Simulizi: Mimi na Mimi

Festo kuwepo uraiani tena huru ni kama time bomb litalipuka tu soon kuwa makini JC
 
MIMI NA MIMI 2

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA

★★★★★★★★★★★★★★★★★★


Sikuchukua muda mrefu sana kuondoka huko Kivukoni baada ya Bertha kuondolewa mahakamani, nikapita kwenye mgahawa mzuri huko Kigamboni na kupiga ugali kwanza, kisha nikaingia kwenye saluni nzuri kupunguza nywele na ndevu kwa mwonekano niliopendelea, halafu ndiyo nikaendelea na safari ya kurudi Mbagala.

Kevin alikuwa amenitafuta, yule bwana wake na dada yangu, akiwa anataka kujua kama nilimuungishia mitambo kwa Jasmine na nini, lakini nikamsihi tu amwache Jasmine kwanza mpaka ajifungue, ndiyo mambo mengine yangefuata. Jambo bora ambalo angetakiwa kufanya ni kutoacha kumwonyesha dada yangu kuwa alimjali kwa kutumia njia mbalimbali, na hata siku ambayo Jasmine angejifungua, angepaswa kwenda hospitali kuwa pamoja naye haijalishi nini kilikuwa kimetokea baina yao. Akaonekana kuridhia hayo.

Nimekuja kufika Mzinga ikiwa imeshaingia saa moja, na nilikuwa nahisi uhitaji wa kuingia kwenye gym kupasha kidogo maana nilikuwa nimekosa kufanya hivyo kwa siku chache. Kulikuwa na gym fulani ndogo maeneo hayo, na nilijua ingekuwa wazi mpaka kufikia mida ya saa nne, hivyo nikaamua kuelekea huko kwa Ankia ili nikabadili mavazi na kugeuka tena niwahi gym kupiga tizi, halafu ndiyo ningeenda kupumzika sasa. Haya mazoezi yangesaidia zaidi mwili kujenga uimara baada ya ile ishu ya sumu hapo juzi, na misuli iwe fiti kwa ajili ya kazi!

Nilipofika kwa Ankia sehemu ya getini, nikaliona gari lake Miryam pale nje ndani ya geti la nyumba yao, kumaanisha bibie alikuwa amesharejea, nami nikaamua kwenda kwanza hapo kuchungulia hali ilikuwaje kwa sasa. Nakumbuka nilimwacha huko dukani kwake muda ule akiwa na mambo mengi sana kichwani, kwa hiyo nikataka kujua tu kwa wakati huu angekuwa vipi kiuhusiano pamoja na mama mkubwa wake. Nilipita tu getini na moja kwa moja kuelekea ndani kwao, nami nikakuta sebule ikiwa imejaa kiasi.

Walikuwepo mama wakubwa hapo, Mariam, Shadya, Ankia, pamoja na mwanadada mwingine rika kama la Mariam tu, ambaye sikumfahamu. Kilichofanya sebule ionekane kujaa ilikuwa ni rundo la nguo zilizotandazwa kwenye kimkeka hapo katikati, huku wanawake wakiwa wanachukua hii na ile kwa kubagua na kuchagua. Zote zilikuwa za kike, nzuri, na zilikuwa spesho. Mariam, huyo mwanadada, na Ankia walikuwa wamekaa hapo chini na kuchukua nguo hii au ile, wakiwapa wengine waangalie na kuchagua, nami nikawa nimemwona bibie Miryam pia.

Alikuwa amekaa upande wa dining, peke yake, akiwa anafanya kazi fulani kwenye laptop, na alionekana makini kweli. Ujio wangu hapo ukawachangamsha zaidi wanawake hao sebuleni, nami nikamwona Miryam akinitazama kwa utulivu, halafu akaachana nami na kuendelea na mambo yake. Mariam alikuwa ananionyesha nguo ambayo alitaka kuchukua, na Ankia akawa anamwambia asiwahi maana zilikuwepo nyingine nzuri kwa hiyo angetakiwa kuchangua kwa umakini.

Shadya ndiye aliyekuwa akiongea zaidi kusifia nguo hizo na aliyofanya mpaka kuzileta hapo kwa ajili ya wengine, na kila mmoja wao angetakiwa kuchagua moja tu kwa ajili ya kuvaa kwenye send-off siku ya kesho. Nikamuulizia Dina kwake, nikisema Tesha aliniambia kwamba angekuja hapa leo pamoja naye Shadya, naye ndiyo akasema hapana, hakuweza. Tena Tesha alikuwa ameenda huko kwao na akina Doris pamoja na Dina leo baada ya kuitwa akawasaidie na vitu fulani kwa ajili ya maandalizi, kwa hiyo jamaa angerejea baadaye sana nadhani.

Nilimwangalia Bi Jamila na kuona aina fulani hivi ya uchangamfu ndani yake alipokuwa akisemeshana na wengine hapo. Na yeye alikuwa amenikaribisha kabisa eti nijiunge nao kuchagua nguo, nami nikacheka kidogo kuneemesha utani wake. Alikuwa sawa zaidi kihisia wakati huu, na hiyo ikanifanya nitambue kwamba Miryam angekuwa amesawazisha ishu zao kwa njia nzuri. Nikawapita wanawake wengine na kuelekea upande wa dining, ili nimsalimie binti maringo, na alikuwa bize kweli yaani asingeweza kuhamisha macho yake kutoka kwenye laptop.

Hivyo, nikafanya kusogea mpaka kufikia sehemu ya kiti alichokalia, halafu nikaegamia meza kwa mikono yote na kujifanya kama naangalia kwa umakini yale aliyokuwa akifanya humo kwenye laptop yake. Hakuwa amebadili mwonekano wake kimavazi toka nilipomwona ile mchana, kumaanisha aidha ndiyo angekuwa amefika nyumbani muda si mrefu sana, ama hakujisikia tu kubadili mavazi na kuamua kufanya kazi kwanza.

Baada ya mimi kusogea hapo karibu yake, akawa ameniangalia kwa jicho makini usoni, nami nikamtazama kwa chini. Si nilikuwa nimesimama huku yeye amekaa, kwa hiyo nikawa namwangalia kama vile natazama mtu mfupi kwa nyodo. Nafikiri aliona umakusudi wangu wa kuja mpaka karibu yake kuwa uchokozi, naye akapeleka macho yake kuwaangalia wengine. Hakuna mtu aliyejisumbua kutazama huku zaidi isipokuwa tu yule mwanadada mgeni, ambaye aliniangalia mimi zaidi na kukwepesha macho nilipomtazama. Miryam akaniangalia tena kwa umakini, mimi nikianza kumtazama kizembe, naye akarudisha macho yake kwenye laptop.

Nikajiinamisha zaidi kama naangalia kwa umakini sana vitu alivyoandika, naye akaacha kubofya keyboard kwa ufupi. Nikajiweka kama mwanzo tena, na najua tayari nilikuwa nimeshamchanganya maana alikuwa akiandika kitu kama barua ya masuala ya kikazi, siyo duka wala nini, yaani zile kazi rasmi, naye akawa anatafakari zaidi huku akijaribu kunipotezea, lakini akashindwa.

Akawaangalia wengine kiufupi, kisha akanitazama na kwa sauti ya chini sana akasema, "Nini wewe?"

Nikamuuliza, "Nini na wewe?"

Akasonya kidogo na kusema, "Usinichanganye."

Nikaendelea tu kumwangalia kizembe.

"Em' toka hapa... nenda huko," akasema hivyo.

Nikashindwa kujizuia kutabasamu, maana alikuwa ananiongelesha kama vile mimi mtoto.

Akaniangalia na kuuliza, "Hujanisikia au?"

"Nimekusikia, ila ni jeuri tu," nikamwambia hivyo.

Akanitazama usoni kiukali kiasi.

Nikatabasamu na kuacha kuegamia meza, naye akarudisha umakini wake kwenye laptop tena. Nilikuwa nafikiria nimuulize kuhusiana na suala la Bi Jamila, lakini sidhani sana kama angekuwa na uhuru wa kunielezea hayo mambo ambayo kwa mtazamo wa haraka, hayakunihusu. Najua tayari wangekuwa wameshaongea, na ningemchokoza zaidi kwa kumwambia mimi ndiyo wa kushukuru maana nilimpa ushauri na nini, lakini nikaona nivunge tu, na labda nimwache kwanza.

Lakini kabla sijamwacha kwanza, jambo fulani likaingia akilini, hivyo nikaegamia meza tena na kumwambia, "Kuna kitu nilikuwa nataka nikuulize."

Akaendelea kuangalia laptop tu huku akibofya-bofya herufi kwa umakini.

Nikasema, "Eti... ile juzi Festo alipokuja...."

Miryam akaacha kubofya na kunitazama usoni kwa utulivu.

"Alikuwa amekuja kukwambia nini?" nikamuuliza hivyo.

Akaendelea kuniangalia machoni kwa umakini tu.

Nikaweka uso kimchezo na kusema, "Siyo kwamba nataka kuweka cheat kwenye riadha yetu ya kuku-win..."

Miryam akaangalia pale sebuleni baada ya mimi kusema hivyo, akiwa anahofia wengine wangesikia maneno hayo, na alipoona wengine hawana habari akanitazama tena kiumakini.

Nikatabasamu kiasi na kusema, "Usijali, hawajasikia."

"Kwa nini unaniuliza hivyo?" akauliza hivyo kwa sauti ya chini.

"Nimetaka tu kujua... kama bado nina competition na nini, ili niwe fiti zaidi, maana...." nikasema hivyo na kumtikisia nyusi kidogo.

Akapiga ulimi kidogo na kuangalia laptop yake tena.

Nadhani hakutaka kumeongelea jamaa, na mimi kwa kuelewa nikaona tu nimwambie, "Basi, haina shida. Siyo lazima ujibu usipotaka, me mwenyewe...."

"Alikuja kuniaga," Miryam akanikatisha kwa kusema hivyo.

Nikamtazama kwa umakini, nami nikamuuliza, "Kukuaga ya... ya kwenda wapi?"

"Kwenda nje ya nchi. Alisema ana safari ya kikazi," akaniambia hivyo bila kuniangalia.

Nikatazama pembeni kwa ufikirio.

"Kuna nini kwani?" Miryam akauliza.

Nikamtazama na kukuta ameniangalia kwa udadisi, nami nikajitabasamisha na kusema, "Hamna kitu... nilitaka tu kujua. Nimepata na relief, maana... si unajua, wivu na nini..."

Nilisema hivyo na kumpandishia nyusi tena kichokozi, naye akaonekana kukerwa hata zaidi na kuifunika laptop yake huku akiniangalia usoni kwa umakini. Nikasimama vizuri kabisa na kumwangalia kimaswali, naye akasimama pia bila kuacha kunitazama. Ilikuwa kama vile anataka kunipiga eti! Kisha ndiyo akatoka hapo sehemu ya dining na kwenda kujiunga na wengine, akiketi kwenye mkono wa sofa karibu na Bi Zawadi na Bi Jamila.

Kwa hiyo hapo nikawa nimepata uhakikisho namba mbili kwamba Festo angekuwa ameondoka kweli. Kama alikuja kumuaga Miryam siku ile, basi uwezekano wa asilimia hamsini wa yeye kuwa ameondoka kabisa uliwezekana. Hizo hamsini zilizobaki ndiyo bado nilitakiwa kuzithibitisha, kwa kuwa sikutaka kuamini kiurahisi tu kwamba huyo jamaa angeondoka ile ya kuondoka kabisa, hapo lazima kulikuwa na mguso fulani hivi wenye dukuduku, kama tu madam Bertha kukiri leo mahakamani kwamba alikuwa na hatia. Nilipaswa kuwa na UHAKIKA. Haya mambo haya!

Basi, nikasogea tu usawa wa ukuta kukaribia sofa na kuegamia hapo, nikiwaangalia wanawake walipokuwa wakibagua-bagua nguo kabla sijatoka kwenda gym kwanza. Ankia na Shadya walikuwa wanasemana kweli, kwamba Ankia ana unene halafu amechagua nguo inayomtoshea Mariam basi lilikuwa ni suala lililomkera Shadya. Bi Zawadi na Mariam walikuwa wakicheka sana kuwasikiliza wanawake hao walivyoanza kuchambana, kiutani lakini, naye Bi Jamila akawa amevuta nguo moja na kumwekea Miryam usawa wa kifua chake.

Mwanamke huyo akawa anamwambia alichukue hilo, likiwa ni gauni, maana bado hakuwa amechangua nguo ya kuvaa na uchaguzi hapo ulikuwa mwingi sana, na Miryam akatabasamu na kuanza kuliangalia. Lilikuwa la kijani, likionekana kuwa refu na laini, na wakina Ankia wakawa wanamwambia achukue hilo maana ni zuri pia. Katika kuligeuza-geuza kabla hajaamua, Miryam akawa ameniangalia, nami nikamtikisia kichwa kidogo sana huku nikikaza macho kama kumwambia hilo gauni halikumfaa. Yaani wote walikuwa wameliruka, halafu yeye ndiyo wamwambie litampendezea? Hapana.

Baada ya mimi kumfanyia hivyo, akaacha kuniangalia huku akionekana kukosa amani, lakini akamwambia Bi Jamila kwamba angetafuta lingine maana aliona kama hilo haliendani na rangi ya ngozi yake. Mama mkubwa wake akaelewa, nao wakaendelea kuchambua nguo zingine. Zilikuwa nyingi, yaani nadhani Shadya alileta duka lake lote hapo, na sekunde chache kupita nikaona Miryam ameshika nguo nyingine yenye rangi ya njano na kuanza kuipima-pima kwenye mwili wake. Kwa mtazamo wangu, sikuona kama ilimfaa, lakini sikutarajia afanye kitu fulani baada ya kuishika hiyo nguo.

Akaniangalia usoni, zamu hii siyo ile ya kinagaubaga, yaani aliniangalia huku ameishika nguo hiyo karibu naye kama vile kuniuliza 'na hili?' Upesi nikatikisa kichwa kukataa kwamba halikumfaa, halafu nikajikausha. Nikaona anaweka uso fulani wa kuvunjika moyo, halafu akairudisha na kuanza kutafuta nyingine. Nikazuia tabasamu langu lisionekane wazu huku nikimtazama kwa umakini, naye akapata nguo nyingine tena na kurudia kunitazama usoni. Nikatikisa kichwa kumkatalia, naye akaweka ule uso kama vile ananiuliza 'unataka ipi sasa?' Ah!

Yaani alikuwa ameshajisahau, ikawa kama vile anataka mimi ndiyo nimchagulie nguo. Nilisikia raha! Ilikuwa kama zile pindi unaenda na mtu wako dukani, anavaa na kubadilisha nguo, halafu anakuonyesha ili umwambie ipi imemfaa, yaani Miryam ndiyo alinipa hilo vibe sasa hivi. Halafu akawa anajifanya kama vile hajali sana mawazo yangu, kama vile maamuzi ni yake, wakati kila aliponyanyua nguo angenitazama na mimi ningemkatalia, kisha angerudi kutafuta zingine. Nilipenda sana hii.

Katika kugeuza-geuza nguo, nikaona moja iliyokuwa na rangi ya maroon, ikionekana kuwa gauni laini, yenye urembo wa vitu vilivyomeremeta. Niliipenda sana hii rangi, na najua ingependezea kwenye ngozi ya bibie Miryam maana alikuwa mweupe. Nguo yoyote ile ingempendezea, lakini najua hii ndiyo ingemfaa. Nikamwonyesha Mariam nguo hiyo na kumwambia ampe dada yake ili aiangalie, naye akampa. Karibia wote waliisifia, wakisema ni nzuri sana, naye Miryam akawa anaitazama kwa ufikirio. Akaniangalia usoni, mimi nikiwa natabasamu, halafu akaikunja tu na kuiweka pembeni, kisha akaendelea kubagua nguo zingine.

Eti alikuwa anajifanya haitaki ili aniumize sijui? Haya bana. Nikatabasamu tu na kisha kuwaaga wanawake wote kwa wakati huu, nikisema naelekea Mzinga mara moja kisha ningerejea, nami huyoo nikasepa. Mambo mengi yalikuwa yanaingiliana sana, lakini haikuwa imefichika kwamba uhusiano wangu na Miryam ulikuwa umeshaanza kuimarika hata kabla ya kuwa amekubali kuuanzisha. Alijali kile ambacho niliwaza juu yake, kwa hiyo najua ingekuwa rahisi zaidi kumvuta kwangu kihisia. Yajayo kwa upande wake yakaonekana kuwa yenye kufurahisha, ningetakiwa kuendelea kuyasubiri.


★★★


Bwana, siku ya Alhamisi ikawa imefika. Hiyo jana mambo hayakuwa mengi sana baada ya mimi kutoka gym kupasha na kurudi tena kwa Ankia, tukala, tukapiga story, kisha tukapumzika. Leo hawa viumbe wangekuwa na mihemko ya hali ya juu kwenda huko kwenye kitchen party kuonyeshana nani kapendeza zaidi ya bibi harusi mtarajiwa na kusemana wee, kwa hiyo Ankia akawa ameamka mapema na kama kawaida kupiga usafi wa ndani. Mimi sikuamka mapema sana, mida ya saa tatu asubuhi, halafu nikaendelea kukaa kitandani mpaka saa nne.

Aliyekuja kunitoa chumbani ilikuwa ni binti Mariam mwenyewe. Alikuja kututembelea nakwambia, na katika hali ya kushtukiza yaani aliingia chumbani na kukuta niko kifua wazi, kwa hiyo nikavaa T-shirt upesi na kwenda sebuleni pamoja naye. Mariam alikuwa ameshaanza kutulia sana kiakili, aliongea vizuri, alikuwa na utani, na alielewa vitu vingi sana. Nilianza kuona ule utu uzima ndani yake, japo kwangu angeendelea kuwa kabinti. Alikuja wakati ambao Ankia alikuwa ameshaandaa chai, lakini tulipokunywa, yeye hakunywa kwa sababu tayari alikuwa amepata kiamsha kinywa kwao.

Ndiyo akawa ametuambia kwamba, Miryam hakwenda kazini leo. Akasema yaani wote walikuwepo kwao, na ndiyo maana alikuja ili kutuchukua twende naye ili kujiunga na wengine kufurahia ushirika pamoja. Lilikuwa ni wazo zuri sana, na kwa kufikiria namna shangwe ya siku nzima ya leo itakavyokuwa, Ankia akaamua kutokwenda dukani kwake pia ili awe pamoja nasi.

Ikawa imeenda hiyo, yaani hatukuchukua muda mrefu sana kuanza kujiandaa, mimi sanasana kwa sababu nilihitaji kuoga kabisa, na mpaka nimekuja kumaliza kuvaa na nini, tayari Ankia na Mariam walikuwa wameshaenda pale kwao na binti. Nilivalia kawaida tu, T-shirt nyeusi ya mikono mifupi na jeans, kisha nikafunga milango na kuelekea huko pia ikiwa imeshaingia mida ya saa sita mchana.

Kweli nikawakuta wote wakiwepo ndani, sebuleni. Bi Zawadi na Bi Jamila walikaa kwenye sofa lao kama kawaida, Shadya na Ankia walikaa kwenye sofa upande wa kulia, na pale ambapo Mariam alipendelea kukaa na mimi, alikuwa amekaa na bibie Miryam pamoja na Tesha. Jamaa akasimama, nasi tukasalimiana vizuri kishkaji, halafu nikawasalimia na wengine pia vizuri. Wote walivalia kiukawaida wa nyumbani tu, na bibie Miryam alikaa kwa kukunja nne huku akiwa bize na simu yake. Nilipenda namna ambavyo alikuwa amezilaza nywele zake upande mmoja wa uso karibia kuficha jicho, na alikuwa ametulia tu kama vile hayupo.

Tesha akaniachia hiyo nafasi aliyokuwa ameketi na kukaa kwenye mkono wa sofa pembeni yake Shadya na Ankia, nami nikakaa pembeni yake Mariam, akiwa katikati yangu mimi na Miryam. Bibie akanyanyuka tu na kuelekea jikoni kwanza, nikiibia nyendo zake kwa kuangalia huko nyuma. Mashallah! Nikarudisha umakini wangu kwa wengine, Mariam akisema angependa sana tukiwa hapo pamoja mpaka jioni, yaani mimi na Ankia tusiondoke, nasi tukamwambia asiwaze. Hata nikamwambia tungecheza na mchezo wa pamoja maana sote tulihitaji kuburudika.

Tesha akawa anatuambia jinsi mambo yalivyoenda huko ambako kitchen party ingefanywa, maeneo ya Kigamboni kwenye ukumbi fulani maridadi, na ndiyo Miryam akawa amerejea tena na kuketi. Mariam akanyanyuka na kwenda kutoa miwa kwenye friji, ambayo imeshakatwa-katwa na kuwekwa kwenye chombo, kisha akaileta hapa kati na kuweka chombo hicho mezani, nafikiri wote tule taratibu. Shadya yeye akakichukua na kukibeba mikononi, akianza kula miwa yeye mwenyewe, na jambo hilo likaonekana kumkera Mariam kiasi.

Sisi wengine tukaendelea na story tu bila kujali kuhusu miwa, lakini niliona jinsi ambavyo Mariam alikuwa akimwangalia Shadya kwa njia fulani kama vile hataki yaani, nami nikamtazama Shadya na kumwona akiendelea kupakia vipande vya miwa na kuweka mabaki pembeni ya chombo hicho. Binti alikuwa amechomwa sana.

Nafikiri Miryam akawa ametambua hilo kwa kuwa akamshika mdogo wake kichini-chini na kumuuliza karibu na sikio lake, "Nini Mamu? Mbona umekunja sura?"

Nikajifanya kuendelea kuwatazama wengine, lakini nikamsikia Mariam akisema, "Dada... mimi... naweka miwa tule wote, halafu shangazi kabeba sahani yote..."

Nikajikaza nisicheke kwa kuibana midomo yangu.

Miryam akacheka kidogo kwa pumzi, naye akamwambia, "Usijali, mingine si ipo kwa friji? Tutaweka baadaye, mwache aenjoy. Unajua ana katumbo kama ka kiboko."

Nikamwangalia Mariam kwa ufupi na kukuta amekunja midomo yake kwa kukerwa. Kama katoto yaani!

Tesha akawa anasema, "Kitchen party ya Doris itakuwa noma. Yaani walipokuwa wanapafanyia maandalizi, we!"

"Wanaandaa mambo motomoto eh?" Bi Jamila akamuuliza.

"Sana," Tesha akasema.

"Eeh, wanapamba vizuri. Nimeona huo ukumbi kwenye status yake Doris," Ankia akasema hivyo.

"Umeona?" Tesha akamuuliza hivyo.

"Eeh. Kuna ka gharama ka juu kametumika, na hiyo ni kitchen party tu," Ankia akasema hivyo.

"We! Acha kabisa! Mume wake anamgharamia. Pazuri yaani, mpaka natamani na mimi kwenda," Tesha akasema.

"Acha uhuni Tesha. Hiyo ni ya wanawake, uende kufanyaje?" Shadya akamwambia hivyo huku akitafuna miwa yake.

"Si ndo' point yenyewe, au? Oya JC, tuvae magauni mwanangu tukavamie hiyo," Tesha akasema hivyo.

"Acha ujinga," nikamwambia hivyo, na mama zake wakubwa wakacheka kidogo.

Nikamwangalia Miryam pembeni na kukuta anatabasamu kidogo, lakini alipohisi kwamba namwangalia, tabasamu hilo likakoma.

"Ana akili haina breki huyu," Shadya akasema hivyo kumwelekea Tesha.

"Halafu na yako? Hivi wewe... miwa yote unakula mwenyewe, sisi hutuoni?* Tesha akamwambia hivyo.

"Kwani imeisha? Si ipo mingine? We' unakuaje, kila kitu nikifanya kwako kibaya tu," Shadya akalalamika.

"Eh, basi yaishe. Kamua mama... tafuna mpaka bakuli," Tesha akamwambia hivyo.

Wengine wakacheka kidogo, nami nikamwona Miryam anamnyooshea kidole Tesha kama kumwonya aache kweli, kimasihara tu yaani.

"Ee, JC..." Shadya akaniita.

"Naam?" nikaitika.

"Wee... si umesema kuna mchezo unataka tufanye? Uko wapi? Tuchangamshe basi kabla ya msosi..." Shadya akaniambia.

"Eeeh, JC. Tucheze sasa," Mariam akaniambia hivyo pia kwa shauku.

"Ahah... eh ndiyo, sawa. Inabidi niwaelezee unavyochezwa kwanza," nikamwambia hivyo.

"Yaani hawa watu wanapenda michezo!" Tesha akasema hivyo kikejeli.

"Kama we' hupendi, toka," Shadya akamwambia hivyo.

Wengine wakacheka kidogo, naye Bi Zawadi akasema, "Sawa baba, tupo tayari. Tuchangamshe na sisi kama Mamu."

Mariam akasogea mbele zaidi ya sofa ili aniangalie vizuri.

Nikawaambia, "Huu mchezo unaitwa charade, wa wazungu hao. Huwa unachezwa hivi; si unaona sisi wote hapa? Mmoja wetu anasimama hapo mbele akiwa na wazo la kitu fulani kichwani, kitu chochote kile yaani... lakini hatakiwi kutuambia hicho kitu ni nini. Anachotakiwa kufanya... ni kukiigiza hicho kitu kwa ishara za mikono na mwili, lakini yaani hapaswi kuongea mpaka mmoja wetu sisi aliyekaa akiseme kwa kupatia..."

"Aaa... hiyo ngoma naijua..." Tesha akasema hivyo.

"Hata me naujua, wanachezaga wazungu. Ni mzuri kweli huo mchezo," Ankia akasema.

"Hata mimi naujua. Nime..nimeuona... aa... aliucheza Olaf na Anna..." Mariam akasema hivyo.

"Enhee, huo huo Mamu. Olaf akatembea kama Elsa, eh?" nikamsemesha namna hiyo.

"Eeeh... hivi... oooh Elsaaa!" Mariam akasema hivyo huku akijaribishia kutembea kama miss.

Sisi wote hapo tukacheka kwa pamoja, naye binti akarudi kukaa sofani.

Nikasema, "Safi sana. Ila sasa... huwa una kanuni zake, lakini mimi nimeubadilisha kidogo. Hapa tutaucheza kwa njia tofauti."

"Enhe..." akasema hivyo Bi Jamila.

"Hapa hatutaucheza kimashindano, ila kidarasa zaidi. Yaani... unapaswa ufikirie kitu fulani unachopenda au kuchukia, ni wewe tu... halafu ukishafanya charade ya hicho kitu tukakipatia, unapaswa uelezee kwa nini umeamua kucheza na hicho. Sijui inaeleweka?" nikawaambia hivyo.

Wakaanza kuonyesha uafiki wa wazo hilo, nami nikamwona Miryam akiwa ananitazama kwa umakini. Ni kama alikuwa ananisoma, na kweli nilikuwa nimepanga kufanya jambo fulani kumwelekea yeye mwenyewe.

"Huo mchezo mzuri. Me kwa maigizo si mnanijua?" Shadya akasema hivyo huku akiendelea kula miwa.

Bi Zawadi akasema, "Yaani... kama niseme, nimechagua jagi... akilini... nikafanya parade..."

"Siyo parade ya mstalini, ni charade..." Bi Jamila akamkatisha.

Bi Zawadi akamkata jicho la kukerwa, huku sisi wengine tukicheka, naye akasema, "Eeh, charade. Mkipatia yaani, kwamba ni jagi... natakiwa nielezee kwa nini nimechagua jagi, si ndiyo?"

"Ndiyo maana yake, cheupe wangu," nikamwambia hivyo.

"Hapo sawa, nimeelewa handsome wangu," Bi Zawadi akasema.

"Okay, poa. Wote tumeelewa. Tuanze sasa. Nani anaanza?" Tesha akasema hivyo.

Mariam akanyanyua mkono wake juu na kusema, "Mimi... mimi, mimi, mimi..."

"Ahahah... haya sawa, anza," nikamwambia hivyo.

Mariam akanyanyuka na kusogea mpaka ile sehemu ya wazi katikati kuelekea upande wa vyumbani na jikoni, naye akatugeukia na kujiweka tayari kwa kuisawazisha miguu yake. Wengine walikuwa wameshaanza kucheka kabla hata hajaanza kufanya charade, ndiyo akakunja ngumi zake, akatanua mikono, kisha akavimbisha mashavu yake.

Akawa anaigiza kitu fulani ambacho kwa haraka kilimfanya kila mtu aelewe kwamba aliigiza ubonge na vitambi, nasi tukawa tunataja mabonge wote tuliofahamu. Mimi nikasema Kingwendu, mwingine akasema JB, huyu Big Show, mwingine Lizzo, mara Mashalavu, lakini inaonekana tukawa hatupatii maana binti aliendelea tu kuigiza. Akawa anatoa ishara za kuogelea na kupiga mihayo kwa nguvu sana, nami nikamwona Miryam anacheka kwa pumzi na kufunika mdomo wake.

Wengine walipokuwa wanajaribu kupatishia ni mtu gani mwenye kitambi anayeogelea, nikasema inaonekana Miryam alikuwa ameshapata jibu na ndiyo maana hata hakuwa akiongea lolote. Mama zake wakubwa wakamwambia aseme mawazo yake pia, asikae kimya tu, naye ndiyo akajituliza na kumtazama mdogo wake.

Mariam akiwa anaendelea kuachama-achama, Miryam akasema, "Kiboko."

Mariam akaanza kurukaruka kwa furaha huku akimsonta dada yake kuonyesha kwamba amepatia.

Sisi wengine tukacheka kidogo, naye Tesha akasema, "Jah! Yaani kumbe kiboko? Af' kweli, huwaga yanaachama mno... na yana shepu! Dah! Point moja kwa da' Mimi hahah... hii kitu raha sana."

Ankia akamuuliza Mariam, "Kwa nini umemfikiria kiboko Mamu?"

"Kwa sababu ya shangazi," Mariam akasema hivyo.

Shadya akasitisha kuendelea kutafuna miwa mdomoni mwake na kuuliza, "Mimi? Me nina undugu gani na kiboko Mamu?"

Maana ya kile ambacho Mariam alikuwa anawaza ikawa imeniingia akilini pia, nami nikamwangalia Miryam na kukuta ameficha tabasamu lake kwa kiganja. Nikajikaza nisicheke.

Mariam akasema, "Unakula sana. Una tumbo kama la kiboko."

Kicheko cha pamoja hapo kilikuwa cha hali ya juu baada ya binti kusema hivyo, hasa Tesha, ambaye mpaka akashuka na kukaa chini kabisa huku akicheka sana. Kila mtu alicheka isipokuwa Shadya, ambaye alibaki kututazama kwa kutoelewa somo vizuri. Mama wakubwa wakacheka mpaka kuanza kujifuta machozi kabisa, na mwili wa Miryam ulitikisika kutokana na yeye kucheka huku akiwa amefunika mdomo wake.

Shadya akaweka bakuli mezani na kisha kusema, "Jamani! Mimi nakula kama kiboko?"

Tesha akiwa hapo chini akasema, "Hamna... yaani una mdomo kama wake kabisa!"

Wengine wakaendelea kucheka kwa furaha.

"Ila Mamu! Nani anakupa hayo mawazo?" Shadya akamuuliza hivyo.

Mariam akamwangalia dada yake kwa ufupi, huku Miryam akiwa ametulia tu vile vile utafikiri siyo yeye, naye binti akasema, "Nimewahi kusikia mtu anasema... ndiyo nikaona nikutanie... kidogo."

"We! Usirudie kunitania hivyo tena, nitakuchapa," Shadya akamwambia hivyo huku akitabasamu.

Mariam akalibana tabasamu lake na kurudi kukaa sofani kwetu huku akaninyooshea kiganja chake kwa chini, nami nikaweka changu juu yake na kuvichezesha vidole vyetu huku kwa pamoja tukisema, "Broop!"

Ilikuwa ni ushindi kwa binti. Aliondoa kero yake.

Bi Zawadi akawa anajituliza kutokana na kucheka, naye akiwa anajifuta machozi kwa kitenge chake akasema, "Ama kweli hii ni nzuri sana. Ahahah... angalau tuongeze siku za kuishi. JC baba... Mungu akubariki."

Nikatabasamu kidogo tu.

Tesha akaanza kujinyanyua kutoka hapo chini, naye akasema, "Hii ni noma sana. Shadya... leo Mamu kakuweza tena, tokea ile ya mzimu... na sasa hivi hii. Dah! Hiyo ni mbili bila mamaa..."

"We' ngoja tu, nitayasawazisha yote na nitafunga lingine la ushindi. Mamu huwezi kunizidi mimi," Shadya akasema hivyo.

Miryam akamsukuma kiasi mdogo wake kwa bega lake kuonyesha uchangamfu, naye Mariam akacheka kwa furaha na kumfanyia dada yake hivyo hivyo pia.

Tesha akasimama na kusema, "Sawa. Zamu yangu sasa hivi, nikitoka mimi anafata JC, halafu Ankia, halafu da' Mimi, halafu kiboko, sawa? Eh... siyo kiboko, Shadya..."

Mama wakubwa na sisi wengine tukacheka kidogo, huku Shadya akimkata Tesha jicho hilo.

"Acha nawe, mwishowe jicho lipasuke," Tesha akamwambia hivyo.

"Haya Tesha, nenda sasa. Zamu yako," Mariam akasema hivyo.

Tesha akaenda pale ambapo Mariam alikuwa ametoka, naye akasimama kwa njia fulani ya kujiamini. Akaanza kutoa ishara kwa maigizo ya mikono na uso, na wote tulikuwa tumetulia tu na kuendelea kumtazama. Akaanza kuigiza mtindo fulani wa kutembea ulionifanya nitabasamu baada ya kutambua alikuwa anamwigiza nani.

Hata wengine wakawa wametambua upesi sana, naye Mariam, Ankia, Shadya, na Bi Zawadi wakanyoosha vidole huku wakisema kwa pamoja, "JC!"

Sote tukacheka kidogo, naye Tesha akasema, "Ah... kumbe ilikuwa rahisi eh?"

"Kila mtu hapa anaijua tembea yake. JC huyo," Ankia akasema.

Nikatabasamu kidogo na kutikisa kichwa.

"Hivi ulimuigaga nani kutembea hivyo?" Shadya akaniuliza.

"Ahahah... Hrithik Roshan... mwigizaji wa kihindi. Nilikuwa namuiga wakati niko mdogo, mpaka ikawa tembea yangu," nikamwambia hivyo.

"Na unatembeaga vizuri kweli, kwa midundo yaani," Bi Zawadi akasema hivyo.

Huku nikiwa nasugua goti langu taratibu kwa kiganja, nikamwambia, "Ah, kawaida tu mrembo wangu."

Nikapiga jicho pembeni na kukuta Miryam ameniangalia kwa yale macho ya kuhukumu, kisha akakunja midomo yake na kutazama pembeni. Nikacheka kidogo kwa pumzi.

"Enhe, tuambiane sasa. JC kafanyaje?" Ankia akamuuliza hivyo Tesha.

Tesha akatabasamu kiasi, kwa hisia makini yaani, naye akasema, "Ah... hajafanya kitu. Yaani... ninataka tu kumshukuru."

Wote tukaendelea kumwangalia kwa utulivu.

"Kwa kila kitu yaani. Sijui ilikuwaje tu mpaka ukafika hapa JC, ila... nakuthamini sana kaka. Kwa kila kitu ulichofanya, kwa kila unachotaka kufanya, kwa mambo mengi uliyonishauri mpaka nikatulia... na Mamu huyu... JC wewe ni zaidi ya ndugu yaani..." Tesha akasema hivyo kwa hisia.

Alifanya wengine waniangalie kwa macho yenye imani sana, nami nikabana tabasamu langu la hisia.

"Yaani wewe ndiyo wa kufa, kufaana. Tena we' ndiyo yule jamaa anayetajwa kwenye methali 17, mstari wa 17... yule... inasema... yule bwege ambaye amezaliwa kwa ajili ya wakati wa taabu... ndiyo wewe kaka," Tesha akasema hivyo.

Akatuacha tukicheka tu maana alionyesha bado bangi ilikuwepo kichwani!

"Lakini Tesha... hahahah... yaani wewe na Mamu... mtakuja kutuua siku moja kwa vituko vyenu," Bi Jamila akasema.

"Yaani! Umeanza vizuri kweli halafu mwisho ovyo!" Shadya akasema hivyo.

"Ih, kwani nimekosea nini, si ndiyo inasema hivyo? Ni Methali, sijasema Zaburi wala sunagogi! Nasoma Bible, nyie mnanionaje?" Tesha akajitetea.

Tukacheka tena kwa furaha, ndiyo nikamwambia, "Nashukuru kaka. Kama sikuzote navyokwambia, tuko pamoja."

Tesha akaja upande wangu, nami nikasimama pia. Tukakumbatiana kiume huku Mariam, Ankia na Shadya wakipiga makofi eti, nami nikamwona Miryam anatuangalia kwa hisia ya amani.

Tulipoachiana, Tesha akanipiga begani na kusema, "Haya, mzee Hrithik Roshan, uwanja ni wako sasa."

Nikatabasamu kidogo tu, naye Tesha akaenda kukaa.

Nikawa nimemwangalia Miryam kwa tabasamu la kichokozi, kama kumwambia 'ngoja sasa,' nami nikaona kama ameishiwa pozi. Nikaenda pale mbele na kuwageukia wote, wakiwa wananiangalia kwa matarajio mengi, nami nikashusha pumzi na kujiweka vizuri. Kisha nikaanza kutoa ishara ambazo ziliwafanya wengine waanze kucheka upesi.

Nilitoa ishara kwa njia iliyoonyesha kwamba nilifikiria mwanamke fulani, kwa kuigiza kurembua na kuzungusha mikono na mwili kama mwanamke, lakini siyo kwa kupitiliza, nao wakawa wanajaribu kusema yeyote waliyedhani namwaza. Mariam ndiye aliyekuwa akitaja wengi wa wasanii na katuni aliowafahamu, lakini kwa pamoja na wengine, hakuwa akipatia.

Walikuwa wananitaka niongeze njonjo eti ili wamtambue mhusika maana nilikuwa nawachanganya bado, nami nikamtazama Miryam machoni. Alikuwa ananikata jicho lile lililoonyesha kwamba tayari alikuwa amesoma vyema kule akili yangu ilipoelekea, nadhani hata Tesha na Ankia walikuwa wameshagundua ila wakatulia tu, nami nikaona niwarahisishie kazi wengine. Nikiwa nimejishika kiuno sasa, nikaigiza kama nafokea mtu, halafu nikampiga kofi.

Mariam akasimama na kusema, "Da' Mimi! Da' Mimi!"

Nikaacha kuigiza na kuachia tabasamu lililoonyesha kwamba binti alikuwa amepatia, nao wengine wakacheka kidogo huku wakimwangalia Miryam.

"Kibano kinachokuja Mimi, jiandae. JC anataka kulipiza kisasi kwa lile kofi la siku ile," Bi Jamila akasema hivyo, nasi kwa pamoja tukacheka kidogo.

"Tuambie JC, Miryam amefanyaje?" Bi Zawadi akauliza hivyo kwa shauku.

Nikamtazama Miryam usoni, yeye akiwa ananiangalia kwa macho yaliyojaa umakini kama vile kuniambia hataki niongee upuuzi, nami nikasema, "Kuna jambo fulani yaani... nimekuwa nataka kusema tokea...."

Miryam akasimama ghafla sana na kusema, "Jamani, tungekula sasa!"

Ih! Wote wakamtazama kama vile hawakuwa wamesikia alichosema. Najua alikuwa anataka kuepuka kile ambacho nilikuwa karibu kuongea, nami nikamwangalia kwa umakini tu.

"Kula?" Tesha akamuuliza hivyo.

"Eeh," Miryam akamjibu.

"Lakini, si tumeshakunywa chai?" Bi Zawadi akasema hivyo.

"Me nimeshaanza kusikia njaa, najua hata nyie mna njaa..." Miryam akajiongelesha kwa namna hiyo.

Shadya akasema, "Kweli, kweli. Tungekula tu."

"Si tusubiri mchezo uishe kwanza dada?" Mariam akamwambia hivyo.

"Eeeh, bado na wengine hawajacheza," Bi Zawadi akasema hivyo.

"Sa... saa saba sa'hivi mama. Kumbuka bado tuna sherehe ya kwenda... bora kula mapema... si eti ma' mkubwa?" Miryam akaongea hivyo na kuelekeza swali hilo kwa Bi Jamila ili aungwe mkono.

"Aaa.... ni kweli. Tungekula tu sasa hivi. Hata hivyo kimeshaiva," Bi Jamila akawaambia hivyo wengine.

Miryam akanitazama usoni kwa kuibia na kukuta nimemkata jicho makini, naye akaweka uso wa kiburi na kumwambia Tesha, "Kaweke mkeka varandani. Tulie hapo nje... wote, twende, twende, twende Mamu ahah..."

Akawa eti anajifanya amechangamka na kumnyanyua mdogo wake aliyekuwa ameishiwa raha, na wengine wakaanza kunyanyuka pia. Tesha akanipita kwenda kufata mkeka huku akinionyesha ishara kwa kutikisa kichwa kwamba alielewa mchezo, lakini hakukuwa na jinsi. Akarudi tena na mkeka na kuelekea nao pale nje, huku mama wakubwa, Shadya, na Mariam wakiwa wameshatoka, halafu Miryam na Ankia wakawa wanapeleka vyombo vya chakula hapo nje.

Nikategea kwanza kutotoka hapo ndani mpaka ilipokuwa wazi kwamba Miryam alikuja kumalizia kubeba vyombo vya mwisho, nami nikasimama katikati ya njia alipokuwa anaelekea kutoka tena. Wengine wote walikuwa nje sasa, na bibie akiwa anatokea huko jikoni, akakutana na mimi hapo ambapo nilisimama muda mfupi nyuma na kukatisha hatua zake. Akaniangalia usoni kimaswali, huku mimi nikimtazama kwa umakini, naye akajaribu kupita pembeni lakini nikamzibia njia makusudi.

Nikamzibia njia kwa makusudi na kusimama mbele yake kwa mara nyingine alipojaribu kunikwepa tena, naye akawa ananiangalia kama anashangaa.

Nikiwa namtazama kwa umakini, nikamuuliza kwa sauti ya chini, "Kwa nini ulinikatisha kabla sijatoa point yangu?"

Alikuwa ameshikilia vijiko, naye akaangalia pembeni na kusema kwa sauti tulivu, "Nilijua tu hiyo point yenyewe ingekuwa ya kipuuzi... ndiyo sababu."

Nikatoa tabasamu hafifu na kusema, "Ingekuwa ni point ya kipuuzi, usingenikatisha. Ila unajua ilikuwa na maana fulani ndiyo maana ukafanya hivyo, ikimaanisha ni maana ambayo ulikuwa umeifikiria."

Akaangalia upande wa mlangoni na kisha kunitazama, kisha kwa sauti ya chini akasema, "Sina muda wa kukaa kufikiria mawazo yako ya kipuuzi!"

Nikamwambia, "Ahaa, kumbe? Kwa hiyo hata tukienda hapo nje nikawaambia wengine nilichotaka kusema kuhusu wewe, haitakuwa mbaya kwa sababu ni ya kipuuzi hata hi...."

Sura yake ikageuka kuwa ya wasiwasi, naye akanikatisha kwa kusema, "Wewe!"

Nikatabasamu kiasi.

Akafumba macho na kushusha pumzi, kisha akasema, "Hebu nipishe bwana..."

"Subiri kwanza," nikamwambia hivyo na kumshika mkono.

Akautoa mkono wake kwa nguvu huku akiangalia mlangoni kama kujihami.

"Mbona kama unaogopa ikiwa haujali nilitaka kusema nini?" nikamuuliza hivyo.

Akanishusha na kunipandisha.

"Okay, kwa hiyo... hutaki kusikia nilichokuwa nataka kusema?" nikamuuliza hivyo.

Akavuta fikira kwanza, kisha akatazama pembeni na kusema, "Ndiyo, sitaki."

Nikatabasamu kidogo na kusema, "Mwongo."

Akanitazama usoni kwa jicho kali.

Nikatabasamu zaidi na kumwambia, "Mwongo-mkweli wewe. Unachokisema kwa mdomo ni tofauti na unachokitaka kwa moyo. Huwezi kukataa kwamba niko sahihi."

"Na kama nikikataa?" akaniuliza hivyo kwa sauti tulivu.

"Utakuwa unaupinga moyo wako mwenyewe..." nikamwambia hivyo.

Akazungusha macho yake na kuangalia pembeni kwa kukerwa.

"Na bado tu huo moyo wako utaendelea kukusumbua kwa sababu unajua utakuwa umepitwa na kitu ambacho kingeufurahisha," nikasema hivyo.

Akaonekana kutojali maneno yangu na kuangalia pembeni tu.

Nikamwambia, "Haijalishi lakini nilitaka kusema nini wakati wa charade, point yangu kwako ni hii. Ninakuona. Ninakuelewa Miryam. Umeshakuwa kama mtu ambaye anaumizwa sana mpaka anazoea maumivu, kwa hiyo unajitahidi kuficha hisia zako mapema kabla hata hujahisi chochote ili usiumie... lakini hiyo haiwezekani kwa asilimia zote. Maumivu yatakuwepo tu. Nimeona hiyo kuwa case kwa Joshua, shangazi zako, na labda hata mtu wa mwisho uliyekuwa naye kimahusiano kabla ya kufikia wakati huu...."

Miryam akaniangalia usoni kwa hisia makini baada ya mimi kusema hivyo.

"Hayo ni mapito, Miryam. Hauhitaji kueleza mengi kuhusu mapito yako... tayari ninaelewa. Na ukweli ni kwamba... siyajali. Nimekupenda wewe kama nilivyokukuta, kwa hiyo yaliyopita hayajalishi zaidi ya yale yanayokuja, hivyo ndivyo navyoamini sikuzote..." nikamwambia hivyo kwa hisia.

Akatazama chini kwa utafakari.

Nikamwambia, "Natumaini hautaacha mapito yako yawe nawe sikuzote Miryam. Baada ya mambo mengi yenye kuumiza ambayo umepitia, hata kama siyajui... natumaini utanipa nafasi... nafasi ya kuwa nawe ili usiogope lolote tena kuhusu maumivu ya kihisia... kwa sababu hata maumivu yaje ya aina gani, nitakuwa mtu pekee wa kukufanya uhisi kwamba hayakuwahi kukupata... na hayatakupata tena."

Miryam akapandisha macho yake taratibu na kuniangalia usoni kwa hisia sana, halafu shingo yake ikalegea kiasi, yaani... akapindisha uso kidogo huku akiniangalia kwa njia iliyoonyesha kutekwa kifikira na kihisia kwa uzito sana. Niliendelea kumwangalia kwa hisia pia, nikiona namna ambavyo kweli maneno yangu yalimpa athari nzuri mno, yaani ule ugumu ulikuwa unayeyuka, naye ndiyo akawa kama ameshtuka baada ya kuniangalia kwa njia hiyo legevu na kutazama chini kama vile mtu anayejiuliza 'hivi nina matatizo gani?'

Nikatabasamu tu kwa hisia na kuchukua vijiko vyake, ambavyo aliviachia kwa wepesi kabisa, halafu tukatazamana machoni kwa hisia tulivu kabla sijamwacha hapo akiwa katikati ya tafakari nyingi mno. Hapo najua nilikuwa nimepigilia msumari wa mapenzi ndani zaidi ya moyo wake, yaani asingeweza kupinga tena hata kama angejifanya mgumu kiasi gani, na nafikiri haingechukua muda mrefu kwa huyu mwanamke kunikaribisha ndani ya huo moyo kwa dhati yote. Sijui ingekuwaje tu!







★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★


Pata Full Story WhatsApp au inbox

Whatsapp +255 678 017 280

Karibuni sana
 
JC we kiboko mzee baba
 
Mchumba somo linazidi kumuingia vzr Kwenye ubongo wake maana moyo wake ulishafunguka kitambo TU sema hapo anatumia akili yake kuucontrol moyo na mihemko yake
 
Mchumba somo linazidi kumuingia vzr Kwenye ubongo wake maana moyo wake ulishafunguka kitambo TU sema hapo anatumia akili yake kuucontrol moyo na mihemko yake
Yuko vizuri wangekuwa madem wasiojielewa angeshachanua kitambo tu ila yeye anataka kuhakikisha hisia zake hazizidi akili zake ili aweze kuamua ipasavyo
 
MIMI NA MIMI 2

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA ISHIRINI NA NANE

★★★★★★★★★★★★★★★★★★


Basi, sote tukawa tumeshiriki mlo mzuri sana hapo varandani, story zikiwa ni zenye kufurahisha hasa kuhusiana na mchezo ule wa charade tulioufanya muda mfupi nyuma. Ni mimi na Tesha ndiyo tulikaa kwenye viti huku tukishika sahani zenye vyakula, na wanawake walikaa mkekani. Miryam alikuwa mtulivu tu, akiongea mara moja moja sana na kula taratibu, nami niliona jinsi ambavyo alikwepa kuniangalia hata mara moja toka tulipoongea muda ule pale sebuleni. Najua maneno yangu yalikuwa yamegonga kengele nzito mno moyoni mwake.

Tulipomaliza kula, ilikuwa imeshaingia mida ya saa nane mchana, hivyo wanawake wakaona ni vyema kuanza maandalizi. Yaani wangeondoka hapa kwenye mida ya saa moja kuelekea huko ukumbini, na usafiri ambao wangetumia ulikuwa wa kukodisha. Dina ndiyo angekuja na huo usafiri baadaye ili kuwapitia wengine, ndivyo ambavyo Shadya alisema.

Kwa hiyo mambo ya urembo kwa wanawake yakaanza kwa Miryam, Shadya, Mariam na Ankia kwenda saluni kuosha ama kutengeneza nywele upesi, na waliamua kujigawa kwenda kwenye saluni tofauti-tofauti ili kuokoa muda; isipokuwa Miryam na Mariam, ambao walikwenda kwenye saluni moja.

Hivyo mimi na Tesha tukabaki hapo kwao pamoja na mama wakubwa, tukipiga story na nini, mpaka inafika saa kumi jioni. Nikawa nimepigiwa simu na mama yangu. Kama nilivyokuwa nimezoea, nilipenda sana kuzungumza naye katika hali yenye utulivu zaidi, na yeye alikuwa amepiga ili aniambie jambo fulani muhimu, kwa hiyo nikakata na kuwaomba marafiki zangu ruhusa ya kuwaacha kwa muda mfupi kwanza ili nikazungumze na simu.

Hawakuwa na shida kwa jambo hilo, kwa hiyo nikatoka hapo na kurudi pale kwa Ankia. Utulivu uliokuwepo hapo sebuleni ulitosha ili niongee na mzazi kwa uhuru, nami nikaketi sofani. Nikampigia tena mama tuzungumze vizuri.

"Vipi ma, mnaendeleaje?" nikamuuliza hivyo baada ya yeye kupokea.

"Safi tu. Na wewe?" akauliza.

"Niko poa. Haya... anza kuangusha mabomu sasa..."

"Anhh... mbona unakuwa mwoga?"

"Siyo uoga, najua tu ukisema 'important' ni lazima iwe ishu nzito..."

"Yeah, na unajua ni nini..."

"Si tuliongea mama, nikakwambia we' na mzee...."

"Stella alikuja tena," akanikatisha.

Nikabaki kimya tu.

"Amekuja jana. Na alikuja naye... mtoto wenu," akasema hivyo.

Nikashusha pumzi kiasi nikiliingiza suala hilo vizuri akilini, nami nikamuuliza, "Anaendeleaje?"

Mama akasema, "Wow! Hii ndiyo mara ya kwanza kabisa nimekusikia unauliza hivyo Jayden."

Nikaingiwa na hisia za kukosa amani kiasi.

"Ahah... anaendelea vizuri. Amekua, sasa hivi ana mbio kama wewe hahah..." akasema hivyo.

Nikatabasamu kiasi.

"Tumekaa wote hapa jana... nikamwambia Stella ulikuja ile juzi. Anatamani sana akuone tena Jayden... ili umwone na mtoto," akaniambia hivyo.

Nikashindwa hata kutoa itikio lolote lile na kutikisa kichwa tu kwa kusikitika.

"J, bado upo?" akauliza.

"Ndiyo mama. Yaani... nawaza tu mambo mengi..."

"Usiwaze sana Jayden. Panga mkutane umwone mtoto, ama upange uje tena nimwambie na Stella amlete ili...."

"Hamna mama, usifanye hivyo," nikamwambia.

"Kwa nini? You still... sawa najua umesema mpaka likizo ikiisha, lakini Jayden kwa nini tu usianze sasa hivi? Jamani, hata ujaribu tu..." akaniambia hivyo kwa hisia.

Nikabaki kimya.

"Yaani nikimwangalia mwanao, nakuona wewe tu. Sura, macho, yaani... mnafanana mpaka raha yaani. Natamani sana niwaone mkiwa wote. Hivi hata umeshawahi kumwona tena toka... toka kipindi kile?" akauliza hivyo.

Nikasema, "Hapana."

"Kwa nini sasa usionane naye sasa hivi? We' hujisikii vibaya kabisa?"

"Najisikia vibaya mama, hujui tu. Ila kwa kile ambacho Stella alifanya nipitie, yaani... hhh... siyo rahisi kihivyo. Siyo makosa ya mtoto, I know... najitahidi sometimes kufikiria... labda ah, nionane nao tu, lakini najikuta nakwama. Imeshakuwa ngumu, yaani mpaka nashindwa kuelewa ni kwa nini iko hivyo..." nikaongea kwa hisia.

"Anza kwa kumwona tu mwanao Jayden. Kwanza. Unanielewa? Kuhusu Stella... Jayden unatakiwa tu kuacha. Acha kuona kile alichokufanyia kuwa sehemu ya maisha yako ambayo haitafutika. Kweli unataka kuniambia baada ya huo muda wote kupita, haujapata jambo la kukusaidia kuyafuta hayo yote?" akaongea hivyo kwa msisitizo.

Kauli yake ikanifanya nimfikirie Miryam. Alikuwa sahihi kabisa!

"Kwa nini usi...."

"Uko sahihi mama, uko sahihi," nikamkatisha kwa kusema hivyo.

"Kwamba?"

"Ahah... umesema kweli. Ninakuwa mnafiki na mwongo nikisema siwezi kumwona mwanangu kwa sababu ya alichofanya mama yake. Nimetambua hilo sasa. Nime... nimekuwa mwoga. Kama ulivyosema, yaani... ni woga ndiyo," nikamwambia hivyo.

"Kwa nini unasema hivyo?" akauliza.

"Kwa sababu ndiyo ukweli. Kuna... kuna jambo limefanya nitambue hilo, na uko sahihi kabisa mama. Nitahitaji kumwona mtoto," nikamwambia hivyo.

"Eeh, Jayden ufanye hivyo. Tena mapema kabisa..."

"Sitaharakisha sana mama, kuna mambo nataka yakae sawa kwanza. Ila nakuahidi. Nitaonana naye. Niamini," nikamwambia hivyo kwa uhakikisho.

Akasema, "Sawa. Wewe weka mambo yako sawa. Lakini ukae ukijua hakuna kitu kingine nachotamani zaidi ya wewe kuanza kuwajibika kama baba kwa mtoto wako. Yaani... itanipa furaha sana. Najua hata wewe itakupa furaha."

"Ndiyo, najua. Nipe muda mfupi tu. Nitarekebisha mambo," nikamtuliza namna hiyo.

"Haya, sawa. Nashukuru umenisikiliza..."

"Always."

"Mambo mengine vipi?"

"Yanasonga. Huu mwezi ukiisha vizuri, nitakuletea surprise kubwa sana," nikamwambia hivyo.

"Mmmm, usiniambie..."

"Ahahah... ndiyo utajua sasa. Ukae tayari," nikasema hivyo kwa furaha.

"Hahah... sawa. Ukuje huku tena na Mariam. Nimem-miss eti, wakati ilikuwa ni juzi tu..."

"Usijali, atakuja. Halafu... kuhusiana na ishu ya Jasmine na Kevin... mambo yamekaaje sa'hivi?"

"Bado Jas kamchunia. Kevin ameshanitafuta tukaongea, nikamwambia atulie tu. Mambo yataenda vizuri nadhani, tusubiri tu huyu ajifungue, wataungana tena," akasema hivyo.

"Safi. Msalimie huyo kwa ajili yangu basi. Nitakuja kuwaona tena," nikamwambia hivyo.

"Haya baba. Uwe salama huko. Na usisahau ahadi yako. Naitaka hiyo surprise..."

"Ahahah... yaani we' na Jasmine mnafanana sana. Huwa hamwezi kukumbuka kusahau..."

"Hahahah... haiwezi tokea. Ukisema unaleta surprise, uilete kweli. La sivyo..."

"Masikio yatavutwa..."

"Hahah... kumbe unajua," akasema hivyo kwa furaha.

"Haya ma. Asante kunicheki. Tutawasiliana," nikamuaga.

"Haya. Msalimie Mariam eh? Mtafutieni na simu tuwe tunawasiliana bwana..."

"Usihofu, atapata tu. Asante kwa kujali," nikamwambia hivyo.

"Sawa. Jioni njema," akaaga.

"Haya."

Baada ya kuzungumza hivyo na mama, nikakaa kutafakari mambo kwa utulivu. Ishu ya mtoto wangu ni suala ambalo najua mama alitamani sana kuona narekebisha haraka, na hasa baada ya haya maongezi ndiyo nikawa nimetambua kuwa kweli kilichofanya nisitake kushughulika nalo ilikuwa ni woga tu, woga wa mambo mengi. Kuna vitu vyenye kuvunja moyo vilivyotokea baina yangu na huyo Stella ambavyo ndiyo vilifanya mpaka nikawa nakwepa kumwona mtoto, lakini kwa wakati huu nikaanza kufikiria suala hilo mara mbili mbili.

Yaani, kuna sehemu ndani yangu ilitamani kumwona huyo mtoto, ingawa bado nilikuwa naogopa kufanya hivyo. Chanzo cha woga wangu ilikuwa ni kwenda kinyume na msimamo niliokuwa nao kuhusiana na hilo suala, na ingekuja kueleweka vizuri baadaye msimamo huo ulikuwa nini, na ulisababishwa na nini. Lakini baada ya mama kuniuliza ikiwa hakukuwa na jambo lolote lililonisaidia kuyafunika mapito, nikawa nimekumbuka maneno yangu mwenyewe niliyomwambia Miryam muda mfupi nyuma.

Nilitaka kumsaidia ayasahau maumivu ya mapito yake kwa kumwonyesha upendo wangu, hata kama sikuyajua, hivyo kama na mimi nilitaka kuyaweka pembeni mapito na kumfikia mtoto wangu, ningetakiwa kuupata msaada kama huo. Na ni nani mwingine ambaye angenipa kama siyo mtu ambaye nilimpenda? Ni Miryam ndiye niliyemhitaji ili kweli nijitahidi kuweka mambo yote sawa. Alikuwa ameshanifanya nijione kuwa mtu bora, lakini kuwa naye kabisa ndiyo kungenisaidia hata niweze kuwa baba bora pia.

Yeye ndiyo angekuwa kikamilisho cha furaha niliyohitaji, kama vile mimi nilivyotaka kuwa furaha yake pia. Kwa hiyo ingekuwa ni kuupiga, kuuua, na kuugalagaza moyo wake mpaka uyeyukie kwangu, na baada ya hapo, najua angenisaidia sana huyu mwanamke kufanya maisha yangu yawe mazuri sana. Safari ingekuwa ngumu hata kama tuseme Miryam angekubali kuwa wangu, lakini najua yeye ndiyo angekuwa kikamilisho cha furaha yangu hata kwenye maumivu, kwa kila kitu yaani. Nlimhitaji sana huyu mwanamke.

★★

Bwana, nilikaa tu hapo hapo sofani nikitafakari na kutafakari mpaka ikafika mida ya saa kumi na mbili kasoro. Ankia akawa amerejea, na alipendeza sana kichwani kwa kusuka nywele za kizungu za mawimbi-mawimbi, ambazo zilikuwa nyingi yaani zilijaa kichwani na kutikisika kwa pamoja kila alipojongea, nami nikamsifia kwa kupendeza. Akasema na wenzake walikuwa wamesharudi hapo kwa Miryam na kuanza kujiandaa, hivyo naye akafanya upesi kwenda kuoga ili avae kabla Dina hajafika.

Nilikuwa nina hamu ya kumwona Miryam, najua angekuwa amejitengeneza vizuri sana, lakini nikaona nitulie tu hapo hapo hadi Ankia akimaliza kujiandaa. Mwanamke akaenda bafuni na kuoga, kisha akarudi ndani kwenda kuvaa. Tesha akawa amenitumia ujumbe kuniambia kwamba ndugu zake walikuwa wamerudi pia na walikuwa wanajiandaa, hivyo niende hapo kwao kutoa support na nini kabla hawajaondoka, nami nikamwambia ningekwenda pamoja na Ankia muda si mrefu.

Ile ndiyo inakaribia kuingia saa moja tu, Ankia akawa ametoka huko chumbani kwake. Alipendeza sana kwa kuvalia gauni la rangi ya samawati, fupi kufikia mapajani, lenye mikono mirefu lakini kuanzia usawa wa juu mikononi kwa kuacha mabega wazi, na lililoubana mwili wake kama limeung'ata. Yaani kwa jinsi alivyokuwa na mikunjo ya aina yake, lilimchora vizuri sana, na miguuni alivaa viatu vyekundu vya kuchuchumia, huku usoni akijiremba vyema kwa kupaka lipstick nyekundu midomoni, na bila kusahau kapini puani. Macho yake yalionekana kuwekewa kope fupi za bandia, yaani alikiwasha!

Akaja hapo karibu yangu na kuanza kuzunguka-zunguka, nami nikamsifia na kumuuliza hizo kope aliziweka saa ngapi. Ndiyo akaniambia alikuwa na seti chache za kupachikia kope huko chumbani kwake, kwa hiyo akaniomba nichukue simu yangu ili nimpige picha chache. Nikamfotoa akiwa amesimama, kisha akiwa amekaa sofani, na baada ya hapo ndiyo akaenda kuchukua pochi yake chumbani ili tuelekee kwa kina Miryam. Akarudi huku akiwa ameshika na kibanio kizuri cha nywele, akisema anampelekea Miryam, nasi ndiyo tukatoka pamoja na kufunga nyumba.

Giza la saa moja lilikuwa limeshateka anga na kuukaribisha usiku vyema, na wakati tukiwa tunaelekea kwa kina Miryam tuliweza kuwaona mama zake, Shadya, na Tesha kwa pale nje sehemu ya uvaranda, nasi bila kuchelewa tukaingia getini kwao. Kulikuwa na gari aina ya Noah nyeusi likiwa imeegeshwa pembeni ya uzio wa nyumba hii hapo nje, ikiwa wazi ndiyo gari ambalo lilikodiwa kuwapeleka huko kwenye sherehe. Dina alikuwa amefika.

Ndiyo sasa baada ya kuingia getini tukaweza kuwaona na wengine hapo, akiwepo mama Chande na mwanaye, Fatuma, Dina, mwanadada mwingine ambaye sikumfahamu aliyeonekana kuwa amekuja na Dina, na mwanaume kijana ambaye sikumjua pia. Tesha alikuwa akiwapiga picha wakina Dina, Shadya, pamoja na Bi Zawadi pia, mwanga wa taa ya nje ukifanya waonekane vyema kwa jinsi wao pia walivyokuwa wamependeza, naye Ankia akaona aliunge pamoja nao.

Nikamsalimia huyo jamaa mwingine aliyekuwa amesimama pembeni tu kama vile anasubiria mke wake, nami nikamsogelea Tesha karibu alipokuwa anawapiga picha wengine. Ndiyo kidogo tu na binti Mariam akawa ametokea ndani kwao na kuja kujiunga nasi, akanionyesha jinsi ambavyo alipendeza sana nami nikamsifia kwelikweli, kisha mama zake wakamwambia na yeye aende kupiga picha.

Mariam alikuwa amependeza kweli. Alivaa gauni refu la blue bahari lililochanua chini kama mwamvuli ulioishiwa nguvu, likiwa na urembo wa vidude vidogo-vidogo vilivyomeremeta, na kichwani alikuwa amesukia rasta nyeusi zilizoweka mtindo wa mafundo makubwa mawili kutokea mbele ya kichwa chake kuelekea nyuma kama mapembe ya ng'ombe yaliyolala, mwishoni zikiwa nyembamba na ndefu sana.

Kalipendeza mno, kama Cinderella! Kuna watu wangekaangalia kwa macho mazuri na mabaya huko ambako wangeenda, hata kama kwa sehemu kubwa ingekuwa ni wanawake. Ila ndiyo ingebidi tu aanze tena kujichanganya na walimwengu ili aujue zaidi ulimwengu uliomzunguka.

Alipoenda kupiga picha pia, Mariam akawa kama amemsemesha kitu fulani Ankia, naye Ankia akasema 'eeh kweli,' halafu akaanza kunifata. Akanisogelea karibu na kunipatia kile kibanio cha nywele ili nikampe Miryam kule ndani, akisema Mariam ndiyo aliagizwa aje kumkumbusha ila picha zilikuwa zimemkolea, hivyo nimsaidie kukipeleka kwa ajili yake. Haikuwa na neno.

Nikawaacha wote hapo nje, na nilifikiri ningemkuta Miryam sebuleni, lakini nilipoingia, hakukuwa na mtu yeyote hapo. Nikasogea mpaka usawa korido na kuangalia jikoni, hakuna mtu, hivyo ikawa wazi kwamba alikuwa chumbani kwake. Nikaamua nimpelekee tu huko, sijui hata ni kwa nini kibanio chake cha nywele alipewa Ankia amtunzie, maana Miryam hakuwa na mambo ya kuazima-nikuazime-tuazimane kabisaaa. Ama labda alimnunulia.

Nikaufikia mlango wa chumba chake na kugonga kidogo, na kutokea humo ndani nikamsikia bibie akisema, "Njoo, ingia."

Sikuwa nimesema chochote, na nilitaka nimwambie kwamba nimemletea kibanio, lakini sikuona haja tena. Kamsisimko kale ka kukaribia kuingia chumbani kwake kakanivaa haswa, jumuisha na tumawazo twa kishetani endapo ikiwa ningemkuta ndiyo anavaa. Wee!

Nikabenjua kitasa na kuusukuma mlango, na nilipofanikiwa kupaona chumbani kwake, nikawa nimemwona na yeye pia. Yaani nilikumbuka vizuri sana kwamba hii ndiyo iliyokuwa mara ya pili kwangu kuingia ndani ya chumba chake tokea ile siku ya kwanza kabisa nimekuja huku Mzinga, na wakati huu kilikuwa kimependezeshwa hata zaidi kwa jinsi ambavyo kilipangiliwa. Kila kitu kilikuwa kizuri, palinukia haswa, lakini mimi nikawa nimekaza fikira zangu kwa mwanamke huyo ndani hapo. Tena nilizubaa kabisa.

Miryam alikuwa amekaa mwishoni mwa kitanda chake, akiwa amegeukia huko mbele, na hivyo ningemwona kwa nyuma zaidi. Alikuwa amevaa gauni refu, lakini, halikuziba mgongo wake, yaani kutokea sehemu ya kiuno chake mpaka shingoni, pote palikuwa wazi. Gauni hilo lilikuwa ndiyo lile la rangi ya maroon nililomwambia achukue ile jana, lilikuwa na sehemu zilizong'aa kama satini, likiwa la mtindo fulani wa nguo nyepesi sana iliyokaribia kuonyesha vile alivyovaa ndani, lakini vilifichika.

Inaonekana sehemu ya kifua chake huko mbele ilizibwa, na mikanda iliyolishikilia ilipitishwa kwa ile njia ya X huko mbele kwake, na ikafungiwa nyuma ya shingo yake, kwa hiyo ni hiyo pekee ndiyo iliyokuwa inaning'inia mgongoni kwake. Aisee, huo mgongo! Yaani ulikuwa mweupeeh... hakuna doa hata chembe!

Alikuwa amekaa kwa kukunja nne, akionekana kufunga kamba za kiatu cheupe cha kuchuchumia kwenye mguu mmoja, hivyo alikuwa ameinama kiasi. Nywele zake hakuwa amesuka, nadhani aliziosha tu zake kabisa, na kweli wakati huu zilikuwa zimerefuka haswa maana alikuwa amezichana vizuri na kuzilazia upande mmoja wa bega lake kwa mbele.

Hayo yote yalikuwa yameniingia vyema sana ndani ya sekunde chache tu baada ya kuingia humo, na nikiwa bado nauangalia mgongo wake, akasema bila kugeuka, "Niletee, nisije nikawachelewesha..."

Nikawa kama nimeondokwa na bumbuazi langu, nami nikayatafakari maneno hayo vizuri. Ooh, alimaanisha kibanio, nami nikakiangalia kiganjani na kutaka kumsemesha pia ili ajue kuwa ni mimi ndiye niliyemletea.

"Wahi basi! Njoo unisaidie kuzibana hizi," akaongea hivyo.

Sasa akawa amemaliza kufunga kiatu chake, naye akazivuta nywele zake laini kutokea mbele na kuanza kuzizungushia nyuma ya kichwa chake. Sijui alifikiri mimi ni Mariam masikini? Kwa vyovyote vile, najua alihitaji msaada, hivyo nikaamua tu kumsogelea karibu zaidi ili nimfungie kibanio chake. Ila kuutazama mgongo wake kwa nyuma mpaka kiunoni, aisee! Ni madhambi tu ndiyo yaliyokuwa yakiiteka akili yangu.

Bila kunena lolote, nikafika nyuma yake na kuanza kumwekea kibanio chake, naye Miryam akasema, "Yaani Ankia ungejua jinsi hii wiki imekuwa ngumu kwangu? Natumaini hii sherehe itanisahaulisha mengi yaliyonisonga angalau kwa huu usiku tu."

Nikajiuliza maneno hayo yangekuwa yamebeba maana gani, lakini inaonekana urafiki wake na Ankia ulikuwa wa karibu zaidi kwa wakati huu, na ulihusisha mambo mengi sana mpaka sasa akawa akimfungukia kwa yaliyomtatiza.

Akashusha pumzi na kusema, "Ulichoniambia saa zile kilikuwa na ukweli, lakini tatizo huyu Jayden hataki kusikia. Anaongea mengi, anafanya vituko vingi, mpaka nashindwa kujua la kuwaza... au kuhisi."

Kauli yake ikanifanya nitabasamu kiasi, nami sasa nikawa nimemaliza kumbania nywele zake vizuri, lakini kwa sababu ya kutaka kuendelea kuwa hapo, nikawa tu bado nimekishikilia kibanio.

Akasema, "Mtu anang'ang'ana, anang'ang'ana tu... anapoanza michezo yake nakosa amani... lakini... eti nikiwa tena simwoni... nakuwa nakosa amani. Ah... yaani sijui hata niwaze nini. Twende tu huko nikaichanganye akili aisee, a-ah..."

Nikawa nikitabasamu kwa kujivuna kiasi, kwamba nilikuwa naisumbua sana nafsi yake kwa njia mbaya lakini nzuri, na ile nilipokuwa naziachia nywele zake ili niondoke kabla hajageuka, kidogo sana kiganja changu kikawa kimegusa mgongo wake. Mabega yake yakapanda juu kiasi kama vile kuonyesha amesisimka, na sikuwa nimetegemea hili lakini mara akasema...

"Jayden!"

Akanyanyuka na kunigeukia upesi, nami nikarudi nyuma kidogo huku nikimtazama kwa utulivu. Aisee, alikuwa amependeza! Kifua chake kilivyokuwa kimetuna mbele, kiuno chake kikionekana kuwa na wembamba kiasi shauri ya kutokuwa na tumbo kubwa, na kutokea hapo kwenda chini jinsi ambavyo umbo lake lilijikata kwa hips matata, ilikuwa kama vile namwangalia mwanamke mgeni au mdoli mpya kabisa!

Mwili wake ulikuwa mweupe, ngozi laini, yaani nilikuwa namtazama kama vile siamini kabisa. Usoni ndiyo alikuwa balaa. Lipstick yenye uzambarau uliong'aa uliipendezesha sana midomo yake, nywele kidogo kwa mbele zilizodondokea upande mmoja wa uso, na macho yake yaliyonitazama kimshangao yalikuwa mazuri kupindukia. Ah, siyo poa! Yaani Miryam alikuwa beyond fire!

Na huyu mwanamke alikuwa na utambuzi wa hali ya juu, yaani sikuwa nimesema chochote kile toka nimeingia, lakini mguso wangu mdogo tu ukamfanya atambue kwamba ilikuwa mimi kabla hata hajageuka. Hisia!

Alikuwa akiniangalia kwa macho yenye taharuki kidogo, akijishika pale nilipomgusa mgongoni kwake huku kiganja chake kikitetemeka kiasi, naye akasema, "Wewe... we... una... umechanganyikiwa? Unafanya nini humu?"

Alikuwa akitumia sauti ya chini, nami nikamwambia, "Nilikuletea kibanio... Ankia alikuwa bize."

"Eh Mungu! Yaani umeingia tu... ungenikuta navaa?" akauliza.

"Mshukuru Mungu sijakuta unavaa," nikamwambia hivyo.

Akanitazama kimaswali kiasi.

"Usiogope... nilikuletea tu kibanio. Sema... nimekuja na kukuta una kesi na mimi," nikamwambia hivyo.

Akanitazama usoni kimaswali zaidi, naye akasema, "Sina kesi na mtu mimi. Nakuomba uende. Nenda."

Akanishika mkono akitaka kunigeuza, lakini nikaweka mgomo na kumwambia, "Niambie huwa mnaongea nini na Ankia. Kama unataka kulalamika, lalamika kwangu. Niko hapa."

"Sihitaji... naomba uende, nipishe me nimalize kuv...."

Nikaishika mikono yake kwa nguvu usawa wa viwiko na kusema, "Toa kero yako Miryam. Niambie, sasa hivi, kwamba ukiniona nakufanya ukose amani, na useme kwa nini usiponiona tena unakosa amani. Wewe unafikiri ni kwa nini?"

Akatulia na kuendelea kunitazama machoni kwa umakini.

Nikiwa makini zaidi wakati huu, nikamwambia, "Unaijua sababu inayokufanya ukose amani Miryam. Lakini bado unaendelea kujitia ugumu, ndiyo maana ni lazima uhisi hivyo. We' hauchoki hiyo hali? Kwa nini tu usikubali kwamba unanipenda? Kwa sababu hata ufanye nini, hata ukatae mara ngapi, ninajua kwamba unanipenda, na mimi sitaacha kukusumbua mpaka ukiri hilo. Unataka nifanye nini zaidi ili uamini pendo langu kwako? Eh?"

Nilikuwa namwongelesha kwa njia yenye hisia zaidi sasa, naye akaangalia chini akionekana kukosa amani.

"Miryam... hebu niambie. Unataka tukae kwa muda mrefu kiasi gani, mimi niendelee kukushawishi ili ukubali hisia zako kwangu? Hm? Miezi? Mwaka? Kwa sababu ninaweza kuendelea kukushawishi ukubali hata kama ikichukua miaka, lakini kwa nini mpaka huo muda wote upite? Kwa nini usikubali kwamba unanipenda ili huo muda ambao ungepotea nikikushawishi tu, ndiyo utumike kukupa mapenzi unayostahili? Eti mama? Kwa nini uogope kujipa nafasi ya kuufurahia upendo wako kwangu?" nikamsemesha kwa kubembeleza.

Akiwa bado ametazama pembeni, akasema, "Hauna uhakika na unachokisema. Naona bado unaota tu. Mimi sikupendi... na... navyoongea na Ankia... haikuhusu..."

Nikawa natikisa kichwa kwa kusikitika kiasi.

"Hebu niachie... me nachelewa...."

Nikamvuta kwa nguvu karibu zaidi na mimi, naye akanitazama usoni kwa macho yenye mshangao.

"Acha kuwa mkaidi. Hakuna faida yoyote unayopata kwa kuwa hivi, zaidi tu naona unaelekea kujiumiza. Kusubiri ninaweza Miryam, lakini sisi siyo watoto wadogo. Unajua kabisa kwamba unanipenda, acha kuwa na kiburi. Uliniahidi usingekuwa hivyo tena baada ya Joshua, kwa nini unataka kurudia yale yale?" nikamsemesha kwa mkazo.

"Kwani ni lazima ni...."

"Enough, Miryam!" nikamkatisha kwa sauti thabiti.

Akawa ananiangalia kwa macho yenye hisia, huku pumzi zake zikipanda zaidi.

"Inatosha. Kiri kwamba unanipenda, unachoona kinakunyima amani, ndiyo ambacho kitakupa furaha. Kwa nini uhisi kuwa kila kitu kitaporomoka ukijiruhusu kufurahia mapenzi? Kwa nini uwe hivyo?" nikamuuliza hivyo kwa hisia.

Nyuso zetu zilikuwa karibu zaidi nilipokuwa namwambia hayo, tukiangaliana kwa hisia mvurugo yaani, na ndipo...

"Mimi..."

Sauti ya Bi Zawadi ikasikika kutokea huko nje, sijui sebuleni, akiwa anamwita. Miryam akatazama sehemu ya mlangoni, palipokuwa wazi bado, naye akaniangalia kwa njia yenye wasiwasi kiasi.

"Jayden, niachie... unapaswa utoke humu!" akaongea hivyo huku akijaribu kujinasua kutoka mikononi mwangu.

Nikamkaza hata zaidi na kumwambia, "No. Leo sitakuachia."

"Jayden!" akaniita kwa sauti ya chini akianza kutaharuki.

"Toa kero yako, Miryam. Sema. Niambie unasumbuka rohoni kwa sababu unanipenda..." nikamsemesha kwa sauti makini.

"Jayden, niachie..." akaendelea kufurukuta.

"Mimi... wahi mama, saa moja ishaingia..." Shadya pia akasikika kutokea huko nje.

Miryam akasema kwa sauti ya chini, "Jayden niachie, unaniumiza... nitapiga kelele..."

"Piga. Lakini sikuachii hadi uniambie ukweli..." nikasema hivyo.

"Unataka ukweli gani? Aa..." akaongea kwa kuudhika.

"Sema unanipenda..." nikasisitiza.

"Mimi? Miryam?" sauti ya Bi Jamila ikasikika ikimwita, lakini ya kwake ilionekana kuwa ndani zaidi, kumaanisha alikuwa anakuja huku.

"Jayden, ma' mkubwa atatukuta! Niachiiie..." Miryam akasema hivyo huku akitikisa mguu mmoja chini.

"Atukute tu. Sikuachii mpaka useme. We' mwenyewe unajua kabisa kwamba sitaacha kukusumbua mpaka ukubali, lakini unafikiri napenda nikijua kwa njia kubwa unakosa amani?" nikamuuliza hivyo.

Akawa akigeuka mara kwa mara kuangalia mlangoni na kuniangalia tena kwa wasiwasi sana.

"Unakosa amani kwa sababu unanipenda ila hutaki kukubali. Kubali kwamba unanipenda Miryam. Unanipenda, ila tu unaogopa, si ndiyo? Si ndiyo Miryam? Unaogopa kukubali kwamba unanipenda Miry...."

"Ndiyo!"

Maneno yangu yakakatishwa na mwanamke huyu baada ya yeye kusema hivyo. Alikuwa ameisema hiyo 'ndiyo' kwa sauti ya chini lakini kiukali, alipokuwa amejaribu kuiondoa mikono yake kutoka kwenye yangu kwa nguvu. Baada ya yeye kusema hivyo, nikabaki nimemtazama usoni kwa umakini sana, huku na yeye akiniangalia machoni na kupumua kwake kukiwa kumepanda zaidi.

Akameza mate na kusema, "Nakupenda..."

Nikajikuta naachama mdomo kiasi. Ilikuwa kama sijamsikia yaani.

Akainamisha uso wake kama mtu aliyechoka fulani hivi na kusema, "Nakupenda... nakupenda..."

Nikaanza kutabasamu kiasi huku nikimwangalia kwa hisia sana.

Akanitazama tena usoni huku akiilegezea shingo yake upande mmoja, naye akaweka kituo kwa kusema, "Nakupenda."

Ah! Nakosa hata maneno ya kusema. Sikuwa nimeiachia mikono yake bado, lakini sasa ndiyo nikaanza kulegeza jinsi nilivyokuwa nimeikaza. Nilihisi kama vile naota yaani.

"Mimi..."

Sauti ya Bi Jamila akiita hivyo ikatufanya tuangalie mlangoni kwa pamoja, kwa sababu ilisikika karibu kabisa kuufikia mlango, nami nikamwachia Miryam upesi sana na kwenda kujifichia nyuma ya mlango hapo hapo pembeni. Niliweza kuhisi kwamba sasa Bi Jamila alikuwa amefika hapo chumbani, nami nikamwangalia Miryam pale pale alipokuwa amesimama na kuona anatazama mlangoni kwa njia ya kujikaza.

Akiwa sehemu ya ndani mlangoni, Bi Jamila akasema, "Mimi, vipi? Mbona nakuita huitiki?"

Kwa kubabaika kiasi, Miryam akasema, "Nili-nilikuwa... naongea na simu... ndiyo nimekata tu sasa hivi, nilikuwa... nakuja..."

"Ee, wahi, Shadya anasema mtachelewa ikipita saa moja na nusu hamjaondoka. Alikuwa anataka mpige na picha kabla hamjaenda..." Bi Jamila akasema hivyo.

"Sawa, nakuja. Navaa tu hereni na... bangili. Nakuja," Miryam akamwambia.

"Haya mama," Bi Jamila akasema hivyo, na ikaonekana alitaka kuondoka.

Nikashusha pumzi kiasi, na ile nataka tu kutoka hapo...

"Halafu Miryam..."

Hee! Sauti ya Bi Jamila akisema hivyo ikanifanya nitulie tena.

Miryam akaitika, "Bee..."

"Umependeza sana. Hii inaweza ikawa hafla nzuri ya Doris, lakini nikikuona hivi... najua ya kwako itakuwa nzuri hata zaidi. Unafaa, na unastahili kabisa kuipata furaha yako. Namwomba sana Mungu akubariki ufanikiwe mama," Bi Jamila akamwambia hivyo.

Maneno yake yaligusa sana hisia zangu, nami nikamtazama Miryam kwa upendo mwingi sana.

Miryam akatabasamu kiasi na kumwambia, "Asante mama. Mungu atajibu tu."

"Amen. Haya... wahi sasa," Bi Jamila akasema hivyo, kisha akaondoka zake.

Miryam akatoka hapo alipokuwa amesimama na kuja mlangoni, naye akaushika mlango na kuufunga kabisa, kisha akaegemia hapo na kufumba macho. Najua tu angeanza misolopa yake huyu. Mimi nikasogea mpaka usawa wa ile ile sehemu tuliyokuwa tumesimama kabla Bi Jamila hajaja, nikimwangalia kwa utulivu tu.

Akafumbua macho yake na kusema, "Unaona lakini jinsi mambo yako yanavyoweza kuleta shida?"

"Naelewa. Samahani. Acha niende, tutaonana baa..."

"Subiri..."

Miryam akanizuia kwa kuninyooshea kiganja nilipokuwa nimeanza kuelekea hapo mlangoni ili nitoke. Nikatulia na kuendelea kumwangalia usoni kwa utulivu. Yeye akatulia kidogo, kisha akanisogelea na kuniangaliaaa, halafu akainamisha uso wake na kufumba macho kama mtu aliyechoka, ama kuvunjika sana moyo. Nikawa nikimtazama kwa hisia sana.

Akanitazama tena usoni, na kwa sauti ya chini akauliza, "Umefurahi sasa?"

Nikatabasamu na kusema, "Sana."

"Je kama mama mkubwa angetuona?" akaniuliza.

"Haikuwa wakati wake, ndiyo maana hakutuona," nikamwambia hivyo.

Akatabasamu kiasi na kupiga ulimi kidogo mdomoni mwake, naye akasema, "Sijui umetumia dawa gani kuniroga we' kaka..."

Nikawa namwangalia huku nikitabasamu.

"Sawa. Ninakiri leo. Ndiyo nakupenda..." akasema hivyo.

Wee! Mimi hapo bichwa hilo!

Akasema, "Na ndiyo kitu ambacho nilikuwa nimehofia tokea mwanzo... kwa sababu nilijizuia, lakini sasa hivi nimeshakupenda. Haya, unafikiri nini kitafuata baada ya hapo?"

Nikatabasamu na kumwambia, "Kuna nini kingine kwani? Ndoa."

Akatabasamu kiasi na kufumba macho, huku akitikisa kichwa taratibu kama kusema 'dah!' Kisha akaniangalia na kuniambia, "Unajua kuna vitu vingine siyo vya kufanyia masihara. Umeshajaribu kupiga hesabu? Ninakuzidi... miaka tisa!"

"Hapana, ni saba tu na nu..."

"Haijalishi!" akanikatisha.

Nikatulia.

"Mimi sitakuwa mzuri sana kama unavyoniona kwa sasa ukishanichezea mpaka ukachoka, ni ndani ya muda mfupi tu utaniona kuwa mzee na kuwageukia wanaoendana na umri wako. Mbali na hilo... hata tu familia zetu haziwezi kuafikiana na hili. Familia yangu... familia yako... jamii... kwa nini tutafute misongo zaidi na kuishi kwa kunyooshewa vidole... eh?" akasema hivyo.

"Lakini Mir...."

"Hapana, nisikilize. Standard za maisha ya watu wengine hazi-apply kwenye ya kwangu, na hata mimi pia nimeshapita kwenye mahusiano kujua vizuri jinsi mambo yanavyokuwa. Usifikiri ilikuwa rahisi kwangu kukaa huo muda wote bila kujiingiza kwenye mahusiano, hata mimi nina hisia pia. Lakini wakati huu sitaki ziwe za kuchezea tu na kutupa kama mabinti wadogo na wanawake wengi wanavyofanyiwa siku hizi, ninataka nikiwa na mtu, hisia zangu zitulie hapo, na sisi kwa pamoja tutulie. Mimi na wewe, Jayden... hata tuwe tumependana vipi... kutulia kabisa haitakuwa jambo rahisi kwa sababu vikwazo vitakuwa vingi. Trust me..." akaongea kwa hisia sana.

Nikashusha macho tu nikiwa nimekosa la kusema, na nikimwelewa vizuri sana.

Akasema, "Nilikuwa nakosa amani kwa sababu nilikuwa naogopa, ndiyo. Nilikuwa naogopa. Nilikuwa naogopa kujikuta nakupenda sana halafu mwisho wa siku nije kubaki na maumivu. Uliyoniambia muda ule kuhusu maumivu, ni kweli. Ninajua kwa njia moja ama nyingine maumivu yatakuja tu, na kiukweli... mimi nimeshapitia na kupewa share yangu ya maumivu kipindi cha nyuma, sitaki na wakati huu nijitafutie mengine tena. Na wewe... mimi kuwa nawe... nayaona yakija kama wimbi kubwa la tsunami, Jayden..."

Alikuwa amepitia vitu vingi vyenye kuumiza kwenye mahusiano inaonekana, na kwa mwanamke wa aina yake ilishangaza kiasi, yaani kweli kuna bwege angetaka kumuumiza huyu kiumbe? Lakini nikataka kumhakikishia kwamba kwangu haingekuwa hivyo. Ila katika kutaka kuongea, nikawa nashindwa nimwambie nini, nikinyanyua tu viganja kiasi na kuachama mdomo kama nataka kuongea lakini maneno yasitoke, naye akaninyooshea kiganja chake kwa chini kama kunizuia nisiseme lolote.

Akaniambia, "Wewe ni kijana mzuri. Ni ndoto ya mwanamke yeyote. Lakini kwa upande wako, mimi... siyo ndoto inayokufaa wewe. Ni sawa umenigusa, nimekupenda, lakini itapaswa tu kuishia hapo. Familia yetu ina viwango tofauti kabisa na jinsi watu wengi huishi, na mimi binafsi sioni kama kutakuwa na uwezekano wa kuishi... pamoja na wewe... kama mwanaume wangu. Ninaweza nikaitia aibu familia yangu, nikaonekana exploiter wa hali ya juu baada ya hayo mambo yote yaliyotokea tangu umekuja hapa... naomba uelewe Jayden..."

Nikamtazama usoni kwa huzuni.

Akalegeza shingo yake kiasi na kusema kwa hisia, "Please nielewe..."

Dah!

Nikainamisha uso tu nikiwa najihisi vibaya mno moyoni, naye akanipita na kwenda kuvaa hereni na virembeshaji vingine. Nikabaki hapo nikimtazama kwa sekunde chache, kisha nikajiondokea tu kabla ya yeye kugeuka. Nilidhani kwamba pindi hiyo ingekuwa ya nderemo na vifijo vya hali ya juu sana, lakini nikaondoka chumbani humo nikiwa nahisi kama vile moyo wangu unapiga midundo ya parapanda.

Yaani Miryam alikuwa ame... amesamaraizi... yaani ameweka vitu vingi sehemu moja na kuvielezea kwa hayo maneno yake machache yaliyotosha kunipa huzuni kubwa sana moyoni. Sikutarajia ushindi wangu ungegeuka kuwa potezo zito namna hiyo, yaani hapo sikuona wala kujua ni namna gani nyingine ningeweza kumfanya Miryam anikubali. Kunipenda alinipenda, ila ndiyo hakutaka mahusiano. Sijui alikuwa amepitia nini, na haikujalisha, kilichokuwepo tu ni kwamba hakutaka kujiingiza kwenye mahusiano. Ilikuwa imeisha hiyo.

Bwana, kinyonge tu nikatokezea hapo sebuleni na kumkuta Bi Jamila na Bi Zawadi, ambao hawakujua kama nilikuwa ndani mpaka sasa, nami nikawaambia tu nilikuwa chooni. Yaani nilikuwa chooni kumwaga hisia zangu zilizoonekana kuwa upuuzi tu. Simaanishi Miryam alikuwa choo, natania tu!

Ila nikaelekea nje tu na kuwakuta wengine wakiwa wanaendelea kumsubiria Miryam, na hata nilipoombwa na Tesha nijiunge nao hapo kwa hili na lile, mzee nikasema tu kuna kitu nafata kwanza kule ndani kwetu, kisha nikawaacha wote na kwenda kujifungia chumbani kwangu. Nikakaa tu kitandani nikitafakari mambo mengi sana juu ya huyu mwanamke. Ningefanya nini sasa kutokea hapa? Ah, Miryam!







★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★


Pata Full Story WhatsApp au inbox

Whatsapp +255 678 017 280

Karibuni sana
 
JC usivunjike moyo MIMI ni wako tu wala ilo halina mjadala ni swala la muda tu.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…