Simulizi ya kichawi: Makaburi ya wasio na hatia (The Graves of The Innocents)

Simulizi ya kichawi: Makaburi ya wasio na hatia (The Graves of The Innocents)

Sehemu ya 44




ILIPOISHIA:

“Niangalie vizuri namna ya kuchimba maana tukitoka hapa inabidi na wewe ukafanye majaribio kama wenzako,” alisema baba. Muda huo ulikuwa ni kama saa sita hivi za usiku, giza nene likiwa limetanda kila sehemu.

SASA ENDELEA…

Huku nikitetemeka, nilianza kumtazama vizuri baba alivyokuwa akichimba, alikuwa akifukua shina la ule mti huku akiuzunguka, akitamka maneno fulani ambayo sikuwa nayaelewa. Baada ya kuuzunguka karibu mara saba, tayari alishakuwa ameifikia mizizi, akatoa kisu na kuanza kuichambua na kuikata mmoja baada ya mwingine.

“Hutakiwi kukata mizizi zaidi ya saba kwenye mti mmoja, na hutakiwi kuchimba mti ambao unaonekana tayari umeshachimbwa katika siku za hivi karibuni,” alisema baba, nikawa natingisha kichwa kumkubalia. Baada ya kumaliza, alinikabidhi tochi, akaniambia niutazame vizuri ule mti, nikaumulika vizuri.

“Sasa na wewe unatakiwa kutafuta mti kama huuhuu, ipo mingi lakini lazima uwe makini kutafuta wa kuchimba dawa,” aliniambia baba, basi nikaanza kumulika huku na kule, baba akiwa upande wa kushoto na baba yake Rahma upande wa kulia.

Muda mfupi baadaye, kweli nilifanikiwa kuupata lakini ulikuwa umezongwa na miiba mingi, baba akaniambia ni lazima niitoe kwanza miiba yote ndiyo nianze kuchimba, nilifanya hivyo na baada ya muda, nilikuwa nimepasafisha pale kwenye shina la mti huo.



Nikaanza kuchimba huku baba akinielekeza hatua kwa hatua, akaniambia kwa kuwa ndiyo kwanza naanza hakuna umuhimu wa kunuiza maneno kama alivyokuwa akifanya yeye bali natakiwa kuweka nia moyoni kwamba nahitaji damu kwa ajili ya kafara.

Nilifanya hivyo, nikawa naufukua ule mti na nilipozunguka mara ya saba, tayari mizizi ilikuwa ikionekana, baba akanipa kisu na kuniambia kwamba natakiwa kuchagua mizizi ya katikati, yaani isiwe mikubwa sana wala midogo sana na isizidi saba.

Nikakata wa kwanza, pale nilipokata pakawa panatoka yale majimaji kama damu, nikakata wa pili, wa tatu mpaka saba ilipotimia, shina lote likawa limelowa na yale majimaji ya ule mti kama damu.

“Haya fukia lakini hakikisha hiyo mizizi hauiweki chini, ishike vizuri,” aliniambia na kunielekeza kwamba wakati wa kufukia, natakiwa kwenda kinyume na vile nilivyokuwa nafukua, yaani kama wakati wa kufukua nilikuwa nauzunguka mti kwa kuelekea upande wa kulia, ninapofukia natakiwa kuanzia upande wa kushoto na hivyo ndivyo nilivyofanya.

Baada ya kumaliza, baba alisema tunapaswa kwenda kuziosha dawa zetu mtoni na kuzitengeneza vizuri. Sikuwa mwenyeji wa Kibaha na hata sikuwa najua kama kuna mto, nikawa kama bendera fuata upepo.

Tulitembea tukikatiza vichaka na mapori, hatimaye tukatokezea mahali palipokuwa na kama chemchemi hivi, pembeni kukiwa na bustani za mbogamboga nyingi, baba akatangulia mpaka pale kwenye chemchemi, kabla ya yote, alitoa kisu chake na kukata jani kubwa la mgomba, akalikata vipande vitatu, kimoja akanipa, kingine akampa baba Rahma na kingine akabaki nacho yeye.

Alitoa ile mizizi aliyoichimba, akaniambia nimtazame kwa makini anachokifanya, ilikuwa imebadilika rangi na kuwa nyekundu kama damu, akaanza kuiosha ikiwa juu ya jani la mgomba, akafanya hivyo kwa dakika kadhaa mpaka ilipobadilika rangi na kurejea kwenye rangi yake halisi ambayo ni kama kahawia fulani hivi.

Ilifika zamu yangu, na mimi nikafanya vilevile, nikaitoa mfukoni na kuiosha vizuri, kisha ikafika zamu ya baba yake Rahma ambapo baba alimtolea na kumpa mizizi yake, akaiosha kwa uzoefu wa hali ya juu kisha tukaondoka eneo hilo.

Hapakuwa mbali sana na barabara kwani hata kelele za magari yaliyokuwa yakipita kwa kasi kubwa tuliweza kuzisikia. Kadiri tulivyokuwa tukisonga mbele ndivyo hofu ilivyozidi kutanda kwenye moyo wangu.

Tulikatiza vichaka, mapori na mashamba ya watu na hatimaye tukawa tumetokezea barabara ya lami. Sikujua eneo lile linaitwaje lakini kwa mzunguko tulioupiga, kuanzia pale tuliposhuka kwenye gari, tulivyoelekea njia ya Tumbi na baadaye kuingia porini kisha kurudi barabarani, nilijua kwamba si mbali sana na pale tuliposhukia.

“Mtu yeyote akikusemesha hutakiwi kujibu chochote, eneo hili lina watu kutoka jamii mbalimbali ambao huwa wanapenda kupimana nguvu, umenielewa?” baba aliniambia, nikatingisha kichwa kuonesha kumkubalia.

“Leo ni zamu yako, kwa hiyo inatakiwa unisikilize kwa makini,” baba aliniambia, akasema kati ya ile mizizi saba, mmoja natakiwa kwenda kuufunga kwenye mti au jani lolote upande wa pili wa barabara, mwingine natakiwa kuuweka katikati ya barabara, mwingine natakiwa kuufunga upande ule tuliokuwepo, mmoja natakiwa kuutafuna na kuumeza na miwili natakiwa kubaki nayo mwilini, mmoja niweke kwenye mfuko wa kushoto wa suruali na mwingine niubane kwenye kwapa langu la kushoto kama kipima joto.

Yalikuwa ni maelezo marefu lakini nilijitahidi kuwa mwelewa maana nilikuwa na shauku kubwa ya kuona nini kitatokea. Kweli baada ya hali kutulia, kwa maana kukiwa hakuna gari kutoka upande wowote, nilivuka barabara kinyumenyume mpaka upande wa pili.

Kwa kutumia uzi mweusi alionipa baba, niliufunga ule mzizi kwenye tawi moja la mti mdogo uliokuwa pale pembeni ya barabara, nikarudi tena kinyumenyume mpaka katikati ya barabara na kukaa chini kabisa, nikaweka ule mzizi kisha nikajiburuza kwa makalio kinyumenyume mpaka pale baba na baba yake Rahma walipokuwa wamesimama.

Nikasimama na kusogea kwenye kimti kingine kidogo kilichokuwa kando ya barabara, usawa wa kile nilichokifunga, nikaenda kufunga ule mzizi kwa kutumia ule uzi kisha kinawasogelea akina baba ambao walikuwa wakinitazama kwa makini kuhakikisha sikosei hatua hata moja.

“Safi sana,” alisema baba kisha akaanza kuniuliza kama mpaka hapo nimeshaelewa ni gari linalotokea upande gani ndiyo litapata ajali. Sikuwa naelewa chochote. Akaniambia kwa sababu nimesota kwa makalio kutokea katikati ya barabara kuelekea upande wa kushoto wa Barabara ya Morogoro, gari litakalopata ajali litakuwa ni linalotoka Dar es Salaam kuelekea upande wa Morogoro.



Sikuelewa anamaanisha nini, ikabidi nitulie kuona nini kinachoenda kutokea. Tulisogea pembeni kabisa, umbali wa kama mita mia moja hivi, vichakani kabisa, tukakaa kwa kukunja miguu na kutengeneza duara. Kulikuwa na mbu wengi lakini wote walikuwa wakiishia kutuzunguka tu, hata sijui kwa nini hawakuwa wakituuma.

“Nataka ufumbe macho halafu utulie huku ukitafuna huo mzizi mmoja, nitakachokuuliza unijibu,” baba aliniambia, nikafanya kama alivyoniambia. Cha ajabu, nilipofumba macho tu, japokuwa tulikuwa mbali kidogo na barabara, niliweza kusikia sauti za magari na pikipiki vikipita kwa kasi, cha kushangaza zaidi, niliweza kusikia hata sauti za madereva na abiria, nikashtuka sana.

Nikiwa nimeendelea kutulia, japokuwa nilikuwa nimefumba macho, kadiri nilivyokuwa nikizidi kutafuna ule mzizi ndivyo nilivyoanza kuona taswira ya kila kilichokuwa kikiendelea barabarani utafikiri nilikuwa nimesimama pembeni ya barabara, tena nikiwa nimefumbua macho.

“Unaona magari mangapi?”

“Mengi tu.”

“Yanayoelekea upande wa Morogoro ni mangapi?”

“Ni matatu.”

“Ambalo lipo nyuma kabisa lina abiria wangapi?”

“Abiria mmoja ambaye ni mtoto na dereva mwanamke.”

“Safi, hiyo ndiyo kazi yako ya leo, likazie macho hilo gari kwa nguvu na likikaribia hapo ulipo fumbua macho ghafla halafu tena hicho kilichopo mdomoni mwako,” alisema baba, kweli nikawa nalitazama gari hilo.

Lilikuwa ni gari dogo na ndani yake kulikuwa na watu wawili tu, dereva mwanamke na mtoto, ilionesha ni kama ni wanafamilia wanarudi makwao. Sikuelewa nini kitawapata lakini kwa sababu ya shauku niliyokuwa nayo, nilijikuta nikifanya kile baba alichoniambia, nikafumbua macho ghafla na kutema mabaki ya ule mzizi, nikashtukia nimemtemea baba usoni.

Mara kikasikika kishindo kikubwa kule barabarani, kilichonishtua mno. Sikuelewa nini kimetokea pale kwa sababu nilipokuwa nimefumbamacho, nilikuwa najiona kabisa kwamba nipo barabarani lakini nilipofumbua tu, nilijikuta nikiwa nimekaa palepale tulipokuwa tumekaa na baba na baba yake Rahma.

Kitu cha mwisho nilichokumbuka, wakati nataka kufumbua machom nilimuona yule mwanamke aliyekuwa kwenye usukani, akikunya usukani gahfla kama aliyeona kitu cha hatari mbele na sasa anataka kukikwepa, ndipo kikafuatia kile kishindo.

“Nenda haraka, hakikisha unamtoa mtoto kwenye gari na kuja naye hapa, pale kwenye gari ulipomtoa utaweka hiki,” alisema baba huku akinipa kipande cha mgomba.

Je, nini kitafuatia?
Wachaw shenz sana
 
Sehemu ya 45

ILIPOISHIA:

Kitu cha mwisho nilichokumbuka, wakati nataka kufumbua macho nilimuona yule mwanamke aliyekuwa kwenye usukani, akikunja usukani ghafla kama aliyeona kitu cha hatari mbele na sasa anataka kukikwepa, ndipo kikafuatia kile kishindo.

“Nenda haraka, hakikisha unamtoa mtoto kwenye gari na kuja naye hapa, pale kwenye gari ulipomtoa utaweka hiki,” alisema baba huku akinipa kipande cha mgomba.

Usipitwe na Matukio, Install ===>Global Publishers App


SASA ENDELEA…

“Nikikamatwa je?”

“Nenda, hakuna mtu yeyote atakayekukamata wala kukuona, usiongee chochote na mtu yeyote, hata wakikusemesha usijibu,” alisema baba. Basi huku nikitetemeka, nilitoka na kile kipande cha mgomba, nikatembea harakaharaka mpaka pale barabarani.

Lile gari dogo lilikuwa limepata ajali mbaya na kupinduka, matairi yakiwa juu, likiwa limegeukia kule lilikotokea. Kwa mtu yeyote lazima angejiuliza sana kilichosababisha ajali hiyo kwa sababu kwanza lilikuwa ni eneo la tambarare na hakukuwa na kona wala tuta lolote.

Damu zilikuwa zimetapakaa kuanzia barabarani mpaka kando ya barabara, pale gari hilo lilipokuwa limepinduka. Ilibidi nifanye kile nilichoambiwa kabla watu hawajaanza kujaa. Niliinama kwenye upande aliokuwa amekaa yule mtoto, nikakitingisha kioo ambacho kilishapasuka kwa sehemu kubwa, kikamwagika chote kwenye lami.

Nikaingiza mikono na kumvuta mtoto huyo aliyekuwa amebanwa pale kwenye siti, kwa kuwa nilikuwa na nguvu za kutosha, nilifanikiwa kumtoa, nikamlaza barabarani kisha nikachukua kile kipande cha mgomba na kukirudishia palepale nilipomtoa yule mtoto, kama baba alivyonielekeza.

Nilipomaliza, nilisimama, mapigo ya moyo wangu yakizidi kunienda mbio kuliko kawaida, nikageuka kutazama pale nilipokuwa nimemlaza yule mtoto. Cha ajabu, niliwaona watu wengine kama wanne hivi, nao wakiwa wanamtazama yule mtoto kama wanaoshauriana kama wamchukue au la.

Nilipowatazama vizuri watu hao, hasa maeneo ya usoni, niligundua kwamba hawakuwa binadamu wa kawaida, nikaona wanataka kunizidi ujanja. Kwa hasira nilipiga kishindo kwa nguvu kwenye lami, wote wakashtuka huku wakinitazama kwa woga, wakaanza kurudi kinyumenyume.

>> Usikose kutembelea Simulizi za Majonzi

Ishara ya kupiga kishindo chini, alinifundisha baba tukiwa bado kule Chunya lakini aliponiambia kipindi hicho, alisema kwamba eti waganga ndiyo huitumia kuwashtua wachawi ambao mara nyingi wanapofanya mambo yao, huwa wanaamini hakuna anayewaona kwa hiyo ukipiga mguu wa kushoto chini, huwafanya waelewe kwamba kumbe umewaona.

Walipokuwa wanarudi nyuma, na mimi nilipata nafasi ya kumnyanyua yule mtoto aliyekuwa akitapatapa kama anayeelekea kukata roho, damu nyingi zikimtoka mdomoni na puani. Cha ajabu, licha ya kwamba sehemu aliyokuwa amekaa ilikuwa imebondeka vibaya, hakuwa na jeraha lolote zaidi ya kuvuja damu kwa wingi.

Hata sijui ujasiri niliupata wapi, nilimbeba begani, kiumri alikuwa na kati ya miaka sita au saba, mtoto wa kike mzuri, akiwa amevalia sare za shule kuonesha kwamba alikuwa ametoka shuleni.

“Pole kwa ajali, tunaomba tukusaidie kumbeba,” alisema mmoja kati ya wale watu, kwa sauti iliyokuwa ikisikika kama mwangwi, nikamkata jicho la ukali bila kumjibu chochote kisha nikazamia kule vichakani, nikawa nakimbia kuelekea pale nilipowaacha baba na baba yake Rahma.

“Safi sana,” alisema baba na kuungwa mkono na baba yake Rahma, wakawa wananipigia makofi kunipongeza.

“Mlaze hapo kwenye hayo majani ya mgomba kisha rudi tena eneo la tukio katoe ile mizizi yote ya mtunguja uliyoifunga, si unakumbuka mahali ulipoifunga? Ukiiacha magari mengine yataendelea kupata ajali hovyo,” alisema baba huku akinipa kisu, harakaharaka nikarudi mpaka eneo la tukio ambapo nilikuta watu wameongezeka lakini nilipowatazama vizuri, niligundua kwamba wote walikuwa ni wa jamii moja.

Walichokuwa wanakifanya kilinishangaza sana, wengine walikuwa wakilamba damu pale kwenye lami bila hofu hata kidogo huku wengine wakiwa bize kutaka kumtoa yule mwanamke aliyekuwa akiendesha gari hilo ambaye ilionesha amejeruhiwa vibaya.

Nilipofika, nilifanya kama nilivyofanya awali, nikapiga mguu chini kwa nguvu, wote wakatawanyika kisha nikaanza kukata zile dawa nilizokuwa nimezifunga pande zote mbili za barabara. Nilivuka barabara, nikakata ya kwanza, nikarudi pale katikati, nikaiokota ile nyingine ambayo ilikuwa imelowa damu kwani pale ndipo gari lilipopatia ajali kabla ya kubinuka na kwenda kugota kando ya barabara.

Niliokota ile nyingine iliyokuwa upande ule ilipotokea ajali, nikaenda kumalizia na ile ya mwisho iliyokuwa upande ule waliokuwepo baba na baba yake Rahma, cha ajabu, nilipomalizia kukata ile ya mwisho tu, wale watu waiokuwa wamejaa eneo lile, walianza kutokomea mmoja baada ya mwingine, wengine nikawa nawasikia wakiachia misonyo mikali. Sikuwajali kwa sababu hata mimi nilitaka kuwahi kuondoka eneo hilo kwani ningeweza kukamatwa ikawa balaa.

>> Usikose kutembelea Simulizi za Majonzi

Bado hakukuwa na gari wala chombo chochote cha usafiri kilichopita eneo hilo, nikatokomea vichakani na kurudi pale nilipokuwa nimewaacha akina baba, mwili wangu ukiwa umelowa damu. Waliendelea kunipongeza, baba akaniambia natakiwa kumalizia kazi yangu.

“Kivipi baba?” nilimuuliza huku nikihema kwani niliamini kazi nzito nimeshaimaliza.

“Inabidi tuelekee kilingeni ukamkabidhi Mkuu alichokuagiza, tukifika itabidi umtenganishe kichwa na kiwiliwili kwa kutumia hicho kisu nilichokupa, hakikisha hizo dawa unazitunza vizuri,” alisema baba na kunifanya nishtuke kupita kawaida.

“Nimchinje?” nilihoji macho yakiwa yamenitoka pima.

“Sasa kazi kubwa umeshaifanya unaogopa nini?” alisema baba huku akiinuka, baba Rahma naye akainuka na wote tukasogea mpaka pale yule mtoto alipokuwa amelazwa juu ya majani ya migomba, akionesha kuwa kwenye hatua za mwisho kabisa za uhai.

Baba alinipa ishara kwamba tuiname pale yule mtoto alipokuwa amelala, mkono mmoja akamshika yule mtoto, mwingine akampa baba yake Rahma ambaye naye mmoja alimshika yule mtoto na mwingine akanipa mimi, na mimi nikafanya hivyohivyo.

“Usifumbue macho mpaka tutakapokwambia, dawa zako zote si unazo maana ndiyo tunaondoka hivyo,” alisema baba, nikatingisha kichwa kama ishara ya kukubali, akahesabu mpaka tatu, sote tukafumba macho.

Baba na baba yake Rahma walianza kuongea maneno fulani nisiyoyaelewa kwa kurudiarudia, wakawa ni kama wanaimba mapambio ya kutisha, mara upepo mkali ukaanza kuvuma kwa nguvu, sikuelewa tena kilichoendelea mpaka niliposikia nikitingishwa begani.

“Tumeshafika, mbona unazubaa,” alisema baba, kufumbua macho, nikashtuka nipo eneo lingine tofauti kabisa, nikageuka huku na kule, kumbukumbu zangu zikanijia kwamba hapo ndiyo pale ambapo usiku uliopita tulikuwa tumekusanyika. Nilitazama huku na kule, hata sura za watu karibu wote zilikuwa zilezile, nikamuona mkuu amekaa katikati kabisa, huku akiwa anajitafuna mapengo kama wanavyofanya watu waliozeeka sana.

Japokuwa huko kote tulikotoka nilikuwa nimevaa nguo zangu, nilishangaa kujikuta eti nimevaa kaniki kama ilivyokuwa jana yake, kila kitu kilikuwa ni zaidi ya maajabu.

“Mpeleke mpaka pale kwenye kile kichanja ulichokuwa umelazwa jana kisha sikiliza maelekezo kutoka kwa Mkuu,” baba aliniambia kwa sauti ya chini, yeye na baba Rahma wakaenda kukaa kule pembeni walikokuwa wamekaa wale watu wengine na kutengeneza duara.

Nilimbeba yule mtoto ambaye kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kuyoyoma ndivyo mapigo yake ya moyo yalivyokuwa yakizidi kufifia huku akianza kulegea, nadhani ni kwa sababu ya kupoteza damu nyingi. Watu wote walikua kimya kabisa, nikambeba mpaka pale nilipokuwa nimelazwa jana yake, kwenye kitanda kilichotengenezwa kwa miti.

Mkuu alisimama na kusogea pale kwenye kile kitanda, akanionesha kwa ishara kwamba nimgeuzie kichwa upande wa Magharibi, nikafanya hivyo kisha akasogea na kumgusa kifuani, nadhani alitaka kuhakikisha kama bado hajakata roho.

Nilimuona akitingisha kichwa kisha akainua mikono juu, watu wote wakapiga makofi kwa wingi, sikuelewa lakini nadhani ilikuwa ni kama sehemu ya kunipongeza. Watu wote walipotulia, bila kusema chochote, alinionesha ishara kwamba niendelee, nikakumbuka maneno ya baba kwamba akinipa ishara, maana yake anataka nimchinje mtoto huyo.

Tangu nizaliwe, sikuwahi kuchinja hata kuku tu, achilia mbali ndege tuliokuwa tukiwawinda kule kijijini kwetu lakini sasa eti nilikuwa natakiwa nimchinje binadamu, mtoto asiye na hatia yoyote ili nifaulu mtihani na kuwa mwanachama kamili, nilijikuta nikitetemeka kuliko kawaida.

Nilikichomoa kisu pale kiunoni nilipokiweka, mikono ikawa inatetemeka kuliko kawaida, nikawa namtazama mtoto yule usoni, nilijikuta nikiingiwa na huruma isiyo ya kawaida.

Je, nini kitafuatia?
 
Sehemu ya 46

ILIPOISHIA:

Tangu nizaliwe, sikuwahi kuchinja hata kuku tu, achilia mbali ndege tuliokuwa tukiwawinda kule kijijini kwetu lakini sasa eti nilikuwa natakiwa nimchinje binadamu, mtoto asiye na hatia yoyote ili nifaulu mtihani na kuwa mwanachama kamili, nilijikuta nikitetemeka kuliko kawaida.

Nilikichomoa kisu pale kiunoni nilipokiweka, mikono ikawa inatetemeka kuliko kawaida, nikawa namtazama mtoto yule usoni, nilijikuta nikiingiwa na huruma isiyo ya kawaida.

SASA ENDELEA…

Kisu kikadondoka na kwenda kujikita kwenye udongo. Nikamuona Mkuu akinikata jicho la ukali, akatembea kwa hatua zenye vishindo vizito mpaka pale nilipokuwa nimesimama, akainama kwa tabu na kukichomoa kile kisu, akanishikisha mkononi.

Baada ya hapo aliingiza mkono kwenye kimkoba chake kidogo cha ngozi, akatoa kichupa kilichokuwa na ungaunga mweusi, akamimina kwenye viganja vya mikono yake kisha akanipulizia usoni bila kusema chochote, nikapiga chafya mbili mfululizo kisha nikaanza kuona kama akili zangu zinabadilika jinsi ya ufanyaji kazi wake.

Hata sijui nini kiliendelea lakini baadaye akili zangu zilipokuja kukaa sawa, nilikuwa nimeshika kisu kwa nguvu huku mwili wangu ukiwa umetapakaa damu, watu wote wakawa wanashangilia kwa nguvu.

Yule mtoto hakuwepo tena pale kwenye kile kitanda cha miti, nadhani alishaondolewa maana niliwaona watu wengine kadhaa wakiwa wamezunguka pale ambapo jana yake palikuwa na furushi la nyama, wakawa ni kama kuna kazi wanaifanya, hakuna hata aliyegeuka nyuma.

>>Usiache kutembelea Simulizi za Majonzi

Mkuu alinisogelea huku uso wake ukiwa na tabasamu pana, sikuwahi kumuona akiwa na furaha kama aliyokuwa nayo, akaja na kunishika kichwani kama mtoto anavyomsalimia mkubwa wake, akanishika pia kifuani kisha akainama na kunishika vidole gumba vya miguu.

Alipoinuka, alifungua kimkoba chake, akatoa hirizi nyeusi na kunifunga kwenye mkono wa kushoto, akaniambia kwamba hicho ndiyo kitambulisho na silaha yangu na kwamba maelekezo mengine nitapewa na watu walionizidi, watu wote wakapiga makofi kwa nguvu na kuanza kuimba nyimbo za ajabuajabu huku wakicheza kwa mtindo ambao hata sikuuelewa.

Nilimuona baba akija mpaka pale katikati, akatoa salamu kwa Mkuu kisha akanikumbatia kwa nguvu. Hakujali zile damu nilizokuwa nazo, akakichukua kile kisu na kukifuta damu kisha akakichomesha kwenye mshipi wake kiunoni, akanishika mkono huku akiendelea kucheza sawa na wale watu wengine, akanipeleka mpaka sehemu aliyokuwa amekaa yeye na baba yake Rahma.

Sauti ya pembe la ng’ombe ilisikika kisha watu mbalimbali wakaanza kuja pale nilipokuwa pamoja na baba na baba yake Rahma, wakawa wananisogelea kisha wanainamisha vichwa vyao kama ishara ya heshima.

Baba aliniambia kwamba hiyo ni ishara ya kukaribishwa kwenye ulimwengu wao na kila mwanachama mpya anayetimiza masharti, huwa anafanyiwa hivyo. Waliendelea kuja kwa wingi lakini wengi sura zao zilikuwa ngeni kabisa kwangu.

Kulikuwa na wazee, watu wa makamo, vijana kama mimi na watoto wadogo, wanaume kwa wanawake. Wengine walikuwa ni wasichana wazuri tu ambao wala usingeweza kudhania kwamba nao wanahusika na yale mambo. Wengine walikuwa ni watu wazima wenye heshima zao.

Unajua watu wengi huwa wakisikia neno ‘mchawi’, tafsiri ambayo wanaijenga vichwani mwao, ni mtu fulani wa ajabuajabu, anayetisha, aliyezeeka au aliyedhoofika mwili. Ukweli ni kwamba mchawi hana alama, mwingine unaweza kuwa unamuona kama bosi fulani, au mwingine unamuona kama msichana mrembo, mzee wa heshima au mtoto mdogo lakini kumbe akawa anahusika na mambo hayo.

>>Usiache kutembelea Simulizi za Majonzi

Wakati wakiendelea kuja, mara nilimuona Isri akitokezea, akanitazama na mimi nikamtazama, tukatazamana kwa sekunde kadhaa, tukio ambalo baba aliliona ‘mubashara’, akanigeukia na kunitazama usoni, nikaacha kumtazama Isri na kumtazama baba kisha harakaharaka nikakwepesha macho yangu.

Isri alisogea mbele kisha akainamisha kichwa kama wale wengine wote kisha tararibu akaondoka na kutoa nafasi kwa watu wengine kuendelea na zoezi hilo. Zoezi likaendelea na baadaye, nilishtuka kuziona sura za watu ambao niliwakumbuka vizuri.

Wa kwanza alikuwa ni yule bibi kizee aliyenizabua kibao siku nilipokuwa mahabusu, usiku walioingia na kuanza kuwanga ndani ya chumba cha mahabusu. Nakumbuka siku aliponipiga na kunisababisha maumivu makali, nilijiapiza kwamba siku nitakayokutana naye lazima nilipize kisasi.

Wakati akinisogelea, nilitazama kushoto na kulia, baba akawa ameshajua ninachotaka kukifanya, akanionesha ishara kwamba sitakiwi kufanya chochote. Yule bibi naye ni kama alinikumbuka, aliponitazama vizuri usoni akawa ni kama ameshtuka, akasogea kwa kujihami na kutoa ishara kwangu huku akinitazama kwa macho ya kuibia, moyoni nikajiapiza kwamba ipo siku yake lazima nilipe kisasi.

Nyuma yake alikuwa ameongozana na wale watu wote alioingia nao siku ile mahabusu, wote wakawa wananitazama kwa macho yenye ujumbe fulani, mwisho akatokeza yule ambaye nilisababisha akanasa ndani ya mahabusu kisha mimi nikatoka kimiujiza.

Tofauti na wenzake wote, huyu alionesha kuwa na hasira na mimi maana jicho alilonikata, mpaka nilijishtukia, baba na baba yake Rahma wakawa wanacheka. Ni kama walikuwa wanajua kila kitu kinachoendelea. Basi pilikapilika ziliendelea kama kawaida, ukafika muda wa chakula ambapo sikuogopa sana kama siku ya kwanza.

Baada ya hapo, ulifika muda wa kucheza ngoma za kienyeji na baadaye tulitawanyika, sikujua nimefikaje nyumbani lakini nilichokuwa nakikumbuka ni kwamba baba na baba yake rahma walinishika mikono, wakawa wanaagana na wenzao na muda mfupi baadaye, nilijikuta nikiwa kwenye kona ya chumba nilichokuwa nalala.

Ni hapo ndipo nilipopata muda wa kutosha kuanza kutafakari kilichotokea, nilijihisi kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo wangu na nikajiapiza kwamba lazima asubuhi niende Kibaha kufuatilia taarifa za ile ajali na kuona nini hasa ambacho watu wengine watakiona.

Sikupata hata lepe la usingizi, nikawa najiuliza maswali mengi yasiyo na majibu, mara kwa mara nikawa naitazama ile hirizi niliyopewa na Mkuu na kuvalishwa kwenye mkono wangu. Ilikuwa nyeusi tii, ikiwa imefungwa kwa kamba nyekundu.

Kwa kuwa muda ulikuwa umeenda sana, muda mfupi baadaye kulianza kupambazuka, kwa kuwa sikuwa nimelala kabisa, nilienda bafuni kutaka kujimwagia maji kupunguza uchovu lakini ghafla nilikumbuka kwamba baba aliniambia sitakiwi kugusa maji kwa muda wa siku saba.

Ikabidi nijifutefute tu usoni na miguuni na kwenye yale madoa ya damu kisha nikarudi chumbani kwangu, nikaanza kujiandaa kuelekea Kibaha. Sikuwa na nauli na sikutaka kumuaga mtu yeyote, nilitaka kwenda kujionea nini hasa kilichotokea.

Wakati natoka kwa kunyata, nilipitia sebuleni, nikafungua droo ambayo wenyeji wetu huwa wanaweza chenji zinazobaki kwenye manunuzi yao, niliijua kwa sababu mara kadhaa nilimuona Rahma akichukua fedha, nikachukua noti mbili za shilingi elfu mojamoja, nikanyata na kutoka mpaka nje.

Tofauti ambayo niliiona dhahiri, safari hii nilikuwa najiamini sana, sikuwa Togo yule wa saa chache zilizopita, mara kwa mara nikawa najishika pale mkononi kuhakikisha kinga yangu ipo sehemu yake.

Nilipofika mita kadhaa kutoka kwenye geti kubwa, nilimuona yule kijana aliyekuwa akinicheka mara kwa mara kwamba eti mimi ni muuaji. Nilikumbuka maneno aliyoyatoa jioni iliyopita wakati nikiwa na baba na baba Rahma tukielekea kule eneo la tukio, nikaona huo ndiyo muda muafaka wa kumaliza hasira zangu.

“Broo vipi unaenda?” alisema huku akisimamisha Bajaj yake jirani kabisa na pale nilipokuwa nimesimama, nadhani kwa sababu ya kigiza kile cha alfajiri hakuwa ameniona vizuri, aliniponisemesha na mimi kumtazama usoni, niliona jinsi alivyoshtuka, akataka kuondoa Bajaj yake haraka lakini alishachelewa.

Je, nini kitafuatia?
 
Sehemu ya 47


ILIPOISHIA:

“Broo vipi unaenda?” alisema huku akisimamisha Bajaj yake jirani kabisa na pale nilipokuwa nimesimama, nadhani kwa sababu ya kigiza kile cha alfajiri hakuwa ameniona vizuri, aliniponisemesha na mimi kumtazama usoni, niliona jinsi alivyoshtuka, akataka kuondoa Bajaj yake haraka lakini alishachelewa.

SASA ENDELEA…

Nilishika bomba la Bajaj yake na kuingia, nikakaa siti ya nyuma, akawa ni kama amepagawa maana hakujua kama akimbie na Bajaj au aiache akimbie kwa miguu.

“Simama kwa usalama wako,” niliongea kwa sauti ya mamlaka, nikamuona jinsi alivyokuwa akihangaika, kijasho chembamba. Hakuwa tayari kusimama, inaonesha alikuwa akiniogopa sana, nilichoamua kukifanya ilikuwa ni kumtumia kutimiza mahitaji yangu.

Nilivuta pumzi ndefu na kuzibana kama baba alivyonielekeza, nikaweka utulivu kidogo kisha nikamuamrisha kunipeleka Ubungo. Nilifanya hivyo kwa kuzungumza moyoni maana ndivyo nilivyoelekezwa, nikamuona akizidi kuichochea Bajaj yake.

Hata hivyo, njia aliyokuwa anapita, ilikuwa ni ileile tuliyoipita jana wake wakati tukielekea Ubungo kupanda magari ya kwenda Kibaha. Alizidi kuongeza kasi, akawa anakimbia kama mshale, mwenyewe alidhani ananikimbia lakini kumbe tayari nilishaingia ndani ya akili yake.

Huwa si kawaida ya Bajaj kukimbia spidi kubwa na kuyapita magari lakini siku hiyo iliwezekana. Baada ya dakika kadhaa za kukimbia kwa kasi kubwa kwenye lami, hatimaye tuliwasili Ubungo, nikavuta tena pumzi na kumpa amri ya kusimama kwenye kituo cha mafuta.

Kilichonishangaza hata mimi, kweli alipunguza mwendo bila mimi kusema kitu chochote, akaiacha barabara kubwa ya lami na kuingia kwenye kituo cha mafuta, nikapeleka mkono wangu kwenye ile hirizi niliyokuwa nimevaa mkononi, nikanuiza maneno kwamba sitaki kuonekana.

“Jamani msaada! Nisaidieni washkajiii,” nilishangaa yule dereva Bajaj akipaza sauti, akazima Bajaj na kushuka huku akikimbia, akaenda kujichanganya na madereva Bajaj wenzake wanaopaki Ubungo, akawa ni kama anawaelekeza kitu fulani huku akihema kwa nguvu.

>>Usiache kutembelea Simulizi za Majonzi

Sikutaka kupoteza muda, kwa sababu nilishakuwa na uhakika kwamba hakuna mtu anayeniona baada ya kufuata maelezo yale niliyofundishwa, niliteremka kwenye Bajaj na kusimama pembeni nikitaka kuona nini kitatokea.

Vijana kama kumi hivi waliongozana naye mpaka pale kweye Bajaj kuja kujionea kuna nini kimetokea.

“Yuko wapi?”

“Alikuwa amekaa siti ya nyuma.”

“Siti gani ya nyuma?”

“Hee! Au ameshuka nini?”

“Nani ameshuka? Mbona sisi muda wote tunakuangalia tangu umefika na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada hatujaona mtu yeyot akiteremka kwenye Bajaj?” alisema kijana mwingine ambaye alikuwa amesimama jirani kabisa na pale mimi nilipokuwa nimesimama.

Mjadala mkali ukazuka, yule dereva Bajaj akikazania kwamba ni kweli kuna mtu alikuwa amembeba kwenye Bajaj yake na alikuwa akitaka kumuua, wenzake wakawa wanamshikia bango amuoneshe huyo mtu.

“Hizo bangi mnazovuta bila kula ndiyo matatizo yake haya!” alisema dereva mwingine na kusababisha wenzake wacheke, wakaanza kutawanyika huku kila mmoja akionesha kumpuuzia. Nilikuwa na uhakika kwamba hakuna mtu yeyote aliyeniona na ndiyo maana hata pale nilipokuwa nimesimama, watu walikuwa wakinipita tu bila kuonesha dalili yoyote kwamba wameniona.

Nilishangazwa sana na kilalichokifanya yule dereva Bajaj, kwa tafsiri nyepesi, kama kweli wale watu wangenikuta kwenye Bajaj ile, nini kingetokea? Bila shaka wangenidhuru wakiamini mimi ni mhalifu, nikaamua kumkomesha zaidi.

Nilisubiri aingie kwenye Bajaj yake, akaiwasha huku mara kwa mara akigeuka nyuma, na mimi nikaingia lakini nikiwa bado nimeishika ile hirizi ya mkononi, kwa hiyo nikawa sionekani. Alipotoka na kuingia barabarani tu, niliachia ile hirizi, akageuka na kushtuka kuona nimekaa palepale kwenye siti ya nyuma, akaanza kuchachawa.

Nilivuta pumzi ndefu na kuzishikilia kisha nikamuamuru kunipeleka Kibaha, nikashangaa akikata kona kali katikati ya barabara, magari mengine yakawa yanapiga honi kwa nguvu an kufunga breki, akavuka kwenye taa za kuongozea magari kwa kasi kubwa, almanusura tugongwe na magari yaliyokuwa yameruhusiwa na taa. Kila mtu alibaki amepigwa na butwaa kwa jinsi Bajaj ilivyovuka kwenye taa zile, akawa anakimbia kwa kasi kubwa kuliko kawaida. Kila alipokuwa akigeuka na kuniona nimetulia kwenye ile siti, ndivyo alivyokuwa akizidi kuongeza kasi.

>>Usiache kutembelea Simulizi za Majonzi

Ikafika mahali Bajaj ikaisha mafuta, nilichoamua ilikuwa ni kumtesa tu, akapaki Bajaj yake pembeni ya barabara, mimi nikashika ile hirizi yangu, nikawa sionekani tena, akashuka na kwenda kusimama mbali kabisa, akionesha dhahiri kuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake.

Niliamua kushuka kwenye Bajaj yake lakini nikajiapiza kwamba bado hatujamalizana, nilitembea kwenda mbele kidogo kwenye kituo cha daladala, tayari kulishaanza kupambazuka. Nikaiachia ile hirizi yangu, nikajichanganya na abiria wengine. Muda mfupi baadaye, gari lilikuja, nikawa wa kwanza kupanda, abiria wengine nao wakapanda.

Tukiwa ndani ya gari safari ikiendelea, mjadala kuhusu ajali iliyotokea usiku, ambayo ndiyo hasa iliyonifanya nifunge safari ile bila kumwambia mtu yeyote ilianza. Abiria mmoja aliamnza kusimua kwamba usiku yeye alikuwa akisafiri kutoka Mlandizi kuelekea jijini Dar es Salaam alipokuta ajali hiyo mbaya na ya kutisha, akaendelea kueleza kwamba aliyepata ajali alikuwa jirani yake, Mlandizi.

Mpaka hapo nilishapata sehemu ya kuanzia kwa sababu nilitaka nifike eneo la ajali lakini pia niende mpaka msibani nikajionee hali halisi. Alieleza jinsi ajali yemnyewe ilivyokuwa ya kutatanisha hukuakieleza kwamba mtoto alikufa palepale huku maiti yake ikiharibika vibaya kiasi cha kutotambulika na mama yake alikuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Tumbi, hali yake ikiwa mbaya.

Nilizidi kupata taarifa nyingi zaidi, lakini moyoni nikawa najiuliza hiyomaiti wanayosemaimeharibika vibaya ni ipi wakati nakumbuka mimi ndiye niliyeenda kuweka mgomba pale kwenye siti aliyokuwa amekaa yulemtoto na kuweka kipande cha mgomba?

Mjadala uliendelea, kila mtu akawa anasema lake lakini kikubwa walichokuwa wakikizungumza wengi, ni kwamba eneo ilipotokea ajali hiyo limekuwa na mauzauza mengi katika siku za karibuni, kwani hakuna mlima, mteremko wala korongo lakini magari yanap[ata ajali za kustaajabisha.

“Naskia kuna mtumishi wa Mungu kutoka Nigeria anakuja wiki ijayo na atafika pale kufanya maombi,” alisema dereva, abiria wote wakawa wanaunga mkono hoja hiyo. Nilichopanga kichwani, ni kuchukua maelekezo vizuri kwa yule mtu aliyesema marehemu ni jirani yake kisha kwenda kwanza mpaka eneo la ajali na baada ya hapo, nitakwenda Tumbi kujionea hali ya mgonjwa na hiyo maiti kama nitapata nafasi. Nilikuwa na shauku kubwa ya kujua kila kitu maana moyo wangu ulikuwa na hatia kugbwa, hasa kutokana na jinsi taarifa za ajali ile zilivyowaumiza mioyo abiria wengi.

Je, nini kitafuatia?
 
Humu tunakimbiza mwizi Kimya Kimya …
Tucheck watu wa kuwaita.

Bonge la story mkuu

Huwa nachungulia huku per day kama nimebandika maharage
 
Back
Top Bottom