MIMI NA MIMI 3
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Siri, Tamaa, Hila, Usaliti, Ukatili, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA TATU
★★★★★★★★★★★★★
Kwa sababu fulani sikutaka nianze kuhukumu mambo kwa njia ambayo huenda ingenifanya nitende bila busara. Nilimjua Miryam vizuri. Hakuwa wa tabia za... yaani... aisee! Mbona ingekuwa ngumu sana? Unajua kuna vitu vingine hutokea kwa njia ambayo huenda ukafikiri ni kinagaubaga, lakini kwa hali hii nilihisi utofauti wa hali ya juu. Kwamba itokee jam ya magari, nitulie hapo mpaka nije kuona jambo hilo, ilikuwa kana kwamba Mungu alitaka kunionyesha kitu fulani. Lakini nini?
Nisingeweza kamwe kuwazia kwamba Miryam wangu angeenda nje ya mahusiano yetu ndani ya siku moja tu tangu tumepatwa na matatizo, lakini hiyo ilikuwa ni alama kubwa sana kuupuuzia uwezekano huo. Lakini hapana, sikutakiwa kuwaza hivyo, labda hata ilikuwa rafiki aliyemleta hapo, huenda walikutana tu leo leo na sasa ndiyo akarudishwa nyumbani. Hivyo. Au? Hapana. Yaani bado nilihisi kutangatanga sana kiakili.
Macho bado yaliikuwa mbele kana kwamba natazama kwa umakini msongamano ule wa magari, lakini akili yangu ilikuwa kwingine kabisa. Nikiwa ndani ya mzubao huo, simu yangu ikaanza kuita, nami nikaangalia mpigaji kukuta ni Stella. Nikapokea, na mwanamke huyo alitaka kuelewa sababu iliyofanya niache kuzungumza ghafla mpaka kumtia wasiwasi, akiuliza kiutani labda ni Miryam alinikuta naongea naye ndiyo kivumbi kikawaka huku, lakini nikamwambia hapana, kuna ishu tu ilizuka na nilihitaji kushughulika nayo upesi. Kwa hilo akawa hana neno, nasi tukaagana kwa kuahidiana kuendelea kuwasiliana.
Baada ya hapo, akili ikarudi kule kule. Ningefanya nini endapo kama jambo nililojionea muda mfupi nyuma lilikuwa na maana hasi? Nikabofya kioo cha simu kumpigia Miryam, ikaita, hakupokea. Nikarudia kufanya hivyo mara mbili zaidi, ikawa vile vile. Ahaa? Nikaweka simu pembeni. Msongamano wa magari sasa uliachia kiasi, nami nikawasha gari na kukanyaga mafuta kuelekea huko nilikotoka. Inaonekana penzi langu liliingiwa na dosari mpya zaidi tu ya ile niliyodhani ndiyo tatizo lenyewe, na kutokea hapo ningefanya kila niwezalo kujua ni nini, na ninadili nalo jinsi gani.
★★★
Siku hiyo ikapita, hii ikiwa ni Jumanne kwa umapema wa alfajiri nilioamshwa kwa mwito wa simu yangu. Nikiwa kitandani nyumbani kwangu, nikaichukua simu kukuta mpigaji ni mmoja wa madaktari wakuu pale hospitali ya Muhimbili, nami nikapokea huku bado nikihisi usingizi. Taarifa aliyonipatia sasa ikanifanya niwe makini zaidi, kwa sababu alinijulisha kwamba ningetakiwa kufika hospitali upesi kuendelea na majukumu kutokana na hali za kidharula zilizohitaji stadi zangu ili nisaidie wagonjwa. Nikamweleza kwamba tayari niliambiwa kuhusu kurudi na sikuwa nimeamua kuja leo bado maana nilikuwa na uchaguzi wa siku ambayo ningeweza kuja ndani ya wiki hii, lakini sasa mambo yakabadilika. Ningetakiwa niingie kazini upesi, kwa kuwa uhitaji uliongezeka.
JC hapo sikuwa na neno, maana nilielewa lazima kuwepo na hali zisizo nzuri sana na kweli ningetakiwa kuwepo kusaidia. Huyo alikuwa mkuu wa madaktari wa kitengo cha upasuaji, nikiwa chini yake ndani ya kitengo hicho kwa miaka mitatu niliyotumikia pale. Hivyo, nikamwambia asiwe na shaka, ningefika hospitalini upesi kuanza kazi tena. Kukiwa na hali ya uharaka, akaniambia nikifika nitakuta orodha yangu ya wagonjwa hususa iliyoandaliwa ambao walikuwa majeruhi wa matukio ya ajali, akikazia kwamba mmoja wao alikuwa kwenye hatari ya kupoteza maisha baada ya kuanguka kutoka kwenye ghorofa ya kwanza ya jengo fulani huko Kariakoo; usiku wa kuamkia sasa.
Kwa kauli hiyo nikaweka simu pembeni, moja kwa moja bafuni, kisha nikajiandaa haraka ili niondoke. Ilikuwa ni saa kumi na mbili wakati ambao nilifanikiwa kutoka hapo kwangu na kuanza kuisaka Muhimbili. Fikira zangu, kwa asilimia kubwa zilitekwa na jambo hili la sasa nililohitaji kwenda kushughulika nalo, lakini hazikuwa mbali sana kutoka kwenye kisa cha usiku wa jana huko Mbagala. Sikuwa nimesahau kile nilichokiona; Miryam, akishuka kutoka kwenye Range ya kifahari, na akiwa ameendeshwa na mtu fulani ambaye hapana shaka ilikuwa ni mwanaume. Kwa jinsi ambavyo hali ilikuwa baina yetu kwa sasa ingehitajika tu nimwache kidogo, lakini nisingeacha kumfatilia. Ningejua tu hiyo yote ilimaanisha nini.
Wakati nikiwa njiani bado, simu yangu ikaita, na mpigaji akiwa ni Tesha, nikapokea.
"Kaka wa damu, shikamoo?" Tesha akasikika.
Nikatabasamu kiasi na kusema, "Marahaba, kivuruge wa familia."
"Ahahahah... kaka huyoo..."
"Uko poa mdogo?"
"Ah, nasukuma mawimbi bro. Nimesikia ulikuja jana ila ukatukosa..."
"Nani amekwambia?"
"Ankia. Ile mida nilikuwa Tandika, nimerudi saa sita hivi... afu' simu yangu ilizima," akasema.
"Ahaa... sawa. Mbona umenipigia sa'hivi? Kuna tatizo?" nikauliza.
"Hamna tatizo, kwani vibaya?"
"Ah, wewe Tesha asubuhi yote hii uwe macho? Sidhani kama kuna afya," nikamwambia.
"Ahah... eeh, nilikuwa nakucheki nikwambie. Sasa hivi naanza kazi kaka," akasema.
"Kweli? Wapi?"
"Kwenye hoteli ya Sudani pale Temeke, nitakuwa receptionist *****..."
"Hahah... reception si wanawekaga wanawake tu?"
"Ah wapi, hadi wanaume. Tena tutakuwa wanne, wanawake wengine watatu pia, na me HB boy nimeongezwa. Ndo' naelekea huko sa'hivi," akasema.
"Ulisomaga hotel management Tesha?"
"Hamna, connection tu..."
"Nani, dada yako?"
"Happy. Kamenisaidia nikapata hapo, sijui kana bwana wake mwingine Manager hapo?"
Nikatabasamu tu na kusema, "Haya, hongera. Angalau uanze kuingiza pesa."
"Uhakika. Sasa wewe... mbona jana hukuingia ndani? Ankia alipowaambia wakina ma' mkubwa umekuja halafu ukaondoka walihuzunika," Tesha akasema.
Nikatulia kidogo, nami nikamwambia, "Pole kwao, sikuwa na maana mbaya lakini. Kuna dharura tu ilitokea."
"Kwa sababu hukumkuta da' Mimi?"
"Hilo pia."
"Kwa hiyo utarudi leo?"
"Sijajua. Hapa naenda kazini, sijui sana..."
"Ih, ushaanza kwenda hospitali?"
"Ndiyo."
"Kwa hiyo... dah, kaka haya mambo yetu unajua bado tunatakiwa..."
"Ndiyo najua, tutatafuta tu muda mzuri tuongee. Pamoja."
"Wote kama familia?"
"Ndiyo. Nitawatafuta na mama zetu. Naona ni muhimu tufanye hivyo pamoja, ila ndiyo kuwakusanya wote kiujumla maana wengine wanakwepana," nikamwambia.
"Eeeh, najua. We' fanya miujiza yako kaka, nakuelewa. Sijajisikia fresh kabisa yaani ndoa yako na da' Mimi ikatishwe kinamna hii, lakini hamna jinsi yaani..." akasema hivyo.
Nikabaki kimya tu nikimtafakari Miryam.
"Bado hujaongea naye hata kidogo?" akauliza.
"Bado. Bado ana... ana-process. Nimeona nimwache tu kwanza," nikamwambia.
"Hiyo ya kumwacha kwanza imekaa sawa kweli JC?"
"Asa' unafikiri nitafanyaje? Nilivyovijaribu kwa sasa havijafanikiwa, subira muhimu. Ni mpaka awe tayari kuongea," nikaeleza.
"Haya bana. Maamuzi ni yenu kaka," akasema.
"Ndiyo, ni kukubaliana tu, ila... sijui huko kwenu unamwonaje, yaani... yukoje sa'hivi?" nikamuuliza.
"Ameishiwa raha. Haongei na mtu yaani, yaani... hana furaha kabisa. Inahuzunisha mno, inakuwa kama Mariam kapona, afu' sa'hivi ni zamu ya Miryam kuumwa sasa. Dah! Siyo poa," akasema hivyo.
Nikafumba macho kiufupi nikihisi huzuni moyoni, nami nikamuuliza, "Na jana? Alikuwa ameenda wapi ile usiku?"
Akasema, "Sijajua. Nilirudi nikamkuta, na alikuwa chumbani tu huko. Ufanye tu kuja JC kama atakuwepo, au mpigie ma' mkubwa mwongee akwambie kama anakuwepo unakuja mnamshtukiza, mnaongea. Nakujua we' King wa kubembeleza, atatulia tu..."
"Ahah... nimbembeleze dada yetu, eti?"
"Ahahah... dah! Utafikiri mazuri! Pole mwamba, yaani... bado siamini-amini kwa kweli," akasema hivyo.
"Ndiyo maisha tu ndugu yangu. Ngoja tujipe ubize kidogo hali zitulie, then tutaona inakuwaje," nikamwambia hivyo.
"Poa kaka."
"Mariam mzima?" nikauliza.
"Eeeh, na yeye si umeshaongea naye?"
"Hapana, sija... sijamwona yeyote kati yenu toka juzi."
"Aah, Mamu nilimpa... aliniomba namba yako jana alikuwa anataka akusalimie, nikafikiri mmeshaongea," akasema hivyo.
"Labda, sijui... hajanitafuta. Nitumie yake nimsalimie," nikamwambia.
"Poa, baadaye basi," akaaga.
"Poa."
Baada ya kumaliza maongezi hayo, nikatulia zaidi nikiendelea kuendesha huku nikiwaza namna gani ningeweza kurekebisha mambo mengi ndani ya familia yetu, familia ya Miryam, kwa pamoja, na kuona ni jinsi gani uhusiano wangu na huyo mwanamke ungeishia mahala penye amani hata kama pasingekuwa penye kuridhisha. Na hilo suala la Miryam jana, dah! Mhm. Haya. Kidogo tu nikapata ujumbe kutoka kwake Tesha, akiwa amenitumia namba ya Mariam ili nimtafute "mdogo wetu," nami nikaweka hilo pembeni ili nikashughulike na kazi kwanza, kisha ningemtafuta baadaye.
★★
Basi, nikafika zangu hospitalini kwenye saa moja kasoro, na kama ingekuwa kwenye ukawaida wa kuja kazini basi ingesemwa nimechelewa. Kwa ukawaida madaktari hapo tulitakiwa kuwepo kuanzia mida ya saa kumi na mbili alfajiri, tufanye kikao cha kila siku kuangalia maendeleo na nini vifanywe kusitawisha huduma bora kwa kila mmoja wetu, ndiyo kazi zingeanza sasa. Lakini kwa sababu wangu ulikuwa mwito wa dharura kutoka kwenye likizo yangu, hiyo haingekuwa na shida. Cha kwanza ambacho ningetakiwa kushughulika nacho kilikuwa huyo mtu aliyeumia vibaya kwa kuanguka kutoka ghorofani. Vya kumtuliza alipewa, ila mimi ndiyo ningepaswa nimweke sawa kabisa.
Mapokezi ya ujio wangu yalikuwa mazuri kwa wengi niliofahamiana nao hapo, hasa mtoto Latifah. Alifurahi sana alipojua kwamba sasa nilirejea rasmi. Lakini mzee nikawa makini tu, moja kwa moja mpaka kwenye ofisi yangu na kuvaa koti la tabibu, kisha upesi nikaelekea jukumuni. Waliokuwemo theater kusubiri nifike walifurahi pia kuniona, na kazi zikaanza. Jamaa niliyetakiwa kumfanyia upasuaji alikuwa amevunjika mguu na mbavu kadhaa, na kuna mishipa ya damu iliyokuwa imepasukia kwa ndani na hivyo kutakiwa kuchana sehemu nyingi za mwili wake ili kuukarabati vyema. Kwenye upasuaji nilikuwa vizuri, na angalau kwa masaa niliyoendelea na kazi akili yangu ilirudi kwenye ukawaida uliofaa kutokana matatizo yangu ya kihisia kuwekwa kando kwanza.
Kwa hiyo ikawa ni ubize mwingi kiasi, nikitoka hapa kwenda pale, nikiangalia mgonjwa huyu na yule, mpaka mida ya mchana kabla ya kutafuta chakula ndiyo Stella akanitafuta. Yeye pia akiwa ameenda kazini mida ya saa saba mchana, akawa akiuliza ningepata nafasi mida gani kwenda kumwona Evelyn maana aliniulizia sana, nami ndiyo nikamjulisha kuwa tayari nilianza tena kazi, hivyo labda ningepata nafasi jioni ama usiku. Yaani ni kwamba moja kwa moja baada ya kutoka hapa ningekwenda kumwona mtoto, hivyo Stella akakubaliana na hilo na kusema angejitahidi kuwahi pia ili ajiunge nasi. Ingekuwa kukutana kwake.
Basi, kazi zikaendelea baada ya msosi na nini, nikijikuta nimezama kweli kwenye mambo mengi ya huku ambayo kwa hiyo miezi michache niliachana nayo, na kwa kadiri fulani nikatambua kwamba niliyakosa sana. Upasuaji nilioufanya ulihusisha watu watatu ndani ya siku moja, na wote nilifanikiwa kuwasaidia kwa usalama, ikihitajika tu muda kwa wao kuendelea kulazwa ili wapone. Ilipofika mida ya jioni bado nikiwa hapo, nikapata muda wa kutulia kiasi baada ya wagonjwa wa kuja upande wangu kupungua, nami nikaona nitumie muda mfupi kuwasalimu wapendwa wangu.
Wa kwanza akiwa ni Jasmine, nikamjulia hali na kupashwa habari kuhusu namna ambavyo ndoa yake na Kevin ilikuwa kwa sasa, naye akaniambia kila jambo lilikuwa sawa kwa upande wake, na ndiyo alianza kuyazoea malezi ya watoto akiwa mama mpya. Nikampa hongera zake, na alipotaka kuanza kuzungumza kuhusu ishu yangu na Miryam nikamkatisha tu kwa kusema tungeyaongelea baadaye. Hakuwa na neno.
Kweli sikutaka kwa sasa kuongelea hilo kwanza, maana kama nilivyomwambia Tesha ile asubuhi, nilitaka yazungumziwe familia zetu zikiwa pamoja, na ndiyo ambacho nilihitaji kifanyike nikishazungumza kibinafsi na Miryam. Kunikwepa kwake sasa hivi kungetakiwa tu kufikie kikomo, maana ni wengi wangekuwa ndani ya kizungumkuti kwenye ni nini kifuate endapo kama tusingechukua hatua yoyote na kubaki kukwepana tu. Haingetakiwa kuishia hivyo, tulikuwa tumepitia mengi sana pamoja. Na hivyo kufikiria tu hayo mengi kukanifanya nikumbuke kwamba Tesha alinipatia namba zake Mariam ile asubuhi, nami nikaamua nimtafute sasa kumjulia hali "mdogo wangu."
Nilipoiangalia namba yake Mariam, nikagundua kuwa tayari ilikuwa imepiga kwangu, jana ile, na ndiyo nikatambua ni wakati ule nipo matembezi na Evelyn niliona ikinipigia ila nikapuuzia. Kumbe kweli Mariam alijaribu kunitafuta, na hivyo ingebidi nimcheki pia maana huenda jana alihisi sitaki kuongea naye. Nilipokuwa tu nataka kumpigia, ujumbe ukaingia simuni, mbali na matarajio yangu yote kabisa ukiwa umetoka kwa Miryam! Nikaachana na namba ya Mariam na kuufungua ujumbe huo upesi, kukuta ameniambia; Njoo tuongee. Niko kazini kwangu.
Kwa sekunde chache nikabaki nikiutazama ujumbe huo, nikianza kukumbukia ni mara ngapi nilizokuwa nimejaribu kumtafuta bila kujibiwa, na ile ishu yake ya jana usiku, kwa hiyo kiukweli niliuchukulia ujumbe huo kwa uzito sana maana ni mengi mno tulihitaji kuongelea. Sikuona hata haja ya kumjibu kwa ujumbe, alieleweka vizuri. Nikanyanyuka tu na kuweka simu mfukoni, kisha nikaondoka hospitalini hapo upesi nikiacha taarifa ya kutokuwepo kwa muda mfupi, kisha ningerejea tena.
★★
Mwendo ukawa ni mmoja tu, kuelekea huko Kijichi, kumwona mpen... ah, hapana. Kumwona dada yangu mpenzi. Hali zisingekuwa zimebadilika namna hii basi ningeelekea huko nikiwa na furaha, lakini hali ya ukakasi ndani ya moyo ndiyo iliyokuwa imenijaa. Nilitarajia mazungumzo yangu na Miryam yawe mazito sana, lakini nisingelazimisha lolote lile kutoka kwenye hisia zangu kwenda kwake yeye. Yaani, ningetanguliza kile ambacho yeye angeona kuwa sahihi kufanywa kutokea hapa na kusonga mbele, lakini ningemsihi yeye pia aelewe nilivyohisi ili tuweze kusawazisha mambo mengi kati yetu vizuri zaidi.
Nimefika hapo Kijichi ikiwa ni saa kumi na mbili kasoro, nami nikaridhika kuliona gari lake Miryam nje ya duka lake. Labda nilitakiwa kutarajia kulikuta lile gari la Range lililomshusha jana usiku na hapo eh? La, sasa hivi hakuiacha Mark X yake mpya nyumbani, kwa hiyo bila shaka ingekuwa mimi na yeye tu kuongea bila bughudhi. Basi, nikasogeza Mazda yangu kulifikia duka lake na kushuka, na kwa hakika niliweza kumwona Soraya akiwa kwa ndani pale. Alionekana kuhesabu-hesabu maboksi sijui, na kwa nje kulikuwa na vijana wa kiume wawili walioketi viti vya kusubiri huku wananitazama nilipoikaribia milango. Nikawasalimu kirafiki tu na wao kuniitikia vyema, nami nikachoma ndani.
Soraya alipogeuza shingo na kuniona, akaachia tabasamu kwa furaha na kunigeukia kabisa. Nikamkaribia huku nikitabasamu kiasi pia, naye akasema, "Karibu."
"Asante. Mambo vipi?" nikamjibu.
"Safi. Za kuadimika?"
"Nipo mbona? Wewe ndiyo umepotea sana, mpaka nilisahau unafananaje..."
"Ahahah... JC bwana!" akafurahi.
Nikatabasamu pia na kumwambia, "Ila nimekukumbuka kweli. Unaendeleaje?"
"Me niko poa tu," akasema.
"Si ndiyo mida ya kuondoka hii?"
"Eeh, namalizia tu hapa... ndiyo naenda. Umekuja kumwona da' Miryam?" akauliza.
Nikatikisa nyusi kukubali.
Soraya akaikunja midomo yake kwa njia ya kucheka kwa kuhukumu, naye akasema, "Yupo ndani, nenda."
"Mbona umefanya hivyo?" nikamuuliza.
"Nimefanya nini?" akaniuliza pia.
Nikamkazia macho.
"Me nimefanya nini jamani?" akauliza tena huku akitabasamu.
Nikaiga kufanya midomo jinsi alivyokuwa amefanya, naye akacheka kidogo kwa haya.
"Sijafanya hivyo bwana..." akasema.
"Wala hauna sababu ya kujieleza. Najua. Sikuwa mwazi kuhusu mimi na Miryam, ila...."
"JC, usijali. Naelewa," akanikatisha kwa kusema hivyo.
Nikatulia tu nikiendelea kutazama uso wake mzuri.
"Nenda tu, usiwaze kuhusu mimi. Leo dada ana mikutano mingi na watu wake," akasema hivyo na kuendelea kuyaangalia maboksi.
"Watu gani?" nikamuuliza.
"Wamekuja wengi leo, wateja, rafiki... Tesha ameondoka muda siyo mrefu," akaniambia.
"Tesha alikuwepo hapa?" nikauliza.
"Eeh, kama dakika ishirini tu katoka na we' umefika. Na yeye sasa hivi ameshaanza kazi huko Temeke, alikwambia?"
"Ndiyo, ameniambia."
"Mmm, kaja kumwona dada yake ndiyo akarudi kazini," Soraya akasema.
Nikatulia kidogo nikiangalia mlango wa ofisi yake Miryam.
Soraya akanitazama tena, naye akauliza, "Vipi? Unaingia au?"
Nikamwangalia tu na kutikisa kichwa kukubali, nami nikajitoa hapo taratibu na kuelekea mlangoni pale. Haikuhitaji nisukumwe wala nini, nikabenjua kitasa na moja kwa moja kuingia ndani humo. Aisee!
Miryam aliketi mezani kwake, siyo kitini, kwenye meza kabisa kama kaiegamia, akiwa anasoma jambo fulani kwenye karatasi zilizobebwa ndani ya kablasha pana aliloshika mikononi. Kunyanyua kwake macho na kuniona nilipoingia ndani hapo kukamshtua kiasi kwamba kablasha hilo likatetemeka kiasi mikononi mwake nusu limponyoke, lakini akaweza kulidhibiti lisianguke na yeye kuamua kusimama kabisa.
Hisia niliyopata baada ya kumwangalia kwa ukaribu huo ilikuwa nzuri sana, yaani ni kana kwamba sikuwa nimekutana naye kwa muda mrefu kweli. Na alipendeza, kwa mwonekano wake tu wa kawaida, lakini kwa macho yangu alipendeza mno. Nikajaribu kumpa tabasamu hafifu kuonyesha jinsi nilivyofurahi kumwona, lakini Miryam akaweka sura yenye kutatizika na kufunga kablasha lake, kisha akaliweka mezani na kugeukia upande mwingine wa ofisi yake kwa kilichoonekana kutotaka kunitazama zaidi. Inawezekana bado alivurugika kihisia, na mimi kuwa hapa ndiyo ningetakiwa kumtuliza zaidi. Kwa hiyo nikaufunga mlango na kusogea upande wake, naye akageuza shingo yake nyuma kiasi kuona nilipomkaribia, halafu akapiga hatua chache mbele zaidi kama kuniepuka.
Ikanibidi nitulie, nikimtazama kwa hisia sana, nami nikasema, "Za saa hizi?"
Miryam akabaki kimya.
Aliendelea tu kutazama upande wa dirisha humo ndani, nami nikamwambia, "Najua ndiyo mnakaribia kufunga, ni vizuri sijachelewa sana. Unaendeleaje?"
Bado, akaendelea kufunga mdomo.
Nikamwambia, "Miryam, at some point unajua utahitaji kuzungumza, na mimi..."
"Sipo tayari kuongea kwa sasa," akanikatisha kwa kusema hivyo.
Nikakunja uso kimaswali. "Unamaanisha nini?" nikamuuliza.
"Namaanisha siwezi kuongea sasa hivi. Naomba uende," akasema hivyo.
Nikatikisa kichwa kwa kutoelewa, nami nikamuuliza, "Umeniita ili uje kuniambia niondoke?"
Akageuza shingo yake kiasi na kuuliza, "Nini?"
"Si umeniambia nije tuongee?" nikasema.
Akanigeukia vizuri zaidi na kuuliza, "Saa ngapi?"
Ikanibidi niitoe simu yangu mfukoni, nikaweka upande wa sms aliyonitumia na kumwonyesha.
Miryam, baada ya kuuona ujumbe huo, akafumba macho kiufupi na kutikisa kichwa kama anasikitika vile, na kwa sauti ya chini akasema, "Tesha."
"Kwamba?" nikauliza.
Akaniangalia na kusema, "Tesha alikuwa hapa. Alishika simu yangu... nafikiri yeye ndiyo amekutumia hiyo. Siyo mimi niliyekuita."
Nikatulia kidogo na kupiga ulimi kiasi, nami nikarudisha simu mfukoni na kusema, "Well... haijalishi Miryam. Mimi na wewe tunahitaji kuongea. Nakutafuta sana lakini unanikaushia tu."
Akatazama pembeni tena.
"Kwa nini unanikwepa?" nikamuuliza.
"Nina mambo mengi sasa hivi, nina..."
"Mambo gani?"
"Kuna kazi nazifanya, nataka kuondoka sasa hivi, siwezi... siwezi kuongea sasa hivi, wewe nenda tu, tuta..."
Nikamsogelea karibu zaidi na kusimama mbele ya uso wake, naye akabaki kuniangalia usoni kwa njia ya kujihami.
"Kwa nini unakuwa hivi?" nikamuuliza kwa sauti ya chini na kwa upole sana.
Akataka kujirudisha nyuma, lakini nikaishika mikono yake kwa pamoja na kumng'ang'aniza atulie hapo hapo.
"Kwa nini hutaki tuongee? Unafikiri tutayasuluhishaje yaliyotokea ukiendelea kuwa namna hii? Eh?" nikamsemesha kwa njia yenye upole.
Akawa hataki kunitazama machoni.
"Unasikia nachokuuliza Miryam?"
"Nimekwambia siko tayari bado ku...."
"Tayari ya nini? Unataka ujiandaeje, uvae shela ndiyo tuongee sasa, au?" nikaongea kwa hisia makini.
Akanitazama machoni kimkazo.
Nikamsogeza karibu zaidi ya uso wangu na kumwambia, "Mimi... tafadhali. Naomba uelewe kwamba siyo wewe peke yako unayeumia, tumeumia sote. Unavyofanya hivi... unaniongezea maumivu. Kwa nini?"
Nilimsemesha kwa hisia nyingi za upendo, wazi wazi kabisa, naye akawa akiniangalia kwa hisia pia. Niliweza kuona namna ambavyo bado Miryam alinipenda, macho yake tu, na hiyo kiukweli ikanipa wakati mgumu kudhibiti hisia nilizokuwa nazo kumwelekea yeye pia. Kuwa karibu naye namna hii, kukafanya nimshike shavuni, nikiwa nimelikosa sana penzi lake lililokuwa limekita mizizi kwelikweli moyoni mwangu, japo kulikosa kwa siku chache tu, nasi tukaanza kuikaribisha midomo yetu kwa pamoja kutokana na hamu kubwa iliyopanda baina yetu. Lakini Miryam akiwa mwanamke awaye yeye, akakisukuma kiganja changu na kujitoa haraka kwenye mikono yangu, naye akanipita na kuulelekea mlango. Nikamgeukia kukuta ameushika na kuufungua upesi, halafu akasimama hapo na kuangalia pembeni tu.
Kisha akasema, "Sipo tayari. Kwa sasa, naomba uende. Tutaongea wakati mwingine."
Nikiwa namwangalia kwa hisia, nikamuuliza, "Lini?"
Akaniangalia.
"Siondoki mpaka nipate uhakika kwa maneno yako mwenyewe. Utakuwa tayari lini, na tutaongea lini?"
Akatazama pembeni tena, naye akasema, "Kesho."
Sikutarajia aseme hivyo, lakini ingawa jibu lake lilitoka kinagaubaga tu, mimi kwangu likawa limetiwa muhuri.
Nikasema, "Sawa. Kesho. Wapi?"
Akabaki kimya.
"Nitakuja hapa bas...."
"No," akanikatisha.
Nikatulia.
"Tutawasiliana tu, tutapanga. Naomba uende," akaniambia.
Mh? Mhm.
Mwamba nikatikisa kichwa kukubaliana na hilo, na hapo bado nilikuwa nimekabwa na presha ya kitendo kilichokuwa karibu kutokea baina yangu mimi na yeye muda mfupi nyuma, nami nikaona nimpe tu alichoniomba kwa sasa. Nikapiga hatua chache na kufika mlangoni, nikasimama kwa ufupi kumtazama kwanza, na yeye asitake tena kuniangalia. Sijui labda haya yote yaliyotupata yalikuwa ni makosa yangu? Yaani alinitendea kana kwamba ndiyo ilikuwa hivyo. Mimi bwana nikaona niwe mpole tu, kwa kuwa aliitoa ahadi ya kuongea nami na siku akaipanga, isingekuwa na shida. Nikajiondokea hapo hatimaye, nikiwa nimeshaanza kuomba kwa Mungu hiyo kesho iwadie ili tumalizane na mambo haya yote yaliyoliletea penzi letu utata.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
WhatsApp +255 678 017 280