SEHEMU YA 23
Jambo la muhimu ni kukutana kwanza na Sauda ambaye atakupa muongozo wa namna ya kushinda vita hii" alielezea Mnaro na hapo nikajikuta najiuliza swali "Sauda ameshindwaje kutoroka huko Muifufu kwa miaka yote hiyo kama kweli anao muongozo?" Niliuliza nikijiambia kama ni kazi ngumu namna hiyo kuondoka Muifufu mbona yeye Mnaro aliweza na kama haiwezekani mimi nitawezaje kuwatoa. "Njia ya kutokea Muifufu ina amrishwa na mtu mmoja tu kufunguka naye ni Magugi, mimi nilikuwa na uwezo huo ambao nilipewa na Magugi kama msaidizi wake ambaye alikuwa akiniamini, baada ya kumuasi nilifutiwa Mamlaka hayo. Nimeishi nikijifunza namna ambavyo naweza kuingia Muifufu mpaka nimefanikiwa lakini namna ya kutoka bado mtamtegemea Magugi ambaye tukishirikiana na kutumia nyenzo ambazo nimekuonesha lazima tumlazimishe awafungulie njia, najua Sauda pia atakuwa amepata udhaifu ambao tunaweza kuutumia kwa Magugi kwa maana ndio kazi pekee ambayo amekuwa akiifanya huko" alimaliza kunielezea Mnaro nikagundua kuwa nina kibarua kizito sana huko Muifufu lakini sikuwa na budi kwenda kwani ndiko aliko mke wangu kipenzi ambaye nilijiona pungufu bila yeye.
"Lazima pia nikwambie kuwa hakikisha mpenzi wangu anatoka Muifufu. Kama ukifanikiwa kutoa wawili basi ni wewe na yeye, kama akitoka mmoja ni yeye na kama akitoka nusu basi ni nusu yake, sitokuelewa ukirudi hapa bila Sauda na nakuhakikishia furaha unayoitafuta hutoipata kama Sauda hatofanikiwa kutoka, nitayaharibu kabisa maisha yako" alisema Mnaro kwa sauti ya msisitizo mkubwa kiasi cha kuogopesha.
"Sawa mkuu, nitahakikisha Sauda anakuwa na wewe hivi karibuni" nilijibu huku nikitetemeka. Ukweli niliujua moyoni mwangu mwenyewe kuwa kama akitoka mmoja basi ni mke wangu Samia na kama ni wawali basi ni mimi na mke wangu.
"Ninaamini tutafanikiwa kuwatorosha wote, mungu atuwezeshe" alisema Mnaro.
"Sasa safari itakuwa sangapi na itaanzia wapi?" Niliuliza.
"Safari itakuwa alfajiri na nitakufuata na kukusindikiza mpaka ambapo ufanikiwa kuingia" alijibu Mnaro, tukaagana na moshi ule ambao ulikuwa unatoka kwenye kioo kile ukakoma mara moja na Mnaro hakuonekana tena.
Nikabaki nikijaribu kulala lakini sikupata hata usingizi, nikawa nikitizama saa kila wakati kuona kama muda wa safari ulikuwa umefika.
Majira ya saa kumi za alfahiri Mnaro akaja na kunitaka tuanze safari, tukaondoka tukitumia wale paka wetu kama kawaida.
Tukaenda mwendo wa kama nusu saa kisha tukaingia kwenye pori kubwa ambalo sikuwa nimewahi kuliona kabla tukaenda mpaka katikati mwa pori lile kisha tukashuka kwenye usafiri ule wa paka na kusimama pembeni ya mti mkubwa sana. Mnaro akanikabidhi ile Mikufu miwili na kunitaka kuuvaa mmoja na kuutunza vizuri ule mwingine.
"Ukifanikiwa Kuingia utatembea kuelekea mbele kisha utafika kwenye njiapanda ambapo utachagua njia ya kushoto kwako ambayo atapita katikati ya pori, wewe endelea kunyoosha na njia hiyohiyo ambayo itakutoa mpaka nnje ya pori, lakini kukikaribia kutoka nnje ya pori utaona miti ikiwa imepangwa kwa mistari kushoto na kulia kwako wewe ukipita katikati, hakikisha mkufu huyo unauvisha kweye tawi la chini la mti wa kulia kwako ambalo limekatwa na ni fupi tu. Kisha utaendelea na safari mpaka utakutana na makazi ya watu ambamo na wewe utajichanganya na kuishi kama mkazi wa huko mpaka utakapoonana na Sauda" alielezea Mnaro kisha akanikabidhi ule mkoba wake wa ngozi "nadhani unajua kila kilichomo humo na matumizi yake, utatumia kila ambacho unaweza kukuhitaji ukiwa Muifufu. Watu wa huko hawaujui uchawi wa kutumia vitu hivi, wanayajua tu hayo mayai ya bundi" alimaliza kunieleza Mnaro, akiongea kwa upole sana siku hiyo, hata sura yake ilionesha kuwa alikuwa na mtu mwenye hudhuni.
"Wewe ni silaha yangu ya mwisho, ninakutegemea sana katika hili. Tafadhali usiniangushe" alisema Mnaro nami nikamuitikia kwa kichwa tu kisha akapiga magoti chini, akatoa mishumaa minne kutoka mifukoni mwake, akaisimamisha vizuri pale chini, mmoja kulia, mmoja kushoto na mingine mbele na nyuma kisha yeye akawa katikati, akanyoosha mikono juu huku na uso wake akiuelekeza juu lakini alikiwa amefumba macho yake kwanguvu sana, akawa anatamka maneno kwa kunong`ona ila kwa msisitizo sana.
mara mishumaa ile ikawaka, kadri alivyozidi kunongona maneno yale ndivyo mishumaa ile ilivyozidi kutoa mwanga mpaka eneo lote likawa kama mchana, Mnaro nae alikuwa akitokwa jasho jingi sana lakini hakuacha, aliendelea kutamka maneno yake kwa kunong`ona. Ile mishumaa ikaanz kutoa moshi mkubwa ambao uliungana kutoka katika kila mshumaa na kutengeneza uwazi mkubwa kama mlango.
Mnaro akasitisha zoezi lake, akafumbua macho na kunitizama, kisha akatizama ambapo moshi ule ulitengeneza mlango nami nikajikuta nikitupia macho yangu kuangalia mlango ule wa moshi, mlango ule ulionekana kuanz kupungua ukubwa kwa kasi.. "KIMBIAAAAAAAA, PITA HAPO UENDEEEE" alipiga kelele