Jibu langu lilimshangaza Jane, “Kwani unatokea wapi?”
Sikuona sababu ya kumficha, “Jela.”
Kiasi nilimwona akishtuka. Lakini, akiwa mwanamke mwenye roho ya chuma, anayeweza kuishi na kuvumilia hasira za ghafla za wanyama hatari kama sokwe, alijirekebisha mara moja. Badala yake aliniuliza kwa upole, “Nini kilitokea?”
Alikuwa binadamu wa kwanza uraiani aliyetaka kujua masaibu yangu toka nilivyofungwa hadi kufunguliwa. Akawa binadamu wa kwanza niliyepata kumsimulia, kwa tuo, yote yaliyonitokea hadi nikatupwa gerezani kwa miaka mingi. Sijui kwa nini niliamua kuwa wazi kwake. Nadhani ni kwa kuwa sikuwa na shaka kuwa ni mtu mwenye huruma sana. Kama anaweza kuishi na sokwe…
Nilipofika sehemu ambayo nilimtaja Dakta Leakey kama mwajiri wangu pekee ambaye niliishi naye kwa muda mrefu nilimuona Jane akishtuka. Mara akanikatiza kwa kuuliza, “Leakey yupi?”
“Leakey unaemjua wewe. Na mke wake Mary… wagunduzi wa fuvu la kale zaidi nchini,” nilimjibu.
Jane aliinuka na kunikodolea macho ya mshangao. “Sasa nimefahamu wapi nilisikia jina lako kwa mara ya kwanza,” alisema baadaye.
“Wapi?”
“Kwa akina Leakey. Walikuwa hawaachi kukutaja. Walishangazwa sana na kutoweka kwako ghafla, bila kuaga, mtu ambaye walidai kuwa walimtegemea sana katika shughuli zao.”
Ikawa zamu yangu kushangaa, “Unawafahamu?” “Vizuri sana,” Jane alinijibu. “Walipata kuniajiri pia.
Kutokana na mapenzi yangu kwa wanyama na mazingira
Leakey alinishawishi kwenda kwenu Kigoma kufanya utafiti
wa wanyama wale, binamu zetu.”
Sikuwa na la kusema, nikauliza, “Hawajambo?” “Nani?”
“Akina Leakey.”
Jane akacheka, “Wazima sana. Kwa nini ulifanya vile?” “Kufanya nini?”
“Kufungwa.Kukubalikufungwabilakuwaarifu.
Wangeweza kukusaidia.”
Ilikuwa wazi kuwa Jane hajui maana ya kufungwa, hasa katika nchi zetu za dunia ya tatu. Mnyama anayefugwa ana uhuru mara mia zaidi ya mfungwa.
Wakati nikizungumza na Jane nilimwona msichana mmoja, msafiri kama sisi, akinitazama sana. Nilimtupia macho. Nikamwona akiyakwepa macho yangu kwa namna ya haya kiasi. Kitu fulani kilinifanya nipate hisia kuwa namfahamu. Wazo ambalo nililipuuza mara moja. Jana tu nimetoka jela, nitamjulia wapi msichana huyu?
Kitu kimoja kilinivutia kumtazama msichana huyu alikuwa ana tofauti kubwa na wasichana wengine wengi niliowaona jijini hapo. Alikuwa Mwafrika halisi. Nywele zake zilikuwa fupi, ambazo hazikupata kuathiriwa na madawa. Ngozi yake laini maji ya kunde, pia haikuwa na dalili zozote za kuathiriwa na madawa hayo. Hata mavazi yake yalikuwa ya heshima. Gauni jekundu lililomkaa vizuri lilimfunika hadi miguuni.