SEHEMU YA KUMI NA MBILI:
Niliingia Mombasa saa kumi na mbili asubuhi, niliamua kusafiri alfajiri sababu ya kukwepa doria, magendo mengi yanapita usiku wa manane, na hivyo kufanya msako wa mara kwa mara baharini mida ya usiku kwa askari wapenda rushwa, nilikua nimebeba silaha nzito kwahiyo nilitakiwa kutumia akili ya ziada kuziingiza Kenya. Nilichepuka kilometa kadhaa kabla ya kuingia bandari ya Mombasa na kuvusha mzigo kwa kutumia mtumbwi hadi Kwale mjini.
Kwa kutumia gari ya kukodi, na kwa msaada wa jamaa aliyenivusha, hawa ni wavuvi wa mchongo, maisha yao wanayaendesha kwa kuvusha magendo kwa asilimia kubwa, uvuvi ilikua ni geresha tu, nilifanikiwa kupata gari ndogo ya kubebea samaki,tulijaza silaha zangu kwenye sanduku maalumu la mbao na kisha kulitanguliza mbele, ikifuatiwa na shehena ya samaki iliyokua kwenye sanduku maalumu lililojaa mabarafu, safari ya kuitafuta Kisumu ilianza.
Nilikua nimewasiliana na kina Tolu kwa code maalumu, hatukutaka kuuza mission maana hadi wakati huo tulijua doria itakua kubwa kusaka washirika wa Inno. Aliekamatwa ni kiongozi hatari wa kundi la vuguvugu nchini Ethiopia aliekua anatafutwa na mamlaka za nchi hiyo. Serikali ya Kenya ilikua inamtaka pia maana jamaa alihusika sana kwenye uuzaji wa silaha na biashara nyingine za magendo ukanda wa Africa Mashariki. Isingekua umuhimu wa Inno kwangu ningeacha tu jamaa akavune alichopanda, nimeshuhudia jinsi biashara ya silaha inavyofanywa kinyambisi na kujaribiwa uzito wa silaha na ubora wake kwa kufumua vichwa vya mateka wa vita, ila sikua nimemalizana na general, acha nifanye anavyotaka.
Niliingia Kisumu usiku sana, tulikua njiani kwa zaidi ya masaa kumi na tano, niliwakuta kina Tolu kwenye kijumba chakavu nje kidogo ya mji wa Kisumu panaitwa Muhoroni. Kwa msaada wa mwenyeji wetu ambae alishaanza kufuatilia lile sakata, tulifanikiwa kupata mawili matatu juu ya taarifa za kutekwa kwa Inno.
Kwa taarifa tu za juu juu ni kua kesho ndio siku ambayo Inno na yule jamaa wa Ethiopia walikua wanasafirishwa kwenda kukabidhiwa kwa mamlaka za Ethiopia. Ilikua ndio nafasi pekee ya kuwaokoa na ilikua ni mission ya hatari sana, tulitakiwa kulala pale hadi majira ya saa kumi alifajiri , nikawaambia hapana, zege halilali, tunaondoka mda huohuo kuweka doria mpakani, tukisubiri masaa yakatike lazma nao watatanguliza watu wachache wa kusafisha njia, itakula kwetu.
Nilichojaaliwa ni uwezo wa kujenga hoja, hatukua na cha kupoteza ,ni heri kuwahi kuliko kuchelewa, tukaamsha hadi mpakani. Tulitafuta sehemu ya kuweka kambi kilomita chache kabla hujafika mpakani, eneo la mpakani liliathiriwa kwa kiasi kikubwa na ukame, palikua na vijichaka vya kusuasua, tulivaa mavazi meusi ambayo yangetubeba na muonekano wa giza, pamoja na kujifunika mashuka maalumu yenye muonekano wa udongo wa mahala pale, hayo mashuka tulipatiwa na mwenyeji wetu ambaye huyatumia wakati wa kuvuka mpaka.
Baada ya masaa manne tuliona gari ya jeshi kwa mbali, wote tukaangaliana, kwa hesabu za harakaharaka yalikua yamebaki masaa mawili mbele ili msafara upite, ikimaanisha kua nilikua sahihi kuwaza kuhusu kutumwa wasafisha njia, tulikua tayari kwa lolote. Lile gari la wanajeshi lilipita kwa kasi, kwa mbele likasimama na wanajeshi baadhi wakashuka , wakasambaa na kuanza ukaguzi kwa maeneo ya karibu na mpaka, kwa kile ambacho hatukukitegemea jamaa waliweka kambi eneo la mpakani. Hadi wakati huo pakafanya idadi ya wanajeshi kumi na nne pamoja na wale nane tuliowakuta .
Niliweka sawa silaha yangu aina ya DENEL NTW - 20, silaha adhimu toka South Africa, ina uwezo wa kudungua hadi kilomita 1 na zaidi, inategemea na uwezo wa shabaha yako, ugunduzi wa bwana Denel Mechem, niliona na wenzangu wakiandaa silaha zao, palikua na bunduki aina tano tofauti pale, mabomu ya kurusha na mabomu ya moshi, kwa idadi jumla tulikua watano, watatu toka Tanzania na wawili tuliwakuta Kenya.
Masaa mawili mbele tukaona msafara wa magari mawili ya jeshi, hapo ndio nilielewa kwanini general alihitaji mimi na Tolu tuwepo. Tuligawana makundi mawili, nilibaki na wale wakenya wakati Tolu akisogea mbele na Gody kwa mtindo wa kutambaa na tumbo. Tungeweza kuwamaliza wale wanajeshi mapema waliotangulia , ila ukimya wao wakati msafara unafanya mawasiliano kusogea mbele zaidi ungefanya root ibadilike, au siku zisogee mbele na ulinzi uzidi kuimarishwa, hatukua na muda zaidi wa kupoteza , ilikua ni lazma tumalize mchezo siku ilele kabla hapajakucha.
Tulisubiri msafara usogee ndani ya kipimo changu , kwa kutumia kifaa cha kuweza kuona mbali, niliweza kuona mateka wawili wakiwa wamefunikwa vichwa, nikafahamu kua wanaweza wakawa mizigo yetu tuliyoifata. Nikajaribu kukagua wanajeshi waliobaki labda kuna namna watakua wametufanyia mchezo maana ilikua michezo yetu Burundi kubadili muonekano wa mateka kupumbaza maadui. Kwa ishara ya mwanga wa tochi mara mbili tulianza kushambulia msafara kama nyuki, risasi zilitembea kama mvua, ilikua ni ghafla mnoo, mimi nilicheza na kuwapunguza waliokua wamening'inia kwenye magari , nikafuatia na madereva wa gari zote mbili, wanajeshi wengine waliruka kwenye magari na kupambana kuzuia risasi zisiwafikie mateka.
Tolu na Gody kwa pamoja waliwashambulia wanajeshi waliokua mpakani, ilikua ambush ya kushtukiza na hawakuitegemea maana walishasafisha njia kwahiyo walikaa kizembe wakisubiri kukabidhi mzigo. Ndani ya dakika kumi risasi zilitembea kama mvua, Kuna mwanajeshi wa Kenya alituotea na bomu la kurusha , mmoja kati ya vijana tuliyekua nae akaliwahi na kulirusha mbali , lililipuka na kufanya mtikisiko wa kuogofya, nilishamalizana na wale waliotakiwa kudunguliwa, tulilisogelea gari lilikuwepo mateka kwa mtindo wa kupeana migongo ,hiyo inasaidia kujilinda zaidi na adui.
Tulifanikiwa kuwaokoa mateka na kuwamalizia wanajeshi wawili waliokua wamejeruhiwa na risasi, mmoja alikua anapambana kufanya mawasiliano ya kupata msaada wa wanajeshi zaidi, nilimtwanga risasi ya kichwa na story yake ikaishia pale. Niliwaacha wale wakenya walinde package na kwenda kutoa msaada kwa akina Tolu, ndani ya dakika ishirini zaidi tukawa tumefanikisha kuweka hali ya usalama, tulijua hatutomudu kutoboa tena Kenya, tulikiwasha usiku ule ule hadi Kisumu. Kwa msaada wa mwenyeji wetu tuliwapatia Inno na yule Muethiopia huduma ya kwanza na kukiwasha hadi Mombasa kwa kutumia usafiri wa lori la mizigo.
Inno alikua anashukuru njia nzima , siamini kama umekuja kuniokoa kaka... nilijua sitokuona tena....kuna namna ya upendo niliuona kwa Inno ulinikumbusha ndugu zangu Rwanda, Ni jinsi gani unapata faraja kuonana na nduguyo ambae hukutaraji kumuona tena. Kwa Mara ya kwanza nilitamani kurudi Rwanda. Kwa namna ileile niliyoingia Mombasa niliitumia pia kuondoka nchini Kenya maana nilijua mipakani kutakua hapafai wakijua tutafanya kosa lilelile alilofanya Inno. Hawakujua wanadeal na mtu wa aina gani. Ile siku ndio lilitoka jina la 'Godfather'...."master of missions, master of plans and master of actions"