Simulizi: Mimi na Mimi

Simulizi: Mimi na Mimi

MIMI NA MIMI 3

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA KWANZA

★★★★★★★★★★★★★★



Furaha kwenye mapenzi ya kweli ni kitu kisichokosa changamoto sikuzote. Walio na furaha kwenye mahusiano yao hawaipati ndani ya siku moja tu na kuidumisha bila kupitia magumu ambayo huja kwa nyuso tofauti-tofauti. Ndiyo ilivyo na kwangu pia. Baada ya kusota kuitafuta furaha ya kweli katika mapenzi, nikaipata, lakini changamoto yenye kutikisa azimio la kuiendeleza furaha hiyo haikuchelewa kutuandama mimi na mwanamke niliyekuwa nimetokea kumpenda sana. Miryam. Mimi wangu. Oh, kuna visa na visasili vingi vilivyokuwa vimetokea hapo katikati tangu nimekutana na huyu mwanamke hadi kufikia wakati nilipompeleka yeye na familia yake kuwatambulisha kwetu, lakini kilichotokea siku hiyo ndiyo kilifunika visa vyote kabisa. Yaani nje ya matarajio yangu na ya wote waliokuwa wakituunga mkono mimi na bibie ili tuweze kufunga ndoa, ikagundulika kwamba tuna uhusiano wa karibu sana wa kifamilia. Iliumiza mno.

Katika hali ya kushtukizwa na jambo hilo, akili zetu hazikufanya kazi upesi kubaini ilikuwaje mpaka jambo hilo kuwezekana, kwa sababu ni hisia za huzuni na hatia ya ghafla zilizotuingia mimi na Miryam kiasi kwamba tukajikuta tunashindwa kusema wala kufanya lolote ambalo lingebadili ukweli wa suala hilo zaidi ya kulia tu. Mama yangu na Bi Jamila walifahamiana, baba yangu mzazi ambaye sikuwahi kumjua akiwa ni mtoto wa mdogo wake na mwanamke huyo, na chanzo cha kutengana wazazi wangu inaonekana kilisababishwa na watu wa familia yake Bi Jamila; kutia ndani yeye pia. Hivyo, nilikuwa na ukaribu sana na Miryam ulioelekea kuzigusa damu zetu kiukoo, na kiukweli hii ilikuwa ni changamoto mbaya sana kwetu mimi na mpenzi wangu.

Miryam alilia hapo ndani, akiwa chini, mimi pia nikipiga magoti na kumwangalia kwa simanzi, baada ya mama kutupasulia ukweli huo siku ambayo nilidhani ingekuwa sehemu ya mwendelezo wa furaha zaidi katika maisha yangu. Tesha na Shadya wakajaribu kumshika ili kumsaidia anyanyuke na kumpatia faraja, lakini hakutaka kabisa aguswe. Hata mzee wangu, Frank Manyanza, akajaribu kutuliza hali kwa ustaarabu, akimsihi Miryam ajikaze ili tuchanganue nini la kufanya kutokea hapo, na mwanamke huyu akajifuta tu machozi na kusimama kana kwamba alikuwa ameyatilia maanani maneno ya mzee wangu kwa uchanya. Lakini hapo alikuwa ndiyo amesimama ili aondoke. Aondoke kabisa. Miryam akageuka tu na kuanza kuelekea mlangoni, akiniacha namwangalia kwa huzuni sana. Tesha akawa ananiambia ninyanyuke na kumfata dada yake, lakini kihalisi ni kwamba alitaka ninyanyuke na kumfata "dada yetu." Ah! Hamu iliniishia kabisa. Yaani pozi lote lilitoweka mpaka nikashindwa kumtii.

Miryam akatoka ndani ya nyumba yetu, huku Bi Zawadi na Mariam wakimfuata kwa nyuma, nami nikamsikia mzee anamwambia Tesha na Shadya waende pamoja na ndugu zao pia kuhakikisha wanafika nyumbani salama, ili tuje kupanga muda mwingine unaofaa kuzungumza pamoja kwa mapana. Wakakubaliana na hilo na kuondoka pia, Tesha akiwa ameniambia angenipigia baadaye. Nilihuzunika sana. Yaani niliendelea kukaa chini utadhani nilikuwa nimepoteza matumaini yote kabisa, na ni Nuru mdogo wangu ndiye akaja kunikumbatia hapo hapo huku akilia pamoja nami kwa huzuni. Sikujihisi amani tena hata pale mzee alipoanza kunisemesha kwa njia ya faraja, lakini sehemu kubwa ndani ya moyo wangu haikutaka kukubaliana na hili kizembe tu. Nilihitaji kuujua ukweli wote wa mambo ambayo mama alikuwa ameyasema, kwa sababu kiukweli mimi na Miryam tulikuwa tumefika mbali sana kurudishwa nyuma tena; hata kwa jambo kama hili. Nikajipa uimara na kusimama, Nuru akiwa karibu yangu, nami nikamgeukia mama kukuta ameshikiliwa na mzee kupatiwa faraja. Bado alilia kwa kwikwi za chini, akinitazama kwa huzuni na huruma, nami nikamsogelea na kumshika mkono.

Nikamwambia, "Mama... naomba unieleze kila kitu."

Aliniangalia kwa masikitiko mengi, naye akatikisa kichwa kukubali na bila kusema lolote kuanza kuelekea ngazini. Ilikuwa ni picha mbaya sana imechoreka hapo sebuleni, yaani moyo wangu haukuamini kama kweli haya yote yalikuwa yametokea, lakini huu ndiyo ungekuwa muda wa kwenda kupata majibu ya ni kwa nini yalitokea. Mimi na mzee tukafuata baada ya mama kuongoza kuelekea chumbani, chumbani kwao, na Nuru akabaki huko sebuleni pamoja na rafiki yake aliyekuja kutembelea na wasaidizi wote wa kazi. Sisi watatu tukaingia humo ndani, mama akikaa kitandani na mzee akienda kukaa karibu naye pia, huku mimi nikisimama pembeni na kumwangalia mzazi wangu huyu aliyekuwa na mambo mengi aliyohitaji kunifunulia. Mama alionekana kuwa na huzuni mno, angenitazama akionekana kutaka kuongea, lakini angeshindwa na kurudisha uso wake chini huku machozi yakimtoka.

Mzee akamwambia, "Leah, jikaze."

Mama akasafisha pua na kusema, "Yaani, eh... sijui tu hata nisemeje jamani..."

Nilikuwa nikimwangalia kwa umakini tu, naye akanitazama usoni kwa huzuni.

"Jayden..." mama akatamka jina langu kwa hisia.

"Naam..." nikaitika.

"Mwanangu najua umeumia sana... kwa... kwa sababu ya hili... yaani... nakosa hata... eh... mengi nayotaka kusema inabidi na Jasmine ayasikie, dada yako pia hajui kuhusu haya. Itakuwa bora...."

"Mama, please... tafadhali niambie tu. Nielezee hayo yote yanamaanisha nini maana kiukweli nahisi sitoweza kusubiri zaidi," nikaongea upesi.

"J, tuliza hisia. Tunajua una...."

"Mzee, acha tu mama ndiyo aongee tafadhali," nikamkatisha.

Wote wakabaki kunitazama tu.

"Mama... nini kilitokea? Huyo... huyo Tino unayemsemea ndiyo nani?" nikamuuliza.

Mama akafumba macho na kutikisa kichwa kwa masikitiko.

"Iweje uwe unajuana na Bi Jamila? Nini kilitokea mama?" nikauliza kwa mkazo.

"Nataka nikueleze kila kitu Jayden, lakini ni muhimu Jasmine awepo pia mwanangu..." mama akasema hivyo.

"Nimpigie?" nikamuuliza.

"Jayden, hebu ji-control basi. Unajua dada yako yuko kwenye hali gani sasa hivi," mzee akaniambia.

"Precisely. Mama... acha kuhofia. Hauna... ahh... najua ulipitia mengi magumu, ndiyo maana nakuomba uniambie, kwa sababu sasa hivi yamekuja kunirudia na mie mwanao... ninaweza kupitia magumu hata zaidi usiponieleza. Mama please," nikazungumza kistaarabu zaidi.

Mama akajikaza zaidi, naye akaanza kuuliza, "Unakumbuka nini kuhusu baba yako Jayden?"

"Kwamba yeye ni mjingammoja aliyetutelekeza sisi watatu," nikamjibu.

"Naelewa umekua ukichukia kila kitu kuhusu baba yako J, ila kusema kweli... haikuwa kwa asilimia zote kwamba... kwamba ni makosa yake... kuwatelekeza," akasema hivyo.

"Ila?" nikamuuliza.

"Familia yake ndiyo haikutaka anioe, kwa hiyo wao walifanya mipango kututenganisha," akaniambia hivyo.

Nikaendelea kumwangalia tu kwa utulivu.

"Mama yake Tino, pamoja na huyo mama mkubwa wake Miryam, na ndugu zao wengine ndiyo walitutenganisha. Kipindi hicho Tino alikuwa anafanya kazi za kusambaza magazeti kutoka kwenye makampuni, alikuwa... alikuwa anayatoa mkoa mpaka mkoa, kwa hiyo tulikuwa tunaonana mara chache sana kwa mwezi. Kipindi fulani amesafirisha magazeti, nilikuja tu kushangaa harudi huko kwetu tena... na nilipomtafuta sikuweza kumpata. Sijui walifanyaje tu, ila walihakikisha simpati tena kabisa, halafu wakaja kuniambia na kunionyesha picha za harusi yake na mwanamke mwingine..." mama akaongea kwa huzuni.

Nikamtazama kwa hisia za huruma.

"Mwanzo... walikuwa wamefanya ionekane kama Tino ameniacha kwa makusudi kabisa na kuoa mwanamke mwenye hela... lakini nafikiri walitumia dawa kumgeuza ili...."

"Akusahau?" mzee akamuuliza.

"Labda, kwa kweli sijui, maana... Tino aliwapenda sana watoto wangu. Alimpenda Jasmine... alikuwaga anaongea sana kuhusu kuja kukupeleka ukatahiriwe Jayden, ahah... awaonyeshe watu amepata kidume eti... lakini ghafla tu... sikuja kumpata tena..." mama akaongea hivyo.

"Kwa hiyo mama ukaona ni bora kutuambia kwamba baba yetu alitutelekeza wakati ulijua haikuwa hivyo?" nikamuuliza.

"Sikujua, Jayden. Nimekwambia mwanzoni nilimtafuta bila kumpata, sikujali hata ndugu zake na marafiki zake wameniambia nini, nilijaribu kumtafuta na sikumpata tena. Nikiwa nimeachwa na watoto wawili wadogo, mimi yatima, na matatizo ya.... unafikiri ningehisije, eh? Ilifikia hatua nilifikiri hayo yote kuwa kweli, na nikawalea nyie kwa nguvu zangu pekee bila msaada wake... hata kama ni ndugu zake ndiyo walimroga ama nini, lakini hakuwepo kwenye maisha yenu. Ninakosea kusema kwamba aliwatelekeza?" mama akaongea kwa hisia.

Nikaangalie chini kwa huzuni.

"Wewe na Jas mnajua vyema ni magumu gani nimepitia, na ninamshukuru Mungu na watu ambao walinionyesha rehema kunisaidia nisonge mbele licha ya hayo. Yule mwanaume alikuwa mzuri kwangu, kwa hiyo aliponiacha niliteseka. Lakini nilikuja kujifunza kusonga mbele bila yeye kwa sababu yenu. Nyie ndiyo mlibaki kunipa nguvu hata ndani ya udhaifu niliokuwa nao. Jayden..."

Nikamwangalia machoni.

"Nisingefikiria, yaani never... kwamba ningekutana tena na huyo mwanamke. Ame... Frank, mmemsikia yeye mwenyewe ananiambia eti nimsamehe kwa yaliyotokea... eh? Ni mmoja wa ndugu zake Tino ambao walijua kabisa kwamba amezaa watoto wawili na mimi, lakini wakamrubuni aniache... akaoe mwanamke mwenye hela sijui... iwe kama wewe na Jas hamna thamani kwa sababu tu mlizaliwa na mwanamke mwenye maisha ya hali ya chini, kama hivyo yaani. Ningehisije Jayden, eh? Hata kama ningekuja kuambiwa baadaye kwamba Tino alirubuniwa tu, unadhani hiyo ingefunika maumivu yote yaliyoachwa kwangu... niyapitie mwenyewe? Lakini si wewe huyo hapo leo? Jasmine si yupo kule? Bado ni mimi ndiyo mwenye makosa? Labda kweli ni makosa yangu..." mama akaongea kwa huzuni.

"Hapana mama..." nikaongea kwa hisia.

"Hamna mtu anayehisi wewe ndiye mwenye makosa Leah, usiongee hivyo..." mzee akajaribu kumtuliza.

Mama akawa anajifuta machozi.

Nikatoka nilipokuwa nimesimama na kumsogelea mama karibu, nami nikakaa chini karibu na miguu yake huku nikimshika kiganja. Akakikaza changu pia.

Nikamwambia, "Samahani mama, sijamaanisha niliyosema. Ninajua. Ninakuelewa vizuri."

Akasema, "Hata me nakuelewa vizuri Jayden. Najua umeumia. Sielewi mengi, lakini nimeumizwa pia kujua kwamba wewe na Miryam mna undugu. Siyo jambo nililokuwa nadhani lingetokea, hata kidogo."

Nikaangalia chini kwa huzuni.

Mzee akasema, "Leah, ikiwa Tino alianza kuwa na wewe kabla hajaoa mwanamke mwingine, inaweza vipi Miryam awe mkubwa kwa Jayden?"

Swali lake nilikuwa nimeshalitafakari pia, lakini uwezekano ukiwa ni mwingi bado halikuwa suala la kuwazua sana. Nikaendelea kutazama pembeni tu.

Mama akasema, "Sijajua Frank. Labda..."

"Labda Miryam siyo mtoto wa Tino. Anaweza akawa alimwoa huyo mwanamke mwingine tayari Miryam akiwa naye, ndiyo hawa wadogo wakafata," mzee akasema.

"Hapana... sidhani. Sikumzaa Jasmine na Jayden kwa kuachana sana lakini ndani ya hicho kipindi bado Tino alikuwa nami hadi Jas ana miaka miwili na J ameanza kutambaa. Na hata kama ingekuwa hivyo, bado kuna kaka yao mwingine mkubwa ambaye yuko jela sasa, si ndiyo? Angekuwa amezaliwa kipindi gani?" mama akauliza.

"Au labda na mwanaume gani?" mzee akadokeza.

"Kwamba labda hao watoto wengine wana baba tofauti kabisa na wanangu?" mama naye akauliza.

"Huwezi jua..." mzee akasema.

Mama akasema, "Uwezekano ni finyu sana, si umeona jinsi ambavyo hao watoto wote wanamtambua Tino kuwa baba yao? Wanamwita...."

"Constantino," mzee akajibu.

"Eeh, wote wanamjua kuwa baba yao. Umeona reaction ya Miryam alipogundua...." mama akaishia tu hapo.

Nilibaki kimya tu, na majadiliano yao yalikuwa yanaiongezea akili yangu kitete zaidi, nami nikaona nivunje ukimya na kusema, "Yanawezekana mengi. Huenda Tino hakurogwa, ila alikuwa mtu wa back and forth."

Mama akaonekana kushangazwa kiasi na maneno yangu, naye akasema, "Jayden..."

"No, mama inawezekana. Labda ni baba yake Miryam kweli, kaanza kuzaa na huyo mwanamke, akarudi kwako, akarudi kwake tena, akarudi kwako tena, ndiyo akaja kwenda kimoja. Wanaume wengi si tunapenda kurukaruka, unaweza kuta ana watoto zaidi ya ishirini kila mkoa... ndugu ambao hatufahamiani nao," nikasema hivyo.

Wazazi wangu wakatazamana kwa huzuni kiasi, wakiwa wanaona jinsi ambavyo suala hilo lilikuwa limenivunja sana moyo, nao wakatulia tu na kuniangalia tena.

Nikashusha pumzi, nami nikasema, "Nimechoka."

"Jay..." mama akaniita kiupole.

"Yaani sijui nafanyaje mama. Baada ya hili yaani najua Miryam hatataka tena kuni... dah!" nikaongea kwa huzuni na kufunika uso wangu kwa viganja.

Mama akanishika kichwani na kuuliza, "Jayden... kwani, Miryam ulikuwa umesham... umeshamgusa?"

Nikamwangalia tu machoni bila kutoa jibu, naye akawa amelipata jibu la swali lake.

Mama akafumba macho na kutikisa kichwa kwa kusikitika.

Mzee akasema, "Haina namna Leah, watoto hawakujua. Hapa kilichopo...."

"No, no, hapana. Inatosha..." nikasema hivyo kumkatisha.

"Jay, unatakiwa ujue unafanya nini kutoka hapa, na upange...."

"No, sihitaji kupanga, au kufanya lolote tena mzee. Nita... nitamtafuta tu Miryam baadaye, tutaongea. Yatakayofata tutajua tu, lakini... kwa sasa... basi," nikaongea kwa hisia za kuvunjika moyo.

Wazazi wangu hawakuwa na neno zaidi, nami nikanyanyuka tu na kuwaacha chumbani kwao, nikiwa nimewaaga kuelekea kwangu huko Bamaga. Pozi, raha, amani yote ilikuwa imekata. Nuru alitaka kunisindikiza, yaani aende pamoja nami kwangu na kulala huko kama sehemu ya faraja na kuniunga mkono, lakini nikamwambia haikuwa na shida. Yeye na waliokuwepo walinitazama kwa hisia kweli kana kwamba nilikuwa mtu wa kuonewa mno huruma, na upesi sana nikaondoka hapo ili hisia za namna hiyo ndani yangu mwenyewe zisiendelee kunivuta chini.

★★

Nimekuja kufika pale kwangu eneo la Bamaga ikiwa imeshaingia mida ya saa tano. Nilikuwa nimeendesha gari kwa mwendo wa taratibu mno yaani, nikiwa kama nimezubaa muda mwingi, na baada ya kuingia ndani nikaketi tu sofani kama vile nimechoka sana. Viganja midomoni, macho mbele, fikira zikiwa zimetekwa na suala la leo, kwa kweli nilihisi kuchoka mno. Miryam, Tesha, Mariam, na hata yule Joshua, walikuwa ni ndugu zangu. Kwa nini ilitakiwa kuwa hivyo?

Sikuelewa bado, maana ni kama vile maisha yangu yalikuwa yanachezeshwa kimazingara na mtu fulani. Ni mchawi gani ambaye hakutaka niwe na Miryam katu katu mpaka kugeuza mkondo wa mahusiano yetu kuwa namna hii jamani? Nilijiuliza sana bila kupata jibu. Kitu ambacho sikuwahi kukaa kuwaza kingenikuta mimi na yule mwanamke ndiyo kikawa kimetukuta. Nilichoka sana moyoni. Sikujua ninafanya nini kutokea hapo kiukweli. Nikatoa simu na kuangalia ikiwa Miryam alinitumia ujumbe wowote ule, lakini upande wake ulikuwa tupu. Dah!

Ambaye alikuwa amenitumia ujumbe ni Adelina, dada ya marehemu Joy wa Masai. Ilikuwa ni ujumbe kuniambia kwamba leo, ikiwa ni Jumapili, nilitakiwa kwenda kwake kumtembelea ikiwa ni ahadi ambayo nilimpatia, lakini alishangaa sikuwa hata nimemtafuta kutokea asubuhi mpaka jioni walau kusema nimepatwa na dharura. Ah, sikuwa hata nakumbuka jambo hilo, na kwa jinsi mambo yalivyokuwa sasa hivi, sikuona hata umuhimu na uhitaji wowote wa kumjibu. Nikaweka simu hapo hapo sofani na kwenda chumbani, nikavua nguo, nikajimwagia maji nikiwa bado na sononeko kubwa moyoni, nami nikakiendea kitanda na kujikunyata mwenyewe hapo. Upweke mkubwa ulioanza kuingia moyoni ukinitawala mpaka usingizi ulipofanikiwa kunichukua.


★★★


Asubuhi ikafika, na kwangu ikaendelea kutembea tu hadi kugeuka kuwa mchana bado nipo kitandani. Usingizi ulikatika alfajiri ya mapema na haukujisumbua kunirudia tena, nikaambulia kukaa macho hadi ilipokuwa wazi kwamba mchana umeanza kuingia. Kuchoka kihisia kulifanya niwe mvivu hata kuamka nione shida, lakini JC najua kuna mambo mengi yaliningoja huko nje. Nisingejilaza kitandani milele. Huku nikihisi uhitaji mkubwa wa kula shauri ya kuliacha tumbo na uhaba kwa masaa mengi, nikajinyanyua hivyo hivyo na kwenda kujisafisha kwanza.

Muda wote niliotumia kujisafisha mpaka namaliza kuvaa ni tukio lile lile la jana kule nyumbani ndiyo likikuwa likijirudia kichwani, nami nikaifata simu yangu sebuleni kuona mangapi yalikuwa yamenipita kuhusiana nayo hadi sasa. Zaidi nikakuta ni mama, Jasmine, Nuru, Tesha, Ankia, ndiyo walionipigia, pamoja na jumbe kadhaa za kunijulia hali kutoka kwao. Daktari ambaye alinioigia siku kadhaa nyuma kuniambia kwamba nitatakiwa nirudi kazini ndani ya wiki moja alikuwa amenitafuta pia, nami nikaamua kuwasiliana naye kwanza. Maongezi yakahusu suala hilo hilo, na mimi nikamjulisha kuwa niko tayari kurudi mapema tena si lazima mpaka wiki ijayo, hata siku yoyote kati ya hizi za wiki hii.

Ilipoeleweka, ndiyo nikamtafuta bibie sasa. Nikaipigia simu yake Miryam mara kumi, hakupokea. Mh? Haya. Nikaona niwacheki wengine. Mama na Jasmine walinijulia hali, ikiwa nimeshaongea na Miryam, nami nikawaambia bado. Dada yangu alikuwa ameshaambiwa yaliyotokea jana, na akanifahamisha kwamba alijaribu kumtafuta Miryam lakini hakumpata. Wakanipa pole, nikiwaambia ningemtafuta tu na kuongea naye. Baada ya hao nikamgeukia Tesha sasa.

Kijana alikuwa anataka kunifahamisha tu namna ambavyo tukio la jana lilimmaliza nguvu dada yake, akisema yaani Miryam alikuwa chumbani mpaka sasa asitake kuongea na mtu yeyote yule. Akaniambia ingenibidi nifanye tu kwenda huko ili nijaribu kuongea naye zaidi ingawa mambo mengi yalikuwa yamebadilika sasa. Nikasema ningejitahidi kuja ndiyo na kumuuliza hali ya wengine hapo kwao, na jibu nililotarajia likawa kwamba ni huzuni ndiyo ilitawala. Ndoa iliyokuwa imengojewa kwa hamu sasa ilifikia hatamu, ni lazima hali ingekuwa ya sintofahamu. Lakini la muhimu lingepaswa kuja kuwa kukaa wote kwa pamoja ili tuzungumze tena, na mara hii ingekuwa kwamba ninaenda kuongea nao wakiwa kama ndugu zangu wa kiukoo, siyo marafiki tena. Aisee!

Tukayaachia maongezi hapo kwa kuagana vizuri, akiwa amesisitiza nisiache kwenda kwao, nami nikatulia tu hapo sofani kutafakari kidogo. Ijapokuwa jambo hili lilionekana kumtikisa sana Miryam, sikuona ni haki atende kana kwamba linamwathiri yeye peke yake. Kuzungumza ilikuwa lazima, kwa hiyo hata kama asingetaka kuongea kwa simu ningemfuata tu huko huko na kuongea naye vizuri. Hilo nikalisimentisha vyema akilini, nami nikajiondoa hapo kwangu hatimaye kwenda kutafuta chakula kwanza.

★★

Niliamua kuchukua gari kwenda kwenye eneo lenye mgahawa maridadi kabisa. Yaani mgahawa uliitwa Mgahawa Mgahawa, sehemu iliyo na bonge moja la ufahari na huduma nzuri za malisho. Nikaegesha gari na kuchoma ndani, nikakaa na kuagiza libaga la maana la kunishibisha siku nzima kabisa, na wakati nikingoja liletwe nikapigiwa simu na mtu ambaye sikuwa nimetarajia. Alikuwa ni rafiki yangu wa kitambo sana, tuliyekula ujana pamoja na kusindikizana kwenye uhuni mwingi, yaani kwenye kutengeneza historia sisi tulikuwa hatujambo. Aliitwa Simba. Kuongea naye mara ya mwisho ilikuwa kioindi kile mwanzoni tu nimefika kwa Ankia, mpaka leo hii, hivyo nikahisi furaha ingawa bado huzuni ndiyo ilinitawala. Nikapokea.

"Oyaaa!" akasikika Simba.

"Niaje?" nikaongea kwa shauku kama yake kiasi.

"Ah, shushashing nya shuwai sha shing?" Simba akaigiliza kuongea kichina.

Akanifanya nitabasamu kiasi, nami nikamjibu, "Shiyajasha. Shaakuyaashing?"

"Hahahah... dah! Kaka ni muda sana..." akaongea kwa shauku.

"Yeah. Naona bado hujaacha bangi zako tu," nikamwambia.

"Kwani nani alianzishaga hii?"

"Nini?"

"Kuongeleshana kichina?"

"Sa' si tulikuwa bado O level, hayo mambo ya kitoto..."

"Na we' unajiona umekua sasa?"

"Me kitambo sana. We' naelewa medula oblongata yako ni ya mtoto bado..."

"Au siyo doctor? Hizo medula unazielewa kichizi yaani, basi unajionagaaa umemaliza kila jambo duniani yaani..."

"Hahah... kwani uwongo?"

"Aa wapi, wasiokujua kama me ndo' wataamini. Yaani me na we' bado manoka wale wale tu, siyo hospitali wala jeshi linaloweza kutubadili," akasema.

"Haya bana. Leta habari za jeshi sasa..."

"Ah, za nini sitaki hata tuziongelee."

"Kisa?"

"Ni mateso tu, bora hata ningeendaga ualimu."

"Hahah ndiyo ishakupita hiyo..."

"Ohoo, napigika kinyama yaani. Ila sasa kuna habari njema, ndani ya hii wiki naeskepu kambi," akaniambia hivyo.

"Unaondoka jeshini? As in... kimoja au? Sijaelewa," nikamwambia.

"Nakula likizo ya miezi mitatu... oya!"

"Oyaa..."

"Mule mule!"

"Hahah huku huku! Unakuja Dar?" nikamuuliza.

"Pigia mstari njemba," akaongea kwa shauku.

"Dah! Hiyo kweli habari njema..."

"Naangushaga sasa?"

"Kweli, huo muda hauna. Kwa hiyo utafika lini?"

"Ndiyo najipanga hapa. Gheto ulipo si pako empty?"

"Nipo mwenyewe, we' njoo tu," nikamwambia.

"Huo ndo' unyama sasa. Nikadhani ushajaza na watoto huko, maana we' mzee wa mapenzi uchwara nakujuaga huchelewi," akasema hivyo.

"Hakuna, me siyo wa hivyo..."

"Haya bana doktaa. Nikija ni kuliamsha dude kweli, nina mastori kama yote ndugu yangu, yaani yaliyonikuta mnyama Simba kama Simba," akasema hivyo kwa shauku.

"Aminia brother," nikamjiibu.

"Poa, mida mida. Shuwaisheshei to you," akaongea kiutani.

Nikatabasamu tu na kutikisa kichwa, nami nikamwambia, "Poa shishiwei wewe."

Tukaachiana hapo na rafiki yangu, ambaye sasa ningetarajia kumpokea akija jijini kwa ajili ya mapumziko yake. Simba angekuwa sehemu bora sana ya kuleta hali yenye uchangamfu kwangu kwa kipindi hiki ingawa mambo yenye kukwaza yalikuwa mengi bado. Na hapa ndiyo ningetakiwa nimalize msosi wangu upesi ili niende kutatua kikwazo kizito zaidi kwa wakati huu.

Haikuchukua muda mrefu nami nikawa nimemaliza chakula changu kwa kushiba, na baada ya kulipia ikawa ni mwendo wa kuelekea nje. Sikuwa hata nimetilia maanani uwepo wa watu wengine waliokuwepo ndani ya mgahawa huo kwa kujali biashara zangu zaidi, na ndiyo ile tu naelekea upande wa kutokea, kwa jicho la pembeni nikawa nimemwona mtu aliyefahamika kwangu upesi. Mwanamke, ambaye huenda kama ningekutana naye siku kadhaa zilizopita basi ningempuuzia tu na kusonga mbele, lakini sasa akanifanya nisitishe hatua zangu. Ilikuwa ni Stella.

Aliketi kwenye meza ya chakula iliyokuwa upande tofauti na ule niliokuwepo awali, ndiyo sababu sikuweza kumtambua mapema, ila sasa kama angetazama tu sehemu niliyosimama angeniona kirahisi. Na kweli, macho yake kunyanyuka tu na kutazama mbele tayari akawa ameniona, na kama ni jambo ambalo lilivuta umakini wangu kwake zaidi ni lile lile lililokuwa limefanya macho yake yawe chini kabla hajaniona. Yaani mezani hapo. Upande wa kiti kilichotazamana naye alionekana kuketi binti mdogo, nikimwona kwa nyuma tu kwa kigauni cha njano na msuko maridadi uliopendezesha kichwa chake, akionekana kufurahia chakula hapo. Hisia zikaanza kurukaruka ndani yangu, yaani msisimko kwa kutarajia mengi sana, na itikio la Stella baada ya kuniona likawa kuachia tabasamu na kisha kuonekana akimsemesha binti huyo kwa njia elekezi. Ndipo kakageuka. Dah!

Kwa mara ya kwanza kabisa JC nikawa nimemwona mtoto wangu, mwanangu, ambaye kwa muda mrefu sasa nilikuwa nimejaribu kumkwepa. Sikutarajia. Binti huyo, baada tu ya kuangalia upande wangu, akaonekana akijitelezesha kutoka kitini na kushuka yeye mwenyewe, kisha akaanza kutembea kwa mwendo wa kitoto akija upande wangu. Nilibaki nimesimama tu nikikaangalia, kakiwa keupe kweli kama mama yake, macho mazuri, na kakipendezeshwa kwa njia iliyopiga kelele kwamba ni katoto kutoka kwa watu wa maisha ya gharama.

Sikujua Stella alikaambia nini, lakini najua hakukaambia kanifuate, yaani wazo hilo kalilijenga kenyewe. Moja kwa moja mpaka kufika kwangu, binti huyu mdogo akaja na kunikumbatia miguuni. Nilisisimka sana kiasi kwamba hata nikashindwa kutoa itikio lolote na kubaki nimemwangalia tu. Mtoto hata hakuwa na shuku yoyote ile kunielekea, yaani alinishikilia kwa njia ya kunijua kabisa. Nikamshika mikononi pia na kuchuchumaa, nikamwangalia machoni kwa hisia sana, nami nikamkumbatia hapo hapo binti yangu. Nilihisi amani ya kipekee sana, sikutarajia kabisa. Hatimaye nikawa nimekutana na mwanangu, Evelyn!





★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★


WhatsApp +255 678 017 280
 
MIMI NA MIMI 3

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA PILI

★★★★★★★★★★★★★



Nilikakumbatia kasichana haka kwa sekunde chache, kisha nikanyanyuka nikiwa nimekabeba mikononi mwangu. Niliweza kumwona Stella akianza kunyanyuka kutoka pale alipokuwa, na kimwonekano alipendeza kama nilivyomzoea. Lakini umakini wangu ukatekwa zaidi na mrembo aliyekuwa mikononi mwangu. Evelyn. Kwa kumtazama tu, nilihisi ni kama vile naangalia kioo kilichoonyesha taswira ya sura yangu ya utotoni. Kiukweli kalinifanana mno, hakuna mtu hapo ambaye angeweza kupinga kwamba hii ilikuwa damu yangu.

Nikakaangalia usoni kwa hisia za upendo ambao sikujua nilikuwa nao kukaelekea, nami nikakasemesha, "Mambo?"

Evelyn hakuwa mtoto mwenye haya, yaani alinitazama sawia kabisa bila kunena lolote, na mama yake akawa ametufikia hapo niliposimama.

"Heey..." Stella akanisemesha.

"Hey," nikamjibu huku nikitabasamu.

"Umeni-surprise, sikufikiria ningekuona hapa," Stella akaniambia.

"Hata me yaani... sikukuona. Nilikuwa pale hivi..." nikamjulisha.

"Ooh sawa," akasema hivyo.

Nikarudi kumtazama Evelyn na kukishika kiganja chake.

"Eve... umemwona daddy?" Stella akanisemesha.

"Ahahah... dah! Amekua sana," nikasema hivyo.

"Yeah, anataka kukufikia," Stella akatania.

Tukacheka kidogo pamoja, nami nikasema, "Sikutarajia pia, yaani... dah! Hii ni surprise kwa kweli."

"Ni Mungu kakusudia tukutane, na yeye alichoka kungoja," Stella akasema.

"I hear you, i hear you... ahah... kaone haka na mashavu," nikasema hivyo .

"Ahahah... basi anaringa," Stella akasema.

"Ndiyo muda wake, hiyo lazima. Hukuingia kazini leo?" nikamuuliza.

"Leo na kesho niko off. Ila, kesho nitaenda clinic mpaka kwenye saa nane hivi, then nita-spend quality time na huyu kama leo. Tumepanga kuzurura haswa," akaniambia.

Nikatabasamu tu na kumtazama binti yangu. Siku ya kwanza tu kumgusa lakini tayari nikawa nahisi kujivunia.

"Na wewe? Misele ya wapi?" Stella akauliza.

"Ah, me nilikuwa round tu. Sina ishu nyingi leo, nilitaka kwenda location then niingie home kulala," nikamwambia huku nikimtikisa-tikisa mtoto.

"Okay, sawa," Stella akasema.

"Alikuwa amemaliza kula huyu?"

"Bado, kakuona tu akakimbia chakula," Stella akasema.

"Ahah... basi, ngoja tumrudishe kwa mama aende kula ashibe. Eti toto?" nikamsemesha Evelyn kwa kudekeza.

Nikajaribu kumpatia Stella binti yetu ili ambebe, lakini Evelyn akagoma kwenda kwa mama yake na badala yake akanilalia begani kabisa kuning'ang'ania.

"Haya sasa..." Stella akasema.

Tukacheka kwa pamoja, hapo nikihisi fahari kweli, nami nikasema, "Basi twende tukale wote eh?"

"Ndiyo kilichobaki, maana me hanijui tena," Stella akasema hivyo huku akigeuka.

Sote tukaanza kuelekea pale ambapo wawili hawa walikuwa, na Evelyn akiwa mikononi mwangu, nikaketi alipokuwa amekaa yeye na kumwongoza ale chakula chake chepesi huku nikimpakata. Iligeuka kuwa pindi nzuri sana kwangu, kiasi kwamba nikazama zaidi kwenye raha ya kuanza kumjua mwanangu mpaka nikasahau yale niliyohitaji kwenda kufanya awali. Stella aliongea kwa shauku yake ya kishua kuhusu tabia za Evelyn, akisema namna ambavyo binti yetu ni mwenye akili na mjeuri kama mimi.

Hapo ndiyo utani mwingi zaidi ukaanzia, tukisemana kuhusu tabia zetu na mambo ambayo tungepaswa kufanya zaidi na zaidi ili kuunga mkono ukuzi wa mtoto ndani ya upendo wa wazazi wote kwa pamoja. Nilifurahia sana pindi hii. Mtoto wangu alionekana kuwa na akili nyepesi na mwerevu sana, akitaka kitu kakitaka, asipokitaka hakitaki. Ilinipa hamu kubwa ya kutaka kushiriki muda mwingi pamoja naye kutokea hapa na kuendelea, nami nikaamua kutoukatiza huu wa sasa ili hilo lianze kufanya kazi.

★★

Basi, muda si muda Evelyn na mama yake wakamaliza kula, nasi kwa pamoja tukaondoka sehemu hiyo. Bado mtoto hakutaka nimwache, na niliona wazi kwamba Stella alifurahia sana jambo hili. Mipango ikawa imebadilika kutoka kwenye mimi kwenda kule kwa Miryam, ili niweze kutumia muda zaidi na mwanangu, kwa hiyo nikaamua ningekwenda pamoja na hawa wawili kokote ambako wangetaka kwenda kwa leo mpaka muda ambao mtoto angenichoka. Stella alipanga wakimaliza kula waelekee madukani kununua vitu mbalimbali, na mimi nikaunga mkono hilo kwa kusema ningeshiriki kumnunulia mtoto vitu vingi vizuri. Tukaamua kuanza mizunguko yetu kwa kutumia gari langu, na Crown ya Stella tukaiacha eneo hilo la Mgahawa mpaka wakati ambao tungerudi tena kulifuata.

Kweli, ikawa ni wakati murua kabisa ambao nisingekuja kujutia kuushiriki hata kidogo. Matembezi yetu yalijawa na furaha na amani kubwa sana, na hata sikutegemea Stella angekuwa mwenye kuburudisha kama namna ambavyo alikuwa wakati huu, lakini akapita matarajio yangu. Evelyn alikuwa mchangamfu sana, mtoto mwenye miaka miwili na nusu lakini alijua vitu vingi sana. Kila alichotaka alipata siku hii. Kwenye sehemu za michezo ya watoto tukaenda na kucheza pamoja. Nikamnunulia midoli, nguo, viatu, vyakula vya kutunza kama keki, chocolate na biskuti, barafu tamu wapendazo watoto, na mama yake alichukua breki kwenye kununua chochote ili aache binti afurahie pesa ya baba tu.

Leo Evelyn ndiyo aliniendesha vibaya mno. Alipotaka niwe, nilikuwa. Alipoudhika, mimi ndiyo nilipaswa kumbembeleza, mpaka akalala mikononi mwangu mara mbili kabisa. Nilihisi furaha sana. Yote ambayo Stella alisema binti yangu anahitaji kutoka kwangu yalikuwa kweli. Leo ndiyo nilijionea. Kwa hiyo tumekuja kurudi pale Mgahawa Mgahawa kulipitia gari la Stella ikiwa ni mida ya saa moja jioni, hasa kwa sababu kwenye safari zetu mara kwa mara tulikawizwa kwa msongamano wa magari hapa na pale. Wakati huu, Evelyn alikuwa amesinzia, yaani hii ikiwa ndiyo mara ya pili amelala mikononi mwangu, na mama yake akamchukua sasa ili tuagane.

"Amechoka kweli," nikasema hivyo.

"Amechoka kwa furaha," Stella akaniambia.

"Yaani! Hadi kukoroma anajua..."

"Hahah... kaitoa kwa nani mikoromo?"

"Kwako," nikamwambia.

"Wee! Me sikoromi hata chembe, ni wewe," Stella akaongea kwa furaha.

"Aa wee, ume-wrong number. Sijawahi koroma mie," nikasema hivyo.

"Hahahah... ipo siku nitakuja kukurekodi, naona umeshajisahau," akaniambia.

Nikatabasamu kwa furaha na kutazamana naye kwa ufupi, nami nikamwambia, "Asante Stella."

Akatabasamu pia na kusema, "Usijali. Ila me ndiyo nikushukuru Jayden. Umenipa furaha sana leo, yaani hata me sikutarajia siku ingekuwa nzuri namna hii."

"Hata mimi," nikamwambia.

"Hapa nitaenda kudili na fujo za huyu mpaka kesho," akaniambia.

"Kwa nini?"

"Si akiamka akakukosa?"

"Ataamsha timbwili?"

"Yaani! Si la Bongo hii," akasema.

"Usiwaze. Akiniulizia tu, nipigie. Video call, eh?" nikamwambia.

"Kweli, wazo zuri," akaniambia.

"Yeah, atatuliza makeke hapo."

"Na anavyojuaga kuzira sasa asipopata anachotaka! Yaani yuko kama wewe," akaniambia.

"Ahahah... tuombe asije kuwa kama mimi kabisa," nikamwambia hivyo.

"Too late. Ni mtoto wa baba yake huyu, anamhitaji zaidi tu ndani ya maisha yake," Stella akaniambia hivyo kwa hisia.

Nikatazama chini kiasi, nami nikasema, "Nitajitahidi kufanikisha hilo. Nalihitaji pia."

Akatikisa kichwa kukubaliana na hilo.

"Okay. Nendeni mkapumzike. Tutawasiliana," nikamwambia huku nikimshika mtoto taratibu.

"Poa. Baadaye," akasema.

"Haya."

Kisha mwanamke akaanza kuelekea gari lake, na kabla hajalifikia nikaamua kufanya ustaarabu wa kumfuata mpaka kumpita, nami nikamwomba alifungue kwa rimoti yake ili nimfungulie mlango wa siti ya nyuma kwa ajili ya kumlaza mtoto. Stella akatabasamu tu na kutii, pindi hii akiwa mdtaarabu kweli tofauti na nilivyomzoea, nami nikamfungulia mlango na kufanikisha kumweka Evelyn ndani vizuri.

"Kafupi kweli," nikatania kidogo.

Stella akatabasamu kiasi, kisha akanisogelea karibu zaidi na kupitisha mikono yake kupita uso wangu. Alitaka tukumbatiane, na hii kiukweli iliamsha hisia zenye uajabu ndani yangu maana bado nilimwona kama mtu wa kuotea mbali, lakini nikalikubali tu kumbatio lake la kuagana na kulipokea kwa wororo. Baada ya hapo ndiyo mama wa binti yangu akaingia kwenye usukani, gari akaligeuza huku mie nikibaki kuangalia upande wake hadi alipoliondoa eneo hilo baada ya kunikonyeza mara mbili kwa taa zake. Wakati wenye furaha na amani fupi kwa leo ndiyo ukawa umekomea hapo, na sasa ikawa muda wa kwenda kule nilikotakiwa kuwa. Moja kwa moja hadi garini, mwendo ukaanza kuelekea Mbagala.

★★

Niliendesha gari mpaka Mzinga huko Mbagala, nikifikia mitaa ya Masai kwenye mida ya saa mbili usiku. Kwa sababu ungekuwa ujio wa "ghafla" kwa wengine, nilikuwa nimeshapanga nini cha kuzungumza nao kwa pamoja kabla sijaongea na Miryam, kwa kuwa ishu yetu ya kuwa na undugu iliwaathiri na wengine pia waliokuwa sehemu ya familia "yetu." Hasa Bi Jamila. Nahisi ningekuwa na mengi sana ya kuongea pamoja naye, na hata ikiwezekana baada ya hapo ningeweka jitihada za kumkutanisha yeye na mama yangu ili yaliyopita yawekwe bayana kwa pande zote mbili na tuangalie tunafanya nini kusonga mbele. Ingekuwa soo!

Kwa hiyo nikaufikia usawa wa nyumba ya mwenye nyumba wangu wa huku Mbagala, Ankia huyo, na ile tu nimelipita duka la Fatuma hapo nje nikamwona Ankia mwenyewe pamoja na wadada wengine watatu, wakikaa kupiga story. Hivyo, nikaegesha gari kukaribia na mwingilio wa nyumba yake, na nadhani alitambua ni mimi kwa kuwa nikamwona ananyanyuka upesi na kuanza kuja nilipo. Nikalituliza gari na kushusha kioo, moja kwa moja Ankia akaja mpaka mlangoni na kusimama hapo karibu na uso wangu. Nikamtazama na kutabasamu kiasi, huku yeye pia akitabasamu kwa mbali.

"Vipi?" nikamuuliza.

"Safi. Mambo?" naye akaniuliza.

"Ukiuliza hivyo, unamaanisha bado hujasikia, au..."

"Nimeshaambiwa."

"Ah, wa Mbagala mnachelewaga sasa..."

"Shadya aliniambia ndiyo, na kwa kweli ilinishangaza. Nikakupigia leo tuongee, lakini hukupokea. Uko sawa?" Ankia akaniuliza kwa kujali.

Nikaishia kumwangalia tu usoni.

"Shuka basi, twende ndani," akasema.

"Nimekuja tu kuongea naye, sikai," nikamwambia.

"Haulali huku leo?"

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Umekuja kuongea na Miryam? Hayupo lakini..." akasema.

"Hayupo?"

"Eeh."

"Alienda kazini kwani? Naliona gari lake humo ndani..."

"Eeh, kaliacha, ila sijajua ameenda wapi. Alikuwepo ndani huko tokea asubuhi, me hii jioni nimemuulizia ndiyo wakasema ameondoka," akaeleza.

Nikatazama mbele tu na kushusha pumzi.

"Hukumwambia unakuja?" akauliza.

"Hamna. Nilidhani ningemkuta, niliwasiliana na Tesha lakini. Ngoja nimpigie," nikasema hivyo na kuvuta simu.

Ankia akaendelea kusimama hapo hapo, akiniangalia huku ameegamiza kiwiko chake juu ya uwazi wa kioo cha mlangoni.

Nikampigia Tesha, lakini simu yake haikupatikana, nami nikasema, "Hapatikani. Yupo ndani?"

"Sijajua. Nenda ukaangalie," Ankia akasema hivyo.

Nikatulia kidogo kutafakari.

"JC?" Ankia akaniita.

"Naam? Yeah, aa... acha tu nigeuke, nitakuja labda kesho," nikamwambia.

"Iih JC! Ndiyo nini sasa?"

"Ndiyo nimejifunza somo la kutowenda mahali bila kutoa taarifa."

"Ndiyo ufike tu na kuondoka? Unaenda wapi sasa?"

"Nyumbani."

"Kwani huku jalalani? Hapa si nyumbani pia?" akaongea kwa kusisitiza.

Nikatabasamu kiasi na kusema, "Kuna sehemu napita kwanza. Nahisi nitatoka nimechelewa."

"Hata wakina Bi Zawadi huendi kuwasalimia?"

"Nitarudi tu, usijali. Wataniona tena," nikasema hivyo na kuwasha gari.

Ankia akasema, "Mh? Haya. Siye tupo. Na... JC..."

Nikamwangalia machoni.

"Pole kwa yote. Tuna mengi ya kuongelea, ukipata muda... niko hapa kwa ajili yako, eti?" akaniambia kwa upole.

"Asante. Nitakuja, tutaongea. Msalimie Bobo," nikamwambia.

Ankia akakunja midomo yake kwa njia ya kukerwa baada ya kusikia hilo jina.

"Eh? Heh. Basi kumbe tuna mengi ya kuongelea. Subiri nirudi," nikamwambia huku nikitabasamu.

Akacheka kidogo na kusema, "Poa. Wasalimie."

Nikatikisa kichwa kukubali na kupandisha kioo, huyoo nikageuza gari na kuondoka eneo hilo.

Labda ningefanya jitihada ya kumtafuta Tesha tena mapema kabla sijaja huku ili nijue kama dada yake yupo, lakini hayo yakawa maziwa yaliyomwagika tayari. Ambacho nikawa najiuliza ni Miryam angekuwa wapi sasa hivi, ikiwa imeshaingia saa tatu sidhani kama angekuwa kule dukani kwake. Wazo la haraka likaja, nimpigie Soraya kumuuliza, lakini kwa mida hii dada wa watu angekuwa kwake tayari.

Nikaona nimpigie bibie mwenyewe, mara tatu, lakini hakupokea. Nikahisi vibaya sana moyoni. Yaani alikuwa ananikwepa kabisa. Sikufikiria mahala pengine pa kumpata zaidi ya kule dukani kwake, hivyo nikaamua kwenda huko kuangalia tu kama yupo labda. Ikiwa ningemkosa huko, na simu hakutaka kupokea, basi ingenibidi nimwache kwanza. Huenda angehitaji muda wa kuwa mwenyewe na kurejesha utulivu wa kihisia ili tuje kuongea vizuri zaidi.

Sasa mwendo wa kurudi ukakwamishwa kabla hata sijaweza kuingia lamini. Yaani ndiyo nilikuwa tu nimeiacha Masai na kufika Mzinga, na gari langu likashindwa kusonga kutokana msongamano mkali uliokuwa umeiteka barabara. Ulikuwa msongamano wa magari yaliyoelekea upande wa huko Rangi Tatu, lakini upande wa kuelekea Kongowe na mbele zaidi magari yalitembea kwa kujinafasi. Wenye kuendesha magari kuelekea Rangi Tatu walitumia na barabara ya pembezoni ya changarawe, na yenyewe ikajaa na kukwamisha magari. Kwa hiyo nikajikuta nimesimama tu kwanza, nikiona askari wa usalama huko aliyejaribu kuongoza mambo na mabodaboda waliolazimisha kupita pande tofauti ya barabara kuelekea huko Rangi Tatu. Wengine walizima kabisa magari yao.

Zikapita kama dakika ishirini gari langu likitulia hapo hapo, nami nikawa napoteza muda kwa kuangalia mambo fulani kwenye simu. Kisha nikarejewa na kumbukumbu muhimu sana. Evelyn. Oh, nilikuwa mpaka nakaribia kusahau kumsalimia tena na sasa muda ulikuwa ni saa tatu kuelekea saa nne usiku. Sijui angekuwa amelala? Nikaona nimpigie Stella, naye alipopokea akanithibitithia kuwa ndiyo, Evelyn alilala tena baada ya kuamka si muda mrefu nyuma na kula. Alikuwa na kauchovu ka siku inavyoonekana.

Basi, nikiwa nimepitwa na hilo nikaendelea kuzungumza kidogo na Stella, na akaniambia kuhusu ratiba zake kwa kesho na kuuliza ikiwa ningeweza kukutana naye tena. Nikamwambia la kukutana lingekuwa lazima, lakini mimi pia ningeanza kujishughulisha na mambo ya kikazi siku si nyingi kutokea hapa hivyo upangiliaji mzuri wa ratiba ungehitajika ili tushirikiane ipasavyo kumpa mtoto muda wetu. Hasa mimi.

Stella alionekana kufarijiwa na hilo, na ndiyo hata maongezi ya utani yakaingia tena, mpaka mie kumwambia kuhusu namna ambavyo msongamano wa magari kwa pindi hii ulivyonikera mno. Wakati simu bado ikiwa sikioni, kutokea lami niliweza kuona gari moja zuri sana, jeusi aina ya Range Rover Discovery modeli mpya zaidi, likionekana kuwa la mtu ghali. Likiwa limetokea barabara ya upande wa huko Rangi Tatu, likaingia hii ya changarawe, taratibu, likionekana kutaka kuelekea huko Masai au mitaa mingine kupita Emirate. Lilinivutia sana, lakini nikaondoa umakini kwa hilo na kuendeleza maongezi na Stella.

Gari hilo halikuendeleza mwendo wake kama ambavyo ningedhani mwanzoni kwa kuwa ni sehemu ndogo tu ya eneo lililoingia kutokea lami nalo likaegeshwa pembeni usawa wa maduka. Macho yalilielekea, lakini akili yangu ikiwa kwenye kile alichokiongea Stella simuni na kumjibu. Alikuwa na njia nzuri za kuleta utani, na mimi nilijitahidi kuurudisha pia na kufanya isiwe rahisi kukatisha mazungumzo. Na ndipo sababu ya kuyakatisha ikatokea. Kwenye hilo gari nililokuwa nikilitazama, mlango wa siti ya pembeni na dereva ukafunguka, na hapo nikamwona mtu akishuka aliyefanya nikunje uso kimaswali. Ilikuwa ni Miryam! Alishuka kutoka ndani ya hilo gari, akionekana kuvaa kwa njia ambayo ungesema ni kawaida tu; T-shirt nyeupe yenye kubana na suruali pana ya jeans ingawa ilichora umbo lake zuri, lakini alikuwa amependeza sana.

Nikajikuta najisawaziaha vizuri zaidi kwenye siti yangu ili nitazame huko nje kwa umakini zaidi. Sikuona vibaya, ilikuwa yeye. Aliposhuka akaufunga mlango wa gari hilo na kuanza kuja upande ambao gari langu lilikuwa, kisha akaita bodaboda mmoja ili apande. Nilishangaa sana! Nini ilikuwa maana ya jambo hilo? Sekunde chache zilizopita nikiwa kama nimepigwa na bumbuazi kutazama tukio hili kukanisahaulisha kabisa kwamba bado Stella alikuwa akinisemesha simuni, nami nikaendelea kutazama mpaka bodaboda iliyombeba Miryam iliponipita na kutokomea. Nikalitazama gari lile tena, na sikuweza kuona vizuri aliyekuwa nyuma ya usukani wake, kwa kuwa hata taa ya ndani haikuwaka.

Nikashusha simu kutoka sikioni bila kumjibu Stella chochote kile, nikitazama tu hilo gari lilipoanza kugeuza taratibu, kisha likaingia barabarani kwa mbinde na kuelekea upande wa kule Kongowe, siyo kule lilikotoka mwanzo. Ahiiii! Mbona majanga! Nilihisi kuishiwa pozi kabisa. Miryam alikuwa ndani ya gari la namna hiyo kwa nini? Nani alimbeba na kumpeleka wapi na kumrudisha usiku, halafu asimpeleke kwake moja kwa moja na badala yake bibie achukue usafiri kwenda huko? Kuna nini kilichoendelea ambacho Miryam aliona kingetakiwa kufichika namna hiyo? Ndiyo kusema nilikuwa nimeshabebewa mali yangu mapema namna hii? Ah, hapana. Ningehitaji kujua, yaani ningetakiwa nielewe kila kitu vizuri. Ikiwa nilichodhani ndiyo kinaendelea kilikuwa sahihi, huyo mwanamke angekuwa amenimaliza kabisa. Yaani angeniua!





★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★


WhatsApp +255 678 017 280
 
MIMI NA MIMI 3

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA TATU

★★★★★★★★★★★★★



Kwa sababu fulani sikutaka nianze kuhukumu mambo kwa njia ambayo huenda ingenifanya nitende bila busara. Nilimjua Miryam vizuri. Hakuwa wa tabia za... yaani... aisee! Mbona ingekuwa ngumu sana? Unajua kuna vitu vingine hutokea kwa njia ambayo huenda ukafikiri ni kinagaubaga, lakini kwa hali hii nilihisi utofauti wa hali ya juu. Kwamba itokee jam ya magari, nitulie hapo mpaka nije kuona jambo hilo, ilikuwa kana kwamba Mungu alitaka kunionyesha kitu fulani. Lakini nini?

Nisingeweza kamwe kuwazia kwamba Miryam wangu angeenda nje ya mahusiano yetu ndani ya siku moja tu tangu tumepatwa na matatizo, lakini hiyo ilikuwa ni alama kubwa sana kuupuuzia uwezekano huo. Lakini hapana, sikutakiwa kuwaza hivyo, labda hata ilikuwa rafiki aliyemleta hapo, huenda walikutana tu leo leo na sasa ndiyo akarudishwa nyumbani. Hivyo. Au? Hapana. Yaani bado nilihisi kutangatanga sana kiakili.

Macho bado yaliikuwa mbele kana kwamba natazama kwa umakini msongamano ule wa magari, lakini akili yangu ilikuwa kwingine kabisa. Nikiwa ndani ya mzubao huo, simu yangu ikaanza kuita, nami nikaangalia mpigaji kukuta ni Stella. Nikapokea, na mwanamke huyo alitaka kuelewa sababu iliyofanya niache kuzungumza ghafla mpaka kumtia wasiwasi, akiuliza kiutani labda ni Miryam alinikuta naongea naye ndiyo kivumbi kikawaka huku, lakini nikamwambia hapana, kuna ishu tu ilizuka na nilihitaji kushughulika nayo upesi. Kwa hilo akawa hana neno, nasi tukaagana kwa kuahidiana kuendelea kuwasiliana.

Baada ya hapo, akili ikarudi kule kule. Ningefanya nini endapo kama jambo nililojionea muda mfupi nyuma lilikuwa na maana hasi? Nikabofya kioo cha simu kumpigia Miryam, ikaita, hakupokea. Nikarudia kufanya hivyo mara mbili zaidi, ikawa vile vile. Ahaa? Nikaweka simu pembeni. Msongamano wa magari sasa uliachia kiasi, nami nikawasha gari na kukanyaga mafuta kuelekea huko nilikotoka. Inaonekana penzi langu liliingiwa na dosari mpya zaidi tu ya ile niliyodhani ndiyo tatizo lenyewe, na kutokea hapo ningefanya kila niwezalo kujua ni nini, na ninadili nalo jinsi gani.


★★★


Siku hiyo ikapita, hii ikiwa ni Jumanne kwa umapema wa alfajiri nilioamshwa kwa mwito wa simu yangu. Nikiwa kitandani nyumbani kwangu, nikaichukua simu kukuta mpigaji ni mmoja wa madaktari wakuu pale hospitali ya Muhimbili, nami nikapokea huku bado nikihisi usingizi. Taarifa aliyonipatia sasa ikanifanya niwe makini zaidi, kwa sababu alinijulisha kwamba ningetakiwa kufika hospitali upesi kuendelea na majukumu kutokana na hali za kidharula zilizohitaji stadi zangu ili nisaidie wagonjwa. Nikamweleza kwamba tayari niliambiwa kuhusu kurudi na sikuwa nimeamua kuja leo bado maana nilikuwa na uchaguzi wa siku ambayo ningeweza kuja ndani ya wiki hii, lakini sasa mambo yakabadilika. Ningetakiwa niingie kazini upesi, kwa kuwa uhitaji uliongezeka.

JC hapo sikuwa na neno, maana nilielewa lazima kuwepo na hali zisizo nzuri sana na kweli ningetakiwa kuwepo kusaidia. Huyo alikuwa mkuu wa madaktari wa kitengo cha upasuaji, nikiwa chini yake ndani ya kitengo hicho kwa miaka mitatu niliyotumikia pale. Hivyo, nikamwambia asiwe na shaka, ningefika hospitalini upesi kuanza kazi tena. Kukiwa na hali ya uharaka, akaniambia nikifika nitakuta orodha yangu ya wagonjwa hususa iliyoandaliwa ambao walikuwa majeruhi wa matukio ya ajali, akikazia kwamba mmoja wao alikuwa kwenye hatari ya kupoteza maisha baada ya kuanguka kutoka kwenye ghorofa ya kwanza ya jengo fulani huko Kariakoo; usiku wa kuamkia sasa.

Kwa kauli hiyo nikaweka simu pembeni, moja kwa moja bafuni, kisha nikajiandaa haraka ili niondoke. Ilikuwa ni saa kumi na mbili wakati ambao nilifanikiwa kutoka hapo kwangu na kuanza kuisaka Muhimbili. Fikira zangu, kwa asilimia kubwa zilitekwa na jambo hili la sasa nililohitaji kwenda kushughulika nalo, lakini hazikuwa mbali sana kutoka kwenye kisa cha usiku wa jana huko Mbagala. Sikuwa nimesahau kile nilichokiona; Miryam, akishuka kutoka kwenye Range ya kifahari, na akiwa ameendeshwa na mtu fulani ambaye hapana shaka ilikuwa ni mwanaume. Kwa jinsi ambavyo hali ilikuwa baina yetu kwa sasa ingehitajika tu nimwache kidogo, lakini nisingeacha kumfatilia. Ningejua tu hiyo yote ilimaanisha nini.

Wakati nikiwa njiani bado, simu yangu ikaita, na mpigaji akiwa ni Tesha, nikapokea.

"Kaka wa damu, shikamoo?" Tesha akasikika.

Nikatabasamu kiasi na kusema, "Marahaba, kivuruge wa familia."

"Ahahahah... kaka huyoo..."

"Uko poa mdogo?"

"Ah, nasukuma mawimbi bro. Nimesikia ulikuja jana ila ukatukosa..."

"Nani amekwambia?"

"Ankia. Ile mida nilikuwa Tandika, nimerudi saa sita hivi... afu' simu yangu ilizima," akasema.

"Ahaa... sawa. Mbona umenipigia sa'hivi? Kuna tatizo?" nikauliza.

"Hamna tatizo, kwani vibaya?"

"Ah, wewe Tesha asubuhi yote hii uwe macho? Sidhani kama kuna afya," nikamwambia.

"Ahah... eeh, nilikuwa nakucheki nikwambie. Sasa hivi naanza kazi kaka," akasema.

"Kweli? Wapi?"

"Kwenye hoteli ya Sudani pale Temeke, nitakuwa receptionist *****..."

"Hahah... reception si wanawekaga wanawake tu?"

"Ah wapi, hadi wanaume. Tena tutakuwa wanne, wanawake wengine watatu pia, na me HB boy nimeongezwa. Ndo' naelekea huko sa'hivi," akasema.

"Ulisomaga hotel management Tesha?"

"Hamna, connection tu..."

"Nani, dada yako?"

"Happy. Kamenisaidia nikapata hapo, sijui kana bwana wake mwingine Manager hapo?"

Nikatabasamu tu na kusema, "Haya, hongera. Angalau uanze kuingiza pesa."

"Uhakika. Sasa wewe... mbona jana hukuingia ndani? Ankia alipowaambia wakina ma' mkubwa umekuja halafu ukaondoka walihuzunika," Tesha akasema.

Nikatulia kidogo, nami nikamwambia, "Pole kwao, sikuwa na maana mbaya lakini. Kuna dharura tu ilitokea."

"Kwa sababu hukumkuta da' Mimi?"

"Hilo pia."

"Kwa hiyo utarudi leo?"

"Sijajua. Hapa naenda kazini, sijui sana..."

"Ih, ushaanza kwenda hospitali?"

"Ndiyo."

"Kwa hiyo... dah, kaka haya mambo yetu unajua bado tunatakiwa..."

"Ndiyo najua, tutatafuta tu muda mzuri tuongee. Pamoja."

"Wote kama familia?"

"Ndiyo. Nitawatafuta na mama zetu. Naona ni muhimu tufanye hivyo pamoja, ila ndiyo kuwakusanya wote kiujumla maana wengine wanakwepana," nikamwambia.

"Eeeh, najua. We' fanya miujiza yako kaka, nakuelewa. Sijajisikia fresh kabisa yaani ndoa yako na da' Mimi ikatishwe kinamna hii, lakini hamna jinsi yaani..." akasema hivyo.

Nikabaki kimya tu nikimtafakari Miryam.

"Bado hujaongea naye hata kidogo?" akauliza.

"Bado. Bado ana... ana-process. Nimeona nimwache tu kwanza," nikamwambia.

"Hiyo ya kumwacha kwanza imekaa sawa kweli JC?"

"Asa' unafikiri nitafanyaje? Nilivyovijaribu kwa sasa havijafanikiwa, subira muhimu. Ni mpaka awe tayari kuongea," nikaeleza.

"Haya bana. Maamuzi ni yenu kaka," akasema.

"Ndiyo, ni kukubaliana tu, ila... sijui huko kwenu unamwonaje, yaani... yukoje sa'hivi?" nikamuuliza.

"Ameishiwa raha. Haongei na mtu yaani, yaani... hana furaha kabisa. Inahuzunisha mno, inakuwa kama Mariam kapona, afu' sa'hivi ni zamu ya Miryam kuumwa sasa. Dah! Siyo poa," akasema hivyo.

Nikafumba macho kiufupi nikihisi huzuni moyoni, nami nikamuuliza, "Na jana? Alikuwa ameenda wapi ile usiku?"

Akasema, "Sijajua. Nilirudi nikamkuta, na alikuwa chumbani tu huko. Ufanye tu kuja JC kama atakuwepo, au mpigie ma' mkubwa mwongee akwambie kama anakuwepo unakuja mnamshtukiza, mnaongea. Nakujua we' King wa kubembeleza, atatulia tu..."

"Ahah... nimbembeleze dada yetu, eti?"

"Ahahah... dah! Utafikiri mazuri! Pole mwamba, yaani... bado siamini-amini kwa kweli," akasema hivyo.

"Ndiyo maisha tu ndugu yangu. Ngoja tujipe ubize kidogo hali zitulie, then tutaona inakuwaje," nikamwambia hivyo.

"Poa kaka."

"Mariam mzima?" nikauliza.

"Eeeh, na yeye si umeshaongea naye?"

"Hapana, sija... sijamwona yeyote kati yenu toka juzi."

"Aah, Mamu nilimpa... aliniomba namba yako jana alikuwa anataka akusalimie, nikafikiri mmeshaongea," akasema hivyo.

"Labda, sijui... hajanitafuta. Nitumie yake nimsalimie," nikamwambia.

"Poa, baadaye basi," akaaga.

"Poa."

Baada ya kumaliza maongezi hayo, nikatulia zaidi nikiendelea kuendesha huku nikiwaza namna gani ningeweza kurekebisha mambo mengi ndani ya familia yetu, familia ya Miryam, kwa pamoja, na kuona ni jinsi gani uhusiano wangu na huyo mwanamke ungeishia mahala penye amani hata kama pasingekuwa penye kuridhisha. Na hilo suala la Miryam jana, dah! Mhm. Haya. Kidogo tu nikapata ujumbe kutoka kwake Tesha, akiwa amenitumia namba ya Mariam ili nimtafute "mdogo wetu," nami nikaweka hilo pembeni ili nikashughulike na kazi kwanza, kisha ningemtafuta baadaye.

★★

Basi, nikafika zangu hospitalini kwenye saa moja kasoro, na kama ingekuwa kwenye ukawaida wa kuja kazini basi ingesemwa nimechelewa. Kwa ukawaida madaktari hapo tulitakiwa kuwepo kuanzia mida ya saa kumi na mbili alfajiri, tufanye kikao cha kila siku kuangalia maendeleo na nini vifanywe kusitawisha huduma bora kwa kila mmoja wetu, ndiyo kazi zingeanza sasa. Lakini kwa sababu wangu ulikuwa mwito wa dharura kutoka kwenye likizo yangu, hiyo haingekuwa na shida. Cha kwanza ambacho ningetakiwa kushughulika nacho kilikuwa huyo mtu aliyeumia vibaya kwa kuanguka kutoka ghorofani. Vya kumtuliza alipewa, ila mimi ndiyo ningepaswa nimweke sawa kabisa.

Mapokezi ya ujio wangu yalikuwa mazuri kwa wengi niliofahamiana nao hapo, hasa mtoto Latifah. Alifurahi sana alipojua kwamba sasa nilirejea rasmi. Lakini mzee nikawa makini tu, moja kwa moja mpaka kwenye ofisi yangu na kuvaa koti la tabibu, kisha upesi nikaelekea jukumuni. Waliokuwemo theater kusubiri nifike walifurahi pia kuniona, na kazi zikaanza. Jamaa niliyetakiwa kumfanyia upasuaji alikuwa amevunjika mguu na mbavu kadhaa, na kuna mishipa ya damu iliyokuwa imepasukia kwa ndani na hivyo kutakiwa kuchana sehemu nyingi za mwili wake ili kuukarabati vyema. Kwenye upasuaji nilikuwa vizuri, na angalau kwa masaa niliyoendelea na kazi akili yangu ilirudi kwenye ukawaida uliofaa kutokana matatizo yangu ya kihisia kuwekwa kando kwanza.

Kwa hiyo ikawa ni ubize mwingi kiasi, nikitoka hapa kwenda pale, nikiangalia mgonjwa huyu na yule, mpaka mida ya mchana kabla ya kutafuta chakula ndiyo Stella akanitafuta. Yeye pia akiwa ameenda kazini mida ya saa saba mchana, akawa akiuliza ningepata nafasi mida gani kwenda kumwona Evelyn maana aliniulizia sana, nami ndiyo nikamjulisha kuwa tayari nilianza tena kazi, hivyo labda ningepata nafasi jioni ama usiku. Yaani ni kwamba moja kwa moja baada ya kutoka hapa ningekwenda kumwona mtoto, hivyo Stella akakubaliana na hilo na kusema angejitahidi kuwahi pia ili ajiunge nasi. Ingekuwa kukutana kwake.

Basi, kazi zikaendelea baada ya msosi na nini, nikijikuta nimezama kweli kwenye mambo mengi ya huku ambayo kwa hiyo miezi michache niliachana nayo, na kwa kadiri fulani nikatambua kwamba niliyakosa sana. Upasuaji nilioufanya ulihusisha watu watatu ndani ya siku moja, na wote nilifanikiwa kuwasaidia kwa usalama, ikihitajika tu muda kwa wao kuendelea kulazwa ili wapone. Ilipofika mida ya jioni bado nikiwa hapo, nikapata muda wa kutulia kiasi baada ya wagonjwa wa kuja upande wangu kupungua, nami nikaona nitumie muda mfupi kuwasalimu wapendwa wangu.

Wa kwanza akiwa ni Jasmine, nikamjulia hali na kupashwa habari kuhusu namna ambavyo ndoa yake na Kevin ilikuwa kwa sasa, naye akaniambia kila jambo lilikuwa sawa kwa upande wake, na ndiyo alianza kuyazoea malezi ya watoto akiwa mama mpya. Nikampa hongera zake, na alipotaka kuanza kuzungumza kuhusu ishu yangu na Miryam nikamkatisha tu kwa kusema tungeyaongelea baadaye. Hakuwa na neno.

Kweli sikutaka kwa sasa kuongelea hilo kwanza, maana kama nilivyomwambia Tesha ile asubuhi, nilitaka yazungumziwe familia zetu zikiwa pamoja, na ndiyo ambacho nilihitaji kifanyike nikishazungumza kibinafsi na Miryam. Kunikwepa kwake sasa hivi kungetakiwa tu kufikie kikomo, maana ni wengi wangekuwa ndani ya kizungumkuti kwenye ni nini kifuate endapo kama tusingechukua hatua yoyote na kubaki kukwepana tu. Haingetakiwa kuishia hivyo, tulikuwa tumepitia mengi sana pamoja. Na hivyo kufikiria tu hayo mengi kukanifanya nikumbuke kwamba Tesha alinipatia namba zake Mariam ile asubuhi, nami nikaamua nimtafute sasa kumjulia hali "mdogo wangu."

Nilipoiangalia namba yake Mariam, nikagundua kuwa tayari ilikuwa imepiga kwangu, jana ile, na ndiyo nikatambua ni wakati ule nipo matembezi na Evelyn niliona ikinipigia ila nikapuuzia. Kumbe kweli Mariam alijaribu kunitafuta, na hivyo ingebidi nimcheki pia maana huenda jana alihisi sitaki kuongea naye. Nilipokuwa tu nataka kumpigia, ujumbe ukaingia simuni, mbali na matarajio yangu yote kabisa ukiwa umetoka kwa Miryam! Nikaachana na namba ya Mariam na kuufungua ujumbe huo upesi, kukuta ameniambia; Njoo tuongee. Niko kazini kwangu.

Kwa sekunde chache nikabaki nikiutazama ujumbe huo, nikianza kukumbukia ni mara ngapi nilizokuwa nimejaribu kumtafuta bila kujibiwa, na ile ishu yake ya jana usiku, kwa hiyo kiukweli niliuchukulia ujumbe huo kwa uzito sana maana ni mengi mno tulihitaji kuongelea. Sikuona hata haja ya kumjibu kwa ujumbe, alieleweka vizuri. Nikanyanyuka tu na kuweka simu mfukoni, kisha nikaondoka hospitalini hapo upesi nikiacha taarifa ya kutokuwepo kwa muda mfupi, kisha ningerejea tena.

★★

Mwendo ukawa ni mmoja tu, kuelekea huko Kijichi, kumwona mpen... ah, hapana. Kumwona dada yangu mpenzi. Hali zisingekuwa zimebadilika namna hii basi ningeelekea huko nikiwa na furaha, lakini hali ya ukakasi ndani ya moyo ndiyo iliyokuwa imenijaa. Nilitarajia mazungumzo yangu na Miryam yawe mazito sana, lakini nisingelazimisha lolote lile kutoka kwenye hisia zangu kwenda kwake yeye. Yaani, ningetanguliza kile ambacho yeye angeona kuwa sahihi kufanywa kutokea hapa na kusonga mbele, lakini ningemsihi yeye pia aelewe nilivyohisi ili tuweze kusawazisha mambo mengi kati yetu vizuri zaidi.

Nimefika hapo Kijichi ikiwa ni saa kumi na mbili kasoro, nami nikaridhika kuliona gari lake Miryam nje ya duka lake. Labda nilitakiwa kutarajia kulikuta lile gari la Range lililomshusha jana usiku na hapo eh? La, sasa hivi hakuiacha Mark X yake mpya nyumbani, kwa hiyo bila shaka ingekuwa mimi na yeye tu kuongea bila bughudhi. Basi, nikasogeza Mazda yangu kulifikia duka lake na kushuka, na kwa hakika niliweza kumwona Soraya akiwa kwa ndani pale. Alionekana kuhesabu-hesabu maboksi sijui, na kwa nje kulikuwa na vijana wa kiume wawili walioketi viti vya kusubiri huku wananitazama nilipoikaribia milango. Nikawasalimu kirafiki tu na wao kuniitikia vyema, nami nikachoma ndani.

Soraya alipogeuza shingo na kuniona, akaachia tabasamu kwa furaha na kunigeukia kabisa. Nikamkaribia huku nikitabasamu kiasi pia, naye akasema, "Karibu."

"Asante. Mambo vipi?" nikamjibu.

"Safi. Za kuadimika?"

"Nipo mbona? Wewe ndiyo umepotea sana, mpaka nilisahau unafananaje..."

"Ahahah... JC bwana!" akafurahi.

Nikatabasamu pia na kumwambia, "Ila nimekukumbuka kweli. Unaendeleaje?"

"Me niko poa tu," akasema.

"Si ndiyo mida ya kuondoka hii?"

"Eeh, namalizia tu hapa... ndiyo naenda. Umekuja kumwona da' Miryam?" akauliza.

Nikatikisa nyusi kukubali.

Soraya akaikunja midomo yake kwa njia ya kucheka kwa kuhukumu, naye akasema, "Yupo ndani, nenda."

"Mbona umefanya hivyo?" nikamuuliza.

"Nimefanya nini?" akaniuliza pia.

Nikamkazia macho.

"Me nimefanya nini jamani?" akauliza tena huku akitabasamu.

Nikaiga kufanya midomo jinsi alivyokuwa amefanya, naye akacheka kidogo kwa haya.

"Sijafanya hivyo bwana..." akasema.

"Wala hauna sababu ya kujieleza. Najua. Sikuwa mwazi kuhusu mimi na Miryam, ila...."

"JC, usijali. Naelewa," akanikatisha kwa kusema hivyo.

Nikatulia tu nikiendelea kutazama uso wake mzuri.

"Nenda tu, usiwaze kuhusu mimi. Leo dada ana mikutano mingi na watu wake," akasema hivyo na kuendelea kuyaangalia maboksi.

"Watu gani?" nikamuuliza.

"Wamekuja wengi leo, wateja, rafiki... Tesha ameondoka muda siyo mrefu," akaniambia.

"Tesha alikuwepo hapa?" nikauliza.

"Eeh, kama dakika ishirini tu katoka na we' umefika. Na yeye sasa hivi ameshaanza kazi huko Temeke, alikwambia?"

"Ndiyo, ameniambia."

"Mmm, kaja kumwona dada yake ndiyo akarudi kazini," Soraya akasema.

Nikatulia kidogo nikiangalia mlango wa ofisi yake Miryam.

Soraya akanitazama tena, naye akauliza, "Vipi? Unaingia au?"

Nikamwangalia tu na kutikisa kichwa kukubali, nami nikajitoa hapo taratibu na kuelekea mlangoni pale. Haikuhitaji nisukumwe wala nini, nikabenjua kitasa na moja kwa moja kuingia ndani humo. Aisee!

Miryam aliketi mezani kwake, siyo kitini, kwenye meza kabisa kama kaiegamia, akiwa anasoma jambo fulani kwenye karatasi zilizobebwa ndani ya kablasha pana aliloshika mikononi. Kunyanyua kwake macho na kuniona nilipoingia ndani hapo kukamshtua kiasi kwamba kablasha hilo likatetemeka kiasi mikononi mwake nusu limponyoke, lakini akaweza kulidhibiti lisianguke na yeye kuamua kusimama kabisa.

Hisia niliyopata baada ya kumwangalia kwa ukaribu huo ilikuwa nzuri sana, yaani ni kana kwamba sikuwa nimekutana naye kwa muda mrefu kweli. Na alipendeza, kwa mwonekano wake tu wa kawaida, lakini kwa macho yangu alipendeza mno. Nikajaribu kumpa tabasamu hafifu kuonyesha jinsi nilivyofurahi kumwona, lakini Miryam akaweka sura yenye kutatizika na kufunga kablasha lake, kisha akaliweka mezani na kugeukia upande mwingine wa ofisi yake kwa kilichoonekana kutotaka kunitazama zaidi. Inawezekana bado alivurugika kihisia, na mimi kuwa hapa ndiyo ningetakiwa kumtuliza zaidi. Kwa hiyo nikaufunga mlango na kusogea upande wake, naye akageuza shingo yake nyuma kiasi kuona nilipomkaribia, halafu akapiga hatua chache mbele zaidi kama kuniepuka.

Ikanibidi nitulie, nikimtazama kwa hisia sana, nami nikasema, "Za saa hizi?"

Miryam akabaki kimya.

Aliendelea tu kutazama upande wa dirisha humo ndani, nami nikamwambia, "Najua ndiyo mnakaribia kufunga, ni vizuri sijachelewa sana. Unaendeleaje?"

Bado, akaendelea kufunga mdomo.

Nikamwambia, "Miryam, at some point unajua utahitaji kuzungumza, na mimi..."

"Sipo tayari kuongea kwa sasa," akanikatisha kwa kusema hivyo.

Nikakunja uso kimaswali. "Unamaanisha nini?" nikamuuliza.

"Namaanisha siwezi kuongea sasa hivi. Naomba uende," akasema hivyo.

Nikatikisa kichwa kwa kutoelewa, nami nikamuuliza, "Umeniita ili uje kuniambia niondoke?"

Akageuza shingo yake kiasi na kuuliza, "Nini?"

"Si umeniambia nije tuongee?" nikasema.

Akanigeukia vizuri zaidi na kuuliza, "Saa ngapi?"

Ikanibidi niitoe simu yangu mfukoni, nikaweka upande wa sms aliyonitumia na kumwonyesha.

Miryam, baada ya kuuona ujumbe huo, akafumba macho kiufupi na kutikisa kichwa kama anasikitika vile, na kwa sauti ya chini akasema, "Tesha."

"Kwamba?" nikauliza.

Akaniangalia na kusema, "Tesha alikuwa hapa. Alishika simu yangu... nafikiri yeye ndiyo amekutumia hiyo. Siyo mimi niliyekuita."

Nikatulia kidogo na kupiga ulimi kiasi, nami nikarudisha simu mfukoni na kusema, "Well... haijalishi Miryam. Mimi na wewe tunahitaji kuongea. Nakutafuta sana lakini unanikaushia tu."

Akatazama pembeni tena.

"Kwa nini unanikwepa?" nikamuuliza.

"Nina mambo mengi sasa hivi, nina..."

"Mambo gani?"

"Kuna kazi nazifanya, nataka kuondoka sasa hivi, siwezi... siwezi kuongea sasa hivi, wewe nenda tu, tuta..."

Nikamsogelea karibu zaidi na kusimama mbele ya uso wake, naye akabaki kuniangalia usoni kwa njia ya kujihami.

"Kwa nini unakuwa hivi?" nikamuuliza kwa sauti ya chini na kwa upole sana.

Akataka kujirudisha nyuma, lakini nikaishika mikono yake kwa pamoja na kumng'ang'aniza atulie hapo hapo.

"Kwa nini hutaki tuongee? Unafikiri tutayasuluhishaje yaliyotokea ukiendelea kuwa namna hii? Eh?" nikamsemesha kwa njia yenye upole.

Akawa hataki kunitazama machoni.

"Unasikia nachokuuliza Miryam?"

"Nimekwambia siko tayari bado ku...."

"Tayari ya nini? Unataka ujiandaeje, uvae shela ndiyo tuongee sasa, au?" nikaongea kwa hisia makini.

Akanitazama machoni kimkazo.

Nikamsogeza karibu zaidi ya uso wangu na kumwambia, "Mimi... tafadhali. Naomba uelewe kwamba siyo wewe peke yako unayeumia, tumeumia sote. Unavyofanya hivi... unaniongezea maumivu. Kwa nini?"

Nilimsemesha kwa hisia nyingi za upendo, wazi wazi kabisa, naye akawa akiniangalia kwa hisia pia. Niliweza kuona namna ambavyo bado Miryam alinipenda, macho yake tu, na hiyo kiukweli ikanipa wakati mgumu kudhibiti hisia nilizokuwa nazo kumwelekea yeye pia. Kuwa karibu naye namna hii, kukafanya nimshike shavuni, nikiwa nimelikosa sana penzi lake lililokuwa limekita mizizi kwelikweli moyoni mwangu, japo kulikosa kwa siku chache tu, nasi tukaanza kuikaribisha midomo yetu kwa pamoja kutokana na hamu kubwa iliyopanda baina yetu. Lakini Miryam akiwa mwanamke awaye yeye, akakisukuma kiganja changu na kujitoa haraka kwenye mikono yangu, naye akanipita na kuulelekea mlango. Nikamgeukia kukuta ameushika na kuufungua upesi, halafu akasimama hapo na kuangalia pembeni tu.

Kisha akasema, "Sipo tayari. Kwa sasa, naomba uende. Tutaongea wakati mwingine."

Nikiwa namwangalia kwa hisia, nikamuuliza, "Lini?"

Akaniangalia.

"Siondoki mpaka nipate uhakika kwa maneno yako mwenyewe. Utakuwa tayari lini, na tutaongea lini?"

Akatazama pembeni tena, naye akasema, "Kesho."

Sikutarajia aseme hivyo, lakini ingawa jibu lake lilitoka kinagaubaga tu, mimi kwangu likawa limetiwa muhuri.

Nikasema, "Sawa. Kesho. Wapi?"

Akabaki kimya.

"Nitakuja hapa bas...."

"No," akanikatisha.

Nikatulia.

"Tutawasiliana tu, tutapanga. Naomba uende," akaniambia.

Mh? Mhm.

Mwamba nikatikisa kichwa kukubaliana na hilo, na hapo bado nilikuwa nimekabwa na presha ya kitendo kilichokuwa karibu kutokea baina yangu mimi na yeye muda mfupi nyuma, nami nikaona nimpe tu alichoniomba kwa sasa. Nikapiga hatua chache na kufika mlangoni, nikasimama kwa ufupi kumtazama kwanza, na yeye asitake tena kuniangalia. Sijui labda haya yote yaliyotupata yalikuwa ni makosa yangu? Yaani alinitendea kana kwamba ndiyo ilikuwa hivyo. Mimi bwana nikaona niwe mpole tu, kwa kuwa aliitoa ahadi ya kuongea nami na siku akaipanga, isingekuwa na shida. Nikajiondokea hapo hatimaye, nikiwa nimeshaanza kuomba kwa Mungu hiyo kesho iwadie ili tumalizane na mambo haya yote yaliyoliletea penzi letu utata.






★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★


WhatsApp +255 678 017 280
 
Festo is back 😂🔥
Anaendelea alipoishia ...
Moto unaanza upya, huku Festo kule Diana

Stella nae anakuja Kasi 😂, JC atapasha kiporo sio muda

Ila Tesha..bonge la midfielder kisheti 😂🔥
Tesha ni mwana Sana yaani alifanya mambo magumu yawe simple tu, hawa ndo watu tunahitaji kwenye cycle zetu😃😃😃
 
Back
Top Bottom