SEHEMU YA 258
Asubuhi na mapema aliamka na kujiandaa kwenda kazini ila kama alivyopanga kuwa hatoenda kazini kwanza hadi apitie kwakina Dora, kwahiyo alimtumia shemeji yake ujumbe kuwa anapitia hospitali halafu ndio ataenda kazini, shemeji yake alimjibu kawaida tu kuwa poa. Hakujiuliza sana akaona labda shemeji hataki kumuhoji hoji sana.
Erica alienda hadi kwakina Dora ambapo alipofika kituoni alipiga simu halafu mdogo wa Dora alifika na kumpeleka hadi kwakina Dora, ambapo aliingizwa hadi chumbani alikolala Dora kisha Yule mdogo wake alimuacha na Dora na kutoka nje.
Erica alikaa karibu na Dora na kumpa pole huku akimuuliza kipi kimetokea,
“Erica sikutegemea Yule shemeji yako ni mshenzi kiasi hiki”
“Mmmh Dora usitukane tafadhari”
“Nisitukane kitu gani? Unajua alichonitenda? Tena ngojea nikuonyeshe namna ya kumtusi”
Dora alianza kuporomosha matusi na kumfanya hadi Erica aogope, kisha akamwambia,
“Dora, ukiendelea na hayo matusi kwakweli sitaweza kuvumilia, unajua kabisa mimi na matusi ni mbalimbali”
“Mbona ukayafanya hadi ukapata mimba na kuzaa”
“Dora, Dora nakuhurumia ndiomana niko hapa, sijaja unipe matusi au unionyeshe uwezo wako wa kutukana. Sijalelewa hivyo tafadhari, kama hayo mengine niliyofanya yaache nilifanya ila siwezi hayo ya kuongea. Wewe nishakupa pole, nimekuuliza nini kimekusibu unaanza kuporomosha matusi hivi hata ukifika mahakamani ukaporomosha hivyo matusi ni nani ataonekana mwenye makosa kati yako na shemeji yangu?”
“Haya yaishe ila shemeji yako kanifanyia kitu kibaya sana, hadi nikawaza kuwa labda umemtuma anifanyie vile maana wewe ulikimbia na kuniacha nae”
“Hapana, mimi tumbo lilinishika na muda ule ningemuaga shemeji angekataa tu si unaona alikuwa akinibishia nisiondoke”
“Haya bhana, shemeji yako Yule nina haki ya kumuita mshenzi maana alichonifanyia hakifai hata kidogo.Tulikunywa pombe na shemeji yako pale balaa, na wewe hukutokea, nilikuwa nimelewa haswaa nikaamua kumuaga kuwa naondoka ila shemeji yako akasema twende club, sababu nilikuwa nimelewa nikaenda nae, huko nako tulikunywa sana na nilikuwa nimelewa sana. Shemeji yako akanichukua sijui akanipeleka chumba cha hoteli kumbuka nilikuwa nimelewa, shemeji yako akanibaka na kunifanyia mchezo mbaya maana alinifanya kinyume na maumbile”
Erica akashtuka na kushangaa sana,
“Kheee shemeji ndio ana tabia chafu kiasi hiko?”
“Ndio hivyo, tena alivyo mshenzi sababu nilikuwa sijitambui kanitoa pale hotelini na kaenda kunitupa karibu na mtaro, watu ndio wameniokota na kunileta nyumbani. Kwakweli alichonifanyia shemeji yako hapana, nimeenda kushtaki polisi ila shemeji yako kanikana kabisa kuwa hafahamu chochote kuhusu mimi, yani Erica nimeumia sana, shahidi yangu ni wewe maana kesi ipo mahakamani”
Kwakweli Erica alisikitika sana maana alichofanyiwa rafiki yake hakikuwa kitendo cha utu hata kidogo, ingawa rafiki yake huyo amewahi kumtendea mambo mabaya ila yeye hakupanga vitu vibaya kwa huyo rafiki yake. Erica alikuwa kimya tu kisha Dora aliendelea kuzungumza,
“Eraca tafadhari nakuomba uwe shahidi wangu maana ni wewe tuliyekuwa pamoja na ndio unajua kuwa uliniacha na shemeji yako. Kanifanyia kitendo cha kikatili sana, sina nguvu sasa nalala tu unadhani kubakwa ni jambo rahisi? Raha ya mapenzi ufanye kwa utayari ila sio kwa kubakwa halafu kitu kinachoniuma zaidi ni kile kitendo cha kuniingilia kinyume cha maumbile, Erica inauma asikwambie mtu”
“Pole sana rafiki yangu yani nawaza nakosa hata jibu”
“Nisaidie rafiki yangu, nahitaji kupata haki kwa kindendo nilichotendewa, najua huyu mtu ni shemeji yako ila kumbuka kuwa mimi ni mwanamke mwenzako”
“Naelewa Dora, nitakusaidia. Pole sana”
Kisha Erica aliamua kumuaga Dora, na kumuachia hela kidogo kwaajili ya kumsaidia saidia,
“Sina pesa ndugu yangu, ila pokea hiki kidogo”
“Nashukuru Erica, ila usiache kuja mahakamani kutoa ushahidi nakuomba”
“Usijali nitafika”
Kisha Erica akaondoka na kumuona shemeji yake ni mtu asiyefaa kabisa kwenye jamii maana hakuelewa ni kwanini katenda kitu kama kile kwa Dora. Alitembea njiani akielekea kituoni huku akiongea mwenyewe,
“Yani wanaume sijui wana akili gani jamani? Kweli kabisa shemeji anafanya ujinga kiasi hiki! Nawachukia wanaume mie, siwataki kabisa, bora niishi mwenyewe kwa stahili hii sio kwa haya jamani, dada yangu namuhurumia maana sijui awe na moyo wa aina gani kuweza kupokea upuuzi huu alioufanya mumewe”
Wakati anaongea peke yake, kuna gari ilikuja na kupaki mbele yake. Mwenye gari alishusha kioo na kumsalimia Erica,
“Habari yako binti”
“Salama”
“Si unaenda stendi, twende nikusogeze”
“Hapana, asante nafanya mazoezi ya kutembea”
“Aaah! By the way naitwa Jimmy, sijui wewe unaitwa nani?”
“Naitwa Erica”
“Sawa Erica, basi naomba namba zako”
Akakumbuka maneno ya mama yake na kumwambia,
“Hapana, siwezi kukupa namba. Mimi ni mke wa mtu, na sipendi kuongea kwenye simu na mtu mwingine zaidi ya mume wangu”
“Hebu acha kunichekesha Erica, umesikia wake za watu huwa hawatoi namba? Unajua namba yako naitaka ya nini? Pengine ni maswala ya kazi? Sio kila mwanaume anayetaka namba zako ni ana lengo la kukutongoza, hebu futa hiyo fikra kwanza. Utakosa bahati kwa kujifanya oooh mimi mke wa mtu. Shauri yako, mimi nahitaji namba yako maana kuna kazi nataka kukushirikisha”
Erica akafikiria kidogo na kuamua kumtajia mtu Yule namba yake sababu mtu Yule alionekana ni mtu wa makamo na mwenye heshima zake, kisha akaagana na Erica.