Simulizi: Nini maana ya mapenzi

Simulizi: Nini maana ya mapenzi

SEHEMU YA 95



Erica alifika hadi alipoahidiana na Rahim, ilikuwa ni hotelini na walikaa mahali Fulani kwenye bustani. Kwakweli Erica alifurahia sana mandhari yale,
“Jamani mbona sijawahio kufika sehemu ya hivi?”
“Ukiwa na mimi utafika kila mahali”
Erica akatabasamu, kisha Rahim aliendelea na porojo zake ambapo cha kwanza kabisa alimuomba Erica simu yake kuwa aangalie picha,
“Mmmh jamani, mbona kuna picha za kawaida tu humu?”
“Naomba hivyo hivyo, nawe chukua yangu uangalie”
Erica hakuona kama ni tatizo kufanya hivyo, akabadilishana simu na Rahim.
Wakati wakiendelea na maongezi, Erica aliomba kwenda msalani na Rahim alimuelekeza, Erica alienda ila alisahau simu yake kwa Rahim.
Huku nyuma simu ya Erica ilianza kuita, Rahim akaitazama ile simu akaona namba imeandikwa Erick, akajua kwa vyovyote vile ni mwanaume, akaipokea
“Hallow”
“Namuomba mwenye simu”
“Una shida nae ipi?”
“Hiyo si simu ya Erica? Namuomba mwenye simu”
“Una shida gani na mke wangu?”
“Erica ni mke wako?”
“Ndio ni mke wangu, wewe una shida nae ipi”
“Aaah basi, mwambie asante”
Ile simu ikakatika, na kumfanya Rahim ajiulize sana kuwa huyo Erick ni nani na anamahusiano gani na Erica.
Basi Erica aliporudi, alianza kupiga nae story akamuuliza,
“Erica una mchumba”
“Kwanini umeniuliza hivyo?”
“Nimekuuliza tu, una mchumba?”
“Aaah hapana sina”
Rahim akapumua kidogo, kisha akaendelea kumwambia Erica
“Je upo tayari kuwa mchumba angu na badae kuwa mke wangu? Tafadhali kubali Erica nakupenda sana”
Kabla Erica hajamjibu Rahim, alifika Bahati kwenye maongezi yao na kusema,
“Nimekuja mbele yako Erica unikane kwa macho yangu kuwa mimi si mchumba wako”
 
SEHEMU YA 96


Rahim akapumua kidogo, kisha akaendelea kumwambia Erica
“Je upo tayari kuwa mchumba angu na badae kuwa mke wangu? Tafadhali kubali Erica nakupenda sana”
Kabla Erica hajamjibu Rahim, alifika Bahati kwenye maongezi yao na kusema,
“Nimekuja mbele yako Erica unikane kwa macho yangu kuwa mimi si mchumba wako”
Kwanza ni kitu ambacho Erica hakukitegemea kwahiyo alipigwa na bumbuwazi hivi kwa muda na kujikuta akiwa hana cha kujibu kwa muda kidogo, ila akakumbuka kuwa simu yake ipo kwa Rahim, akamuangalia na kumpa simu yake kisha akamwambia,
“Na mimi nipe simu yangu”
Rahim alimshangaa kwa muda kidogo Erica na kumuuliza kwa mshangao,
“Kwani imekuwaje? Huyu kijana ni nani?”
“Simjui”
Bahati akaongea kwa mshangao,
“Leo hii hunijui mimi Erica sababu ya huyu kijana wa kitajiri? Unanidharau sababu sina uwezo wa kukupeleka sehemu za aina hii Erica? Nilihisi yote haya maana huyu kijana simsahau kabisa toka siku ile beach”
Rahim akashangaa,
“Mlikuwa wote beach?”
“Ndio, huyu Erica ni mpenzi wangu”
Rahim akamuangalia Erica na kumwambia,
“Erica kwanini unakuwa muongo hivyo? Hupendezi kuwa muongo msichana mzuri kama wewe, kumbuka umeniambia hapa muda sio mrefu kuwa huna mchumba, kumbe unaye. Basi sema hapa ni yupi unayempenda kati yetu!”
Bahati akadakia,
“Ukweli ni kuwa Erica ananipenda mimi, ila wewe kakudanganya sababu kakuona ni tajiri”
Erica alichukizwa sana na maneno ya Bahati na kujikuta akiongea kwa jazba,
“Tena wewe Bahati unikome, nikome kabisa. Sijawahi kukupenda maisha yangu yote, nilikuwa na wewe sababu ya kukuonea huruma tu. Katika maisha yangu nampenda kijana mmoja tu anayeitwa Erick, na kwa ujinga wako huu huu umefanya nimkose Erick wangu”
Kisha akachukua mkoba wake na kuondoka, halafu akawaacha pale Rahim na Bahati wakiwa wanashangaa tu. Na wao hawakuweza kuendelea kuongea kwani muhusika alishaondoka na walimuona akipanda bodaboda na kutokomea, kwahiyo waliangaliana kisha Rahim akamwambia Bahati,
“Hakuna haja ya kugombana mimi na wewe ikiwa muhusika ameondoka, hata angekuwepo bado yeye ndio angekuwa na muafaka, sio mimi na wewe”
“Sawa lete simu yake”
“Hukunikabidhi wewe, nitairudisha mwenyewe”
“Usiwe mbishi, jua mimi ni mpenzi wake”
“Ila amekukana mbele yangu kuwa hajawahi kukupenda. Yani tusibishane bure hapa, si wewe wala si mimi anayependwa na Erica bali ni Erick. Kwaheri”
Rahim aliondoka zake, ikabidi Bahati nae aondoke zake ila bado alikuwa hajaridhika na moyo wake.
 
SEHEMU YA 97


Erica alirudi nyumbani kwao huku akijua wazi kuwa siku hiyo amechanganya mafaili vilivyo, ila akajisemea,
“Natakiwa kuachana kabisa na mambo ya mapenzi maana yataniumiza kichwa tu. Sitaki tena mapenzi kwasasa, huyu Bahati hapana kwakweli simtaki tena anikome kabisa”
Akaingia chumbani kwake na kuoga, aliporudi kukaa akakumbuka kuhusu simu yake,
“Mungu wangu, simu yangu jamani nitafanyaje na nimemuachia Rahim!”
Akawaza sana kuwa aende muda huo akawaza, kuwa mama yake akirudi bila kumkuta itakuwaje na muda utakuwa umeenda akaona ni vyema aende kesho yake kuchukua hiyo simu yake maana hakuwa na namna.
Alitulia hadi mama yake aliporudi na kumkuta nyumbani, ila alimuona kama binti yake hakuwa na raha kabisa, alimuita na kujaribu kuongea nae,
“Erica vipi mwanangu, mbona unaonesha huna raha?”
“Nilipoenda leo nilisahau simu yangu yani ndio nawaza sasa”
“Sasa kwanini hukwenda kuifata?”
“Niliona muda umeenda sana mama”
“Sawa, basi usiwaze sana utaenda hata kesho kuichukua”
Basi akakubaliana na mama yake kuwa ataenda kesho yake kuchukua hiyo simu, aliona ni vyema kumwambia vile ili kesho akiwa anatoka asiulizwe chochote na mama yake.
Alienda kulala ila kiukweli alikuwa na mawazo sana, aliwaza mno kuhusu simu yake na akawaza pia alivyomjibu Rahim na Bahati na pia akiwaza jinsi ya kuachana na mapenzi kabisa maana yalizidi kuivuruga akili yake.
 
SEHEMU YA 98


Kesho yake baada ya kazi zake za hapa na pale alijiandaa kisha akamuaga mama yake na kuondoka, moja kwa moja kuondoka alienda nyumbani kwakina Rahim yani kwa Mrs.Peter, ambaye alimkaribisha vizuri sana, Erica alikaribia ndani ila kabla hajasema chochote, Yule Mrs.Peter alimwambia Erica,
“Tena kuna mzigo wako, bora umekuja leo maana ningesahau bure”
Yule mama alienda ndani kumletea Erica huo mzigo, Erica alijua kwa vyovyote vile ni simu aliyoisahau kwa Rahim ila hakujua ni kwanini Yule mama kamwambia ni mzigo.
Muda kidogo Yule mama alirudi na kiboksi kidogo kwenye mfuko, na kumkabidhi,
“Mzigo wako huo, Rahim alisema nikupe”
“kwani yeye yuko wapi?”
“Rahim hayupo mbona, kasafiri leo ameenda Marekani kuna mambo anaenda kumalizia, alirudi mara moja tu”
“Aaah sawa”
“Basi, kaniachia mzigo wako tu huu anasema sijui siku ile mlivyoondoka mlipitia supermarket ila ukasahau mzigo kwenye gari yake, ndio kakufungia humo”
“Aaah asante sana, nashukuru. Nilijua bado yupo”
“Hapana, kaondoka leo. Yule mwanangu angekuwa na mambo ya wanawake basi ningehisi anataka kukutongoza ila Yule mwanangu namwamini sana, hana kabisa mambo ya wanawake”
“Ila mimi na yeye ni kama dada na kaka”
“Ni vizuri sana hivyo Erica, mi sipendi nione kuna mtu anachezea maisha yako au kuna mtu anachezea maisha ya mwanangu. Nashukuru Mungu mwanangu Yule, sio mlevi, havuti sigara na wala hana maswala ya wanawake, na sijui kama ataweza kutongoza mwanamke yule”
Erica akacheka na kumuuliza tena,
“Unapenda aoe mwanamke wa aina gani?”
“Mwanamke mwenye hofu ya Mungu tu basi, yani huyo atakuwa mke mwema kweli kwa mwanangu”
“Na atampataje ikiwa kutongoza hawezi?”
“Nadhani mwanangu ataoa mzungu Yule sababu wale ndio waelewa hata wasipotongozwa ila sio waafrika hawa, au labda nitamtafutia mwenyewe mwanamke ila mwanangu Yule kutongoza hawezi kabisa, na sijawahi kumuona na mwanamke.”
Erica akacheka tu kisha akaongea ongea kidogo na Yule mama kisha akaaga na kuondoka.
Alikuwa akirudi nyumbani kwao huku akiwaza kuwa kwenye boksi lile kuna kitu gani zaidi ya simu, ila akaamini tu kuwa kuna simu labda Rahim ameweka kwenye boksi lile ili mama yake asijue kama alikutana tena na Erica.
 
SEHEMU YA 99


Alifika nyumbani na cha kwanza kabisa ni kuingia chumbani kwake na kufungua lile boksi kuona kuna kitu gani, aliona simu yake halafu kuna boksi lingine, alivyolifungua alikuta kuna simu mpya ya kisasa na kumfanya ashangae sana, kisha kulikuwa na bahasha iliyokuwa na pesa taslimu shilingi laki mbili, kisha kuna karatasi lililokuwa limeandikwa,
“Erica, najua upatapo ujumbe huu sitakuwepo nitakuwa nimeshaondoka. Nakumbuka neno lako ulilosema kuwa unampenda sana Erick ila tambua kwamba na mimi nakupenda sana na nategemea kuwa wewe ndiye utakuwa mke wangu. Achana na watu ambao hawaeleweki kwako kama Yule kijana, sijapenda kujikuta nikibishana eti na Yule kijana tukikugombea wewe, sijapenda kwakweli. Ile sio type yako Erica, nakupenda sana. Nimekupa hiyo simu ya kisasa ili iwe rahisi kuwasiliana, maana humo utapata mitandao ya kijamii na tutawasiliana kwenye facebook, itakuwa rahisi sana. Nimekuwekea na laini yenye vocha kabisa, nadhani itakusaidia kwa siku kadhaa. Erica nakupenda sana, sijamwambia ukweli mama ila nataka nae tumshtukize tu siku nikimwambia kuwa nataka kumtambulisha mchumba wangu, nakupenda sana Erica. Nimerudi Marekani ila tutakuwa tunawasiliana, jitunze Erica, nakupenda sana sana”
Kwakweli Erica alichanganywa sana na ujumbe huu na alichanganywa zaidi na zile zawadi alizopewa na Rahim,
“Mmmh huyu ndio mwanaume sasa, natumai hata mama atampenda. Ila mmmh nampenda Erick sijui nifanyaje?”
Akawaza na kuchukua ile simu mpya aliyopewa na kuiweka kwenye chaji ilia aanze kuitumia.
Aliwasha simu yake ya siku zote na kukuta ikiwa haina jumbe hata moja wala haina simu yoyote iliyopigwa, hapo hakuelewa kuwa inawezekana Rahim amefuta au alibadilisha vitu kwenye simu yake, ila haikumuuma chochote kwani cha msingi alikuwa amepata simu mpya.
 
SEHEMU YA 100



Asabuhi alianza kuitumia ile simu mpya, aliipenda sana kwani siku zote alitamani kupata simu nzuri zaidi ila hakuweza kumwambia mama yake kuwa anataka simu nyingine, kwahiyo kitendo cha kupata simu hiyo kiliufurahisha sana moyo wake, akakumbuka kuwa ni Tumaini ambaye alimuona akitumia simu ya aina ile, aliamua kumpigia simu ilia amuelekeze baadhi ya vitu.
Aliongea na Tumaini, naye Tumaini alimuelekeza jinsi ya kufanya kwenye ile simu, kitu cha kwanza kabisa aliitafuta facebook na kujiunga nayo, huku akisubiri kwa hamu pale ambapo Rahim atamtafuta, ila rafiki yake wa kwanza facebook alikuwa ni Tumaini na kumshauri aweke picha zake mbali mbali kwani ndio itakuwa rahisi kwa watu kumfahamu.
Siku hiyo alijiweka vizuri kabisa na kuchukua ile simu kisha kujipiga picha kadhaa na kuziweka kwenye facebook,
“Mmmh hapo atajua tu ni mimi”
Simu yake ya kawaida ikaanza kuita, akaona anayepiga ni Bahati, na kumfanya achukie sana ila akapokea,
“Erica jamani, Erica mpenzi wangu nakupenda sana”
“Bahati, tafadhari achana na mimi”
“Kwahiyo Erica ulienda kwa Yule jamaa kuchukua simu au alikuletea kwenu?”
“Hayakuhusu”
“Erica, wewe ni mwanamke wa muhimu sana kwangu. Kumbuka mimi ni mwanaume wako wa kwanza Erica”
“Hivi wewe una kichaa nini? Hukuwa mwanaume wangu wa kwanza wewe, ulikuwa watatu”
Erica akakata ile simu huku akisema kuwa Yule asimzoee zoee, kwani alikuwa yupo makini na kutafuta marafiki kwenye mtandao wa facebook yani siku hiyo hata akasahau kufanya majukumu yake mengine sababu ya simu.
Mamake akamuita maana ilikuwa ni jioni na siku hiyo mama hakumuona kabisa Erica akitoka nje zaidi ya mara moja moja tu,
“Erica, hivi umekula wewe leo?”
Erica akagundua kuwa siku hiyo hata kula hakula kwani alikuwa na simu tu akihangaika nayo kila kurasa akiangalia vitu mbali mbali.
“Vipi mwanangu unaumwa?”
“Hapana mama”
“Sasa mbona upo hivyo?”
Hakuwa na jibu la kumpa mama yake kwahiyo kwa kujigelesha ilibidi aende jikoni na kuanza kufanya kazi za hapa na pale.
Kisha akarudi chumbani kwake kwa lengo la kulala ila hakulala mapema siku hiyo kwani alijikuta na simu tu ingawa mtu pekee aliyekuwa akiwasiliana nae kwa muda huo alikuwa ni Tumaini, ila muda mwingi alikuwa akiwaza kuhusu Rahim na kujaribu kumsahau Erick,
“Hata hivyo natakiwa kumsahau kabisa Erick, kwanza hawezi kunisamehe maana amenihisi kuwa na tabia mbaya. Ila pia nikimkataa mwanaume kama Rahim nitaonekana ni msichana mjinga sana kati ya wasichana wote, hivi ni nani asiyependa mwanaume anayejua kuhonga? Kila mwanamke anatamani ampate mwanaume anayejua kuhonga kama Rahim, hebu ona sifahamiani nae vizuri ila kapata uthubutu wa kuninunulia simu na kunipa pesa. Erick nampenda ndio, na hela anazo ila hajawahi kunihonga tofauti na huyu Rahim ambaye hata hanijui vizuri, nadhani huyu ndiye mwenye upendo. Ila sijui nitamsahau vipi Erick!”
Aliwaza waza kiasi, yani kwa wakati huo Bahati hakuwepo hata kidogo kwenye akili yake, alishamfuta kabisa. Kisha akalala.
 
SEHEMU YA 101


Kulipokucha aliamka na kuendelea na shughuli za hapa na pale, kisha alipomaliza alienda tena chumbani na kuzama kwenye simu yake. Ila leo mama yake alimuita tena na kumkalisha kitako,
“Erica mwanangu kakuona upo busy sana, ngoja nirudie hoja yangu niliyokugusia gusia siku zilizopita. Kwenye nyumba yangu sitaki uniletee mwanaume aliyechoka, yani mwanaume asiye na uwezo sitaki umlete yani ukithubutu nitamtoa na panga kwakweli”
“Jamani mama”
“Jamani nini? Unajua kwanini nimekwambia hivi?”
“Sijui mama”
“Nimekwama kwenye hela zangu za vikoba huko, sasa kila siku namtegemea Bite tu maana ndio kaolewa na mwanaume anayeeleweka ila dada yenu Mage uuuh sijui alikumbwa na zimwi gani, kaolewa na mwanaume hana mbele wala nyuma. Leo nimewapigia simu kuwa nimekwama hela ya kikoba wanasema hawana hela, yani wameniudhi sana, hivi kila siku nimtegemee Bite tu wakati nina watoto wengine? Huyo kaka yenu naye ameenda kuoa masikini huko yani wanamtegemea yeye tu, Erica tafadhari sana usije ukaolewa na waliochoka. Umenielewa eeh!”
“Nimekuelewa mama”
“Haya sasa, kaendelee na shughuli zako ila jua kabisa mauza uza siyataki kwenye nyumba yangu. Hapa nina mawazo kweli na hela ya kikoba”
Erica aliingia ndani na kutoka na elfu hamsini kisha akamkabidhi mama yake, kitendo hiko kilimfurahisha sana mama yake,
“Jamani huyu mkwe aliyekupa hizi pesa ndio namtaka kwakweli, ila tutaongea vizuri ngoja niende kwenye kikoba kwanza”
Mama yake aliondoka kisha Erica akaenda chumbani na kuendelea kuperuzi mtandao wa facebook.
Leo alipigiwa simu na namba mpya, aliipokea kwa shauku sana maana ilikuwa ni namba ya marekani na akahisi tu atakuwa ni Rahim, na kweli alikuwa ni yeye, Erica aliongea nae huku akicheka cheka tu.
“Naona umefurahi sana Erica!”
“Ndio nimefurahi”
“Furahi mama na jua kwamba Rahim anakupenda sana”
Erica alizidi kutabasamu, kisha Rahim akamuuliza Erica kama ameshajiunga na mtandao ambapo alimkubalia na kuamua kuhamia kwenye mtandao sasa na kuendelea kuwasiliana nae.
Erica alitabasamu muda wote alipokuwa akiwasiliana na Rahim, kwa wakati huo alianza taratibu kusahau kuhusu uwepo wa Erick, ingawa akimtaja anahisi kumkumbuka ila alijitahidi kwa kadri awezavyo amsahau kabisa. Simu yake ya kawaida iliita mara kwa mara na mpigaji alikuwa ni Bahati, Erica aliamua kuizima ili kuepuka usumbufu.
Aliwasiliana sana na Rahim siku hiyo kwa njia ya ujumbe bila ya kujua kuwa kule aliko Rahim kumekucha na kwao ni usiku, aliwasiliana nae sana hadi kuja kushtukia ni saa kumi na moja kasoro,
“Mmmh nimekesha jamani”
Ikabidi amuage Rahim na kulala.

Asubuhi aliamshwa na mama yake, kwenye mida ya saa nne,
“Erica, umelala mpaka muda huu kweli? Hebu njoo kuna kijana anakuulizia na wala simuelewi”
Erica aliinuka na kujiuliza kuwa ni nani huyo aliyekuwa anamuulizia, aliamka na kuvaa, kisha akatoka kumuona aliyekuja kumuulizia, alishangaa kuona ni Bahati ndio yupo sebleni akimsubiria.
 
SEHEMU YA 102




Asubuhi aliamshwa na mama yake, kwenye mida ya saa nne,
“Erica, umelala mpaka muda huu kweli? Hebu njoo kuna kijana anakuulizia na wala simuelewi”
Erica aliinuka na kujiuliza kuwa ni nani huyo aliyekuwa anamuulizia, aliamka na kuvaa, kisha akatoka kumuona aliyekuja kumuulizia, alishangaa kuona ni Bahati ndio yupo sebleni akimsubiria. Yani Erica alishindwa hata cha kusema na alishindwa jinsi ya kushangaa maana alikuwa anaona maajabu tu ya huyu Bahati, alisimama akimuangalia, mama yake Erica nae alikuwa ametulia pembeni akisubiri utambulisho ila alishangaa kuona kimya kikitawala, Bahati aliamua kutoa ule ukimya,
“Erica, mambo vipi?”
Erica alisogea na kumshika mkono Bahati kisha kutoka nae nje, mama yake alikuwa pale pale sebleni akishangaa tu.
Erica alifika nje na Bahati na kumwambia
“Umekuja kufata nini wewe?”
“Nimekufata wewe Erica”
“Si nishakwambia sikutaki”
“Erica nakupenda”
Akapiga na magoti huku akitaka kulia, Erica akaona hilo balaa lisije kuonekana na mama yake akamuinua pale chini na kumtaka aondoke,
“Erica sitaondoka hapa hadi uniambie kuwa unanipenda”
“Haya nakupenda, basi nenda”
“Erica, niahidi kwamba utapokea simu zangu”
“Ndio nitapokea, haya kwaheri”
Bahati alisogea ili ambusu Erica ila Erica alisogea kwa nyuma kidogo akiashiria kuwa hataki busu la Bahati, ila aliamua kumuaga kwa uzuri ili asimtie aibu kwa mama yake.
Aliporudi ndani tu, mama yake alimuuliza,
“Erica, ni nani Yule?”
Erica alifikiria kidogo na kumjibu mama yake,
“Yule ni kijana anayenileteaga samaki hosteli sasa nilimuelekeza kwetu ndio leo amekuja kupafahamu”
“Jamani, sasa mbona hujanitambulisha na unajua fika mama yako napenda samaki? Mwambie awe ananiletea”
“Sawa mama nitamwambia”
Erica aliitikia ila kiukweli hakupanga kumwambia kabisa Bahati kwani alijua wazi kwa jinsi Bahati anavyopenda sifa basi yupo tayari kupeleka samaki kila siku ilimradi apendwe.
 
SEHEMU YA 103



Alirudi ndani kujiweka sawa kwa siku hiyo maana hata kuoga hakuoga, kwahiyo alienda kuoga na alipomaliza alivaa kabisa na kutoka tena sebleni, mamake akamwambia,
“Mwanangu, Yule kijana ametuletea samaki”
Erica alishangaa sana kuwa Bahati amejuaje kama mama yake anataka samaki, na amewezaje kuwapata kwa muda mfupi vile, alijiuliza sana ila alitabasamu tu kwa mama yake.
Aliporudi ndani alimpigia simu Bahati na kumuuliza kuhusu samaki alizozileta,
“Nilirudi nje kwenu na nikasikia uliyokuwa ukiongea na mama yako, najua usingeniambia Erica ndiomana nilijiongeza na kuleta wale samaki”
“Yani wewe akili zako loh!”
“Usinifikirie vibaya Erica, familia yako ni sawa na familia yangu ndiomana nikafanya hivyo”
“Haya kwaheri”
Erica alikata ile simu na kujiuliza kuwa huyu Bahati ataacha usumbufu wake lini, maana alishangaa kuwa ni mtu wa aina gani anakataliwa lakini bado anang’ang’ania.
Na ikawa vile mara kwa mara alipeleka samaki kwakina Erica kiasi kwamba mamake Erica alimzoea vilivyo hadi pale Erica alipofungua chuo na kurudi hosteli bado Bahati alikuwa akipeleka samaki nyumbani kwakina Erica.
 
SEHEMU YA 104


Safari hii Erica hakuwa na marafiki wa kuongea nao zaidi ya kuongea na Tumaini na kumalizana na simu yake baada ya masomo, leo Tumaini alimuuliza
“Erica, ulichukua namba ya Erick vipi uliishia nae wapi maana Sia anaulizia”
“Erick hajawahi kupokea simu yangu hata mara moja”
“Ila nae ana facebook mtafute, andika tu Prince Erick utaona picha yake. Mule anaweza akakujibu”
“Sawa, nitajaribu”
Hakutumia muda mwingi sana kuongea sababu muda wake uliishia kwenye masomo na kwenye simu.
Siku ya leo alitafutwa na dada yake Bite, ambapo alionana nae na kuongea nae,
“Mdogo wangu dadako natafuta msichana wa kunisaidia kazi za ndani, niulizie ulizie huko”
“Dada msichana wa kazi wa nini na wakati pale mko wawili tu wewe na shemeji?”
“Dada yako nina ujauzito, yani unanisumbua huo balaa”
“Kumbe! Ila mimi nilikuwa sishauri kuweka mdada wa kazi”
“Kwanini?”
“Bora hata uweke mkaka wa kukusaidia”
“Mkaka? Shemeji yako hawezi kukubali huo ujinga, niulizie bhana mdada anisaidiage”
“Wadada siwaamini dada, unaweza shangaa akakusaidia vyote. Unashangaa akamchukua na mumeo”
“Unaongea nini wewe Erica, mume wangu unamchukulia kirahisi eeh! Sio wa hivyo shemeji yako anajiheshimu sana, na pia ananipenda sana mimi yani mimi ndio kila kitu katika maisha yake”
“Dada naomba nikuulize tu, hivi ni kitu gani kilikufanya ugundue kuwa shemeji anakupenda sana?”
“Mume wangu si mtu wa wanawake, na alinikuta bikra akaniambia Bite sitakuja kutembea na mwanamke mwingine yeyote zaidi yako, mume wangu hata akisafiri na kukaa miaka hata miwili najua anavumilia mpaka arudi kwangu. Muombe sana Mungu akupe mume wa dizaini hii, mwenye upendo wa kweli”
“Wewe dada una uhakika gani kuwa hanaga wanawake wengine zaidi yako?”
“Erica, naona unaanza mada zisizoeleweka. Wewe elewa tu kuwa ananipenda mimi tu na hana mwanamke mwingine zaidi yangu”
Ilibidi Erica asiongee zaidi maana yeye kwa siku chache alizokaa na shemeji yake aliona kuwa ana tabia zisizofaa kwahiyo swala la dada yake kumsifia kiasi kile lilimchanganya sana, aliongea ongea nae pale na kumuahidi kumsadia ila kiukweli hakupanga kumsaidia wala nini ila alimpa moyo tu kwani alielewa tabia ya shemeji yake kuwa lazima atapita na huyo dada wa kazi.
 
SEHEMU YA 105


Erica alifikiria sana kuhusu wanaume, alifikiria zaidi kuhusu dada yake aliyekuwa anajiona anapendwa asilimia mia moja wakati mwanaume mwenyewe anamtongoza hadi mdogo wake, aliwaza sana,
“Naweza nikaona Rahim ananipenda sana ila nyuma ya pazia kumbe ana wanawake wengi, ila mama yake alisema kuwa hana maswala ya wanawake. Kwa upande wa Erick, ni kweli ananipenda nampenda ila Yule kashakuwa na wanawake wa kila aina ataacha kweli? Mwenye asili haachi asili, kwa upande wa Bahati, naona huyu mtu ni msumbufu tu na sidhani kama ataacha usumbufu kwangu, labda nikiolewa ndio atakoma”
Aliwaza sana kuhusu wanaume na kukosa jibu la moja kwa moja, akiwa pale hosteli aliambiwa kuwa kuna mgeni wake anamuita nje.
Erica alitoka, na kumkuta George, akamshangaa
“Kheee George si umemaliza chuo wewe?”
“Ni kweli nimemaliza chuo ila kuna kitu bado sijakikamilisha na kinaumiza sana moyo wangu”
“Kitu gani hiko?”
“Niliahidi kukuoa Erica, na sijafanya hivyo kwakweli moyo unaniuma sana”
“Hata usiumie, mimi sina mpango tena wa kuolewa”
“Kwanini Erica?”
Kabla hajamjibu alitokea Bahati, kiukweli kipindi hiki Erica alikuwa hata hapendi kumuona Bahati kabisa kwahiyo kile kitendo cha kumuona tu pale alijua ni wazi lazima atapaniki kwa kumuona amesimama na mwanaume, Erica alimuacha George pale kasimama kisha akaondoka zake na kumuacha George akiwa amesimama pale, muda ule Bahati nae alikuwa na hasira sana kwahiyo alihisi moja kwa moja ni Yule anayemsumbua Erica kwa kipindi hiko ndiomana Erica hataki kumuona tena.
Bahati alienda moja kwa moja alipo George na kumkunja, hata George alimshangaa sana Bahati, ambapo Bahati akampiga ngumi George iliyomuangusha hadi chini na kisha kuanza kumshambulia ila George hakumgusa popote Bahati, watu wakaanza kujaa lile eneo la tukio na mwisho wa siku walinzi wa pale hosteli walisogea na kuwakamata kisha wakawapeleka kituo cha polisi.
Ikawa gumzo pale hosteli kuwa vijana wawili wamepigana sababu ya Erica, ila Erica mwenyewe alikuwa ndani na wala hakufatilia kilichotokea nyuma.

ITAENDELEA
 
SEHEMU YA 106



Alienda msichana mmoja na kumwambia Erica,
“Kheee Erica, ama kweli wewe ni kiboko yani inatokea mpaka wanaume wanapigana kwasababu yako!”
“Wanaume gani?”
“Ina maana kelele za hapo nje hujazisikia?”
“Kelele gani? Sijasikia chochote”
“Wale wanaume zako uliowaacha nje, wamepigana sababu yako. Wewe ni noma Erica? Mmmh nipe siri ya mafanikio, na mimi nataka wanaume wapigane sababu yangu”
Erica akacheka tu, na kuamua kutoka nje ili akaone kuwa imekuwaje, alipokuwa nje aliona kuna askari mmoja kafika kumbe alikuwa anamuulizia yeye mwenyewe, kwahiyo akachukuliwa na kupelekwa kituoni.
“Erica, vijana hawa wameletwa na imesemekana kuwa wamegombana kwasababu yako. Je una mahusiano nao wote?”
“Hapana, kwanza siwajui. Mimi nina mtu wangu”
Polisi wakaandika maelezo ya Erica na kumpa ruhusa aondoke. Aliondoka ila hakutaka tena kurudi hosteli, siku hiyo alimpigia simu dada yake Mage ili aende kwa dada yake huyo akalale huko sababu hakutaka kurudi hosteli na hakutaka kwenda nyumbani kwao kwani alihisi kuwa mama yake angemuuliza maswali mengi sana ukizingatia sio mwisho wa wiki na kwenda kwa dada yake Bite alipopazoea hakutaka kwani bado alikuwa na hofu na Yule shemeji yake.
 
SEHEMU YA 107



Erica alifika kwa dada yake Mage kwenye mida ya saa kumi na mbili jioni, na dada yake alimkaribisha vizuri sana,
“Kwa mara ya kwanza leo umeamua kuja kwangu kulala? Unanitenga sana mdogo wangu”
“Nisamehe dada”
“Haya, usijali karibu. Ila mimi ni dada yako, mimi ndio dada yako mkubwa, hutakiwi kunikwepa”
Basi Erica alikaribia pale kwa dada yake na kuongea ongea nae, kisha watoto wa dada yake walifika kumsalimia maana alikuwa na watoto watatu, na aliona jinsi watoto walivyokuwa wakubwa. Walipoondoka akamuuliza dada yake,
“Ila kwanini wanao huwa huwaleti nyumbani waje kukaa na bibi yao?”
“Mdogo wangu, hujui tu. Mama ni mama yetu, napenda sana kumletea wajukuu zake akae kae nao ila mama alinisema toka siku naolewa hakumpenda mume aliyenioa kabisa ila alikubali tu sababu nilikuwa mjamzito”
“Kheee kumbe uliolewa na mimba?”
“Ndio, niliolewa na mimba mdogo wangu”
“Sasa mbona mimi mlienda kunitoa mimba?”
“Erica, sitaki upitie tuliko pitia wengine. Napenda umalize shule, ndio uolewe na kuzaa. Hapo unakuwa kwenye maisha yenye furaha sana , tofauti na kuishi kwa stahili hii”
“Mmmh dada jamani, kwahiyo nyie mnataka niolewe mwanaume wa aina gani?”
“Swala sio kuolewa na mwanaume gani, swala ni kutokupata mimba kabla ya ndoa. Subiri uolewe kwanza, kuna njia nyingi tu za kujizuia kupata mimba”
“Ila wewe binafsi ungependa niolewe na mwanaume wa aina gani?”
“Mimi sikuchagulii mwanaume wa kuolewa nae, ila kwa ushauri wangu ukitaka kufurahia maisha basi olewa na mwanaume anayekupenda kwa dhati. Kwa hakika hutojutia maisha yote”
“Na nitamjuaje mwanaume anayenipenda kwa dhati?”
“Siku uje tena nikupe darasa kabisa la mapenzi, ila kwa leo tuendelee na mada zingine.”
Erica alitamani sana dada yake amwambie jinsi ya kumjua mwanaume anayempenda kwa dhati ila aliamua asikilize shauri lake kuwa atamueleza siku nyingine, kwahiyo akazungumza nae mazungumzo mengine kabisa kwa wakati huo, na mwisho wa siku walienda kula na kulala. Erica alielewa kwanini mama yake anataka wanaume wenye hela sababu mazingira aliyokuwa akiishi dada yake hayakuvutia kabisa, na alilala sababu ni kwa dadake ila ingekuwa vinginevyo asingelala pale, ila alimuheshimu sana mume wa dada yake kwani mwanaume huyu siku zote alimuona Erica kama mtoto wake, na akiongea nae ni kama baba anaongea na mtoto na si vinginevyo, Erica alijisemea moyoni,
“Mtu anaweza asiwe na pesa nyingi ila akawa na mapenzi ya dhati, na mtu anaweza akawa na pesa na akakosa mapenzi ya dhati. Nadhani mapenzi ni jinsi mtu anavyofanya yeye mwenyewe tu, ni tabia ya mtu bila kujali kipato chake”
Basi kesho yake akajiandaa vizuri na kuwaaga kisha kurudi hosteli ambapo alienda kubadilisha nguo na kwenda chuo.
 
Back
Top Bottom