SEHEMU YA 48 & 49
Katika maongezi yao, ingawa walipenda sana kuzungumza kisukuma, nilibaini kuwa mmoja wao alikuwa ‘
akida’ ambaye ni mwakilishi wa serikali katika kaya mbili tatu za eneo hilo. Wale wengine walikuwa wasaidizi wa ‘
Mwanangwa’ aliye msaidizi wa Chifu. Aidha, nilibaini kuwa jukumu walilopewa na chifu lilikuwa la kukamatwa kijana au vijana wenye umri wangu na kuwakabidhi kwake. Hakuna kati yao aliyefahamu Chifu alimhitaji kijana huyo kwa lipi, nilibaini kupitia maongezi yao.
Laiti wangefahamu hofu iliyonishika kwa taarifa hiyo, nina hakika kuwa watekaji wangu hao wangenihurumia na kuniacha niendelee na hamsini zangu badala ya kunipeleka kwa mtemi huyo. Hawakujua kuwa nilitoroka nyumbani kuja Uhayani kwa ajili ya Watemi haohao ambao walitaka kunitoa kafara ili kuleta mvua! Hivyo, ni dhahiri kuwa hawakujua pia kujihusisha na mtu yeyote mwenye madaraka au mamlaka ya Utemi au Uchifu kwa namna yoyote ile, kwani lolote lingeweza kutukia.
Nilitetemeka! Machozi yalinilengalenga. Kwa bahati nilikuwa nyuma yao, hawakuiona hali yangu. Nikaamua kujikaza huku nikianza kubuni njia za kutoroka mara itakapotokea fursa yoyote ile.
Wakati huo kichwa changu kilikuwa kikijiuliza maswali mengi kuliko majibu. Inawezekana kuwa mganga mwingine ametabiri shida ya mvua na kupendekeza kafara ya binadamu ambaye ameondokea kuwa mimi tena? Au watu weupe huko kwao wamenzisha vita nyingine kubwa kama ile iliyoitwa vita kuu, ya mwaka 1914 hadi 1918 ambayo waliwakamata babu zetu kwenda kuwasaidia bila khiari yao? Au ameibuka Mtemi Milambo mpya, aliyewachachafya sana Waarabu na
kuwakomboa mateka wao hadi alipofariki 1884, ambaye Mwingereza ameona hana jinsi ya kumshinda bila vijana wenye asili yake? Au kazi ya ujenzi wa reli ya kati, uliokamilika mwaka 1914 imeibuka tena hivyo wanahitajika manamba wenye damu changa?
Nilijiuliza mengi. Hadi tunafika katika himaya ya Mtemi au Chifu Masanja mwana Kasanga, sikuwa na jibu lolote zaidi ya mzigo wa hofu, mshangao na mashaka tele kichwani.
Mapokezi niliyoyapata katika himaya hiyo yalikuwa muujiza mwingine. Nilipelekwa moja kwa moja katika nyumba ambayo baadaye nilifahamu kuwa ilikuwa ya mke mkubwa wa Chifu. Mmoja kati ya wake zake kumi, ambao kila mmoja alijengewa nyumba yake na kuishi na wasaidizi wake, wake kwa waume, jambo lililoufanya mji huo wa Chifu kuwa kama kijiji kidogo chenye watu wapatao mia mbili hivi. Ng’ombe mia saba, mbuzi elfu moja, kuku, bata na njiwa wasio na hesabu walifanya kijiji hicho kiwe kama mji mdogo ndani ya mji.
Mama Chifu, mtu mnene wa maungo, ambaye mvi zilianza kumeza sehemu kubwa ya nywele zake fupi, alinitazama kwa makini kwa dakika mbili au tatu. Akatikisa kichwa. “Mara akawageukia wale walionikamata na kuwauliza, “Kwa nini mmemfunga kamba?” hakusubiri jibu lao, “Mfungueni mara moja,” aliamuru, amri ambayo ilitekelezwa mara moja.
“Chifu amepumzika,” mama huyo aliongeza. “Hapendi kuamshwa katika usingizi wake wa mchana. Kijana huyu amefika. Mwache aoge, ale, alale. Kesho ataonana na Chifu.”
Watekaji wangu waliondoka zao. Wasaidizi wa mama huyo wakapokea jukumu hilo. Nilitayarishiwa maji ya moto, ambayo sikupata kuyaoga kwa muda mrefu. Nilipotoka kuoga nilipewa ugali mkubwa kwa kuku mzima. Niliula karibu wote.
Nikaushushia kwa kibuyu cha maziwa ambayo pia nilikuwa na hamu nayo. Baadaye nilionyeshwa chumba cha kulala ambacho kilikuwa na kitanda chenye godoro la sufi.
Kama haya ni maandalizi ya kunitoa kafara, kwa fadhila hii niko radhi! Niliwaza wakati nikijibwaga kitandani na kuchukuliwa na usingizi mnono uliofanya nisahau shida za mkesha, uchovu na malazi mabaya ya muda mrefu katika safari yangu hiyo.
* * *
Sikuonana na Chifu hadi baada ya siku tatu. Zikiwa siku za kula vizuri, kulala vizuri na kupumzika, huku tayari nimepewa nguo na viatu vipya, nywele zangu zikiwa zimekatwa vizuri, nilimwona Chifu akinitazama kwa makini kabla ya kutikisa kichwa kama alivyofanya mkewe na kisha kutabasamu.
Nilikuwa nimepelekwa kukutana naye katika ‘
Ikulu’ yake, chumba kikubwa chenye viti vipatavyo mia moja vilivyoelekea kwenye kiti chake cha enzi, ambacho kilichongwa kwa mbao za mpingu na fundi anayejua kila aina ya nakshi. Sehemu kubwa ya kiti hicho kilimeremeta kwa aina fulani ya mawe ambayo baadaye nilikuja kufahamu kuwa ni almasi.
Chifu alikuwa amekikalia kiti hicho, mimi nikiwa nimesimama wima mbele yake. Tulikuwa wawili tu chumbani humo baada ya walinzi ambao huwa wako nyuma yake siku zote kuamriwa kuondoka.
“Karibu mwanangu!” Chifu alitamka baada ya kunitazama kwa muda mrefu. “Karibu katika himaya ya Masanja mwana Kasanga, Msukuma halisi aliyewashinda wavamizi na wahamiaji wote. Jisikie uko nyumbani.”
Nilitikisa kichwa kumkubalia ingawa nilikuwa sijamwelewa.
“Hata hivyo, ningependa kukufahamu vizuri, wewe ni nani, kabila gani, ulikuwa ukitokea wapi na kwenda wapi kabla vijana wangu hawajakuleta hapa?” Chifu aliniamuru. Sauti yake ilionyesha upole na upendo kama ya mkewe. Ikanitia moyo.
Nilieleza ukweli juu ya kwetu, Buha, ambako nilizaliwa na kukulia. Kwa hofu kuwa ule mweleka ulikuwa umemwua padri Backhove na kwamba habari za kifo chake zilikwishawafikia huku, nilidanganya juu ya maisha yangu ya elimu. Nilimwambia Chifu kuwa ingawa nilifuata elimu huko kwa Wahaya niliishia kuvua samaki katika ziwa kwa kukosa mtu wa kunisomesha.
Kwa mshangao wangu habari hiyo ilimfurahisha sana Chifu. Alipotabasamu, akacheka kabla hajakohoa kwa kupaliwa na kicheko chake. Baadaye alisema, “Mungu amekuleta nyumbani, upate elimu uliyokuwa ukiitafuta. Utasoma shule ya watoto wa Machifu. Kama ubongo wako unachemka barabara utafika hadi Ulaya. Utakuwa Cheyo lakini Cheyo ataendelea kuwa Cheyo.
Sikumwelewa. Nikamtumbulia macho ya mshangao na kutoamini, macho yaliyojaa maswali ambayo Chifu aliyaona na akaamua kuyajibu, “Nitakuibia siri moja. Nataka ibakie siri, kati yangu na wewe tu. Unaweza kutunza siri?”
Nilikubali.
“Pamoja na umri huu,” Chifu alisema. “Pamoja na kuwa na wake tele hadi leo nimejaliwa kupata mtoto mmoja tu, wa kiume. Anaitwa Cheyo. Tena ana umri kama wako.” Alisita kidogo kabla hajaongeza, “Himaya yangu iko mashakani. Nikifa himaya itapotea mali zangu zitaparanganyika. Hivyo, walipokuja wazungu kutaka kumchukua mwanangu huyu wa