga chini ila mara gafla naiona tena kwenye sahani, hapa naelewa kabisa kuwa inawezekana leo sio siku yako ya kuzaliwa ila hizi tarehe zimechanganywa changanywa ndani kwetu. Hivi mama hakuna kingine cha kufanya kweli kudhibiti hili maana naona mbona kama hao waganga wako wanashindwa”
“Hapana mwanangu, basi leo tulale wote tufanye vitu wenyewe tuone inakuwaje kuwaje”
“Mmmh mama sijawahi kufikiria kama kuna kiumbe kitakuja kunisumbua sumbua mimi”
“Usijali mwanangu, cha kuhakikisha ni kuwa kila mmoja akalale chumbani kwake halafu mimi na wewe tulale pamoja tushughulike na majanga ya humu ndani”
“Usijali juu ya hilo, yani wale wakimaliza tu kula najua kila mmoja ataena kulala chumbani kwake”
Basi Ana na mama yake wakakubaliana siku hiyo walale pamoja, kisha Ana akaenda chumbani kwake kujipanga kwaajili ya mashambulizi ya usiku huo.
 
SEHEMU YA 114


Pale sebleni wale mapacha na Sara, walikula ile keki, walikula chakula na kunywa kwa furaha sana yani siku hiyo walikuwa kama watu waliolewa vile. Kisha walienda kukaa kwenye kochi na kuendelea na maongezi, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa wao kufanya maongezi usiku huo sebleni maana muda kama huo kila mmoja kati yao huwa chumbani kwake anajiandaa na kulala ila siku hiyo walikuwa sebleni wakipiga stori, Salome nae alikuwepo sebleni ila alikuwa kimya kabisa kamavile hayupo.
Muda kidogo, wote pale sebleni walipitiwa na usingizi na wakalala pale pale kwenye makochi. Ana alikuja kuwaangalia kama washaondoka, alishangaa sana kuwaona bado wapo sebleni na ubaya wamelala kabisa, Ana aliwashangaa na kumsogelea Sara kisha kuanza kumtikisa,
“Sara, Sara”
“Niache bhana nina usingizi”
“Inuka ukalale ndani”
“Niache bhana”
Alienda kuwatingizha nao kaka zake walimjibu vile vile ila aliposogea ili amtingishe Salome alijikuta mkono wake ukishindwa kumshika Salome, kisha akainuka na kwenda kumwambia mama yake,
“Mwanangu hakuna namna hapo, ila Yule mganga nitaongea nae aje tu hivyo hivyo maana kila tunachokifanya hatuwezi”
“Sawa basi mama tusubiri usiku wa saa nane kasoro ndio mzuri ili na sisi tujaribu ya kwetu”
“Sawa mwanangu”
Walikazana kufanya mambo mengine huku wakisubiria usiku wa saa nane kasoro ufike, ila kila walipoangalia saa iliwaonyesha kuwa ni saa sita yani kila walipoangalia iliwaonyesha ni saa sita. Kuja kutahamaki walisikia jogoo akiwika na walipoangalia saa muda huo ilionyesha ni saa kumi na moja alfajiri,
“Mama tumepitiliza wapi?”
“Kivipi? Muda si bado haujafika”
Ana akamuonyesha saa mama yake, ambaye alishangaa pia kwahiyo siku hiyo wamefanya mkesha usiokuwa na faida yoyote ile. Ila mama yake akamuahidi Ana kuwa siku hiyo watahakikisha kila kitu kitafanikiwa,
“Asubuhi ya leo naenda kuongea na dereva tax amlete Yule mganga hapa kwa gharama zangu, najua akiletwa na mtu mwingine haitotokea zengwe kabisa. Atafika na mambo haya yatafika mwisho”
“Itakuwa vizuri mama, kwahiyo leo nisiende shule eeh!”
“Ndio usiende shule”
Rose alikubaliana pale na mwanae Ana jinsi atakavyofanya siku hiyo.
 
SEHEMU YA 115



Kulipokucha kabisa, pale sebleni kila mmoja aliamka na kujinyoosha huku wakiwa na uchovu wa hali ya juu na kila mmoja kusema kuwa hatotoka kwa siku hiyo, watabaki tu nyumbani. Pacha mmoja alimwambia dada yake,
“Leo nitamwita na wifi yako aje umfahamu”
“Sawa ila mama asijue kama ni wifi”
“Mama atajulia wapi? Hakuna kumwambia, atajua siku ya ndoa”
Wakawa wanacheka pale, mama yao nae alitoka sebleni wakamsalimia akaitikia na kutaka kwenda nje. Ila Salome alimuuliza,
“Mama, unataka kwenda wapi?”
“Safari zangu hazikuhusu”
Rose akataka kufungua mlango, ila kabla hajafungua Salome alimwambia,
“Usihangaike, mgeni wako nimekuletea”
Kisha Salome ndio akaenda kufungua mlango na mara akaingia Yule mganga.
 
Back
Top Bottom