The President And I(Mimi Na Rais) - Sehemu Ya Kumi Na Sita
Mwinda Anapowindwa
Usiku ule pale New Continental Casino kulijaa watu wengi. Ilikuwa ni siku ya Alhamisi, siku ambayo wacheza kamari huamini ni siku yao ya bahati, hivyo watu huhudhuria kwa wingi.
Mara baada ya Meshack kumuona Sylvanus na kumkwepa alielekea upande wa kaunta na kuagiza kinywaji. Alichukua kinywaji chake na kufungua simu upande wa WhatsApp ili aweze kumwambia Joe kinachoendelea. Alishtushwa aliposikia ameguswa bega na kuitwa kwa jina wakati yeye aliamini kwa jinsi alivyovaa hakuna ambaye angeweza kumtambua.
“Meshack niaje”, jamaa aliyemgusa bega alimsalimia Meshack.
Bila kujibu huku akiwa ameshtuka sana Meshack aligeuka ili kutazama ni nani amemuita. Hakuamini macho yake alipokuta ni Sylvanus. Mwendo wa mapigo ya moyo wake yalibadilika na kuanza kwenda kasi. Ni kweli aliujua uwezo mkubwa wa Sylvanus wa kuhisi na kugundua mambo lakini hakujua kama ni uwezo uliofika kiwango kile alichokishuhudia wakati ule.
“Ah! Sylvanus, na wewe upo viwanja hivi?”, Meshack alijikaza na kujibu.
“Haya ndio mambo yangu mzee labda nikuulize wewe huku umeanza lini au kuna lead unaifatilia?” Sylanus alihoji.
Lead ni neno linalotumika kuashiria mtu anaefatiliwa kwa sababu fulani. Yaweza kuwa yeye ndiye ‘target’ ama unamfatilia ili akupeleke kwa ‘target’ lakini bila yeye kujua. Mfano, kama mtu amehisiwa kuwa anafanya utakatishaji wa fedha na kuwa hana shughuli maalumu bali anatumiwa na watu basi watu wa usalama waweza kumfatilia mtu huyo ili kujua anatumiwa na kina nani. Ufuatiliaji huu huwa wa siri na bila muhusika kujua kama anafuatiliwa.
“Hapana mzee, nimeamua kuja kupumzika tu”, Meshack alijibu kwa kujikaza.
“Si kwa mavazi hayo kaka. Ha ha ha”, Sylvanus alionekana kukomalia.
Baada ya maongezi mawili matatu Sylvanus aliondoka na kumuacha Meshack. Meshack alivuta pumzi kwa nguvu sana na kutoamini kama Sylvanus amemshtukia pale. Alianza kuhisi yamkini Sylvanus ameshajua kitu, aliingiwa na woga sana.
Siku ile ilikuwa ni lazima amuue Sylvanus kwa sababu akimuacha akapanda ndege kuelekea China kesho yake alfajiri basi Joe asingekuwa salama tena. Meshack alijua wazi kuwa Joe hawezi kukwepa mkono wa Sylavanus. Ni gwiji wa mauaji ya siri aliyewahi kutumiwa na serikali kadhaa za nchi za kiafrika kuwamaliza wapinzani wao. Hakuwa mtu mwenye huruma na hakuwahi kujali jambo lolote Zaidi ya amri aliyopewa. Hata wanausalama wenzake walimuogopa.
***********************************
Sylvanus alipomaliza kuongea na Meshack hakuridhika. Hisia zake zilimwelekeza afuatilie zaidi. Aliwaza kama kweli Meshack hajaja pale kufuatilia lead basi ni lazima kuna suala jingine amekuja kufuatilia. Anafahamu wazi kuwa si hulka ya Meshack kukaa sehemu kama zile. Lakini pia kama amekuja kufuatilia lead kwanini amesita kumwambia ni nani wakati wote ni watendaji wa idara moja na pengine angeweza kumsaidia? Maswali mengi yalimsumbua sana kichwa Sylvanus.
“Oya Nyari, hivi baada ya mkuu Sabinasi kupangua safu Meshack alimpanga kitengo gani?” Sylanus aliamua kumpigia simu Nyari na kumuuliza.
Fredrick Nyari ni mwenzake na Sylvanus, wote wapo Idara ya Usalama wa taifa Stanza kitengo cha Mauaji na Uhujumu. Tungekuwa Israel basi kitengo chao hiki kingekuwa sawa na kile cha Idara ya Ujasusi ya Israel Mossad kwenye kitengo wanachokiita Metsada ambacho kazi yao kuu kwa kiingereza wanasema Assasinations and Sabotage.
“Alimtupa jimbo la Kinyunyu. Kwani vipi mzee?”, Nyari alihoji.
“Ah, namuona New Continental hapa. Nimemuuliza ikiwa ana lead ila amekana na kusema kuwa amekuja kupumzika tu wakati mimi nafahamu haya si mambo yake kabisa. Ila poa mwanangu baadae”, Sylvanus alimaliza na kukata simu.
Hapo ndipo Sylvanus alipopata wasiwasi kamili kuwa lipo jambo Meshack amemficha. Aliamua kuanza kumfatilia amemficha jambo gani. Aliwaza iweje muda ule Meshack awe pale wakati Kinyunyu ni mbali sana na Peron, mji mkuu wa Stanza. Amefuata nini?
Alianza kumuwinda. Wawindaji walianza kuwindana.
****************************************
Meshack alianza kumtaarifu Joe jinsi alivyoshtuliwa na Sylvanus. Alimweleza wasiwasi wake kuwa misheni ile inaweza kukwama kwani sasa Sylvanus ameshajua kuwa yeye yupo pale na hiyo inamuweka kwenye wakati mgumu kufanya alilokusudia. Wao kwenye usalama husema kugundulika tu kuwa wewe ni nani kwa adui tayari kunakupunguzia asilimia 50 ya kumshinda. Alihisi kuanza kushindwa.
Meshack aliamua kumtumia Joe picha ya Sylvanus na kumwambia popote anapokuwa ahakikishe mtu huyo hayupo karibu yake. Alimsihi kuwa anapomuona tu ajihami nae mara moja maana wao walizoea kumwita Sylvanus upepo kwasababu huweza kuonekana na kutoweka kwa haraka isiyotarajiwa. Kupotea mara unapohisi kugundulika ni mbinu ya kawaida kwa majasusi wabobezi.
Alikuwa pia na uwezo mkubwa wa kufanya mauaji kwa uharaka uliopitiliza na kutoacha hata alama kidogo tu ya kutenda hivyo, na iliwawia vigumu wachunguzi kujua ni nani muhusika wa mauaji yale. Alimsihi Joe kuwa atajaribu lakini kama akishindwa basi Joe hana budi kujilinda dhidi ya Sylvanus.
*********************************
Elizabeth, mke wa Joe kwa mara ya kwanza tangu mume wake aondoke kuelekea Korea Kaskazini aliingiwa na hofu sana. Hofu hii ilijengwa kwa sababu kubwa mbili. Moja, Joe mume wake alimuaga kuwa misheni ile haitamchukua zaidi ya wiki moja ama akichelewa sana basi wiki mbili lakini mpaka siku hiyo tayari alishafikisha wiki ya tatu.
Sababu ya pili ni kuwa Joe hana utaratibu wa kukaa zaidi ya wiki moja bila kumtafuta. Yeye Elizabeth alishajaribu sana kumpigia simu Joe bila mafanikio na sasa aliamua kumpigia kwa njia ya WhatsApp. Alifanikiwa kumpata kwa mara ya kwanza.
“Dear, mnaendeleaje huko? Mbona simu yako nikipiga kawaida inakataa na wewe hunitafuti hivi kweli hujanimiss mke wako?”, Eliza alianza kudeka kwa mumewe Joe alipopokea simu yake.
“Nipo China, Costa amenipa kazi nyingine hapa ila nitarudi mke wangu. Watoto wanaendeleaje lakini?” Joe aliuliza kwa sauti ya upole.
“Wapo vizuri tu Mi Amor”, Eliza alijibu nae kwa sauti ya mahaba akimwita Joe Mi Amor, maneno ya lugha ya kihispanyola yenye maana ya mahabuba wangu.
Joe na Eliza walikuwa ni maana halisi ya watu wanaopendana. Japo umri wao ulikuwa mkubwa na tayari walishakaa kwenye ndoa kwa miaka 21 sasa lakini mapenzi yao hayajawahi kupungua. Walitofautiana na wana ndoa wengi wenye kuamini kuwa baada ya kuoana kuna mambo wanapaswa kuacha. Wao hawakuwahi kuacha mambo yaliyowafanya wapendane enzi za ujana wao.
“Derrick anaendelea na lile zoezi la kujiwekea akiba? Amekwambia mwezi huu ana mpango gani? Hakikisha anakwambia ni kitabu gani atakisoma mwezi huu cha uwekezaji lakini pia kwa sababu yupo likizo aseme anataka kwenda kutembea wapi. Utaratibu wa kukaa kucheza game tu ndani nilishakataa”, Joe alimwagiza mke wake.
“Afadhali umenikumbusha, nilishasahau. Unajua wiki hii imekuwa ngumu sana kwangu maana tulikuwa tunasimamia usambazaji wa mbolea kwa wakulima. Benki ya wakulima ndio Costa ameipa jukumu la kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati sasa hawa watendaji wanataka kunivuruga, imebidi nilale nao mbele. Ila nimemalizana nao nitafatilia hayo baba Derick.” Eliza alijibu kwa heshima ya uanamke.
Joe ni baba aliyetaka kuleta mapinduzi kwa kizazi chake. Aliamini jamii ya watu wa magharibi huanza kuwafunza na kuwakuza watoto wao katika hali ambayo humfanya mtoto ajielewe na kujiamini angali bado mdogo.
Mathalani, kusoma vitabu, kutembelea maeneo mbalimbali, kuanza kuwafundisha watoto namna ya kuweka akiba, kuwekeza, kupanga malengo na kuyatimiza ni mambo ambayo kwa jamii za kiafrika yapo nyuma sana na hivyo kumfanya mtoto mpaka anakuwa mtu mzima anajikuta amezaliwa eneo hilo na kusoma hapo hapo akapata kazi na kuoa hapo hapo. Tena hajui kuweka akiba, hajui uwekezaji na huishi bila malengo.
Kuishi bila malengo ni sawa na mtu anayeendesha gari pasi kujua anaelekea wapi. Anayekwenda bila kujua anaelekea wapi ni sawa na asiekwenda popote. Wazungu husema “If you don’t know where you’re goin, then you’re going nowhere”. Joe alikataa kizazi chake kuwa cha namna hii.
“Eliza afadhali umenipigia nilikuwa nataka kuwaambia nawapenda sana familia yangu. Umwambie Derick na mdogo wake ‘wabehave’. Dunia ipo kwa ajili yao ni kazi yao kuitawala”, Joe alionekana kama kutoa maneno ya usia kwa mkewe Eliza.
Joe alijua kabisa kama Meshack atamkosa Sylvanus usiku ule basi yeye hatammudu. Aliwaza akimbilie ubalozi wa Korea Kaskazini kujificha lakini aliona haitakuwa na maana. Alitaka kufa kiume.
“Joe hujawahi kuniaga kwa staili hii, leo kulikoni? Kwani Costa kakutuma nini kinachokupa wasiwasi namna hiyo?” Eliza alihoji.
“Hapana Eliza kwani mimi kusema nawapenda nimeanza leo?” Joe alimuhoji mkewe.
Eliza aliona asiendelee kuuliza asije akasababisha wakamaliza maongezi kwa hasira, aliamua kukaa kimya na kuagana na Joe.
Lakini kama wanavyosema wengi kuwa mwanamke ana uwezo mkubwa wa kuhisi mambo yajayo kuliko mwanaume, Eliza usiku ule alisikia tumbo kumuuma mara baada ya kuongea na mume wake. Hakulala wala kupata usingizi. Alianza kuhisi hali ya hatari kumnyemelea mume wake lakini hakujua ni nini wala ni lini. Alikesha macho usiku mzima.
**********************************
Meja Byabato hakuamini alichokuwa akikishuhudia mbele yake. Wale vijana wanne waliokuwa wamesimama mbele ya mlango wa ofisi yake walikuwa wameshiba kisawasawa. Wote wakiwa wamekunja sura na kuvaa miwani meusi sawa na aliyoivaa yeye walikuwa wamesimama huku wakiwa wamepanua miguu kidogo na kuweka mikono yao nyuma.
Meja Byabato aliekuwa akitembea kwa hatua ndefu na kubwa kutokea nje ilibidi apunguze mwendo na kuanza kutembea kwa taratibu huku akiwatazama akiwaza afanye nini na wale vijana wapo pale kwa ajili gani. Aliwaza au alikuwa akifuatiliwa nini? Lakini hata kama alikuwa akifuatiliwa mbona hakuna lolote la maana aliloongea na Gideon zaidi ya kupokea ile taarifa ya siri tena kwa maneno machache? Aliwaza pia kuwa labda Gideon alitumwa kuja kumtega na kuthibitisha kuwa anahusika na mpango ule, lakini pia aliwaza kama ndivyo basi ni Macha atakuwa ameamua kumsaliti.
Wakati huo huo aliwaza isingewezekana Gideo kupata ile ‘code’ kama sio kupewa na Macha na kwa anavyomfahamu Macha asingeweza kumpa mtu asiyemwamini. Lakini alidhani labda Gideon aliaminiwa na Macha na sasa kaamua kumsaliti Macha. Hakika alijawa na maswali mengi ndani ya sekunde chache yasiyo na majibu.
Meja Byabato aliamua kutoa miwani yake na kuwatazama wale vijana kwa macho makavu akiwa amesimama kama hatua kumi hivi kutokea walipokuwa wamesimama. Byabato alikuwa ni mtu wa mazoezi kwa hivyo akiwa amesimama pale alikusanya nguvu zake zote na kujiweka tayari kwa mapambano kama wale vijana wangemwanzishia varangati. Alijisemea moyoni ni bora awe mkimbizi kuliko kudakwa kama kuku.
Vijana wale kicheo walikuwa ni wadogo sana kwa Meja Byabato hivyo alitegemea wao ndio waanze kumpa salamu. Meja aliwatambua kuwa ni vijana wake tena isitoshe wapo kwenye kikundi chake cha mazoezi ya viungo kwa hiyo na wao walikuwa wameshiba kweli kweli.
Baada ya kusimama kama sekunde kadhaa bila yeye kusema neno wala wao kusema neno ghafla walipiga saluti ya kumsalimia. Meja nae alijibu.
“Kwanini mmesimama hivyo ofisini kwangu. Kuna nini?” Meja alihoji kwa sauti ya ukali sana.
Wale askari walibaki kimya sekunde kadhaa na kisha wote kwa pamoja walimwendea Meja kwa kasi ya ajabu na kumvaa.
Meja alidaka ngumi ya mmoja wapo aliyokuwa ameirusha kwa kasi ya kimbuga na kumpiga kichwa kimoja kilichomfanya aweweseke. Wakati akimdhibiti huyu mmoja kijana mwingine alimpiga Meja ngumi moja ya juu ya sikio iliyompata kwenye mshipa wa fahamu wa kichwa na kumfanya Meja nae aanze kuweweseka.
Akiwa anaweweseka mwingine alirusha ngumi nzito iliyokuwa inamwendea Meja maeneo ya pua lakini Bahati nzuri aliiona na kuikwepa ikapiga ukuta, na kwa sababu ilikuwa na kasi kubwa na uzito mkubwa yule kijana alijikuta ametengua vidole vyote vinne vya mkono wake wa kulia. Meja alijua hilo na haraka alimchota juu na kumpigiza chini kama gunia.
Mapigano hayo yalikuwa yakienda kwa kasi sana na haraka. Meja alijua hapo hali si shwari tena, alianza kuwaza ni namna gani awatoke wale vijana wake. Tatizo lilikuwa ni moja tu vijana wale aliwafunza mapigano yeye mwenyewe na walijua mbinu zote, walikuwa warefu kama yeye na walishibwa kweli kweli.
Wakati akiwaza hayo tayari king’ora cha hatari kilishapigwa na askari pale kambini walianza kuja kuamulia maana pale ilikuwa mmoja awe maiti. Kambini pale waliwajua wale vijana na waliujua vizuri uwezo wa Meja Byabato, ilikuwa huwezi kuamulia kwa mikono bila kutumia silaha.
Haraka kijana mmoja aliminya Sehemu ya nyonga ya Meja na kumfanya achutame chini kidogo na hapo mwingine alimshushia Meja ngumi moja Sehemu ya shingo na kumfanya Meja adondoke kwa magoti. Vijana wale walidhani wamemuweza Meja, wakiwa watatu wamesimama na mmoja amelala chini hajitambui Meja alishika mguu wa mmoja na kumvuta kitendo kilichosababisha adondoke na kupiga kisogo kwenye sakafu na kulala palepale akigugumia maumivu makali, na haraka Meja alinyanyuka kwa staili ambayo wachina wanaiita Jùfēng, yaani unanyanyuka kama upepo wa kisulisuli. Alinyanyuka na kumkanyaga shingo kwa nguvu kwa buti lile la jeshi alilokuwa amevaa huku akichutama kidogo na kuwapiga wale wawili maeneo ya chembe ya moyo kwa vidole viwili vya mikono wote kwa mpigo.
Eneo la chembe ya moyo pakiingizwa kidole basi ni lazima uende chini na ndicho kilichotokea. Baada ya Meja kuona angalau wote amewadhibiti huku akiwa hoi na akitokwa damu nyingi puani alianza kukimbia kuelekea nje. Hakuna askari aliyethubutu kumzuia wote walikuwa wakimpisha na alikuwa akipita kati kati yao kwenye korido ile.
“Happy birthday Sir”, Alisikika askari mmoja kati ya wale aliokuwa akipambana nao akiita kwa nguvu.
Meja Byabato alishtuka na kusimama kisha aligeuka kwa taabu mzima mzima maana shingo ilikuwa imepigwa ngumi moja na kuteguka.
“Happy birthday mkuu”, Kijana mwingine aliekuwa akijitahidi kunyanyuka kwa taabu alipokea naye huku akijitahidi kupiga saluti, salamu maalumu ya kijeshi akitokea pale chini.
Walinyanyuka vijana wawili kati ya wale aliokuwa akipambana nao na kupiga saluti huku wakiimba wimbo wa kumpongeza Meja kuashiria kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya Meja Kairuki Byabato. Askari wote waliokuwa wamekuja pale kusuluhisha walipiga saluti huku wote wakimwimbia Meja Byabato wimbo wa kumbukizi ya siku ya kuzaliwa, au Watoto wa mjini wangesema ‘’Happy Birthday’’
Meja hakuamini alichokuwa akikishuhudia. Ni ukweli kuwa ilikuwa ni siku yake ya kuzaliwa na hakuwahi kuisherehekea kwa zaidi ya mwaka wa 20 sasa. Vijana wake wale walianza kucheka huku wakimsogelea na Meja nae alianza kutabasamu kama kawaida yake kwa kubinua shavu moja tu bila hata kuonyesha jino hata moja.
Alitoa kitambaa cha mkono na kuanza kujifuta damu iliyokuwa ikimchuruzika puani.
“Meja upo vizuri”, Kijana mmoja aliekuwa akipambana na Meja Byabato alimsifia huku akimkumbatia.
“Nani aliwaza huu mpango”, Meja Byabato aliuliza kwa sauti ya kunguruma.
“Tulipanga siku nyingi na mazoezi yote uliyokuwa unatuona tunafanya wiki hii nzima ilikuwa ni kwa ajili yako, tulipanga tukuzimishe leo”. Kijana mwingine alijibu huku akimkumbatia Meja.
“Dah, sasa ningeua mtu hapo maana nilijua mnaniwashia kweli”, Meja nae alijibu kwa sauti ya maumivu.
Askari wengine waliokuwa watazamaji walimpa hongera Meja Byabato kwa kuweza kuwamudu wale askari wanne. Waliondoka na kuwaacha Meja na vijana wake.
“Tuingie ofisini kwangu mara moja”, Meja aliwaambia wale askari vijana wanne aliokuwa akipambana nao. Wote waliingia ofisini kwa Meja Byabato huku kila mmoja akijikokota kwa staili yake kutokana na eneo analosikia maumivu.
***********************************
Baada ya Meshack kuhakikisha kuwa ameshampa taarifa Joe ya kila kinachojiri kati yake na Sylvanus pale New Continetal Casino aliizima simu na kuiweka mfukoni ili sasa kuona ni namna gani atatimiza misheni ile.
Alibugia kwa mkupuo toti yake moja ya Godowns na kukaa tayari kumuwinda Sylvanus. Maskini hakujua kama na yeye alikuwa akiwindwa vile vile.
Alinyanyua kichwa na kumuona Sylvanus anacheza kamari pale kwenye ile mashine yake lakini kama baada ya dakika tatu hivi alimuona akitoka na kuelekea uelekeo wa vyooni. Meshaki hapo ndipo alipoona ni muda mzuri wa kujaribu Bahati yake. Hakujua ule ni mtego aliokuwa amewekewa na Sylvanus. Wanasema ili kumpata muhalifu lazima uwaze kama muhalifu. Sylvanus alimudu sana hili alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwaza sawa na ‘target’ wake anavyowaza ndio maana aliweza kujua kwa haraka lililo mbele yake.
Sylvanus aliingia kwenye ukumbi wa vyoo na kurudishia mlango. Casino ile ilikuwa na eneo kubwa la vyoo na ukumbi mkubwa. Uligawanywa sehemu kama msala ambapo hakukuwa na milango bali kulitengwa tu kwa kioo kidogo kisichoonyesha, halafu kukawa sasa na vyumba kwa ajili ya wale wanaotaka kujisaidia kile wazungu wanaita ‘long call’.
Tena katika ukumbi ule kulikuwa na sehemu ya kuvutia sigara na sehemu ya kujitengeneza vizuri iliyotengwa pia kwa kioo kisichoonyesha. Hakukuwa na watu wengi vyooni, ni kawaida kukuta zinapita hata dakika tano bila mtu yeyote kuingia kabisa.
Meshack aliingia akiwa amevaa zile raba zake zilizokuwa hazitoi sauti na kuanza kunyemelea kujua Sylvanus yupo wapi. Akiwa anapita mlango kwa mlango akijaribu kuugusa na kuusukuma kama unafunguka Sylvanus alikuwa akimchungulia kwa upenyo mdogo sana kutokea eneo la kuvutia sigara alilokuwa amejitega huko akimsubiri Meshack.
Sylvanus alijiridhisha kuwa kumbe Meshack alikuwa akimfatilia yeye. Kwenye mambo ya usalama huwezi kumwamini mtu, wakati wowote mwenzako aweza kutumwa kukumaliza kama ikionekana uwepo wako unakwamisha masuala ama umeanza kuwa tishio.
Sylvanus hakujua ni kwanini Meshack ametumwa kumuwinda wakati ana kazi aliyopewa na Rais Costa na safari ni kesho yake. Aliwaza huyu aliemtuma Meshack ni nani na ana dhamira gani. Alitaka kuwasiliana na mkuu wao wa Idara ndugu Sabinasi, lakini aliona bora amalizane kwanza na Meshack ndipo atoe taarifa.
Meshack alisikia kama kwenye moja ya vyumba vile vya vyoo kuna mtu ana ‘flash’ na yeye haraka alikimbilia kwenye sehemu ya haja ndogo na kujifanya anajisaidia huku akiangalia kwa kioo ni nani anatoka. Alimuoana mtu mmoja akitoka na hakuwa Sylvanus. Alishangaa kwani alikuwa na uhakika Sylvanus yupo pale ndani.
Baada ya kujiridhisha kuwa ndani ya vyumba vyote vya vyoo Sylvanus hayupo alijua lazima atakuwa eneo la kuvuta sigara akivuta sigara huko. Alitoa ile kofia maalumu inayofunika sura. Akatoa glavu na kuvaa kisha alinyoosha vizuri vidole. Alivuta pumzi kwa nguvu na kwa kuambata na kioo alianza kunyemelea kuingia kwenye ile Sehemu ya kuvutia sigara.
Sylvanus alikuwa akifuatilia kila hatua ya Meshack na hakika alikuwa amewasha sigara akawa anaivuta na kuipuliza kwa juu makusudi. Moshi ule uliokuwa ukivuma kwa juu ulimpa Ushahidi Meshack pasi shaka kuwa Sylvanus yupo kule.
Meshack alisogea taratibu mpaka akafika kwenye ukingo wa kioo kile na sasa alijipanga kuingia kwa kasi ya upepo ili kumvaa Sylvanus na kupambana nae. Alikusanya nguvu na kuhesabu kimya kimya Moja…. Mbili….
Kabla hajamaliza tatu alishtukia amevutwa kwa nguvu na kupokelewa na pigo moja eneo la chini ya mbavu lililofanya mbavu za upande wa kushoto kupanda na kubaki juu hivyo kusababisha maumivu makali yaliyomfanya ashindwe kuhema na kuishiwa nguvu.
Pigo lile lilikuwa ni la uhakika yaani lisilokwepesha matokeo. Mbavu za Meshack zilibaki kwa juu kama nguo iliyotundikwa kwenye msumari nyuma ya mlango. Alikuwa akigugumia huku amejikunja. Sylvanus alimvuta kwa ndani vizuri ili kusababisha wanaoingia chooni kutoona.
“Nimpelekee ujumbe gani Gloria”, Sylvanus alimuhoji Meshack aliyekuwa akitapatapa pale chini. Gloria ni mke wa Meshack.
Meshack hakuweza kujibu, mbavu zilibana kisawasawa. Sylvanus hakuwa mtu wa kupoteza muda haraka alivaa glavu zake na kumpindua Meshack na kuiegamiza shingo ya Meshack kwenye goti lake la kulia na kisha kumpiga kabari Meshack iliyotukuka. Kabari hii wakorea wanaiita ‘gong-gan eobs-eum’, yaani unakabwa kuhakikisha hakuna nafasi ya hewa kupita kwa namna yoyote ile.
Kwa sababu tayari Meshack alikuwa ameishiwa nguvu kwa pigo la kwanza lililosababisha mbavu za upande wa kushoto kubaki juu na kusababisha apumue kwa shida, kabari hii ilikuwa ni ya kummalizia tu. Alitapatapa kidogo sana na kisha alitulia. Uuaji wa Sylvanus ulionekana ni rahisi kwa macho lakini ukiujaribu kama si mtaalamu basi hauwezi kufanikiwa.
“Nitamjua aliekutuma”, Sylvanus alikuwa akimwambia Meshack aliyeonekena kuanza kufumba macho taratibu huku akitulia kimya bila kutapatapa tena. Sylvanus alizidi kuminya kabari ile ili kujiridhisha kuwa huo unakuwa ndio mwisho wa uhai wa Meshack.
*****************************************
Nini Kitaendelea Katika Simulizi Hii Ya Kusisimua?Usiache Kuifuatilia Sehemu Ya 17 Siku Ya Ijumaa.
the Legend☆