Simulizi: Mimi na Mimi

Dah
We Mimi 🌝
Sema utulivu wa Festo ni moto 🔥
Jamaa ana akili sana, Huwa hatumii hisia kwenye haya mambo
 
Elton Tonny, mwendelezo Mkuu, ikikupendeza wikiendi hii iende poa
 
MIMI NA MIMI 3

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA KUMI

★★★★★★★★★★★★★



Baada ya kuwa tumeondoka club, niliamua tu kumrudisha Adelina nyumbani kwake kutokana na muda kuwa umeenda sana na hamu ya kufanya mambo mengine zaidi ikiwa imevurugwa. Adelina alikuwa mwelewa, na akanisihi niendelee kuendesha kwa mwendo wa taratibu sana kwa kuwa nguvu ya pombe ilikuwa nyingi kichwani, na Simba ndiyo alikuwa kabisaa. Nilijihisi vibaya kiasi kumwacha mwanamke huyo na taswira mbaya kutokana na kilichotokea huko tulikotoka kumhusisha Miryam, lakini sikugusia lolote na kufanya ionekane ni jambo lililosahaulika. Nikamwambia kesho ningemtafuta kama kawaida na kuangalia kama ratiba zingeruhusu kukutana tena, naye akaridhia na kunitakia usiku mwema.

Mwendo wa kurejea kwangu ungekuwa na umbali mrefu, kwa hiyo kuendesha taratibu mno haikuonekana kuwa sahihi kwa maeneo ya barabara ambayo hayakupita magari mengi. Umakini nilikuwa nao hata kama pombe ilikuwepo kichwani, lakini hasa ni kwa sababu bado akili ilikuwa imekazia fikira jambo lililotokea club. Miryam, alinifata yeye mwenyewe, machozi yakimtoka, akanishika na kuniomba msamaha, akiniita "mpenzi wangu" wakati ambao mpenzi wake wa kipindi hiki alikuwa pale pale pia. Sikuelewa vizuri. Hisia zake za majuto kuachana na mimi zilimlemea kiasi kwamba akashindwa kujizuia kufanya kile kitendo mbele ya Festo?

Niliwaza, ikiwa ingekuwa ni hivyo, hiyo ingemtia Festo hasira, kwa sababu angeona kwamba moyo wa Miryam bado ulikuwa kwangu licha ya yeye kujaribu sana kujiondoa maishani mwangu majuzi hapo. Sasa kufikria ni gani itikio la huyo jamaa kwa kitendo hicho ndiyo jambo lililofanya niwaze, nikijua alikuwa mtu wa aina gani kihalisi, huenda angechukua maamuzi mabaya kwa kuhisi kuwa Miryam alimchezea. Pamoja na yote yaliyotokea, bado nilijali usalama wa Miryam, na bado sikumwamini kabisa Festo. Moyo wangu uliniambia kwa njia moja ama nyingine mwanaume huyo angekuja kufanya jambo baya kama si kwangu, basi kwa Miryam na familia yake. Hayo yote ya yeye kuwa mwema kipindi hiki yalisikika kuwa upuuzi tu kwangu. Lakini ningefanya nini? Niwe sahihi au la, ningefanya nini juu ya hili suala la Miryam? Kwa nini bado alinivuta sana?

Ukimya uliokuwepo ndani ya gari ukavunjwa baada ya Simba kunisemesha kwa sauti ya chini, tukiwa bado mwendoni. "Kaka..."

Nikajitahidi kumwangalia na kuona kuwa alinitazama kwa hisia makini, akiwa siti ya pembeni, nami nikatazama mbele na kuitika kwa kuguna.

"Huna mpango wa kuniambia yule alikuwa nani?" Simba akauliza.

Nikabaki kimya tu nikiendelea kuendesha.

"Okay. Ile mode ya Aisha naona imerudi tena. Isipokuwa sa'hivi tutaiita Miryam mode," akasema hivyo.

Nikatikisa kichwa kwa kukerwa.

"Sijui una nini tu na wanawake waliokuzidi umri, boy. Ukiondoa Stella. Ila sikulaumu. Huyo Miryam ni pisi la aina yake! Mtoto alikuwa anakulilia kabisa mpaka nikasema eeh... kumbe dawa imemwingia! Hahah... alikuwa anadengua nini? Kuna wakati wanawake...."

Maneno ya Simba yakazidi kunichanganya, nami nikakosa utulivu na kusababisha mikono itetemeke, jambo lililofanya gari liweweseke baada ya usukani kutikisika.

"Hey, oya! Vipi?"

Simba akashtuka namna hiyo, maana tulikosa-kosa kuingia mtaroni aisee, nami nikajisawazisha na kujitahidi kulituliza gari pembeni ya barabara. Nikainamishia kichwa kwenye usukani nikiwa nimeishiwa pozi yaani.

"Mambo gani hayo mwanangu, unataka kutuua?" Simba akauliza hivyo.

Nikiwa bado nimeinama, nikasema, "Sorry."

"Ah, sore kitu gani bana? Tungekufa bwege wewe! Hayo mapenzi yasiku...."

"Simba, naomba utulie, yaani nakuomba usiseme jambo lingine kutoka kwenye huo mdomo wako nisije hata nikakutukana kaka! Umenisikia?" nikaongea kwa ukali na kumwangalia.

"Unitukane? Kisa nakwambia ukweli?"

"Ukweli gani? Ukweli unajua wewe?"

"Usinipandishie bangi JC..."

"Asa' unafikiri me unanikuna wapi labda?!"

"Acha ujinga JC!"

"Mjinga mwenyewe!"

"Kama ulikuwa huwezi kuendesha si ungesema..."

"Ningesema nini, we' unaweza kuendesha hapo? 'Akati umekunywa viroba kama...."

"Unanipandishia jazba kisa wanawake, una wazimu?"

"Oya, kama vipi shuka, sitaki unitibue sa'hivi..." nikamwambia.

"Ooh, okay," Simba akasema hivyo.

Rafiki yangu akafungua mlango wa gari na kushuka, akiwa hata hajui tuko wapi, naye akaanza kuelekea mbele huko akiniacha namtazama kwa umakini. Hisia zilikuwa zimevurugika mno, na kwa sekunde chache nikimwangalia hivyo nikatambua niliruhusu hasira yangu iniongoze vibaya.

Nikashuka pia, na baada ya kutembea kumwelekea, nikasema, "Oya, Simba... tulia basi..."

Simba akasimama na kuniangalia.

Nikamkaribia, nami nikasema, "Oya, swagger gani sasa hizi tunaanza kuleteana?"

"Si umeniambia nishuke, nimeshuka..."

"Tusiwe kama watoto wadogo, hizi... ni tension tu bro, and... I'm sorry... yaani..." nikakosa hata namna ya kuendelea.

Simba, akiwa anaangalia upande mwingine, akatikisa kichwa kuonyesha amekwazika na kusema, "Mambo gani haya sijui..."

"Oya, twende turudi kwenye gari. Kuna mambo muhimu kesho, twende tuwahi..." nikamwambia hivyo.

Nilianza tu kutangulia kulifuata gari, naye Simba akafuata tu hivyo hivyo nasi sote kuingia tena.

Tukiwa tumekaa sasa, Simba akatikisa kichwa tena na kusema, "Miryam mode ni kali kuliko nilivyofikiria."

Nikalaza kichwa kwenye siti huku nikifumba macho na kusema, "Ni kali mno. Sijui na me tu nakuwaje. Afanye hiki, ama kile... bado tu nitavurugwa, nitahangaika, nitayeyuka yaani... dah!"

Simba akasema, "Wanawake ni matatizo tu bro. Toka walipompa mzee wetu tunda, hawatakagi kutuacha salama."

"Okay, labda tusiende mbali sana, siyo wote wako kama mama yao," nikamwambia.

Akaniangalia usoni, mimi pia nikiwa namtazama, naye akasema, "Kwa hiyo Miryam anataka mrudiane, si ndiyo?"

Nikatazama tu mbele kumwonyesha sina uhakika.

"Utafanya nini kuhusu Adelina?" akaniuliza.

"Si... sijui Simba. Miryam amenichanganya. Yuko na mtu wake hapo club, nimemwona naye, wako wote, halafu ananifata kuanza kuniambia hivyo..."

"Yule jamaa tall aliyekuwa amesimama kwa pale juu..."

"Eeh. Anaitwa Festo. Ndiyo kalisema katampenda huyo, na sa'hivi naona wanapeta, sa' sa'hivi sijui anatak...."

"JC nisikilize," akanikatisha.

Nikamwangalia kwa umakini.

"Achana na hizo habari. Tulia upande mmoja. Unanielewa?" akasema.

Nikabaki nikimtazama usoni tu.

"Amua unapotaka kubaki, baki hapo hapo. Naongea kilevi, lakini naelewa nachosema. Ushanisoma? Masuala ya kuanza kuwaza ooh sijui nini.. a-ah! Unajiumiza kichwa ili iweje? Wewe fuata moyo wako, sijui kama ni bandama yako ndiyo inapenda, wewe ifuate... simama sehemu moja, utulize kichwa. Adelina... pisi! Miryam... matatizo! Full stop," akaniambia hivyo.

Nikatazama pembeni kwa ufikirio.

"Kwa hiyo ni juu yako. Me sijui mengi, lakini nakushauri kama mwana. Chagua pisi, iliyotulia, safi. Chagua matatizo, uendelee kuonja maafa, good. Ni juu yako, lakini simama sehemu moja. Umenipata?" Simba akaongea kwa mkazo.

Nikatikisa kichwa kukubali kinyonge tu.

"Endesha gari," Simba akasema hivyo na kujiegamiza kwenye siti.

Hakutaka mjadala zaidi, kwa upande wake hapo alimaliza. Kilichokuwa kimebaki ikawa mimi kufanya kweli kile ambacho moyo wangu ungenituma kufanya, na matokeo yake ningetakiwa kuyakubali na kusonga nayo hivyo hivyo. Ni mengi sana yalihusika. Nikageuza gari tu tena na kulirudisha mwendoni, safari hii kuelekea kwangu bado ikiendelea kukijaza kichwa changu na mawazo mengi sana.


★★★


Siku ikakucha. Niliamshwa mapema kabisa kwa kengele ya simu, na maandalizi yakaanza ili niweze kuelekea hospitalini. Tulipofika kwangu na Simba hiyo usiiku ilikuwa ni kulala tu, hali bado ikiwa yenye utata kihisia hakukuwa na jambo lingine la kufanya kutokea pale. Lakini hata wakati huu nimemaliza kujiandaa, bado sikuweza kuacha kutafakari kisa cha jana. Ilinifanya niikose amani kiasi kwamba wakati nimeingia kwenye gari ili niondoke, nikajikuta nimetulia tu humo humo nikiendelea kuwaza na kuwaza. Niliwaza mno nifanye nini. Haingekuwa na maana tena kujaribu kuepuka mikazo ya kwenye maisha yangu maana ilikuwa na njia za kujirudisha tu hata nikifanya nini. Na Miryam ndiye aliyekuwa mkazo mkuu kwa kipindi hiki.

Nikiwa nimeona sasa kwamba kuyaepuka haingekuwa na faida, nikachukua simu yangu na kupiga huko hospitali. Nikatoa kisingizio kupatwa na dharula fulani ambayo ingefanya nichelewe kufika, nikiwa nimeongea na daktari wangu mkuu hapo, na kumwomba atafute njia ya kufidishia muda wangu siku hii ili mimi nije kufanya mara mbili ya kazi nitakazokosa kufanya kwa leo. Hakuwa na neno, lakini akaniambia nisichelewe mno kufika maana alikuwa akiniachia sana kutumia muda mwingi nje ya hospitali, nami nikamshukuru na kuagana naye. Baada ya hapo, nikatafuta namba ya mtu fulani kwenye simu yangu na kumpigia. Alipopokea, nikaongea naye kwa ufupi kumwambia tukutane mahali fulani asubuhi hii hii ili tuweze kuzungumza juu ya ishu muhimu sana, naye akakubali. Simu ikakatwa, mwendo wa gari ukaanza.

★★

Nilifika eneo hilo nililompangia mtu huyo kukutana kwenye mida ya saa moja tu, hii hii asubuhi, nami nikaegesha gari. Ilikuwa ni kwenye jengo moja la biashara lenye ghorofa kama tano hivi maeneo ya Kariakoo Fire, na nilimwelekeza kuwa akija akutane nami huko juu kabisa ya jengo. Kwa misingi hiyo mimi tayari nikawa nimejipeleka huko juu na kusimama tu kwenye hilo dari (terrace) la ghorofa, ambapo kulikuwa na wamasai kama wawili hivi waliohusika na ulinzi nadhani. Nikawaambia nilikuja tu kuonana na mtu, aliyekuwa njiani kuja, na hata niikawapatia pesa kidogo ili kuniruhusu nikae tu hapo maana walionekana kunihukumu fulani hivi. Ah, ya soda haikuwa mbaya, nilitengeneza mazingira rafiki tu. Kwa hiyo wakaanza kuondoka kwa kusema wangeenda kuangalia mambo fulani ya kwenye jengo, nami nikawakubalia na kubaki nikingojea.

Nikiwa kwa hapo juu ningeweza kuyaona majengo mbalimbali kuzungukia eneo hilo, watu, na vyombo vya usafiri vikizunguka huko na huko. Fikira zangu zikitekwa zaidi na jambo lililonileta hapa, nilikuwa nimesimama kwa subira tu nikiendelea kutazama mbele, na hatimaye, ikiwa imeingia mida ya saa mbili sasa, nilichokingoja kikafika. Kusikika kwa hatua zilizokuja upande wangu kukanifanya nigeuke, na kwa hakika ilikuwa ni mtu niliyemtarajia, bibie Miryam mwenyewe.

Ndiyo, muda ule niliamua kuchukua simu na kumpigia, maongezi yakiwa ni mafupi tu kugusia mahali pa kukutana ili tuje kuyarefusha zaidi ana kwa ana. Mwanamke alivalia T-shirt nyeupe yenye kubana, suruali ya kitambaa ya blue iliyochora umbo lake zuri vyema, na alivaa miwani pana myeusi ya urembo kwa ajili ya kukinga macho jua. Hata kabla hajanifikia karibu zaidi tayari harufu yake tamu ikazitekenya pua zangu kwa makusudi ya kuamsha hisia, nami nikajikuta nashindwa kuzizuia na kuendelea kumwangalia kwa uvutio wa wazi. Athari aliyokuwa nayo kwangu bado ilikuwa nzito sana, lakini nikajitahidi kuondoa fikira zangu kwenye urembo wake na kuangalia pembeni tu.

Miryam akafika mpaka mbele yangu na kusimama, naye akaitoa miwani yake machoni. Sikumwangalia, lakini najua alikuwa akinitazama kwa hisia sana, na alingoja niseme kitu fulani labda kumkaribisha. Nikajitia ugumu tu kwa kuendelea kuangalia upande mwingine huko, naye akasafisha koo kidogo na kutazama nilikokuwa natazama pia.

"Samahani kama nimechelewa sana Jayden," akasema hivyo.

"Haina shida. La muhimu umefika," nikamwambia hivyo bila kumtazama.

Akaniangalia usoni.

"Siyo mimi ndiyo nitakuchelewesha kazini?" nikamuuliza hivyo.

"Hapana. Leo sitaingia," akaniambia.

Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa, kisha nikashusha pumzi kiasi na kumwangalia. Alikuwa ananitazama kwa njia fulani yenye imani sana, nami nikasema, "Ile jana pale... tulipoonana... ulipotaka tuongee, nili...."

"Haina shida, Jayden. Usiwaze," akanikatisha.

Nikaangalia pembeni na kusema, "Usifikirie vingine. Sikutaka kuomba samahani, nilitaka kusema hisia zilipaa tu ndiyo maana sikuweza kukusikiliza."

Miryam akatikisa kichwa kuonyesha uelewa, naye akaangalia chini.

"Kwa hiyo sa' hivi niko poa, unaweza kuongea," nikamwambia.

Akanitazama usoni kwa njia yenye hisia sana.

"Niambie, ikiwa kuna jambo la muhimu kweli. Najua una mambo mengi, na... si vyema tucheleweshane. Mm?" nikaongea kwa njia ya kutojali.

"Jayden, naomba unisamehe..." akaniambia hivyo.

"Oh, Miryam kama una...."

Akanishika kiganjani na kusema, "Tafadhali Jayden."

Nikatulia kidogo, nami nikamwambia, "Tuko past kuombana samahani Miryam. Haijalishi tena kwangu."

"Jayden..."

"Ulimaanisha kila kitu ulichosema, siyo? Ulikuwa unajua kabisa yale uliyokuwa unayaongea, shida ni nini sasa hivi?"

"Jayden please... nisikilize..."

Akaongea kwa kubembeleza na kunishika mikononi huku akisogea karibu zaidi na uso wangu. Nikabaki nikimtazama kwa njia ya kawaida.

"Nilikosea Jayden. I know, I know nimekuumiza kwa niliyosema siku ile, ndiyo maana nakuomba unisamehe. Ninakupenda sana, naku-miss mno mpenzi wangu..." akaongea kwa hisia hadi machozi kumlenga.

Nikatazama pembeni tu kwa kuudhika.

"Please. Nakuhitaji sana Jayden, now more than ever... sijui nitafanyaje kuhusu hili bila ya wewe," akaniambia hivyo.

Nikamwangalia machoni.

Akashusha pumzi kujikaza, kisha akaniambia, "Nina ujauzito."

Kauli yake ilisikika vyema sana kwangu, nami nikakaza hisia na kumtazama kama vile sijashangazwa nayo.

Akaniambia, "Jayden, acha kufanya hivyo. Siyo fresh."

Kweli, ikanibidi tu niondoe ukaidi huu wa kipuuzi, nami nikamuuliza, "Unasema kweli?"

Akatikisa kichwa mara moja kukubali. Hisia fulani nzuri ikaanza kujijenga ndani yangu, nikimtazama tumboni kwa hisia za furaha zaidi sasa, naye akawa anabana tabasamu lake la hisia. Lakini hapo ndipo lile wazo la jambo lililokuwa limetupata likanijia akilini, nami nikatazama pembeni kwa kutatizika kiasi.

"Jayden..." Miryam akaniita.

Nikaendelea tu kuangalia pembeni.

Akanishika mkono na kunitikisa kiasi huku akisema, "Jayden, vipi? Una..."

Nikamwangalia na kusema, "Ngoja. Kuna sehemu nataka twende kwanza."

"Wapi?" akauliza.

"Twende," nikamwambia tu hivyo na kumshika kiganjani.

Pamoja na kutonielewa, Miryam hakuweka kipingamizi chochote na kunitii, akinifuata hadi tuliposhuka na kufika chini. Nikaona gari lake alipoliegesha, nami nikamwambia akaingie na kulifuata langu nitakapoelekea. Niliweka umakini wa aina fulani ambao ulimfanya Miryam aniangalie kwa njia ya kuumia kiasi, nami nikamwacha tu na kuelekea kwenye gari langu. Nilipoingia, nikamwangalia kwa huko nje na kumwona anaingia kwenye lake, nami nikageuza upesi kuondoka eneo hilo huku bibie akinifuata.

★★

Mwendo wa dakika chache tu, nami nikafanikiwa kumwongoza Miryam kufikia hospitali ya Muhimbili. Najua hakutarajia nimlete huku, na tulipofanikiwa kuegesha magari huko ndani, tukakutana na kuanza kuelekea upande wa majengo ili kwenda kufanya vipimo. Miryam hakuhitaji kuniuliza chochote, alitulia tu. Najua akili yake ingemfanya afikiri tumekuja kupima mimba yake, ndiyo maana akaniacha tu bila kuuliza chochote, lakini hilo halikuwa lengo langu.

Tumefika upande fulani wa vyumba vya vipimo vya damu, nami nikamwongoza kuingia chumba kimoja kilichoandikwa DNA testing. Hapo ndiyo Miryam alianza kunitazama kwa utambuzi zaidi, naye akasimama kwanza akinitazama kwa subira. Nikamwangalia tu pia na kumtikisia kichwa kumwambia tuingie baada ya kuwa ameelewa lengo langu sasa, naye akaingia pamoja nami.

Hakukuwa na wasubiriaji sehemu hiyo kabisa, na baada ya kuingia humo, tukamkuta daktari mmoja, mwanamke kijana aliyeitwa Rita, na kwa kuwa tulifahamiana vyema nikamsalimu vizuri, naye pia akaitikia vizuri. Nikamtambulisha kwa bibie pia, nao wakasalimiana, kisha nikamwambia Rita kwamba nilihitaji vipimo vya DNA chap.

Rita akasema, "Oh J, nilikuwa nataka kutoka..."

"Najua, lakini nakuomba tu. Vial mbili, faster tu," nikamwomba.

"Muda wa kusubiri ndo' sina. Tufanye kesho..."

"Kesho? Hapana, Rita nahitaji unisaidie sasa hivi. Bado mapema. Usijali. Nitakufidishia with something, I promise. Ni muhimu sana, maana... ni kwa ajili ya dada hapa, na mimi. Inahitajika leo leo. Please Rita," nikamwomba.

Rita akalegeza kidogo na kuingia ndani ya chumba kidogo ndani humo humo.

Miryam, akiongea kwa sauti ya chini, akasema, "Kwa hiyo unataka kusema huamini kwamba hii ni mimba yako?"

Nikamwangalia.

"Unataka tupime DNA ili uthibitishe?" akauliza.

"Hamna. Hii ni ya mimi na wewe," nikamwambia hivyo.

Miryam akaniangalia kama anatafakari maana yangu, kisha ndiyo akaonekana kunielewa sasa.

"Vipi, ulidhani ninashuku kwamba siyo yangu?" nikamuuliza.

Miryam akaniangalia kwa njia ya kukwazika kiasi.

Nikafanya kukaza tena, nami nikasema, "Lakini ngoja. Nitakuwaje na uhakika?"

"Uhakika wa nini?" akauliza.

"Kwamba ni ya kwangu?" nikamuuliza tena.

"Ni ya nani sasa?" akaniuliza kiumakini.

Nikaangalia pembeni na kutikisa kichwa tu.

Bado hali tata baina yetu ilikuwepo, na yeye alilihisi hilo, hivyo naona alikuwa akijisikia vibaya. Hapa tulikuja kupima kama mimi na yeye kweli ni ndugu, maana suala la ujauzito lingekuwa zito zaidi endapo kama hilo lingine lingekuwa kweli. Nilikuwa na wasiwasi sana, na doctor Rita alipotoka na vifaa vya kuchukua damu kwa ajili ya vipimo, tukakaa na jambo hilo kufanyiwa utaratibu, naye akatuambia tungojee kwa dakika kama thelathini kwa ajili ya majibu. Kulikuwa na kifaa kipya kilichowahisha jambo hilo tofauti na ilivyokuwa zamani; kupima DNA kungehitaji kungoja kwa siku au hata wiki, lakini sasa, dakika mpaka saa. Kwa hiyo Rita alipoweka vyombo mahala pake, akatuambia tungojee, naye akaondoka kwanza.

Mimi na Miryam tulikaa kwenye viti vya kusubiria, na hatukusemeshana chochote kile. Ningeangalia upande huu na ule bila kumtazama yeye, nami ningeona namna alivyokuwa akiniangalia kwa kutarajia hata nimsemeshe, lakini haikuwa hivyo. Kuna muda akawa anajaribu hata kugusisha kiganja chake kwangu, na mimi nikiona hilo wazi, nikawa namwachia tu. Alikuwa na hamu kubwa sana ya mimi kuirudisha ile... hamu yangu kwake, sana inaonekana. Alikuwa amenikosa. Lakini nilihitaji kutuliza hisia aisee. Tayari nilikuwa nimeanza uhusiano na Adelina, na sikatai, bado nilikuwa nina hisia kwake Miryam. Kwa hiyo nilitatizika kwa kuwaza haya yote yangeelekea wapi kutokea hapa. Nilijiuliza ikiwa yangeishia pazuri ama pabaya, ikitegemea na matokeo ya kipimo cha DNA, na yale ambayo tungeamua kufanya baada ya hapo.

Lilipita saa zima tukiwa hapo, doctor Rita akiwa hajarejea, nami nikaona nimpigie. Alipopokea akasema anakuja hivyo ningoje kidogo, nami nikatulia. Adelina alikuwa ameanza kunitumia jumbe kadhaa kwa simu, lakini sikujibu yoyote na kuendelea kutulia tu. Hatimaye Miryam akawa amefanikiwa kugusisha kidole chake kwenye changu, akianza kukikaza taratibu, nami nikamtazama usoni. Aliniangalia pia, kwa hisia sana, nami nikajihisi kuyeyuka sana moyoni kumtazama namna hiyo. Hakuogopa tena kunionyesha namna alivyonikosa, lakini mimi ndiyo bado nikawa najizuia. Ni wakati huo huo ndiyo Rita akawa amerejea, akiwa na daktari mwingine, nao wakaingia mule ndani na kutuacha tukingoja kwa utulivu.

Dakika chache tu kupita naye Rita akawa ametoka tena, akiwa ameshika karatasi iliyochapishwa. Tukasimama, na baada ya kunipatia karatasi hiyo, Rita akaniambia tu hongera, kana kwamba alikuwa ameshaelewa kilichokuwa kikiendelea baina yangu na Miryam, naye akarejea humo ndani akiniacha nimeweweseka kiasi moyoni. Nikamtazama Miryam usoni na kuona jinsi alivyokuwa akinitazama kwa subira, nami nikaiangalia karatasi hiyo. Nikayasoma majibu. Taratibu kushusha macho mpaka chini, nami nikaliona jibu pekee nililohitaji kulijua. Hisia zikapanda hata zaidi kutokea hapo, nami nikamwangalia Miryam mbele yangu kwa macho yaliyojaa simanzi kubwa.

"Vipi?" Miryam akaniuliza kwa kujali.

Nikampatia karatasi hiyo, naye akaiangalia kwa hisia makini, kisha uso wake ukageuka kuwa wa simanzi pia na yeye kuuziba mdomo wake kwa kiganja kuonyesha hisia kali iliyomwingia. Akaniangalia usoni tena, machozi yakiwa yameanza kumjaa machoni, nami nikamkumbatia kwa nguvu nikiwa nahisi furaha tele moyoni!

Miryam akarudisha kumbatio langu na kujibana kwangu kwa nguvu pia, akianza kulia wa sauti ya chini, naye akasema, "Jayden..."

"Dah! Miryam, yaani hizo fujo zote, kumbe sisi siyo...." nikaishia hapo tu na kucheka kidogo kwa hisia.

"Ahh... nisamehe Jayden... yote ni makosa yangu..." Miryam akasema hivyo.

Nikamwachia na kumwangalia usoni kwa hisia, nami nikasema, "Hapana. Usijlaumu."

"No, ni lazima niseme ukweli. Nilikuwa tu... hh... najifanya mgumu, najifanya najua, ona sasa hayo yote yametokea mpaka... nimekuumiza sana," Miryam akasema kwa hisia.

Nikamshika usoni kwa mikono yote.

Akavikaza viganja vyangu na kusema, "Naomba unisamehe tu. Sasa hivi nimejifunza kuwa tayari kupambana kwa ajili ya penzi letu Jayden, kwa sababu sikuzote ni wewe ndiyo umefanya hivyo kwa ajili yangu. Hili ni jambo zuri sana kwetu, hata kama vikwazo vingi havitaki tuwe pamoja, kwa sasa haipaswi kuwezekana tena kututenganisha..."

Nikatabasamu kwa furaha.

"Ninaomba turudi kuwa kama mwanzo mpenzi wangu. Na nakuahidi, zamu hii ni mimi ndiyo ambaye sitaruhusu lolote litusambaratishe tena..." akaniambia hivyo huku machozi yakimtoka.

"Hata wewe mwenyewe?" nikamuuliza hivyo.

"Hata mimi mwenyewe," akanijibu kwa hisia.

Nilipenda sana maneno yake, mtazamo wake mpya kuelekea hali yetu uliifariji sana nafsi yangu, na kutokana na burudisho jipya ambalo mwanamke huyu alikuwa ametoka kunipatia kwa alichoniambia, nikahisi maumivu yote ya kihisia kuisha ghafla. Sikuweza kujidhibiti tena, nikapitisha mikono yangu mgongoni kwake, na yeye vilevile akapitisha yake kwangu tena na sote kukumbatiana kwa upendo. Nilijihisi uafadhali wa hali ya juu, ile kukiachilia mbali kinyongo na kuirudia amani ya penzi la mwanamke huyu, kulinipa uradhi mkubwa sana. Sikujali kingine tena. Miryam alionekana kufurahi sana mpaka akashindwa kuzuia kilio chake.

"Mbona unalia sasa?" nikamuuliza huku bado akiuficha uso wake kifuani kwangu.

Akasema, "Nalia kwa furaha tu."

"Utakuwa na undugu na K-Lynn wewe," nikamtania.

"Ahah... itakuwa. Na we' ndiyo Bushoke wangu," akasema hivyo.

Nikatabasamu na kumwachia taratibu, huku miili yetu bado ikiwa kwa ukaribu, lakini Miryam akanivuta na kuning'ang'ania zaidi ndani ya kumbatio lake. Nikatabasamu zaidi na kumkumbatia tena.

"Usiniachie Jayden. Naomba usije kuniachia tena tafadhali," akaongea kwa kasauti kake ka mideko.

Nikawa nambembeleza kwa kiganja taratibu, nami nikasema, "Usijali Mimi. Zamu hii sitakuacha kamwe, hata nikihitaji kusimama dhidi yako mwenyewe."

Akatoa mguno ulioonyesha hali ya mridhiko.

"Dah, mahusiano yetu haya ni sinema!" Nikasema hivyo.

Akacheka kidogo na kusema, "Na ma-starring ndiyo sisi."

"Ahahah... kabisa," nikamwambia.

Kisha nikamwachia tena taratibu na kumshika usoni kwa wororo, nikimpangusa chozi lake la furaha pia, na yeye akawa amenishika kiunoni huku akiniangalia kwa hisia.

"Sahau bullshit yote iliyotokea hapo kati, Mimi. Kutokea hapa tunasonga mbele, na tunasonga mbele strong," nikamwambia huku nikiitomasa shingo yake taratibu.

Akatikisa kichwa kukubaliana na hilo.

"Lakini kwanza... kuna mambo nahitaji kurekebisha," nikamwambia.

"Mambo yapi?" akaniuliza kwa kujali.

Nikashusha pumzi kujipa utulivu, hapo nikijua uhitaji wa kuanza kumwelezea kuhusiana na Adelina ulikuwa wa lazima.






★★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★★


Whatsapp +255 678 017 280
 
Dah
Nampenda sana Mimi ila kumfanya Adelina alie ni jambo linalohuzunisna kiasi chake
Ila ngoja kwanza..we JC, mbona hujamuuliza kuhusu Festo? Una uhakika mahusiano yalikuwa hayaanza? Mwamba atakuacha salama kweli? 😂
 
Daah… afadhali nilikuwa siupendi uhusiano na Adelina basi tu, yaani kwenye sehemu za Adelina nilikuwa nasoma huku nimenuna
 
Daaaah Leo nimerudia kusoma sehemu ya 1 sio Kwa kucheka huku [emoji23][emoji23][emoji23]
 
Kwann lakini 😂
Mtoto na shape lake kabsa
Ila JC buana, kwahyo kapiga mtu na dada ake
Eti jamani😃😃 halafu hamkatai mtu, alijitahidi kwa Mariam tu na yeye ilibaki kidogo amkule angekoma angekua kala mdogo ake sijui angemuangaliaje baada ya kujua wameshare baba
 
MIMI NA MIMI 3

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA KUMI NA MOJA

★★★★★★★★★★★★★★★★★



Nilihitaji muda zaidi kumeza haya yote yaliyokuwa yametokea leo, na niliona kazi hazingefanyika kwa utimilifu wote hata kidogo. Nikiwa na Miryam hospitalini bado, nikaamua kwenda kuongea na daktari wetu mkuu kumwambia kwamba nilikuwa nimefika mimi mwenyewe hapo kumpa taarifa kwamba nisingeweza kuwepo kazini leo, kwa sababu ya safari ya dharura iliyonihitaji kuondoka jijini haraka sana. Yaani ilinibidi nidanganye tu, na utaratibu mwingine wa kufidishia muda ambao nisingekuwepo ungetakiwa uwekwe.

Nilionwa kuwa muhimu kwenye kitengo changu na masuala mengine, lakini siyo kwamba nilikuwa daktari pekee hapo. Walikuwepo wengine pia, na mimi kusema kweli nilihitaji sana kuielekeza akili yangu kwa Miryam angalau kwa muda fulani kwanza, kisha kazi zingeendelea. Mkubwa wangu akasema hiyo ingeweza kuniletea shida hata kwenye masuala ya malipo na nini, lakini nikamwambia haikuwa na tatizo kabisa; yaani hapo ndiyo nilikuwa napita tu kumtaarifu hilo, na moja kwa moja ningeelekea stendi kupanda basi. Mh?

Hakuwa na namna ila kukubaliana nami, nikiwa nimemwambia ni tatizo tu la kifamilia nje ya jiji lililonihitaji kwa uharaka, na kwa misingi hiyo akawa amenipatia kibali cha kuondoka. Ilikuwa kama shule yaani. Kwa hiyo nilipomaliza hilo, nikamrudia Miryam wangu, ndiyo, "wangu," nami nikaondoka pamoja naye tukiwa na furaha isiyopimika ukubwa yaani. Nilihitaji kutumia muda pamoja naye, na mpango ukawa kwenda kule kwangu ili tutulie kwanza na kuzungumzia mengi yaliyotokea na yaliyohitajika kufanywa kutokea hapo. Nikamwongoza kwa gari langu, naye akanifuata kwa lake.

★★

Tulifika kwangu ikiwa ni mida ya saa tano sasa, hii hii asubuhi, na sikumkuta Simba hapo maskani. Inaonekana alitoka, na hiyo kwangu ikawa ni jambo zuri kwa kuwa ningehitaji kuwa na muda wa kibinafsi zaidi na Miryam. Tulipoingia ndani, Miryam akasema kitu kama 'pamebadilika, umeongeza nini?' lakini mimi sikujali maneno yake na kumshika mkononi, kisha nikamgeuzia kwangu na kumkumbatia kwa nguvu kiasi. Nilimkumbatia kwa njia ya kushtukiza kwa hiyo hakurudisha kumbatio langu haraka, naye ndiyo akacheka kidogo kwa pumzi na kunikumbatia pia.

Nilihisi kuridhika, hisia ya mwanzo tu maana ni kama vile yale yote mabaya yaliyotokea baina yetu yalifutika ndani ya sekunde moja tu, na matazamio yakawa mengi kutokea hapo. Nilipitisha kama dakika mbili nzima nikiendelea kumshikilia namna hiyo hiyo, nikimbembeleza taratibu kwa kuyumbisha miili yetu, na yeye akinibana kwake hata zaidi kufurahia upendo wangu. Haukuwahi kutoweka. Hilo nililijua. Na kama maneno ya Simba jana, ikiwa Miryam alikuwa ni matatizo tu kwangu, basi niliamua kuyachagua matatizo haya kwa moyo mkunjufu. Sikujali kingine tena. Suala la sisi kuwa ndugu lilifutika, na sasa ingekuwa ni kurudisha kile tulichodhani kilipotea jumla baina yetu.

Miryam akaguna kidogo na kusema, "I missed you so much..."

Nikamwambia, "Me hata kidogo."

"Mhmhmhm... huna lolote..."

"Dah! Naweza kukushikilia hivi hivi mpaka usiku uingie," nikasema hivyo.

"Ningependa sana. Sema mwenzio nawahi kuchoka kweli sa'hivi," akaniambia.

Nikamwachia taratibu na kumwangalia usoni, miili yetu bado ikiwa imegandana, nami nikamwambia, "Bado hata mwezi haujaisha, tayari ushaanza mideko? Eti 'nachoka sana sa'hivi...'"

Miryam akatabasamu na kukilaza kichwa chake kifuani kwangu.

"Ahah... mahusiano yetu yanahitaji check-up, siyo kwa hivi visa na mikasa aisee," nikamwambia.

Akaniangalia usoni tena na kusema, "Na me ndiyo nimechangia sana kufanya iwe hivyo. I'm sorry."

Nikazilaza-laza nywele zake na kumwambia, "Usijali. Na... me pia niombe samahani. Nilikutia pressure sana."

Miryam akatikisa kichwa kukubali samahani yangu.

"Nitakuwa nimepitwa na mengi kwa hizo siku eh?" nikamuuliza hivyo.

Akatikisa kichwa kukanusha na kusema, "Hamna. Labda wewe ahah..."

"Ahahah... yeah. Vingi vimetokea," nikamwambia.

"Nisimulie basi," akasema hivyo kwa sauti ya chini.

"Sawa."

Nikaonyesha nia ya kumtaka akae ili tuongee vizuri, naye akalisogelea sofa na kuketi hapo, mimi nikikaa karibu naye pia.

"Kuna mambo mengi yaani... nakosa kujua hata nianze na lipi," nikamwambia hivyo.

"Niambie chochote mpenzi wangu. Niko tayari kukusikiliza," Miryam akasema hivyo kwa hisia.

Nikatabasamu kiasi, nikiwa nimekishika kiganja chake, nami nikamwambia, "Unajua... nimeshakutana na Evelyn."

Akakunja uso kimaswali na kuuliza, "Evelyn ndiyo nani?"

Nikatabasamu na kusema, "Mwanangu."

"Ahaa... kwa Stella?"

"Ndiyo. Ulifikiri naongelea demu, ama?"

"Ahah... wala."

"Mmm?"

"Mmm. Mie siyo wa namna hiyo kabisa," akasema hivyo.

"Mhm, haya bana."

"Umekutana naye lini?" akauliza.

"Kama mwezi unaenda kuisha. Yaani... ni siku chache tu kabla sijaja pale home kwako, mpaka yale kutokea na nini..."

"Eeh..."

"Yeah, ndiyo nilimwona kwa mara ya kwanza. Tulikutana restaurant," nikamfahamisha.

"Okay. Yuko poa?" akauliza.

"Ndiyo, kapo fine sana."

"Nionyeshe picha yake basi..." Miryam akaniomba.

Nikatoa simu na kuweka picha ya Evelyn, niliyopiga siku ile tumekwenda kutembea, naye Miryam akatabasamu.

"Hee! Mnafanana!" akasema hivyo.

Nikacheka kidogo kwa pumzi.

"Ulihisije ulipokutana naye?" akauliza.

Nikaweka simu pembeni na kumwambia, "Vizuri mno. Mwanzoni nilikuwa sijui hata namna ya ku-handle hiyo hali, ila mtoto alifanya iwe rahisi sana kuzoea..."

"Alikuzoea haraka?"

"Yaani ni hiyo hiyo tu mara ya kwanza tumekutana and she was all over me! Huwezi amini, ilikuwa kama vile ananijua vizuri kuliko hata navyojijua..."

"Mm? Lakini Jayden..."

"Ahahah... siyo siri, nilipenda sana hiyo hali. Ndiyo nikagundua ni namna gani nilikosa mengi mno kwa kujiweka kando muda mrefu," nikaongea kwa hisia.

"Naona Stella alifanya kazi kubwa kumwambia mwanao kukuhusu," Miryam akasema hivyo.

Nikabaki kimya na kumwangalia kwa utulivu.

"Ni mama mzuri. Wazazi wengine walio single huwa hawajisumbui kuwaambia watoto juu ya wazazi wao, ama wanawafundisha kuwachukia," akasema hayo.

"Yeah, siku hizi Stella kapunguza ujeuri. Yuko tofauti na nilivyomwelewa zamani," nikakiri hilo.

"Kwa hiyo ni mara moja tu hiyo ndiyo ulikutana na mwanao?" akauliza.

"Hapana. Tangu hiyo siku, naweza kusema karibia mara tatu kila wiki. Yaani mara chache sana hatujaonana, hasa shauri ya kazi, ahah... anajua kulalamika huyo asiponiona!"

"Eeh... daddy yuko wapi?"

"We! Akianza timbwili kisa hajaniona mpaka mama yake anachoka, inabidi nikache kazi nimpigie video call, ama nitimue kwenda kumwona hahahah..." nikaongea kwa furaha.

"Kwake Stella?" Miryam akauliza.

"Yeah. Basi akiniona eti anaanza maringo, halafu na me nikianza maringo ananibembeleza eti nimsamehe. Ana akili fulani hivi yaani... pamoja na kwamba ni miaka mitatu kasoro lakini... sijui hata nielezeeje..."

"Ana kile kitu nilichokwambia unacho pia," Miryam akasema.

"Kitu gani?"

"Inaonekana ana sense nzuri ya direc...."

"Good sense of direction, yes! Umepatia. Hivyo hivyo yaani. Kama baba yake hapa," nikajitutumua.

Miryam akatabasamu na kusema, "Haya bwana. Napenda sana unavyofurahi. Kumpata mwanao naona imekuridhisha sana. Nitapenda kukutana naye pia."

Nikakiunganisha kiganja changu kwenye chake, nami nikamwambia, "Kumjua Evelyn kumenibadilisha sana. Yaani... nimekuwa tofauti kimtazamo, Mimi. Natamani zaidi kuwajibika kama baba, ndiyo sababu nina hamu kubwa zaidi na zaidi kwamba unamleta kijacho wetu wa kwanza."

Miryam akacheka kidogo kwa kufumba mdomo.

"Seriously yaani, I'm so happy," nikamwambia kwa hisia.

"Nafarijika kujua hilo. Asante Jayden," Miryam akasema hivyo kwa hisia.

Nikatikisa kichwa kwa uthamini pia, nami nikamwambia, "Tuongelee upande wako pia."

Miryam akasema, "Kuhusu..."

"Nilikuwa najaribu tu kufanya hali iwe na sss... wepesi kidogo ahah... ila hiki kitu bado kinazunguka sana akilini," nikamwambia hivyo.

"Kitu gani?" akauliza.

"Kuhusu ule usiku. Huwa haiko mbali na fikira zangu kila nikikumbuka namna ulivyoongea, yaani... najua mambo mengi yalichangia, ila... bado nilikuwa... nahisi kama vile haikuwa akili yako, au... kama kuna la ziada lililofanya mpaka ukaniambia haunihitaji tena, na utampenda mtu mwingine..." nikaongea kwa upole.

"Naelewa, Jayden. Najua ulishangaa, na uliumia sana mimi kukwambia vile... hata mimi ni kitu kilichoniumiza pia," Miryam akasema hivyo na kuangalia chini.

Nikaendelea kumtazama kwa hisia.

Akasema, "Niliyoyasema ule usiku yalikuja vibaya si kwa sababu tu ya mambo yaliyotupata, yaani... nilitaka tu kila kitu ambacho nilihisi kingeendelea kuniumiza, kiache... na... labda..."

"Kuniondoa mimi maishani mwako ndiyo kungekuondolea hayo maumivu?" nikamkatisha.

Akapindisha shingo kiasi huku akiniangalia kwa hisia, naye akasema, "Ndiyo. Ni.. nilifikiri hivyo."

Nikaangalia pembeni.

"Lakini haikutoka moyoni. Siyo baada ya siku, wala wiki... ni baada tu ya wewe kuondoka pale ule ule usiku nilibaki na majuto makubwa sana moyoni... lakini... nikawa sina namna ya kufanya mambo yarudi kuwa sawa tena. Hakuna kitu chochote kilichoweza kunifanya niache kukupenda. Sema..." akaishia hapo.

Nikiwa namwangalia sasa, nikamuuliza, "Ila?"

Akabaki kunitazama kwa hisia.

"Niambie. Nataka kujua," nikamsihi kwa upole.

Akaangalia chini kwa ufupi na kusema, "Nilikuwa tu nimeumia."

"Uliumizwa na nini kingine?" nikamuuliza.

Akaniangalia usoni kwa hisia.

"Ni mimi?" nikamuuliza tena.

Akaangalia pembeni.

Nikakikaza kiganja chake na kusema, "Niambie Miryam. Nilikosea wapi? Kwa sababu uko sahihi, nilijua kabisa kuna kitu kingine kilikuwa kinakusumbua, lakini... labda kilikuwa kizito kusema. Ila, sasa hivi unaweza kuniambia. Ikiwa ni jambo ambalo naweza kurekebisha...."

"Hapana, Jayden... hauhitaji kurekebisha lolote," akaniambia kwa upole.

"Basi nakuomba uniambie tu. Nilifanya nini kilichokufanya... usiache kunipenda, lakini upoteze imani?" nikamuuliza hivyo.

Akatulia kwanza, kisha akasema, "Ni Mamu."

Nikamwangalia kiumakini.

"Aliniambia kuhusu... kuhusu mlichofanya," akasema hivyo.

Nikafumba macho na kuinamisha uso.

"Na, siyo kwamba mlifanya, anasema... ilikuwa karibu mfanye siku hiyo, ila... ukamzuia, na..."

"Nilifanya makosa Miryam, nisamehe," nikamkatisha kwa kusema hivyo.

"Hapana, wala usi...."

"No, kiukweli haikuwa sahihi hata kidogo. Nili... nilishindwa tu kujua... njia rahisi ya kumsaidia Mamu aongoze hisia zake siku hiyo, na me nikajikuta nashindwa kuongoza zangu, yaani...."

Miryam akanishika usoni na kusema, "Jayden, usijali. Najua."

Nikamtazama kwa hisia.

"Mamu hakuniambia hayo kwa sababu ya hisia zake kwako, alikuwa tu ameogopa... tulipojua kuhusu haya ya undugu. Alijihisi vibaya kulazimisha mapenzi kwako wakati ungeweza kuwa kaka yake, lakini hayo siyo makosa yake, wala yako. Ni kitu ambacho hamna aliyeweza kuona," akaniambia hivyo.

Nikaendelea tu kumwangalia.

Akaniachia na kusema, "Na... mimi tu kusema kweli ilinichanganya. Nilianza kufikiria kuhusu jambo hilo mno, nikawaza kama ni kweli tuna undugu halafu ungekuwa umelala naye... ingekuwaje? Vitu kama hivyo, lakini siyo kwamba...."

"Miryam najua uliumizwa na tendo langu la kutoweza kujizuia haraka. Hata kama isingekuwa Mariam, najua ungeumia endapo ungetambua nimetoka na mwanamke mwingine wakati tukiwa na mahusiano," nikamwambia hivyo kwa upole.

Akaendelea kunitazama kwa hisia.

"Kwa hilo naomba unisamehe tu. Na sikuwa nimekwambia kuhusu Mamu kwa sababu... sikutaka tu kuchanganya mambo baina...."

"Naelewa Jayden, hilo halina shida. Kama nilivyokwambia, hauhitaji kurekebisha lolote, limeshapita. Sawa? Kuwa na amani mpenzi wangu," akaniambia hivyo kwa uhakikisho.

Nikatabasamu kiasi na kusema, "Asante."

Yeye pia akatabasamu.

Nikatazama pembeni na kushusha pumzi, kisha nikamwambia, "Hivi vitu vimesababisha mambo mengi ku-change ndani ya muda mfupi sana."

Miryam akatikisa kichwa kukubali na kusema, "Yeah. Mambo mengi."

"Nilidhani... baada ya huo usiku nikadhani kweli ulimaanisha ulichosema, kwa hiyo..." nikaishia hapo.

Nikamwangalia na kukuta ananitazama kwa njia yenye subira.

Nikashusha pumzi na kusema, "Nimeanza kutoka na Adelina, Miryam."

Miryam akaangalia chini kwa ufupi.

"Ilikuwa haraka, I know, yaani... nilipondeka sana moyoni, nikajua tayari una kitu na Festo, sasa... Adelina akawa sehemu kubwa ya comfort kwangu. Siyo kusema hisia zote kwako ziliondoka... ila..."

"Na yeye ukampenda," Miryam akasema hivyo bila kunitazama.

Nikamwambia, "Siyo kitu kilichokaza mizizi, Mimi. Nitaongea naye, nita..."

"Ni makosa yangu hata hivyo..."

"... zungumza... naam?" nikaitikia kauli yake.

Akaniangalia usoni tena na kuniambia, "Sitalaumu. Ni makosa yangu mpaka ukafikia hiyo hatua."

Nikatazama pembeni kwa kutatizika.

"Heey, usijali. Naelewa. Sema... kwa jinsi mambo yalivyo sasa hivi, sijui kama Adelina ataweza kuelewa ukimwambia..." akaishia hapo.

Nikasema, "Nitaongea naye. La muhimu ni kuongea naye. Nitarekebisha hilo."

Akatikisa kichwa kukubali.

"Ni hivyo hivyo na kwako pia I suppose," nikamwambia hivyo.

Akaniangalia kwa njia ya kutoelewa.

"Bila shaka utahitaji kuongea na Festo wako... maana sioni ya kwetu yakisonga bila upande wako kuwa clear pia," nikamwambia.

Miryam akatabasamu kiasi na kusema, "Hapana Jayden. Mimi sikuwahi kutoka na Festo."

Nikakunja uso kimaswali.

"Alirudi tu kutoka huko kwenye biashara zake, akawa amenitafuta, kirafiki tu. Hakuna chochote baina yetu zaidi ya urafiki..." akaniambia.

"Seriously?"

"Ndiyo."

"Urafiki... yaani, kuna usiku nilikuona unashuka kwenye gari lake, kabla hata hatujagombana yaani, tena ulishukia pale Mzinga barabarani, ukachukua boda, ndo' ukaenda nyumbani. Hiyo ilikuwa nini?" nikamuuliza.

"Ooh, hiyo siku... subiri, ulikuwa wapi?"

"Nilikuwa hayo hayo maeneo, hiyo siku nimekuja kukuona tuongee ndo' sikukukuta kwako," nikamwambia.

"Sawa. Yaani... ndiyo alikuwa amerudi, akanitafuta, akaomba tukutane. Alitaka tu tufurahie kinywaji, na me bado nilikuwa na stress, yaani jana yake ndiyo tumetoka kwenu eh... na yale mambo yote, kwa hiyo nikaenda tu kuwa kwenye company mpya. Basi," akanifahamisha.

"Ndiyo alikuwa ameanza kujisogeza eh? Ili arudishe romance?"

"Ahh, Jayden hakukuwahi kuwa na kitu kama romance baina yangu mimi na Festo. Amekuwa rafiki mzuri tu kwangu... ame... amenisaidia kwa vitu fulani, ushauri... hata ule usiku umemkuta pale nyumbani ni kwamba alikuja kuwasalimia tu akina mama. Hakuna kingine baina yetu, ni rafiki tu," akasisitiza.

Nikamuuliza, "Na jana?"

Miryam akanikazia macho.

"Namaanisha... mlikuwa wote club. Hiyo ni...."

"Ilikuwa kwa sababu yako," akanikatiza.

"Kwamba?"

"Nilishindwa kujizuia tena. Nilitaka kukuona, nikwambie kuhusu hali yangu, lakini sikujua namna gani ya kushika simu... nikupigie. Nilijua hata usingepokea. Lakini Festo ndiyo akanisaidia. Alinishauri ni vyema nikikutana na wewe ana kwa ana, ndiyo tuongee. Alikuwa na njia fulani aliniambia, ya kuweza kumtrack mtu ili kumpata, na akanitia moyo nikutafute kwa njia hiyo ili niku-surprise... halafu ndiyo tuongee..." akaeleza.

Nikaendelea kumwangalia kwa umakini.

"Jana... alikuja nyumbani. Akaniambia tu tutoke mara moja, na ilikuwa kama anitembeze kidogo. Tena alikuwa amesema angenionyesha kwa rafiki yake wa muhimu, lakini bila me kutarajia, akanileta mpaka pale tulipowakuta we' na wenzako. Akaniambia uko humo, na akanitia moyo twende nikuone... tuyajenge," akaeleza.

Mh? Nilishindwa kuamini. Huyo alikuwa ni Festo aliyefanya hayo yote?

"Na tena hata hapo sikuwa na uhakika ingekuwaje... bado masuala yetu, na ya ma' mkubwa na mama yako, yaani... pamoja na yote nilitaka tu kukuona pia. Niliku-miss mno, na Festo ndiyo alinipa ujasiri hadi nikaweza kukufata pale. Nilikuwa na wasiwasi mwingi," akaniambia.

Nilibaki nimetulia tu, nikiangalia pembeni kwa umakini.

"Kwa hiyo usiwaze kuhusu huyo mwanaume. Ni rafiki tu, na ukimjua vizuri, we' mwenyewe unaweza ukajenga naye...."

"Hapana, Miryam. Hapana," nikamkatisha.

Akabaki akiniangalia kwa hisia makini.

"Siyo... Festo siyo mtu unayemdhania, Mimi. Si mtu mzuri," hatimaye nikamwambia.

Alichanganywa kiasi, naye akauliza, "Kwa nini useme hivyo?"

"Festo ni mtu aliyehusika na... ah, yaani hata sijui nikwambieje..." nikasema hivyo na kutulia kidogo.

Miryam hakuacha kunitazama kwa subira.

Nikamwambia, "Unakumbuka kipindi kile nimefanya kazi na yule askari Ramadhan kuwakamata wale wauzaji wa madawa ya kulevya? Yule mwanamke, Bertha, ambaye alimuua mdogo wake Adelina..."

Miryam akatikisa kichwa kukubali.

"Sasa Festo... ndiyo alikuwa partner wake," nikamwambia.

Miryam akakaza macho kwa njia ya kushangazwa na maneno yangu.

"Tena, alikuwa kama boss wao. Yaani yeye ndiyo alitengeneza njia za wao kuyapata hayo madawa na kuyasambaza, na hata walikuwa na kundi la watu waliokaa kama... kama majambazi, walikuwa wanafanya kila aina ya unyama Mimi. Hata kuua watu," nikamfahamisha.

Miryam akaangalia pembeni, akionekana kushangaa kweli.

"Festo aliwageuka wenziye mwishoni hapo, wakati tunakaribia kuwakamata, eti akawa amefanya kama dili na maaskari kuwafichua wenziye, halafu akawa kama amelipa fidia sijui... ili yeye asiwekwe hatiani nao. Yaani, mambo yalienda faster sana, me mwenyewe nilishangaa sana alipokuja kuonekana yuko upande wa mazuri, wakati mabaya mengi aliyofanya niliyaona. Kuna siku alimpiga risasi tatu mwanaume mmoja, mbele ya macho yangu!"

Miryam akaniangalia kwa umakini.

"Na sijui yapi zaidi amefanya ili kuhakikisha yuko huru mpaka sasa. Lakini sidhani yako kwa njia nzuri. Hiyo safari yake kuondoka nadhani ilikuwa kama kukimbia kwa muda mfupi, hali itulie, na sasa hivi Bertha amepoteza maisha ni kama Festo hana tati..."

"Huyo Bertha alikufa?" akanikatiza kwa kuuliza hivyo.

"Ndiyo Mimi. Bertha alipatwa na ajali kabla hawajampeleka magereza. Festo alikuwa anadai kwamba, alitaka kubadilika, kwa sababu anakupenda... kwa hiyo aliachana na hayo yote ili aweze kuwa mtu ambaye wewe utamtaka. Miryam..."

Mwanamke akabaki kuniangalia kwa mkazo.

"Festo ni muuaji. Anaweza akasema sa'hivi ameacha, lakini kwa huo muda mfupi nilioshiriki meza pamoja naye, nimemjua. Nimemsikiliza. Nimemwelewa. Siyo mtu wa kuachia mambo kirahisi. Maaskari wanaweza wakawa labda wanamwangalia, wakaona ah sa'hivi yuko safi, lakini nia zake unakuta hazijabadilika. Na ninajua... nia yake ya kukupata wewe bado iko pale pale," nikaongea kwa njia yenye mkazo.

Miryam alionekana kuchoka. Aliishia kuniangalia tu kana kwamba bado hakuelewa chochote kati ya mambo yote niliyomwambia.

"Kwa hiyo kwa kweli... sielewi kwa wakati huu itakuwaje. Yeye kurudi namna hiyo, sidhani kama ilikuwa ghafla. Nahisi alijua kabisa kwamba me na wewe tuna mahusiano, na akajua tulipoanza kutengana. Yaani alingojea wakati mwafaka kwake ili arudi na kuingia katikati yetu, sawa? Halafu sasa ameanza kufanya mambo fulani ili kukuaminisha kwamba yuko upande wako kama rafiki. Mpaka anaangalia ninakokuwa, ili akulete kwangu, hiyo inamaanisha ana-monitor maisha yangu na yako kwa njia fulani... na lazima ziwe za gharama, na illegal. Sijui hiyo inampa faida gani, lakini nahisi anaweza kuwa anapanga kitu Miryam. Na sasa hivi tunarudiana... naanza kuona kama kuna jambo baya atalileta upande wetu," nikamweleza.

Miryam akatikisa kichwa kwa kusikitika sana, na kwa sauti ya chini akaniuliza, "Kwa nini hukuniambia haya Jayden?"

Nikafumba macho na kuinamisha uso, nami nikasema, "Mambo yalikuwa mengi sana. Sijui hata... sijui niseme sababu nini, lakini... lakini hiyo ndiyo hali halisi."

Miryam akaniangalia kwa njia yenye huzuni mno.

Nikamshika shingoni na kumwambia, "Lakini usijali, Mimi. Sitaruhusu huyu mtu atuingilie vibaya. Nitafanya kila kitu kuhakikisha penzi letu linabaki salama. Sawa?"

Miryam akaushika mkono wangu na kuniambia, "Bado sielewi. Yote uliyosema... yanaonekana kuwa impossible yaani."

"Ndiyo hivyo, najua. Lakini niamini. Festo siyo mtu wa kuweka karibu, hata asemeje kwamba amebadilika...."

"Point ya yeye kunisaidia ili nirudiane na wewe ni ipi sasa?" akanikatiza.

Nikatulia kwanza.

"Ikiwa... ana nia ya kulazimisha mapenzi kwangu, si angetumia advantage hata ya sisi kuachana kujaribu kunitongoza labda... au..." Miryam akaonekana kutatizika.

Nikabaki nikimtazama kwa hisia.

"Naogopa," akasema hivyo.

"Mimi..."

"Naogopa nisije kukupoteza Jayden..." akaniambia hivyo.

"No, usiogope. Kama nilivyokwambia, nitafanya jambo fulani kuhakikisha haji kutusumbua tena. Hasa wewe," nikamwambia hivyo.

"Yaani haonekani kabisa... ah... singefikiria angeweza kuwa mtu wa aina hiyo," Miryam akasema.

"La muhimu sasa umejua. Jitahidi tu kuweka distance, endapo kama ana mpango fulani, ni vyema uwe tayari kiakili kupingana nao. Anajaribu kuthibitisha kitu fulani naona, na labda angedhani hatutaweza kurudiana kwa sababu ya suala la undugu, ama tu jinsi nilivyokutendea jana. Lakini sasa hivi ndiyo tutapaswa kusimama imara Miryam, lolote atakalorusha upande wetu, kwa pamoja tutalishinda," nikamtia moyo namna hiyo.

Miryam akaniangalia kwa hisia sana, naye akajilaza begani kwangu kujipa ahueni kidogo.

Hapo tayari tulikuwa tumeanza kujenga kitu fulani imara baina yetu, kwa kumfungua macho Miryam juu ya hatari zingine zilizozunguka mahusiano yetu ingekuwa njia bora ya kujitahidi kuyalinda kadiri ambavyo tungesonga mbele. Na kama nilivyomwambia, ningehitajika kutafuta njia ya kumwondoa Festo kutoka maishani mwetu, mwanzo mwisho. Huyo kwetu najua angekuwa kama kupe asiyetaka kung'oka, na mimi ndiyo ningekuwa dawa yake kuhakikisha anatutoka milele.







★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★


Whatsapp +255 678 017 280
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…