MIMI NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI NA SABA
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Nikamfata tu askari Ramadhan baada ya hapo na kujiunga pamoja na huyo Festo kutia saini karatasi za kuthibitisha hiki na kile, na kiukweli sikukazia fikira mambo hayo kwa sababu akili yangu bado ilikuwa imetatizwa na suala zima la Festo kuwa hapa, huru, na akionwa kama malaika pia na hawa jamaa. Tena kwa jinsi tu alivyokuwa amenisemesha sekunde chache nyuma yaani ndiyo alizidisha kuthibitisha kwamba hakuwa upande mzuri kikamili, kwa hiyo ningesubiri kusikia aliyotaka kuniambia ili niamue ningemchukulia vipi zaidi.
Baada ya kumaliza kusaini, askari Ramadhan akatuaga kwa kusema kuna mambo mengine tena angeanza kushughulika nayo, nasi tukaondoka hapo ofisini kwao. Kufikia sasa sikuwa nikihisi maumivu tena kutokea kwenye nyonga mpaka sehemu za siri. Nilikuwa nyuma ya Festo, yaani yeye alitangulia mbele yangu na kuelekea mpaka kwenye lifti ili ashuke chini, na najua alitarajia nipande lifti hiyo pamoja naye lakini mimi nikaamua kutumia ngazi kushuka. Sikujali angechukuliaje hilo, yaani angejua mwenyewe.
Nikatoka mpaka kufikia nje ya jengo hilo nikiwa ninafikiria kwenda kuchukua usafiri, ndipo kutokea upande mwingine wa eneo hilo honi ya gari ikawa imepiga mara mbili. Nikaangalia huko na kumwona Festo akiwa amesimama kwa kunitazama karibu na gari zuri jeupe, aina ya Lexus 600
View attachment 3068067
kama lile jipya la Bertha ila la gharama zaidi, nami nikasimama tu na kuendelea kumwangalia. Akaniita kwa kiganja chake tena na kisha kuingia garini bila kusubiri jibu.
Nikatulia kwanza nikitazama huko kwa ufikirio, kisha nikaamua kwenda. Nilipokuwa natembea kulielekea gari hilo, nikatoa simu yangu na kuweka ule mfumo wa kurekodi sauti, kisha nikairudisha mfukoni ili mfumo huo utembee tu katikati ya maongezi yote ambayo ningefanya na huyo jamaa.
Kama alikuwa anapanga tuongee tu, basi mengi ambayo angesema ningeyanasa na hata kuja kuyatumia baadaye ikiwezekana, na kama alkuwa anataka kunidhuru, nilikuwa tayari kupambana pamoja naye. Yaani sasa hivi sikujua na sikujali alikuwa nani huyu mtu. Kama ni chini, basi tungeenda pamoja.
Nikafika kwenye gari lake na kuingia siti ya pembeni na usukani alipokaa yeye, nami nikatulia tu, nikitazama mbele kwa utulivu.
"Utapenda tukiongelea hapa, au tutafute sehemu nyingine?" akauliza hivyo.
"Hapa hapa," nikamjibu.
"Uko sawa? Nimeambiwa umekoswa na risasi leo...."
"Unataka nini, Festo?" nikamkatisha.
"Nataka kujua uliyosema kwa mkubwa kabla sijafika. Ulikuwa umeshaanza kutembeza mdomo wako huko ndani, ulitaka kuwaambia nini kuhusu mimi?" akaniuliza hivyo.
"Kwani itajalisha mimi nasema nini kuhusu wewe?"
"Ndiyo, haijalishi."
"Sasa? Si wamesema toka mwanzo u... si umekuwa unaigiza tu? Unataka nini sasa?"
"Mbona una hasira sana? Hm? Ulikuwa unatarajia na mimi ningekamatwa, si ndiyo?" akaniuliza hivyo.
Nikatazama pembeni tu.
"Kwa hiyo matarajio yako kwenda ndivyo sivyo imekunyima furaha... mhm... umejiona fala," akasema hivyo.
"So, ni uwongo then. Ni uwongo kwamba uko upande wa maaskari, kila kitu ulichofanya kuwasaidia ni nothing but a sham. Si ndiyo?"
"We' unaonaje?"
"Oh, naona jinsi navyoona. Najua haiwezekani kabisa eti kwamba ulikuwa unaigiza tu, Festo. Najua ulikuwa pamoja na Bertha. Tena kwa mengi tu, siyo madawa pekee. Najua we' ndiyo mbaya kuliko hata yeye, ni kwamba tu umeweza kugeuza hilo wimbi lote limzamishe yeye peke yake na wewe usilowane hata kidogo, because...."
"Kwa nini umeumia sana Bertha kukamatwa wakati ni wewe ndiyo umem-snitch tokea mwanzo?" akaniuliza hivyo.
Nikabaki kimya, nikimtazama kwa umakini tu.
"Acha unafiki. Unajua... siku ile umekuja kwangu ukaongea bullshit yote kuhusu wewe kumpenda Bertha, nilikuwa nawaza 'huyu dogo anaongea pumba tu hapa kuni-convince na nini,' lakini sa'hivi nimeanza kuona haikuwa pumba. Umempenda Bertha kiukweli kabisa," akaniambia hivyo.
"Simpendi," nikasema hivyo kwa uhakika.
"Really? Well, kwa nini ulihatarisha maisha yako kumsaidia ulipojua Sudi alitaka kumuua?" akaniuliza hivyo.
"Sikutaka tu auliwe. Hiyo haimaanishi kwamba nampenda. Na... ilikuwa njia nzuri ya kumfanya aendelee kuniamini."
"Mmm?"
"Eeeh. Wewe je? Huo muda wote ulikuwa unajua kila kitu eti, kwa hiyo ukawa unanichora tu, si ndiyo? Umefanyaje Festo mpaka ikawa hivi? Hm? Umewalipa hawa jamaa?"
"How dare you!" akaongea hivyo kwa mkazo.
Nikatulia na kuendelea kumwangalia.
"Unafikiri kwa kuwa nimeficha mambo mengi mabaya basi sina honour hata kidogo?" akaniuliza hivyo.
"We' ndo' uniambie," nikamsemesha kwa ujasiri.
"Nikuelezee nini mtoto mdogo kama wewe? Unafikiri kwa sababu umekuwa ukifanya kazi na maaskari basi hiyo inakufanya uwe msafi? Kwa kila kitu? Hata wewe ni mchafu JC, umecheza tu haka kamchezo kujiaminisha kwamba una nia nzuri, lakini sote tunajua kwamba mimi na wewe ni wabinafsi wa hali ya juu, na tunafanya lolote ili kupata tunayotaka. Kabla ya kujifanya unajua sana kujaji, jiangalie kwenye kioo kwanza," akaniambia hivyo kwa hisia kali.
Nikaangalia pembeni kwanza, nikiwa natafakari maneno yake.
Akasema, "Njia zetu zinatofautiana, lakini we are the same. Ni kwamba me nimekuzidi tu katika mengi mabaya, lakini haimaanishi nimepoteza kabisa nia ya kufanya mazuri. JC..."
Nikamwangalia.
"Ninataka kuacha. Haya maisha ya gizani haya? Ninataka kuyaacha kabisa... ndiyo maana nikafanya hivi," akaniambia.
Nikaendelea kumwangalia kwa umakini.
"Unajua nini mdogo wangu? Toka siku ya kwanza Bertha kakuleta kule Red Room, nilihisi tu kulikuwa na kitu hakiko sawa. Nilikufatilia na kujua ulikuwa pamoja na hawa watu, lakini unajua kwa nini nilikuacha tu?" akaniuliza.
Nikatulia kusubiri ajijibu mwenyewe.
"Nilikuacha kwa sababu ulinisaidia kuona kwamba hayo maisha hayakuwa sahihi kwangu kuendeleza. Oh, na siyo kwamba wewe ndiyo ulifanya nikaona hayo maisha hayafai tena, ni kwamba tu ulikuja kwenye wakati mwafaka ambao nilitaka kuyaacha. Ukafanya boost up tu. Ramadhan anajua kwamba nilikuwa nafanya hizo biashara kweli," akaniambia hivyo.
Nikamwangalia kiumakini zaidi.
"Anajua. Kwa sababu nilimfata mimi mwenyewe kumwambia. Na nilimwambia najua kuhusu wewe kushirikiana naye, na sikuwa na nia ya kukuumiza hata baada ya kujua hilo kwa sababu nilitaka kutoka kwenye hizi ishu. Kwa hiyo tukafanya makubaliano, nijitoe kusaidia kukomesha haya yote mwanzo mwisho. Ningekuwa nataka kuendelea na madawa JC... ungekuwa umeshakufa nilipojua tu unatu-snitch," akaniambia hivyo.
Nikatulia kidogo na kisha kumuuliza, "Kwa nini? Kwa nini ulitaka kuacha?"
Akaangalia mbele na kusema, "Miryam."
Nikafumba macho na kisha kuangalia pembeni. Mada ikarudi kwa bibie. Yaani yeye ndiyo alikuwa katikati ya kila jambo!
"Siku ile ulikuwa unasema 'ooh, kama utajifanya malaika kwa Miryam, hata me nitajifanya Shetani kwa Bertha.' Ahah... nilikuangaliaaa... unajua kweli kuigiza mdogo wangu. Lakini hata me sikuwa nyuma. Niliendelea kuigiza, kukufanya ufikiri kwamba naweza hata kuwaumiza watu wa familia ya huyo mwanamke ili unijaji kama unavyonijaji sasa, lakini mimi siyo mbaya kiasi hicho, na sijali unachofikiri kunihusu JC. Nilikuwa na-play part yangu vizuri ili hii siku ifike, na imefika kama nilivyotaka, lakini sikuwa mtu uliyenidhania nilikuwa. Sikutaka... kujifanya malaika ili nimpate Miryam, nimetaka KUWA huyo malaika ili niweze kumpata Miryam..." akasema hivyo.
Nikiwa nimetazama mbele tu, nikamuuliza, "Kwa hiyo ni kwa sababu ya Miryam ndiyo ukataka kubadilika?"
"Yeah. Tayari nina kila kitu, chochote kile naweza kupata, lakini furaha, bado haikuwepo ile niliyoitaka. Ni kwa sababu nilitaka kuwa na furaha zaidi... hizi mali na nini, siyo furaha. Ndiyo nikaliona hilo jambo kwa Miryam, na... ukweli ni kwamba imekuwa too late kwa sababu hata kama ningefanya nini... huyo mwanamke hajaweza kunipenda," akasema hivyo.
Nikamtazama na kuona uso wake umeshikwa na simanzi kiasi.
"Kuna siku hadi nili-snap kidogo... ahah nikamwambia nitampa, na nitafanya yote kwa ajili yake, lolote lile ili tu akubali nimwoe, na hapo ndiyo nikawa nimeharibu zaidi, maana nilimfanya afikiri kuwa labda namwona kama kitu cha kununua. Lakini yeye bila kujua kuhusu haya maisha yangu na nini... akasema napaswa kujitahidi kufanya vitu vingi kwa wema wa moyo, siyo kwa matarajio ya kupata faida tu, maana... wakati mwingine zinaweza zisije faida, ila hasara. Na mimi hasara yangu ikawa kumpoteza," akasema hivyo na kuniangalia.
Dah! Nikaangalia tu pembeni, maana nilielewa vizuri sana kwamba huo ulikuwa ni ukweli. Huyo alikuwa ndiyo Miryam.
"JC nachukia kuwa dramatic kama hivi, lakini... nimeongea hayo yote kwa sababu umeniona... umeniona nikiwa huko, kwenye familia yake nikijaribu kum-win huyo dada. Sikuwa na ulterior motive, nilimkubali kweli. Lakini hata baada ya kumkosa, haikumaanisha ningetaka kurudi tena kwa hizi mishe, no. Nimetaka kuacha siyo kwa ajili ya Miryam tu tena... but for me. Nataka tu ni..toke. Nime... nimeumiza watu, nimelaghai watu, nimevunja sheria, nimeua... na nikiangalia... sioni faida yoyote ile kubwa niliyopata kufikia sasa hivi zaidi ya majuto, na hilo limenibomoa sana," akasema hivyo.
Nikashusha pumzi kiasi na kuangalia pembeni zaidi.
"Lakini kila mtu si anastahili msamaha? Nikitambua kwamba nimekosea, na kuna uwezekano wa kubadilika, nafanya hivyo. Ndiyo ninachokifanya. Nataka kusafisha maisha yangu kabisa, sitaki kuwa mbinafsi tena, yaani... nataka nianze upya..." akasema hivyo.
"Kwa kuharibu zaidi maisha ya wengine ili kupata hilo unalotaka, huoni kwamba bado unaendelea kuwa mbinafsi?" nikamuuliza hivyo bila kumwangalia.
"Unamwongelea Bertha?" akaniuliza hivyo.
Nikamwangalia na kusema, "Hapana. Namwongelea mtu kama Saidi."
Akabaki kimya.
"Kwa nini ulimuua shefu Saidi?" nikamuuliza.
Akatikisa kichwa kidogo na kusema, "He was collateral damage."
"Ooh kumbe? So maisha yake, familia yake, haikujalisha kabisa... ukaamua tu kumu...."
"Nimeua wengi, JC. Hata wewe ningekuua!" akaniambia hivyo kwa sauti kali.
Nikatulia na kuendelea kumwangalia kwa umakini.
"That's my point! Nimefanya mabaya, I want to stop. Bertha na wengine walikuwa contended kuhusu maisha waliyochagua, hakuna hata mmoja aliyeonyesha kutaka kuyaacha maana huwa yanazidisha kiu tu ya kutaka zaidi, na zaidi, na zaidi... ndiyo maana ilikuwa lazima kuwaacha watumbukie kwenye shimo la simba..."
"Halafu wewe ujiokoe mwenyewe..."
"Tell me, ulitaka nifanye nini? Nijishikishe kwa maaskari kwa yote niliyofanya baada ya kina Bertha kukamatwa, si ndiyo?"
"Yes! Hapo ndiyo ungekuwa umeondoa ubinafsi. Siyo kwamba ukijiona wewe una haki ya kubadili maisha, wengine hawana... na wewe ungejitoa ufungwe," nikamwambia hivyo kwa uhakika.
"Ingesaidia nini? Yote niliyofanya yangekuwa reversed? Huyo Saidi wako angerudi kuwa hai?" akaniuliza hivyo kimkazo.
Nikameza mate kwa hasira huku nikimtazama kwa umakini.
Akashusha pumzi kujipa utulivu, naye akasema, "It doesn't matter. Tunafanya lolote lile ili ku-survive. Okay? Nimetoa... pesa nyingi sana, nimejiachia kutoka kwenye hizo biashara haramu, nimekata tie zote na watu wote wabaya niliokuwa nafanya nao hayo mambo ili niweze kuwa mtu mwingine kuanzia wakati huu, haitoshi? Ni lazima mpaka niende jela, au na me niuwawe ili JC ndo' aridhike sasa eti Festo hakuwa mbinafsi? Hiyo siyo akili, na mimi siishi kwa misingi unayotaka wewe. Unanielewa? Kuanzia sasa nitaishi maisha yangu navyoona fit baada ya kuachana na haya yote... haijalishi ulikuwa unajua nini, maaskari wanajua na hawajui nini, au Bertha ama nani amefanya nini... imekuwa ilivyokuwa. Na itapaswa kuishia kuwa hivyo."
Nikatazama pembeni tu na kutikisa kichwa kwa kutoamini kiasi. Hata kama alikuwa anataka kubadilika lakini bado niliona alikuwa mbinafsi sana, yale mambo ya mtu unaweza kubadili tabia lakini siyo utu wote, ndiyo alilokuwa nalo hilo jambo.
"Sijakuita hapa ili uwe kama judge wangu mkuu, ama labda nikuombe msamaha. Sijakukosea kwa lolote. Nimekuita hapa kwa sababu we' ni mwanaume. Unanielewa vizuri. Sijui sana kama ulikuwa umeshampenda Bertha, lakini najua ulikuwa unamjali. Hata ukatae. Kuna sehemu ndani yako ilikuwa inataka na yeye abadilike... aache haya maisha. Uwongo?" akaniambia hivyo kistaarabu.
Nikainamisha uso wangu tu na kutikisa kichwa kukubali.
"Najua. Lakini kama wengine, ilikuwa imesham-consume sana, hangeacha. Na mimi... namjali pia. Namwonaga kama mdogo wangu, ni bora kumshikisha kwa mapolisi aka-serve miaka mingapi jela, atoke, akiwa salama... labda. Kuliko aje kufa kwenye hili game ambalo.... haina faida yoyote, JC. Na nimekwambia, imeshakuwa jinsi ilivyo, kilichopo kutokea hapa, ni kusonga mbele kwa mengine. Basi," akaniambia hivyo.
Nikiwa bado nimeshusha macho yangu, nikamuuliza, "Kwa hiyo utafanya nini kutokea hapa sasa?"
"Bado kuna vitu natakiwa kuweka sawa. Nataka nimalize kuuondoa uchafu wote kwenye maisha yangu, mengine yatafata tu," akaniambia hivyo.
"Na Miryam?" nikamuuliza hivyo huku nikimtazama kwa jicho la chini.
"Sijui. Huwa najipa matumaini kwamba labda sijampoteza kabisa, lakini kama imeshafika hiyo hatua... nataka kuhakikisha. Na nitajua la kufanya baada ya hapo," akasema hivyo.
Mh! Mwana nikajikausha tu kama vile sikuwa na langu jambo kumwelekea mwanamke yule pia. Hapa nilikuwa na fahali mwenza, lakini nilitulia zaidi tu maana hakujua kwenye zizi alilotaka kulalia mimi pia nilikuwa namendea kuingia.
Akasema, "No hard feelings, JC. Really, yaani kati yangu me na wewe, hakuna ubaya wowote. Sawa? Nataka tu ifike mahali iwe kama hatujawahi kujiingiza kwenye hizi biashara pamoja, yaani... iwe kama hatukuwahi kujuana hivi. Hiyo peace angalau kwa upande wako naihitaji. Sitaki kabisa tuvurugiane maisha mdogo wangu. Naomba ukitoka hapa, usinijue, nisikujue tena. Siyo kwa ubaya, bali kwa usalama, na ndivyo inavyotakiwa. Unanielewa?"
Nikiwa nimetazama mbele sasa, nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa.
Akashusha pumzi na kusema, "Naweza kukusogeza hapo mbele ukitaka, uchukue usafiri. Unaenda Mbagala?"
"Hamna, kuna sehemu nyingine naenda kwanza. Nitashuka tu na kutembea mpaka hapo," nikamwambia hivyo kwa utulivu.
"Sawa. Good talk. Tutaonana tukionana basi. Safari njema," akasema hivyo.
Sikumjibu lolote na kuamua tu kuufungua mlango, na kabla sijatoka, akaita jina langu. Nikamtazama.
"Be careful," akaniambia hivyo.
Kwa mara nyingine tena, akawa ameniambia maneno hayo yenye kutahadharisha sana, na kabla hata ya kusubiri kuelewa yalimaanishia nini kabisa nikaona nishuke tu na kusimama pembeni, kisha ndiyo yeye akaliwasha gari lake. Nikaanza tu kujiondokea hapo na kuelekea upande wa pili wa barabara, nikiliona gari la jamaa lilipoingia barabarani na kutokomea upande mwingine kutokea eneo hilo.
Nikiwa nasubiria tu usafiri, nikaitoa simu yangu na kukuta bado ikiwa inarekodi sauti, na yote ambayo nilikuwa nimeongea na jamaa iliyaingiza vyema kabisa. Kutokana na yote tuliyozungumzia, sikuona uhitaji wa kutunza rekodi hiyo, lakini katikati ya ile fikira ya "huwezi jua baadaye itakuwaje," nikaamua kuitunza tu kwa ajili ya lolote ambalo lingeihitaji mbeleni. Nilikuwa na mambo mengi sana ya kufikiria baada ya hizi ishu zote kutokea leo, nami nikapanda tu daladala ili niondoke maeneo hayo upesi.
★★
Niliamua kupanda daladala moja baada ya nyingine na kufika Mbagala ikiwa imekwishaingia saa kumi jioni, na mpaka wakati huu sikuwa nimeweka chochote kile tumboni. Hivyo nikaamua kwenda pale Zakhem mgahawani, na nilipapenda, nikaagiza msosi mzuri tu na kula taratibu, kisha shibe ilipokaa vizuri ndiyo nikaelekea kuchukua usafiri tena kwenda Mzinga.
Hali ya hewa kwa leo ilitulia zaidi, mvua haikunyesha japo kuna nyakati wingu lilikuwa linavizia hapa na kule, na nilipofika Mzinga kama kawaida nikatembea mdogo mdogo kuelekea kwa Ankia. Halafu niliona nipite upande usio wa duka lake ili nisihitajike kupita hapo na kumsalimia, maana nilitaka nikatulize tu mwili na akili kwanza. Kwa hiyo nimekuja kufika ndani kabisa ikiwa imeshaingia saa kumi na moja.
Nikafanya kupiga push-up kidogo na kwenda kuoga kwanza, kisha nikajiweka sawa kimwili tena na kuvaa nguo nyepesi, halafu nikaona nicheki jambo fulani. Zile pesa alizonipatia askari Ramadhan bado nilikuwa nazo, zikiwa kibunda, nami nikazotoa mfukoni na kuamua kuzihesabu. Yaani kwa jinsi zilivyokuwa zimebanwa na rubber band ungefikiri siyo nyingi sana, lakini nilipozifungua mpaka zikamwagika chini. Jumla ikawa ni milioni moja, nami nikahisi kuchoka tu na kuzishindilia kwenye kimfuko kidogo, kisha nikaziweka kwenye begi.
Nikatoka humo chumbani na kwenda kukaa sebuleni, nikiangalia kama kungekuwa na jambo fulani kwenye simu la kuweza kunisaidia kuhamisha akili, lakini nayo ikaboa tu. Nikaamua kuwasha TV, niangalie filamu yoyote ya kichina iliyorushwa Azam Kix, nami nikapata moja na kujilazimisha kuiangalia huku nikimsubiri mwenye nyumba wangu arejee.
Nikaendelea kukaa tu hapo hapo sofani nikiangalia TV ikiwa imeshapita saa kumi na mbili jioni kuelekea saa moja, na hata yaliyokuwa yanaonyeshwa filamuni hayakuingia akilini kabisa. Nilikuwa kama nimeganda yaani, akili yangu ikirudi kule kule ilikotoka kwa asubuhi hiyo mpaka kufikia wakati huu, na ndipo Ankia akawa amerejea hapa kwake hatimaye.
Alikuwa amejipendezea mwenyewe kwa kuvaa T-shirt mikono mifupi ya zambarau na suruali ya jeans iliyombana vyema, na sasa hivi alikuwa ameanza kunukia harufu fulani hivi mpya, nzuri, kitu ambacho kilionyesha mtoto alikuwa amebadilisha manukato ili awe mpya zaidi. Akiwa katika hali ya uchangamfu akanisalimia vizuri na kukaa nami sofani, naye alikuwa amekuja na mfuko wenye vyakula na mbogamboga kwa ajili ya usiku.
"Ffff... nina kazi ya upishi hapa, ila nimechoka! Naona uvivu kweli, lakini kula lazima, au siyo?" akawa ameniambia hivyo.
Nikatikisa kichwa kukubali huku nikitazama runinga tu.
"Vipi, umekula mchana?" akaniuliza hivyo.
Nikatikisa nyusi kukubali.
"Umekula nini?"
"Ugali, nyama."
"Nani amekupikia?"
"Ray C," nikamjibu kiutani.
"Umekutana naye wapi?" na yeye akaniuliza kiutani.
"Kwenye kamgahawa kake. Hujui ni mama'ntilie?"
"Ooh, ahahah... sawa. Alikuwa anakujazia-jazia na nyama eh..."
"Tena akanikomesha na pilipili..."
"Ahahahah... JC bwana..."
Nikaangalia tu TV na kutoa tabasamu la kujilazimisha.
"Ulikuwa umeenda Makumbusho tena? Leo umeondoka mapema, hatukuagana," akasema hivyo.
"Eeh... nilikuwa huko..."
"Hivi huwa unaenda kufanya nini huko JC?" akauliza.
Nikamwangalia usoni tu na kubaki kimya.
"Maana huu mwezi wote ulioisha, hutulii. Upo likizo ya kazi gani sasa kama unaondoka tu tena kwenda kujichosha? Ama umeoa huko yakhe? Tuambiane..." akasema hivyo.
"Kwo' kuwa likizoni ndo' imaanishe nikae tu ndani muda wote kama kobe?"
"Aa, tatizo unarudi mara nyingi na sura ya kinyoonge... ndo' maana nakuwa nashangaa. Mambo yako poa?"
Nikamwonyesha kidole gumba kama kukubali.
"Mhm... haya. Me ngoja nianda... eh, halafu subiri kwanza. Vipi suala lako na Miryam? Umeshaongea naye?" akaniuliza hivyo.
"Ah, we' nenda huko kapike bana..."
"Siendi mpaka uniambie..."
"Sikwambii sasa. Toka hapa," nikamfukuza kimasihara.
"Sitoki. Niambie JC," akasisitiza na kunishika shingoni.
"Ih, we' em' niachie bwana. Usianze bangi sa'hivi..."
Nikamwambia hivyo na kusimama kabisa, nikiashiria kutaka kwenda chumbani, naye akasimama pia na kunishika mkononi kwa nguvu.
"JC, acha kuogopa, niambie tu kama umeshamsemesha. Me rafiki yako, naweza nikakusaidia kwa hili au lile, kama bado hujamwambia, ukipenda naweza kukutengenezea mitambo. Maana yule ni mwanamke mwenzangu, namwelewa..." akaniambia hivyo kistaarabu.
Nikawa namtazama tu kwa utulivu, nami nikamwambia, "Huu moto wa kutaka sana kunisaidia, unautoa wapi?"
"Ahah... umekuja tu wenyewe. Nataka kukuona unafurahi... na ukimpata Miryam, najua na yeye atafurahi sana. Nitapenda kuwaona mnafurahi pamoja maana nawapenda nyote," akaniambia hivyo.
Nikatabasamu kiasi na kusema, "Yeah. Nimeshamwambia."
"Kweli?" akauliza hivyo kwa shauku.
Nikatikisa nyusi kukubali.
Alipotambua sikuwa na shauku kama yeye, akaweka uso makini na kuuliza, "Amekujibuje?"
"We' unafikiriaje?" nikamuuliza pia.
"Dah! Kakataa. Pole JC. Ila... usikate tamaa. Labda uendelee kumjaribu," akaniambia hivyo.
"Nani kasema nakata tamaa?" nikamuuliza hivyo.
Akatabasamu kiasi.
"Na siyo labda, ninataka kuendelea kum-please mpaka kieleweke Ankia. Sitaki kushindwa kabisa," nikamwambia.
"Hapo ndo' umeongea. Usiache. Atayeyuka tu," akanitia moyo.
"Unajua nini?"
"Nambie."
"Ninahisi kwamba Miryam ana hisia kwangu pia, lakini bado hajataka kukubali hilo kwa sababu ya mambo mengi yanayomchanganya," nikamwambia.
"Eti eh? Nini kinakufanya uhisi hivyo?" akaniuliza huku akitabasamu kiasi.
Nikageuka pembeni na kuanza kutembea taratibu kama naelekea chumbani, kisha nikasimama na kusema, "Moyo tu, Ankia. Kwa hizi wiki chache zilizopita nimejiachia sana kuamini na kufata kile moyo wangu unahisi... na siyo kwamba matokeo muda wote yanakuwa mazuri lakini nimeona kuwa siyo jambo baya kufuata moyo... kama nilivyokuwaga naogopa kufanya zamani. Moyo unaniambia kwamba Miryam ni wangu, na unanisukuma kufanya yote ambayo nitaweza ili kumleta karibu yangu. Ankia... nampenda sana Miryam. Yaani... mno..."
Ankia akawa amekuja mbele yangu na kuniangalia huku akitabasamu kwa furaha, naye akasema, "Unaongea kama vile unasoma script ya movie yaani. 'Nitafanya lolote kwa ajili yake, moyo wangu unaniambia ye' ni waaangu,' ahahah... hadi raha kukusikia unaongea namna hii. Kumbe mapenzi unayajua vizuri."
Nikatabasamu kiasi na kuangalia chini, nami nikamwambia, "Natamani tu angetambua haraka umuhimu wake kwangu... aniruhusu niingie moyoni mwake upesi ili nimpe upendo anaostahili. Changamoto zote anazopitia, naziona... natamani tu yaani aniruhusu...."
Kabla sijamaliza kuzungumza, nikaona Ankia anashtuka kiasi machoni huku akitazama kuelekea upande wa mlangoni nyuma yangu, nami nikaingiwa na msisimko kwa kuhisi kulikuwa na mtu mwingine ameingia hapo. Nikageuka upesi na kukuta ndiyo, kulikuwa na mtu ameingia hapo, na haikuwa mwingine ila kijana Tesha mwenyewe!
Alikuwa amesimama mlangoni, akituangalia mimi na Ankia kwa umakini sana, nami nikageuka vizuri zaidi na kumtazama usoni kwa utulivu makini. Alisimama kwenye uwazi mdogo uliokuwa umeachwa baada ya Ankia kufika na kuingia bila kufunga mlango, kwa hiyo nikaelewa wazi kwamba kijana angekuwa amesikia niliyokuwa namwambia Ankia.
"Eh, Tesha! Jamani, si ungepiga hata hodi, umenishtua," Ankia akamwambia hivyo kwa sauti ya chini.
Lakini Tesha akaendelea tu kuniangalia kimkazo kiasi, naye Ankia akanitazama usoni kwa wasiwasi. Jamaa akaanza kuja mpaka kufikia sehemu tuliyosimama na kutulia mbele yangu, akiniangalia kwa utafakari mwingi, nami nikaendelea kujipa utulivu pia nikisubiri kusikia ambacho angesema. Sijui angechukuliaje hilo suala yaani!
Tesha akasema, "JC uko sawa kweli? Kuna... hakuna tatizo lolote linalokusumbua?"
Nikabaki kimya tu huku nikimtazama kwa umakini.
"Tesha, ona... labda tukae ili tuongee vizuri eh..." Ankia akamwambia hivyo.
"Kwamba tukikaa ndiyo nitasikia vizuri zaidi ya tukisimama, au? Ni swali simple tu, anaweza kujibu hata akiwa amesimama..." Tesha akasema hivyo.
Nikaendelea tu kumwangalia usoni kwa utulivu. Alionekana kukerwa.
"Kaka, nimesikia yote uliyosema. Siyo yote, yaani... ndiyo nimefika hapo mlangoni nikasikia uliyosema kuhusu Miryam. Ni kweli?" Tesha akaniuliza hivyo.
Ankia akanitazama usoni kwa subira, nami nikamtikisia kichwa Tesha kumpa 'ndiyo' ya swali lake.
"Ahah... JC bana! Uko serious kabisa?" Tesha akaniuliza hivyo kwa kutoamini.
Nikaangalia pembeni tu.
"Tesha, hili ni jambo serious ndiyo. JC anampenda Miryam. Siyo masihara," Ankia akasema hivyo.
"Na wewe ndiyo mwenye uhakika? Wewe Ankia?" Tesha akamsemesha hivyo.
Ankia akamwambia, "Nani sasa mwingine awe na uhakika kama siyo mimi? We' si ndiyo umejua leo? Me naishi naye hapa, ni rafiki yake, najua..."
"Eti rafiki yake! JC, umemlisha nini huyu mpaka akaamini hii kitu bro? Ndo' anakupa support ili uje kumzuzua na dada yangu, halafu ukishamla, na yeye umgeuze rafiki yako," Tesha akasema hivyo.
Nikamwangalia kimkazo na kumsogelea karibu zaidi kwa hasira, naye akarudi nyuma kidogo kwa kushtushwa na hilo.
"JC..." Ankia akaniita kwa sauti ya chini huku akiziba mdomo kwa viganja vyake.
Nikajizuia zaidi kupandisha hasira na kujituliza kihisia, nami nikatazama pembeni na kushusha pumzi.
Tesha, akiwa ananiangalia kwa njia ya kutatizika, akaniambia, "Uko serious."
Nikamwangalia usoni kwa hisia.
"Da' Mimi anajua?" Tesha akaniuliza hivyo.
Nikatikisa kichwa kukubali.
"Ameshamwambia," Ankia akasema hivyo pia.
"Amesemaje?" Tesha akaniuliza.
"Amekataa," nikamwambia hivyo.
"Ahah... ulitegemea Miryam akukubali? JC... huko ni mbali sana umeenda mwanangu. Yaani... bado siamini yaani kama unaweza kumfikiria Miryam hivyo," Tesha akaniambia.
"Ninampenda dada yako Tesha kwa sababu ni kitu ninachohisi, siyo kufikiria," nikamwambia.
"Kumbe ndiyo maana ulikuwa na hasira sana siku ile alipopigwa na yule fala..." Tesha akasema hivyo.
Nikaangalia pembeni tu.
Tesha akanisogelea na kuuliza, "JC unajua Miryam ana miaka mingapi?"
"Kwani miaka ndiyo inazuia mtu kumpenda mtu, Tesha?" Ankia akamuuliza.
"Ankia subiri kwanza. JC nijibu. Unajua miaka yake?" Tesha akasema hivyo.
"Ndiyo," nikamjibu.
"Ana miaka mingapi?" akaniuliza.
"Thelathini na tano," nikamjibu.
"Okay, thelathini na tano. Thelathini na tano JC, ananizidi me miaka kumi, wewe sijui... nane? Na unasema unampenda ile... kwamba imetoka moyoni, unataka awe wako wa moyo, si ndiyo? Hapo tu, yaani hapo tu kwenye umri hata wewe unajua Miryam atakuona kama mtoto unayemfanyia mchezo, ukienda kumfata sijui kumwambia mambo gani... kweli una uhakika una... unaelewa unacho...."
"Ndiyo, Tesha!" nikamkatisha kwa uhakika.
Akatulia na kuendelea kunitazama kwa umakini.
"Nampenda Miryam. Yote niliyokwambia ufanye kwa Happy ile juzi, ndiyo mimi nayotaka kufanya kwa dada yako... na hata zaidi ya hapo. Nafikiri umenielewa," nikamwambia hivyo kistaarabu.
Tesha akaonekana kutathmini maneno yangu na hata kumwangalia Ankia, ambaye naye akamwonyesha ishara kwa macho kuwa sikutania kwelikweli, ndiyo akasema, "Mh! Aisee bro, sikuwa nimetegemea. Hii kali zaidi ya kali niliyokuwa nimeileta."
Nikaangalia pembeni tu.
"Kali gani nyingine?" Ankia akamuuliza.
"Nimeambiwa Chalii Gonga amekufa bwana," Tesha akasema hivyo.
Nikamwangalia usoni.
"Wewee! Lini?" Ankia akamuuliza hivyo.
"Sijajua. Yaani moja juu ya lingine, Chalii amekufa, na sasa hivi nimesikia yule mke wake amekamatwa. Sijui amehusika na hayo mauaji?" Tesha akasema hivyo.
"Mauaji? Kumbe Chalii ameuliwa? Yaani... huyo Bertha ndiyo amemuua mume wake?!" Ankia akashangaa.
"Ndiyo navyosikia, sina uhakika. Kulikuwa na bonge la msako leo huko mbele Kariakoo, Sinza, Mbezi, Kinondo, wapi, yaani... mapolisi walikuwa wanazunguka mno leo. Wamewakamata wengi! Ishu inaonekana ni za mambo kama madawa ya kulevya, hawa madada poa sijui na mashoga, wameunganisha yote mpaka kwenye madangulo yao huko, na huyo mke wake Chalii... amekamatwa..." Tesha akasema.
"Umeyasikia wapi?" Ankia akamuuliza.
"Bobo kaniambia. Habari ya jiji zima sa'hivi. Usiangalie tamthilia leo, angalia habari," Tesha akasema hivyo.
"Mh! Haki ya Mungu. Kama Chalii amekufa na Bertha kakamatwa, nani atasimamia Masai sasa? Hesabu si ni zao?" Ankia akauliza hivyo.
"Watajua tu. Nitamuuliza tena Bobo," Tesha akasema.
"Eeh, kweli ngoja na me nimuulize," Ankia akasema.
Nilikuwa nimetulia tu utafikiri sikujua kuhusu hayo mambo, maana ni mada ya muda mfupi nyuma ndiyo hasa iliyokuwa ikizunguka kichwani kwangu.
"Si ulikuwa huko leo kaka?" Umeona vurugu-vurugu?" Tesha akaniuliza.
"Eeh, nimeona," nikamjibu hivyo kifupi tu.
"Oy, kaka... hii ishu ya da' Mimi, we' jua tu kwamba me niko peace. Sawa? Nilikuona chizi mwanzoni, na... bado nakuona kama chizi, ila... fanya unavyoona kuwa sawa. We' ni mtu mzima. Ukitaka kuendelea kumtongoza, mjaribu. Akiendelea kugoma... usifosi. Unamwacha tu. Maana akiwaga hataki kitu, ndo' hataki. Kama tu kwa yule jamaa mwingine. Hivyo yaani," Tesha akanipa ushauri.
Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa.
Akanisogelea na kunishika begani, naye akasema, "Sikia JC. We ni blood. Nakukubali kinoma. Tumesaidiana kwa vingi na kufanya ujinga mwingi, ila kwa hili najua uko serious. Lifanye serious kweli. Nampenda dada yangu. Kama kweli na we' unatafuta kutulia halafu umempenda Miryam, basi fight. Huwezi jua. Akikukubali mwishowe, mambo yanaweza yakawa mazuri zaidi. Unaweza ukaoa kwetu kabisa."
Akanifanya nitabasamu kwa kufarijika, naye akatabasamu pia.
"Ahahah... itakuwa poa sana. Tesha, ila usije kumwambia mtu mwingine kabisa kuhusu hii, eti? Hata dada yako usimwambie kama unajua," Ankia akasema hivyo.
"Dah, Ankia anaku-support! Ahah... usijali mama, naelewa. Sitamwambia mtu yeyote," Tesha akasema hivyo.
Nikamwangalia usoni na kusema, "Asante Tesha. Kwa kuwa mwelewa. Samahani pia, nilikasirika mpaka..."
"Nini, ukataka kunipiga ngumi? Tungeziruka hapa hapa, we! Najua taekwando," akasema hivyo kimasihara.
"Unaniacha wapi? Ni meza na TV za Ankia ndo' zingeumia," nikamwambia hivyo kiutani.
"Ahahah... tungevuruga sebule nzima, halafu tungemwacha aisafishe, sisi haooo... Masai," Tesha akasema hivyo.
"Nyooo... thubutu!" Ankia akamwambia hivyo.
Sote kwa pamoja tukacheka kidogo kwa furaha, nami pamoja na Tesha tukaunganisha viganja vyetu hewani na kuvutana, tukikumbatiana kwa bega kishkaji na kisha kuachiana tena.
Tesha akanipiga kiasi begani na kusema, "Komaa kaka. Nenda kwa akili tu, Mimi anaweza akakupa chance. Ila, itakuwa kwa msoto."
Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa.
"Yupo nyumbani tayari?" Ankia akamuuliza.
"Yupo eeh. Si utakuja baadaye JC?" Tesha akauliza.
"Yeah, nitakuja kusalimia," nikamwambia.
"Fresh, uje. Nilikuwa naenda kuchukua na Magnesium kwanza hapo dukani, tumbo linajaa migesi tu, kujamba sijambi. Ndo' nikaona nipite..." Tesha akasema hivyo.
"He! Wewe, em' toka hapa usije kunichafulia hali ya hewa ndani kwangu. Nenda huko!" Ankia akamwambia hivyo kiukali wa kimasihara.
"Aaa, tulia basi niachie hapa hata kimoja tu," Tesha akasema hivyo kiutani.
Ankia akasonya na kusema, "Shenzi, em' nenda kajambie huko!"
Akaanza na kumsukuma kabisa ili aondoke, naye Tesha akacheka na kunionyesha ishara ya kwa heri.
Nikabaki tu hapo nikiwa natabasamu baada ya kujisikia faraja kutokana na kuungwa mkono na Tesha pia katika ishu yangu ya kumpenda Miryam, na baada ya jamaa kuondoka, Ankia akanigeukia na kuachia tabasamu la ushindi eti, nami nikatabasamu pia na kuamua kuelekea tu chumbani kwangu. Angalau nikawa nimepunguza stress kidogo baada ya Tesha kuniunga mkono pia.
★★
Saa moja haikukawia kuingia, na mimi nilikuwa chumbani tu nikiwa nimetumia muda mfupi kuiweka akili yangu sawa juu ya mambo ambayo yangefuata baada ya visa vyangu pamoja na madam Bertha kuwa vimefikia ukomo wake. Kwa sasa umakini wangu wote ungetakiwa kuwa kwa Miryam, nifanye kila niwezalo kuhakikisha anakiri kuwa na hisia za kimapenzi kwangu, hata kama ingenihitaji kumroga ningefanya hivyo. Siyo kuroga kwa waganga, kuroga kwa mapenzi. Angeelewa tu!
Ikiwa inakimbilia kuingia saa mbili, nikaamua kutoka kwa Ankia ili nikaisalimu familia ya bibie Miryam hapo kwake, na kwa wakati huu Ankia alikuwa ameshaanza kupika zake wali na nyama. Nikamwacha tu na kwenda hapo kwa marafiki zetu, na kama ilivyokuwa jana, nikawakuta wanafamilia hao wakiwa wamekaa nje kwenye uvaranda wao ili kula upepo kidogo, wote wakiwepo isipokuwa Miryam na Shadya tu, na Shadya hakuwepo kabisa hapa kwa siku hii.
Nikasalimiana na mama wakubwa vizuri, Mariam akiwa amenisalimia pia na kuendelea kuwa bize na simu yake Tesha, na jamaa pia alikuwa hapo akipiga story na mama zao. Mariam alionekana kuwa makini sana kwenye kile alichofanya kwenye simu ya kaka yake, nami nikatambua kuwa alicheza game. Kwa sababu lilikuwa game la kuchangamsha ubongo kwa kupangilia maneno, lilifaa sana hali yake ya kutakiwa kuendelea kuimarisha uwezo wake wa kufikiri, na kwa hilo nikawa nimempa kongole Tesha kulifanya kwa niaba yangu.
Bi Zawadi akamwambia Tesha, "Mfatie mwenzako kiti."
"Ah, hamna shida, ngoja nikafate mwenyewe. Nataka kumsalimia na Miryam. Si yupo ndani?" nikasema hivyo.
"Eee, yupo jikoni anapika. Mhm... tunategea kama kawaida ili atushushie msosi wa maana," Bi Jamila akasema hivyo kama vile ananinong'oneza.
Nikatabasamu kiasi kumwambia, "Sawa. Nakuja."
"Haya," mama wakubwa wakaitikia hivyo kwa pamoja.
Nikaangaliana na Tesha kwa ufupi, ambaye akanitikisia nyusi kama kunipa ishara ya 'nenda,' akinipa kichwa kwenda kumwona dada yake ili nikajaribu kuweka mitambo sawa. Nikamtikisia kichwa pia na kuingia tu huko ndani, nami taratibu nikaelekea mpaka upande wa jikoni na kusimama pale pale ambapo nilisimama pamoja na mwanamke huyo jana alipotaka kunilazimisha nichukue pesa zake, na hapo nikawa nimemwona humo jikoni.
Miryam alisimama usawa wa kaunta la jikoni mwanzoni, pembeni yake likiwepo jiko lao lililowekewa sufuria lililofunikwa na kuonyesha kuchemsha chakula fulani. Kwa mtazamo wa haraka alikuwa akipika ndizi na samaki, na hapo aliposimama ndiyo alikuwa akikatakata viungo kwa ajili ya kuchanganyia pamoja na ndizi zikishachemka vya kutosha. Alikuwa amevaa T-shirt la mikono mifupi lenye rangi mbalimbali pamoja na khanga iliyomsitiri vyema kutokea kiunoni, na nywele zake alizifunika kwa kinguo-kofia cha satini.
Nikaendelea kusimama hapo hapo tu na kumwangalia. Nilifurahi sana moyoni kumwona. Na najua tayari alikuwa ameshatambua uwepo wangu sehemu hiyo, lakini hakugeuka kuniangalia hata mara moja. Nikatabasamu kiasi baada ya kukumbuka nilivyomtania kidogo jana kwa kusema kofi la mpenzi haliumi, na mpaka sasa bado alionekana kuwa tayari kunilabua kofi kabisa kisawasawa kama ningemfanyia mchezo.
Nikajisogeza tu mpaka karibu kabisa na mwingilio wa humo jikoni, pakiwa na mwonekano safi na vyombo vilivyopangiliwa vyema kwenye makabati ya ukutani, nami nikaegamia ukuta usawa wa sehemu aliyokuwa amesimama, na hakuniangalia hata mara moja kwa kukazana kukatakata karoti.
"Za leo Miryam?" nikamsalimia.
Akabaki kimya tu kama vile hajanisikia.
"Umepata habari kuhusu yaliyotokea leo?" nikamuuliza.
Kimya.
"Utakuwa umesikia. Maaskari waliyoyafanya jijini leo kuwakamata watu wengi kwenye biashara haramu na nini... hiyo ndiyo ilikuwa mishe yangu. Wale niliokuwa nakwambia... wamekamatwa leo. Si unaona? Nimefanikiwa kama nilivyosema," nikamwambia hivyo.
Akaendelea tu na kazi yake kwa kuonyesha hajali.
"Oh, usiwe grumpy namna hii Miryam, nimekuja tu kukusalimia," nikamwambia hivyo kwa upole.
Akaendelea kubunda tu, na akikatakata viungo kama vile ana kisirani.
Nikatabasamu kiasi na kuangalia chini, nami nikasema, "Najua una sababu nzuri ya kunichunia, lakini haifai bwana. Me bado rafiki yako, na ni daktari wa Mamu. Unajua tutapaswa kuongea tu."
Nikiwa nimemwangalia sasa, akaacha kukatakata karoti na kufunua sufuria la ndizi kwa kasi, halafu mfuniko akauelekeza kwangu kwa makusudi huku akijifanya kuchungulia ndizi zake kwa umakini, na mvuke ukawa umenifikia usoni. Nikatabasamu kiasi na kusogea nyuma kidogo, naye ndiyo akalifunika na kurudi kukatakata vitu vyake.
Nikaegamia ukuta tena na kumwambia, "Usiwe hivyo. Kuna kitu nahitaji kukuomba... uniruhusu nifanye."
Kakabaki kimya tu na kuanza kupalanganisha vyombo huku na huko.
"Kesho baada ya birthday, namaanisha, kesho-kutwa... nilikuwa nataka kwenda kumwona mama mara moja kule nyumbani. Ikiwa itakuwa sawa kwako, naomba niende na Mamu," nikamwambia hivyo kistaarabu.
Akawa akiendelea kukatakata, nyanya wakati huu, ikiwa kama vile hakujali nilichotoka kusema.
"Ni... mama ndiyo ameomba niende naye. Angependa kumwona Mariam," nikamwambia hivyo kwa upole.
Miryam akasitisha kukatakata nyanya na kuleta macho yake taratibu upande wangu, lakini hakuniangalia usoni. Hapo nikawa nimevuta umakini wake, najua alijiuliza mama yangu alitaka kumwona mdogo wake kwa nini.
Nikasema, "Niliwahi kumzungumzia Mariam kwa mama yangu, na alipenda... alitamani aje kumwona maana, mama yangu ana-relate na shida kama zilizompata Mamu. Anataka tu kuona progress yake maana amempenda hata kabla hajakutana naye..."
Miryam akarudisha umakini wake kwenye ukataji mboga bila kunipa itikio lolote.
"Nikwambie kitu? Hizi siku chache zilizopita, tokea yule jamaa alipotukuta kule Jogoo na kutishia kukuumiza mbele yangu... yaani mambo yameenda faster like crazy. Kila kitu juu ya hiki na hiki, imekuwa overwhelming. Nimeponyoka kifo karibia mara tatu Miryam, hata leo... ilikuwa karibu nife..." nikamwambia hivyo.
Akaendelea tu kufanya kazi yake kama hajali.
"Kuna... hisia fulani ndani yangu ilikuwa inanifanya nisihofie kufa kwa kufikiri labda mwisho wangu tu ndo' umefika... lakini baada ya kuipata hii nafasi ya kuendelea kupumua, mpaka sasa niko hapa tena... nimegundua huo mwisho bado sana. Bado ninatakiwa kuwa na wapendwa wangu, kufanya mengi kwa ajili ya wote naowapenda, nyie wote... hasa wewe Miryam..." nikamwambia hivyo kwa hisia.
Akasitisha tena kukatakata nyanya ambazo tayari zilikuwa zimeshakatwa mpaka zikachoka, naye akaonekana kuweka umakini kwangu zaidi.
"Kwa nini? Unawaza kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu ndiyo kwanza safari yangu pamoja nawe imeanza, Miryam... na hii nafasi ya kuendelea kuishi niliyoipata ndiyo itakuwa msingi mzuri sana kwangu kuhakikisha naufikia mwisho wa hiyo safari pamoja nawe... no matter what. Baada ya kila kitu kilichotokea leo... sitaki kingine tena zaidi ya jambo hilo. Yaani... haitapita siku yoyote kutokea hapa ambayo sitakukumbusha namna navyokupenda, uwe tayari kupokea hilo ama usiwe tayari, ndiyo purpose yangu kutokea hapa Miryam. Na sitaacha... sitaacha mpaka nihakikishe uko tayari kuufungua moyo wako kwangu..." nikamwambia hivyo kwa hisia sana.
Miryam akapandisha macho yake mazuri hatimaye na kunitazama usoni kwa umakini sana, akionekana kuitikia maneno hayo kwa mtazamo wa aina fulani tofauti kutokana na jinsi ambavyo niliyasema bila utani, nami pia nikaendelea kumwangalia kwa hisia.
Macho yake bado yalikuwa yamejaa mashaka makubwa kunielekea, labda akidhani kwamba bado nilikuwa najitafutia tu faida za kizembe au kucheza na hisia zake, lakini muda siyo mrefu nilitaka kumthibitishia kwamba alikuwa amekosea. Nilimaanisha kila neno nililomwambia, na ningehakikisha kweli anakuja kuliona hilo na kutokuwa na jinsi tena ila kuniruhusu nimfanye awe wangu. Yaani hilo ndiyo lilikuwa limebaki. Kama nilivyosema, angeelewa tu!
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Full Story WhatsApp or inbox
Whatsapp +255 678 017 280