SEHEMU YA 331
Basi Erick aliondoka na kwenda dukani, wakati anarudi kufika tu getini akamuona Sia, kiukweli hakupenda kumuona wala nini, basi Sia akasogea ili amuongeleshe ila kabla hajasema neno lolote, Erick alimsukuma Sia na kumuangusha chini, kitendo kile kilimkera sana Elly na hapo hapo alijikuta akimvaa Erick na kuanza kupigana nae.
Mama Angel alisikia kile kishindo cha Sia kuanguka, kwahiyo alitoka nje kwa haraka kujua ni nani anaanguka ndipo alipokutana Elly akimpiga Erick kwani Erick hakuwa mtu wa kupigana kwahiyo alikuwa amesimama tu, basi mama Angel alienda na kumsukuma Elly kisha akamnasa kibao na kumwambia kwa ukali,
“Unawezaje kupigana na mtu ambaye hapigani na wewe?”
Kisha mama Angel alimuangalia Sia, halafu akamsogelea na kumnasa kibao na kumwambia,
“Chezea vyote na sio watoto wangu”
Mama Angel akamshika mkono Erick na kuingia nae ndani, kwahiyo pale nje alibaki tu Elly na mama yake, ambapo waliangalia kisha Elly akamwambia mama yake,
“Yani mama umeshindwa kabisa kunitetea kwa yule mama?”
“Sasa mwanangu hata mimi mwenyewe nimeshindwa kujitetea maana nilikuwa namshangaa tu yule mwanamke, baada aulize chanzo ni kitu gani anavamia tu watu na kuwachapa makofi, ila ipo siku atajutia jambo hili”
“Utamfanyaje mama?”
“Si unajua huwa mama yako hakuna kitu kinachonishinda, basi subiri tu utaona picha lenyewe litakavyoenda, anamuona huyu Erick kama dhahabu ila atalia kilio mbuzi kachoka”
Kisha Sia akaondoka na mtoto wake muda huo.
Mama Angel nae akiwa ndani alimfokea Erick,
“Na wewe unakuwa kama mzembe jamani, unaachaje mtu akupige namna ile?”
“Mama, mimi huwa sipendi ukorofi na hujanifundisha hivyo”
“Oooh sawa, hata hivyo nimeogopa sana jamani, ungezimia na pale mwanangu je!”
“Jamani mama, inamaana mimi nitakuwa nazimia hata nikiguswa kidogo tu!!”
“Sina maana hiyo mwanangu, haya nipe hiyo vocha”
Erick aliangalia vizuri na kugundua kuwa hiyo vocha ameiangusha nje ya geti lao, akamwambia mama yake,
“Dah! Nadhani pale wakati yule ananitingisha na vocha ilianguka pale, ngoja nikaifate mama”
“Hapana, kaa hapo naenda kuifata mwenyewe”
Mama Angel aliinuka na kutoka, basi alipotoka tu nje ya geti wakati anaangalia ile vocha na kuinama ili aiokote, alishangaa kuna mtu kainama pia na kushika mkono wake, kwahiyo alipoinuka aligongana nae macho kwa macho mtu huyo alikuwa ni Rahim,
“Kheee Rahim!”
“Ndio ni mimi, nipo hapa kipenzi changu. Mwanamke wa roho yangu”
“Kwenda zako huko”
Mama Angel aliinuka sasa, ila Rahim alimwambia,
“Kumbuka mimi ndiye mwanaume wa kwanza kabisa kukupa heshima wewe ya kuwa mama, halafu unapokumbuka mabaya yangu basi jaribu kukumbuka na mazuri yangu. Wanawake wangapi huwa wanapewa mimba na kutelekezwa kabisa yani mwanaume hata hajali kuwa una kiumbe chake, ila mimi wakati umeniambia kuwa una mimba yangu, nilikutumia pesa ya kupanga chumba na kununua kila kitu ndani na bado nilikuwa nakujali kwa kukutumia pesa kila mara, hata ulipojifungua bado nilikuwa nakujali Erica, ila tatizo lako wewe ni kukazana kuwa lazima nikuoe ndio ikawa tatizo kwangu sababu kwa kipindi hiko sikuwa na maamuzi sahihi ila ukiniambia kwasasa Erica nakuoa tu tena bila ya kipingamizi”
“Unajua usitake kuniletea uchizi hapa, jisahaulishe tu mambo yako, ni kweli ulikuwa ukinitumia pesa ila ulisahau jambo moja tu kuwa utu ni bora kuliko kitu. Nimekaa mimi, nimedhalilishwa mimi, nimechekwa mimi, nimeitwa majina yote mabaya sababu tu ya kumbeba Angel, na bado baba wa mtoto nikikwambia kitu unanijibu vibaya, hivi ulikuwa unawaza hata kwa mbali ni uchungu gani niliokuwa naupata kwa yale majibu yako? Naomba Rahim niache kwa amani, niache niishi vyema na familia yangu”
“Na mimi kamwe sitokuacha kwa amani, yani hilo sahau kabisa, tena nikome nakwambia”
“Bado, nitakuja tena”
Rahim alimsogelea mama Angel na kumbusu kwenye paji la uso, lile tukio lilikuwa la haraka kidogo kwahiyo hata mama Angel hakujipanga nalo, ila muda huo huo aliamua tu kuingia ndani halafu Rahim nae alirudi kwenye gari yake, kumbe kwa muda huo Tumaini nae alikuja akija hapo kwa mama Angel ila alipoona vile alijibanza mahali, kwahiyo Rahim aliporudi kwenye gari tu alimfata na kumuuliza,
“Kuna nini kinaendelea kati yako na Erica?”
“Kwani wewe ni nani?”
“Mimi ni wifi yake”
“Oooh ni dada yake Erick, yule ulikuwa bonge kipindi kile unakula kila kitu, ila saivi umekuwa mmama na mwili umekupendeza, sio kipindi kile, binti ila bonge shavu hilo utafikiri…”
Tumaini alimkatisha na kumuuliza,
“Kwani wewe ni nani?”
“Sijui unijui au kiburi tu au umenisahau? Au nimezidi kuwa mtanashati, maana kila siku nazidi kuchanganya macho ya wanawake, usikute na wewe umeanza kuchanganyikiwa na mimi”
“Vipi wewe?”
“Mimi naitwa Rahim, mimi ndio mwanaume wa kwanza kabisa kuwa na Erica, mimi ndio nilimfundisha Erica nini maana ya mapenzi, mimi ndio nilimfanya awe mama kwa umri ule, mimi ndiye niliyemfanya, apate mtoto mzuri hadi kuchukuliwa na makampuni mbalimbali kwa matangazo. Mimi ni mzuri na ninajivunia hilo”
“Mbona unajisifia kama mwanamke?”
“Ukitaka kujua uanaume wangu tafadhari twende chumbani”
“Mjinga wewe”
Tumaini akaondoka zake, na wala hakuingia tena kwa mama Angel, naye Rahim akaondoka zake pia.
Tumaini alivyofika tu nyumbani kwake, alimpigia simu mdogo wake na kumueleza kile alichokikuta kwenye nyumba yake,
“Kiukweli nimeshindwa hata kuingia, usidhani nakuharibia ndoa ila nakwambia ukweli halisi.”
“Nimekuelewa na wala siwezi hisi kuwa unaniharibia ndoa, sababu najua jinsi gani Erica anavyonipenda, hakuna kiumbe yoyote wa kukatisha mbele yake halafu akanisahau mimi”
“Na alivyombusu je?”
“Itakuwa ni bahati mbaya, Tumaini hujaingia kwenye moyo wa Erica wewe. Yule hata umchane chane, basi damu yake itaanguka chini na kuandika Erick”
“Mmmh siwawezi”
“Na hakuna anayetuweza hata mmoja, mimi na Erica tunapendana, kwahiyo hakuna kiumbe yoyote wa kukatisha kwenye penzi letu. Kama kuna mwanamke alinikosa mimi kwa kipindi kile basi asitegemee kunipata kwa kipindi hiki, na kama kuna mwanaume alimkosa Erica kwa kipindi kile asitegemee kumpata kwa kipindi hiki, namuamini sana mke wangu na kumthamini”
“Haya basi yaishe, mbea mimi kukuletea huo ujumbe”
“Hujafanya vibaya kuniambia ila tu nilikuwa nakusahihisha kuwa huyo jamaa hawezi kuharibu penzi langu na Erica sababu sisi tuna nguvu iliyopo ndani ya mioyo yetu”
Tumaini hakuwa na la kuongeza zaidi ya kumuaga tu kaka yake, ila mumewe alikuwepo siku hii basi alimsikia kwenye yale maongezi na kumuuliza vizuri, na yeye alianza kumuelezea kuaznia mwanzo hadi jinsi alivyojibiwa na Erick,
“Kheee huyo Rahim bado tu anamfataga mdogo wangu?”
“Kumbe unamfahamu”
“Namfahamu ndio, ila Erick hajakosea ni kweli kabisa ukimchana Erica basi damu yake itaanguka chini na kuandika Erick. Kwakweli mdogo wangu ni amependa tena kapitiliza, hakuna hata mmoja wa kumbabaisha”
“Mmmh ila wanavutia na mapenzi yao, hivi na wewe unanipenda hivyo kweli mimi!”
“Kwani ushawahi kunifumania?”
“Sijawahi? Ila ndio kusema huna wanawake wa nje?”
“Mwanaume yoyote ambaye hujawahi kumfumania jua kuwa huyo anakupenda sana, kama mwanaume ana wanawake nje ila anamficha mkewe yani anafanya juu chini mkewe asijue basi huyo mwanaume anaupendo wa dhati na mkewe, na hataki mke wake atambue kitu cha namna hiyo. Kwahiyo ukiishi na mwanaume bila kumfumania, acha kumuwazia mawazo potofu maana anakupenda sana kiasi hawezi fanya ujinga mbele yako”
“Kwahiyo wewe una wanawake wengine huko eeeh!”
“Hapana sina maana hiyo ila nilikuwa nakuelekeza tu, wanawake wengine mimi wanini jamani wakati nakupenda wewe mke wangu! Tumetoka mbali Tumaini, acha kunihisia vibaya, jua mumeo nakupenda sana na hakuna wa kukuzidi”
Hapo Tumaini alifurahi sana na kutabasamu kwa furaha aliyokuwa nayo, maana kitu ambacho kilikuwa kinamfanya achukie mapenzi ni ile hali ya kusalitiana.
Mama Angel aliongea na simu kwa muda mrefu sana maana alikuwa akiongea na dada yake Mage, kwahiyo aliongea nae kwa muda mrefu sana, na alipomaliza kuongea alisinzia kwa muda huo.
Alishtuka usiku sana, basi akachukua simu yake na kuona kuwa siku hii hakumtafuta mume wake hewani, ikabidi ampigie simu muda huo, simu iliita sana ikakatika, basi akapiga tena na mumewe akapokea ila akiwa katika hali ya usingizi,
“Mke wangu mbona usiku huu!”
“Aaah nimekukumbuka tu mume wangu, usiku mwema”
Basi mama Angel aliridhika kwa muda huo na kukata ile simu kisha na yeye akalala sasa.
Asubuhi kulivyokucha tu baada ya wakina Erick kwenda shuleni, muda kidogo alifika mgeni na mgeni huyo alikuwa ni madam Oliva, alimshangaa kwa kwenda ila alimkaribisha kwanza na kumwambia,
“Baada ya kunipigia mwanangu hadi kuzimia, na kuniletea mgeni wa maajabu, leo umekuja bila aibu?”
“Kwanza naomba unisamehe, sikuwa na lengo la kumchapa Erick azimie, nilimchapa fimbo moja tu hata nashangaa alizimia sijui tatizo ni nini? Na nyie wazazi mna makosa, kwanini msingesema tangu mwanzo kuwa mtoto wenu ni mgonjwa? Yani na nyie pia mna matatizo, ila naomba unisamehe sana”
“Nimekusamehe ila kama mwanangu angepatwa na matatizo zaidi sidhani kama ningesikiliza huo msamaha wako”
“Asante, na pia nisamehe kwa kumleta yule mgeni, sikujua kama mna ugomvi wenu, nilijua ni kawaida tu ndiomana nikamleta. Naomba unisamehe na hilo pia”
“Nimekusamehe, haya sema kilichokuleta”
“Ni hivi, nilimchapa Erick siku ile kwa makosa mawili, moja la kutokumsalimia yule baba ila sikuelewa kumbe mna ugomvi wenu, na la pili kuwa na mahusiano ya kimapenzi shuleni wakati mapenzi shuleni yamekatazwa”
“Unamaana gani? Yani mwanangu ana mwanamke shuleni?”
“Ndio, ana mahusiano na Sarah”
“Mmmh hainiingii akilini hiyo”
“Ndio hivyi, Erick ana mahusiano ya kimapenzi na Sarah, na nilimsema pia siku ile kuwa azingatie masomo bado mdogo mapenzi yatampoteza. Sasa kilichotokea, Sarah kafikisha maneno kwenye uongozi wa shule na mimi nimesimamishwa kazi”
“Sikuelewi, yani usimamishwe kazi kwa maneno ya mwanafunzi! Uache kusimamishwa sababu ya kumpiga Erick ila usimamishwe sababu ya Sarah!”
“Ndio, unajua Sarah ile ni shule ya marehemu baba yake, kwahiyo kamuachia mali nyingi sana Sarah, yani Sarah anajivunia sana, yule mtoto hachapwi wala hafanywi kitu chochote, mama yake mwenyewe anamlea yule mtoto kama Mungu mtu nakwambia”
“Mmmh!!”
“Jinsi unavyomuona Sarah, hawezi kufua hata nguo yake ya ndani ila walimu tukiongea tunaonekana kuwa tunapiga kelele, kwahiyo nimesimamishwa kazi. Kilichonileta hapa, ingawa nimesimamishwa kazi ila bado Erick ni kama mwanangu lazima nimuhurumie, ongea nae mwambie mapenzi na shule ni vitu viwili tofauti yani yeye akazane tu na masomo wala asiangalie mapenzi yatampoteza”
Mama Angel akapumua kidogo na kusema,
“Haya nimekusikia ingawa nimeshangaa sana”
“Ndio hivyo, kuwa makini na mtoto wako. Mfunze yaliyomema bado mdogo sana, ndio kwanza kidato cha pili”
“Nimekusikia mwalimu nakuahidi kuwa nitaongea nae, ila nikiweza pia nitaenda kuongea na uongozi wa pale shuleni, na hata nitaongea na Sarah na wewe utarudi shuleni kama kawaida kwani najua Sarah ni muelewa yani ni mtoto wa kumuelewesha tu”
“Nashukuru kwa hilo”
Leo madam Oliva wala hakuongea mengine zaidi ya hayo, kisha akaaga na kuondoka zake.
Erica alitoka shule kabla ya kaka yake, kwahiyo alimkuta mama yao na kumsalimia pale, ambapo mama yao alimuuliza,
“Jipya la shuleni leo?”
“Mmmh hakuna jipya mama, ila njiani nimemuona mama yake Samia”
“Wewe unamfahamu mama yake Samia?”
“Hapana, ila alisimamisha gari ya shule na Samia akashuka akisema ni mama yake”
“Kwahiyo ni hilo tu leo mwanangu? Niambie kama kuna lingine”
“Mmmh lingine sina uhakika nalo”
“Lipi hilo?”
“Yule mnayemsemaga Samir Samir kuwa anamsumbua dada Angel nahisi ni kaka yake Samia”
“Mmmh!! Samir na Samia wana undugu?”
“Ndio mama, maana hata Samia huwa anamtajataja, halafu tabia za Samia na tabia za huyo Samir kama zinafanana”
“Tabia gani hizo?”
“Mmmh mama jamani, leo unanikaba na maswali hadi nashindwa kujieleza”
“Kheee makubwa, Erica wewe ndio ushindwe kujieleza kweli!! Hapana haiwezekani hiyo kabisa, hebu niambie ukweli”
“Ni hivi mama, huwa nawasikia kuwa Samir anamsumbua dada Angel mara kwa mara, na imetokea kuwa Samia anamsumbua Erick mara kwa mara na leo kanipa….. Aaah mama hakuna kitu”
“Mjinga wewe, yani habari umenianzishia halafu unataka kuikatisha hebu nipe alichokupa”
Erica alitoa barua nyingine aliyopewa na Samia kuwa amletee Erick, kisha mama yake akamtaka akabadili nguo tu kwa muda huo, basi Erica akaondoka zake ila alitaka kujua hitimisho la yeye kuikabidhi ile barua kwa mama yao.
Muda huu Erick alikuwa chumbani kwake, basi mama yake alimfata na kuanza kuongea nae,
“Erick mwanangu ni kitu gani kinaendelea shuleni?”
“Hakuna kitu mama”
“Ni nini kinaendelea kati yako na Sarah?”
“Mmmh hakuna kitu mama”
“Nimepata habari kuwa una mahusiano na Sarah, mwanangu mahusiano na shule ni mbaya sana. Je ni kweli una mahusiano nae?”
“Hapana mama, ila ngoja nikwambie ukweli, ni kwamba Sarah aliniambia kuwa ananipenda sana ila nilimwambia kuwa siwezi kuwa nae”
“Kheee watoto wa siku hizi jamani, mna mambo sana sijapata kufikiria kama mna mambo kiasi hiki. Sikia mwanangu nikwambie jambo, kata hivyo hivyo usijihusishe na mapenzi kabisa, zingatia masomo, wazazi wenu tunahitaji msome na mfike mbali kielimu ila mkiendekeza mapenzi mtaishia njiani. Hivi kesho si Ijumaa!! Naomba mwambie Sarah aje hapa nyumbani, nina maongezi naye halafu nitaongea nanyi wote ili muwe kitu kimoja”
“Sawa mama”
“Ila zingatia, yoyote anayekufata kwa habari za mapenzi usikubali”
Kisha mama Angel aliinuka na kwenda chumbani kwake, ila baada ya muda mfupi tu alifatwa na Erica ambaye alimuuliza mama yake,
“Mbona hujamwambia Erick kuhusu barua ya Samia niliyokupa?”
“Una uhakika gani kuwa sijamwambia?”
“Nilikaa pale mlangoni kwake wakati ukiongea nae, nilikuwa nasikiliza”
Ilibidi mama Angel acheke na kusema,
“Dah!! Hivi huo umbea wa hivyo Erica umeutoa wapi jamani kheee yani mtoto mbea sijapata kuona, kwahiyo uliupoona naenda kuongea na Erick basi na wewe ukanyata ili usikilize hayo maongezi, loh! Hebu nenda kalale huko”
Basi Erica aliondoka zake, na muda huo mama Angel alimpigia simu mumewe na kumueleza hayo ya watoto wake,
“Jamani huyu Erick kaanza kuwa kama Erick wewe, kurithisha watoto majina nako ni balaa”
“Kawaje kwani?”
“Anatongozwa na watoto wa kike, ila tofauti ya wewe na yeye ni moja tu. Mwenzio hawakubali”
“Kwani mimi nilikuwa nawakubali?”
“Ndio, tusizungumze hayo maana utachukia bure. Sasa huyu Erica jamani ni mbea yani kama mtoto wa Sia”
Mama Angel alikuwa akiongea huku akicheka sana, basi mumewe akasema,
“Mmmh usimuite mtoto kama mtoto wa Sia, yule Sia sio mzima kwenye akili yule na hafai hata kuwa mama yani hata yule Elly namuhurumia kwakweli”
“Haya mume wangu, ila unarudi lini? Nimekukumbuka mwenzio, sina raha ujue na sijazoea kuishi mbali na wewe, yani nahisi kama kuna kitu kimepungua katika maisha yangu”
“Hata mimi nimekukumbuka sana mke wangu ila nitakaporudi kwa hakika utafurahi sana, kwani nitakuja kivingine wala hatutohangaika tena kufanya kazi muda wote bali tutafanya kwa afya kwa tu”
“Sawa nakusubiri”
“Nisubiri tu, unajua ni jinsi gani nakupenda mke wangu”
Hapo mama Angel alikuwa anahisi amani sana moyoni mwake kila alipoambiwa na mumewe kuwa anapendwa, ni mara kwa mara mumewe alisema hivi ila kwa mama Angel mara zote aliona kama ni kitu cha muhimu sana katika maisha yake.
Asubuhi ya leo mama Angel aliona ajitahidi yeye mwenyewe kwenda kiwandani ilia one ni kitu gani kinachoendelea, basi alijiandaa na kuondoka zake.
Alipofika pale kiwandani kwakweli alishangaa kwani kila mfanyakazi aliendelea na mambo yao tu kwani msimamizi wao alichelewa kufika, mama Angel alichukia na kumfata mlinzi,
“Hivi hapa huwa wanafika muda gani? Yani huyo msimamizi anakuja muda gani?”
“Mara nyingi anafika saa tatu au saa nne”
“Kwahiyo muda huo ndio hawa wafanyakazi wanaanza kufanya majukumu yao?”
“Ndio, sababu hawawezi kufanya chochote bila kuelekezwa cha kufanya”
“Hivi kiwanda kitaendelea kweli kwa mambo kama haya jamani!”
“Unajua mwanzoni wakati Erick anakuja kila siku kidogo ilikuwa afadhali na walikuwa wakifanya kazi kwa bidii ingawa wanachelewa ila wanahakikisha hadi muda Erick anafika basi wanakuwa wametimiza malengo ya Erick. Unajua Erick ana hasira sana, kuna mfanyakazi Fulani alimfukuza kazi hapa bila hata kumsikiliza vizuri, ila asipokuja ndio kama hivi”
“Aaaah jamani, majitu mazima haya ndio yakasimamiwe na Erick kweli!! Ngoja aje huyo kiongozi wao nimpe habari, na kila siku asubuhi nitakuwa nakuja mwenyewe, huu ni ujinga, kiwanda hakiwezi kuendelea kwa ujinga huu”
Mama Angel alienda kukaa pembeni kwanza akimsubiria kiongozi wa hapo afike, na baada ya muda alifika, ila kwakweli hakutegemea ujio wa mama Angel kwahiyo aliogopa kiasi, kisha mama Angel alimpa masharti anayoyataka pale nakumwambia kuwa atakuwa anaenda kila asubuhi kuangalia vile walivyofanya,
“Kumbe kuna umuhimu sana wa kuja Erick mahali hapa! Sasa tumeweka wafanyakazi wa kazi hgani? Mbona kutaka kurudishana nyuma jamani! Naomba ratiba izingatiwe, sitaki hiki kiwe kiwanda cha kwanza na cha mwisho, nataka maendeleo kutoka hapa, msiniletee ujinga mimi.”
Kisha mama Angel alienda nae yule kiongozi ndani ya kiwanda na kukagua vizuri mambo yanavyoendelea pale, alikagua kila kitu na aliporidhika na mahesabu ndio aliondoka muda ule.
Kwakweli alivyoondoka yule kiongozi alipumua kidogo na kumfata mlinzi,
“Wewe lazima kuna kitu umemwambia huyu mama”
“Nimwambie nini mimi? Sina undugu nae, siwezi kumwambia chochote”
“Ila huyu mama mzuri sema anaonekana kuwa na roho mbaya sana, yani hacheki wala nini. Nadhani ndio kamlandisha yule mwanae Erick maana kale katoto kagumu hatari, siku ile laki tatu tu sababu haikuwa na mahesabu ya kueleweka akaondoka nayo, yani katoto kale ni balaa. Ila ngoja tupige kazi”
“Ndio bosi, ni kheri kuendelea na kazi maana ndio zinazotufanya tucheke hizi”
“Usiniite bosi bhana, mabosi wenye viwanda vyao. Niite jina langu tu”
“Sawa Yuda”
“Eeeeh hapo sawa”
Kisha alienda kuendelea na kazi kama kawaida ila kwa siku hiyo aliweza kutambua ukali wa mama Angel.
Siku hii mapema kabisa, Erica na Erick walienda shuleni, wakati Erick yupo shuleni alifatwa na Sarah kama kawaida na yeye alimpa ujumbe wa kuonana na mama yake.
“Jamani, mama mkwe kanikumbuka eeeh!”
Erick alikuwa kimya tu maana hakuwa na cha kumjibu kwa muda huo, halafu Sarah aliendelea kuongea,
“Hivi unajua ni kiasi gani nakupenda Erick?”
“Tuachane na mambo hayo jamani Sarah, kuna vitu vya muhimu vya kujadili na sio mapenzi”
“Ila mimi nakwambia ukweli kuwa nakupenda sana, siku moja nitaenda na wewe kwenye kaburi la baba yangu, najua atafurahi kuona binti yake nimepevuka na kufikia hatua ya kupenda”
Erick aliamua kwenda darasani tu kwani maongezi ya Srah hayakumvutia hata kidogo.
Walipotoka shule, leo kama ambavyo walipanga ni kuwa Sarah alishuka na Erick na moja kwa moja kwenda naye ndani kwao na alimkuta mama yao yupo ndani na alionekana muda sio mrefu katoka kufika mahali hapo, basi mama Angel alimkaribisha na kuanza kuongea nae kama mama, alimfundisha kwa kiasi maswala ya madhara ya mapenzi shuleni na jinsi mwanamke unavyokuwa ukimtongoza mwanaume,
“Ipo hivi binti yangu, mtoto wa kike unapomtongoza mwanaume kwanza kabisa unadharaulika, hakuna mwanaume anayependa kutongozwa na mwanamke. Unaishusha heshima yako, kama mwanaume anakupenda mwache aje akwambie mwenyewe, umejifunzia wapi kumueleza mwanaume mambo kama hayo?”
“Mama, mimi sijakurupuka kufanya hivi ni kutokana na malezi ambayo mama amenipa. Huwa ananiambia kuwa nikimpenda mtu ni bora kuwa muwazi, kumueleza mtu huyo mapema kuwa nampenda ili awe anajua kuliko kuishia kumuonyesha kama nampenda tu, inatakiwa ajue kwani itamfanya yule mtu apate urahisi wa kuwa na mimi kwani ataona ni jinsi gani nimejivika ujasiri wa kumueleza ukweli kuwa nampenda sana”
“Muulize vizuri mama yako alikuwa akikufundisha hayo kwa misingi ipi maana sifikirii kama mama yako alikuwa na hiyo nia ambayo wewe unaisema. Ngoja nikwambie kitu kingine, kuhusu Erick. Kwanza kabisa ile picha ya baba yako kama unakumbuka nilishtuka sana nilipoiangalia, na kama yule ndio baba yako basi wewe na wakina Erick ni ndugu sababu yule ni babu yao”
Sarah alishtuka sana na kusema,
“Hapana, baba yangu alikuwa ni mtu wa nje na hakuwa na ndugu hapa nchini”
“Ngoja nisiongee mengi zaidi, kesho ni Jumamozi naomba niletee mama yako ili niongee nae, Natumai amerudi”
“Ndio, amerudi jana”
“Basi kesho naomba uje nae niongee nae kwani najua nikiongea nae atanielewa zaidi na yeye kukuelekeza itakiwa vizuri zaidi”
“Sawa nitamwambia tu”
“Sawa, ila weka akilini mwako kuwa mtoto wa kike kumtongoza mwanaume hiyo haifai kabisa, unaondoa thamani yako kama mwanamke, yani hutaonekana kabisa, unatakiwa kuwa makini kwa yote uyafanyayo. Sarah wewe ni binti mzuri sana, Mungu atakujaalia na utapata mume mzuri mwenye moyo wa upendo. Mimi nakupenda ndiomana nimekuita na kukueleza haya, nakupenda sana sijui kwanini ila nakupenda na sipendi upotee kabisa, napenda uje kuwa mwanamke bora hapo badae, uwe ni mwanamke wa kuigwa na wengine. Natumaini Sarah unanielewa ninayoyasema”
“Ndio nimekuelewa”
Sarah aliamua kuaga kwani lile swala la kuambiwa kuwa ana undugu na Erick hakulipenda kabisa, na bado akajiapia kuwa hata kama ana undugu na Erick bado hakutaka kuacha kumpenda kama mpenzi wake.
Kisha mama Angel alimtaka Erick kumsindikiza Sarah nyumbani kwao, ila Erica nae alitokezea na kusema kuwa na yeye anaenda ikabidi waende wote wawili kumsindikiza Sarah.