Darkhorse001
JF-Expert Member
- Dec 19, 2020
- 306
- 538
DahMIMI NA MIMI 3
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA TISA
★★★★★★★★★★★★★
Siku ikaja mpya, Jumatano. Baada ya kuondoka huko Mzinga hiyo jana nilipotoka kumwona Bi Zawadi, moja kwa moja nilielekea hospitalini tena kuendelea na majukumu. Hakukuwa na longolongo lolote, kazi ziliendelea tu mpaka mida ya saa tano ambapo Adelina alinitafuta hatimaye kujibu ujumbe wa salamu niliomtumia awali. Kiuhakika alikuwa amebanwa na kazi sana jana na alichoka, akitoka huko kazini kwake baada ya kumaliza masaa ya ziada. Kwa hiyo nilimsihi tu apumzike, na huenda leo tungeonana kwa kuwa ningeweza kupata mbadilishano wa zamu na daktari mwingine ambaye angefanya kazi kwa upande wangu kuanzia jioni.
Sasa ikiwa ni alfajiri tu, baada ya kuamka na kujiweka safi kuelekea jukumuni, simu yangu ikaita, na baada ya kutazama mpigaji nikatulia kidogo. Ni kutotarajia kabisa kwamba askari Ramadhan angenipigia, siyo kwa sababu ya muda, bali kwa kukumbukia mambo mengi tuliyopitia wiki chache nyuma. Mwanaume huyo alinisaidia kwa vingi, na hasa kwa sababu vingi hivyo vilihusisha mambo mabaya, mwito wake kwangu sasa ukaniwekea hali makini. Hakuwa amenitafuta wala mimi kumtafuta tokea mara ya mwisho nimeongea naye kuhusiana na mdogo wake yule madam Bertha, aliyeitwa Beatha, hivyo udadisi wa akilini juu ya nini angetaka kuniambia wakati huu ulikuwa mwingi.
Nikapokea, na upande wa pili sauti yake Ramadan ikasikika akisema, "Hallo..."
"Yeah, kaka... habari?" nikajibu.
"Safi. Za siku?"
"Mungu anasaidia. Vipi wewe?"
"Kwema kabisa. Mambo yamekaaje huko kwenu?"
"Ah, kwa kipindi hiki mambo mengi yamebadilika ndugu yangu. Nilishatoka kule, sasa hivi niko Muhimbili," nikamwambia.
"Oooh, umerudi hospitali?"
"Ndiyo, likizo imeisha..."
"Okay..."
"Vipi harakati za usalama zinakwendaje?"
"Bomba tu."
"Eti eh? Mission mission kama zote mnamaliza bila shida kabisa?"
"Ah, hamna. Pamepoa sana sasa hivi toka tulipomalizana na yale ya Bertha, ndiyo maana nikaona nikucheki tujue kama umepata mkate mpya uturushie..."
"Ahahahah... hamna, hata mie kwa upande wangu ni utulivu tu sa'hivi," nikamwambia.
"Mwezi umepita sasa, nimeona nikusalimie kijana wetu wa faida," akaniambia hivyo.
Aliongea kwa njia iliyoonyesha hakukuwa na lolote zito, nami nikasema, "Asante mkubwa. Ila alfajiri yote hii, mwanzo nikadhani kuna case mpya."
"Haapana... ni kujuliana hali tu. Ulitusaidia sana kwa zile ishu, we' ni kama comrade hapa," akasema hivyo.
"Asante sana," nikamwambia.
"Basi, tutawasiliana wakati mwingine, ni vizuri kujua uko poa. Wasalimu familia," akaniambia.
Nikasema, "Sawa sawa. Halafu hivi, kuna na...."
"Ndiyo?" akaitikia.
"Ile ishu nilikwambia kuhusu mdogo wake Bertha..." nikamkumbusha.
"Ooh, sawa. Yule mweupe... uliniambia anaitwa...."
"Beatha."
"Sawa. Ndiyo, tulifanya research kuwahusu, na inaonekana hilo siyo jina lake," akaniambia hivyo.
Nikawa makini zaidi.
"Huyo mdogo wake Bertha anaitwa Tamiah Celestine. Hiyo Celestine ni surname yao wote, na wametoka kwa watu wa ukabila fulani wa huko Kenya," akaniambia hivyo.
Nikashangazwa kiasi na taarifa hii, nami nikamuuliza, "Unataka kusema Bertha alikuwa mkenya?"
"Ni watu wa huko, ukoo yaani, wenyewe wamezaliwa Tanzania na sijui sana kama walikuwa na uhusiano na wanaukoo wao, ila hawa wawili wamezaliwa na mwanamke mtanzania," akasema.
"Kwa hiyo ni kusema baba yao, ukoo wa baba yao... ndiyo wa huko nje?"
"Ndiyo. Detail zao nyingi zipo derailed, kwa mambo aliyofanya Bertha huku na wenzake hayakuhusiana na familia yake iliyo huko nje..."
"Wanaukoo wake wapo Kenya?"
"Kwa inavyoonekana, ila sina uhakika. Hakuwa na tie zozote na watu hao."
"Aliwahi kuniambia alipofungwa jela hakutaka wazazi wake na familia ijue kuhusu hilo, nilichukulia ni huku huku Tanzania. Labda alimaanisha wa huko Kenya," nikamwambia.
"Tutajuaje? Hakuna chochote kinacho-suggest kwamba alikuwa na mawasiliano na watu wa huko, na hata huyu Tamiah tumemcheki ila haonekani kujihusisha na biashara alizokuwa akifanya dada yake," akaniambia hivyo.
"Kabla Bertha hajafa kalinifata kunionya kabisa... kana ule moto kama wa dada yake, sikuona ni busara kumchukulia easy maana you never know... wanaweza kuwa na ishu zao mahala pengine na njia tofauti na zile tulizotibua," nikamwambia.
"Ahah... uko makini sana JC. Yote unayosema ni kweli, lakini kama nilivyokwambia... hatujaona lolote tena. Huyo Tamiah... mara ya mwisho najua alikuwa spotted huko Arusha... anasoma, kwa pesa za dada yake. Siyo muda mrefu atasahau yote hayo na kugeuka jiko la mtu huyo. Kama walikuwa na mipango wamebakiza kufanya, sa'hivi imeshindikana tena maana wameogopa tulipoporomosha himaya zao. Kwa hiyo usiwaze. Vile vitisho na nini... chukulia kama upepo tu, havitakuumiza..." akaniambia hivyo kiuhakika.
"Tamiah..." nikasema hivyo kwa sauti ya chini.
"Usimuwaze sana, yaani sasa hivi yale mambo yote yameshakufa na Bertha, tunaangalia vingine," akaniambia.
"Sawa sawa mkuu, asante sana. Hujaacha kuwa baraka kwangu," nikamwambia.
"Hah... kama wewe tu. Take care, wacha tuingie kazini," akaniambia.
"Likewise," nikamjibu kwa kuaga.
Simu ikakatwa, na kwa sekunde chache nikatafakari mazungumzo hayo mafupi niliyofanya na askari huyo. Uhakika alionipatia kuelekea suala la Beat... oh, hapana. Ni Tamiah. Jina la mdogo wake Bertha ndiyo lilikuwa hilo, ikiwa ni mara ya pili napata kujua kwamba majina yake niliuofahamu mwanzo yalikuwa ya uwongo. Hii ilikuwa sababu tosha kunifanya nihisi kwamba kuna kitu zaidi kilifichika kuelekea mwanamke yule, tofauti kabisa na mambo yote askari Ramadhan aliyonijulisha leo hii. Ingeonekana kama upepo wa Bertha kwenye bahari ya maisha yangu ulikuwa umekatika, lakini bado sikuwa na uhakika wa kutosha kama upepo wa Tamiah ulitoweka kabisa. Ulianza kidogo siku ambayo alinisemesha kwa kitisho, na ungeweza kugeuka kuwa mkubwa na kusababisha dhoruba kali sana kwenye maisha yangu wakati ambao nisingetarajia. Nilikuwa mpaka nimeshaanza kuyaweka pembeni kabisa mambo hayo baada ya kifo cha Bertha, lakini sasa ningejitahidi kutafuta mwanga zaidi juu ya huyu Tamiah ili niondoe hasara yoyote ambayo angeweza kuniletea; endapo kama ingekuwa hivyo. Hii tunaita tahadhari kabla ya hatari.
★★
Basi, kazi zikaanza, taratibu muda ukisogea mpaka kwenye saa sita mchana nikapigiwa simu na mama. Akanijulisha kuhusu Stella, akisema aliongea naye jana na kuhisi furaha yake baada ya mimi kuanza kumhudumia mtoto na hata kwenda kwake, na ni jambo ambalo lilimpa furaha mama pia. Ushauri wote aliokuwa amenipatia kuhusiana na hilo sasa akaona umezaa matunda mazuri, na akaomba nafasi ikipatikana tuje tukutane wote kwa pamoja nyumbani kufurahia ushirika na mwanangu Evelyn. Nikamwambia ningeutafuta muda huo, na siku siyo nyingi tungeonana kutimiza hilo.
Maongezi yalipoingia kwenye kujua hali zetu binafsi zilikuwaje, mama akataka kujua endapo kama nilishaongea na Miryam kwa lolote tena lililohusiana na zile ishu zilizozuia mipango ya ndoa, na ndiyo nikawa nimemtaarifu kwamba kwa sasa hatukuwa pamoja, wala kufikiria kuwa pamoja tena maana tuliachana kwa urasmi. Nikamwambia hatukuhitaji kuongelea chochote zaidi maana Miryam alitaka kusonga mbele, na mimi tayari nilikuwa nimeshaanza kusonga mbele pia, kwa hiyo yale yote yangebaki kuwa historia.
Mama alifikiri kwamba kuna sehemu ndani yangu bado iliumizwa sana na haya yote na akataka nije niende tuongee kwa mapana zaidi, lakini nikamwambia hilo halikuwa na haja kabisa. Kuwa sawa nilikuwa sawa, na ningeendelea kuwa sawa zaidi kwa kutojilazimu kurudi-rudi nyuma kuyaangalia hayo tena. Kwa hilo akasema haikuwa na shida, na kwamba kwa wakati huu alijihisi yuko sawa hata zaidi kuja kuzungumza na mama mkubwa wa Miryam, Bi Jamila, kuhusu yaliyopita, na akiwa anataka kusawazisha hali baina ya familia zetu iwe nzuri. Jambo hilo likaonekana kuwa jema sana kwangu, nami nikamwambia tungepanga kuja kuonana na mwanamke yule ili kwanza afanye maongezi naye, halafu baadaye familia kiujumla. Amani na mpangilio mzuri ungefuata bila shaka.
Baada ya kumaliza maongezi na mama, nikawa nataka kwenda kupata chakula kwanza maana asubuhi yote sikuwa nimetia chochote tumboni, lakini ni hapo hapo tu Ankia naye akawa amenipigia. Nikapokea, na baada ya kujuliana hali mwanamke huyo akafanya maongezi kuhusu jinsi nilivyofika pale kwao jana kumsalimia Bi Zawadi ndiyo yawe dhumuni kuu la kunipigia. Ankia alitaka kujua ni kwa nini nilitenda kwa jinsi nilivyotenda kumwelekea Miryam. Mh? Nikamuuliza alimaanisha nini, naye akasema nilimtendea vibaya kwa kutomsemesha na kumwacha akijisikia vibaya sana.
Alikuwa akinilalamikia yaani, kwamba Miryam aliishiwa raha kabisa kwa sababu yangu, nami nikamwambia Ankia ishia hapo hapo. Alitaka niongee nini na yule mwanamke? Nilikuja kwa ajili yake ama Bi Zawadi? Na kumsemesha, sikumsemesha? Alikuwa anataka nimbebe au hayo mawazo Ankia alikuwa anayatoa wapi? Nikamwambia Ankia kama amenipigia kunitibua ni bora akate simu na asinipigie tena ikiwa hana jambo lingine la kusema. Ndiyo akaanza kuja chini et ooh... siyo hivyo, nilimwonea tu huruma, hakusema chochote lakini yeye ni rafiki yangu namwelewa.
Nikamwambia sikufanya chochote kibaya pale, labda kama kibaya kwa Miryam ilikuwa mimi kufika hapo kwake, ndiyo sababu sikutaka hata kuingia ndani. Nikamweleza kwa ufupi kwamba mawazo ya namna hiyo hayakufaa, kwa yeye Ankia, kwa sababu tayari Miryam aliweka uamuzi wake mbele ya watu wote kuhusu mahusiano yetu wiki chache nyuma, na ni kwamba tumeachana, sasa sijui angekuwa na matarajio yapi kwa sasa hivi tena wakati alinibwaga yeye mwenyewe. Mimi hata kujenga hali ya urafiki na Miryam sikufikiri ni jambo ambalo lingewezekana, kwa hiyo nikamwomba Ankia aweke hizo mada pembeni kabisa; akitaka tuongee mambo, yawe mambo yaliyonyooka. Akawa anaguna-guna tu na kusema sawa, ila ikitokea nafasi ya mimi kuongea na Miryam, eti nisikwepe maongezi na nijaribu kumsikiliza mwanamke huyo.
Ankia alinishangaza kwa kweli, ni kama vile alikuwa akitaka kusema jambo fulani hivi, lakini akajizuia, mpaka nikahisi labda hapo aliweka simu kwa mfumo wa sauti ya juu na Miryam mwenyewe alikuwa pembeni yake, kwa hiyo nikaamua tu kumuaga na kukatisha mazungumzo hayo. Yaani nilikuwa nimetoka tu kwenye hali ya amani baada ya kuzungumza na mama halafu Ankia naye akaja kunivutugia mambo. Sasa mimi na Miryam kwa wakati huu tuongelea nini? Tuanze kuongea na kujichekesha kinafiki utadhani hakukuwa na damu mbaya kati yetu, ndiyo walitaka hivyo? Sikuhitaji hayo mambo tena. Na sikutaka kuendelea kuyafikiria. Nikaweka namba ya mpenzi wangu Adelina na kumpigia hapo, nami nikatoka ofisini kwenda kutafuta chakula kwanza huku nikiwa nimeanza kuzungumza naye. Araah!
★★
Siku ikaendelea kutembea vyema, na hata Ankia kunipanda kichwani muda ule kukasahaulika. Nimekuja kumaliza kazi zangu saa moja jioni na kuachia wengine ili nikapumzike, lakini tayari nikawa na mipango mingine kwa usiku huu. Muda ule nimeongea na Adelina, tulipanga kutoka baadaye kwenda kujifurahisha kidogo, yeye akiwa na nafasi kutoka kazini saa mbili, hivyo nikamwambia ningempitia kule kwake akishafika. Alikuwa amenikosa mwenyewe, akitaka kweli tufurahie usiku huu hata kwa masaa machache, kwa hiyo nisingemvunja moyo. Moja kwa moja nikarudi kule kwangu, na tayari rafiki yangu Simba alikuwepo akifurahia kutazama mechi kwa utulivu. Tukasalimiana vyema na kujuliana hali, nami nikatulia pia kwa muda mfupi kisha nikamwambia ningetoka tena kwenda sehemu fulani na mtu.
Simba kama Simba akataka kujua ni nani, na nilipomfahamisha kuwa ni Adelina, akataka kuja pamoja nami pia ili amwone kwa mara ya kwanza. Ilitakiwa kuwa kitu ya mimi na mpenzi wangu pekee, lakini Simba akasisitiza kuja, akisema angekunywa mbili tatu tu pamoja na "shemeji mpya" kisha angetuacha baadaye tuwe pekee. Sikuona shida kwa hilo. Kwa hiyo tukajiandaa kikawaida tu, ikiwa inaelekea saa tatu, tukaondoka hapo nyumbani nikiwa naelewa Adelina tayari angekuwa ameshaondoka kazini. Simba akawa ananipigisha story kama zote wakati tuko njiani kuelekea huko Kinyerezi, na katikati ya safari Adelina akanipigia kuniambia kuwa aliningojea huko kwake tayari hivyo niwahi kabla muda haujayoyoma mno.
Kweli, nikajitahidi kuwahisha, mpaka tumefika kwake mrembo ilikuwa inaelekea kuingia saa nne, shauri ya umbali. Nikamwita, kwa sababu tayari alikuwa amejiandaa ingepaswa kuwa atoke, apande kwenye gari, twende. Simba alikuwa ameketi siti ya mbele pembeni yangu, lakini hapo akashuka na kwenda kukaa ya nyuma ili Adelina akija akae ndiyo pembeni yangu. Baada ya dakika chache, kweli mwanamke huyo akatoka, tukimwona namna alivyopendeza kwa kuvalia kiblauzi chekundu chepesi na suruali nyeusi ya skinny iliyoling'ata umbo lake nono vyema, na Simba akawa amekubali. Kwamba kweli nilijua kuchagua wanawake. Sikumwambia kihalisi ni mimi ndiye niliyekuwa nimechaguliwa na mwanamke huyo, ila hiyo ikaishia hapo. Adelina kusifiwa ilikuwa jambo zuri kwangu. Alikuwa ameumbika kweli.
Kwa hiyo akaja mpaka ndani ya gari, akiwa amependeza kweli usoni, nasi tukapiga busu ya kinywa akiwa hajamwona Simba huko nyuma. Ndiyo ile nimemwonyesha, akacheka kwa haya na kufunika mdomo wake, nao wakatambulishana sasa mmoja na mwenzake; nikimwambia Adelina kwamba huyo Simba ndiyo rafiki aliye "best" katika marafiki wote nilionao. Nikageuza gari, mwendoni tukaingia tena, na Adelina akiwa ameniuliza tunakokwenda, nikamwambia leo tungeenda kujiburudisha club. Hakuwa ametarajia hilo, hasa kwa kuwa alipitisha muda mrefu kwenda sehemu kama hizo, kwa hiyo nikamwambia ajiandae kupagawa na burudanj leo mpaka asahau uchovu wowote wa kazi. Akaonyesha utayari wa hilo. Simba alikuwa mtulivu tu.
Basi, tukafika na kuegesha gari mbele ya jengo la club moja kubwa kwenye maeneo ya Mbezi Luis, sijui ndo' panaitwa hivyo, nasi tukaingia huko na kukuta tayari watu wameshajaa na kufurahia muziki na vinywaji. Aisee watu walijua kujitumbuiza. Yaani ulikuwa unaingia club unahisi ni kama umefika nyumbani. Palichangamka sana. Nikamwambia Adelina tucheze, lakini kwa jinsi alivyokuwa, mwanzoni aliona uzito na hata kudai hajui kucheza. Ahaa? Nikamvuta mpaka sehemu tuliyoweza kusimama na kuagiza vinywaji, hapo tukaanza kupiga pombe sasa. Mwanamke alitaka kuwa mstaarabu kwenye kunywa lakini nikamshinikiza anywe mpaka ahisi kichwa kimebondwa japo kidogo, na hilo lilipofanikiwa, ndiyo nikamwingiza sasa kati. Simba hakuwa nyuma.
Hali ya hewa ikiwa imechangamka, watu wakijirusha, kunywa, kula, kulana, tukaanza kucheza muziki. Adelina alijirusha pia, kila mara muziki mpya uliopendwa na wengi ukipigwa alikuwa akirukaruka na kunichezea kwa ukaribu kwa mitindo iliyonisisimua sana, na kadiri muda ulivyokwenda nikazidi kufurahia sana pindi hii. Watu hata ambao sikuwafahamu walikuja kujichanganya na sisi, wakicheza na mimi, wakicheza na Adelina na Simba, na pombe ikiendelea kunyweka kila nafasi ndogo ilipopatikana ya kupumua. Kuna wakati nikawa nikiangalia simu na kukuta namba ngeni kabisa ikiwa imenipigia mara kadhaa, lakini mvutano wa burudani hapo club ukanizuia kuijali na kuweka simu mfukoni tu. Nikawa nahisi muda umeanza kwenda sana, na nilitaka kujirusha hapa club lisiwe jambo la mwisho kufanya mimi na mpenzi wangu mpya. Leo nilitaka tuvaane angalau kidogo.
Nikataka nimfate, nimshike ili kumvuta pembeni na kumwambia tuondoke kwenda kujilia bata yetu faraghani, na nilipomkaribia alikuwa akicheza pamoja na Simba kwa shangwe nyingi. Nikamsemesha, lakini hakunielewa, macho yake yakiwa yamelegezwa na pombe kiasi, hivyo nikawaomba wote wawili tusogee usawa wa kaunta moja ili tupumue kidogo. Wakatii, na tulipokwenda upande ambao haukuwa mbali sana na kaunta, nikamwambia Simba kimasihara kuwa muda uliisha, hivyo abebe virago vyake asepe ili mimi na Adelina twende kwingine. Wote wakacheka sana, utani na masihara zaidi yakianza hapo huku Adelina akinishikilia kiunoni na kusikiliza maneno ya Simba, nami nikazungusha macho huku na kule kwanza kabla sijawaambia tuondoke kwa pamoja; ilhali Simba hakutaka kuondoka. Pisi nyingi amwachie nani eti? Si ndiyo ile nimepiga jicho hivi tena nikawa nimemwona Miryam pale usawa wa kaunta! Heel
Nilishtuka. Niliganda. Nilihisi pigo zito kiasi moyoni mwangu kutokana na kutotarajia kabisa kumwona sehemu hiyo, na nikajikuta nimeendelea kutulia na kubaki nimemtazama kwa umakini. Yaani alikuwa amesimama umbali mfupi kutokea sehemu ambayo sisi tulikuwa, pale kwenye kaunta la tender wa vinywaji, akitazama kwangu moja kwa moja kabisa. Alikuwa amevaa vizuri, T-shirt nyeupe na suruali jeans yenye kubana, na macho yake yaliniangalia kwa njia iliyoonyesha wazi kwamba alitegemea kabisa kuniona, yaani hakushtuka, ni kwamba alikuwa ameshaniona kwa muda mrefu tangu tumefika sehemu hiyo. Sikuwatazama wenzangu tena baada ya macho yangu na Miryam kukutana namna hiyo, lakini nilielewa wao pia walikuwa wameshaona nilikoangalia, na najua Adelina akabaki kusubiri jambo fulani litokee.
Nilimwangalia Miryam kwa mkazo, lakini kihisia, nikiwa nahisi mapigo yangu ya moyo yanadunda kwa kasi zaidi kumwelekea yeye. Sijui kwa nini tu, ni kama bado alikuwa na athari kubwa moyoni mwangu. Kuna kitu nilianza kuhisi kinanitia msukumo, yaani msukumo wa kama kutaka kumwelekea pale alipokuwa amesimama, na hata nyendo za mwili wake zilionyesha hivyo pia, sema ikawa kama vile sote tunasubirishiana. Ndipo kikatokea kitu ambacho kikafanya msukumo huo uvurugike kabisa. Kutokea upande wake wa kulia akamfikia mwanaume ambaye nilimfahamu vyema sana, Festo mwenyewe! Tarajio lolote ambalo kona ndogo ya sehemu ya moyo wangu lilikuwa limeanza kujengwa likatokomea papo hapo. Nilijisikia vibaya sana kuona picha hiyo.
Festo alikuwa ameshikilia bia mbili za kopo, akimfikia Miryam na kuonekana kutaka kumpatia moja, jambo lililonihakikishia kwamba walikuja sehemu hiyo pamoja. Ah, kudadeki! Sijui kwa nini, lakini nikahisi nikichomwa kweli na jambo hilo. Si nilijiambia nisingejali tena? Lakini bado nikahisi kuumia. Sikutoa macho yangu kwao, na najua wenzangu pia walikuwa wakitazama upande wake Miryam. Simba akawa akinitikisa kuniita 'oya, vipi?' lakini sikumwitikia hata kidogo. Miryam hakupokea kinywaji ambacho Festo alitaka kumpa kwa kuwa aliendelea kunitazama tu, na hilo likafanya jamaa atazame upande wangu. Aliponiona, hakuonyesha hisia zozote za kushangaa na kutulia tu, nami nikaacha kuwaangalia wao kwa pamoja na kumtazama Adelina na Simba pembeni. Adelina alinitazama kwa hisia makini kiasi.
"Tuondoke," nikamwambia Adelina hivyo.
Na sikusubiri anipe jibu, hapo hapo nikageuka nikiwa nimeushika mkono wake na kuanza kuondoka. Simba akaniomba nisubiri kwanza, akiuliza tunaenda wapi, lakini sikukatisha hatua zangu, na hata nilipouachia mkono wa Adelina najua wote kwa pamoja walinifuata kwa nyuma. Ingekuwa kwamba nimemwona Miryam pekee hapo basi labda ningevunga tu na kuendelea na mambo mengine, ila kumwona akiwa na Festo, kulinikata stimu kabisa. Tena yaani hata sijui ilikuwa vipi eti na wenyewe wakawa ndani ya club moja na sisi kwa muda huo huo. Hapa pasingekalika tena kwangu, ila najua bado wenzangu walihitaji kuendelea kupata wakati mzuri, na mimi nisingeacha matatizo yangu yawavurugie furaha yao. Hivyo nikawaza tu tukiondoka sehemu hiyo tuelekee nyingine eneo tofauti, na huko tungesaidiana zaidi kusahau mikazo yetu; yangu sanasana.
Nikiwa nimetangulia, tukazifikia ngazi kupitia mlango wa nyuma wa jengo hilo na kuanza kuelekea chini, pale niliposikia jina langu likiitwa na sauti niliyoifahamu vyema kabisa.
"Jayden..."
Ilikuwa ni Miryam. Sikugeuka, na hatua zangu zikafifia kiasi lakini sikuacha kutembea. Kwa jinsi ilivyosikika, sauti yake ilionyesha kwamba alikuwa akitufuata kutokea kule ndani, bado akiwa hajazifikia ngazi, nami nikaona niongeze kasi ya kushuka ili nimwepuke upesi.
"Jayden..." sauti yake ikasikika tena.
"JC... kuna mtu anakuita..." Simba akanisemesha kutokea nyuma yangu.
Sikujibu wala kugeuka na kuendelea kuukata mzunguko wa ngazi ili niwahi kutoka sehemu hiyo, na sasa ikawa wazi kwamba Miryam alikuwa ametukaribia, akishuka ngazi upesi pia kama vile anakimbia.
"Jayden... subiri..."
Ih! Alikuwa anataka nini? Yaani, wakati huu niliokuwa najitahidi kusonga mbele bila yeye, yeye tena akaanza kunikimbiza ili kunirudisha nyuma, siyo? Tena alinionyesha wazi kwamba na yeye alikuwa ameshaanza kusonga mbele na huyo Festo wake, sasa sielewi alihitaji nini zaidi kutoka kwangu. Mizinguo, ama? Sikutaka kabisa kusimama, na ikiwa ndiyo imebaki mistari miwili kuzimaliza ngazi kufikia chini, Miryam akawa amefanikiwa kuwapita Simba na Adelina na kunishika mkononi upesi, jambo lililofanya nigeuke kwa kasi kumwangalia. Alishikilia mkono wangu kwa nguvu, akiuvuta fulani hivi yaani kunizuia, ili nisimame, huku akipumua kwa kasi kiasi, na macho yake yakinitazama kwa hisia nyingi za huzuni.
"Jayden..." akaita.
Nikaendelea kukaza macho yangu usoni kwake kwa umakini.
"Samahani..." akaniambia hivyo huku machozi yakimlenga.
Nikaendelea tu kumwangalia.
"Tafadhali... naomba unisamehe mpenzi wangu..." akasema hivyo.
Sauti yake tamu aliyotumia kuniambia hivyo ilifanya nihisi kuyeyuka moyoni, yaani aliongea kwa hisia huku akikikaza zaidi kiganja changu, nami nikajikuta nalengwa na machozi kwa sababu ya hisia nilizokuwa nikificha kulazimisha kutoka.
Machozi yake yakamwagika, akikinyanyua kiganja changu kukikaribisha na uso wake, na kwa sauti tetemeshi akaniambia, "Nakuomba... naomba tuongee... tafadhali..."
Alionekana kutaka kusema kitu fulani muhimu sana zaidi tu ya kuomba samahani kwa maneno aliyoniambia ule usiku. Nikakosa hata cha kumjibu, hapo tukiwa tumesimama sehemu ambayo watu na wapenzi wao wangepita na kututazama kwa kudhani tunatengeneza sinema, na ndipo kutokea ngazini kuelekea juu nikamwona Festo akiwa amefika hapo na kusimama. Alisimama kwa huo umbali akitungalia, nami pia nikimwangalia, na Miryam pamoja na wengine wakamwangalia. Miryam akiporudisha macho yake kwangu, nikamwangalia pia, kisha nikakivuta kiganja changu kutoka kwake kistaarabu tu, yeye akiwa kama hataki kukiachia, na nilipofanikiwa kukiondoa, hapo hapo nikamwacha na kuendelea kushuka ngazi.
Bila kugeuka nyuma wala nini, nilisikia sauti yake ya chini ya kilio, akionekana kuhuzunika sana, nami nikakaza hisia zangu kiume na kuelekea moja kwa moja mpaka garini kwangu; Adelina na Simba wakiingia pamoja nami. Sikutaka hata kuzungumza, nikawasha tu gari, na hapo ndiyo hisia zikanilemea zaidi na kujikuta tu naishia kuukaza usukani kwa mikono yangu. Miryam bado alikuwa anaudundisha mno moyo wangu, mpaka sasa nikawa sielewi kile nilichotaka au kuhitaji mimi binafsi kuelekea suala langu na huyo mwanamke. Nadhani Adelina aliona namna ambavyo nilikuwa nimevurugika kihisia, naye akiwa kwenye siti pembeni yangu, akakishika kiganja changu na kukikaza kama kunitia moyo bila maneno. Sikumwangalia, bali nikashusha tu pumzi kujipa utulivu, kisha ndiyo nikaliondoa gari sehemu hiyo.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★★
WhatsApp +255 678 017 280
We Mimi 🌝
Sema utulivu wa Festo ni moto 🔥
Jamaa ana akili sana, Huwa hatumii hisia kwenye haya mambo