Simulizi: Nitawatetea

Simulizi: Nitawatetea

Ms Yahaya

Member
Joined
Apr 14, 2022
Posts
6
Reaction score
12
Simulizi; "NITAWATETEA"

Sehemu Ya Kwanza (01)

Mwandishi; MARIAM YAHAYA

Namba; +255744654969

*****************************

RORYA

Ni katika kijiji cha Nyanchabakenye, ilikua siku ya jumamosi tulivu sana ambayo ilipambwa na jua la alfajiri lisilokuwa na makali. Kwa mbali walisikika ndege wakiburudisha anga baada ya kuiona siku nyingine tena, huku ndege wafugwao yaani kuku nao walisikika wakinon’gona wakisubiri kufunguliwa lango la gereza lao.

Wazee nao walionekana wakipita pita wakiwa wanaelekea kwenye vijiwe vyao vya kahawa ambavyo walipendelea kukaa mida ya asubuhi na jioni ili kupanda hadithi za ukweli na uongo wakisindikizwa na kahawa pamoja na mziki mtulivu wa asili.

Zilikua ni pilika pilika za kuhakikisha ratiba na mipango ya siku hiyo mpya ziende sawia, wanawake wengi walionekana na vifaa vyao vya kuchotea maji wakielekea mtoni lakini viajana nao walibeba majembe kuelekea shambani.

‘’Hivi bado amelala tu …?, mwanamke mzima hana hata haya …’’ ni maneno yaliyomtoka mama mmoja baada ya kutoka nje na kukuta pakiwa pamepooza, uwanja uliozunguka nyumba hiyo ukiwa mchafu huku kuku wakijidonolea mabaki ya magimbi katika vyombo vilivyoegeshwa barazani. Haraka sana alipiga hatua kadhaa kuelekea chumbani wanakolala wanae.

‘’……hivi bhoke kweli na utu zima huo unataka nikukumbushe kuamka mapema na kufanya usafi hapa?... huoni kua umeshakua mtu mzima, eeh? Hivi ni kitu gani kinachokufanya ulale hadi mda huu?".

Mama huyo alisimama mlangoni huku akifunga vizuri kanga yake ambayo Ilionekana imechahakaa lakini haikupoteza maneno yake ambayo bila shaka mnunuzi aliinunua si kwa uzuri wa maua yake bali kwa maneno yale ‘’kisichoridhiki hakiliki’’ ni maandishi yaliyoipamba kanga hiyo.

‘’Lakini mama…’’ ‘’lakini nini?’’ mama huyo hakusubiri mwanae amalizie lalamiko lake, alimkatisha akiendelea kumfokea.

"Unataka kusemaje mwanahizaya wewe… eeeh! Hivi unadhani watu watanichukuliaje…? Kwamba mimi sijui kulea au...?"

"Mama kwanini huna huruma na mimi lakini?, Wiki nzima tangu jumatatu kuanzia jua linachomoza hadi linazama nimekunja mgongo tu, kwanini na mimi nisipumzike hata siku mbili hizi….’’ Neema alilalama kwa mama yake huku akijivutia kushuka kitandani. Lakini haikusaidia kitu, ni kama aliyoyaongea yalipita kama upepo karibu na sikio la mama huyo.

Mama Bhoke huku akisogea na kuketi kitandani hapo alisema na mwanaye kwa sauti ya upole “Mhh... Mwanangu kama unavyojua humu ndani wananwake tupo wawili tu, mimi na wewe…” mama huyu alisita kidogo ili kurusu mate yaliyojaa mdomoni kushuka.

"...haya nambie nani natakusaidia hizo kazi kwa siku hizi unazotaka kupumzika…? Au unataka mimi nikunje mgongo kukusidia kufagia na kuosha vyombo eti…. Mmh halafu nikupikie chai mtoto mzuri, nikutengee maji ya kuoga halafu nije hapa nikuamshe ule... Eeh au nikubebee kabisa chakula nikuletee humu chumbani si ndio mama eeeh?....” aliendelea kusema na mwanae Mama Bhoke, mishipa ya shinggo nayo haikuwa mbali kutoa ushahidi ni kwa kiasi gani mama huyo alivyokasirika.

Ghafla, Bhoke aliruka; ni wakati mama yake alipokua akimfinya, kisha kwa haraka, Mama Bhoke alishika maskio na kuyavuta kwa nguvu mithili ya nywele zivutwavyo wakati wa kusukwa.

"Mamaaaaaa…” ni ukunga uliomtoka Bhoke baada ya kuona hali si shwari kwani mama yake alikua amekasirishwa na alichokisema.

“Nyamaza mjinga, mbwa wewe….” Huku akiwa amekunja sura, nidhahiri kua mama huyu alichukia haswa siku hiyo. Lakini baada mda alitulia tena huku uso wake ukionesha manunguniko, alimkazia macho mwanae aliyekua amesimama mbele yake.

‘’Mwanangu kafanye hizo kazi kwanza kabla baba yako hajarudi, kisha tuongee… sawa mamaa?’’ mara hii mama bhoke aliongea kwa sauti ya upole iliyojaa simanzi na yenye kubembeleza huku akimwangalia mwanae kwa macho ya huruma. Ni kama alikua akiona namna mwanae anavyoteseka nyumbani kwao bila ya msaada wowote kutoka kwa wadogo zake.

Baada ya mzozano huo uliochukua dakika kadhaa, bhoke alivuta miguu yake kuelekea nje, huku akiwa amekaza shingo dhahiri kua maisha yale yalimchosha haswa.

Ni maisha ya kuamka asubuhi na kuanza kufanya kazi zote za nyumbani, kumuhudumia yeyote yule atakayekuwepo ndani kwa vyote walivyohitaji bila kusahahu kutumwa huku na kule siku nzima.

Sio kwamba Bhoke alikuwa mtoto wa pekeee, hapana. Walikuwepo wengine lakini kwakua ni watoto wakiume basi kazi yao ilikua ni moja tu, nayo si nyingine zaidi ya kuchanja kuni. Ndo kitu pekee walichofanya.

Bhoke ni mtoto wa tano kati ya watoto kumi na mbili wa mzee Wambura, kati ya watoto hao watoto nane ndio wa tumbo moja na bhoke, lakini wengine wanne walikua wa baba yake na wanawake wengine wa nje, na kila mtoto alikua na mama yake kama mjuavyo, eti mwanaume aridhike na chungu kimoja hahahah…! haiwezekani.

Familia yao waliishi kiafrika zaidi kwani ilijaa watu kweli kweli, alikuwepo babu yake mzaa baba, binamu, baba zake wadogo wawili, bila kusahau hao ndugu zake wengine amabao nao wote walikua jinsia ya kiume.

Katika familia hiyo wenye jinsia ya kike walikua wawili tu yaani mama bhoke na bhoke mwenyewe, na familia yao ni moja ya familia ambazo mtoto wa kike hubebeshwa majukumu makubwa sana ikiwa na pamoja na kufanya shughuli zote za ndani na hata nje kama shambani na kuchota maji.

Kwa watoto wakiume maisha yalikua rahisi sana, kwao ni kuchanja kuni na kula tu, mara chache wangeonekana shambani.

Na kwa bahati mbaya kati ya watoto saba wa mzee Wambura, hakuna mtoto hata mmoja aliyepata kuendelea na masomo baada ya kumaliza darasa la saba, isipokua Bhoke peke yake, bahati iliyoje.

Sasa watoto wakiume wangesoma ili wapate nini?, maana ufahari wao ilikua mashamba na mifugo kama ng'ombe na kondoo, na babu yao pamoja na baba yao walikua navyo vya kutosha, walijihakikishia umiliki wa vitu hivyo tu baada ya wazee hao kuwatoka.

.
 
Simulizi; NITAWATETEA

Sehemu ya PILI (02)

Mwandishi; MARIAM YAHAYA

Namba; 0744654969

__________________

(Ilipoishia)

Familia yao waliishi kiafrika zaidi kwani ilijaa watu kweli kweli, alikuwepo babu yake mzaa baba, binamu, baba zake wadogo wawili, bila kusahau hao ndugu zake wengine amabao nao wote walikua jinsia ya kiume.

Endelea nayo...

Kwa watoto wakike ilikua ni nadra sana kwenda shule lakini bhoke alipata bahati, tena bahati kweli kweli, naam! naweza ifananisha na bahati ya mtende kuota jangwani au eeh! et simba kupata point tatu msimu huu hahah..! na hizi zilikuwa juhudi za bibi yake kipindi cha uhai wake mungu amlaze mahali pema peponi wote tuseme ..aminaa..

____

Ilikua imepita miezi miwili baada ya kumaliza kidato cha nne na sasa alikua anangoja matokeo kujua kile alichokipanda ndani nya miaka minne. Ndiyo maana mda mwingi alikua nyumbani akiishughulikia familia yake iliyojaza vidume ambavyo viliweza kula na kunywa, kurudi nyumbani mda watakao wao bila kuulizwa.

Kwakifupi ni kwamba aliishi maisha ya kua mfanyakazi asiyelipwa. Najua utasema chakula gani sasa anachokula? Hikihiki cha yeye kula mifupa tu na minofu kuliwa na wanaume. Au kula wa mwisho baada ya wao kushiba. Hivi itakuaje kama hawatashiba na kulazimika kula chakula chote kilichopikwa na labda ni mida ya usiku. Na vipi wao kula nyama ya kuku nayeye kuambulia mchuzi peke yake aagh!! Natamani kuwatia vibao khaaaaaa.

Bhoke alitoka nje ili apate kutimiza ratiba za siku hiyo, alitafuta beseni kubwa na kuweka vyombo vyote vilivyokuwa vimetumiwa usiku wa jana na kuviweka kwenye chanja, alianza kufagia ndani hadi nje jikoni na uwanja unaozunguka nyuma yao. Baada ya dakika kadhaa alipomaliza zoezi hilo ilifatia zamu ya vyombo kuoshwa.

Aliekea ndani yalipo madumu ya maji,

"Aaghh! nini hiki?" Sauti ilimtoka Bhoke baada ya kujaribu kubeba dumu la kwanza na la pili, lakini alijipa moyo na kuendelea kutikisa yaliyokuwa yamebakia, lakini bahati haikuwa upande wake hakua hata moja lililokua na maji.

"Nakumbuka jana jioni nilichota dumu saba za maji..! yameenda wapi..?" ni maswali aliyojiuliza kwa sauti iliyoishiwa matumaini.

"Moja, mbili, tatu , nne, tano mhh tano?, inakuweje tano sasa wakati yalikuwa saba..?" Ni maswali aliyojiuliza lakini hakuna lililojibiwa, angejijibu vipi sasa wakati hakushuhudia kilichotokea kwa madumu yale, na hata yenyewe hayawezi kusema kipi kimeyasibu.

Kwa hatua za harakaharaka alielekea jikoni akiwa na matumaini ya kukutana japo na dumu moja.

"Eeeh! Sijui hili litakua na maji..? kwahiyo nahumu hamna maji kabisa." Chozi lilimdondoka bila kutarajia, hakutegemea kwa ambavyo alihangaika jioni ya jana yake kupata maji yale ili siku hiyo naye apate kupumzika lakini mwishowe anakutana na dhahama hiyo.

Bhoke alitoka nje akiwa amenyongonyea mithili ya mtoto yatima asiyekua na mtetezi katika ulimwengu huu wa manyanyaso kwa watoto wa kike.

Alielekea kwenye kalo la vyombo, alivitazama kwa kitambo kidogo huku akiwaza.. "Sasa hivi ni saa mbili na robo, halafu ni jumamosi, maji yatakuwa yameisha tayari, itakuweje sasa? Eeh, kwamba niende kisimani au!, na palivyo mbali, kuna foleni, itanichukua masaa matatu na nusu kupata maji" Binti Bhoke hakutarajia kukutana na adha hiyo.

Binti bhoke alitikisa kichwa ishara ya kukubaliana na jambo fulani baada ya kukumbuka kitu.

"Jana usiku nilitaka kuoga lakini sikuoga, hivi alikua mnyama gani yule mbwa au chui? kheee..!"

Alipiga hatua na kukunja kona kuelekea nyuma ya jiko baada ya kukumbuka kua usiku huo aliandaa maji ya kuoga lakini hakufanikisha baada ya kutolewa mbio na mnyama ambaye kwa harakaharaka hakujua ni mnayama gani.

“Eeeh asante Mungu, sijui ingekuwaje…” Alijisemea Bhoke, hii ni baada ya kugundua kua lile dumu bado lilikua mahala pale alipoliweka usiku wa jana.

“Mhhh.. ndo maana wanasema Mungu hua na kusudi lake kwa kila jambo analoruhusu likupate, kweli nimeamini…’’ Bhoke alijisemea hayo huku akionyesha tabasamu kwa mbali iliyombatana na shukurani kimyomoyo.

Bhoke hakuwahi kuhudhuria ibada yeyote ile ambayo ingemfanya amtambue Mungu, hivyo aliishia tu kumsikia katika hadithi lakini kwa siku hiyo alimshukuru japo yeye amekulia kwenye familia yenye kuamini uwepo wa nguvu za mababu.

Alibebea dumu lake na kuelekea jikoni, ili arahisishe mambo, aliona bora aanze na chai. Alianza kukoka moto na baada ya moto kuwaka, alibandika maji kwa ajili ya chai. Na sasa ilikua zamu ya kuosha vyombo.

Wakati anaosha vyombo wadogo zake walitoka ndani na kukaa barazani mwa nyumba yao. "Hivi dada sasa hivi saa ngapi..?, ndio unaosha vyombo, kwamaana chai bado au….?"

Bhoke alishazoea malalamiko kama hayo, hvyo aliendelea na shughuli yake bila kujali kama kuna mtu alikua anamuogolesha.

Baada ya sekunde kadhaa kaka yake alitokea huku akipiga miayo na mkono mmoja ukiwa umeshikiria tumbo lake." Oya nyie mbona mmekaa kama mayatima hapa wakati wazazi wapo si uchuro huu….’’

Lakini hakuna aliyemjibu, kwa Bhoke naye hakujali uwepo wa nduguze hao. Aliacha kuosha vyombo, alisimama na macho kuelekeza mlango wa jikoni, alipiga hatua kuelekea huko jikoni kukoleza moto na aliirudia kazi yake hiyo.

Mda huo kaka yake alikua akipitisha macho wadogo zake mmoja baada ya mwingine kwani ni kama alikuwepo peke yake pale hakuna hata aliyesikika akihema.

"Haya nyie wenye wazazi mnaulizana kukaa kama mayatima na sisi ambao ni nusu yatima tutasemaje… Mama yangu angekuwepo nadhani ningekuwa nimeshiba mda huu….’’ Ni maneno yaliyomtoka ndugu yao mwingine aliyekuwa amesimama katikati ya mlango.

Kimya kilitawala kidogo, Bhoke alisimama na kuelekea jikoni aliipua chai na kuweka sufuria la magimbi amabayo yalibakia usiku wa jana ambayo kwa siku hiyo ndiyo kitafunio.

Alirudi nje, na sasa alitafuta jamvi na kutandika, chini ya mti uliokua pembezoni kwa nyumba yao, pamoja na kuweka vikombe na sahani kwa ajili ya chakula cha asubuhi.

Aliingia ndani na kumuita mama yake, lakini pia haikuchukua mda Baba Bhoke na babu yake nao waliwasili kutoka huko walipoenda kuangalia mifugo alfajiri ya siku hiyo.

‘’Mhh… kwahiyo mliamua kutusubiri sisi eeh…’’ ni maneno aliyoyatoa Baba Bhoke baada ya kuwasili hapo.

‘’Si bora ingekua hivo naona leo walitaka kutukomoa na njaa, bora umekuja….’’ Ni jibu alilolitoa kitinda mimba cha familia hiyo ambalo halikua na uhusiano wa moja kwa moja na swali lililoulizwa.

Bhoke alimfata baba yake na kumpokea fimbo yenye urefu wa fito.

"Karibu baba...’’ , Shikamoo; aliitikia salamu hiyo ambayo iliiambata na salamu za wengine waliokuwepo maeneo hayo.

Chakula kiliandaliwa, nao wanaume wa familia hiyo walianza kula na kunywa huku wakicheka.

Upande wa Bhoke yeye alikua pembeni tu akisubiri wamalize kula nayeye apate kula... na mama yake yeye alikua amekalia kijamvi chake upande wa pili wa walipokua wao akipukuchua mahindi.

Baba Bhoke aliinuka kuashiria kua ameshiba sasa akifatiwa na baba yake, ndugu wale waliendelea kula bila kujali kuwa dada yao bado hajala.

‘’Kumbukeni kumbakishia dada yenu…’’ ni kauli iliyomtoka Mzee Wambura ambayo sidhani kama alichokiongea alikimaanisha kweli maana angekua na uchungu na binti yake huyo baasi angemuita ili waweze kujukuika pamoja lakini eti baada ya yeye kushiba ndipo anapomkumbuka.

‘’Sasa kwanini umekaa hapo, huoni mama yako anaandaa mahindi kwanini humsaidii…’’ Baba Bhoke alifoka

"Utakaaje mbali sasa anahisi tutakula tumalize chakula, chakula chenyewe kidogo hata sijashiba….’’ Aliongezea kaka mkubwa wa Bhoke.

Bhoke aliwaangalia ndugu wale ambao waligawana kipande cha gimbi kilichokua kimebaki kisha kila mmoja kuinuka na kutokomea ndani bila hata kutoa shukurani.

Bhoke aliinuka alipokuwa amekaa alitoa vyombo walivyolia ndugu wale waliokosa heshima na utu ndani yao, alielekea jikoni ambapo alibakiza kipande cha gimbi na kumpelekea mama yake maana anajua bila kufanya hivyo mama yake asingekula kitu asubuhi hiyo japo ni kosa moja kubwa sana na la jinai kufanya hivyo yaani kubakisha chakula kwenye chungu.

.

.

.

Inaendelea, Usisahau kulike na kukoment ili kuipata simulizi hii kwa wakati.
 
Back
Top Bottom