Simulizi : Nguvu ya Mapenzi

Simulizi : Nguvu ya Mapenzi

SEHEMU YA 17

Siku hiyo usiku watoto wa familia hii waliambiwa kuwa wawahi kulala ili kesho yake wawahi ibadani, basi mama yao akawaambia kuwa kesho wawahi kuamka kwaajili ya kwenda Kanisani basi kila mmoja alienda kulala ambapo Angel alilala hoi kabisa ila Erica alijihisi kutokuwa na usingizi kabisa kwa wakati huo basi alikaa tu chumbani kwake mara Erick nae akaenda chumbani kwa dadake na kuanza kuongea nae,
“Yani mama katufukuza mapema sana kulala, mimi sina hata usingizi”
“Hata mimi sina usingizi jamani”
“Sasa tufanye nini?”
“Tucheze karata”
“Kheee karata umezipata wapi?”
“Usiulize, ngoja nizitoe tucheze”
Basi Erica akatoa karata kisha yeye na kaka yake wakaanza kucheza karata yani walicheza karata hadi usiku sana bila kugundua ni usiku sana, mara mama yao alienda chumbani na kuwashtua,
“Yani nimepita hapa na kushangaa taa inawaka, nikajiuliza huyu Erica hajalala au kasahau kuzima taa au anaogopa, kumbe mnacheza karata nyie wajinga, mnajua saa ngapi saa hizi?”
“Tusamehe mama”
“Tusamehe mama ndio nini, haya Erick inuka nenda chumbani kwako na ulale nakuja kukuangalia muda sio mrefu na wewe Erica lala muda huu sitaki ujinga wa kucheza karata usiku’
Wote walifanya vile ambavyo mama yao alisema kisha mama yao akazima taa na yeye kwenda chumbani kwake kulala huku akilalamika tu.
 
SEHEMU YA 18

Kulipokucha, mama yao aliamka mapema kabisa na kwenda kuwaamsha watoto wake, kiukweli Erick na Erica walikuwa na usingizi sana ila mama yao aliwaambia wajiandae na kwenda ibadani, basi Erick akasema,
“Mama, naomba mimi niende mchana”
“Mjinga wewe, niliwatuma kucheza karata usiku eeeh!”
Pale Angel akasikia habari za wadogo zake kucheza karata ila hakusema neno lolote zaidi zaidi alienda kujiandaa kisha wote watatu wakaondoka na dereva wao sababu wazazi wao walienda na usafiri mwingine.
Walipotoka Kanisani, Erick na Erica walikaa siti ya nyuma na walikuwa wamesinzia huku siti ya mbele akiwa amekaa dereva na Angel, basi dereva akamwambia Angel,
“Yani umependeza leo Angel balaa, kama malaika vile. Asubuhi nilishindwa kukusifia ila kiukweli Angel wewe ni mzuri sana”
“Ushaanza maneno yako, mimi ni mzuri ndio na najitambua kwahiyo sitaki porojo zako”
“Porojo zangu kivipi? Kwakweli Angel unaonyesha mtamu kama jina lako”
“Ila nahisi wewe huipendi hii kazi, unajua siku nikimwambia baba au mama yani wewe ndio basi tena kwenye hii kazi! Sitaki ujinga”
“Basi Angel, ila kiukweli nakupenda sana. Katika maisha yangu sijawahi kuona mwanamke mrembo kama wewe”
Angel alikaa kimya ila muda huo Erica alishtuka na kusema,
“Kheee dada huko si ndio kutongoza, yani anko Ayubu anakutongoza naenda kusema kwa mama”
“Hivi wewe Erica una nini lakini? Unajua kutongoza wewe?”
“Mama alisema mtu akikutongoza basi umwambie, ila mbona wewe hutaki kusema kuhusu anko Ayubu? Mimi nitasema”
Yule dereva aliona aibu kiasi kwamba hakutaka hata kuongea ila alijua ni namna gani Angel anaweza kuongea na wadogo zake.
Walivyofika nyumbani, Angel akatoka na kumvuta pembeni Erica na kuanza kuongea nae,
“Wewe mtoto, huo mdomo wako uufunge. Ni kweli kanitongoza ila kumbuka yule anko ana familia yake, tukimsemea tu kwa wazazi wetu lazima atafukuzwa kazi, tunatakiwa kuwa na huruma, yule anajisemea tu ila usiende kusema kwa mama”
“Mmmh ila sijui”
“Halafu wewe unataka kusema ya watu tu, haya na karata mlizokuwa mnacheza mlizitoa wapi? Nimwambie mama akuulize, unafikiri sikuona wakati ukipewa hizo karata?”
“Basi dada yaishe”
Basi wakaingia ndani na mama yao akaingia na muda huo huo alimuita Angel na kuanza kuongea nae,
“Wewe Angel una ajenda gani na huyo Hanifa? Maana amepiga sana simu, una ajenda gani?”
“Hakuna kitu mama, labda alitaka kuniambia kuhusu kesho shuleni”
“Aaaah eeeh! Ngoja tumpigie na niweke sauti kubwa ili nisikie mazungumzo yenu”
Mara simu ya Angel ilianza kuita pale pale basi mama yake akaichukua na kuiangalia akakuta mpigaji ni Samir, yani mama Angel alipoona hili jina alichukia na kukunja sura kabisa.
 
SEHEMU YA 19

Mara simu ya Angel ilianza kuita pale pale basi mama yake akaichukua na kuiangalia akakuta mpigaji ni Samir, yani mama Angel alipoona hili jina alichukia na kukunja sura kabisa.
Kisha akamuangalia angel na kumuuliza kwa ukali,
“Samir ndio nani? Unamahusiano nae yapi na kwanini amekupigia simu?”
kisha mama Angel aliipokea ile simu na kuweka sauti kubwa kisha kumpa Angel kuongea nayo ile simu, kwakweli Angel aliongea nayo kwa uoga sana,
“Hallow”
“Mbona sauti yako inatetemeka hivyo Angel?”
Angel alikuwa kimya tu kwani alishindwa kusema lolote sababu ya mama yake kisha Samir aliendelea kuongea,
“Au umechukia sababu sikukuongelesha tena! Nilifanya vile sababu ya yule mwalimu, halafu nahisi anakutaka yule, sikutaka aone tukiwasiliana tena, ila nikwambie kitu Angel?”
Angel akakata ile simu kwani alijua mada itakayoendelea pale haitomfurahisha mama yake hata kidogo, ila mama yake alikuwa makini sana kumuangalia kisha akamwambia,
“Mbona umekata? Angel naomba uniambie kila kitu kinachoendelea juu ya huyo Samir kabla sijaenda shuleni kwenu, nieleze kila jambo”
Angel alikaa kimya tu bila ya kusema chochote kisha mama yake akamwambia tena kwa ukali,
“Unanyamaza kimya una maana gani? Umeanza kiburi Angel eeeh! Yani unaongea na mwanaume hapo mbele ya macho yangu halafu unanikalia kimya? Najua unanijua nilivyo, sijali umekuwa kwasasa, naweza kukubutua hapo hadi ukasahau njia ya chumbani kwako”
Mara Erick akatokea na kumwambia mama yao,
“Mama, unaitwa na baba”
Basi akainuka na kumuacha Angel pale sebleni kisha yeye akaenda kuongea na mume wake.
 
SEHEMU YA 20

Mama Angel alifika chumbani na kumkuta mumewe ameshika kitabu tu na kuanza kuongea nae,
“Nimeitikia wito”
“Nimekuita ili tukae wote kidogo, mke wangu hayo malezi yako kwa watoto kwakweli sio malezi”
“Kivipi?”
“Nimekuangalia pale wakati ukiongea na Angel, yani mtoto hadi kakosa amani kabisa, hivi unafikiri kwa hali ile utawezaje kuongea na mtoto?”
“Sikia baba Angel nikwambie, yani mimi sitaki watoto wapiti njia mbaya, au wapiti maisha niliyopitia mimi”
“Kwahiyo wewe umepitia maisha mabaya? Hebu mkumbuke mama yako, alikuwa mkali sana ila je alikuwa mkali kama wewe kwa watoto? Umezidisha mke wangu jamani kwakweli sijapenda”
“Najua umeumia moyo sababu namsema Angel”
“Hata kama, yani hata ungemsema Erick au Erica kwa stahili hiyo lazima ningeumia, hebu kaa vizuri na mtoto umsikilize anasumbuliwa na kitu gani sio kumfokea kiasi kile, unamtisha mtoto kwakweli”
“Ila mume wangu mtoto akiharibikiwa yule, aibu kwa nani?”
“Sasa ukifanya ukali ndio utamuokoa asiharibikiwe? Hebu kuwa kama rafiki yake na umuulize kwa utaratibu akujibu”
“Sawa nimekuelewa mume wangu, ngoja nifanye hivyo ingawa nina hasira sana”
Basi mama Angel alitoka na kurudi tena sebleni ambapo Angel alikuwa amekaa pale pale kwani hata kuinuka alishindwa sababu ya uoga wa maneno ya mama yake, basi mama yake akaanza kumwambia,
“Angel mwanangu, mama anatakiwa kuwa mzazi, mlezi na rafiki wa milele. Usimfiche mama kitu chochote kile kinachokusibu katika maisha, usimdanganye mama jambo lolote lile, sema ukweli ili upone mwanangu. Samir ni nani? Na kwanini anakupigia simu? Na huyo mwalimu imekuwaje?”
Angel hakuwa na namna nyingine zaidi ya kumueleza mama yake ukweli kwani alijua hata angeficha basi mama yake angefukunyua hadi ukweli aujue maana mama yake alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo, basi akaanza kumueleza,
“Mama naomba unisamehe, Samir ni mwanafunzi mwenzangu nasoma nae, nilimpa namba ya simu na nilikuwa nikiwasiliana nae, kuna siku nilijisahau nikaenda na simu shuleni ndio mwalimu Harun akanikamata nayo ila kanirudishia ndio hiyo hapo, naomba unisamehe mama”
“Kwahiyo Samir kakutongoza eeeh!”
“Hapana mama, hajawahi kunitongoza wala kuniambia habari za mapenzi”
“Una uhakika huyo Samir hajawahi kukutongoza?”
Mara Erica akaenda pale na kusema,
“Dada mwambie ukweli mama kuwa anko Ayubu kakutongoza”
Mama yao akashtuka na kuuliza kwa makini,
“Inamaana na Ayubu kakutongoza?”
Kwakweli Angel hakuweza kuficha zaidi na kuamua kusema ukweli tu kisha mama yake akamwambia kuwa akabadili nguo na aweze kula maana alianza kumbana hata kabla hajapumzika kwa siku hiyo.
Kisha mama yake aliinuka moja kwa moja kwenda kwa mumewe na kumueleza kile alichogundua,
“Unaona mume wangu, kumbe na Ayubu nae yupo katika harakati za kutaka kutuharibia mtoto”
“Kivipi?”
Basi akamueleza aliyoambiwa na watoto wake na pale pale mumewe akachukua hatua nae maana hakupenda kusikia kuna ujinga unataka kutendeka kwa watoto wake ingawa hakuwa mkali kwa wanae, akachukua simu yake na kumpigia Ayubu,
“Uje nyumbani uandike ni kiasi gani unatudai kisha uache gari yetu maana kazi tena basi”
“Kwani nimefanyaje mzee?”
“Ukija utatambua hilo”
Kisha ile simu na kumwambia mkewe,
“Hili la Ayubu nitashughulikia, usijali mke wangu”
Basi mkewe alifurahi sana kwani alikuwa akipenda vile ambavyo alishirikiana na mumewe kwa kila kitu.
 
SEHEMU YA 21

Erica aligundua kuwa dada yake amechukia kwa kitendo chake cha kusema kuhusu dereva wao, akaamua kwenda kumuomba msamaha,
“Nisamehe dada, nilipitiwa tu kusema vile”
“Ulipitiwa wapi? Umbea tu, kione vile, toka zako hapa”
Erica akatoka ila alinyong’onyea sana kwani hakupenda kumkwaza dada yake, basi Erick akamfata na kumuuliza kilichomfanya apooze,
“Si nilimwambia mama ukweli kuwa anko Ayubu alikuwa akimtongoza dada Angel”
“Eeeh Erica, hebu niambie kutongoza unaanzaje?”
“Mimi sijui”
“Kama hujui umejuaje kama anko Ayubu alikuwa akimtongoza dada Angel?”
“Sijui, mimi nilikuwa namsikia tu anamsifia basi”
“Kumbe kusifia ndio kutongoza, na ukishatongoza ndio inakuwaje?”
“Sitaki hayo maswali Erick, kamuulize mama”
“Basi, nilikuwa nakuchangamsha akili tu. Twende tukacheze tena karata”
Basi wakaenda chumbani kwa Erica na kuanza kucheza tena karata, walicheza sana karata hata jioni iliwakutia mule mule chumbani wakicheza karata ila Erick alijihisi kuchoka na kuanza kusinzia basi akajiegesha kwenye kitanda cha dada yake na kujilaza pale, naye Erica kuona Erick amelala basi akajikuta nae akilala hoi kabisa.
Mama yao ndio alienda kuwakurupua wakati wa chakula cha usiku, alikuta wamelala hoi kabisa, alitikisa kichwa na kuziona zile karata pembeni, na kusema,
“Yani walikuwa wakicheza karata tena, jamani hawa watoto aah”
Akaanza kuwatingisha ambapo waliamka na kuanza kujinyoosha, kisha mama yao alianza kuwasema,
“Hivi nyie hizi karata ndio kila kitu kwenu, mnajisahau mnacheza karata na kulala hapahapa, kwakweli sijapenda na kuwahakikishia kuwa sijapenda naenda kuchoma hizi karata”
Erica akakurupuka vizuri sasa na kumsihi mama yake asiende kuchoma zile karata,
“Tena msinikere, nendeni mkale, hizi karata naenda kuzichoma”
Kisha mama yao akatoka na zile karata, kiukweli Erica alitoka chumbani ila toka mama yao azichukue zile karata alikosa raha kabisa na kujikuta akiwa na mawazo sana hadi wanamaliza kula na kwenda kulala tena bado alikuwa na mawazo.
 
SEHEMU YA 22

Leo kama kawaida Angel na wadogo zake walikuwa wameenda shule, basi Erica akiwa darasani pamoja na kaka yake Erick, alifatwa pembeni na mwanafunzi mwenzao na kuanza kuongea nae,
“Erica, ziwapi karata zangu?”
“Mmmh nimezisahau nyumbani”
“Ila kumbuka ulisema leo utazileta?”
“Ndio, ila nimezisahau. Samahani”
Erick aliingilia yale mazungumzo kwani hakupenda yule aongee na dada yake, na vile alipojua kuwa dada yake alipewa karata na huyo akajikuta akichukia sana, alimwambia
“Erica asikuongopee, hajasahau karata wala nini bali mama amezichoma moto”
Erica alimuangalia kwa hasira kaka yake kwani hakupenda wala nini ila yule mwanafunzi alimuangalia Erica na kumwambia,
“Usijali kuhusu hilo Erica, nitakuletea karata zingine”
Erick akachukia na kumuangalia kwa hasira yule mwanafunzi na kumwambia,
“Hivi wewe una nini lakini? Yani ndio kwanza shule tumeanza, ila una mambo ya ajabu kichizi”
“Sijasema kwa ubaya, usitake kuniletea kama mambo ya siku ile ya kupigana, hapana mimi nilikuwa naongea na Erica tu”
Kisha yule mwanafunzi akainuka na kwenda kukaa sehemu nyingine, basi Erica akamwambia kaka yake,
“Na nitaenda kuongea na mwalimu atuhamishe madarasa yani wewe sijui ukoje”
“Ndio kamwambie, na nikirudi nyumbani leo na mimi namwambia mama kuwa zile karata ulizitoa kwa Abdi”
Erica alikaa kimya na kumuangalia kaka yake, muda wa mapumziko Erica alienda kumtafuta dada yake na kumueleza ambayo huwa yanatokea darasani,
“Kweli wewe na Erick inatakiwa msome madarasa tofauti, yule nae sijui vipi! Hataki mashemeji au?”
“Mashemeji? Wa nini dada?”
“Aaaah na wewe nawe, ngoja nikaongee na mwalimu awaweke madarasa tofauti’
Basi Angel akamuaga Erica pale na moja kwa moja alienda kuongea na mwalimu wa taaluma sababu ndiye aliyekuwa akipatana nae sana kuliko walimu wote katika shule yao.
Basi alienda kuongea nae kisha mwalimu akamwambia,
“Ni jambo jema ulilosema ila nadhani kama na kidato cha nne tungekuwa na madarasa mawili basi wewe na Samir tungewatenganisha”
“Ila mwalimu Samir sio ndugu yangu”
“Ni kweli, sasa madhara ya mdogo wako Erick na Erica hayawezi fikia madhara ambayo wewe utakumbana nayo kwa Samir, unajua mara nyingine walimu tunaonekana kama tunapiga kelele ila huwa tunaona mbali sana, Angel natamani siku moja nikuone katika maisha mazuri, yani umesoma kwa bidii, umepata kazi nzuri na unaishi vizuri, na mwisho wa siku uolewe na kufurahia maisha ya ndoa ili uheshimike ila sio kuruka ruka na wakina Samir, kwanza huyo Samir atakudanganya tu na kuichanganya akili yako maana hatokuja kukuoa wala nini, watu wazima tunapoongea inapaswa tusikilizwe, natumaini umenielewa”
“Nimekuelewa mwalimu”
“Sikutaka maisha ya shule yawe magumu kwako, sikutaka kukufanyia jambo baya hata uchukie shule ndiomana sikuita mzazi wako kwaajili ya swala la wewe kuja na simu shuleni. Angel hujawahi kuja na simu shule ila nina uhakika ni yule Samir ndio kakushawishi, sasa kwa usalama wako Angel kaa mbali na Samir na utaweza muendelea mbele na kuona mafanikio ya maisha yako kwa ujumla.”
Angel alimuitikia mwalimu kisha akaamua kurudi darasani ili kumalizia vipindi na muda wa kutoka ufike arudi zake nyumbani.
 
SEHEMU YA 23

Leo walipotoka shule, wadogo zake walimfata kuondoka ila ilionekana kuwa wamenuniana maana hakuna aliyeonekana kumuongelesha mwenzie, basi aliongozana nao hadi nyumbani kwao na kumuuliza Erica,
“Mbona inaonekana huongei na Erick?”
“Kachukia eti mimi na yeye kutengwa madarasa”
“Aaaah achana nae, mwache avimbe apasuke, kwani kutengwa madarasa ndio nini? Mwache achukie”
Basi wakaingia ndani ambapo Erick alishaingia mud asana, basi walipoingia walimkuta yule dada yao wa kazi na kuuliza kuhusu mama yao alipo,
“Kaniaga kasema anaenda kwa dada yake, ila na nyie kwani mama yenu ni mtu wa kushinda nyumbani?”
“Yani mama akiwa ametoka ujue kuna mambo muhimu anafatilia, na huwa tusipomkuta ni mlinzi anakuwa ameachiwa maagizo ila leo hajatuambia kitu ndiomana tukakuuliza”
“Kwahiyo mama yenu huwa anashinda nyumbani?”
“Hapana, ila kazi anayoifanya sio ya kufanya tusiwe nae kwa muda mrefu”
“Aaaah sawa, chakula kipo tayari”
“Asante”
Walienda kubadilisha nguo na kwenda kula ila Erick hakuonekana kwenda kula kabisa, basi Angel alianza kusema,
“Yani Erick kasusa hadi kula, jamani hii tabia sijui kaitoa wapi huyu kiumbe?”
Erica alijihisi vibaya na kutaka kuinuka kwenda kuongea nae ila dada yake alimshika nguo na kumkalisha kisha akamwambia,
“Sasa unataka kwenda wapi na wewe? Si ni yeye ndio kagoma kula? Achana nae, mtu mwenyewe ana njaa ya kufa yule, atakuja mwenyewe, hebu tujilie sie, mamake akirudi ataenda kumbembeleza”
Angel aliendelea kula ila Erica hakuonekana na furaha tena, akavizia dadake akiwa makini na chakula akainuka na kuelekea moja kwa moja chumbani kwa Erick.
 
SEHEMU YA 24

Erica alifungua mlango na kukuta Erick kajilaza tu, basi akaenda karibu yake na kumuamsha,
“Erick twende ukale”
Erick aliinuka na kumuangalia Erica kisha akamwambia,
“Kwanini umenifanyia vile?”
“Kwani nimefanyaje? Nisamehe Erick”
“Yani kweli Erica unaonekana kufurahi mpaka jino la mwisho kisa nimehamishwa darasa?”
“Nisamehe jamani”
“Ngoja baba arudi, kwakweli na shule ile nitahama maana naona hupendi kuona nikisoma pale”
“Jamani Erick usiwe hivyo kaka yangu, nisamehe tafadhali, naomba twende ukale”
Basi Erica akatumia muda mrefu sana kumbembeleza Erick ili ainuke na aweze kwenda kula, mwishowe Erick alikubali ila kishingo upande kwani bado alikuwa na kinyongo sana ukizingatia hakupenda jinsi dadake alivyomcheka wakati anahamishwa darasa.
Basi Erick alienda kula ila alipomaliza tu alirudi chumbani kwake yani hata hakutaka kufanya mazungumzo kama siku zote anavyofanyaga
Basi kila mmoja mule ndani kwao aliendelea na mambo yake ila siku hiyo baba yao aliwahi kurudi nyumbani na Erick alienda kuongea na baba yao,
“Baba, naomba unihamishe shule”
“Kwanini unataka kuhama shule? Mbona ile shule ni nzuri sana mwanangu?”
“Baba, ili mtu usome ni lazima uridhike na mazingira ya shule, wanafunzi na kila kitu kinachokuzunguka. Kwa mimi kama nitaendelea kusoma pale lazima nitafeli baba, nakuomba unihamishe”
“Kwahiyo Erica nae nimuhamishe?”
“Hapana, mimi nimejisemea mimi kama mimi, naona Eria amepapenda pale”
“Sawa mwanangu usijali, ngoja tu wiki hii ipite na nitakupa jibu”
Kwakweli Erick alifurahi sana kwani alijua kama ataendelea kusoma shule moja na dada yake basi itakuwa ni tatizo kwake maana atagombana na kila mtu.
 
SEHEMU YA 25

Mama yao alirudi usiku na kukuta wanae wapo sebleni wakiangalia Tv basi akawasalimia pale na kuanza kuongea nao,
“Jamani Junior atakuja kusoma nanyi pale shuleni, kwahiyo Angel unapata nduguyo darasani”
“Khee mama, Junior si yupo kidato cha nne, atapataje uhamisho?”
“Atapata tu, mamake ashaongea na mwalimu wenu kwahiyo subiri tu utamuona shuleni Angel”
“Haya mama”
Basi mama yao akainuka na kwenda chumbani kuongea na mume wake, ambapo alimpa taarifa ya Junior ambaye ni mtoto wa dada yake kwenda kusoma shule moja na Angel, basi mumewe alimuuliza,
“Na kwanini anamuhamisha shule aliyokuwa akisoma?”
“Mmmh yule mtoto ni pasua kichwa mume wangu, yani sijui kachukua tabia za babake, pale kashahamishwa shule hadi dada yangu anahisi kuumia kichwa sababu ya yule mtoto”
“Ila yule mtoto nae balaa, kumbe hajabadilika tu!!”
“Hajabadilika ndio, yani ndio kwanza amepamba moto, kwakweli dada yangu pale ana kazi. Ndiomana nimemwambia ampeleke shule anayosoma Angel ili Angel amuangaliage”
“Mmmh nawe mke wangu mambo mengine unayataka, yani huyo junior ndio aangaliwe na Angel kweli? Katoto kenyewe kale kameanza tabia chafu siku nyingi jamani, huoni kama ukikaweka karibu na Angel kataanza kumnyemelea?”
“Mmmh jamani mume wangu, ndugu yetu yule ujue, mimi na mama yake tumezaliwa tumbo moja jamani! Inawezekana vipi hiyo?”
“Hapana ila Junior ana tabia chafu bhana, labda umkanye kwanza na huyo Angel umkanye pia maana mmh!”
“Unataka kusema nini sasa? Inamaana Angel nae muhuni?”
“Sina maana hiyo mke wangu, hata usipaniki”
Basi wakaongea ongea pale na kuendelea na mambo mengine ila mumewe hakumueleza habari za Erick kutaka kuhama shule kwani alijua ni lazima mke wake angepinga tu.
 
SEHEMU YA 26

Usiku wa leo Erica alienda chumbani kwa dada yake na kumueleza kuhusu maamuzi ya Erick baada ya kwenda kumbembeleza kula mchana,
“Achana nae huyo, unafikiri mama anaweza kumuhamisha shule? Yani asahau kabisa hilo swala”
“Anasema eti sisi hatupendi kusoma nae shule moja”
“Muache aahame mdogo wangu kwanza hatupunguzii kitu, kumbuka Junior nae anahamia pale shuleni kwahiyo kuhama kwake wala hakuleti tatizo. Ila pia kumbuka mama hawezi kumkubalia upuuzi wake huo”
Basi erica aliongea na dada yake siku hiyo na kuamua kulala pamoja nae hadi kulipokucha ambapo waliamka na kwenda kujiandaa kwaajili ya kwenda shuleni.
Njiani Erick alimwambia Erica,
“Kwahiyo ukaamua kuhama na chumba chako kwasababu nimekwambia nahama shule!”
“Kheee mimi sijahama chumba changu, ila jana nililala kwa dada”
Wakaachana na kila mmoja kuingia kwenye darasa lake.
Leo Angel alifurahi sana kwani alimkuta Hanifa akiwa amefika shule, kwahiyo alimkumbatia na kumkaribisha ambapo Hanifa alianza kumpa lawama,
“Tabia mbaya hiyo Angel, yani mimi nimekusubiria hujatokea jamani”
“Oooh nisamehe, halafu simu kaichukua mama yani siwezi kuwasiliana na yeyote”
“Mmmh mama yako nae anakuchunga utafikiri kitu gani jamani, nina uhakika hata hufurahii maisha Angel, kwenu kuzuri, wazazi wako wana pesa ila hauna uhuru, katika maisha hakuna kitu bora kama uhuru yani yote hayana maana ila uhuru ndio una maana kubwa katika maisha”
“Sasa nitafanyaje na mama hataki?”
“Sikia, Ijumaa tukitoka naomba twende pale dukani kwenu”
“Kwani naenda kufanya nini jamani!”
“Kun jambo la muhimu sana huko, hata leo tungeenda ila ni vizuri twende Ijumaa. Tuwahi kutoka shule halafu twende yani utafurahi nakwambia”
“Sawa, hakuna shida”
“Halafu Angel, kuna sura ngeni nimeiona humu darasani, yule kaka ni mgeni?”
“Ndio, anaitwa Samir”
“Oooh basi atakuwa wangu”
“Mmmh na wewe Hanifa jamani”
“Ndio, unataka awe wako jamani! Angel kuwa na huruma na wenzio, kila mkaka anakupenda wewe, je sisi tupendwe na nani jamani? Kisa wewe ni mzuri? Hivi unadhani wanakupenda kweli? Hamna lolote, wakaka kama hao huwa wanapenda wadada kama sisi”
Angel akaguna tu, kisha akaingia mwalimu wa kipindi na baada ya muda aliwaachia kazi na kutoka, ambapo alimuita Hanifa ofisini sababu hakuonekana shule kwa siku zote, basi Hanifa alivyoondoka ndipo Yusra aliposogea kwa Angel na kumwambia,
“Mimi huyu Hanifa simpendi jamani yani simpendi kabisa”
“Kwanini?”
“Anajishauwa sana”
“Wakati kuna watu humu darasani hawanipendi hata mimi jamani! Ndiomana nikaanza kuwa na urafiki na Hanifa maana humu darasani wadada hawataki kuongea na mimi zaidi yako na Hanifa halafu wewe na Hanifa hampatani jamani!”
“Humu darasani ni wivu tu, wanakuonea wivu sana Angel, na vile wengi wana kusifia basi wao wanaumia sana kwenye roho zao ila usijali mimi nipo, sema huyu Hanifa simpendi”
“Ila kwanini humpendi?”
“Anajishauwa, inaonyesha sio rafiki mzuri wala nini”
Angel akacheka tu ila alijua ugomvi wa hanifa na Yusra ulisababishwa na nini na aliwahi kuelezewa na hanifa kwahiyo alibaki kucheka tu.
Basi wakaendelea na ile kazi ya mwalimu waliyopewa.
 
SEHEMU YA 27

Wakati Angel amekaa darasani alishangaa kuona hanifa akitoka ofisini na moja kwa moja kwenda kwenye dawati alilokaa Samir, kwa mara ya kwanza Angel alijihisi kuwa na wivu juu ya Samir na moyo ulimuuma sana, basi akamngoja Hanifa amalize mazungumzo yake halafu Hanifa alirudi kukaa na Angel na muda ule ule Angel alimuuliza Hanifa,
“Ulikuwa unaongea nini na yule mkaka?”
“Nilikuwa namwambia ukweli kuwa yeye ni mzuri sana na nimemuomba namba yake ya simu, amenipa kwahiyo nitakuwa nikiwasiliana nae. Ila nimemkuta yupo busy sana sijui hata anaandika vitu gani jamani!”
“Kwanini umefanya hivyo Hanifa?”
“Kivipi?”
“Sikia Hanifa, sijawahi kujihisi hivi kabla juu ya mwanaume yoyote ila ulivyokaa na Samir roho imeniuma sana”
Hanifa alianza kucheka yani alicheka sana kisha akamwambia Angel,
“Na ushamba huo wa mapenzi ulionao unataka kujitwika gunia la kumpenda huyo Samir wakati anaonekana macho juu juu kweli, Angel rafiki yangu tulia kuna watu wenye wadhifa wao wanaokupenda na watakufanya ufurahie maisha sio hao wakina Samir, ingia kichwa kichwa kwenye mapenzi na urudi kwenu na mimba ya Samir sijui utamueleza nini mama yako na alivyo makali vile, kwa hakika atakufanya supu wewe na kitoto chako. Kuwa makini Angel”
“Mmmh!”
“Usigune, hao wakina Samir tuachie sisi tulioshindikana ndio tunawaweza, unaweza kuona kama najipigia debe ila nakuonea huruma, ungekuwa ni binti machepele ningekwambia sawa Samir anakufaa ila Angel umetulia jamani hadi vibaya kupata mtu wa kukusumbua akili, mimi nahitaji upate mwanaume mwenye hadhi yake yani ambaye akikupata tu basi tunakula pilau la harusi yenu sio huyo Samir”
Angel akamuangalia Hanifa kw amuda huo bila ya kumjibu chochote kisha wakaendelea na masomo hadi muda wa kutoka.
 
SEHEMU YA 28

Wakati wa kutoka ulipofika, basi Angel akabeba begi lake kwaajili ya kuondoka ila alivyofika nje akavutwa kidogo kwa nyuma, kuangalia akaona ni Samir amemvuta huku akitabasamu. Basi Angel alisimama na kumuangalia, basi Samir akamwambia,
“Najua hatuwezi kuongea vizuri hapa kwani kila jicho lipo juu yako, ila nina ujumbe wako”
Samir alitoa karatasi iliyokunjwa vizuri na kumkabidhi Angel, kisha Angel alichukua karatasi ile na kuiweka kwenye mfuko wa sketi yake ya shule basi akaondoka na kurudi nyumbani kwao akiwa na wadogo zake.
Walipofika tu nyumbani mama yao akawaambia,
“Haya nendeni kavueni sare zenu mlete niwafulie”
Nao wakafanya hivyo kisha mama yao akazikusanya na kwenda kuzifua, sasa Angel akakumbuka kitu, yani akakumbuka ujumbe ambao alipewa na Samir akaona ni tatizo basi akaenda haraka haraka ambapo mama yake alikuwa akifua, akashtuka kwani alimkuta mama yake ndio kashika lile karatasi akilisoma.
Kwakweli Angel alishtuka sana na akatamani kurudi nyuma ila mama yake alimuona na kumuita,
“Angel hebu njoo haraka, kwakweli huyu Samir hapana jamani nahitaji kumfahamu”
Angel akamuangalia tu mama yake bila kusema chochote kwani hata kilichoandikwa kwenye karatasi hakujua ni kitu gani.


Kwakweli Angel alishtuka sana na akatamani kurudi nyuma ila mama yake alimuona na kumuita,
“Angel hebu njoo haraka, kwakweli huyu Samir hapana jamani nahitaji kumfahamu”
Angel akamuangalia tu mama yake bila kusema chochote kwani hata kilichoandikwa kwenye karatasi hakujua ni kitu gani.
Mama yake akamwambia tena,
“Njoo Angel nimekuita”
Basi Angel akamsogelea mama yake huku akitetemeka kisha mama yake akamuuliza,
“Umeisoma hii karatasi uliyopewa na Samir? Niambie ukweli mwanangu”
“Hapana mama sijaisoma”
“Haya nenda kaendelee na mambo yako”
Angel alishindwa hata kumwambia mama yake ampe ile karatasi ili na yeye aweze kusoma zaidi zaidi aliondoka huku akiwa kanyong’onyea.
Mama Angel alifua nguo za wanae huku akisikitika sana kuhusu Samir na ile karatasi aliitunza vizuri sana.
Usiku baada ya kula chakula mama Angel alienda kuongea na mumewe ambapo kwanza alimpa lile karatasi lenye ujumbe aweze kusoma, kwakweli mume wake nae alitikisa kichwa na kuuliza,
“Huyu kijana ndio nani?”
“Ndio huyo Samir ambaye Jumapili ile ndio alimpigia simu Angel na nikaanza kumfokea Angel”
“kwahiyo hii karatasi umekuta ndio Angel anaisoma?”
“Kwa bahati hajaisoma yani nimeikuta kwenye sketi yake ya shule, yani kama Mungu tu nikawaambia leteni sare zenu nifue ndio nakutana na ujumbe wa namna hii”
“Sasa mke wangu unajua cha kufanya?”
“Nifanye nini hapo unadhani?”
“Unafikiri kwa maneno ya huyu kijana Angel anaweza kuchomoka? Hapa Angel hachomoki yani kujana anajua kutongoza hatari, ana maneno yaliyoenda shule, nimemvulia kofia”
“Mmmh kama wewe kipindi kile unanifatilia”
Baba Angel akacheka na kuendelea kusema,
“Sasa cha kufanya kaa chini na Angel, zungumza nae, mueleze kuhusu mambo ya vijana na mbinu zao, mimi nikipata muda nitazungumza nae pia, mueleze Angel ajue maana bila kujua kwa maneno ya huyu kijana Angel hachomoki yani hatumpati tena Angel, muda wote atakuwa akimuwaza huyu”
“Sasa, mume wangu jamani unanitisha ujue. Sitaki mtoto wetu aharibike, nahitaji Angel asome na afike mbali na elimu yake”
“Kama unahitaji hilo basi jua jinsi ya kumfundisha, natambua jinsi wanaume tulivyo ila mfundishe Angel vizuri”
“Yani niliposoma huu ujumbe hadi nimehisi ukucha unanicheza, namuhurumia mwanangu Angel jamani, ndio kuna wakware hivi sheleni kwao? Isingekuwa kidato cha nne ningemuhamisha kwakweli”
Basi mama Angel aliongea kwa kulalamika sana na mwishowe waliamua kulala tu.
 
SEHEMU YA 29

Siku ya leo walienda shuleni, basi Angel aliingia darasani na Samir alipomuona Angel alikuwa akimchekea tu na kumpa kama ishara ambayo Angel hakuielewa wala nini ila alipomuangalia vizuri midomo yake aliona akisema “I love you” Angel akainama chini na kuogopa kumuangalia Samir vizuri ila Hanifa aliona na kuguna kisha akainuka na kumfata Samir,
“Mmmmh wewe muhuni, yani ni mgeni ila umemuanza Angel jamani”
“Mimi sio muhuni ila Angel nampenda tena nampenda sana”
“Mimi je hujanipenda?”
“Hapana”
“Inamaana mimi sio mzuri?”
“Sijasema wewe sio mzuri ila upendo wa kweli hauangalii uzuri wala sura ila upo moyoni, kwakweli Angel nampenda na nitasema hivi siku zote hata mbele ya wazazi wake”
“Mmmh unajiamini eeeh! Ila yule Angel ni binti mlokole, mama yake ni mkali hatari”
“Simba ni mkali ila anazaa, mimi siogopi ukali wa wazazi wake, ila naangalia moyo wangu, ni kweli nampenda Angel”
“Kheee una ujasiri wewe kijana!”
“Mbele ya Angel lazima nipate ujasiri, nampenda sana”
“Mmmh!”
Hanifa akainuka na kwenda alipokuwa Angel baada ya muda kidogo walipata mgeni mpya kwenye darasa lao, kwakweli Angel alifurahi sana kumuona kwani alikuwa ni Junior mtoto wa mama yake mkubwa, basi mwalimu alimtambulisha pale kisha aliwaacha wamkaribishe darasani na yeye akatoka, kwakweli Angel alifurahi sana na kumkaribisha nduguye ila kile kitendo cha Angel kumfurahia Junior kiliumiza sana moyo wa Samir na kujikuta akikosa raha kabisa hadi aliamua kutoka nje ya darasa.
Basi Angel alikuwa akiongea na Junior pale mpaka mwalimu alipoingia na kuanza kipindi.
 
SEHEMU YA 30


Muda wa kutoka Angel aliongozana na Junior ambapo Junior alikuwa akimuuliza Angel kuhusu mazingira ya ile shule yao, basi Yusra nae akasogea kwa Angel na kumuaga kuwa wataonana kesho, muda huo huo ambapo Yusra kaondoka tu basi Junior aliacha kuuliza habari za shule bali alianza kuuliza kuhusu Yusra,
“Angel, yule rafiki yako anaishi wapi?”
“Mmmh Junior, nini sasa kaka yangu jamani! Siku ya kwanza hii”
“Kwani siku ya kwanza kitu gani? Hupendi yule awe wifi yako?”
“Mmmh sikuwezi, muulize mwenyewe kesho atakujibu anapoishi”
Basi Erick na Erica nao walifika pale na kumsalimia Junior huku wakifurahia uwepo wake halafu wakaondoka zao kurudi nyumbani.
Walimkuta Vaileth akiendelea na kazi za pale ndani, wakamsalimia na kwenda kubadili nguo kisha Vaileth alienda chumbani kwa Angel na kuongea nae,
“Samahani Angel, kwani dereva wenu alikuwa anakufanya nini?”
“Mmmh alikuwa akinisifia tu, kwani vipi?”
“Yani nimemuonea hadi huruma leo, anasema alikuwa akikusifia tu na asingeweza kufanya chochote na wewe. Yani mama yako kamfukuza kazi hadi huruma”
“Ila sio kosa langu, sikutaka kusema kwa mama ila ni kosa la Erica yani katoto kambea kale balaa”
“Mmmh ila wewe ndio ulitakiwa umuombee msamaha kwa wazazi wako”
“Weee wale wazee wakiamua lao unadhani naweza kupinga? Haswaa mama yani mama yetu ni mkali sana”
Basi Vaileth akamuacha pale Angel na kuondoka zake kwenda kuendelea na kazi zake.
Muda kidogo mama yao alirudi na wote walienda kumpokea na kumsalimia maana walikuwa na utaratibu huo, basi mama yao akawauliza pale baadhi ya maswali kisha akawaambia,
“Kesho kuna anko mpya nitawatambulisha”
“Sawa mama”
Basi wote wakainuka na kwenda kuendelea na kazi zao ila muda kidogo mama yao alitoka nje na kuwaita watoto wake,
“Jamani wanangu kwa bahati anko mpya kafika leo, huyu anaitwa anko Maiko”
“Shikamoo anko”
Wote walimsalimia na Maiko aliitikia ile salamu kisha mama yao aliwaruhusu kwenda ndani tu kuendelea na mambo mengine.
 
SEHEMU YA 31

Kwakweli Erica hakupenda mwenendo wa Erick maana toka siku aliyonuna basi hadi leo alionekana hana furaha kama siku zote, basi aliaenda tena chumbani kwake kuongea nae,
“Kwani Erick una tatizo gani?”
“Sina tatizo wala nini?”
“Sasa mbona unakuwa hivyo jamani?”
“Kwani wewe nikiwa hivi unaumia nini/ Si unaongea vyema na Abdi eeeh! Basi mthamini Abdi”
“Sio hivyo Erick jamani, haya niambie nikupe zawadi gani ili ufurahi kama zamani”
“Zawadi yangu mimi ni moja tu, sitaki kukuona ukizungumza na Abdi”
“Kama ni hivyo tu sawa, nakuahidi sitazungumza na Abdi tena kaka yangu, sawa eeeh! Basi furahi kidogo, twende nje tukacheze”
“Oooh tutakuwa kama mitoto, unajua tumekuwa kwasasa, lazima tuenende kikubwa”
Mara dada yao Angel akafika na kusema,
“Eeeh Erica, nimekufata chumbani kwako sijakukuta, nikajua tu upo huku kwa kisirani wako. Nataka nikutume kitu mdogo wangu”
“Kitu gani dada”
“Njoo nikwambie”
Basi Erica alitoka nje na dada yake ili kumsikiliza ni kitu gani anataka kumtuma,
“Sikia, nenda chumbani kwa mama halafu nichukulie ile simu ambayo mimi nilikuwa naitumia, naomba fanya hivyo mdogo wangu halafu nitakupatia kitu kizuri sana”
“Mama, akinibamba je?”
“Hakubambi, kwanza bado yupo nje anaongea na yule dereva”
Basi Erica akatoka pale na kwenda chumbani kwa wazazi wao, na kweli simu aliikuta mezani tu, basi akaichukua na kutoka nayo ila alipotoka tu njiani akakutana na mama yao nae akiwa anaelekea chumbani ila simu ilianza kuita na kumshtuka mama yao, Erica alishtuka pia na kutamani hata kukimbia, basi mama yake alimuangalia kwa hasira na kumwambia,
“Lete hiyo simu mjinga wewe”
Basi Erica akamkabidhi mama yake ile simu ambapo alinaswa kofi na kuambiwa,
“Kaniitie huyo Angel sasa maana najua ndiye aliyekutuma”
Erica aliondoka akiwa kanyong’onyea sana hadi chumbani kwa dada yake, ambapo Angel alimpokea kwa bashasha,
“Eeeeh hiyo simu iko wapi?”
“Mama, kanibamba nayo anakuita”
“Nilijua tu, bora hata ningemtuma Erick”
Angel aliinuka kwa hasira na kumsukuma kichwa mdogo wake.
Erica alimuangalia dada yake na kutoka kule chumbani kwa dada yake ila aligongana kikumbo na Erick ambaye alimuhurumia pia kisha akamwambia,
“Mama kakupiga halafu aliyekutuma nae kakutia sinki, pole mdogo wangu jamani”
Halafu Erick akamkumbatia na kuondoka nae kuelekea sebleni ili wakaangalie Tv na aweze kupunguza machungu ya kutumwa kitu kisichoruhusiwa.
 
SEHEMU YA 32

Angel alienda chumbani kwa mamake sasa ila alishangaa sana siku hiyo wala mama yake hakumfokea wala hakumwambia kiukali zaidi zaidi alimwambia akae ili wazungumze, basi Angel alikaa na kuanza kuongea na mama yake,
“Eeeh niambie mwanangu Angel ulikuwa unataka simu umpigie nani?”
“Nilitaka nimpigie Hanifa mama”
“Niambie ukweli, kumbuka mimi ni mama yako Angel”
“Naelewa mama ila huo ndio ukweli”
“Haya, simu hii hapa mpigie huyo Hanifa hapa nisikie unachotaka kuongea nae”
Muda huo huo akakumbuka kile alichoahidiana na Hanifa kuwa watoroke Ijumaa, akaona akimpigia simu itakuwa ni msala kwake kwahiyo akajigelesha kupiga ile simu.
“Ila mama jamani, naomba tuache tu hata sikutaka kupiga simu”
“Kwahiyo unanidanganya mimi Angel eeeh!”
“Hapana mama”
“Haya, piga ulipotaka kupiga, au ulitaka kumpigia Samir”
“Jamani mama mbona hivyo, yani mama mambo yako kama askari hadi tunakosa uhuru humu ndani”
Basi Angel akainuka ili aondoke, mama yake akamvuta nyuma na kumnasa kofi kisha akamfokea,
“Mjinga wewe, umeona leo nimeongea nawe kwa upole basi unajifanya kuleta kiburi, mimi sio shangazi yako wa kumfanyia jeuri”
Muda huo simu ya mama Angel ikaanza kuita kwahiyo mama Angel alimwambia Angel atoke mule chumbani kwake na kupokea ile simu, ila mpigaji alikuwa ni dada yake na kuanza kuongea nae,
“Mbona unaongea hivyo mdogo wangu jamani”
“Si huyu Angel jamani, ataniua kwa presha huyu mtoto dah!”
“Kafanyaje tena?”
“sheleni kwao kuna kivulana kinaitwa Samir sijui sasa ndio kinamsumbua akili, kweli leo hii naongea halafu Angel ananiambia naongea kama askari, eti nawanyima uhuru kweli Angel wa kunijibu hivi!”
“Ila mdogo wangu mambo mengine umeyataka mwenyewe, huyo mtoto toka mdogo kazi kumsifia tu, oooh mwanangu mzuri sana, mwanangu mzuri kama malaika, haya sasa ndio anakuonyesha mambo ya uzuri wake, nilikwambia mdogo wangu ni kweli mwanao ni mzuri ila usimsifie kupitiliza, umeona sasa ameanza kukujeuria hadi wewe. Pole mdogo wangu, nisingekuwa na majanga ningesema huyo Angel aje kukaa kwangu kidogo ila na mimi mwanangu tu huyu ananitoa pumu, dawa ya Angel mpeleke kwa mama yani akikaa na bibi yake huyo atashika heshima na adabu”
“Sawa dada, nashukuru kwa ushauri wako nitaufanyia kazi. Eeeeh niambie”
“Sasa mwenzangu ni kuhusu huyu wifi yetu maana sio wifi yangu tu ila ni wifi yetu, kwakweli kuolewa ukoo mmoja ni vibaya jamani, miukoo mingine ni shida tupu jamani”
“Unamaanisha Tumaini? Kafanyaje?”
“Ndio huyo huyo, kwani mimi na wewe tunashea wifi yupi? Si ndio huyo mdogo wangu, yani ananipasua kichwa kwakweli”
“Anafanyaje dada”
“Yani kaleta mitoto yake kwangu, mwezi umepita sasa halafu yeye nasikia yupo Arusha anakula bata na mumewe”
“Khee wote wanne?”
“Ndio, watoto wenyewe kawazaa kama ngazi halafu wote kawaleta kwangu jamani, kisa nyumba zetu zipo karibu, najuta kuwafahamu, wakati huo ana dadake nae katuma wanae wawili waje kwangu jana, kwakweli Napata mawazo mimi jamani. Junior anisumbue kichwa na mawifi nao wanisumbue kichwa kwanini lakini!”
“Pole sana dada yangu jamani”
“Ongea na mumeo jamani, aongee na dada yake”
“Ila kumbuka na mumeo nae ni dada yake”
“Hamsikilizi ila mumeo atamsikiliza, kuna vitu Tumaini anamuheshimu sana kaka yake huyo, naomba umwambie jamani nimechoka, yani nimechoka la sivyo nawaleta hawa watoto na kwenu ili tusaidiane majukumu ya kulea, aliona raha kuzaa kila siku halafu kulea kunamshinda jamani loh!”
Dada wa mama Angel alionekana kuongea kwa hasira sana kuhusu wifi yao huyo ambaye wamechangia undugu yani mume wa mama Angel ni kaka wa Tumaini ambaye wamechangia baba na mume wa mama Junior ni kaka wa Tumaini kwa upande wa mama yani amechangia nae mama halafu huyo Tumaini kaolewa na kaka yao.
Basi waliongea pale na kuagana ila mama Junior alionekana kuwa na hasira sana na huyo wifi yao.
 
SEHEMU YA 33

Basi wakati mumewe amerudi aliamua kuongea nae pia na habari ya Angel na jinsi alivyoongea na dada yake,
“Dada kanishauri kuwa Angel tumpeleke kwa mama yani akalelewe na bibi yake”
“Hebu acha ujinga huo Erica, hayo ni mawazo ya kijinga. Mama aliwalea ninyi na kuwahudumia, kila kitu alifanya juu yenu, huu ni wakati wa yeye kupumzika sio kuanza tena kusumbuana na wajukuu kama alivyokuwa akisumbuana na nyie, ni wakati wa kumuonea huruma mama yenu, huyu Angel shughulika nae mwenyewe maana wewe ndiyo mama wa Angel, sasa unataka nani akabebe mzigo wa mwanao? Usitake kumtesa bibi wa watu, waende kumsalimia tu sio kumsumbua”
“Mmmh na wewe mume wangu jamani, haya dadako nae ni mwezi sasa katupia watoto wake wote kwa dada yangu”
“Haya ndio mambo ya familia kuoana jamani, hebu ona sasa, yani dada pale anahisi kuwa ana uhuru na haki ya kufanya hivyo akiangalia pale kuna wifi yake ambaye ni dada wa mumewe na kuna kaka yake pale, yani ana uhuru wa kufanya chochote kile”
“Mmmh mbona huku hawaleti?”
“Tumaini hawezi kufanya hivyo nyumbani kwangu sababu anajua mimi sipendi ujinga, ila haya ndio madhara ya kutambua starehe ukubwani jamani, yani Tumaini katambua starehe ukubwani basi ndio anajifanya anatumia muda wake, na usinge mshauri vizuri nadhani kwasasa angekuwa na watoto hata kumi”
Mama Angel alicheka sana na kusema,
“Ila Tumaini jamani anafanya mambo kama sio msomi”
“Kusoma sio ndio njia ya kukufanya uelewe kila kitu, kuna mambo mengine ni elimu jamii yani ukiwa mtu wa jamii ndio utaelewa zaidi, sasa yule dada yangu alikuwa mshamba wa mwisho kabisa, kaolewa ndio kafanya kazi ya kuzaa double double”
“Wewe una utani na dadako, haya mama Junior kasema ataleta watoto wa Tumaini hapa kwahiyo ongea na dadako vizuri”
“Weee huo ujinga nani atautaka? Napenda sana watoto ila sio kwa stahili hiyo kwakweli, awapeleke kwa bibi yao kama alivyotaka Angel aende kwa bibi yake”
Kisha baba Angel akaamua kulala ikabidi na mama Angel nae alale tu.
 
SEHEMU YA 34

Kulipokucha walienda shule kama kawaida na kila mmoja alienda kwenye darasa lake, basi leo Angel alivyoingia darasani tu akapambana macho na Samir ambaye alimuangalia sana ila Angel alikwepesha macho yake kwani aliogopa kumuangalia Samir usoni, basi aliondoka na kwenda kukaa kwenye dawati lake, Hanifa akamfinya kidogo na kumwambia,
“Nimekuona hapo ulivyogongana macho na Samir, mmmh kweli unampenda ila hakufai mwali wangu jamani”
“Mmmh na wewe Hanifa, mbona sijamuangalia wala nini jamani! Nimeangalia sehemu nyingine tu”
“Mmmh nimeona jamani, unampenda yule ndiomana umemuangalia vile”
Basi Angel akacheka tu na kuendelea na mambo mengine pale darasani.
Mwalimu akaingia na kufundisha ila siku hiyo Angel alijihisi kabisa mawazo hayapo darasani kabisa hadi mwalimu akamshtua kwa kumpiga na chaki,
“Wewe Angel, unawaza nini? Niambie unawaza kitu gani Angel? Baada ya kipindi unifate ofisini”
Basi kipindi kilipoisha ilibidi Angel aende ofisini alikoitwa na mwalimu ambapo alianza kuongea nae,
“Unawaza nini Angel? Kwanini huzingatii masomo? Bado Samir anakuumiza kichwa”
Angel akashtuka kidogo na kukaa kimya, kisha mwalimu akamwambia,
“Niambie Angel, yule Samir niliongea nae siku ile ya simu. Je anakuumiza kichwa? Unahisi kumpenda Samir? Angel, wewe ni kama mwanangu naomba nikwambie kuwa Samir hakufai, yule ni mwanaume tu mchezaji yani kazi yake ni kuchezea mabinti kama wewe, usiumize kichwa chako kumfikiria Samir, zingatia masomo ndio ya muhimu kwako”
“Ila mwalimu mimi simfikirii Samir, kwanza sina mahusiano nae na wala hajawahi kunitongoza”
“Ila alikiri wazi kwangu kuwa anakupenda sana”
Angel alinyamaza kimya na kuangalia chini, kisha mwalimu alimuuliza Angel,
“Kwani na wewe unampenda?”
“Hapana mwalimu, mimi napenda masomo”
“Ooooh usiwaze nilikuwa nakutania tu nione utasemaje, Samir hajawahi kuniambia kuwa anakupenda ila nilitaka kujua kama kuna chochote kati yako kinaendelea. Ila bado nasisitiza hata akikwambia jua kuwa Samir sio mwanaume sahihi kwako, soma umalize shule salama nami nitakuonyesha mwanaume sahihi katika maisha yako. Haya kaaendelee na masomo”
Basi Angel akatoka na kurudi darasani ambapo Hanifa alianza kumwambia,
“Mmmh Angel huyu nduguyo Junior ana matatizo gani?”
“Kwanini?”
“Ni mgeni ila kashamtongoza Yusra na kashanitongoza na mimi”
Angel akacheka sana maana tabia aliyokuwa analalamikiwa Junior ni tayari alishaionyesha kwenye shule nyingine.
 
SEHEMU YA 35

Muda wa kutoka ulivyofika, leo wakiwa katika harakati za kuondoka wakati tu wamepanda kwenye gari, akasogea Abdi na kwenda kumnong’oneza kitu Erica ambapo Erica alionekana akicheka baada ya kuambiwa na Abdi ila kile kitendo kilimchukiza sana Erick na siku hiyo walirudi nyumbani akiwa na kinyongo sana kwani aliona Erica amevunja ahadi yake ya kutokuzungumza na Abdi maana yeye hakupenda Abdi awe karibu na dada yake.
Walipofika nyumbani dada yao wa kazi alitambua tofauti aliyokuwa nayo Erick maana alionekana kuchukia zaidi siku hiyo, basi alimuuliza tatizo ni nini,
“Kwani Erick una tatizo gani?”
“Hapana dada, sina tatizo”
“Unaonekana haupo sawa yani, pole sana”
Kisha akawakaribisha chakula ambapo kwa siku hiyo kila mmoja alikula kivyake tu, na hata Erica hakwenda kumbembeleza Erick kama ambavyo huwa anafanya.
Mama yao alirudi mapema siku hiyo na aliwaita kuwaambia jambo,
“Jamani watoto zangu, kesho alfajiri yani nitaondoka saa kumi kabisa kuna mahali inabidi niende ila baba yenu ameenda leo”
Angel akauliza,
“Halafu mnarudi lini mama?”
“Nadhani kesho hiyo hiyo au keshokutwa”
Basi wakamtakia mama yao safari njema na kila mmoja kuendelea na shughuli zake za hapa na pale.

Alfajiri na mapema mama Angel aliondoka kama ambavyo aliwaaga watoto wake, na wenyewe palipokucha walijiandaa kwa lengo la kwenda shule kama kawaida ila mpaka wanahitaji kutoka Erick hakujiandaa wala nini ilibidi Angel amuite na kumwambia kuwa inakuwaje haendei shule maana hata kujiandaa hakujiandaa,
“Leo siendi”
“Kwanini huendi?”
“Nimejisikia tu kutokwenda”
“Kheee hivi wewe Erick una wazimu au kitu gani eeeh!”
“Nimesema siendi”
“Aaaah umeona mama katoka mapema ndio na wewe kusema huendi shule, sasa subiri uone mama akirudi yani nitamwambia mambo yako yote. Yale ya kupigana shuleni, kuchukia bila sababu na leo kutokutaka kwenda shule”
“Kwani lazima kwenda shule jamani? Kwanza leo Ijumaa, nitaenda Jumatatu. Tusipangiane maisha”
Halafu akaondoka zake na kurudi chumbani, ila kiukweli Angel alichukia na kutamani hata kumzaba makofi ingawa walilingana nae urefu ila alijivunia kwakuwa yeye ni dada.
Ikabidi tu aongozane na Erica kwenda shuleni na kuachana na Erick pale nyumbani.
 
SEHEMU YA 36

Vaileth alijihisi vibaya kwakweli na kuona yule mtoto lazima kuna tatizo linamsumbua ndiomana yupo vile basi alimuita ili kuongea nae,
“Kwani Erick una matatizo gani?”
“Sina matatizo yoyote”
“Sikia, naomba mimi na wewe tuongee kama marafiki na wala sitamwambia yoyote, nieleze una matatizo gani ila niweze kukusaidia rafiki yangu jamani”
“Kwakweli hata mimi sielewi nina matatizo gani, Erica ni pacha wangu yani najikuta muda wote nikitamani kuwa karibu yake tu, natamani mimi tu ndio niwe rafiki yake wa kiume, ila Erica sijui vipi anaanza kuongea na wanaume shuleni kwakweli moyo unaniuma sana hata nimemwambia baba anihamishe shule ingawa sijamwambia sababu, yani mimi sipendi kabisa. Sasa kuna mmoja anaitwa Abdi kwakweli simpendi yani simpendi kabisa, sasa tulikubaliana na Erica kuwa hatoongea tena na Abdi halafu jana wananong’onezana na kucheka, kwakweli nimekasirika na kuona bora nisiende shule kabisa”
“Sasa kwanini unakuwa hivyo eeeh! Yule Erica si dada yako wewe!”
“Ndio ni dada yangu ila najikuta namjali sana, naona kama hawa vijana watamuharibia maisha yake”
“Kwakweli mimi naafiki swala la wewe kuhama shule ila hutakiwi kuchukulia hasira kiasi hiko hadi leo kugoma kwenda shule jamani. Kama kweli unahitaji kumlinda Erica basi unahitaji kuwa nae karibu sana ili aweze kupita njia sahihi. Usichukie Erick, mpende dada yako, wapende dada zako usiwanunie”
“Sawa nimekuelewa”
Basi Erick alikubaliana na huyu mdada wao wa kazi na kufanya mambo mengine.

Leo kama ambavyo hanifa alipanga na Angel, basi walipokaribia mapumziko tu wakajiandaa ili waweze kutoroka, sasa wakati wanatoka nje ya eneo la shule, Hanifa alitangulia ila wakati Angel anatoka akadakwa na mwalimu na kuulizwa kuwa anaenda wapi, kwakweli Angel alikosa maelezo basi mwalimu aliamua kumpa adhabu.
“Sasa leo, muda wenzio wanatoka darasani wewe nataka ubaki na utafanya haya maswali, hakikisha unayaleta nayasahisha ndio unaenda nyumbani”
Sasa mwalimu kuangalia pembeni akamuona Samir nae kabeba begin a kutaka kupita njia ile ile aliyopita Angel, basi mwalimu alimuita pia na kumpa adhabu ile ile aliyompa Angel,
“Mmenielewa nyie”
“Sawa madam”
Waliamua kurudi darasani huku wakisubiri muda wa kutoka waweze kuianza adhabu yao.
 
Back
Top Bottom