MIMI NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA
★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Sikuchukua muda mrefu sana kuondoka huko Kivukoni baada ya Bertha kuondolewa mahakamani, nikapita kwenye mgahawa mzuri huko Kigamboni na kupiga ugali kwanza, kisha nikaingia kwenye saluni nzuri kupunguza nywele na ndevu kwa mwonekano niliopendelea, halafu ndiyo nikaendelea na safari ya kurudi Mbagala.
Kevin alikuwa amenitafuta, yule bwana wake na dada yangu, akiwa anataka kujua kama nilimuungishia mitambo kwa Jasmine na nini, lakini nikamsihi tu amwache Jasmine kwanza mpaka ajifungue, ndiyo mambo mengine yangefuata. Jambo bora ambalo angetakiwa kufanya ni kutoacha kumwonyesha dada yangu kuwa alimjali kwa kutumia njia mbalimbali, na hata siku ambayo Jasmine angejifungua, angepaswa kwenda hospitali kuwa pamoja naye haijalishi nini kilikuwa kimetokea baina yao. Akaonekana kuridhia hayo.
Nimekuja kufika Mzinga ikiwa imeshaingia saa moja, na nilikuwa nahisi uhitaji wa kuingia kwenye gym kupasha kidogo maana nilikuwa nimekosa kufanya hivyo kwa siku chache. Kulikuwa na gym fulani ndogo maeneo hayo, na nilijua ingekuwa wazi mpaka kufikia mida ya saa nne, hivyo nikaamua kuelekea huko kwa Ankia ili nikabadili mavazi na kugeuka tena niwahi gym kupiga tizi, halafu ndiyo ningeenda kupumzika sasa. Haya mazoezi yangesaidia zaidi mwili kujenga uimara baada ya ile ishu ya sumu hapo juzi, na misuli iwe fiti kwa ajili ya kazi!
Nilipofika kwa Ankia sehemu ya getini, nikaliona gari lake Miryam pale nje ndani ya geti la nyumba yao, kumaanisha bibie alikuwa amesharejea, nami nikaamua kwenda kwanza hapo kuchungulia hali ilikuwaje kwa sasa. Nakumbuka nilimwacha huko dukani kwake muda ule akiwa na mambo mengi sana kichwani, kwa hiyo nikataka kujua tu kwa wakati huu angekuwa vipi kiuhusiano pamoja na mama mkubwa wake. Nilipita tu getini na moja kwa moja kuelekea ndani kwao, nami nikakuta sebule ikiwa imejaa kiasi.
Walikuwepo mama wakubwa hapo, Mariam, Shadya, Ankia, pamoja na mwanadada mwingine rika kama la Mariam tu, ambaye sikumfahamu. Kilichofanya sebule ionekane kujaa ilikuwa ni rundo la nguo zilizotandazwa kwenye kimkeka hapo katikati, huku wanawake wakiwa wanachukua hii na ile kwa kubagua na kuchagua. Zote zilikuwa za kike, nzuri, na zilikuwa spesho. Mariam, huyo mwanadada, na Ankia walikuwa wamekaa hapo chini na kuchukua nguo hii au ile, wakiwapa wengine waangalie na kuchagua, nami nikawa nimemwona bibie Miryam pia.
Alikuwa amekaa upande wa dining, peke yake, akiwa anafanya kazi fulani kwenye laptop, na alionekana makini kweli. Ujio wangu hapo ukawachangamsha zaidi wanawake hao sebuleni, nami nikamwona Miryam akinitazama kwa utulivu, halafu akaachana nami na kuendelea na mambo yake. Mariam alikuwa ananionyesha nguo ambayo alitaka kuchukua, na Ankia akawa anamwambia asiwahi maana zilikuwepo nyingine nzuri kwa hiyo angetakiwa kuchangua kwa umakini.
Shadya ndiye aliyekuwa akiongea zaidi kusifia nguo hizo na aliyofanya mpaka kuzileta hapo kwa ajili ya wengine, na kila mmoja wao angetakiwa kuchagua moja tu kwa ajili ya kuvaa kwenye send-off siku ya kesho. Nikamuulizia Dina kwake, nikisema Tesha aliniambia kwamba angekuja hapa leo pamoja naye Shadya, naye ndiyo akasema hapana, hakuweza. Tena Tesha alikuwa ameenda huko kwao na akina Doris pamoja na Dina leo baada ya kuitwa akawasaidie na vitu fulani kwa ajili ya maandalizi, kwa hiyo jamaa angerejea baadaye sana nadhani.
Nilimwangalia Bi Jamila na kuona aina fulani hivi ya uchangamfu ndani yake alipokuwa akisemeshana na wengine hapo. Na yeye alikuwa amenikaribisha kabisa eti nijiunge nao kuchagua nguo, nami nikacheka kidogo kuneemesha utani wake. Alikuwa sawa zaidi kihisia wakati huu, na hiyo ikanifanya nitambue kwamba Miryam angekuwa amesawazisha ishu zao kwa njia nzuri. Nikawapita wanawake wengine na kuelekea upande wa dining, ili nimsalimie binti maringo, na alikuwa bize kweli yaani asingeweza kuhamisha macho yake kutoka kwenye laptop.
Hivyo, nikafanya kusogea mpaka kufikia sehemu ya kiti alichokalia, halafu nikaegamia meza kwa mikono yote na kujifanya kama naangalia kwa umakini yale aliyokuwa akifanya humo kwenye laptop yake. Hakuwa amebadili mwonekano wake kimavazi toka nilipomwona ile mchana, kumaanisha aidha ndiyo angekuwa amefika nyumbani muda si mrefu sana, ama hakujisikia tu kubadili mavazi na kuamua kufanya kazi kwanza.
Baada ya mimi kusogea hapo karibu yake, akawa ameniangalia kwa jicho makini usoni, nami nikamtazama kwa chini. Si nilikuwa nimesimama huku yeye amekaa, kwa hiyo nikawa namwangalia kama vile natazama mtu mfupi kwa nyodo. Nafikiri aliona umakusudi wangu wa kuja mpaka karibu yake kuwa uchokozi, naye akapeleka macho yake kuwaangalia wengine. Hakuna mtu aliyejisumbua kutazama huku zaidi isipokuwa tu yule mwanadada mgeni, ambaye aliniangalia mimi zaidi na kukwepesha macho nilipomtazama. Miryam akaniangalia tena kwa umakini, mimi nikianza kumtazama kizembe, naye akarudisha macho yake kwenye laptop.
Nikajiinamisha zaidi kama naangalia kwa umakini sana vitu alivyoandika, naye akaacha kubofya keyboard kwa ufupi. Nikajiweka kama mwanzo tena, na najua tayari nilikuwa nimeshamchanganya maana alikuwa akiandika kitu kama barua ya masuala ya kikazi, siyo duka wala nini, yaani zile kazi rasmi, naye akawa anatafakari zaidi huku akijaribu kunipotezea, lakini akashindwa.
Akawaangalia wengine kiufupi, kisha akanitazama na kwa sauti ya chini sana akasema, "Nini wewe?"
Nikamuuliza, "Nini na wewe?"
Akasonya kidogo na kusema, "Usinichanganye."
Nikaendelea tu kumwangalia kizembe.
"Em' toka hapa... nenda huko," akasema hivyo.
Nikashindwa kujizuia kutabasamu, maana alikuwa ananiongelesha kama vile mimi mtoto.
Akaniangalia na kuuliza, "Hujanisikia au?"
"Nimekusikia, ila ni jeuri tu," nikamwambia hivyo.
Akanitazama usoni kiukali kiasi.
Nikatabasamu na kuacha kuegamia meza, naye akarudisha umakini wake kwenye laptop tena. Nilikuwa nafikiria nimuulize kuhusiana na suala la Bi Jamila, lakini sidhani sana kama angekuwa na uhuru wa kunielezea hayo mambo ambayo kwa mtazamo wa haraka, hayakunihusu. Najua tayari wangekuwa wameshaongea, na ningemchokoza zaidi kwa kumwambia mimi ndiyo wa kushukuru maana nilimpa ushauri na nini, lakini nikaona nivunge tu, na labda nimwache kwanza.
Lakini kabla sijamwacha kwanza, jambo fulani likaingia akilini, hivyo nikaegamia meza tena na kumwambia, "Kuna kitu nilikuwa nataka nikuulize."
Akaendelea kuangalia laptop tu huku akibofya-bofya herufi kwa umakini.
Nikasema, "Eti... ile juzi Festo alipokuja...."
Miryam akaacha kubofya na kunitazama usoni kwa utulivu.
"Alikuwa amekuja kukwambia nini?" nikamuuliza hivyo.
Akaendelea kuniangalia machoni kwa umakini tu.
Nikaweka uso kimchezo na kusema, "Siyo kwamba nataka kuweka cheat kwenye riadha yetu ya kuku-win..."
Miryam akaangalia pale sebuleni baada ya mimi kusema hivyo, akiwa anahofia wengine wangesikia maneno hayo, na alipoona wengine hawana habari akanitazama tena kiumakini.
Nikatabasamu kiasi na kusema, "Usijali, hawajasikia."
"Kwa nini unaniuliza hivyo?" akauliza hivyo kwa sauti ya chini.
"Nimetaka tu kujua... kama bado nina competition na nini, ili niwe fiti zaidi, maana...." nikasema hivyo na kumtikisia nyusi kidogo.
Akapiga ulimi kidogo na kuangalia laptop yake tena.
Nadhani hakutaka kumeongelea jamaa, na mimi kwa kuelewa nikaona tu nimwambie, "Basi, haina shida. Siyo lazima ujibu usipotaka, me mwenyewe...."
"Alikuja kuniaga," Miryam akanikatisha kwa kusema hivyo.
Nikamtazama kwa umakini, nami nikamuuliza, "Kukuaga ya... ya kwenda wapi?"
"Kwenda nje ya nchi. Alisema ana safari ya kikazi," akaniambia hivyo bila kuniangalia.
Nikatazama pembeni kwa ufikirio.
"Kuna nini kwani?" Miryam akauliza.
Nikamtazama na kukuta ameniangalia kwa udadisi, nami nikajitabasamisha na kusema, "Hamna kitu... nilitaka tu kujua. Nimepata na relief, maana... si unajua, wivu na nini..."
Nilisema hivyo na kumpandishia nyusi tena kichokozi, naye akaonekana kukerwa hata zaidi na kuifunika laptop yake huku akiniangalia usoni kwa umakini. Nikasimama vizuri kabisa na kumwangalia kimaswali, naye akasimama pia bila kuacha kunitazama. Ilikuwa kama vile anataka kunipiga eti! Kisha ndiyo akatoka hapo sehemu ya dining na kwenda kujiunga na wengine, akiketi kwenye mkono wa sofa karibu na Bi Zawadi na Bi Jamila.
Kwa hiyo hapo nikawa nimepata uhakikisho namba mbili kwamba Festo angekuwa ameondoka kweli. Kama alikuja kumuaga Miryam siku ile, basi uwezekano wa asilimia hamsini wa yeye kuwa ameondoka kabisa uliwezekana. Hizo hamsini zilizobaki ndiyo bado nilitakiwa kuzithibitisha, kwa kuwa sikutaka kuamini kiurahisi tu kwamba huyo jamaa angeondoka ile ya kuondoka kabisa, hapo lazima kulikuwa na mguso fulani hivi wenye dukuduku, kama tu madam Bertha kukiri leo mahakamani kwamba alikuwa na hatia. Nilipaswa kuwa na UHAKIKA. Haya mambo haya!
Basi, nikasogea tu usawa wa ukuta kukaribia sofa na kuegamia hapo, nikiwaangalia wanawake walipokuwa wakibagua-bagua nguo kabla sijatoka kwenda gym kwanza. Ankia na Shadya walikuwa wanasemana kweli, kwamba Ankia ana unene halafu amechagua nguo inayomtoshea Mariam basi lilikuwa ni suala lililomkera Shadya. Bi Zawadi na Mariam walikuwa wakicheka sana kuwasikiliza wanawake hao walivyoanza kuchambana, kiutani lakini, naye Bi Jamila akawa amevuta nguo moja na kumwekea Miryam usawa wa kifua chake.
Mwanamke huyo akawa anamwambia alichukue hilo, likiwa ni gauni, maana bado hakuwa amechangua nguo ya kuvaa na uchaguzi hapo ulikuwa mwingi sana, na Miryam akatabasamu na kuanza kuliangalia. Lilikuwa la kijani, likionekana kuwa refu na laini, na wakina Ankia wakawa wanamwambia achukue hilo maana ni zuri pia. Katika kuligeuza-geuza kabla hajaamua, Miryam akawa ameniangalia, nami nikamtikisia kichwa kidogo sana huku nikikaza macho kama kumwambia hilo gauni halikumfaa. Yaani wote walikuwa wameliruka, halafu yeye ndiyo wamwambie litampendezea? Hapana.
Baada ya mimi kumfanyia hivyo, akaacha kuniangalia huku akionekana kukosa amani, lakini akamwambia Bi Jamila kwamba angetafuta lingine maana aliona kama hilo haliendani na rangi ya ngozi yake. Mama mkubwa wake akaelewa, nao wakaendelea kuchambua nguo zingine. Zilikuwa nyingi, yaani nadhani Shadya alileta duka lake lote hapo, na sekunde chache kupita nikaona Miryam ameshika nguo nyingine yenye rangi ya njano na kuanza kuipima-pima kwenye mwili wake. Kwa mtazamo wangu, sikuona kama ilimfaa, lakini sikutarajia afanye kitu fulani baada ya kuishika hiyo nguo.
Akaniangalia usoni, zamu hii siyo ile ya kinagaubaga, yaani aliniangalia huku ameishika nguo hiyo karibu naye kama vile kuniuliza 'na hili?' Upesi nikatikisa kichwa kukataa kwamba halikumfaa, halafu nikajikausha. Nikaona anaweka uso fulani wa kuvunjika moyo, halafu akairudisha na kuanza kutafuta nyingine. Nikazuia tabasamu langu lisionekane wazu huku nikimtazama kwa umakini, naye akapata nguo nyingine tena na kurudia kunitazama usoni. Nikatikisa kichwa kumkatalia, naye akaweka ule uso kama vile ananiuliza 'unataka ipi sasa?' Ah!
Yaani alikuwa ameshajisahau, ikawa kama vile anataka mimi ndiyo nimchagulie nguo. Nilisikia raha! Ilikuwa kama zile pindi unaenda na mtu wako dukani, anavaa na kubadilisha nguo, halafu anakuonyesha ili umwambie ipi imemfaa, yaani Miryam ndiyo alinipa hilo vibe sasa hivi. Halafu akawa anajifanya kama vile hajali sana mawazo yangu, kama vile maamuzi ni yake, wakati kila aliponyanyua nguo angenitazama na mimi ningemkatalia, kisha angerudi kutafuta zingine. Nilipenda sana hii.
Katika kugeuza-geuza nguo, nikaona moja iliyokuwa na rangi ya maroon, ikionekana kuwa gauni laini, yenye urembo wa vitu vilivyomeremeta. Niliipenda sana hii rangi, na najua ingependezea kwenye ngozi ya bibie Miryam maana alikuwa mweupe. Nguo yoyote ile ingempendezea, lakini najua hii ndiyo ingemfaa. Nikamwonyesha Mariam nguo hiyo na kumwambia ampe dada yake ili aiangalie, naye akampa. Karibia wote waliisifia, wakisema ni nzuri sana, naye Miryam akawa anaitazama kwa ufikirio. Akaniangalia usoni, mimi nikiwa natabasamu, halafu akaikunja tu na kuiweka pembeni, kisha akaendelea kubagua nguo zingine.
Eti alikuwa anajifanya haitaki ili aniumize sijui? Haya bana. Nikatabasamu tu na kisha kuwaaga wanawake wote kwa wakati huu, nikisema naelekea Mzinga mara moja kisha ningerejea, nami huyoo nikasepa. Mambo mengi yalikuwa yanaingiliana sana, lakini haikuwa imefichika kwamba uhusiano wangu na Miryam ulikuwa umeshaanza kuimarika hata kabla ya kuwa amekubali kuuanzisha. Alijali kile ambacho niliwaza juu yake, kwa hiyo najua ingekuwa rahisi zaidi kumvuta kwangu kihisia. Yajayo kwa upande wake yakaonekana kuwa yenye kufurahisha, ningetakiwa kuendelea kuyasubiri.
★★★
Bwana, siku ya Alhamisi ikawa imefika. Hiyo jana mambo hayakuwa mengi sana baada ya mimi kutoka gym kupasha na kurudi tena kwa Ankia, tukala, tukapiga story, kisha tukapumzika. Leo hawa viumbe wangekuwa na mihemko ya hali ya juu kwenda huko kwenye kitchen party kuonyeshana nani kapendeza zaidi ya bibi harusi mtarajiwa na kusemana wee, kwa hiyo Ankia akawa ameamka mapema na kama kawaida kupiga usafi wa ndani. Mimi sikuamka mapema sana, mida ya saa tatu asubuhi, halafu nikaendelea kukaa kitandani mpaka saa nne.
Aliyekuja kunitoa chumbani ilikuwa ni binti Mariam mwenyewe. Alikuja kututembelea nakwambia, na katika hali ya kushtukiza yaani aliingia chumbani na kukuta niko kifua wazi, kwa hiyo nikavaa T-shirt upesi na kwenda sebuleni pamoja naye. Mariam alikuwa ameshaanza kutulia sana kiakili, aliongea vizuri, alikuwa na utani, na alielewa vitu vingi sana. Nilianza kuona ule utu uzima ndani yake, japo kwangu angeendelea kuwa kabinti. Alikuja wakati ambao Ankia alikuwa ameshaandaa chai, lakini tulipokunywa, yeye hakunywa kwa sababu tayari alikuwa amepata kiamsha kinywa kwao.
Ndiyo akawa ametuambia kwamba, Miryam hakwenda kazini leo. Akasema yaani wote walikuwepo kwao, na ndiyo maana alikuja ili kutuchukua twende naye ili kujiunga na wengine kufurahia ushirika pamoja. Lilikuwa ni wazo zuri sana, na kwa kufikiria namna shangwe ya siku nzima ya leo itakavyokuwa, Ankia akaamua kutokwenda dukani kwake pia ili awe pamoja nasi.
Ikawa imeenda hiyo, yaani hatukuchukua muda mrefu sana kuanza kujiandaa, mimi sanasana kwa sababu nilihitaji kuoga kabisa, na mpaka nimekuja kumaliza kuvaa na nini, tayari Ankia na Mariam walikuwa wameshaenda pale kwao na binti. Nilivalia kawaida tu, T-shirt nyeusi ya mikono mifupi na jeans, kisha nikafunga milango na kuelekea huko pia ikiwa imeshaingia mida ya saa sita mchana.
Kweli nikawakuta wote wakiwepo ndani, sebuleni. Bi Zawadi na Bi Jamila walikaa kwenye sofa lao kama kawaida, Shadya na Ankia walikaa kwenye sofa upande wa kulia, na pale ambapo Mariam alipendelea kukaa na mimi, alikuwa amekaa na bibie Miryam pamoja na Tesha. Jamaa akasimama, nasi tukasalimiana vizuri kishkaji, halafu nikawasalimia na wengine pia vizuri. Wote walivalia kiukawaida wa nyumbani tu, na bibie Miryam alikaa kwa kukunja nne huku akiwa bize na simu yake. Nilipenda namna ambavyo alikuwa amezilaza nywele zake upande mmoja wa uso karibia kuficha jicho, na alikuwa ametulia tu kama vile hayupo.
Tesha akaniachia hiyo nafasi aliyokuwa ameketi na kukaa kwenye mkono wa sofa pembeni yake Shadya na Ankia, nami nikakaa pembeni yake Mariam, akiwa katikati yangu mimi na Miryam. Bibie akanyanyuka tu na kuelekea jikoni kwanza, nikiibia nyendo zake kwa kuangalia huko nyuma. Mashallah! Nikarudisha umakini wangu kwa wengine, Mariam akisema angependa sana tukiwa hapo pamoja mpaka jioni, yaani mimi na Ankia tusiondoke, nasi tukamwambia asiwaze. Hata nikamwambia tungecheza na mchezo wa pamoja maana sote tulihitaji kuburudika.
Tesha akawa anatuambia jinsi mambo yalivyoenda huko ambako kitchen party ingefanywa, maeneo ya Kigamboni kwenye ukumbi fulani maridadi, na ndiyo Miryam akawa amerejea tena na kuketi. Mariam akanyanyuka na kwenda kutoa miwa kwenye friji, ambayo imeshakatwa-katwa na kuwekwa kwenye chombo, kisha akaileta hapa kati na kuweka chombo hicho mezani, nafikiri wote tule taratibu. Shadya yeye akakichukua na kukibeba mikononi, akianza kula miwa yeye mwenyewe, na jambo hilo likaonekana kumkera Mariam kiasi.
Sisi wengine tukaendelea na story tu bila kujali kuhusu miwa, lakini niliona jinsi ambavyo Mariam alikuwa akimwangalia Shadya kwa njia fulani kama vile hataki yaani, nami nikamtazama Shadya na kumwona akiendelea kupakia vipande vya miwa na kuweka mabaki pembeni ya chombo hicho. Binti alikuwa amechomwa sana.
Nafikiri Miryam akawa ametambua hilo kwa kuwa akamshika mdogo wake kichini-chini na kumuuliza karibu na sikio lake, "Nini Mamu? Mbona umekunja sura?"
Nikajifanya kuendelea kuwatazama wengine, lakini nikamsikia Mariam akisema, "Dada... mimi... naweka miwa tule wote, halafu shangazi kabeba sahani yote..."
Nikajikaza nisicheke kwa kuibana midomo yangu.
Miryam akacheka kidogo kwa pumzi, naye akamwambia, "Usijali, mingine si ipo kwa friji? Tutaweka baadaye, mwache aenjoy. Unajua ana katumbo kama ka kiboko."
Nikamwangalia Mariam kwa ufupi na kukuta amekunja midomo yake kwa kukerwa. Kama katoto yaani!
Tesha akawa anasema, "Kitchen party ya Doris itakuwa noma. Yaani walipokuwa wanapafanyia maandalizi, we!"
"Wanaandaa mambo motomoto eh?" Bi Jamila akamuuliza.
"Sana," Tesha akasema.
"Eeh, wanapamba vizuri. Nimeona huo ukumbi kwenye status yake Doris," Ankia akasema hivyo.
"Umeona?" Tesha akamuuliza hivyo.
"Eeh. Kuna ka gharama ka juu kametumika, na hiyo ni kitchen party tu," Ankia akasema hivyo.
"We! Acha kabisa! Mume wake anamgharamia. Pazuri yaani, mpaka natamani na mimi kwenda," Tesha akasema.
"Acha uhuni Tesha. Hiyo ni ya wanawake, uende kufanyaje?" Shadya akamwambia hivyo huku akitafuna miwa yake.
"Si ndo' point yenyewe, au? Oya JC, tuvae magauni mwanangu tukavamie hiyo," Tesha akasema hivyo.
"Acha ujinga," nikamwambia hivyo, na mama zake wakubwa wakacheka kidogo.
Nikamwangalia Miryam pembeni na kukuta anatabasamu kidogo, lakini alipohisi kwamba namwangalia, tabasamu hilo likakoma.
"Ana akili haina breki huyu," Shadya akasema hivyo kumwelekea Tesha.
"Halafu na yako? Hivi wewe... miwa yote unakula mwenyewe, sisi hutuoni?* Tesha akamwambia hivyo.
"Kwani imeisha? Si ipo mingine? We' unakuaje, kila kitu nikifanya kwako kibaya tu," Shadya akalalamika.
"Eh, basi yaishe. Kamua mama... tafuna mpaka bakuli," Tesha akamwambia hivyo.
Wengine wakacheka kidogo, nami nikamwona Miryam anamnyooshea kidole Tesha kama kumwonya aache kweli, kimasihara tu yaani.
"Ee, JC..." Shadya akaniita.
"Naam?" nikaitika.
"Wee... si umesema kuna mchezo unataka tufanye? Uko wapi? Tuchangamshe basi kabla ya msosi..." Shadya akaniambia.
"Eeeh, JC. Tucheze sasa," Mariam akaniambia hivyo pia kwa shauku.
"Ahah... eh ndiyo, sawa. Inabidi niwaelezee unavyochezwa kwanza," nikamwambia hivyo.
"Yaani hawa watu wanapenda michezo!" Tesha akasema hivyo kikejeli.
"Kama we' hupendi, toka," Shadya akamwambia hivyo.
Wengine wakacheka kidogo, naye Bi Zawadi akasema, "Sawa baba, tupo tayari. Tuchangamshe na sisi kama Mamu."
Mariam akasogea mbele zaidi ya sofa ili aniangalie vizuri.
Nikawaambia, "Huu mchezo unaitwa charade, wa wazungu hao. Huwa unachezwa hivi; si unaona sisi wote hapa? Mmoja wetu anasimama hapo mbele akiwa na wazo la kitu fulani kichwani, kitu chochote kile yaani... lakini hatakiwi kutuambia hicho kitu ni nini. Anachotakiwa kufanya... ni kukiigiza hicho kitu kwa ishara za mikono na mwili, lakini yaani hapaswi kuongea mpaka mmoja wetu sisi aliyekaa akiseme kwa kupatia..."
"Aaa... hiyo ngoma naijua..." Tesha akasema hivyo.
"Hata me naujua, wanachezaga wazungu. Ni mzuri kweli huo mchezo," Ankia akasema.
"Hata mimi naujua. Nime..nimeuona... aa... aliucheza Olaf na Anna..." Mariam akasema hivyo.
"Enhee, huo huo Mamu. Olaf akatembea kama Elsa, eh?" nikamsemesha namna hiyo.
"Eeeh... hivi... oooh Elsaaa!" Mariam akasema hivyo huku akijaribishia kutembea kama miss.
Sisi wote hapo tukacheka kwa pamoja, naye binti akarudi kukaa sofani.
Nikasema, "Safi sana. Ila sasa... huwa una kanuni zake, lakini mimi nimeubadilisha kidogo. Hapa tutaucheza kwa njia tofauti."
"Enhe..." akasema hivyo Bi Jamila.
"Hapa hatutaucheza kimashindano, ila kidarasa zaidi. Yaani... unapaswa ufikirie kitu fulani unachopenda au kuchukia, ni wewe tu... halafu ukishafanya charade ya hicho kitu tukakipatia, unapaswa uelezee kwa nini umeamua kucheza na hicho. Sijui inaeleweka?" nikawaambia hivyo.
Wakaanza kuonyesha uafiki wa wazo hilo, nami nikamwona Miryam akiwa ananitazama kwa umakini. Ni kama alikuwa ananisoma, na kweli nilikuwa nimepanga kufanya jambo fulani kumwelekea yeye mwenyewe.
"Huo mchezo mzuri. Me kwa maigizo si mnanijua?" Shadya akasema hivyo huku akiendelea kula miwa.
Bi Zawadi akasema, "Yaani... kama niseme, nimechagua jagi... akilini... nikafanya parade..."
"Siyo parade ya mstalini, ni charade..." Bi Jamila akamkatisha.
Bi Zawadi akamkata jicho la kukerwa, huku sisi wengine tukicheka, naye akasema, "Eeh, charade. Mkipatia yaani, kwamba ni jagi... natakiwa nielezee kwa nini nimechagua jagi, si ndiyo?"
"Ndiyo maana yake, cheupe wangu," nikamwambia hivyo.
"Hapo sawa, nimeelewa handsome wangu," Bi Zawadi akasema.
"Okay, poa. Wote tumeelewa. Tuanze sasa. Nani anaanza?" Tesha akasema hivyo.
Mariam akanyanyua mkono wake juu na kusema, "Mimi... mimi, mimi, mimi..."
"Ahahah... haya sawa, anza," nikamwambia hivyo.
Mariam akanyanyuka na kusogea mpaka ile sehemu ya wazi katikati kuelekea upande wa vyumbani na jikoni, naye akatugeukia na kujiweka tayari kwa kuisawazisha miguu yake. Wengine walikuwa wameshaanza kucheka kabla hata hajaanza kufanya charade, ndiyo akakunja ngumi zake, akatanua mikono, kisha akavimbisha mashavu yake.
Akawa anaigiza kitu fulani ambacho kwa haraka kilimfanya kila mtu aelewe kwamba aliigiza ubonge na vitambi, nasi tukawa tunataja mabonge wote tuliofahamu. Mimi nikasema Kingwendu, mwingine akasema JB, huyu Big Show, mwingine Lizzo, mara Mashalavu, lakini inaonekana tukawa hatupatii maana binti aliendelea tu kuigiza. Akawa anatoa ishara za kuogelea na kupiga mihayo kwa nguvu sana, nami nikamwona Miryam anacheka kwa pumzi na kufunika mdomo wake.
Wengine walipokuwa wanajaribu kupatishia ni mtu gani mwenye kitambi anayeogelea, nikasema inaonekana Miryam alikuwa ameshapata jibu na ndiyo maana hata hakuwa akiongea lolote. Mama zake wakubwa wakamwambia aseme mawazo yake pia, asikae kimya tu, naye ndiyo akajituliza na kumtazama mdogo wake.
Mariam akiwa anaendelea kuachama-achama, Miryam akasema, "Kiboko."
Mariam akaanza kurukaruka kwa furaha huku akimsonta dada yake kuonyesha kwamba amepatia.
Sisi wengine tukacheka kidogo, naye Tesha akasema, "Jah! Yaani kumbe kiboko? Af' kweli, huwaga yanaachama mno... na yana shepu! Dah! Point moja kwa da' Mimi hahah... hii kitu raha sana."
Ankia akamuuliza Mariam, "Kwa nini umemfikiria kiboko Mamu?"
"Kwa sababu ya shangazi," Mariam akasema hivyo.
Shadya akasitisha kuendelea kutafuna miwa mdomoni mwake na kuuliza, "Mimi? Me nina undugu gani na kiboko Mamu?"
Maana ya kile ambacho Mariam alikuwa anawaza ikawa imeniingia akilini pia, nami nikamwangalia Miryam na kukuta ameficha tabasamu lake kwa kiganja. Nikajikaza nisicheke.
Mariam akasema, "Unakula sana. Una tumbo kama la kiboko."
Kicheko cha pamoja hapo kilikuwa cha hali ya juu baada ya binti kusema hivyo, hasa Tesha, ambaye mpaka akashuka na kukaa chini kabisa huku akicheka sana. Kila mtu alicheka isipokuwa Shadya, ambaye alibaki kututazama kwa kutoelewa somo vizuri. Mama wakubwa wakacheka mpaka kuanza kujifuta machozi kabisa, na mwili wa Miryam ulitikisika kutokana na yeye kucheka huku akiwa amefunika mdomo wake.
Shadya akaweka bakuli mezani na kisha kusema, "Jamani! Mimi nakula kama kiboko?"
Tesha akiwa hapo chini akasema, "Hamna... yaani una mdomo kama wake kabisa!"
Wengine wakaendelea kucheka kwa furaha.
"Ila Mamu! Nani anakupa hayo mawazo?" Shadya akamuuliza hivyo.
Mariam akamwangalia dada yake kwa ufupi, huku Miryam akiwa ametulia tu vile vile utafikiri siyo yeye, naye binti akasema, "Nimewahi kusikia mtu anasema... ndiyo nikaona nikutanie... kidogo."
"We! Usirudie kunitania hivyo tena, nitakuchapa," Shadya akamwambia hivyo huku akitabasamu.
Mariam akalibana tabasamu lake na kurudi kukaa sofani kwetu huku akaninyooshea kiganja chake kwa chini, nami nikaweka changu juu yake na kuvichezesha vidole vyetu huku kwa pamoja tukisema, "Broop!"
Ilikuwa ni ushindi kwa binti. Aliondoa kero yake.
Bi Zawadi akawa anajituliza kutokana na kucheka, naye akiwa anajifuta machozi kwa kitenge chake akasema, "Ama kweli hii ni nzuri sana. Ahahah... angalau tuongeze siku za kuishi. JC baba... Mungu akubariki."
Nikatabasamu kidogo tu.
Tesha akaanza kujinyanyua kutoka hapo chini, naye akasema, "Hii ni noma sana. Shadya... leo Mamu kakuweza tena, tokea ile ya mzimu... na sasa hivi hii. Dah! Hiyo ni mbili bila mamaa..."
"We' ngoja tu, nitayasawazisha yote na nitafunga lingine la ushindi. Mamu huwezi kunizidi mimi," Shadya akasema hivyo.
Miryam akamsukuma kiasi mdogo wake kwa bega lake kuonyesha uchangamfu, naye Mariam akacheka kwa furaha na kumfanyia dada yake hivyo hivyo pia.
Tesha akasimama na kusema, "Sawa. Zamu yangu sasa hivi, nikitoka mimi anafata JC, halafu Ankia, halafu da' Mimi, halafu kiboko, sawa? Eh... siyo kiboko, Shadya..."
Mama wakubwa na sisi wengine tukacheka kidogo, huku Shadya akimkata Tesha jicho hilo.
"Acha nawe, mwishowe jicho lipasuke," Tesha akamwambia hivyo.
"Haya Tesha, nenda sasa. Zamu yako," Mariam akasema hivyo.
Tesha akaenda pale ambapo Mariam alikuwa ametoka, naye akasimama kwa njia fulani ya kujiamini. Akaanza kutoa ishara kwa maigizo ya mikono na uso, na wote tulikuwa tumetulia tu na kuendelea kumtazama. Akaanza kuigiza mtindo fulani wa kutembea ulionifanya nitabasamu baada ya kutambua alikuwa anamwigiza nani.
Hata wengine wakawa wametambua upesi sana, naye Mariam, Ankia, Shadya, na Bi Zawadi wakanyoosha vidole huku wakisema kwa pamoja, "JC!"
Sote tukacheka kidogo, naye Tesha akasema, "Ah... kumbe ilikuwa rahisi eh?"
"Kila mtu hapa anaijua tembea yake. JC huyo," Ankia akasema.
Nikatabasamu kidogo na kutikisa kichwa.
"Hivi ulimuigaga nani kutembea hivyo?" Shadya akaniuliza.
"Ahahah... Hrithik Roshan... mwigizaji wa kihindi. Nilikuwa namuiga wakati niko mdogo, mpaka ikawa tembea yangu," nikamwambia hivyo.
"Na unatembeaga vizuri kweli, kwa midundo yaani," Bi Zawadi akasema hivyo.
Huku nikiwa nasugua goti langu taratibu kwa kiganja, nikamwambia, "Ah, kawaida tu mrembo wangu."
Nikapiga jicho pembeni na kukuta Miryam ameniangalia kwa yale macho ya kuhukumu, kisha akakunja midomo yake na kutazama pembeni. Nikacheka kidogo kwa pumzi.
"Enhe, tuambiane sasa. JC kafanyaje?" Ankia akamuuliza hivyo Tesha.
Tesha akatabasamu kiasi, kwa hisia makini yaani, naye akasema, "Ah... hajafanya kitu. Yaani... ninataka tu kumshukuru."
Wote tukaendelea kumwangalia kwa utulivu.
"Kwa kila kitu yaani. Sijui ilikuwaje tu mpaka ukafika hapa JC, ila... nakuthamini sana kaka. Kwa kila kitu ulichofanya, kwa kila unachotaka kufanya, kwa mambo mengi uliyonishauri mpaka nikatulia... na Mamu huyu... JC wewe ni zaidi ya ndugu yaani..." Tesha akasema hivyo kwa hisia.
Alifanya wengine waniangalie kwa macho yenye imani sana, nami nikabana tabasamu langu la hisia.
"Yaani wewe ndiyo wa kufa, kufaana. Tena we' ndiyo yule jamaa anayetajwa kwenye methali 17, mstari wa 17... yule... inasema... yule bwege ambaye amezaliwa kwa ajili ya wakati wa taabu... ndiyo wewe kaka," Tesha akasema hivyo.
Akatuacha tukicheka tu maana alionyesha bado bangi ilikuwepo kichwani!
"Lakini Tesha... hahahah... yaani wewe na Mamu... mtakuja kutuua siku moja kwa vituko vyenu," Bi Jamila akasema.
"Yaani! Umeanza vizuri kweli halafu mwisho ovyo!" Shadya akasema hivyo.
"Ih, kwani nimekosea nini, si ndiyo inasema hivyo? Ni Methali, sijasema Zaburi wala sunagogi! Nasoma Bible, nyie mnanionaje?" Tesha akajitetea.
Tukacheka tena kwa furaha, ndiyo nikamwambia, "Nashukuru kaka. Kama sikuzote navyokwambia, tuko pamoja."
Tesha akaja upande wangu, nami nikasimama pia. Tukakumbatiana kiume huku Mariam, Ankia na Shadya wakipiga makofi eti, nami nikamwona Miryam anatuangalia kwa hisia ya amani.
Tulipoachiana, Tesha akanipiga begani na kusema, "Haya, mzee Hrithik Roshan, uwanja ni wako sasa."
Nikatabasamu kidogo tu, naye Tesha akaenda kukaa.
Nikawa nimemwangalia Miryam kwa tabasamu la kichokozi, kama kumwambia 'ngoja sasa,' nami nikaona kama ameishiwa pozi. Nikaenda pale mbele na kuwageukia wote, wakiwa wananiangalia kwa matarajio mengi, nami nikashusha pumzi na kujiweka vizuri. Kisha nikaanza kutoa ishara ambazo ziliwafanya wengine waanze kucheka upesi.
Nilitoa ishara kwa njia iliyoonyesha kwamba nilifikiria mwanamke fulani, kwa kuigiza kurembua na kuzungusha mikono na mwili kama mwanamke, lakini siyo kwa kupitiliza, nao wakawa wanajaribu kusema yeyote waliyedhani namwaza. Mariam ndiye aliyekuwa akitaja wengi wa wasanii na katuni aliowafahamu, lakini kwa pamoja na wengine, hakuwa akipatia.
Walikuwa wananitaka niongeze njonjo eti ili wamtambue mhusika maana nilikuwa nawachanganya bado, nami nikamtazama Miryam machoni. Alikuwa ananikata jicho lile lililoonyesha kwamba tayari alikuwa amesoma vyema kule akili yangu ilipoelekea, nadhani hata Tesha na Ankia walikuwa wameshagundua ila wakatulia tu, nami nikaona niwarahisishie kazi wengine. Nikiwa nimejishika kiuno sasa, nikaigiza kama nafokea mtu, halafu nikampiga kofi.
Mariam akasimama na kusema, "Da' Mimi! Da' Mimi!"
Nikaacha kuigiza na kuachia tabasamu lililoonyesha kwamba binti alikuwa amepatia, nao wengine wakacheka kidogo huku wakimwangalia Miryam.
"Kibano kinachokuja Mimi, jiandae. JC anataka kulipiza kisasi kwa lile kofi la siku ile," Bi Jamila akasema hivyo, nasi kwa pamoja tukacheka kidogo.
"Tuambie JC, Miryam amefanyaje?" Bi Zawadi akauliza hivyo kwa shauku.
Nikamtazama Miryam usoni, yeye akiwa ananiangalia kwa macho yaliyojaa umakini kama vile kuniambia hataki niongee upuuzi, nami nikasema, "Kuna jambo fulani yaani... nimekuwa nataka kusema tokea...."
Miryam akasimama ghafla sana na kusema, "Jamani, tungekula sasa!"
Ih! Wote wakamtazama kama vile hawakuwa wamesikia alichosema. Najua alikuwa anataka kuepuka kile ambacho nilikuwa karibu kuongea, nami nikamwangalia kwa umakini tu.
"Kula?" Tesha akamuuliza hivyo.
"Eeh," Miryam akamjibu.
"Lakini, si tumeshakunywa chai?" Bi Zawadi akasema hivyo.
"Me nimeshaanza kusikia njaa, najua hata nyie mna njaa..." Miryam akajiongelesha kwa namna hiyo.
Shadya akasema, "Kweli, kweli. Tungekula tu."
"Si tusubiri mchezo uishe kwanza dada?" Mariam akamwambia hivyo.
"Eeeh, bado na wengine hawajacheza," Bi Zawadi akasema hivyo.
"Sa... saa saba sa'hivi mama. Kumbuka bado tuna sherehe ya kwenda... bora kula mapema... si eti ma' mkubwa?" Miryam akaongea hivyo na kuelekeza swali hilo kwa Bi Jamila ili aungwe mkono.
"Aaa.... ni kweli. Tungekula tu sasa hivi. Hata hivyo kimeshaiva," Bi Jamila akawaambia hivyo wengine.
Miryam akanitazama usoni kwa kuibia na kukuta nimemkata jicho makini, naye akaweka uso wa kiburi na kumwambia Tesha, "Kaweke mkeka varandani. Tulie hapo nje... wote, twende, twende, twende Mamu ahah..."
Akawa eti anajifanya amechangamka na kumnyanyua mdogo wake aliyekuwa ameishiwa raha, na wengine wakaanza kunyanyuka pia. Tesha akanipita kwenda kufata mkeka huku akinionyesha ishara kwa kutikisa kichwa kwamba alielewa mchezo, lakini hakukuwa na jinsi. Akarudi tena na mkeka na kuelekea nao pale nje, huku mama wakubwa, Shadya, na Mariam wakiwa wameshatoka, halafu Miryam na Ankia wakawa wanapeleka vyombo vya chakula hapo nje.
Nikategea kwanza kutotoka hapo ndani mpaka ilipokuwa wazi kwamba Miryam alikuja kumalizia kubeba vyombo vya mwisho, nami nikasimama katikati ya njia alipokuwa anaelekea kutoka tena. Wengine wote walikuwa nje sasa, na bibie akiwa anatokea huko jikoni, akakutana na mimi hapo ambapo nilisimama muda mfupi nyuma na kukatisha hatua zake. Akaniangalia usoni kimaswali, huku mimi nikimtazama kwa umakini, naye akajaribu kupita pembeni lakini nikamzibia njia makusudi.
Nikamzibia njia kwa makusudi na kusimama mbele yake kwa mara nyingine alipojaribu kunikwepa tena, naye akawa ananiangalia kama anashangaa.
Nikiwa namtazama kwa umakini, nikamuuliza kwa sauti ya chini, "Kwa nini ulinikatisha kabla sijatoa point yangu?"
Alikuwa ameshikilia vijiko, naye akaangalia pembeni na kusema kwa sauti tulivu, "Nilijua tu hiyo point yenyewe ingekuwa ya kipuuzi... ndiyo sababu."
Nikatoa tabasamu hafifu na kusema, "Ingekuwa ni point ya kipuuzi, usingenikatisha. Ila unajua ilikuwa na maana fulani ndiyo maana ukafanya hivyo, ikimaanisha ni maana ambayo ulikuwa umeifikiria."
Akaangalia upande wa mlangoni na kisha kunitazama, kisha kwa sauti ya chini akasema, "Sina muda wa kukaa kufikiria mawazo yako ya kipuuzi!"
Nikamwambia, "Ahaa, kumbe? Kwa hiyo hata tukienda hapo nje nikawaambia wengine nilichotaka kusema kuhusu wewe, haitakuwa mbaya kwa sababu ni ya kipuuzi hata hi...."
Sura yake ikageuka kuwa ya wasiwasi, naye akanikatisha kwa kusema, "Wewe!"
Nikatabasamu kiasi.
Akafumba macho na kushusha pumzi, kisha akasema, "Hebu nipishe bwana..."
"Subiri kwanza," nikamwambia hivyo na kumshika mkono.
Akautoa mkono wake kwa nguvu huku akiangalia mlangoni kama kujihami.
"Mbona kama unaogopa ikiwa haujali nilitaka kusema nini?" nikamuuliza hivyo.
Akanishusha na kunipandisha.
"Okay, kwa hiyo... hutaki kusikia nilichokuwa nataka kusema?" nikamuuliza hivyo.
Akavuta fikira kwanza, kisha akatazama pembeni na kusema, "Ndiyo, sitaki."
Nikatabasamu kidogo na kusema, "Mwongo."
Akanitazama usoni kwa jicho kali.
Nikatabasamu zaidi na kumwambia, "Mwongo-mkweli wewe. Unachokisema kwa mdomo ni tofauti na unachokitaka kwa moyo. Huwezi kukataa kwamba niko sahihi."
"Na kama nikikataa?" akaniuliza hivyo kwa sauti tulivu.
"Utakuwa unaupinga moyo wako mwenyewe..." nikamwambia hivyo.
Akazungusha macho yake na kuangalia pembeni kwa kukerwa.
"Na bado tu huo moyo wako utaendelea kukusumbua kwa sababu unajua utakuwa umepitwa na kitu ambacho kingeufurahisha," nikasema hivyo.
Akaonekana kutojali maneno yangu na kuangalia pembeni tu.
Nikamwambia, "Haijalishi lakini nilitaka kusema nini wakati wa charade, point yangu kwako ni hii. Ninakuona. Ninakuelewa Miryam. Umeshakuwa kama mtu ambaye anaumizwa sana mpaka anazoea maumivu, kwa hiyo unajitahidi kuficha hisia zako mapema kabla hata hujahisi chochote ili usiumie... lakini hiyo haiwezekani kwa asilimia zote. Maumivu yatakuwepo tu. Nimeona hiyo kuwa case kwa Joshua, shangazi zako, na labda hata mtu wa mwisho uliyekuwa naye kimahusiano kabla ya kufikia wakati huu...."
Miryam akaniangalia usoni kwa hisia makini baada ya mimi kusema hivyo.
"Hayo ni mapito, Miryam. Hauhitaji kueleza mengi kuhusu mapito yako... tayari ninaelewa. Na ukweli ni kwamba... siyajali. Nimekupenda wewe kama nilivyokukuta, kwa hiyo yaliyopita hayajalishi zaidi ya yale yanayokuja, hivyo ndivyo navyoamini sikuzote..." nikamwambia hivyo kwa hisia.
Akatazama chini kwa utafakari.
Nikamwambia, "Natumaini hautaacha mapito yako yawe nawe sikuzote Miryam. Baada ya mambo mengi yenye kuumiza ambayo umepitia, hata kama siyajui... natumaini utanipa nafasi... nafasi ya kuwa nawe ili usiogope lolote tena kuhusu maumivu ya kihisia... kwa sababu hata maumivu yaje ya aina gani, nitakuwa mtu pekee wa kukufanya uhisi kwamba hayakuwahi kukupata... na hayatakupata tena."
Miryam akapandisha macho yake taratibu na kuniangalia usoni kwa hisia sana, halafu shingo yake ikalegea kiasi, yaani... akapindisha uso kidogo huku akiniangalia kwa njia iliyoonyesha kutekwa kifikira na kihisia kwa uzito sana. Niliendelea kumwangalia kwa hisia pia, nikiona namna ambavyo kweli maneno yangu yalimpa athari nzuri mno, yaani ule ugumu ulikuwa unayeyuka, naye ndiyo akawa kama ameshtuka baada ya kuniangalia kwa njia hiyo legevu na kutazama chini kama vile mtu anayejiuliza 'hivi nina matatizo gani?'
Nikatabasamu tu kwa hisia na kuchukua vijiko vyake, ambavyo aliviachia kwa wepesi kabisa, halafu tukatazamana machoni kwa hisia tulivu kabla sijamwacha hapo akiwa katikati ya tafakari nyingi mno. Hapo najua nilikuwa nimepigilia msumari wa mapenzi ndani zaidi ya moyo wake, yaani asingeweza kupinga tena hata kama angejifanya mgumu kiasi gani, na nafikiri haingechukua muda mrefu kwa huyu mwanamke kunikaribisha ndani ya huo moyo kwa dhati yote. Sijui ingekuwaje tu!
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Pata Full Story WhatsApp au inbox
Whatsapp +255 678 017 280
Karibuni sana