Simulizi:The President and I(Mimi Na Rais)

Simulizi:The President and I(Mimi Na Rais)

SEHEMU YA TANO

Joe Awasili Pyongyang. Siri Nzito Yawashtua Habibu Na Pius.

“선량한 동지들” seonlyanghan dongjideul (Habari za asubuhi kamaradi). Ndugu En Ki, waziri anayehusika na masuala ya kigeni wa Korea Kaskazini aliwasalimia kiKorea Joe na ujumbe wake mara tu baada ya kuwapokea uwanja wa ndege wa Pyongyang.

“좋은 아침” joh-eun achim(Salama) Joe nae alijibu kiKorea huku akiwa ameshikana mkono na ndugu En wakiwa wameinamishiana vichwa. “평양에 오신 것을 환영합니다. pyeong-yang-e osin geos-eul hwan-yeonghabnida, (Karibuni Pyongyang), Waziri En aliendelea.
“고마워. 우리의 즐거움 동지 야”gomawo. uliui jeulgeoum dongji ya. (Asante sana. Ni furaha yetu kubwa sana kuwa hapa), Joe nae alijibu huku akitabasamu.

Joe akiwa mwanadiplomasia mbobevu alielewa itifaki za mataifa mengi. Alikuwa ni mtu makini ambaye ukikutana nae unajua kabisa kuwa ameiva kwelikweli katika masuala ya mahusiano ya kimataifa, diplomasia na hata lugha za kigeni.

Ndugu En aliwaongoza Joe na ujumbe wake mpaka kwenye magari yaliyoandaliwa kwa ajili ya msafara kuelekea Ikulu ya Pyongyang. Kutokea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pyongyang Sunan jijini Pyongyang mpaka makazi ya Rais Kim ni mwendo wa kama dakika 40 hivi kwa gari, hivyo msafara ulianza kwa kuifuataHeeecheon Expressway.
Yalikuwa jumla ya magari manne, la mbele likiwa linaongoza msafara, la pili alipanda Waziri En na Joe, la tatu alipanda Habibu na Pius na la nne likiwa ni la ulinzi. Wakiwa njiani, Joe alikuwa akiongea mawili matatu na En. En alikuwa ni mjuzi wa lugha nne ukiacha ya kiKorea.

Alizungumza kwa ufasaha kiingereza, kichina, kirusi na kifilipino. Alikuwa ni mtu mwenye uelewa mkubwa sana wa masuala ya kimataifa na mwenye akili nyingi sana. Aliaminiwa na Rais Kim Jon Un wa Korea Kaskazini tangu alipoingia madarakani kurithi mikoba ya baba yake alipofariki.
“Comrade Kim has high expectations of your visit”, (Rais Kim ana matarajio makubwa na ujio wenu huu). En alimwambia Joe huku akitabasamu kwa shauku. “Same to President Costa”, (Hata Rais Costa), Joe nae alijibu kwa ufupi. Joe alijua mbinu za mazungumzo, alijua wapi pa kuongea sana na wapi pa kuongea kwa uchache, alijua lipi la kujibu na lipi la kukaa kimya. Tangu anawasili Pyongyang kila jambo analofanya alitumia umakini mkubwa.
Safari iliendelea huku Joe akishangaa na kustaajabu namna barabara ilivyokuwa tupu na nyeupe. Hakuona hata mtu mmoja tokea walipouacha uwanja wa ndege. Alikuwa akistaajabu na alipouliza kwa En alijibiwa hivyo ndivyo wanavyowaheshimu wageni muhimu kwa taifa. Joe hakuelewa.
**************************************
Ryongsong ndilo jina la makazi ya Rais Kim. Wengine hupenda kuyaita Residence No. 55 auCentral Luxury Mansionkutokana na umaridadi wake. Ni makazi yanayosemekana kulindwa na kuwa salama kuliko makazi yoyote duniani. Ukubwa wa eneo yaliyopo makazi haya ni kilometa za mraba 12 pakiwa na kila aina ya kitu kinachohitajika kwa kiongozi mkuu wa nchi.
Wataalamu wa masuala ya ulinzi na ujasusi wanaamini kuwa askari kati ya 95,000 – 120,000 wapo maalumu kwa ajili ya kulinda eneo hili pamoja na usalama wa Rais Kim na maeneo mengine yote yalipo makazi ya familia ya Rais Kim. Wakiwa chini ya kikosi namba 963wakiongozwa na Jenerali Yun Jong-Rin, wanakifanya kikosi hiki kuwa moja ya vikosi vikubwa kabisa vya ulinzi wa Rais duniani.
Ryongsong imezungukwa na machimbo yaliyotegwa kulipuka kama kuna mvamizi yeyote atataka kusogelea makazi haya kwa njia ya ardhi, lakini pia kuna wigo mkubwa wa umeme pamoja na vituo vingi vya ukaguzi kwenye njia ya kuingilia na kuzunguka makazi haya. Makazi haya pia yamezungukwa na vituo vya kijeshi vyenye makombora makubwa ya maangamizi na ya masafa marefu na mitambo ya kunasa chochote kinachoikaribia eneo lile bila taarifa na kuweza kutuma kombora kukisambaratisha.
Hakuna ndege wala kifaa chochote kinachoruhusiwa kupita juu ya anga lililopo jengo hili la sivyo kitatunguliwa hapohapo. Ndani ya makazi haya, chini ya ardhi kuna Sehemu salama ya kumficha Rais ikiwa itaonekana yupo hatarini. Eneo hilo limejengwa kwa kuta za chuma kizito na zege zito lililofunikwa na madini ya leadili kuzuia nyumba hiyo kuathirika hata kwa shambulio la nyuklia.
Lead ni moja ya madini yenye myeyuko hafifu (Low melting point), hivyo huhitajika joto la kuanzia nyuzi joto 327 ili yaweze kuyeyuka. Ni katika Sehemu hiyo Rais Kim huweza kuishi huko kwa usalama bila chochote kutoka kwa maadui kuweza kumvamia ama kumdhuru kwa miaka zaidi ya mitatu mfululizo bila kutoka, huku akiweza kutoa maelekezo ya kivita na kiutawala.
Makazi haya pia yameunganishwa na makazi mengine ya Rais ya Changgyongau huitwa Residence No.26. Makazi haya yote yamewekewa mfumo utakaoruhusu kutumia njia iliyopo chini ya ardhi ikitokea kuna uvamizi. Pia chini ya ardhi kutokea kwenye nyumba hii kuna reli maalumu kwa ajili ya Rais tu na kitu cha kustaajabisha kwa wachambuzi wengi wa masuala ya kiusalama ya peninsula ya Korea ni kuwa reli hii ilitengenezwa kuelekea mahali kusikojulikana.
Inadhaniwa kuwa mwisho wa reli hii hubadilikabadilika kulingana na mahitaji ya wakati husika lakini lengo kuu likiwa kuhakikisha kuwa Rais na familia yake wanakuwa salama likitoea shambulio. Mbali na mambo mengine mengi ya kiulinzi na kiusalama, nyumba hii imepambwa sana kwa nakshi, taa na samani nzuri. Nje kukiwa na bustani nzuri na za maua zenye kuvutia, mito na maziwa ya bandia yaliyotengenezwa kupendezesha eneo hili. Hakika makazi haya yalivutia.
Joe, Habibu na Pius walikuwa wanakuja kuingia hapa kwa mara ya kwanza.
*******************************************
“Wananchi wenzangu mlinichangua ili nilete maendeleo na maendeleo ndiyo haya. Nimesema na nimemwagiza Waziri wa Kilimo na Chakula hapa kuwa Sitaki kusikia mkulima yeyote anakatwa tozo eti ya kusafirisha mazao. Mtu hata kuuza hajauza unamkata tozo kivipi? Vibali vya kusafirisha mazao vitolewe bure kama mtu amelima mazao yake kihalali anayatoa shamba anayapeleka mjini ama mkoa fulani kuuza unamwambia alipe, sasa alipe na nini wakati hata kuuza hajauza? Tena sitataka kusikia ukiritimba katika kutolewa vibali hivi.
Waziri upo hapa unanisikia na viongozi wengine wote hili nalifuta kuanzia leo”, Rais Costa alikuwa akiongea huku akishangiliwa kwa nguvu na wananchi wa Kisasampara, Jimbo la Kengwe alipokwenda kuzindua ghala kubwa za chakula za hifadhi ya Taifa.
“Tumeanza mazungumzo na serikali ya China na tutaingia nao ubia kutujengea soko kubwa la kimataifa la matunda. Soko letu likikamilika litakuwa la kwanza kwa ukubwa bara la Afrika, hivyo vijana anzeni kujikita kuzalisha matunda. Neema inakuja!” Rais Costa aliendelea huku umati mkubwa wa watu ukimshangilia. Alikuwa ameanza utekelezaji wa ushauri aliowahi kupewa na Joe siku za nyuma namna ya kujadiliana na Rais wa China juu ya kuingiza vijana wa kichina zaidi ya laki moja kuja nchini Stanza kufanya biashara ndogondogo.
Rais Sylvester Costa alimaliza kuhutubia na kushuka jukwaani na kusalimiana na wananchi wawili watatu kisha kuanza kutembea kuelekea kwenye zile ghala kuzikagua. Alikuwa amefuatana na mawaziri, viongozi wengine wa serikali kuu na ya Jimbo pia alikuwepo na bi. Eliza, mke wa Joseph ambae kwa wakati huo ni Mkurugenzi wa Benki ya Kilimo ya Stanza. Aliingia akayakagua na kuridhika kisha msafara uliondoka kuelekea kwenye nyumba ya mapumziko ya viongozi wa kiserikali kwa ajili ya mapumziko iliyopo pale Kengwe.
Wakiwa kwenye nyumba ya mapumziko Rais alipata chakula pamoja na Waziri wa Kilimo na Chakula, Waziri wa Fedha ambaye ndiye alikuwa Waziri wa zamu kwa wiki hiyo, Gideon, mshauri wa karibu wa Rais Costa na Eliza mke wa Joe.
“Eliza Watoto wanaendeleaje”, Rais Costa aliuliza. “Wanaendelea vizuri Mh Rais’’, Eliza alijibu pasi kumtazama Rais usoni. “Nimeipata mikakati yako ya kuboresha ufanisi wa benki na hakika taifa lilikumisi sana”, Rais Costa aliendela kuongea huku akikata kipande cha nyama kwa uma na kisu. “Nafurahi kutoa mchango wangu kwa taifa”, Eliza alijibu kishupavu na maongezi mengine yaliendelea. Mara baada ya kumaliza kula Eliza, Waziri wa Fedha na Waziri wa Kilimo na Chakula waliaga na kuondoka kuelekea mahali walipoandaliwa kupumzika.
“Mh. Umeona wananchi wanavyokupenda? Umesikia walivyokuwa wapiga kelele uendelee kubaki madarakani? Mimi nadhani hata tulivyobadili katiba kuruhusu miula mitatu ya utawala tuliwarahisishia kazi sana”, Gideon alikuwa akimjaza upepo Rais Costa wakiwa pale sebuleni wakisoma magazeti huku wakitazama habari kwenye runinga.

“Ninaona hapa huyu Kibwe ameanza kupiga kelele juu ya azma yangu ya kubadili umri wa kugombea urais. Ni vyema tukamdhibiti mapema, si mtu wa kubeza, ana ushawishi mkubwa ndani na nje ya nchi. Hawa jamaa wa magharibi watatusumbua tukimwacha aliongelee ongelee”.
Badala ya kujibu aliloambiwa na Gideon, Rais Costa yeye alimwonyesha habari katika gazeti inayomwonyesha Julius Kibwe, kiongozi kijana na machachari wa upinzani akipinga vikali tetesi za muswada wa kutaka kubadili umri wa kugombea urais uongezwe kutoka miaka 40 mpaka miaka 55.
“Nitamshauri Waziri wa Sheria na Masuala ya Bunge njia nzuri ya kulipeleka hili, lakini wakati huo huo ni vema wewe ukazidi kuongeza imani na mapenzi kwa wananchi”, Gideon alimjibu Rais Costa.
‘’Umetoka kusema kuwa wananchi wananipenda. Hiyo Imani na mapenzi unayoshauri niongeze kwa wananchi ni kwa njia zipi?’’, Rais Costa alimuuliza Gideon akionekana wazi kuwa hajaelewa hilo lingefanyikaje kwani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, pamoja na ukandamizaji wa demokrasia na kufunga wapinzani wake, lakini alianza kuhisi umaarufu wake umeshuka na kwa namna fulani wapinzani wake kisiasa walizidi kumkalia kooni wakimtaka aheshimu haki za binadamu, Sheria na Katiba ya nchi. Aliona kama alichosema Gideon hakiingii akilini kwa hali ya sasa.

‘’Tengeneza tatizo kupitia viongozi wa chini yako kisha wewe jiweke mbali nalo, hakikisha kuwa linamgusa kila mmoja au watu wengi, acha watu wapige kelele, wanasiasa waongee, kisha litatue na kulaumu watu wengine aidha kwa kuwataja hadharani au hata kwa kuwataja kwa ujumla tu katika makundi yao, ikiwezekana tumbua baadhi yao. Hii itakufanya wewe uonekane usiye na hatia, tena mkombozi haswa’’, Gideon alijibu na kumfanya Rais Costa kumpa usikivu zaidi na hata kubadilisha mkao.
“He he he he!”, Kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu, Rais Costa alicheka na kuonekana kuvutiwa na mipango ya Gideon ambayo ingemuongezea umaarufu na kupendwa. Rais Costa alipenda kusifiwa zaidi, hakutaka kusikia mtu anayemkosoa au asiyemuunga mkono. “Tatizo kama lipi kwa sasa?’’, Rais Costa alihoji kutaka kufahamu zaidi kuhusu mpango wa Gideon ambao ulishaanza kumvutia.
“Leo umetoka kuwafurahisha wakulima, ina maana vijijini tayari umezidi kupendwa kwani tozo hizi zilikuwa ni kero. Lakini ukumbuke kwa kufanya hivi umepunguza chanzo cha mapato kwa halmashauri nyingi hivyo ni lazima tutafute pa kulipia, sasa waite Waziri wa Fedha na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Taifa ya Mapato na Makusanyo. Wape maagizo waanze operesheni ya kukamata wote ambao hawajalipa kodi hata kama mhusika biashara yake mtaji ni wa chini ya shilingi laki moja, alazimishwe kulipa kodi kwanza kabla hajaanza bishara kwa kukadiriwa”, Gideon alishauri na kukaa kimya huku akimtazama Rais Costa.
“Ukweli kuna uliyosema ya msingi hasa kutafuta vyanzo mbadala vya mapato lakini hili la kulipisha watu kodi hata kabla ya biashara kuanza tena hata wenye mitaji ya chini kabisa sijaliunga mkono. Halina afya kwa mwananchi wa kawaida na tunajiua kiuchumi wenyewe”, Rais Costa alionekana kutoelewa.
Gideon alicheka sana kisha akamwambia Rais, “Hilo ndio litakuwa tatizo, na baada ya miezi mitatu hivi hadi sita ya watu kupata taabu na Mamlaka za Ukusanyaji Mapato na Kodi na kulalamika sana, utafuta huo utaratibu kwa kisingizo kuwa ni kumkandamiza mnyonge na wewe haupo kwa ajili ya kutesa wanyonge”, Gideon alimaliza.
Rais Costa alimwangalia Gideon kwa sekunde kama tatu akiwa kimya kisha aliangua kicheko kikubwa “Gideon you are a genius”, (Gideon una akili sana). Alifungua chupa ya wine na kuanza kummiminia Gideon.
***************************************
Msafara wa Joe na En uliwasili kwenye makazi ya Rais wa Korea. Rais Kim alikuwa mlangoni akiwasubiri na mara baada ya kushuka walipokelewa. Joe akiwa mbele ya Habibu na Pius alifika mbele ya Rais Kim kwa heshima kubwa, akainama kidogo na kumkabidhi nembo ya Rais wa Stanza (‘The Republic of Stanza’s Presidential Seal’), kama ishara haswa ya ujumbe maalumu wa Rais wa Stanza. “Karibuni sana”, kwa mshangao mkubwa Rais Kim aliwakaribisha kina Joe kwa kutumia Kiswahili. Walikumbatiana na kuelekea chumba maalum kwa ajili ya mazungumzo ya awali na kufikisha ujumbe Rais wa Stanza aliotaka umfikie Rais Kim.

Walifika na kuketi, Kim akiwa sambamba na En Waziri wake wa masuala ya kigeni huku kina Joe wakiwa wamepewa mkalimani waliulizana habari za hali na maendelo baina ya nchi hizo mbili. Joe alimkabidhi faili maalumu la siri alilopewa na Rais Costa lililo na barua na maelezo ya lengo la ujumbe ule. Hata hivyo maelezo yote aliyaandika Joe.
Baada ya Rais Kim kupokea faili lile alitoa maelekezo kuwa siku ile ya kwanza wangekutana ujumbe wa Joe na ujumbe wa serikali ya Korea Kaskazini. Joe na ujumbe wake wangeeleza kila jambo lililowapeleka Korea na kisha ujumbe wa Rais Kim ungeenda kutafakari na kisha kukutana nae kutafakari kabla ya kukutana tena wote kwa makubaliano na maazimio kesho yake.
Ilipangwa kuwa ni ugeni utakaodumu kwa siku mbili wakianza siku hiyo waliyowasili mpaka watakapoondoka. Mara baada ya kupata ratiba hiyo Joe na wenzake walielekezwa eneo la mapumziko na kuachwa hapo watatu wakiwa wamepewa kahawa kama walivyohitaji.

Joe akiwa na wenzake aliwaambia sasa muda wa kuonyesha vipawa vyao vya majadiliano ya kimataifa umefika. Wakiwa wanajadiliana, Pius alionekana kutotulia kiakili. Suala walilokuwa wamezungumza kwenye ndege lilikuwa likimsumbua sana.

“Upo sawa?”, Joe alimuhoji Pius. “Hapana, suala lile bado linanitafuna akili nataka kujua ni nani mwingine anafahamu”, Pius alimjibu Joe. Kwa kujua kuwa maongezi yao yaweza kuwa yanarekodiwa ndani ya makazi yale kwa kutumia vinasa sauti vyenye uwezo mkubwa ilikuwa ni lazima watumie maneno machache sana kuzungumza mambo yao au hata kwa ishara. Joe alishajua Pius anazungumzia nini, alijua anataka kujua ni nani mwingine yupo kwenye ule mpango aliowashirikisha wa kumpumzisha Rais Costa nje ya madaraka pasi yeye kutaka kwa hiari kuyaachia.
Joe aliwaangalia Habibu na Pius usoni. Aligundua kuwa bila kuwafumbulia fumbo hilo wasingefanya vizuri kwenye mazungumzo yao kwasababu akili zao zilitekwa na mpango ambao Joe aliwashirikisha kwa kifupi. “Ok, nitawaambia ili akili zenu mzirudishe hapa. Stanley Macha ni mmoja wapo kwenye mpango huu, mwingine sitawatajia kwa sasa” Joe aliwadokeza kwa kifupi.

Habibu na Pius walionekana kushtuka. Hawakuamini kama Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa nae yupo kwenye mpango huo. “This is serious guys”, (hili suala ni nyeti). Joe aliwaambia huku akiwatazama usoni. “Tutaamini vipi kama ni kweli?”, Habibu alihoji.
“Nitawapa namba za siri (codes). Sasa kila mtu kwa wakati wake na ikiwa umekubaliana na mpango huu kwa ustawi wa nchi yetu na kuwa mmoja kati ya watakaoleta chachu ya mabadiliko ya kweli, utamtumia Stanley hiyo namba ya siri kwa njia ya WhatsApp nae atajibu kama utakavyomwandikia, na baada ya hapo hamtaendelea na mazungumzo yoyote. Hiyo itakuwa ndio ishara kuwa nimeshawaambia na kuwa tupo pamoja”, Joe aliwaeleza.
“Tupe hizo codes”. Habibu na Pius walijikuta wakiuliza kwa pamoja. “Ego testor”, Joe aliwajibu (Hili ni neno la kilatini lenye maana ya kuapa/kula kiapo). Haraka Pius na Habibu walitoa simu zao za mkononi kwa shauku kutaka kuhakikisha kile wanachokisikia.

Waligundua simu zao hazinasi mtandao wowote, wapo ugenini lakini hata kama wangekua wanaweza kuwasiliana kwa wakati ule isingewezekana kwani ukikaribia tu makazi ya Rais Kim mawasiliano yote hukatika na ni mfumo wao tu maalumu wa mawasiliano ambao wanao watu wachache sana ndani ya makazi yale ndio hutumika. Walihema wote kwa pamoja na kutulia.
************************************
Je, Mazungumzo Jijini Pyongyang Yatafanikiwa?Vipi Usalama Wa Stanley Macha Baada Ya Kutajwa Na Joe?Usikose Sehemu Ya Sita
 
SEHEMU YA SITA

Mazungumzo Mazito Yarindima Pyongyang. Timu Ya Joe Na Timu Ya Waziri En Zaonyeshana Ujuzi

“Gentlemen, it’s time” (Ndugu, muda umefika), Waziri En, anayehusika na masuala ya kigeni na mahusiano ya kimataifa wa Korea Kaskazini aliingia akiwaita Joe na wenzake wamfuate.
Huku En akitangulia, Joe alifuata na kisha Habibu na Pius. Mara baada ya wote kutoka mlango wa chumba namba 315 ulijifunga lakini ghafla Pius aligundua kuwa amesahau simu yake juu ya meza ndogo ya kahawa iliyokuwa pembeni yake. Simu ile aliitoa mara baada ya kutaka kuwasiliana na Stanley Macha ili kujiridhisha kama kweli kuna mpango wa kumpumzisha Rais Costa nje ya madaraka kabla ya muda wake kuisha. Hivyo alipokumbuka alitaka kurudi ndani ya chumba kwa haraka ili aichukue.
“Aaaaaaaaaaaaaah”, alisikika Pius akilia kwa nguvu mara tu baada ya kugeuka na kuusogelea mlango ule wa chumba namba 315. Haraka En alitoa ishara fulani na hapo hapo walitokea askari wawili wa usalama kama upepo wa kisulisuli na kumnyakua Pius kumpeleka ambapo Joe hakupafahamika.

“What’s going on here?” (Nini kinaendelea?), Joe aliuliza kwa mshangao huku akimwangalia En.
“Relax, it is just a normal security measures that have been taken. He has been exposed to methylbenzene, a chemical substance that is irritants when contacted to an eye, so they have taken him to wash it out and he will join us soon. He should have told me that he was returning to the room, I would have given him security clearance. My apologies for the inconvenience”.
(Tulia, ni utaratibu wa kawaida wa kiusalama umechukuliwa. Ameingiwa machoni na kemikali iitwayo methylbenzene, ni kemikali ambayo ikikuingia machoni inawasha sana, kwahiyo wamemchukua kwenda kumuosha na ataungana nasi muda si mrefu. Alitakiwa anitaarifu kuwa anarudi kwenye chumba ili nimuombee kibali. Samahani sana kwa usumbufu huu). Alikuwa ni Waziri En akimwelezea Joe nini kimetokea huku wakiingia kwenye chumba cha mkutano.
***********************************
Jengo la makazi ya Rais Kim lilikuwa na ulinzi usio wa kawaida. Katika vyumba na korido zote kumefungwa kamera ambazo zina scan sura yako. Kila mtu aliyepo ndani ya jengo lile hupimwa nyuzi joto la mwili wake pamoja na mapigo ya moyo na sensors zilizofungwa kila kona, hivyo ni kusema joto lako likipanda ama mapigo ya moyo yakipanda ama kushuka kuliko kawaida haraka utaanza kufatiliwa nini kinaendelea kwenye mwili wako.
Si hivyo tu, ilikuwa hairuhusiwi kuelekea popote ambapo sio eneo lako la kazi bila kutoa taarifa kwenye chumba cha usimamizi (Control room) ili wakupe ruhusa na kuzuia hatua zozote za kiusalama kuchukuliwa dhidi yako la sivyo ni lazima udhibitiwe. Hivyo ni kusema mienendo ya kila mtu ndani ya jengo lile inajulikana kwa kila hatua na kila dakika.
Katika kila eneo kuna matundu madogo na sensors zinazofatilia lenzi ya macho ya mtu. Matundu hayo hurusha maji ya kuwasha pale tu mtu anapokatiza eneo ambalo hajapewa kibali. Maji hayo hupigwa moja kwa moja machoni kufuatana na mahali unapotazama labda uwe umeyafunga.
Milango yote hufunguliwa kwa rimoti kutoka chumba cha usimamizi. Hivyo ni kusema kamwe huwezi muona mtu yeyote akifungua mlango wowote na milango yote haina vitasa. Kuta za jengo lile zina unene sawa na mita moja zenye kujengwa na chuma kizito na juu kuweka simenti kali. Kuta na milango yote havipitishi risasi.
Kitendo cha En, Joe, Habibu na Pius kutoka ndani ya chumba namba 315 kilitoa taarifa chumba cha usimamizi kuwa watu hawa wametoka na wanaelekea chumba namba 441 hivyo kila hatua za kiusalama zilirudishwa kwenye chumba namba 315. Mlango ulifungwa,sensors za maji washa zilifunguliwa na za kupima joto zilifunguliwa kuonyesha kuwa eneo lile halihitaji tena kuwa na joto lolote bila taarifa.
Kitendo cha Pius kurudi kilasensor ilimdhania ni mvamizi na haraka kuchukua hatua. Mlango ulikuwa umebana na sensor inayofata macho ilifanya kazi na kuruhusu methylbenzenekurushwa moja kwa moja machoni mwa Pius. Ni sahihi kusema kuwa Ryongsong si makazi ya kawaida.
Wakiwa wameketi, Joe na En pamoja na wajumbe wao walimwona Pius akiingia huku akitabasamu. “This place is crazy”, (Hili eneo ni la ajabu). Pius alimnong’oneza Joe akiwa anaketi upande wa kulia kwake.
“Gentlemen, my apologies once again, now we can start our conversation. Shall we?” (Ndugu, niwaombe radhi kwa mara nyingine tena na sasa tunaweza kuanza mazungumzo yetu. Au siyo?). Waziri En aliwaalika Joe na wenzake huku akitabasamu. “확실한” Hwagsilhan (Sawa), Joe alijibu kwa kiKorea.
Wakati Upande mmoja akiwa amekaa Joe, Habibu na Pius, upande wa pili wa meza alikaa Waziri En, Jenerali Uk In ambae ni Mkuu wa Jeshi la Ukombozi la Korea Kaskazini na wajumbe wengine wawili. Kikao kilianza.
***************************************
“Tetesi hizi ninazozisikia za chama Tawala kinachoongozwa na Rais Costa za kutaka kubadili umri wa kumruhusu mtu kugombea Urais kutoka miaka 40 mpaka 55 sisi kama wafanya siasa mbadala tunakataa na muswada huo ukija tutaupinga kwa nguvu zote, kwanza haufai hata kuingia bungeni, vuguvugu la kutaka kuruhusu Rais agombee muhula wa tatu tena kwa kipindi kirefu zaidi ya awali lilianza hivihivi’’. Alikuwa ni ndugu Julius Kibwe kiongozi mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Stanza akizungumza wakati wa mahojiano katika kipindi cha Tarumbeta la Alasiri, kipindi cha Luninga kinachorushwa na stesheni ya MULIKA.
Akiwa ni miongoni mwa wageni walioalikwa kwenye mjadala huo akiwemo na Katibu Mkuu wa chama tawala ndugu Stanslaus Kaberege. Wote walikuwa wakimulika hali ya kisiasa na Uchumi nchini Stanza.
“Kwani shida ni nini”, Stansalaus aliuliza kwa kebehi.
“Ndugu yangu usijitie upofu kwa sababu upo hapo kutetea maslahi ya tumbo lako. Madhara yapo wazi kabisa katika hii hatua na tunajua lengo la Rais Costa ni kutaka kuminya upinzani katika uchaguzi ujao akijua fika wengi wa viongozi wa upinzani wenye matamanio na nafasi ya Urais watakuwa hawajafikia umri huo hivyo kutaka tupate wagombea wasiojulikana na kupunguza ushindani kwake.
Lakini la pili, hata ndani ya chama tawala na wewe mwenyewe unajua vijana wengi machachari na wenye uzoefu mkubwa wa uongozi watakuwa hawajafikia miaka 55. Vijana kama kina Habibu alioamua kuwanyamazisha kwa kuwapa ubalozi ni miongoni mwa watu aliowatoa kwenye ulingo wa kisiasa ili kupunguza upinzani dhidi yake hata ndani ya chama chenu”, Kibwe aliongea kwa msisitizo.
“Unajua ndugu mtangazaji, hata kama tetesi hizi zina ukweli maana nikiri wazi hazijafika kwenye meza yangu, sisi kama chama tunaamini na tunatambua kuwa uRais ni taasisi nyeti inayohitaji mtu aliyetulia kiakili na aliyekomaa, hivyo sioni shida kabisa kama wabunge wakipima wakaona hili linafaa wakaliafiki”. Stanslaus aliamua kujibu kiunyonge kwa kumuelekezea majibu mtangazaji badala ya Julias Kibwe alietoa hoja.
“Wakati nchi za wenzetu wakifikiri kupunguza umri ili kuwapa vijana nafasi ya kujiamulia hatma ya kizazi chao wewe unatetea kuongeza umri kuwapa wazee watuamulie hatma ya Maisha yetu? Hatutakubali.” Kibwe alionekana kukasirika kidogo na jibu la Stanslaus.
“Sawa, labda kwa sababu suala hilo ni tetesi tuliache na kwasasa tuangazie uchumi na hatua za maendeleo anazochukua Rais Costa, kwako katibu”, mtangazaji alimrushia Stanslaus swali.
“Juhudi zinaonekana. Tumeshuhudia mapinduzi makubwa ya kilimo, mapinduzi makubwa ya kibiashara katika bandari yetu. Leo tu Rais ametoka kuzindua maghala makubwa ya chakula na kutoa kodi zote sumbufu kwa wakulima achilia mbali mapinduzi makubwa yaliyotangazwa na benki ya kilimo kuwawezesha wakulima.

Tumeshuhudia miundombinu ikitengenezwa na mambo mengine mengi. Unajua ubaya wa wapinzani kama kina Kibwe, japo tunaheshimu michango yao lakini huwa hawaoni mazuri serikali inayofanya. Inawezekana ni kwasababu tu hawalitakii mema taifa letu au wana tamaa ya madaraka badala ya kuonesha uzalendo na kuungana na serikali kuwalete wananchi masikini maendeleo”, Stanslaus alionekana kujibu kwa bashasha.
“Miundombinu gani? Tuache kucheza na maisha ya watu. Hospitalini hakuna madawa wala madaktari, mashule hayana hata matundu ya vyoo, walimu wala madawati. Maji bado ni tatizo halafu mnasimama kusema maendeleo yanaonekana? Maendeleo ya Vitu na siyo maendeleo ya Watu ndugu Stanslaus.

Unawezaje kujenga uwanja mkubwa wa kimataifa wa ndege jimbo la Nungu kisa tu ndipo Rais alipotokea wakati ungeweza kufanya uwekezaji huo maeneo ya kimkakati ambayo yangekuza biashara za ndani za utalii na usafiri wa anga wa kikanda. Tija ipo kwenye uwekezaji wa kimkakati. Sasa kiwanja kile kimegeuka eneo la Kunguru kufanyia mashindano ya kuruka badala ya ndege, ndege gani itatua kule na ili iweje?
Mmejenga kituo kikubwa cha sayansi na teknolojia mkijinasibu mnataka Stanza iwe kitovu cha TEHAMA ukanda huu lakini mmewezaje kujenga kituo hicho huku mkijua elimu yetu bado ni tia maji tia maji? Kwanini tusingeanza kuimarisha kuanzia elimu ya msingi kuja juu hivyo kituo hiki kingekuja kuwa na manufaa?”, Kibwe alionekana kuongea mfululizo.
“Tatizo ni moja tu, ni wewe, sio Rais”, Stanslaus alionekana kujibu tena kwa kebehi.
“Ndio maana tutahakikisha Rais Costa harudi tena madarakani”, Julias alijibu kwa hasira tena kwa ufupi.
“Muda wetu unakaribia kufika ukingoni, labda kwa kumalizia ningependa kujua ni kwa vipi na hasa wewe Julius umejipanga kwa ajili ya kuchukua nafasi ya juu ya uongozi wa nchi, na Stansalaus kwa upande wa chama tawala mmejipangaje kuhakikisha vijana wanasimama na kugombea nafasi hii?” Mtangazaji alimalizia kuuliza.
“Kwanza, chama chetu kina uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa vijana. Tumefanya utafiti na kugundua kuwa kama uchaguzi ungefanyika leo, chama tawala kingepata asilimia 22 tu ya kura katika nafasi ya Urais. Ninachoweza kusema ni kuwa, uchaguzi mkuu ujao hakutakuwa na wizi wa kura ambao chama tawala kimezoea kufanya. Kila kura itahesabiwa.
Tutaamkia na kulala kwenye kila kituo cha kupiga kura. Huu ni mwisho wa Costa na mabavu yake. Lakini pia tumejipanga kupigana kwa njia zozote zile kuhakikisha kuwa katiba haibadilishwi ili kuzuia wagombea vijana kuwania nafasi ya Urais. Mwambieni Costa kuwa hilo haliwezekani’’, alisema Kibwe akionekana waziwazi kujipanga haswa kwa uchaguzi mkuu ujao.
“Sisi tumejipanga. Chama chetu ni chama tawala na kitaendelea kuwa chama tawala milele kwasababu kinapambania maslahi ya nchi yetu. Namshauri tu Kibwe na wenzake wamuunge mkono Rais Costa ili tuwaletee maendeleo wanastanza’’. Alihitimisha Stanslaus akionekana kutokuwa na wasiwasi na utawala wa Rais Costa.
*************************************
Mazungumzo kati ya timu ya Joe na Waziri En yalikuwa mazito na ya ndani sana.
“I think the issue of establishing a secured communication system for Stanza should be handled by our Chinese friends who are more technologically advanced than us. Over the last few decades, China has been able to develop the best technology, second to none and they are our very good partners. We also use their technology in our communications. If that is something of interest to you, we can assist you to establish conversation with the Chinese who are also good friends with your country. So, lets put that aside and focus on the military assistance and technology”.
(Nafikiri suala la mtandao wa mawasiliano salama tuwaachie China. Wao wana teknolojia ya hali ya juu ya mawasiliano na ni marafiki zetu wazuri. Kwa kipindi cha miongo michache iliyopita, wao wameweza kuendeleza teknolojia kubwa ya mawasiliano salama ambayo haina mshindani. Tunaweza kusaidia mazungumzo nao maana hata sisi tunatumia teknolojia yao. Hivyo suala hili tuliweke pembeni kwa sasa na tuangazie suala la msaada wa kijeshi na teknolojia), alikuwa ni Waziri En akiweka sawa majadiliano baada ya kuona suala la masuala ya mawasiliano ni vema wakapewa China.
Alitoa maoni yale kwa sababu kuu mbili ambazo Joe alizing’amua lakini akamezea. Kwanza ni ukweli teknolojia ya mawasiliano wanayotumia Korea Kaskazini ni muunganiko wa teknolojia ya Uchina kwa asilimia kubwa na Urusi na yao kidogo. Lakini kiufundi, En hakutaka kuharibu wala kuleta sintofahamu kati ya taifa lake na China. China ni chanda na pete na Korea Kaskazini.
Kwake En aliona si sawa kwa Stanza kuivuka China au kwenda kuongea na Korea kuhusu masuala ya kusimika mifumo ya mawasiliano salama na kuiacha China, ambayo ni mbobevu wa siasa za Afrika na mwekezaji mkubwa.
En alitaka China ahusike katika mchakato huo. Korea haikutaka iwe katika sintofahamu na China hata kidogo hivyo En alionelea kwa namna moja ama nyingine hiyo iwe ni fursa kwa Korea kuiambia Rafiki yake wa karibu China kuwa kuna jambo tunataka kutekeleza Africa nchini Stanza. En alianza kutabiri mbele kurudi nyuma kwa kuelewa nguvu kubwa itakayoibuka kutoka mataifa ya magharibi mara tu mambo fulani yakianza kutekelezwa na sasa Korea ilihitaji iwe na mshirika mapema.

Joe alikubali kuwa wajadili kwanza kuhusu rada na misaada ya kijeshi kama ilivyopendekezwa na Waziri En. Waziri En alimwambia wana uwezo wa kuwapa rada zote za kuangazia usalama wa maji, hewa na nchi kavu.
“Comrade En, our priority is installing AN/SPF-71 generation radar’’. (Kamaradi En tungependa kupata rada kizazi cha AN/SPF-71 kama kipaumbele chetu cha kwanza), Luteni Jenerali Pius aliingilia kama eneo lake la uzoefu.
AN/SPF-71 ni kizazi cha rada za hali ya juu zenye uwezo wa kunasa aina zote za mawimbi na kwa maeneo yote. Huitwa kwa kizungu three surfaces radar detection, huweza kunasa mawimbi ya makombora ya masafa marefu yatupwayo angani, majini na nchi kavu. Pia kizazi hiki kina mfumo wa kunasa mazungumzo na uwezo mkubwa wa kuingilia mazungumzo mengine.
“No, that is an outdated generation, we have invented new version, TI/333-A. As our good partners, Stanza will be the first country outside Pyongyang to have such technology.’’ (Hapana, kizazi hicho ni cha zamani, tunacho kipya chaTI/333-A, kwasababu Stanza ni marafiki zetu wa kihistoria, tunaweza kuwapa kama nchi ya kwanza kuwa na teknolojia hiyo baada yetu). Jenerali Uk In Mkuu wa majeshi ya ukombozi wa Korea Kaskazini alidakia.
Pius hakuamini kama kuna kizazi kingine cha rada chenye uwezo zaidi ya AN/SPF-71. Kizazi hiki alielezwa kina uwezo wa kunasa mawimbi ya rada nyingine mfano ya adui na kuharibu kabisa isifanye kazi tena na uwezo mkubwa wa kunasa mawimbi ya targets mbalimbali kwa wakati mmoja yaani Multi-targets sensors detection.
“Excuse me, when did this invention happen? Because the latest generation even in the USA, China and Russia is AN/SPF-71.” (Ningependa kujua ugunduzi huu ulifanywa lini kwa sababu hata Marekani, China na Urusi kizazi chao cha mwisho ni kile cha AN/SPF-71). Pius alionekana kushangaa na kutokuamini. Kwa uchunguzi wake alijua hakuna rada zenye teknolojia ya hali ya juu zaidi ya zile za kizazi cha AN/SPF-71ambazo ndio hutumiwa na mataifa makubwa matatu ya Marekani, China na Urusi.
“You have no idea about the military supremacy of North Korea my friend, it is the very reason why we have managed to keep our country safe over the past 50 years. We develop our technology in utmost secrecy, arguably undetected. TI/333-A is more powerful than any radar generation in this world so far. With it’s Wang-C3NKR series, you can put your three neighbor countries in range all at once. Ha ha ha”.
(Hujui chochote kuhusu nguvu za kijeshi za Korea Kaskazini Rafiki yangu na ndiyo maana tumeweza kuifanya nchi yetu kuwa salama kwa kipindi cha miaka 50 sasa. Tunaendeleza teknolojia yetu kwa usiri mkubwa, naweza kusema bila kufahamika na washindani wetu. TI/333-A ni kizazi cha rada chanye nguvu kuliko kizazi chochote katika ulimwengu huu. Kwa kutumia toleo lake moja tu la Wang-C3NKR unaweza ukaziweka nchi zako tatu majirani kwenye uzio wako zote kwa wakati mmoja. Hahaha’’. Jenerali Uk In alimjibu Pius kwa majivuno ya kicheko.
Pius aliendelea kuwapa maombi mengine na kutaka kujua marekebisho yatakuwaje na nani atakuwa anazisimamia. Walikubaliana kuwa wanajeshi kutoka Stanza wangeenda Korea kupata mafunzo lakini zaidi ya hayo marekebisho yote yatakuwa yakifanyika na wa Korea wenyewe.
Maongezi yaliendelea na sasa walijadiliana misaada ya kijeshi.
“Well, president Costa is intending to mordenize the military. We require technical trainings backed up with high mordenised military equipments”. (Sasa, Rais Costa anakusudia kuliimarisha jeshi. Katika eneo hili tunahitaji mafunzo ya kijeshi na vifaa vya kisasa kabisa), Joe alitoa maoni.
“Mr. Joe, there is a lot of highly advanced military equipments that we can offer, but there is one which we think is more interesting and ofcourse unmatched by enemies, nucler weapons”. (Joe, kuna vifaa vingi vya kisasa vya kijeshi tunavyoweza kuwapa lakini kuna hii moja tunafikiri ni nzuri zaidi ya yote, silaha za nyuklia), Waziri En alijibu kwa haraka. Maneno ‘silaha za nyuklia’ iliwafanya Joe na wenzake waangaliane.
“Mmmh mmmh (Joe alisafisha koo). Comrade En…I don’t think if at all, we can handle such equipments. We can talk about other military equipements, that do not include nuclear weapons”. (En, sidhani kama tupo kwenye nafasi nzuri ya kumiliki silaha za nyuklia. Tuongelee vifaa vingine ambavyo havihusishi matumizi ya nyuklia), Joe alijibu kwa haraka.
“Are you afraid of America and her allies?”, (Mnawahofia Marekani na washirika wake?) Jenerali Uk In aliuliza.
“No we are not, but our visit here is rather focused on acquiring a new friend without jeopardizing friendship with others. (Hapana, lakini lengo la safari yetu ni kupata Rafiki mpya bila kuathiri urafiki tulio nao na mataifa mengine), Pius alidakia.
“You can’t have a friendship with North Korea without jeopardizing some of your other friendships even if that doesn’t include acquiring nuclear weapons from us”. (Huwezi kuwa na urafiki na Korea Kaskazini bila kuathiri urafiki na baadhi ya marafiki zako wengine hata bila kupata silaha za nyuklia kutoka kwetu), Waziri En aliwasisitizia kina Joe.
“If we take your proposal of acquiring nuclear weapons, how will you support us against pressure from international community, particularly from America?” (Kama tukichukua wazo lenu la kuwa silaha za nyuklia kwenye taifa letu, mnatuhakikishia vipi usalama wetu wakati tutakapoanza kupata vitisho vya kimataifa hasa Marekani?) Habibu alivunja ukimya wake wa muda mrefu.
“We should be able to ensure that Stanza remain safe against aggression of the West and so-called international community. In fact China and Russia has been secretly looking for an African country that will be able to join the East in balancing the world’s power by acquiring nuclear weapons technology. All you need to do is to escalate your relationship with China and Russia and, potentially India so that you will still be able to remain afloat if they sanction you, but security-wise you will be fine”.
(Tutawalinda kikamilifu dhidi ya tishio lolote kwa Stanza kutoka kwa magharibi na kinachoitwa Jumuiya ya Kimataifa.Hata hivyo China na Urusi zimekuwa zikitafuta mshirika imara kutoka Afrika atakayekuwa na teknolojia ya Nyuklia ili nchi ziheshimiane duniani. Mnachotakiwa kufanya ni kuongeza mashirikiano ya kiuchumi baina yenu na China na Urusi na labda India pia ili msitetereke kutokana na vikwazo vya kiuchumi vitakavyowekwa, lakini kiusalama mtakuwa sawa kabisa), Waziri En alimjibu Habibu.

“If I am correct, you haven't provided nuclear weapons to any country so far, we will be the first country in the world to get such a technology from you. So, you claim that you will ensure our country is safe against any aggression. Let us remind you a few things; where is Abdul Qadeer Khan, a Pakistanian nuclear scientist who was exporting nuclear technology to your country, Libya and Iran including centrifuges and consequently caught by Americans in 2004?. What did you do to assist India to clear the 2016 UN allegations that the country through her Technology Institute was giving specialized training on Space Instrumentation to one of your students that lead to the launch of Unha-3 rocket in 2012?”
(Kama nipo sahihi, hamjawahi kutoa silaha zozote za nyuklia kwa nchi yoyote, sisi tutakuwa taifa la kwanza duniani kupata teknolojia hiyo kutoka kwenu. Hivyo kama mnataka kutuaminisha kuwa mnaweza kutulinda, mnaweza kutuambia yupo wapi Abdul Qadeer Khan, mwanasanyansi wa nyuklia wa Pakistan aliyekuwa akiingiza teknolojia ya nyuklia hapa kwenu, Libya na Iran na hatimaye kukamatwa na Marekani mwaka 2004? Pia, mlifanya nini kusaidia India kusafisha jina lao mbele ya Umoja wa Mataifa uliotuhumu kuwa kwa kutumia chuo chao cha teknolojia walitoa mafunzo kwa mmoja wa wanafunzi wenu yaliyomsaidia akaongoza timu ya kutengeneza roketi aina yaUnha-3 mwaka 2012?). Habibu alionekana kuwa na taarifa za kutosha na aliuliza maswali mfululizo. Joe alionekana kutabasamu kwa uwezo wa vijana alioambatana nao.

“About Abdul Khan, he is fine. If you are more interested to know what happened, we can talk to him right now. He was put under house arrest by the then General Perves Musharaf and to correct you, he was never touched by the Americans. Do you know why? I can assure you that you will be fine.
Abdul was a double-agent, used by both Americans and UK for the same job, we managed to have him work for us while the Americans believed he was their covert asset. When they learned that he is working for us too they reacted, but we managed them.
About India, after the UN report, what happened next? Have you heard anyone talking about it again? Mr Habibu come on, you are better than that”
(Kuhusu Abdul Khan yupo salama na unaweza kuongea nae hata sasa kama ukitaka. Alihifadhiwa sehemu salama na aliyekuwa Jenerali Perves Musharaf na kukusahihisha tu hakuguswa na Marekani. Unajua ni kwa nini? Sasa unaweza kuelewa ninaposema tutahakikisha mpo salama.
Abdul alikuwa akitumiwa pia na Wamarekani na Uingereza kwa kuwapa teknolojia ya nyuklia. Wakati huohuo alifanya kazi na sisi huku wao wakiamini kuwa ni mtu wao. Walipofahamu kuwa anafanya na sisi pia wakachukia na kutaka kumkamata, lakini tuliweza kuwadhibiti.
Kuhusu India, baada ya ile tariifa ya UN ni nini kilifuata? Kuna yeyote unaemsikia akiiongelea tena. Habibu vipi bwana?). Waziri En alijibu kwa majigambo.

“Why is it necessary that we agree with you on this matter of nuclear weapons?”, (Kwanini inaonekana ni muhimu sisi kukubaliana nanyi katika suala hili la silaha za nyuklia?), Joe alidakia baada ya ukimya kidogo.
“Because this is one of the terms and condition of our partnership, along with others that Comrade Kim will suggest after we present our today’s deliberations’’. (Kwasababu hili ni mojawapo ya vigezo na masharti ya msaada na ushirika wetu nanyi, pamoja na mambo mengine ambayo kiongozi wetu Kamaradi Kim atatuambia baada ya kujadiliana nae, nasi tutawaambia kwanini tunahitaji hili liwe miongoni mwa mahitaji yetu), Wazir En alimjibu Joe.

Joe aliwaangalia wenzake na ilionekana ni vyema wakapewa muda kulijadili hivyo wapumzike halafu wakutane tena baadae kuendelea na mazungumzo. Walikubaliana na kurudishwa kwenye chumba namba 315.
Walipofika kila mmoja alipumua kwa nguvu. Kila mmoja alikaa kimya kwa dakika chache. Mazungumzo yale yalikuwa nyeti na mazito yaliyohitaji hekima kubwa. Suala la kukubali silaha za nyuklia kwenye taifa la Stanza lilikuwa kubwa. Kwanza sio jambo walilotumwa na lingeleta mtikisiko usio kawaida. Kila mmoja hakuwa tayari kuliingiza taifa la Stanza kwenye mtafakuru na robo tatu ya dunia kwa sababu tu ya kumiliki silaha hizo.

Waliwaza hivi siku ikatokea Korea wakawasusa itakuwaje? Maswali mengi yalirindima kwenye vichwa vyao. Lakini waliwaza kama hilo ndilo hitaji namba moja la Korea Kaskazini ili waweze kuwapa msaada walioufuata sasa wao wakakataa watarudi kumwambia Rais Costa kuwa wameshindwa? Joe hakutaka kukubali kushindwa.
Baada ya ukimya wa kama dakika tano nzima kila mmoja akiwa anamtegea mwenzake aanze kuongea Joe alivunja ukimya. “Guys come closer”, (Jamaa, sogeeni karibu). Joe aliwaita wamsogelee.
************************************
Joe Anataka kuwashauri Nini Wenzake? Kwanini Korea Inasisitiza Silaha Za Nyuklia Kwa Stanza?Usiache Kufuatana Nami Kwenye Msimu Wa Pili wa Simulizi Hii.

Imeandikwa na Lello Mmassy.

The Book.
With Great Pleasure.
 
Back
Top Bottom