Simulizi : Nguvu ya Mapenzi

Simulizi : Nguvu ya Mapenzi

SEHEMU YA 138

Walipofika shuleni, moja kwa moja Erica alipelekwa kwenye usahili na kupewa mitihani ambayo aliifanya kwa umakini mkubwa sana kiasi kwamba walimu walipoichukua ile mitihani walifurahi sana na kumwambia baba Angel kuwa mtoto wake apelekwe tu kesho akaanze shule maana anaonekana yupo vizuri sana.
Basi wakapanda kwenye gari na kuanza safari ya kurudi nyumbani, wakiwa njiani Erica aliuliza,
“Sasa baba mbona hatuendi tena kule shuleni ili nikawaage rafiki zangu?”
“Tutaenda kesho, ngoja leo turudi tu nyumbani kwani nina mambo mengi sana ya kufanya”
Yani Erica kilichokuwa kikimuumiza moyo ni kuhusu habari ambayo Elly alimwambia kuwa atamwambia, basi alichukia sana ila hakutaka tu kumuonyesha baba yake kuwa amechukia.
Kuna mahali walikuwa wakikatisha na gari mara Erica alimuona mtu na kumshtua baba yake,
“Kheee baba, yule sio kaka Junior?”
Baba Angel alisimamisha gari na kuangalia vizuri ni kweli kabisa alimuona Junior akiingia kwenye nyumba ya kulala wageni tena akiwa ameongozana na mwanamke aliyemzidi sana kwa umri, kwakweli baba Angel alichukia sana hivyo alipaki gari lake vizuri na kushuka hadi kwenye ile nyumba ya kulala wageni.
Alifika pale na kumuulizia Junior, ila pale alikuwa ameandikisha jina lingine,
“Hakuna Junior hapa mzee wangu”
“Aaaah namtaka yule mtoto aliyeingia hapa muda huu, hivi mnajua kama yule ni mwanafunzi? Nitawafunga nyie”
Wale wahudumu wakaogopa hivyobasi wakamuonyesha baba Angel chumba ambacho Junior ameelekea na yule mwanamke, basi baba Angel akiwa na hasira sana alienda hadi kwenye kile chumba na kujaribu kufungua ila kilikuwa kimefungwa kwa ndani hivyo na kuamua kugonga ambapo mlango ulifunguliwa na Junior mwenyewe akijua ni muhudumu wa ile guest, kwakweli baba Angel alichukia sana na kumvuta kisha alimzaba vibao vya kutosha na kuondoka nae ambapo alimpakia kwenye gari lake na moja kwa moja kwenda nao nyumbani kwake.

Kwakweli mama Angel pia alisikitika sana baada ya kusikia habari za Junior, basi baba Angel alikaa nae chini na kujaribu kuzungumza nae,
“Hivi wewe Junior una tatizo gani lakini?”
“Sina tatizo mimi baba mdogo ila sina raha kabisa”
“Kwanini?”
“hakuna mtu anayenipenda”
“Hivi wewe mtoto una kichaa au nini? Familia yako yote tunakupenda, mama yako na sisi wote tunakupenda tena sana tu. Sasa kwanini useme hakuna anayekupenda?”
“Sijawahi kuishi na baba yangu mimi, muda wote mama hunitukana na kuniambia kuwa tabia zangu ni kama za baba yangu, hata akinituma nikimwambia nimechoka basi huwa anasema tabia zangu ni kama za baba yangu na mara nyingi huwa anasema anajuta kunizaa anasema angejua angetoa hata mimba yangu. Haya na baba ninayeishi nae pia, hataki hata kuniona ingawa mama analea watoto wa baba vizuri tu ila yule baba hanitaki mimi kabisa na hata hanipendi. Kwahiyo mimi sina furaha yoyote ya maisha zaidi ya hii, yani kuzunguka na wanawake ndio furaha yangu”
“Sasa Junior, hayi sio maisha ujue mwanangu, yani sio maisha kabisa. Naomba kwasasa uishi hapa nyumbani kwangu, nitaenda kukuchukulia nguo zako na kukuletea hapa, kwahiyo utakuwa ukienda shule na kurudi hapa, ila Junior sitaki ujinga hapa nyumbani kwangu, achana na habari kusema kuwa watu wote hawakupendi wakati tupo tunaokupenda sana tu, sawa!”
“Sawa, bamdogo nimekuelewa”
Basi baba Angel alipanga kwenda kesho yake kumchukulia Junior nguo zake ila kwa siku hiyo alimtaka ake hapo hapo na asiende popote pale.
 
SEHEMU YA 139


Siku hii asubuhi kabisa, baba Angel alimuita Vaileth kwanza na kuanza kuongea nae tena,
“Vaileth, mimi nitakupatia pesa ili uwatumie wazazi wako waweze kukarabati nyumba yenu”
“Oooh asante sana jamani, mungu akubariki baba. Nashukuru sana”
“Ila naona kama bado haupo sawa, najua kinachokuumiza akili ni ndugu yako ambayo bado yupo rumande, ila nilimpeleka kule aweze kupata adabu kidogo”
Vaileth alinyamaza kimya tu, kisha baba Angel akamwambia,
“Ila usijali kitu kwani leo kabla sijaenda kwenye shughuli zangu basi nitapita kwanza polisi na kumtoa ndugu yako”
Vaileth alionyesha tabasamu na kumfanya baba Angel aelewe wazi kuwa jambo lile lilikuwa likimuumiza sana kichwa Vaileth.
Basi aliondoka na kama alivyoahidi ni moja kwa moja alienda polisi kumtoa Prisca, kisha alienda kwenye shughuli zake za kila siku, maana Erica alipelekwa leo na mama yake kwenye ile shule mpya sababu baba yake alisema kuwa kuna mambo anayafatilia kwanza, ikiwa na kwenda kuchukua nguo za Junior.
Alipomaliza shughuli zake ni moja kwa moja alienda kuchukua nguo za Junior kwa shemeji yake, ambapo alimueleza tu kwa kifupi na shemeji yake alisikitika sana juu ya mtoto wake ila alimwambia,
“Shemeji, kuna siku nitakuja ili tuzungumze vizuri juu ya hili swala la Junior, naimani utanielewa”
“Sawa, shemeji hakuna tatizo. Msalimie sana mdogo wangu na watoto”
Basi baba Angel aliagananae na kuaondoka zake.
Wakati anakaribia nyumbani kwake alishangaa sana kuona watu watatu nje ya geti lake na wote walikuwa ni wanawake na katika watu hao mmoja alikuwa mtupu kabisa na walionekana wanafanya mambo kama ya kishirikina.



Wakati anakaribia nyumbani kwake alishangaa sana kuona watu watatu nje ya geti lake na wote walikuwa ni wanawake na katika watu hao mmoja alikuwa mtupu kabisa na walionekana wanafanya mambo kama ya kishirikina.
Baba Angel alishtuka sana hadi alitamani kushuka kwenye gari yake ili aende kuwauliza vizuri pale getini, ila alisita kushuka, hivyobasi akaanza tu kupiga honi ambapo mlinzi alifungua geti na moja kwa moja baba Angel aliingiza gari ndani na yule mlinzi alifunga geti lao yani wale watu nao walisogea pembeni na walijifanya kama hawaoni ile gari ingawa walisogea pembeni.
Basi baba Angel alishuka na moja kwa moja alienda sebleni na kumuita mke wake ambapo alimueleza kile alichokiona getini kwao basi mama Angel nae aliamua kutoka ili akashuhudie, muda huo Vaileth nae alisikia na Junior pia alisikia kwahiyo wote waliongozana na kwenda nje ili kushuhudia kitu ambacho kinaendelea nje ya nyumba hiyo, na walipotoka tena kweli waliwakuta pale wakiendelea na walichokuwa wanafanya, kwakweli Vaileth alikuwa wa kwanza kushangaa na kuona aibu sana kwani wale watu walikuwa ni Prisca, shangazi yake na yule mganga yani yule mganga ndio alikuwa mtupu kabisa.
Junior nae alichukia sana na pale pale alienda kumkaba yule mama aliyekuwa mtupu kabisa na kuanza kumpiga yani kile kitendo kilikuwa kama kimewazindua wale watu kwani walikuwa kama wamepigwa na bumbuwazi hivi, kisha mlinzi nae aliwakamata na kuwaingiza ndani ambapo waliwakalisha chini, kwakweli baba Angel alisikitika sana kumuona tena Prisca,
“Hivi wewe si nimetoka kukutoa tu asubuhi ya leo jamani!! Sasa unapata faida gani kufanya haya?”
Prisca aliishia tu kusema nisamehe yani hata hawakujua wanaongelea kitu gani, inaonyesha walichanganyikiwa, basi shangazi akaanza kumlaumu yule mganga,
“Si ulisema hatutaonekana?”
“Hata mimi nashangaa imekuwaje tumeonekana”
Mama Angel aliwaambia,
“Nyumba ya maombi hii, mlidhani mtafanya ujinga wenu tusiwakamate/ nyumba yangu daima naifunika kwa damu ya Yesu, hakuna mtakalofanya kwangu likafanikiwa. Hivi siku zote tunawakamata, hata hamjishtukii kuwa hiki tunachokifanya hakifai?”
Kisha mama Angel alimuangalia Vaileth ambaye alikuwa kajiinamia akilia kwani ni aibu kubwa sana ndugu zake wamemletea,
“Vai, hebu waulize ndugu zako vizuri ni lini wataacha kufanya huu ujinga? Au wanataka tukufukuze kazi?”
Junior akadakia,
“Sasa mamdogo umfukuze kazi sababu ya hawa wanga? Yani hawa ni wakuwashughulikia tu, mimi mkiniachia hawa lazima maji wataita mma na siku hiyo sijui kama wataendelea tena na uchawi maana kipigo nitakachowapatia wakizinduka watakuwa hoi na watakufa kabisa”
“Mmmmh Junior jamani, hayo mambo sio kabisa. Ngoja niongee na nyie watatu, jamani hili ni onyo la mwisho, nawaambia hamnijui mimi nilivyo, mimi ni katili sana kupita mnavyoniona, nasema kuwa hili ni onyo la mwisho, nimemaliza”
Kisha mama Angel akasema kuwa waachiwe tu, ila Vaileth akaomba jambo moja,
“Naomba jambo moja toka kwako mama, naomba hawa ndugu zangu wapelekwe tu kanisani, muwaache huko wafanyiwe maombi”
Mama Angel na baba Angel waliona hilo ni wazo zuri basi waliwapandisha wale watu kwenye gari lao huku yule aliyekuwa mtupu akipewa kanga na shangazi mtu ili ajistiri kisha wakaondoka nao kuelekea kanisani ili wakawaache kwenye maombi.
 
SEHEMU YA 140


Ndani ya nyumba alibaki Vaileth na Junior, ila muda huu Vaileth alikaa sebleni huku kajiinamia akilia yani alikuwa akiona aibu sana kwa kitendo kile hata hakujua ni kwanini ndugu zake waliamua kufanya vile, basi Junior alienda kumbembeleza,
“Pole sana, usilie wala nini ni mapito tu”
“Kwakweli sielewi kabisa, ndugu zangu wananitakia nini mimi? Wanataka mimi nifukuzwe kazi jamani! Nitaenda wapi mimi wakati hapa nilipo sina lolote mimi”
“Hamna usiseme hivyo Vai, wewe ni mtu wa maana sana, achana na hao ndugu zako vichaa. Kuwa na amani Vaileth, nyamaza”
Basi Vaileth aliinua kichwa chake na Junior alikuwa akimfuta machozi yake, muda huo Erick na Erica walirudi kutoka shuleni kwahiyo walivyoingia ndani walimkuta Junior akimfuta machozi Vaileth, basi waliwasalimia tu na moja kwa moja Vaileth nae aliinuka na kwenda jikoni kufanya mapishi ya jioni.
Basi Junior nae alimfata kule jikoni na kumwambia,
“Kama kuna kitu cha kukusaidia niambie maana mimi naweza kupika vyakula vya aina zote”
Vaileth akatabasamu tu na kusema,
“Basi nisaidie kukuna nazi”
“Oooh hiko tu, nipe nikune”
“Aaaah mimi natania bhana”
“Ila si kweli unataka kupika chakula cha nazi?”
“Ndio ni kweli ila nitakuna mwenyewe”
“Kwani hizo nazi ziko wapi?”
Junior aliuliza hivyo huku akiangaza jikoni na alivyoziona tu zikiwa tayari zimeshavunjwa kwahiyo Vaileth alishaziandaa kwaajili ya kukuna, basi Junior alivuta kibao cha kukunia nazi na kuanza kukuna ile nazi, kwakweli Vaileth alimuangalia tu na kumshangaa sana maana yeye alikuwa akimfanyia masikhara tu ila alishangaa kuona Junior alimaanisha na alianza kukuna nazi hiyo.

Basi muda huo Erica na Erick kila mmoja alikuwa chumbani kwake, ila Erica alipomaliza tu ni moja kwa moja alienda jikoni ili kuangalia chakula ila alivyomkuta Junior akikuna nazi alishangaa sana hadi Junior alimuuliza,
“Unashangaa nini Erica? Kwani hujawahi kumuona mwanaume akikuna nazi?”
“Hamna kitu”
Kisha Vaileth akamwambia,
“Chakula kipo cha mchana kwenye hotpot ya pale juu”
“Hamna hata sitaki chakula ila nilikuja kuangalia tu chakula cha usiku unapika chakula gani?”
“Napika wali na njegere, walindio huu namalizia na njegere naziunga muda sio mrefu”
“Sawa, mimi nitakula hiko”
Kisha Erica aliondoka na moja kwa moja alienda chumbani kwa kaka yake na kuanza kumwambia,
“Erick, hivi tulivyoingia ndani uliwaelewa dada Vaileth na Junior?”
“Sikuwaelewa ila nahisi kama Junior alikuwa akimbembeleza Vaileth”
“Sasa muda huu nimeenda jikoni na nimemkuta Junior akikuna nazi”
“Mmmh!”
“Ndio hivyo kaka, unahisi nini kinaendelea?”
“Jamani, huyo Junior kaja jana tu halafu leo ndio kaanza kumnyemelea na huyo dada!”
“Ila akimkubali ni ujinga wake, maana kila siku humu ndani inaongelewa tabia mbaya ya Junior halafu yeye amkubali kweli mmh!”
Kisha Erica akaenda kitandani kwa Erick na kujilaza ambapo usingizi ulimpata pale pale.

ITAENDELEA KESHO
 
SEHEMU YA 141

Basi baba Angel na mama Angel walirudi usiku na kuita pale na kuanza kuwasimulia kilichotokea kwenye maombi, ila muda huu Erica hakuwepo maana bado alikuwa amelala chumbani kwa Erick, basi mama Angel alipomaliza kuelezea aliuliza,
“Erica yuko wapi?”
Erick alijibu,
“Amelala, ngoja nikamuite”
Basi Erick aliinuka na mama Angel nae aliinuka na kumfata kwa nyuma, alishangaa kuona Erick akielekea chumbani kwake, basi alimuuliza,
“Kwani Erica kalala huko kwako?”
“Ndio mama”
“Jamani, si nimeshawakataza hiyo tabia lakini!”
“Ila mama jamani, Erica si dada yangu! Kwanini unanitenga nae kiasi hiki!”
“Sitaki kusikia hayo”
Basi moja kwa moja mama Angel alienda hadi kule chumbani kwa Erick na kuanza kumuamsha Erica kwa kumpiga vibao ambapo Erica alishtuka kisha mama yake alianza kumsema,
“Hivi wewe mtoto unanitaka nini lakini? Siku zote nakukataza kuingiliana vyumba na kaka yako, mmekuwa wakubwa sasa, nimewatengea kila mtu chumba chake nikiwa na maana nzuri kabisa, niondolee balaa hilo mimi, haya inuka upesi hapo”
Basi Erica aliinuka na kuelekea chumbani kwake, yani muda huo mama Angel nae alielekea chumbani kwake huku akilalamika ila mumewe nae alikuwa huko na kumsikiliza mkewe akilalamika kisha kumuuliza vizuri ambapo malalamiko ya mkewe yalikuwa ni yale yale ya siku zote kuhusu Erica na Erick,
“Ila mke wangu utafatilia hao watoto hadi lini jamani! Hebu kuwa na imani maana hao ni ndugu ujue, acha kuwawazia mabaya watoto”
“Mimi siwawazii mabaya ila sipendi tabia ambayo wanaifanya wakati kila mmoja ana chumba chake, haswaaa Erica jamani ameanza tabia mbaya sana”
Basi waliongea kidogo pale na kuamua tu kulala kwani walikuwa wamechoka sana kutokana na shuruba za siku hiyo.

Tangu Junior aanze kuishi hapa nyumbani kwa mamake mdogo alibadilika sana kitabia, kwani alikuwa akitoka shuleni ni moja kwa moja anarudi nyumbani na alionekana kusoma kwa bidii sana tofauti na siku zote, mpaka shuleni alifatwa na Husna ili kuulizwa vizuri,
“Junior mtoro mwenzangu, siku hizi nini kimekukumba? Maana sikuelewi ujue, yani siku hizi kila siku upo shuleni na hata hukosi hata siku moja”
“Nimegundua kuwa elimu ni kila kitu katika maisha, unaweza kuwa na mali nyingi na pesa nyingi ila bila elimu ni ngumu sana kuendesha hizo mali, utajikuta tu utazitapanya na mwisho wa siku unarudi tena kwenye ufukara. Acha nisome kwa bidii, naelewa ninachokifanya”
“Na lile ombi lako la kunitaka, nimekubali”
Junior alicheka na kumwambia Husna,
“Hiyo ni sawa na mtu aliyekuwa kwenye mfungo wa Ramadhani halafu wewe uje kumwambia kuwa umekubali awe mpenzi wako, unataka afanye nini sasa? Atende dhambi au kitu gani?”
“Sina maana hiyo Junior, kwani wewe upo kwenye mfungo?”
“Hapana ila kwasasa nimeamua kuwa makini na masomo kwanza, kama umeamua kunikubali basi na wewe uamue tu kuwa busy na masomo yani hapo tutaenda sambamba”
“Jamani Junior, unanikatili ujue! Mimi masomo hayapandi wala nini na ubaya ni kuwa kila muda nakuwaza ndiomana nimeamua kukwambia haya”
“Husna, mimi ni kijana nisiyefaa kabisa, unionavyo hapa ni kijana mdogo ila nishatembea na watu wa kila dizaini unayoijua wewe, yani hata wewe hutokuwa na jipya kwangu”
“Sasa kwanini ulinitongoza?”
“Mimi kutongoza ni kawaida yangu tu ndiomana hata hapa shuleni ukifatilia unaweza kuta karibia kila msichana nilimtongoza, atakayenikubalia ndio huyo huyo, ila kwasasa nimestaafu kwanza”
Husna alichukia sana kusikia vile, aliona kumbe Junior siku zote alizokuwa anamfatilia alikuwa akimjaribisha tu, basi alichukia mno na moja kwa moja akaondoka zake.
Muda wa kutoka, Junior kama kawaida ni moja kwa moja alirudi nyumbani kwa mamake mdogo na Vaileth alikuwa sebleni, kumbe kwa siku hizo Junior alikuwa akikaguliwa daftali zake na Vaileth,
“Umeona, nipo makini sana kwasasa”
“Hivi ndio inavyotakiwa, usijali kuhusu mimi ila ninachohitaji ni kuona kuwa umesoma na umefika mbali kimaendeleo na kimaisha”
“Asante sana Vai ndiomana upo kwaajili yangu”
Leo Erica aliwahi kurudi kushinda Erick kwahiyo alimkuta Junior akiongea lile neno la mwisho na kumfanya agune sana, kisha aliwasalimia na kuondoka zake, ila Vaileth na Junior walimuangalia tu, ndipo Junior alipomwambia Vaileth,
“Usijali matendo ya huyu dogo ndio zake, anapenda umbea umbea tu”
“Namjua mambo yake”
Basi Junior aliinuka na Moja kwa moja alienda chumbani kwake yani kwa kipindi hiko ilikuwa ni masomo tu masomo na yeye.
 
SEHEMU YA 142

Leo Elly wakati katoka shuleni alionekana kumkumbuka sana Erica, yani alitamani mno uwepo wake, kwa siku hizo alikuwa ni mpweke sana ukizingatia Erica hata kuaga hakuaga wala nini basi roho ilimuuma sana.
Siku hiyo wakati wanatoka shule, Abdi alimfata na kumuuliza,
“Vipi dada yako Erica yuko wapi?”
“Aaaah usiniulize bhana”
Basi Abdi alicheka sana na kusema,
“Dada, dada halafu dada mwenyewe hujui chochote kinachoendelea juu yake. Kaka wa Erica ni Erick tu, wewe sijui ulitokea wapi, ungemuona Erick alichokuwa akifanya kwa dada yake ndio ungeelewa maneno yangu kuwa kaka wa Erica ni Erick tu lakini sio wewe wa kujipendekeza kama mimi, ukanivizia chooni na kunipiga juu ila mbona hujui dada yako alipo!!”
Abdi aliondoka huku akimcheka, yani maneno yale yaliumiza sana moyo wa Ellyn a siku hiyo alivyorudi kwao alimsimulia mama yake jinsi alivyomkumbuka Erica na jinsi Abdi alivyomshushua, basi mama yake akamwambia,
“Usijali mwanangu, nitahakikisha napafahamu wanapoishi wakina Erica na nitakupeleka tu”
“Uuuh asante mama kwa kunijali”
“Usijali mwanangu, mimi mama yako niko tayari kufanya chochote kwaajili yako hii yote ni sababu ya upendo nilionao juu yako”
Elly alitabasamu na kufurahi sana kwani aliona kuwa mama yake anamjali sana.

Mama Angel kwasasa kidogo mimba yake ilianza kumchosha ingawa bado ilikuwa ni ngumu kuonekana, mumewe alikuwa akifanya jambo moja kwake kila siku yani ilikuwa kama siku hiyo mkewe alitoka basi muda wa kurudi lazima aende kumchukua yani kile kitendo kilikuwa kikiwatia wivu watu wengi sana.
Basi siku hiyo baba Angel aliamua kwenda kumfata mke wake kama kawaida yake, basi alivyotoka tu walishangaa kukutana na mtu ambaye walikuwa wakimfahamu kwa muda mrefu sana, mtu huyo alikuwa ni Dora yani yule rafiki wa mama Angel, basi aliwasimamisha na kuanza kuongea nae,
“Kheee jamani wapendanao, yani nyie mnafanya kila mtu atamani maisha ya mahusiano huku akifikiria kuwa maisha yote ya mahusiano yapo hivi kumbe ni bahati tu”
“Hapana jamani, sio bahati ili ni kufanya maamuzi tu, wote wawili mkiamua kwa nia ya dhati basi inawezekana”
“Ila nashukuru kuwaona jamani, shemeji najua una miradi mbalimbali naomba umsaidie mdogo wangu”
“Mdogo wako!!”
“Ndio, yule mdogo wangu Steve yani yupo tu hana kazi yoyote ya kufanya, naomba mumsaidie jamani”
“Kwani huyo Steve yuko wapi?”
“Yupo nyumbani”
“Kheee huyo Steve si alioana na Sia! Inamaana yupo nyumbani kwenu na mke wake!”
Mama Angel aliuliza kwa mshangao sana na Dora alimjibu,
“Kwa kifupi ni hivi, Steve haishi tena na yule mwanamke, waligombana na kutalikiana, si unajua mapenzi ya dawa huwa hayadumu! Sasa Steve na udogo ule wa kipindi kile akaishi na mwanamke mkubwa kama Sia ili iweje jamani! Kwahiyo Steve yupo nyumbani tu”
“Na mtoto wao je?”
“Mmmh jamani, maswali mengine mtamuuliza mwenyewe, ila naomba tu mnipe kibali ili nimwambie aje kwenye ofisi zenu na mumpatie hiyo kazi”
Mama Angel na baba Angel waliangaliana kwa muda kisha baba Angel alitoa kadi yake yenye namba za simu na kumkabidhi Dora kisha akamwambia kuwa huyo Steve amtafute halafu atawasiliana nae, na baada ya hapo walimuaga na kuingia kwenye gari lao kisha safari ya kwenda nyumbani kwao ikaanza.
Wakati Dora nae akitaka kuondoka eneo lile alishangaa mtu akimsimamisha na kumuuliza,
“Unawafahamu vizuri wale?”
“Ndio nawafahamu”
“Yule mama anajishauwa sana, yani anaona kamavile kaibeba dunia”
“Mmmh, kwanini unasema hayo?”
Yule mwanamke aliondoka zake, ila Dora aliona ni vyema akipata muda amtahadharishe rafiki yake kwani aliona kuwa kuna watu hawana lengo zuri na rafiki yake.
 
SEHEMU YA 143

Leo wakati Tumaini kaamka akifanya usafi kidogo wa nyumba yake, alipigiwa simu basi aliamua kuipokea na kuanza kuongea nayo,
“Tumaini, ni mimi Sia”
“Oooh jamani kumbe, halafu sijui namba yako sikuaiandika jamani!”
“Hamna bhana ila sikukupa, ila leo nimekukumbuka sana nahitaji kukutembelea ili niongee kidogo tu na wewe”
“Oooh karibu nyumbani kwangu basi, karibu sana”
“Nielekeze basi ili nije, maana nataka kuja le oleo”
Basi Tumaini alimuelekeza Sia mahali ambapo anaishi kisha akaagana nae na yeye aliendelea na kazi zake kama kawaida.
Basi alivyorudi kupumzika, alikaa kidogo na Sia alimpigia tena simu maana tayari alishafika nje ya geti lake, basi Tumaini alienda kumfata nje na kumkaribisha vizuri sana, ambapo Sia nae alikaribia ndani na moja kwa moja walianza kuongea mambo mbalimbali ya zamani,
“Nikikumbuka kipindi kile nacheka sana, yani Tumaini tulikuwa tukienda nyumbani kwakina Erica na kufanya vurugu zetu ila leo hii umenisahau kabisa, kweli nimeamini maneno ya watu yani mawifi sio wa kuwaamini kabisa maana ufata upande ule wa kaka zao”
“Mmmh na wewe Sia bado una hay ohayo tu jamani!!”
“Sikia nikwambia Tumaini yani kamwe siwezi kusahau, ujue Erick nilimpenda sana yani nilimpenda kiasi kwamba hadi kesho bado nampenda”
“Duh! Ila ni mume wa mtu tayari”
“Najua hilo na ninaheshimu ndoa yake ten asana tu, ila natamani kuonana nao ili angalau hata niwaombe msamaha maana hata sikumbuki kama walinisamehe”
“Mbona walikusamehe kitambo sana, tena Erick aliniambia kuwa kuna siku alikuona akasimamisha gari na kukupigia honi ila ukaondoka kwa haraka haraka”
“Mmmh jamani, sijamuona mbona, ila unaonaje tukienda kwao muda huu!!”
“Dah! Sijajipanga kabisa kwenda huko jamani, yani leo hata sijajipanga”
“Mimi nakuomba shoga yangu, nikawasalimie tu”
Mara simu ya Tumaini ilianza kuita na mpigaji alikuwa ni kaka yake basi aliinuka na kutoka nje ili aongee nayo, na alipoipokea tu alianza kusema,
“Mwenzangu leo Sia kaja nyumbani kwangu na amekazana nimlete kwenu”
Kumbe kwenye ile simu alikuwa ni mama Angel ambaye alishtuka sana na kusema,
“Aaaah Tumaini, kumbe bado una ushirika na huyo mtu!! Simtaki nyumbani kwangu kabisa”
“Oooh samahani wifi”
“Haya niambie ni ajenda gani ambayo huwa unapanga na kaka yako dhidi ya huyo mwanamke?”
“Hakuna lolote ndugu yangu, nisamehe bure tu”
Ilionekana mama Angel kachukia sana hata Tumaini aligundua hilo basi alivyorudi ndani ilibidi amdanganye maneno mengine Sia,
“Yani nimepigiwa simu na mume wangu hapa, kasema nimfate sasa hizi kazini kwake, samahani shoga yangu sitaweza”
“Basi nielekeze, niende mwenyewe”
“Hapana Sia, yani hata kukuelekeza sijui naanzia wapi yani sehemu yenyewe haielekezeki ujue”
“Mmmmh Tumaini, unanifanyia kusudi, haya bhana kajiandae tuondoke wote”
Yani Tumaini hakuwa na namna zaidi ya kwenda kujiandaa ili kuondoka tu na moja kwa moja alielekea ofisini kwa mume wake ingawa hakutaka kufanya hivyo.

Tumaini alipofika ofisini kwa mume wake hakuwa na wasiwasi wowote ule kwani moja kwa moja aliamua kwenda ndani ya ofisi, alishangaa mumewe kaka halafu kuna mwanamke amekaa mbele ya mumewe na huyo mwanamke alikuwa amevaa nguo za mitego sana.
Tumaini akapatwa na hasira kwani alimsogelea yule mwanamke na kumkunja halafu alimzaba vibao kama vitano ila alipomuachilia yule mwanamke alianguka chini


Tumaini akapatwa na hasira kwani alimsogelea yule mwanamke na kumkunja halafu alimzaba vibao kama vitano ila alipomuachilia yule mwanamke alianguka chini kabisa.
Ilibidi mumewe asogee karibu na alipo mkewe ila Tumaini wala hakushtuka kitendo cha yule dada kuanguka wala nini, mumewe alianza kumfokea,
“Ndio mambo gani haya umefanya mke wangu jamani! Ona sasa”
“Ulitaka nifanyeje sasa? Kumbe unakawia kurudi nyumbani sababu ya malaya kama hawa!”
Mumewe aliinama chini na kujaribu kumuamsha yule dada, kumbe alikuwa amezimia kwahiyo ilibidi ampatie huduma ya kwanza kwa kummwagia maji ambayo yalikuwepo mule ofisini na mdada alizinduka na yule mume wa Tumaini akawa anafanya kazi ya kumuinua pale chini ila kile kitendo ndio kwanza kilizidi kumuumiza Tumaini na muda huo huo Tumaini aliinuka na kuondoka zake bila ya kusema chochote kile.
Alirudi kwenye gari lake na kukaa kwa muda kisha alijikuta akianza kulia yani alitokwa sana na machozi na kwa muda huo hakujua ni wapi aende ilia pate faraja ya kile kilichomtokea, akaona ni vyema aende kwa wifi yake mama Angel ili akaongee nae kidogo kwani alihisi pengine atamfariji.
Muda ule ule aliwasha gari yake na kuondoka mahali pale, moja kwa moja alienda hadi kwa mama Angel ambapo mlinzi alimfungulia geti na alipoingia ndani tu alimuomba mama Angel ili akaongee nae kwenye bustani kwani hakutaka kuongea nae ndani, kwa haraka haraka mama Angel alijua kuwa wifi yake anataka kuongelea habari za huyo Sia, basi aliondoka nae huku kajipanga ya kumjibu ila alishangaa alichoanza kumueleza,
“Sikia Erica ni hivi, nilipomkatalia Sia kumleta huku basi nikamdanganya kuwa mume wangu kanipigia simu na anataka niende ofisini kwake, basi akasema hakuna shida nakusubiri twende wote, sikuwa na jinsi kweli zaidi ya kwenda nae tu ambapo nilimshusha pale ofisini na tuliagana halafu mimi nikaingia ofisini kwa mume wangu, nilichokutana nacho sasa!!”
Tumaini aliangusha machozi kwa mara ya kwanza na kumfanya mama Angel amuulize kwa makini,
“Kwani kitu gani ulichokutana nacho?”
Tumaini akaanza kumsimulia wifi yake jinsi alivyomkuta mumewe na yule mwanamke ofisini, kisha akasema,
“Yani mimi ndiomana katika maisha yangu nilikuwa sipendi kuolewa, sipendi kuwa na mahusiano, wanaume hawaaminiki kabisa. Nampenda mume wangu, namuheshimu namjali na sijawahi kufikiria kumsaliti hata mara moja, wala kuongea na wanaume wengine sitaki kwani mimi hawanitongozi? Nina ubaya gani wa kushindwa kufatwa na wanaume wengine? Kwanini yeye nimkute ofisini kaka na yule mwanamke kwa mikao ya kihara namna ile halafu anajifanya kumjali zaidi yule mwanamke kuliko mimi!! Najuta kwanini hata nilikubali kuolewa”
“Jamani wifi yangu ndio umepaniki hivyo jamani!! Ila sidhani kama kaka yangu ana mahusiano na huyo mwanamke jamani!”
“Najua unamtetea tu”
“Kweli Tumaini, kaka yangu hawezi kufanya hivyo jamani”
“Hebu kaniitie Erick, labda anaweza akanielewa”
Basi mama Angel aliinuka na kwenda kumuita mume wake ambaye baada ya muda mfupi alifika nae kwenye ile bustani, basi Tumaini alianza kumueleza kaka yake kuhusu kile kilichotokea ambapo nae kaka yake alimtia moyo na kumwambia kuwa haiwezekani kwa shemeji yake kuwa na mahusiano na huyo mtu,
“Hapana, nyie mnamtetea tu, natamani niondoke nyumbani kwangu”
“Jamani mama Leah, sasa uondoke nyumbani kwako kwasababu hiyo kweli! Hebu kumbuka ni miaka mingapi mmeoana na kaka yangu je kuna lolote baya amewahi kukutendea? Ni wazi kuwa kaka yangu anakupenda sana ila nadhani hujaelewa kilichotokea kabisa wifi yangu, ila najua akirudi nyumbani mtayasuluhisha tu”
Basi walijaribu pale kumshauri na kumpa moyo ambapo kidogo alifurahi na mwisho wa siku aliaga na kuaondoka zake.
 
SEHEMU YA 144

Usiku wa leo Elly akiwa nyumbani na mama yake, alipewa ujumbe ambao ulimfurahisha sana kwani mama yake alimwambia,
“Mwanangu Elly, tayari nimeshapafahamu anapoishi Erica”
“Jamani mama, ni kweli!”
“Ndio mwanangu, si nilikwambia kuwa, kwako wewe nipo radhi kufanya chochote kile sababu nakupenda sana”
“Asante sana mama”
Elly aliinuka na kumkumbatia mama yake kwa furaha kwani alijihisi rah asana kwa mama yake kumtimizia hitaji lake, kisha akamuuliza tena,
“Eeeeh mama, na lini nitaenda kumuona baba yangu au ndugu zake baba?”
“Sasa utaendaje kumuona baba yako wakati alikukataa ukiwa mdogo kabisa mwanangu! Yani ulipozaliwa, sijui baada ya miezi miwili, baba yako akaanza oooh huyu mtoto mbona sifanani nae, mara hii miguu mikubwa sio yangu, mara haya macho sio yangu yani alikuwa akitoa kila kasoro, huyo bibi yako na shangazi yako walipofika ndio kabisa yani walikataa katakata kuwa wewe ni damu yao, hivyobasi waliondoka na baba yako na toka kipindi hiko hakurudi tena kabisa, kwahiyo mwanangu ningefanya nini tena mimi? Niliamua tu kukulea kwa nguvu zangu zote ili ukue na uwe mtoto mzuri na badae uweze kunisaidia, kwakweli nashukuru sana kwa hilo kwani nimekulea kwa kipindi chote hiki hadi leo”
“Ila mama, je ni kweli huyo hakuwa baba yangu?”
“Mmmh sasa swali gani unaniuliza hilo mwanangu jamani! Utaniumiza kichwa change bure, ila amini kuwa nakupenda sana mwanangu, hakuna ninayempenda maishani mwangu kama wewe, nakupenda sana”
“Asante sana mama ila lini tutaenda kwakina Erica mama?”
“Subiri mwanangu, tutaenda tu”
“Nashukuru mama”
Elly alifurahi sana na kumkumbatia mama yake kwa furaha.

Mume wa Tumaini aliporudi nyumbani na kumkosa mke wake, moja kwa moja aliamua kwenda nyumbani kwa baba Angel kwani alihisi kuwa lazima mke wake amekimbilia huko, kumbe wakati kaondoka ndio wakati huo huo mkewe nae alikuwa kaondoka kwa mama Angel.
Basi alivyofika nyumbani kwa mama Angel moja kwa moja dada yake alimkaribisha vizuri sana na kuanza kuongea nae,
“Oooh yani wifi yako sijamuelewa ujue, yani kilichomfanya achukie hivyo ni nini?”
“Kwani huyo msichana alikuwa ni nani kaka yangu?”
“Yani unafikiri naelewa basi, yule msichana alifika ofisini kwangu, yani hata dakika mbili hazijapita yani hata kuongea nae sijaongea nae ila mke wangu aliingia muda huo huo na kuanza kufanya varangati lake, kwakweli mimi sielewi na yule msichana hadi nimemmwagia maji ndio kazinduka basi nikamuinua na kumuweka kwenye kiti ndio mke wangu kachukia na kuondoka, ila yule msichana nae aliondoka baada ya muda mfupi tu yani hata mimi mwenyewe binafsi sijaelewa chochote. Yule msichana alifata nini ofisini kwangu? Unajua hata kama nataka kufanya ujinga basi siwezi kufanya huo ujinga kwenye ofisi yangu jamani!”
“Duh! Pole sana kaka, ila kaa vizuri na mkeo tu umueleweshe unajua mara nyingine kuna mambo mengine yanatendeka bila kujua ni kwanini yametendeka kumbe lengo kubwa ni kusambaratisha ndoa yenu, mueleweshe vizuri mkeo”
“Asante dada yangu, ngoja niondoke kwanza”
Basi mume waTumaini aliaga na kuondoka zake na wala hakuonana na baba Angel kwa muda huo maana baba Angel alikuwa kalala.
Basi mama Angel moja kwa moja alienda chumbani kwake na kuamua kupumzika tu.

Kwakweli Erica kwenye hii shule mpya alikuwa kapooza sana kwani alijikuta akipenda sana shule zenye mchanganyiko wa jinsia kuliko shule za jinsia moja, basi siku hiyo alipokuwa darasani kuna msichana mmoja alikaa nae karibu na kuanza kuongea nae,
“Erica mbona unaonekana hupendi kukaa karibu na wengine? Yani wewe hujishughulishi na maongezi ya aina yoyote ile”
“Aaaaah mimi ni msikilizaji tu na sio muongeaji”
“Ila mimi nakupenda sana, yani natamani uwe rafiki yangu”
“Usijali basi, tumekuwa marafiki. Si unaitwa Samia eeeh!”
“Ndio, ndio jina langu hilo”
“Basi, kuanzia leo sisi nimarafiki”
“Oooh nimefurahi sana, nitamuhadithia mama yangu kuhusu wewe na kwa hakika atafurahi sana, ujue nini eeeh! Mama yangu lazima atataka kukufahamu si hautakuwa na tatizo kwa hilo eeeh!”
“Aaaah sina tatizo juu ya hilo, hata mama yangu atapenda kukugfahamu pia na kufahamu kwenu pamoja na kumfahamu mama yako”
“Basi tunakuwa marafiki wazuri”
Erica na Samia walikumbatiana na kufurahi juu ya hilo kuwa wamekuwa marafiki sasa.
Mpaka muda wanaenda nyumbani waliagana vizuri sana na kila mmoja kupanda kwenye basi la shule linaloelekea mitaa ya kwao.
 
SEHEMU YA 145

Erica alivyofika nyumbani kwao, jambo la kwanza alianza kumsimulia mama yake kuhusu rafiki yake mpya aitwaye Samia,
“Oooh ushapata rafiki eeeh! Naimani mwanangu hautopooza tena”
“Ndio mama, nimefurahi sana ila naimani mara moja moja utaniruhusu nikamtembelee kwao”
“Hakuna hiyo kitu labda yeye ndio aje hapa”
“Sawa mama, napo hakuna tatizo”
Basi Erica aliingia chumbani kwake na alipomaliza kubadili nguo tu alienda kumwambia Erick kuhusu rafiki mpya aliyempata maana kwake ilikuwa ni kawaida kwa jambo lolote likitokea kwake basi ni lazima aje kuhadithia,
“Ooooh hongera sana mdogo wangu, nimefurahi kusikia hivyo kwani najua sasa utaanza kuwa na furaha, tatizo lako hupendi kuwa na urafiki na wasichana wenzio ila leo Mungu ni mwema maana umeweza kuwa na urafiki na msichana mwenzio kwakweli nimefurahi sana mdogo wangu”
Basi wakaongea ongea pale na kisha wote kwa pamoja kutoka na kwenda kula.
Muda wanakula, ni muda ambapo Junior na Vaileth nao walikuwa wanakula kwahiyo mezani walikuwa wanne ila macho ya Erica yalikuwa yakigonga kwa Junior na Vaileth ila aliwaona kama wakikonyezana vile, basi alikuwa akiwaangalia sana na wao hata hawakuwa na habari kuhusu lile swala na walipomaliza kula, Vaileth alitoa vyombo vyake pamoja na vyombo vya Junior huku Erica akitoa vyombo vyake na vya kaka yake.
Waliporudi chumbani, Erica alienda tena kuongea na kaka yake,
“Mmmmh leo sasa, ndio dada Vaileth na Junior nimewaona kabisa wakiwa wanakonyezana”
“Ila usishangae sana Erica, yule ndio shemeji yangu kwa Junior ujue na wewe ndio wifi yako”
“Ila mbona dada Vain i mkubwa kwa Junior?”
“Mapenzi hayana umri Erica!”
“Mmmmh!”
“Ndio hivyo, mapenzi hayachagui umri, hayachagui kabila wala rangi, mapenzi ni kama nyasi yani huota popote”
“Aaaah kumbe! Basi nimekuelewa”
Siku hiyo Erica alirudi tu chumbani kwake na kwenda moja kwa moja kulala tu.

Leo mama Angel alienda kwenye biashara yake, ila alipofika na kukaa kaka kidogo alipigiwa simu na rafiki yake Dora,
“Nipo mitaa ya ofisi yako hapa, uko wapi?”
“Mbona nipo ofisini”
“Basi nakuja”
Baada ya muda kidogo Dora aliwasilia kwenye ofisi ya mama Angel na kuanza kuongea nae mambo mengi ikiwa ni pamoja na kusifia ile ofisi yake,
“Unajua sikuwahi kuingia humu jamani, kwakweli hongera sana rafiki yangu”
“Asante”
“Kwasasa naamini kuwa mara nyingine maisha ni jinsi wewe binafsi unavyochagua, yani Mungu ni mwema kwetu ila sisi wanadamu tuna mtindo wa kulazimisha mambo na mwisho wa siku tunaharibu kusudi la Mungu katika maisha yetu. Nakumbuka mimi nilikuwa muhuni sana, na uhuni ulikuwa kama sehemu ya maisha yangu, sikutaka mtu aniambie chochote kile, yani mtu akisema swala la Dora acha uhuni basi mtu huyo nilimuona ni mbaya na sikutaka hata kumuona tena, ila kwasasa sitamani hata kidogo mwanangu Jesca kuwa na tabia kama zangu, mimi nikawa kama sijasoma vile yani kama nimesomea uhuni sasa maana kila aina ya umalaya niliifanya, kwakweli kuna muda mwingine nastahili kukupongeza sana tu”
“Mmmh ila shoga yangu nami nimepitia makubwa sana, yani dah huwa nikikumbuka hadi huwa siamini kama niliwezaje kukwepa ile misumari, loh! Nimeandamwa mimi jamani, nimeandamwa hatari, kila niliposhika palikuwa hapashikiki na kote naambulia machungu tu, ila kwa Erick nashukuru sana Mungu maana alinisimamia”
“Nakumbuka shoga yangu, na yule mjinga Sia ndio angekuvuruga kabisa nay ale madawa aliyotaka kumpa Erick, uwiii ule ndio ulikuwa muda ambapo Erick angekusahau nadhani sijui ungeenda kuolewa mke wa pili kwa Bahati maana ulikuwa na mawazo wewe”
Mama Angel alicheka kisha akamwambia,
“Tena umenikumbusha kuhusu huyo Sia”
“Eeeeh kafanyaje tena?”
Basi mama Angel alianza kumsimulia mlolongo mzima wa jinsi alivyompigia simu Tumaini na jinsi ilivyokuwa hadi muda ambao Tumaini alienda kwake akilia, kwahiyo yote alimsimulia basi Dora akamwambia,
“Mmmmh shoga yangu, unajua mimi hadi leo simuamini Sia kabisa, yani simuamini yule mwanamke kama kweli aliamua kwa moyo safi kuachana na nyie!! Sijui kwakweli ila sina imani nae”
“Ila kwanini unasema hivyo?”
“Hebu angalia hata hilo tukio la Tumaini, alimgomea kuja nae kwako, Tumaini akadanganya anaenda ofisini kwa mumewe ila hajakubali hadi kamsindikiza, haya sasa nini kimetokea baada ya kumshusha? Tumaini kamkuta mumewe na mwanamke ofisini hivyo Tumaini akapaniki na moja kwa moja akaja kwako, yani hapo jua kuwa Tumaini alivyokuja kwako basi nae alikuwa nyuma yake yani hapo tambua kuwa nyumbani kwako panajulikana na Sia tayari”
“Mmmmh!”
“Usigune, angalia tena hilo tukio huyo mwanamke kaingia dakika mbili kwenye ofisi ya kaka yako na muda kidogo Tumaini nae kaingia, kamzaba vibao kidogo kazimia, haya kazinduka Tumaini kaondoka kwa hasira na huyo mwanamke nae kaondoka, je kwanini asieleze shida yake kama ni kweli alikuwa na shida?”
“Inamaana ni ushirikina?”
“Mambo mengine sio hata ushirikina ila watu wana mbinu zao za kijasusi”
Dora alicheka kidogo kisha akasema tena,
“Yani ni hivi, yule Sia mimi simuamini ujue yani simuamini kabisa, kwa alichokifanya kwa Steve hapana kwakweli”
“Alifanyaje kwani?”
“Kwanza, alienda kujifungua kimya kimya tena kwa operesheni, hivi jamani mtu unajifungua kwa kisu kimya kimya kweli! Haya sasa, karudi kwa mumewe baada ya mwezi mmoja, hivi nani atamuamini yule mwanamke kama hajatoka kwa mwanaume wake mwingine kulelewa huko? Steve nae akachekelea tu mtoto wangu, mtoto wangu loh siku hiyo tumeenda na mama kumuona mtoto Mungu wangu yani mtoto hafanani na sisi hata ukucha, tukamuomba kwenda kupima kagoma, sasa tufanyeje jamani! Unajua Sia hajatulia kabisa, yani yule ana wanaume wengi hadi mwisho wa siku hajui baba wa mtoto ni nani, ila baada ya hayo ikawa kama akili ya Steve imerudi hivi basi tukaondoka na mdogo wetu tena kutugelesha mwanzoni alianza kumuita mtoto Steve, mwanamke shetani kabisa yule”
“Kheee kumbe ndio alifanya hivyo jamani!”
“Ndio, kuna siku nilikutana nae wakati mtoto sijui ana miezi saba nikakuta mtoto anasura nyingine yani sio ile ya udogoni, kwakweli ndio hafanani na sisi hata kidogo, kama hajazaa na wavua samaki huko ilia pate samaki wa bure sijui, nikamuuliza, ndio huyu Steve? Akasema ooh nyie si mlimkataa, nimembadilisha jina, anaitwa John, nikasema huyu mwanamke hajielewi yani anatanga tanga tu, sasa nadhani anampelekea baba yoyote na kumwambia mtoto wake na kumpa jina la huyo baba ila mtu aamini kuwa ni mwanae. Nikakumbuka hadi kipindi kile alichodai kuwa ana mimba ya Erick”
“Yani yule msichana ana wazimu ujue, sikapendi kweli. Kalinichanganya sana akili kipindi kile, ila ushanitisha tayari, inamaana amepafahamu kwangu?”
“Usichanganyikiwe ila kuwa makini tu shoga yangu yani mimi nimefanya kukutahadharisha tu na si vinginevyo”
“Sawa, nashukuru”
Kisha Dora akamkumbusha swala la kumtafutia mdogo wake kazi, kisha alimwambia kuwa atamkumbusha mumewe juu ya swala hilo.
Kwa muda huo waliongea sana hadi muda ulipofika ambapo mama Angel alienda kufatwa na mumewe ili waende nyumbani kwani mama Angel alikuwa anaenda hapo ofisini kwake ili asilale sana nyumbani.
 
SEHEMU YA 146

Baba Angel na mama Angel muda huu waliona ni bora kupitia hotelini ili wapate chakula cha hoteli kwa siku hiyo na wakirudi nyumbani wawe wameshiba tayari.
Basi walienda hotelini, wakati wameanza tu kula walishangaa kuna mtu alienda kukaa kwenye meza yao na kuwasalimia, mama Angel alishtuka sana ila kumuangalia mtu huyo alimuona ni baba Abdi, basi akamwambia,
“Bahati!!”
“Ndio ni mimi, mbona umeshangaa hivyo kwani umeona miujiza?”
Ila siku ya leo baba Angel alikaa kimya kabisa akiangalia tu kinachoendelea kanakwamba hakimuhusu vile, basi baba Abdi akaanza kusema,
“Nasikia umemuhamisha mwanao shule?”
“Ndio, ulitaka asome pale ili iweje? Abakwe na mtoto wako?”
“Jamani, mwanangu sio mbakaji. Samahani Erick, naongea haya ila kiukweli huyu mwanamke ni mwanamke ambaye nilimpenda sana nab ado ninampenda yani nusu na robo ya maisha yangu ipo kwenye mikono ya huyo mwanamke, unionavyo mimi nimebakiwa na robo tu ya maisha hapa nilipo”
Baba Angel hakujibu lolote lile, ila gafla pale walipokaa alienda mwanamke mmoja na kumkunja baba Abdi kisha akamwambi,
“Bahati! Bora leo nimekuona, wewe mwanaume ni mbaya sana, uliniacha na mimba, nimehangaika nayo peke yangu na nimekutafuta sana ila sikukupata kabisa, nimelea mtoto kwa shida sana tena peke yangu kwahiyo leo mguu wako mguu wangu twende nyumbani ukamuone mtoto wako na ikiwezekana tutaondoka wote kwenda kwako ili mwanangu nae apate maisha mazuri, yani unatanua tu wakati mtoto anapata shida”
“Duh utaniumiza jamani, hebu niachie kwanza”
Yule mwanamke akamuachia kisha baba Abdi akamwambia mama Angel,
“Haya ndio madhara uliyonisababishia baada ya kuniacha, sijui sasa huyu ni mtoto wangu wa ngapi!”
Kisha akainuka na kuondoka na yule mwanamke, kwa upande mwingine mama Angel alimsikitikia sana Bahati kwani kwa tabia alikuwa akimfahamu vizuri sana, hakuwa na tabia mbaya kusema labda kachukua mwanamke huyu mara yule ila kuna madawa alipewa ndio yamesababisha awe katika hali ile na kumsababishia kuwa na watoto wengi sana mpaka anahisi kuchanganyikiwa kabisa.
Basi walipomaliza kula ni moja kwa moja waliinuka na kuelekea nyumbani ambapo moja kwa moja waliamua kwenda kuoga tu na kupitiliza kulala.

Kilikuwa ni kipindi cha kujiandaa na mitihani ya taifa, kwahiyo kwa kipindi hiko Junior alikuwa anakaa macho mpaka usiku sana akijisomea, na siku hiyo alikaa sana usiku akijisomea mwisho wake kesho yake alichelewa kuamka, kwahiyo alipitiliza.
Vaileth alishangaa sana kwa siku hiyo kutokumuona Junior akienda shuleni asubuhi, basi aliamua kwenda moja kwa moja chumbani kwa Junior ili kumuamsha,
“Junior, wewe Junior, muda umeenda sana huendi shule?”
Junior alikurupuka sana na moja kwa moja kwenda kuoga, sasa wakati Vaileth akitoka chumbani kwa Junior mama Angel nae alikuwa akipita pale na kugongana macho na Vaileth, kwakweli mama Angel alimshangaa sana Vaileth kwani tabia za Junior zilikuwa zinajulikana.
 
SEHEMU YA 147

Junior alikurupuka sana na moja kwa moja kwenda kuoga, sasa wakati Vaileth akitoka chumbani kwa Junior mama Angel nae alikuwa akipita pale na kugongana macho na Vaileth, kwakweli mama Angel alimshangaa sana Vaileth kwani tabia za Junior zilikuwa zinajulikana.
Basi akamshtua pale Vaileth ambaye alishtuka utafikiri kashtuliwa na nini, kisha mama Angel akamuuliza,
“Wewe umeenda kufanya nini chumbani kwa mtoto wa kiume?”
“Aaaah mmmh mama….”
“Acha kujiuma uma, hebu eleza maelezo kamili”
“Mama ni hivi, leo sikumuona Junior kwenda shule, siku hizi huwa anasoma sana nikahisi labda kapitiliza kulala basi ndio nikaja kumuangalia na kweli nimemkuta alipitiliza kulala”
“Ni hivyo tu na hakuna lingine?”
“Kweli mama, ni hivyo tu mama”
“Mmmmh! Sema kama kuna mengine!”
“Sasa mama, mengine yapi na Junior ni mtoto mdogo”
“Mtoto mdogo! Anatembea na wakubwa kushinda hata umri wangu huyo mtoto hata haaminiki”
Mara Junior nae alitoka chumbani akiwa kavaa sare za shule sasa huku ana haraka kweli kiasi kwamba hata hakuangalia kama mamake mdogo pamoja na Vaileth walisimama kwani aliwapita pale pale na kuondoka, ilibidi mama Angel amkimbilie nje na kumsimamisha,
“Wewe Junior vipi?”
“Nimechelewa kweli leo mamdogo”
“Ngoja nikuwaishe shule basi”
Ilibidi mama Angel akachukue funguo haraka haraka na moja kwa moja kutoka nje halafu kupanda na Junior kwenye gari na kumpeleka moja kwa moja shule.
Ila njiani mama Angel alikuwa akimuuliza baadhi ya maswali Junior,
“Nasikia unasoma sana Junior?”
“Ndio mamdogo, sitaki kufeli”
“Hongera sana kwa hilo”
“Asante sana, yani namshukuru bamdogo sana kwa kuniokoa toka kwenye njia mbaya, pia nakushukuru nawe mamdogo ila shukrani zangu za pekee nitakujakumwambia mtu huyu wa kuitwa Vaileth yani huyu amekuwa msaada mkubwa sana kwangu na kunifanya nisome kwa bidii, amekuwa akiniambia vitu vyenye uhalisia sana, naona niliyokuwa nayafanya yote hayana maana tena kwenye maisha yangu”
“Oooh nafurahi kusikia hivyo”
Basi safari iliendelea hadi shuleni kwakina Junior.

Walipofika shule, Junior alimshukuru sana mamake mdogo basi alimshusha, na wakati amemshusha tu mwalimu wa nidhamu katika shule hiyo ambaye ni mwalimu Harun alimfata mama Angel na kusalimiana nae kisha alimuuliza,
“Kumbe ni wewe ndio unakaa na Junior siku hizi?”
“Ndio ni mimi”
“Oooh hongera sana, kwakweli unastahili pongezi yani umeweza kuibadili tabia ya Junior kiasi hiki!! Hongera sana, siku hizi yupo vizuri kwa maudhurio shuleni, siku hizi anasoma kwa bidii na anafanya mitihani vizuri naamini Mungu atamsaidia hata mtihani wa mwisho atafanya vizuri sana”
“Asante sana mwalimu”
Basi mama Angel aliongea ongea kidogo pale na mwalimu na kuagana nae halafu akaondoka zake, ila wakati anakatisha gari lake kuna mtu alimuona na kuamua kulisimamisha gari lake mahali kisha akashuka na kumfata yule mtu ambapo alimshika bega yani yule mtu alishtuka sana kwani hakutarajia kukutana na mama Angel, basi mama Angel alimuangalia na kumsalimia,
“Za siku nyingi Sia”
Sia alijibu kwa kujiumauma,
“Nzuri tu”
“Nasikia ulitaka kupafahamu kwangu, haya twende basi ukapafahamu”
“Aaaah hapana, leo nina kazi nyingi sana”
“Maana niliposikia nikasema sio vizuri wakati muhusika nipo, leo nimekutana na wewe nimefurahi sana na kukuomba twende ukapafahamu kwangu”
“Hapana Erica”
Kisha Sia akaondoka zake, basi mama Angel alimuangalia sana kisha akarudi kwenye gari lake na kuelekea nyumbani kwake.
 
SEHEMU YA 148

Mama Angel alivyofika kwake alijiandaa tena na kutoka kwani alijikuta akimkumbuka sana mama yake, basi aliamua kwenda kwa mama yake siku hiyo ili akamsalimie.
Alipofika kwa mama yake alishangaa sana kukutana na rafiki yake wa muda mrefu sana Fetty, basi walikumbatiana pale na kusalimiana, kisha alikumbatiana na mama yake na kusalimiana nae, basi walianza kuongea mawili matatu,
“Kwanza kabisa Fetty sikutegemea kama ningekukuta huku ujue!”
“Ni kweli, ila leo jamani nimesema acha nije kwa mama kupumzisha mawazo na akili kidogo, yani mimi ndoa imenifikia kooni jamani! Maji ya shingo kabisa yamenifika”
“Vipi tena?”
“Unajua karibu tunaanzisha timu ya mpira pale nyumbani maana sio kwa watoto wale jamani! Kweli nilijitoa muhanga kuishi na Bahati, niliamua kuolewa nae maana alipokuwa anaelekea kipindi kile ni kuwa kichaa, basi nikasema isiwe kesi ngoja nijitoe niolewe nae, na kweli tulioana na mwanzoni tukaishi vizuri tu. Kivumbi kilipoanza ni pale mtoto mmoja baada ya mwingine kuja kubwagwa kwangu yani naletewa watoto wa kila sampuli, sasa majuzi nimeletewa tena mtoto mwingine, kwakweli nachoka ujue yani nachoka sana”
“Eeeeh pole jamani Fetty”
“Asante, ndiomana nipo hapa ili mama anipe busara zake”
“Mwanangu, sijui kama nitakupa busara nzuri sana mimi sababu mimi nina hasira mno ten asana. Baba yao hawa alizaa mtoto huko na mama wa mtoto pamoja na mtoto wakaja hapa, hakika niliwatimua kama mbwa, najua unamfahamu Derrick, yule usishangae undugu wake na Erica ukoje, yani ni baba mmoja hawa ila mimi niliwatimua, jamani mimi nina hasira sana. Ila sikushauri mwanangu kuwatimua ila ongea na mumeo ajenge nyumba kwaajili yako na watoto wako kwani leo na kesho ni ugomvi mkubwa utatokea hapo”
“Mama, hata akijenga nyumba kwaajili yangu na watoto wangu kumbuka ile moja haiwezi kuwatosha watoto wote wale, yani lazima watanifanyia fujo tu”
“Basi mwambie akupe hela hata za mtaji ili ufanyie kitu cha maana, ila Fetty si ulikuwa unafanya kazi wewe lakini?”
“Ni kweli nilikuwa nafanya kazi mama, ila kuolewa huku nako ni balaa, yule mume wangu alinishauri jambo na kwa muda huo niliona ni jambo la msingi sana kuwa tushirikiane nae kwani alisema ni vyema tushirikiane na biashara alizokuwa akifanya, na kweli tumeshirikiana vizuri tu na ile biashara inaingiza hela kw asana tu ila kwasasa nilipumzika kidogo kwani aliniaomba nikae nyumbani kuangalia viumbe vyake yani ndio kila leo vinaongezeka, kwakweli nimechoka”
Basi mama Angel alimuuliza,
“Kwahiyo kuna watoto wangapi kwasasa?”
“Yani, kwasasa nyumbani kwangu kuna watoto kumi, ndiomana nimechanganyikiwa kwasasa. Halafu rika lao sasa linafanana mwanzo mwisho”
“Kheee pole sana”
“Asante yani hata sijui cha kufanya”
Basi mama Angel akamshauri jamabo,
“Kama utaweza Fetty, naomba siku umshauri mumeo mje nae hapa ili niongee nae kidogo”
“Sawa mama, hakuna tatizo”
Kiukweli hata mama Angel aliumia moyo, ingawa yeye hakuwahi kuletewa mtoto wan je ya ndoa ila aliweza kuona ni kwa jinsi gani ile hali ya kuletewa watoto inavyoumiza moyo wa mwanamke mwenzie.
Basi mama Angel aliamua kuaga kwa mama yake na hivyo kuondoka akiwa ameongozana na Fetty ambaye aliomba aachwe njiani kwanza maana kuna mahali alikuwa akipitia, basi alifika njiani na kumshusha halafu mama Angel akaondoka na kurudi nyumbani kwake.
 
SEHEMU YA 149

Junior alipotoka shuleni leo, moja kwa moja alipitiliza jikoni ambapo Vaileth alikuwa akipika, basi alikuwa akimuangalia sana anavyopika huku akitabasamu yani kwa muda huo hata Vaileth hakujua kama kuna mtu anamuangalia wala nini, kisha Junior alisogea karibu yake na kumkumbatia kwa nyuma, yani Vaileth alishtuka sana ila alipogeuka alimkuta ni Junior,
“Jamani Junior, umenishtua ujue”
“Ulijua ni nani?”
“Aaaah mimi sikujua bhana, sijui umeninyatia, muone vile”
“Usishtuke jamani Vaileth ila nashukuru sana kwa kunijali, yani leo umefanya kitu kikubwa sana kwangu. Asante sana Vaileth”
Vaileth alitabasamu tu, kisha Junior aliondoka na kwenda chumbani kwake ambapo nae Vaileth alimaliza kupika na kueleka chumbani.
Muda wa kula ulipofika ni wote walifika mezani na kula kile chakula halafu kila mmoja alielekea chumbani kwake ikiwa ni pamoja na Vaileth.
Ila usiku wa leo ulikuwa ni wa tofauti sana kwa Vaileth kwani alijikuta kichwa chake kikiwa kimezongwa na lile tukio ambalo lilitokea jikoni la Junior kumkumbatia kwa nyuma, alijikuta kila akikaa anapatwa na wazo hilo, akajisemea,
“Jamani! Nini sasa, kwanini Junior lakini. Mmmmh mtoto mdogo huyu jamani, kwanini namuwaza hivi!!”
Alijitahidi mno asimuwaze Junior ila kwa siku hiyo hilo wazo liligoma kutoka katika akili yake zaidi zaidi lile wazo likaanza kukumbusha na matukio ya nyuma, kamavile ambavyo anakaa karibu na Junior akimpa ushauri, jinsi Junior alivyokuwa akimfuta machozi na kummbembeleza, na jinsi alivyomsaidia kukuna nazi, alijikuta akimuwaza sana Junior yani hadi alikosa amani katika moyo wake.
Basi palivyokucha aliamka na kufanya shughuli zake ila alijikuta kwa siku hiyo akiwa na hamu sana ya kumuona Junior kwanza.
Wakati anaosha vyombo huku akiwa na mawazo hayo, nyuma yake alitokea Junior na kumkumbatia tena kwa nyuma halafu akambusu na kumwambia,
“Naenda shule Vaileth, badae”
Halafu Junior akaondoka na kumuacha Vaileth akiwa kama amesizi kwa muda kidogo na kupumua kwani kile kitendo ndio kwanza kinamzidishia mawazo maradufu.

Leo baba Angel ndio aliamua kumuita Steve ambaye ni mdogo wake Dora kwenye ofisi yake, basi Steve nae alifika kwa muda muafaka kabisa na kuanza kuongea nae,
“Karibu sana, sasa nilishaongea na Dora tayari na nilikuwa na biashara yangu mpya ni vyema nikakuweka ili uisimamie”
“Oooh asante sana”
“Sawa, ila kwasasa unaishi wapi?”
“Kwasasa naishi nyumbani kwetu”
“Ila wewe ni kijana mkubwa ujue!”
“Ni kweli, ila sikuwa na uelekeo sahihi ndiomana ikatokea hivi”
Basi baba Angel akainuka na kutoka nae ambapo aliondoka nae hadi kwenye biashara yake mpya na kumuonyesha huko, ambapo walikubaliana kuwa kesho yake aende kusaini mikataba yake halafu aweze kuanza ile kazi ambapo waliagana na baba Angel kisha Steve akaondoka zake.
Steve akiwa njiani, alishikwa began a mtu kugeuka akamuona Sia, basi alishangaa sana,
“Kheee Sia!”
“Kama umeona mzuka eeeh! Ndio ni mimi”
“Za siku? Mtoto hajambo?”
“Kheee leo hata unakumbuka kuhusu mtoto kweli! Si ni wewe uliyemkataa yule mtoto na kusema sio wako? Leo unamkumbuka wa nini? Poa tuachane na hayo ila ngoja nikwambie kilichonileta”
“Kwanza umejuaje kama nipo mitaa hii?”
“Hujui tu Steve ila huwa nakufatilia kupita maelezo ya kawaida, huwezi kunikimbia mimi, sikukufata sio sababu sijui pa kukupatia ila sikuwa na sababu ya kukufata ndiomana niliacha uende”
“Mmmh!”
“Haya, tuachane na hayo kwanza, ngoja tuongee ya maana. Kuna kitu nataka tufanye mimi na wewe”
“Kitu gani hiko?”
“Nitakwambia, ila najua siku moja utakaa chini na kusema katika maisha yako yote hujawahi kuona mwanamke mwenye akili kama Sia, mimi nina akili wewe usinione hivi!! Kuwa na akili sana sio mpaka usome sana, wengine tuna akili zetu tu za kuzaliwa. Kwakweli mimi nina akili na nina haki ya kujisifia. Kwanza kitu nilichokuwa nakitaka kwako kwa muda mrefu ni kuona ukifanya kazi kwenye kampuni ya Erick na ili limeenda kutimia, kwakweli hiyo ni moja ya furaha yangu. Ila naomba chondechonde usimwambia dada yako kuwa umeonana na mimi. Achana na habari za ndugu zako, mimi na wewe ni wazazi, achana na mambo yao, hawakuwepo wakati wa kupeana mimba na wala hawakuwepo leba na mimi kwahiyo achana nao. Mimi ndio mama wa mtoto na wewe ndio baba wa mtoto, kwahiyo achana na maneno ya ndugu zako. Nitakufata tena ili tuongee vizuri, kwaheri”
Halafu Sia aliondoka na kumuacha Steve akimuangalia pale bila hata ya kummaliza, ila tu na yeye aliamua kuondoka tu.
 
SEHEMU YA 150

Mama Angel alikuwepo tu nyumbani kwake, basi muda huu alikaa sebleni na Vaileth ila alishangaa kumuona Vaileth kila muda akionyesha tabasamu, yani alitabasamu peke yake basi akamuuliza,
“Vipi wewe? Kitu gani hiko kinachokufanya utabasamu mwenyewe?”
“Hamna kitu mama”
“Mmmmh jamani! Hamna kitu kweli!! Yani kwa jinsi unavyotabasamu basi ni lazima kuna kitu kinakufurahisha tu”
“Hamna mama, kuna kitu cha zamani sana nimekumbuka ndio kilikuwa kinanichekesha”
“Jamani tuwe tunashirikishana ili tucheke wote basi!!”
Vaileth akatabasamu tu na kuendelea na mambo mengine kwani aliinuka na kwenda jikoni, baada ya muda kidogo Erick na Erica walirudi na moja kwa moja walipomsalimia mama yao tu Erica alibaki pale na kuongea na mama yao,
“Mama, kesho kutwa yani Jumamosi Samia anakuja hapa nyumbani kwetu”
“Hamna tatizo, mwambie anakaribishwa”
“Oooh mama, asante sana”
“Mimi nilikwambia sina tatizo lolote na huyo Samia, hata akitaka kuja kulala mwambie ni ruksa tu”
“Jamani mama, asante sana”
Basi Erica aliondoka zake na moja kwa moja kwenda kumpa habari kaka yake kuwa mama yao amemkubalia kwa ujio wa Samia, maana kwa kipindi hiko ndio ilikuwa habari yake kuu yani kila alichozungumzia ni kuhusu Samia.
Basi moja kwa moja alienda chumbani kwa Erick, na kama kawaida yake alifungua tu mlango bila hata kubisha hodi ambapo alimkuta Erick akiwa anavaa,
“Oooh samahani Erick”
“Unajua wewe, siku hizi unafanya makusudi maana hii bahati mbaya mmmh! Ndio kila siku jamani!”
“Si unisamehe!”
“Yani nahisi mwili wangu unaujua kama wako vile, itabidi na mimi siku nikuvizie ili nikuchungulie vizuri”
Basi Erica alicheka tu halafu akaondoka mule chumbani kwa kaka yake na kurudi chumbani kwake.
Basi Erica alifika chumbani kwake na kujiandaa kuoga, na alipotoka kuoga alijiuliza sana kwanini kila akienda chumbani kwa Erick basi alimkuta akiwa ametoka kuoga, anavaa au amejilaza mtupu kabisa,
“Mmmmh kwanini sasa inakuwa hivi jamani!! Yule Erick anaweza kuona kweli nafanya makusudi ila mimi sifanyi makusudi bali inatokea tu hata mimi sielewi ni kwanini inatokea”
Aliwaza ila akaona haina maana kuwaza kitu kama hiko kwakuwa kimeshatokea tayari.
 
SEHEMU YA 151

Usiku a leo baba Angel alimueleza mama Angel namna alivyozungumza na Steve na kazi ambayo alimpatia kwenye duka lao jipya,
“Duka lipi hilo?”
“Lile duka ambalo nilimpeleka hata Erick”
“Aaaah kumbe duka lile!! Kumbe hakukuwa na msimamizi pale?”
“Ndio, sababu sikupata mtu ninayemuamini, ila kwasasa imekuwa afadhari sababu msimamizi huwa napenda nimfahamu ndugu zake na wazazi wake”
“Aaaah nimekuelewa mume wangu, umefanya vizuri kwa hilo”
Muda wa kulala ulifika wakalala tu.
Kulipokucha siku hiyo mama Angel alitoka nyumbani kwake mapema kabisa akienda hospitali, kwani kwa kipindi hiko alikuwa ameanza kliniki.
Basi moja kwa moja alienda kwenye hospitali ambayo alikuwa akitibiwa kwa kipindi hiko maana kwa yule dokta Maimuna alishaacha kabisa kwenda, basi alifika hospitali na kufanyiwa huduma zote alizozitaka na baada ya hapo akaanza kuondoka ila wakati anatoka akakutana na dokta Maimuna, ambaye alimfurahia kumuona na kumsalimia vizuri sana,
“Jamani mama Angel, za siku nyingi jamani!”
“Nzuri tu, za wewe!”
“Salama, ndio umenikimbia jamani toka siku ile. Yale mambo ya kawaida tu ndugu yangu hakukuwa hata na haja ya kunikimbia wala nini, mimi na wewe tungeongea kiuanamke na kuyamaliza, asiyeyajua matatizo ya hawa wanaume nani? Tunawaelewa vizuri sana, hawa wanaume wana matatizo balaa, yani unaweza ukaona kama wewe ndio ulitendewa jambo baya ila ukisikia la mwenzio utasema kumbe wewe hakuna baya ulilotendewa”
“Oooh nimekuelewa”
“Tupate siku tuzungumze kuhusu hili, wala sikulazimishi sijui umuonyeshe mtoto Rahim au umpeleke Rahim kwa mtoto, huo ni uamuzi wako, wewe ni mama na ndiye mwenye maamuzi na mtoto wako, mimi naongea tu kwa upande kama dokta na kwa upande mwingine kama mwanamke mwenzio, mimi mwenyewe nishawahi kupitia matukio mbalimbali ya kukataliwa ila kwasasa niliruhusu maisha yaendelee mbele na wala sioni kama nina kasoro yoyote zaidi ya kuishi kwa amani na furaha”
“Nimekuelewa”
“Usiseme umenielewa tu, inatakiwa tuzungumze jambo hili kwa upana sana ndugu yangu, basi naomba nikikutafuta upokee simu yangu”
“Sawa hakuna tatizo, nitapokea simu yako na tutawasiliana vizuri sana”
Basi dokta Maimuna aliagana nae na moja kwa moja mama Angel alienda kupanda kwenye gari yake na kuondoka ila siku hiyo hakwenda nyumbani kwake kwani moja kwa moja alikwenda ofisini kwa mume wake, yani kwenye ile ofisi hata walivyokuwa wakimuona amefika basi wote walitulia kimya kwani wengi wao walionekana hawapendi mama Angel kufika ofisini kwa mume wake.

Leo ilikuwa siku ya Ijumaa na wanafunzi wa kidato cha nne walikuwa kwenye maandalizi ya mwisho kwaajili ya mtihani wa taifa unaoanza Jumatatu, kwahiyo wengi walionekana wapo makini sana na masomo yao.
Siku hiyo darasani kwakina Angel kila mmoja alikaa kwenye kona yake akijisomea, yani kwa siku hiyo kila mtu aliona kuwa ajikumbushie yale waliyoyasoma kwa kipindi kirefu.
Muda wa kutoka darasani ulifika na darasa lilikuwa kimya sana, basi Angel alifunga daftari zake na kuzirudisha kwenye begi lake ili aondoke, ila alipoangalia vizuri darasani aliona hakuna mwanafunzi zaidi ya mmoja tu ambaye nae alikuwa makini na kujisomea kwa muda huo ila walijikuta wakitazamana macho na mwanafunzi huyo, huyu hakuwa mwingine bali alikuwa ni Samir, yani walipotazamana hivi moyo wa Angel ulilia pa yani alijikuta kwa muda huo akitamani sana hata akimbatiane tu na Samir halafu moyo wake utaridhika yani alijiona akifanya hivyo basi Jumatatu ataingia kwenye chumba cha mtihani akiwa na furaha moyoni.
Wakati Angel akitafakari hayo alishangaa tu kuona Samir akiinuka na kwenda karibu yake halafu alimkumbatia kwa nguvu sana inaonyesha hata yeye alikuwa na wazo kama la Angel.
 
SEHEMU YA 152

Wakati Angel akitafakari hayo alishangaa tu kuona Samir akiinuka na kwenda karibu yake halafu alimkumbatia kwa nguvu sana inaonyesha hata yeye alikuwa na wazo kama la Angel.
Yani ilipita kama dakika tano kila mmoja kushtuka na kugundua kuwa wanachofanya pale si sahihi, basi waliachiana halafu kila mmoja akatoka darasani ila walipofika nje waliona kumbe wenzao kuna mahali wamekutanishwa kwa muda huo ndiomana mule darasani walibaki wenyewe tu, basi walisogea walipo wenzao yani wote waligeuka nyuma kuwaangalia wao wawili, basi mwalimu aliwauliza,
“Angel na Samir, nyie ndio mlikuwa wapi?”
Wote wawili walitazama chini tu, basi mwalimu aliendelea na mada ambayo alikuwa akizungumza pale na wanafunzi wote,
“Yani kama nilivyowaambia umakini unahitajika kwa kiasi kikubwa sana, yani jitahidi kusoma maelekezo vizuri kabisa kabla ya yote yale, halafu kumbuka kuandika namba yako ya mtihani, sio jina ni namba jamani maana kuna watu kwenye moko mlitufanyia ujinga, sasa mkirudia tena kwenye taifa mjue imekula kwenu na zero itawahusu”
Wanafunzi walikuwa kimya kabisa wakisikiliza maelekezo ya mwalimu, na pale mwalimu alipomaliza kutoa maelekezo ndipo alipowaruhusu kwenye nyumbani.
Muda huo dereva wa kumfata Angel tayari alishafika na kumfanya Angel aende kupanda lile gari na kuanza safari ya kwenda nyumbani kwa shangazi yake.

Samir nae leo alienda moja kwa moja kwao kama kawaida, na aliona ni vyema apumzike kwanza halafu ndio aamke na kuendelea kujikumbushia masomo yaliyopita kwani aliona kama kila kitu ameshasoma ila tu ni kujikumbushia kwaajili ya mtihani.
Basi muda alipoanza kujisomea alifika dada yake na kumwambia,
“Kaka, kesho kuna mahali nitaenda kwa rafiki yangu”
“Kheee haya, sina pingamizi mimi”
“Asante kaka”
Basi dada wa Samir alifurahi sana baada ya kuruhusiwa na kaka yake, hivyobasi aliondoka na kwenda kufanya maandalizi ya siku ya kesho ambayo ameapanga kwenda kwa rafiki yake.
Samir alitulia na mama yake aliporudi siku hiyo alimuita mwanae na kuongea ongea nae kidogo,
“Mwanangu, nakutakia mitihani mema jamani, maana mimi kesho asubuhi nasafiri”
“Ooooh kumbe hutokuwepo mama!”
“Ndio sitakuwepo, kuna mahali inabidi niende nadhani nitarudi baada ya miezi miwili au mitatu”
“Jamani mama, inamaana hata kwenye mahafali yangu hutokuwepo?”
“Sitakuwepo ila tutakuwa pamoja mwanangu jamani, hata usijisikie vibaya wala nini”
“Ila ile shule nayo, sijui kwanini mahafali wameyapanga baada ya mitihani!”
“Sio, vibaya lakini kwani mnakuwa huruzaidi tena ni vizuri zaidi. Ila mwanangu usijali”
Basi mama Samir alimpa Samir ushauri idogo pale kisha akaondoka zake kwani alitakiwa kupata muda wa kutosha kujiandaa kwaajili ya safari ya kesho yake.
 
SEHEMU YA 153

Mama Angel akiwa bado ofisini kwa mume wake, aliamua kuongea nae jambo ambapo mumewe aliamua kuondoka nae kwa muda huo ili kwenda nae anapopataka mkewe.
Basi muda huu baba Angel aliwaaga wafanyakazi wake na kuondoka zake na mkewe ila kiukweli waliumia sana kwenye mioyo yao kwani hawakupenda hata kidogo kabisa kuona mama Angel akiongozana vile na mumewe.
Basi walitoka pale na moja kwa moja walienda sehemu ambapo mama Angel alihitaji kupelekwa na mume wake ambapo palikuwa ni kwenye biashara mpya ya mumewe ambapo kamuweka Steve kuwa msimamizi wa biashara hiyo, na kweli walivyofika pale Steve alikuwa tayari yupo mahali pale basi walimuita na kusalimiana pale, kisha mama Angel alianza kuhojiana nae,
“VIpi Steve, umepaonaje hapa?”
“Pako vizuri tu, hata wateja wapo”
“Ila unadhani ni kipi kifanyike ili tuweze kutengeneza wateja wengi zaidi eneo hili?”
“Aaaah mama, kwanza bado nipo kuangalia mazingira ya hapa ila nikishafanikisha basi nitawaambia cha kufanya, ila kwasasa ngoja niangalie kwanza mambo yalivyo”
“Basi sawa, ila nakuomba jambo moja kubwa”
“Jambo gani?”
“Hapa kwenye biashara sitaki umkaribishe Sia”
Kisha mama Angel akamtazama mumewe na kumwambia,
“Baba Angel, hii biashara ya hapa nitakuwa nakuja mwenyewe mara kwa mara kuiangalia”
“Sawa, hakuna tatizo mke wangu”
Basi baada ya hapo waliizungukia zungukia ilebiashara halafu wakaondoka zao.
Steve na alikaa kaa kidogo na kuamua kufunga ili kuondoka ila wakati anaondoka tu, njiani akakutana tena na Sia ambaye alimsimamisha na kuanza kuongea nae tena,
“Steve, naona leo mabosi wako walikuja na walikuwa wakitembelea biashara yao”
“Unajua kuna mara nyingine huwa sikuelewi kabisa Sia, yani mimi hata huwa sielewi kuwa ni wewe ndiye mwanamke niliyekuwa naishi nae”
“Na kamwe huwezi kunielewa hadi ile siku itakapofika na wewe kukaa chini na kugundua ni akili za kiasi gani zilizokuwa katika kichwa changu”
“Mmmmh!!”
“Haya, acha kuguna kwanza. Nataka kuongea nawe mambo ya maana”
“Mambo gani hayo?”
“Kwanza, wote ambao huwa wanaachiwa duka na Erick basi huwa anawaachia vibali vyote vya duka lake dukani, vipi na hapo?”
“Mmmh ndio, hivyo hivyo”
“Sasa tulia mimi nikufundishe jambo wewe, tena jamabo la akili mno. Kesho nitakuja hapo dukani yani nitaingia ndani ya duka”
“Kufanya nini?”
“Utaona hiyo kesho ninachokuja kufanya”
“Unajua mwenyewe kasema nisikualike kabisa wewe kwenye duka lake? Unajua tayari kapatwa na mashaka kuhusu wewe! Yani limekuwa ni onyo lake namba moja kuwa nisikualike pale dukani”
“Hebu na wewe muda mwingine kuwa kama mwanaume, sasa wewe unatishiwa na mwanamke? Kwani mwanamke yule ndio nani? Nilijua Erick kakuambia hivyo!! Kumbe ni yeye ndio kasema hivyo, hebu acha ujinga huko. Mimi kesho nafika hapa. Kwaheri”
Basi Sia akamuaga na kuondoka zake.
Kiukweli kwa muda huo Steve akaona hata asiende kwao kwanza, kwani moja kwa moja aliondoka na kwenda nyumbani kwa dada yake, ingawa muda ulikuwa umeenda ila aliona kuwa ni vyema kwenda kwa dada yake kwanza ili kujaribu kuongea nae kuhusu hilo na aone ni kitu gani atamshauri.
Na alipofika tu kwa dada yake alimkuta akiendelea na mambo yake mengine, basi alianza kuongea nae pale na kumuelezea kuanzia siku ya kwanza ilivyokuwa na mpaka siku hiyo,
“Mmmmh mimi ndiomana huwa nasema yule Sian i jasusi, maana ana mipango hiyo sijawahi kuona, yani hapo anachokipanga anajua yeye na roho yake ila mdogo wangu unatakiwa kuwa mwanaume kweli, hebu simama katika nafasi yako usiruhusu mwanamke akakuharibika sababu ya raha zake. Unajua yule Sia hata wa kumgananisha nae sijaona kwakweli, yani iko hivi Sia alimpenda sana Erick tena alitamani mno mali za Erick na alipenda yeye ndio awe mmiliki na sio Erica kama ilivyokuwa. Ila kwasasa roho inamuuma sana kila anapoona kuwa wanapendana, yani mdogo wangu huyo Sia atakudanganya tu ila anachokitaka hapo lazima mwisho wa siku atakuliza tu na kukufanya ukose kazi kabisa”
“Sasa dada nifanyeje?”
“Usikubali aingie kwenye ofisi ya duka, kwanza anafata nini? Erick sio mjinga kiasi hiko, ni kweli huwa anaweka vibali dukani ila hainamaana kwamba, hivyo ndio vibali pekee vya biashara yake, jamani yule kafanya biashara toka siku nyingi sana, yani hiyo sio biashara yake ya kwanza wala nini ila hiyo ni kati ya biashara nyingi alizonazo, hebu acha kusikiliza ujinga wa Sia kabisa, yani usitake kufata anachokisema, kwanza ni mwanamke gani huyo? Anajishughulisha na nini? Anapata wapi pesa za kukufatilia? Mmmmh!”
Dora akawaza kitu na kusema tena,
“Unajua kuna jambo nimewaza hapa, usikuite Sia kuna watu anashirikiana nao halafu hao watu wanaugomvi na Erick, itakuwa hao watu wana lengo la kumshusha Erick kwahiyo wanamtumia huyo mjinga kutekeleza mambo yao, ila bado nabaki na msimamo wangu ule ule usimkubalie Sia kabisa, na ikishindikana, mwambie ukweli bosi wako”
“Sawa dada, nimekuelewa vizuri sana”
Basi waliagana na dada yake pale na kuondoka kwani muda ulikuwa umeenda kwakweli na aliona kuwa ni vyema kama akiwahi na kupata muda wa kupumzika kidogo ili kesho yake aweze kuwahi kwenye kazi yake.
 
SEHEMU YA 154

Mama Angel na baba Angel muda huu walikuwa nyumbani kwao, na walikaa pamoja mezani na watoto wakila, na walipomaliza walikaa kidogo sebleni huku wakiongea ongea ambapo wakakumbuka kuwa Jumatatu kidato cha nne wanaenda kuanza mtihani wa taifa, basi mama Angel alamwambia baba Angel,
“Itabidi Kesho twende kumuona Angel kidogo na kumtakia mtihani mwema”
“Kweli kabisa, umeamua vyema”
Waliongea pale na moja kwa moja kila mmoja alienda kulala tu.
Kulipokucha, baba na mama Angel walifanya kwanza mambo mengine waliyotakiwa kufanya asubuhi hiyo maana siku hiyo hawakwenda kwenye biashara zao wala nini.
Walipomaliza mambo yao walijiandaa na kutoka.
Walipoondoka tu, pale nyumbani walibaki Vaileth na watoto kama kawaida ila Junior na leo ndio alikuwa chumbani kwake kabisa kajifungia mwenyewe akiendelea na masomo yake kama kawaida.
Sebleni walikaa Erica na Erick, muda kidogo rafiki wa Erica aitwaye Samia alifika kwakweli Erica alifurahi sana na kumkaribisha vizuri sana rafiki yake, ila siku hiyo ndio ilikuwa mara ya kwanza kwa Samia kumuona Erick maana siku zote alikuwa akihadithiwa tu na Erica kwamba ana pacha wake wa kuitwa Erick, basi alifika pale na kumuangalia sana huku akiongea ongea, ambapo aligundua kuwa Erick alipenda sana mikanda ya ngumi yani ile mikanda yenye muvi za mapigano, basi akasema pale,
“Wiki ijayo Erica nitakuja tena na nitawaletea mkanda mmoja hivi wa ngumi, ni mzuri huo”
Erick aliposikia hivyo basi alianza kusapoti na yeye huku akiulizia vizuri kuhusu huo mkanda, alipenda uletwe hata Jumatatu,
“Kama utaweza, basi Jumatatu mletee ilia je nao nyumbani niuone”
“Oooh sawa, hakuna tatizo. Unapenda mikanda ya ngumi eeeh!”
“Napenda sana yani”
“Basi usijali, kwetu zipo muvi nyingi sana za ngumi maana hata kaka yangu pia huwa anapenda kuangalia”
“Nitafurahi sana ukizileta”
Basi Erick alianza kumfurahia Samia sababu ya hizo muvi alizosema kuwa angezileta kesho yake.

Leo Steve akiwa dukani, kama ambavyo Sia alipanga, ni muda alifika pale dukani na kukutana na Steve na kumtaka kuwa waende ofisini,
“Hapana haitawezekana, maana ofisi bado ipo kwenye matengenezo kwahiyo kuna mafundi”
“Ila mimi nahitaji kuiona tu”
“Kwani ukishaiona utapata faida gani wakati bado haijaisha?”
“Hivi mbona Steve umekuwa na tabia kama za kike jamani! Ndiomana unashikiliwa akili na ndugu zako, hivi wewe huwezi kujisimamia mwenyewe jamani! Hujui kama wewe ni mwanaume unatakiwa usimame mwenyewe jamani! Hebu ifike wakati uwe mwanaume Steve”
“Mimi ni mwanaume ndio na siwezi kukuruhusu leo kuingia kwenye ofisi hii”
“Huo sio uanaume Steve, yani endelea kujidanganya ila huo sio uanaume wala nini”
Kisha Sia akaondoka zake, ila alionyesha kwa kiasi Fulani amechukia sana ingawa alionekana kuwa amekubaliana na hali halisi.
Basi Steve alikaa na kujiuliza kuwa kitu ambacho yule mwanamke alikuwa akikitaka ni kitu gani, yani kwanini ang’ang’anie ofisini kwa Erick kiasi kile? Ila ukweli wote alikuwa nao mwenyewe Sia kwani hata yeye awaze vipi bado asingeweza kupata jibu la aina yoyote ile.
 
Back
Top Bottom