Simulizi:The President and I(Mimi Na Rais)

The President And I(Mimi Na Rais)- Sehemu Ya Kumi Na Nne

Stanza Mambo Ni Vululu Vululu

“Gideon, did you manage to get any intel from that grand traitor? (Gideon, umepata taarifa zozote za kiintelijensia kutoka msaliti mkuu?), Rais Sylvester Costa alimuuliza Gideon huku wakitembea kulekea ofisini kwake.

Rais Costa alikuwa kitoka kwenye kikao cha kuhabarishwa yanayojiri kwenye vyombo vya habari hususani suala la yeye kumiliki visiwa vya kitalii huko Ufilipino lilifikaje kwenye vyombo vya habari na ilikuwaje ikachapishwa bila watu wa usalama kujua na hivyo kuanza kuharibu taswira yake mbele ya wana Stanza. Alitaka kufahamu kiongozi wa upinzani, Julius Kibwe alifahamu vipi taarifa ambazo hakuwahi kumwambia hata msaidizi wake wa karibu, Bw. Gideon.

“Nimeongea kwa kina na Macha na amenipa ushirikiano wa kutosha, nadhani wazo langu lilikuwa sahihi kuwa watu kama hawa wanaona kuhojiwa na mtu kama Inspekta Majita ni kumdhalilisha. Ameniambia mpaka sasa ameteswa sana na ni kweli nimemkuta kwenye mateso makubwa.

Kimsingi Macha anasisitiza kuwa anataka kuzungumza na wewe, na ili kusema kile anachotaka anasisitiza kuwa ni vyema akaja hapa Ikulu au kule ofisi za Idara, na si nyumba za maficho za usalama.” Gideon alimjibu Rais Costa huku wakitembea wakiwa wamezungukwa na vijana wanne wa Idara ya Usalama.

“Gideon, kwa hiyo hilo ndilo alilokwambia? Sijaona cha maana hapo, anataka kuongea na mimi? Mimi huwa siongei na wasaliti, never!” Rais Costa alijibu kwa dharau.

“Mh. Rais, tumejiridhisha vipi kuwa taarifa alizotupatia Pius ni za hakika na kweli? Je, tuna hakika gani kuwa Macha au Joe hawakufanya jambo lile kwa sababu fulani? Kumbuka hawa ndio waliokusaidia kuzuia jaribio la wewe kupinduliwa na jeshi, leo wao kupanga kukupindua hainiingii akilini. Macha ameniarifu kuwa hatoniambia lolote, na wala hatosema chochote kwa maafisa wanaomtesa, alichosisitiza ni mimi nimuombee kwako ili uruhusu yeye kukuona.

Lakini pia kumbuka watu kama Macha ni watu wa usalama waliobobea katika fani yao, wapo tayari kufa kama usipofikiana nao makubaliano fulani. Macha yupo tayari kufa. Ni aidha ukubali kuonana nae ili upate kujua mambo mengine mengi ama umwache auwawe na baadae ujikute unapinduliwa na masalia yao maana mpaka sasa Idara imeshindwa kupata mawasiliano ya Macha na Joe kwa namna yoyote ile. Ipo gizani”, Gideon aliendelea kushauri kwa kumjaza upepo wa uoga Rais Costa.

Ushauri ule ulionekana kumwingia Rais Costa kidogo, alipiga hatua kama kumi hivi akiwa kimya kisha…

“Sawa Gideon nitaongea na Sabinasi aandae utaratibu nionane na Macha, Rais alimjibu Gideon huku akiwa anaingia nae ofisini kwake.

“Sawa mkuu lakini pia nashauri Inspekta Majita aache mara moja kumtesa Macha, yafaa siku unayokutana naye awe hana maumivu ili muongee vizuri lakini pia isilete picha mbaya kwa watu watakaomwona”, Gideon alishauri.

“Sawa, na hilo nitamwambia Sabinasi. Halafu Gidi, kuna suala hili la Marekani kututishia juu ya hali ya demokrasia na utawala bora nchini kwetu. Rais Chris wa Marekani ametuma waraka mrefu wenye lugha ya mabavu na kukemea. Bado nafikiria namna bora ya kumjibu. Uhusiano na Marekani ukiingia dosari zaidi ya ulivyoingia sasa inaweza ikaleta shida kubwa”. Rais Costa alimkubalia Gideon ushauri wake lakini pia akamuuliza Gideon juu ya barua aliyoipokea kutoka Ikulu ya Marekani Washington.

Barua ile iliyotoka kwa Rais Chriss Donald ilikuwa imeainisha masuala kadhaa ya yanayotokea Stanza kubwa likiwa hali ya demokrasia na utawala bora iliyoonekana kudorora kwa kasi katika kipindi kifupi. Rais Costa hakujua ajibu nini kwani huwa ni mtu wa hasira na asiyependa kupewa amri na yeyote, bali afanye anavyotaka yeye.

“Nipe nikaisome kwa utulivu kisha tutaona tunaijibu vipi Mh. Rais”. Gideon alijibu huku akisogea kuichukua ile barua.

“Sio tutaijibu vipi, wewe isome uijibu uje kunionyesha ulichoandika. Sina muda wa kupoteza kujadiliana na mataifa ya magharibi yanayokusidia kuingilia uhuru wetu. Stanza ni taifa huru’’. Rais Costa alijibu kwa hasira huku akiirusha ile barua mezani ili Gideon aichukue.

Gideon aliichukua ile barua na kutoka haraka. Alikuwa akitembea kwenye korido ile inayotoka ofisi ya Rais pale Ikulu upande wa Magharibu mwa jengo lile akielekea upande wa Kaskazini-Magharibi zilipo ofisi zake.

Tabasamu lilijaa moyoni kwasababu kuu moja, alihakikisha mateso kwa Stanley Macha yanasitishwa mara moja. Hakujua Macha anakuja kuongea nini na Rais lakini alijua Macha ni mtu mwerevu na atajua namna ya kufanya mbeleni.

“One step at a time”, Gideon alijisemea mwenyewe huku akitabasamu sana na kuingia ofisini kwake.

Wakati hayo yakiendelea, tayari familia za Joe na Macha zilishaanza kuingiwa na hofu pamoja na kufahamu asili ya kazi za wapendwa wao. Mke wa Joe ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Benki Ya Kilimo Stanza alianza kupata wasiwasi kwasababu ilikuwa kimepita kipindi kirefu tangu awasiliane na Joe, lakini pia wakati Joe anaondoka alimwarifu kuwa wasingechukua Zaidi ya wiki mbili kuwa wamerudi nyumbani.

Sasa ilikuwa zimetimia wiki tatu tangu Joe na wenzake kusafiri kwenda Korea Kaskazini kufikisha ujumbe wa Rais Costa kwa Rais Kim.

Mke wa Joe alifikiri kuwa pengine mume wake ameingia katika mgogoro na Korea na wao wakamshikilia kama ambavyo wamewashikilia watu wa mataifa mengi ambao walivunja sheria ndani ya nchi yao.

Wakati huohuo, Mke wa Stanley Macha hakuzoea mume wake asiwasiliane na familia kwa kipindi kirefu cha Zaidi ya wiki moja. Pamoja na kufahamu asili ya kazi ya mume wake kuwa anaweza akawa anasimamia misheni maalumu za usalama wa nchi, alipatwa na wasiwasi hasa kutokana na simu ya Macha kutopatikana na jumbe anazotuma kutojibiwa.

Familia hizi zote mbili zilianza kuingiwa na wasiwasi sana.
*********************************

Kikao cha taarifa zinazoendelea kwenye vyombo vya habari kilikuwa kichungu siku hiyo. Rais aling’aka kama mbogo akiwatuhumu vijana wake kuruhusu taarifa kama ile kumfikia Kibwe na hatimaye kuchwapwa wao wakiwepo.

Aliwashangaa walikuwa wapi mpaka gazeti linasambaa mitaani. Aliwaambia alishawaagiza kweye kila chombo muhimu cha habari iwe gazeti, kituo cha luninga na radio kuwe na mtu angalau mmoja alieajiriwa mule atakayekuwa anawapa taarifa za kishushushu ya kila kilichochapwa ili kuzuia kuharibu taswira yake ama ya serikali ili wajue namna ya kulizima suala hilo haraka iwezekanavyo.

Pamoja na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa lakini bado kuna vyombo vya Habari walishindwa kupenyeza watu wao kwasababu tu watu hawa huwa hawapenyezwi kwa lazima, bali hupitishwa katika mchakato wa kawaida wa uajiri ili wasitambulike na yeyote. Katika utawala wa Rais Costa, vyombo vya Habari vilikuwa matatani wakati wote. Vingi vilifungiwa, wahariri kutishiwa na wengine wakisimamishwa na uongozi wa vyombo vyao kwa amri kutoka Ikulu bila kukiuka miiko yoyote ya uandishi wa Habari.

Lakini pia waandishi walitekwa na kupotezwa katika mazingira ya ajabu. Lengo kuu likiwa kuwazima wasichape habari za masuala mbalimbali yanayofanywa na serikali lakini pia kuwatisha waandishi wengine ili kuwaondoa katika kujikita kuandika Habari za serikali na kujikita katika masuala mengine ambayo ‘yasingechafua taswira ya serikali’. Vyombo vya Habari chini ya Rais Costa vililazimika kujifanyia ukaguzi na udhibiti wa kile wanachokichapisha au kwa kimombo inaitwa ‘’self-censorship’’ ili kuepuka dhahma ya serikali ya Rais Costa. Tasnia ya Habari haikuwa inayowavutia wanafunzi kusoma tena kama ilivyokuwa hapo awali.

Rais Costa aliendelea kuwakoromea vijana wake kwa kushindwa kuzuia habari ile pamoja na kwamba mazingira tayari yalishatengenezwa ya kuvitia hofu vyombo vya habari. Aliwaambia kuwa alishatoa agizo hilo na kuwa watu wapenyezwe kwenye kila chombo na wangelipwa kwa utaratibu maalumu, alishangaa ni kwanini mpaka muda huo agizo hilo halijatekelezwa mpaka Julius Kibwe anafanikiwa kumchafua namna ile.

Kwenye kikao kile hakuna aliyethubutu kuongea, kila mtu alikuwa kimya. Rais Costa alitoa agizo kuwa Julius Kibwe asiguswe maana kutamfanya azidi kuongea zaidi hivyo alitaka apuuzwe kwanza, lakini muhariri wa STANZA TODAY gazeti lililochapisha habari ile aitwe chemba aminywe na apewe onyo kali kutoendelea na habari ile.
****************************************

“Sabinasi, nimepata ushauri kutoka kwa Gideon kuwa tusitishe mateso anayopata Macha ili kumfanya azungumze na kuwa yupo tayari kuzungumza nikiwa nae, hivyo nakuagiza haraka Macha atolewe kule anaposhikiliwa na ahamishiwe nyumba salama, nitaonana nae huko siku nitakayoamua baadae kidogo.” Alikuwa ni Rais Costa akitoa maagizo kwa Sabinas, mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Stanza aliyechukua nafasi ya Stanley Macha.

“Lakini mkuu Macha yupo kwenye hatua ya mwisho ya uvumilivu, ata-break muda si mrefu. Tumuache Inspekta Majita amalizie kazi aliyokwishaianza. Akija kwako atakuanzishia siasa”, Sabinasi alikazia mateso kwa Macha yaendelee.

“Sabinas, do as I say. No questions!” Rasi Costa alionekana kukwazwa na ushauri wa Sabinas. Nani ana uwezo wa kupindua ushauri wa Gideon bwana? Hakuna mtu Rais Costa alikuwa akimwamini wakati ule kama Gideon.
**************************************

“Mh. Rais”, Alikuwa ni kijana wa Usalama akifungua mlango wa ofisi ya Rais Costa pale Ikulu ili kumpisha mtu aingie ndani.

“Sara, karibu nyumbani”. Rais Costa aliyekuwa ameanza kusoma makabrasha yaliyopangwa pale mezani kwake alinyanyua macho na kuona aliyeingia ni mke wake Sara.

“Baba Brian kuna nini?”, Sara mke wa Rais Costa aliuliza katika hali ya taharuki. Aliuliza kwa kumwita Rais Costa jina la mtoto wao anaeitwa Brian Sylvester Costa aliyepo nchini Denmark kimasomo.

“Let’s go home and have some conversation”, (Twende nyumbani tukaongee). Rais Costa alimjibu mke wake huku akisimama na kutoka nae kuelekea upande wa Mashariki kwenye makazi ya Rais pale Ikulu.

Wakiwa wanatoka wanakatiza korido ya mwisho ili wauache upande wa Magharibi kwenye kona ya mwisho walikutana na Gideon akiwa anatoka upande wa ofisi yake ni kama alikuwa anelekea ofisini kwa Rais Costa.

“Shemeji habari. Canada wanasemaje?”, Gideon alimsalimia Sara kwa bashasha.

“Salama tu shemeji. Canada wazima, nadhani next time nitabebana na Alicia”. Sara alimjibu Gideon kwa ucheshi. Alicia ni mke wa Gideon.

“Atafurahi sana….Mh. Rais ninatoka kidogo naelekea wizara ya Mambo ya Nje kuna jambo nikajadiliane na Katibu Mkuu kule”, Gideon alimjibu Sara na kisha kutoa taarifa kwa Rais Costa.

“Sawa si ndio kazi zako bwana. Nimeshampa maelekezo Sabinasi juu ya Macha, lakini na wewe pia usiache kushughulikia ile barua ya Rais Chriss” Rais Costa alisisitiza.

“Definitely Sir, actually ni moja kati ya agenda yangu ya kwenda wizarani” Gideon alijibu kwa nidhamu.

“Please proceed”, Rais Costa alimjibu Gideon na kuendelea na safari ya kuelekea kwenye kazi yao.

Gideon alipomuona Sara alikumbuka kuwa Sara hakurudi kwasababu kongamano lililompeleka Canada limekwisha bali ni kwa sababu Rais Costa aliagiza arudishwe baada ya kuhusishwa na mpango wa kumpindua Rais. Alianza kuwaza sana juu ya hilo suala.

Rais Costa na Sara walifika kwenye makazi yao na waliingia moja kwa moja mpaka Chumbani.

“Sara wewe ni mke wangu ninaomba uniambie lipi ninalolifanya ambalo huwa ninakukosea”, Rais Costa alianza kuuliza kwa utaratibu.

“Baba Brian mimi sikuelewi, nenda moja kwa moja kwenye lengo. Unanikosea mengi, ninafahamu umalaya unaofanya na changudoa wako Ketina, unadhani silijui lakini najua kila kinachoendelea na huyo hawara wako. Sasa ukitaka niorodheshe yote hatutafikia muafaka”. Sara alijibu kwa hasira baada ya kuona mume wake anazungumza kwa mafumbo bila uwazi.

Kitendo cha Sara kumtaja Ketina, kimada wake kilimchanganya sana Rais Costa. Yeye Rais Costa akijua uhusiano wake na Ketina ni siri kubwa alistaajabu kugundua kuwa mke wake anajua na hakuwahi kumuuliza hata siku moja.

Kitendo cha Sara kumtaja Ketina kama tungekuwa kwenye medani zetu za mijadala kinzani tungekiita opponential confusion, yaani unamvuruga mpinzani wako wa mada hata kwa kuibua suala ambalo haliendani moja kwa moja na kile kilichopo mezani. Sara hakuwa na lengo hilo, isipokuwa kwa Rais Costa hakika ilikuwa ni pigo la kwanza katika mjadala kwasababu alikosa nguvu ya kuendelea na hoja. Alianza kuamini kwamba kila siri anayofanya kuna watu wanavujisha.

“Sara suala la Ketina tuliache kwanza, taarifa za kiintelijensia tulizopokea ni kuwa unashirikiana na Macha na Joe kutaka kunitoa madarakani. Hivi kweli mama Brian unaweza kunifanyia kitendo kama hicho?”. Rais Costa aliuliza kwa upole uliopitiliza.

“Costa hebu tusichanganye hapa saa hizi, niambie ulichonirudishia Stanza kabla ya kongamano kuisha maana naona unazidi kunipandisha hasira kwa mambo yasiyokuwa na kichwa wala miguu. Hebu kuwa serious, stop acting like a little boy. Huyo Ketina umeyataka mwenyewe, sikutaka kukuuliza mimi. Umenilazimisha niseme kama uliwahi kunikosea na nimekwambia sasa unaniambia nini tena”. Sara mke wa Rais Costa aliongea mfululizo. Si kawaida yake kuongea kwa namna hiyo lakini ilimbidi.

“Suala ni kuwa kuna taarifa zisizoshaka kuwa unashiriki kwenye mpango wa kutaka kunipindua ukitumiwa na Macha na Joe.” Rais Costa alihoji, safari hii akiwa amejikaza kidogo.

“Kukupindua? Mimi nikupindue wewe? Yani kama kukupindua ningeanza kupindua ndoa yangu siku niliyothibitisha kuwa unatoka na Ketina. Sikufanya lolote leo unaniambia nataka nikupindua kutoka kwenye nafasi yako ya Urais? Hivi kama mke aweza kumpindua Rais aliyepo madarakani, sasa huyo atakuwa Rais au Rahabu?”. Sara alijibu kwa dharau.

Walianza kuzozana kila mmoja akimtupia maneno mwenzake. Rais Costa akitaka aambiwe ukweli huku Sara akimshangaa Rais Costa na kutoonesha hamuelewi hata anaongea nini. Rais Costa aliishia kubaki njiapanda kwa kutokuwa na uhakika na taarifa za mkewe kuhusika na jaribio la mapinduzi.

Alitoka kule chumbani na kuelekea sehemu anayopenda kufanyia mazoezi na kujifungia na kufikiri mambo mengi. Kwanza, alianza kufikiria kama ni kweli mkewe hahusiki ama la, lakini cha pili kuhusu mkewe kujua mahusiano yake na Ketina ni jambo lililomshtua.

Gideon alipotoka pale hakuwa akielekea Wizara ya Mambo ya Nje kama alivyomuaga Rais Costa bali alikuwa akielekea mgahawa wa Goldern Spoon kuonana na Meja Kairuki Byabato kwa malekezo ya Macha alipomtembelea. Alihitajika kuonana nae ili mpe ile code aliyopewa ya ‘Sienta-go’. Hakuielewa ina maana gani lakini alijua watu wa usalama wana namna yao ya kuwasiliana na angeelewa.

Aliwasili pale mgahawani na alikuwa amewahi kidogo, hivyo alikaa ili kumsubiri. Meja Byabato alimtaarifu kuwa yupo karibu kufika.

Akiwa pale, mawazo ya uhusika wa Sara kwenye sakata la kutaka kumpindua Rais Costa lilimjia kwa mara nyingine na alipenda kujua ni kwa vipi. Aliona bora aingie kwenye game ya Clash royale ili awasiliane na Joe.

“Che, nipo hapa Goldern Spoon namsubiri Meja Byabato kuna code nimepewa nimpe na Tiger. Ila wakati natoka Ikulu nilipishana na Rais akiwa na mkewe Sara ambaye mlimtaja kuwa anahusika na hii misheni. Hili limekaaje? Maana sasa mnatakiwa mniweke kwenye picha kamili nijue nachezaje”. Gideon anaetumia jina la Sadam Hussein alimwandikia ujumbe Joe anayetumia jina la Che Guevara ama Che kama walivyozoea kuitana. Tiger ni jina la Macha kwenye game ile.

Ujumbe ulimfikia Joe aliekuwa akikatiza mitaa ya Beijing akiambatana na Habibu wakielekea mahali ambapo Habibu hakuwa anapafahamu mpaka wakati huo. Ujumbe ule ulimfanya Joe asimame mahali ili kuusoma. Ilikuwa ni muhimu sana Joe kusoma na kujibu kila ujumbe kwa wakati maana kuchelewa hata kidogo kunaweza kuharibu misheni nzima au hata kuhatarisha maisha yake.

“Sadam kwanza ulifanikiwa kuhakikisha Tiger anatoka kule detention?”, Joe aliandika.

“Mimi tena, ila sasa sijajua ataongea nini?” Gideon alijibu kwa kujitapa.

“Cha kuongea hicho kisikusumbue, mwachie yeye anajua”, Joe alijibu.

“Sara vipi anahusikaje?” Gideon aliuliza.

“Sara tulimtaja kwa lengo maalumu, hahusiki. Kwa kawaida kwenye misheni huwa anawekwa mtu mmoja ambaye atapoteza uelekeo wa kiuchunguzi na kuleta taharuki ikitokea mambo hayajaenda kama yalivyopangwa, huyo huitwa disturbing agent. Kimsingi Sara tunamuhitaji sana baadaye ila hatukuwa tunajua namna ya kumwingia kwahiyo tulikubaliana na Macha kumuimplicate kwenye kila maongezi na mawasiliano yetu ili aonekane anashiriki kama siku tukishtukiwa kama hivi.

Lengo ni kuhakikisha Rais Costa anachanganyikiwa na kushindwa kuunganisha nukta. Lakini sasa ndiyo wakati wewe wa kufanya hatua ya pili”, Joe alimalizia kuandika ujumbe na kuutuma.

“Hatua ya pili ipi? Ya kwanza niliifanya lini?” Gideon aliuliza.

“Unakumbuka Macha alipokwambia umtonye Sara juu ya Rais Costa kuwa na mahusiano na Ketina na kuwa umsihi asimwambie mumewe chochote?”, Joe aliuliza.

“Ndio, kwani na wewe ulikuwa unajua? Mlipanga mniframe?” Gideon alihoji.

“Ndio, hakuna kinachotokea kwa Bahati Mbaya Gideon. Sasa ile ilikuwa ni hatua ya kwanza. Sasa utatekeleza hatua ya pili. Ukirudi Ikulu hakikisha unaenda kumdodosa Sara ni kwanini amerudi mapema kabla ya Kongamano kuisha. Najua wewe ni rafiki yako na mnaelewana atakwambia shutuma atakazokuwa amepewa na mumewe.

Akikueleza wewe onyesha masikitiko yako kisha mwambie kuwa umepata fununu kuwa Rais ameamua kumzushia ili apate sababu ya kumpa talaka na amuoe rasmi Ketina. Ukimaliza kumwambia hivyo utajidai unataka kufuatilia kama chokochoko hizo za kupinduliwa ni kweli au vinginevyo na kisha utaona atakavyopokea suala hilo.

Jinsi atakavyopokea utatutaarifu ikiwa ataonekana kufurahia mumewe kupinduliwa au la. Kama ataonyesha kufurahia, taratibu tutaendelea hatua ya tatu ya kumfanya awe sehemu ya misheni kwani atakuwa ana hasira ya mumewe kutaka kumwacha kwa siri hivyo atakuwa anataka kulipiza kisasi.

Akionyesha kutokuunga mkono utamrudia mara nyingine na kumwambia hakuna mpango kama huo na utaachana nae.” Gideo alimalizia.

“Che, huu mpango mliupanga lini?”. Gideon alionekana kutoamini mpango ule ulivyosukwa.

“Sadam, hatuna muda wa kujadili hayo kwa sasa”, Joe alijibu.

“Sasa akimgusia mumewe si litakuwa balaa Joe?” Gideon alionyesha mashaka yake.

“Huwezi kushindwa kujitetea, kwanza Costa hajui kama unajua mahusiano yake na Ketina. Wewe utamkana na utamwambia wazi kuwa asipoangalia atawamaliza marafiki zake wote kwa kusikiliza maneno ya watu. Ataogopa, wewe ni mtu wa karibu wa pekee uliyebaki nae, hawezi kukutupa.” Joe alimuhakikishia Gideon.

“Sawa, naona Meja Byabato anaingia hapa nitakurudia baadae. Stay safe”. Gideon alimalizia na kutoka kwenye ile game.

“Meja, heshima yako Mkuu”. Gideon alimsalimia Meja Kairuki Byabato alipowasili eneo alilokuwa amekaa.

Meja Byabato alikuwa ni mwanajeshi katika jeshi la Stanza. Alikuwa kikosi cha anga. Akiwa ni mrefu wa futi 6, ilikuwa ni rahisi kuona utofauti wake na binadamu mwingine yoyote aliyesimama au hata kukaa karibu nae. Mikono yake ilikuwa mikubwa na iliyojaa kwasababu ya mazoezi makali ya kunyanyua uzito na muda mwingi alipendelea kuvalia makombati ya jeshi na sio nguo za kiafisa.

Alikuwa ni mmoja wa makomandoo katika jeshi la Stanza. Aliongea kwa kuunguruma na akitabasamu hutabasamu kwa shavu moja bila kuonyesha meno. Alipendelea kuvaa miwani mieusi inayoziba macho kabisa.

Gideon yeye kwa sababu ya kucheza sana Rugby nae alikuwa ni mrefu na mwenye kifua kikubwa. Gideon alikuwa mweupe wakati Meja Byabato alikuwa mweusi hadi weusi wenzake wakiwa wanamtania kuwa ni mweusi kama makaa ya mawe yanayozalishwa kwenye migodi ya Liganga na Mchuchuma huko Tanzania. Kuna wakati baadhi ya Marafiki zake walimwita kwa majina ya utani ‘’Mchuchuma au Liganga’’ na wala hakukasirika.

“Gideon”, Meja Byabato alimsalimia Gideon huku wakishikana mikono yote miwili na kutingishana.

Kwa namna walivyotingishana na jinsi miili yao ilivyo kama huna afya vizuri basi ungeweza kudondoka. Lakini wao waliwezana.

“Habari za Ikulu”, Meja alianza kwa kumuuliza Gideon walipoketi kwenye viti vyao.

“Nchi ipo salama chini yenu Meja”, Gideon alijibu kidiplomasia.

“Tell me Gidi what is it”, Meja Byabato alifungua maongezi.

“Nimetumwa na Stanley Macha nikuletee ujumbe, amenipa codes nikuletee”, Gideon alianza kumwambia Meja Byabato.

“Codes gani Gidi, na yeye yupo wapi? Meja Byabato alihoji.

“Sienta-go” Gideon alimtamkia Meja Byabato.

“What? Unafahamu mahali aliposhikiliwa? Should I trust you?” Meja Byabato alionekana kushangaa sana.

“Kwani mimi nimekwambia ameshikiliwa?” Gideon aliuliza kwa mshangao.

“Gideon, hapo Macha ameniambia mambo mengi. Labda nikuulize unafahamu nini juu ya huu mpango?” Meja alihoji.

“Mpango gani?” Gideon alijitia haelewi.

“Gidi we don’t have time to play. Save some sh*t please”, Meja Byabato aliunguruma.

“Ninafahamu vyote na ndio maana nimeweza kukufikishia taarifa hii”, Gideon alijibu.

“Sawa. Tutawasiliana acha nikafanye alichoniagiza”. Meja Byabato alijibu huku akinyanyuka pale kwenye kiti.

“Ukafanye nini Meja?” Gideon aliuliza.

“Gidi umeshatimiza majukumu yako, umefikisha kijiti, acha mimi nikikimbize. Go go and keep pampering that man, Meja alijibu huku akiingia kwenye gari lake aina ya Ford Ranger.

Gideon alibaki mdomo wazi. Aligundua kuwa suala lile ni zaidi ya yeye alivyolipa uzito, wazungu wanasema ni covert operation, yaani mpango wa siri kuu. Kila mtu ana kipande chake tena kisichofanana na wa mwenzake lakini vipande vyote vikiunda kitu kimoja.

Kumtoa Rais madarakani katika hali ya utulivu bila raia kuwa na taarifa wala kusababisha sintofahamu ilihitajika akili kubwa na mkakati wa muda mrefu uliosukwa kitaalamu na kuhusisha watu wengi tofauti na alivyowaza Gideon.

Haraka Gideon alitoka pale na kuelekea Wizara ya Mambo ya Nje kuonana na Katibu Mkuu. Hakuwa na hata la maana la kuongea nae lakini alimjua Rais Costa hachelewi kudodosa kama kweli alifika wizarani ama la.

Rais Costa ana akili yenye kuwa na wasiwasi na kila suala, muda wote hujihisi hayupo salama. Gideon alijua kula na na kipofu, alimjua bosi wake na alijua namna ya kwenda nae.

Gideon alionana na Katibu wa Kudumu wa Wizara na kumpa taarifa ya barua ya Rais wa Marekani ili pia Wizara yenye jukumu la mahusiano ya kimataifa ifahamu kinachoendelea kati ya Marekani na Stanza, lakini pia kwa ushauri wa jinsi ya kuenenda katika suala lile ili hata huko mbeleni wakipokea nchi isiwe katika misukosuko. Gideon alianza kuona picha kubwa zaidi.
***********************************

“Mh. Rais Luteni Jenerali Pius Kihaka amewasili”, alikuwa ni mmoja wa wasaidizi wa Rais akimtaarifu Costa juu ya kuwasili kwa Pius akitokea nchini China.

Ilikuwa ni jioni mishale ya saa kumi. Siku nzima ya siku hiyo tangu asubuhi baada ya Rais Costa kutupiana maneno na mkewe Sara hakutoka tena kwenye makazi yake kurudi ofisini.

“Oh, mleteni kijana wangu huku nyumbani. Ameambatana na nani?” Rais Costa aliuliza.

“Yupo na Sabinasi Paulo na Jenerali Ernest Nduta”, Yule kijana alijibu.

“Sawa waje huku mtafute na Gideon”, Rais Costa alijibu huku akielekea eneo lililoitwa Presidential Lounge. Ni eneo dogo lililojengwa kwa ajili ya Rais kupumzika na wageni wake maalumu kwenye makazi yake.

Ni eneo zuri dogo kiasi lililopangwa kiustadi na kuwekwa katika hali ya kustarehesha likiwa mbele ya bustani nzuri ya maua na mandhari ya kupendeza pale kwenye viunga vya Ikulu. Mbele yake walizunguka ndege aina ya tausi na aina mbalimbali za wanyama walioletwa Ikulu ili kuboresha mandhari.

“Hongera sana Luteni. Hakika umefanya jambo la kishujaa”. Gideon alimwambia Pius wakati wakiwa wote wanaelekea kuonana na Rais Costa. Gideon ndiyo alikuwa ameingia tu viunga vya Ikulu akitokea kwenye harakati zake.

“Sikuweza kukubali kuona ujinga Joe aliotaka kuufanya”, Pius alijibu kishujaa.

Wote walipiga hatua wakiwa waasindikizwa na vijana wa Usalama na walifika kwenye Presidential Lounge na kupokelewa na Rais Costa.

“What a courageous and brilliant young man!” Rais Costa alinyanyuka pale alipokuwa ameketi na kumlaki Pius kwa kumbatio kubwa. Wengine walikuwa wamesimama kando wakiwa wanatabasamu ishara ya kuungana na Rais kihisia katika kumlaki Pius.

Waliketi na Pius alianza kuwapa muhtasari wa safari nzima. Aliwaeleza namna walivyopokelewa kwa heshima nchini Korea Kaskazini na majadiliano yalivyokwenda.

Giden wakati wote alikuwa akisikiliza kwa makini sana mrejesho ule. Alikuwa akipata maswali mengi kichwani kwa kila hatua Pius aliyokuwa akieleza. Alikuwa anajitajidi kuunganisha nukta lakini zilikuwa zinakataa. Wengine wote walikuwa wakionekana kumwamini na kumuitikia Pius kwa kila hatua.

Katika maongezi yale Pius hakuacha kuelezea namna Joe alivyokuwa akipata taarifa fulani kwa njia isiyo ya kawaida na hivyo kubadili muelekeo wa jambo au kuondoka eneo walilopo kwa haraka.

“Lazima kuna watu walikuwa wakimpa taarifa waliopo karibu na wewe Mh. Rais”, Sabinas alidakia.

“Ni Macha, ndiyo maana nasita sana kuonana nae. Nilikusudia atumbukizwe kwenye pipa la tindikali ayeyukie humo. Sitaki hata kumuona”, Rais Costa alionekana kutibuliwa tena ghadhabu.

“Hapana Mh. Rais mimi nawaza tofauti kidogo, mimi nawaza kuwa bado ipo haja ya kuonana na Macha umsikilize. Unajua Macha alikuwa mtu mkubwa sana kwenye Idara ni vema akatuambia alikuwa akiwatumia vijana wake nani na nani ili kutekeleza azma yake hii maana lazima alikuwa na vijana.

Sasa kumteketeza Macha na kuwaacha hawa vijana ni sawa na kuteketeza mzinga wa nyuki wakati nyuki wenyewe wakiwepo, ukifanya hivyo uwe na uhakika kuwa hawa vijana wanakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutumiwa na mtu mwingine au wenyewe kupanga uasi”, Gideon alimalizia.

“Anyway, nitaonana na Macha”, Rais Costa alijibu.

Hakika kulikuwa na mpambano mkali kati ya Sabinasi na Gideon. Wakati Sabinas akitaka Macha amalizwe ili asipate nafasi ya kujitetea na yeye asimikwe rasmi kuwa mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Stanza, yeye Gideon alikuwa anapambana kumwokoa mmisheni mwenzake. Kila mtu akivutia upande wake kwa ustadi mkubwa.

Gideon alizidi kuona umuhimu wa yeye kutobanduka viunga vya ikulu na kujua kila anaemkaribia Rais anataka kumwambia nini maana asipokuwepo kidogo tu aweza kuta mambo yameharibika.

“Pius, umeongelea suala la silaha za kinyuklia hili mliafiki vipi?” Jenerali Ernest Ndutta alihoji.

“Suala hili kwa ukweli nililipinga sana”, Pius alianza kujitoa kwenye hilo sakata.

Alianza kujitoa baada ya kuona sura ya Rais Costa imebadilika aliposikia suala la silaha za kinyuklia kuzalishwa Stanza. Yeye ndiye haswa alieshauri wenzake walipokuwa Korea Kaskazini kuwa wakubaliane na sharti la silaha za nyuklia lakini leo imemlazimu kukaa mbali nalo ili kuendelea kuibeba sifa ya ushujaa wake ambayo amekwishavikwa.

“Aliyesababisha na kukubaliana na Korea ni Joe, kwahiyo ni lazima tuone tunafanyaje kwa sababu Korea wameliweka hili kama sharti la muhimu sana”, Pius alimalizia.

“I see, na sasa Korea wapo tu kimya inanipa mashaka nadhani wanaweza kudhani sisi tuna dharau. Ha ha ha!”, Rais Costa aliongea kwa kucheka.

Walizungumza mengi na kisha Rais Costa aliwaomba wakutane kesho yake ili waweze kuzungumza na Rais Kim. Alimwagiza Gideon aandae majibu wawaambie nini Korea lakini alisisitiza masuala ya silaha za nyuklia hayawezi kuja Stanza, hataki kusikia. Waliondoka lakini Gideon alibaki kidogo.

“Gidi, unamuonaje Luteni Pius?”. Rais Costa alimuuliza Gideon huku akinywa juisi ya Embe iliyokuwa imemiminwa kwenye glasi pale walipoketi.

“Ninamwonaje kivipi Mkuu?”, Gideon aliuliza kwanza ili ajue ajibu vipi.

“Jenerali Ernest Nduta muda wake wa utumishi unakwisha nilitaka nimuongezee miaka miwili ili Pius akomae kidogo lakini ni kama namuona anafaa sana kwasasa kushika nafasi hiyo ya Ukuu wa Majeshi”, Rais Costa alimweleza Gideon.

Katika vitu vilivyompasua moyo na kumuudhi Gideon basi suala hilo ni namba moja. Aliwaza yani huyu huyu Pius ndio anakuwa mkuu wa majeshi? Huyu huyu msaliti mkubwa. Aliona jinsi misheni inavyozidi kuwa ngumu maana Pius anajua mambo mengi na yupo haraka sana kung’amua mambo. Alikosa ajibu nini, alikasirika sana moyoni.

“Mkuu, nilikuwa nawaza bado Pius apewe muda akomae”, Gideon alishauri.

“Akomae kitu gani Gideon?” Rais Costa alionekana kuuliza kwa mshangao.

Gideon kwa mara ya kwanza alibaki kimya hakujua atetee vipi kuzuia Pius kupewa ukuu wa majeshi.

“Sikiliza Gidi, Jenerali Nduta amelitumikia taifa hili kwa weledi sana na sasa amechoka, nimwache akapumzike. Kuna jambo linanisukuma kusema Nduta akapumzike nalo ni kitendo cha Pius kutaka kuwasiliana na yeye na kushindwa. Yani kama Macha aliweza kuzuia mawasiliano yasinifikie bila Jeshi kujua, hii ni hatari. Isingekuwa ujanja wa Pius tusingejua na labda Macha angetumia njia zozote kumnyamazisha Pius huko huko China”, Rais Costa alikazia.

“Lakini unachosema ni kweli Mkuu, sikufikiria hilo. Umefikiria kwa kiwango kikubwa sana Mh Rais, naungana na wewe. Pius mpe nafasi”, Gideon ilibidi aungane na Rais Costa bila kupenda.

Walikubaliana kuwa watamtaarifu Jenerali Nduta maamuzi hayo na aanze kumkabidhi Pius kijiti kabla ya yeye kuweka wazi kwa taifa.

Gideon alimwaga Rais na kuondoka akiwa amekata tamaa kwa mara nyingine kutokana na kubadilika kwa hali ya mambo ghafla, kwa kimombo ingeitwa ‘’twist of events’’
*******************************************

Meja Kairuki Byabato aliendsha gari lake kwa aksi ya ajabu sana. Alikuwa akiwaza mengi kichwani na aliona kama imekuwa mapema sana kwa Macha kukamatwa. Meja alikuwa ni miongoni mwa wale wanajeshi waliokuwa kwenye mpango wa mwanzo wa kutaka kumpindua Rais Costa, mpango uliozimwa na Macha na Joe.

Katika uchunguzi wa Macha alibainisha baadhi ya wakuu wa vikosi waliokuwa katika mpango ule na alihakikisha wote wamestaafishwa na kutolewa kwenye jeshi isipokuwa Meja hakumjua kwa haraka kwa wakati ule.

Ulipita kama mwaka mmoja hivi ndipo Stanley Macha alipokuja kugundua na kupata uthibitisho pasi shaka kuwa Meja Byabato alikuwa ni mmoja wao. Macha alistaajabu umaridadi wa kuficha taarifa aliokuwa nao Meja Byabato kufikia kiasi cha yeye kutojulikana kabisa kama alikuwa ni Sehemu ya misheni na wanajeshi wenzake.

Ni hapo Macha alipoamua kumfata na kuongea nae. Alimweleza kinaga ubaga kuwa anao uthibitisho pasi shaka wa uhusika wake katika jaribio la kutaka kumpindua Rais Costa lakini hatamshtaki kwa Rais.

Alimtaka Meja amweleze ni kwa nini haswa walikuwa wanampango ule wakati ule. Ni katika maongezi yale kati ya Macha na Meja Byabato yaliyowafanya wawe marafiki. Mara baada ya Joe kuleta mpango wa kutaka Rais Costa atolewe madarakani Macha aliona ni muda mzuri wa kumtumia Meja Byabato kama kiungo mshambuliaji kwenye misheni.

Meja aliendesha gari na kufika kwenye kambi yao ya jeshi. Alishuka kijasiri na kuanaza kutembea kuelekea kwenye ofisi yake. Alipofika karibu na ofisi alishangaa kuona vijana wanne wakakamavu wa kijeshi wamesimama mbele ya mlango wake wakiwa wamemkazia macho. Aliishiwa nguvu.
***************************************
Usiache Kufuatilia Sehemu Ya 15 Itakayokujia Siku Ya Kesho Ijumaa.

the Legend☆
 
Leo Nimelala saa Tisa ajili ya hii hadithi... sitakagi arosto mie nitarudi huku after two weeks.
But mwandishi yuko vizuri sana!!

Sent from my GT-I9300 using Tapatalk
Hahaha una subiri ziongezeke siyoo
 
Ni hatari sana, meja amegundulika

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom