SHETANI RUDISHA AKILI ZETU
MTUNZI:SINGANOJR
SEHEMU YA 39.
Iliishia Hamza anapokea simu ya mwanamke ambae anaanza kwa kumuita Prince Rich.
Endelea sasa:
Hamza mara baada ya kusikia lafudhi hio ya uingereza alijua nani aikuwa akiongea kwenye simu.
“Don’t be coquettish Flora , you are already old enough to be my grandmother , how can I stand such coquetish words?”Aliongea Hamza kwa kingereza akiwa na tabasamu.
“Sio tabia nzuri kuongelea umri wa mwanamke kwa staili hio , wewe ni mkubwa kwangu lakini kwanini unanishambulia?”
“Kama unajua mimi ni mkubwa kwako basi unapaswa kuwa siriasi kidogo, halafu kumbuka kuniita Hamza Mzee ndio jina langu jipya ,usiniite majina ya zamani”Aliongea Hamza.
“Nimekuelewa , sasa uniambie Mr Hamza wapi tunakutana , nimekumisi mno”
“Kwasasa kuna mambo nataka kuyaweka sawa , tukutane jioni , tutapata chakula cha usiku pamoja , usije na walinzi wako sitaki attention”
“Nimekuelewa , hapa karibu na hoteli niliofikia kuna McDonalds , itakuwa vizuri tukikutana hapo”
“Naona umesafiri na uzungu wako mpaka Tanzania , hutaki kujaribu radha ya vyakula vya kitanzania?”
“Sio kama unavyofikiria ,nyumbani chakula changu ni cha kupimiwa sana na siruhusiwi kula vyakula vya madukani, nipo Tanzania nitakula kila ninachoona kinanifaa”
Hamza hakutaka kubishana nae, hivyo aliamua kumuacha afanye anavyotaka , aliuliziaa tu hoteli aliofikia na wakakubaliana muda wa kukutana na kisha akakata simu.
Baada ya hapo moja kwa moja Hamza alienda moja kwa moja mpaka kwenye idara ya mauzo , alihitaji kumpatia taarifa Eliza juu ya dokta ambae anapaswa kumwangalia mama yake amefika Tanzania.
“Kwanini upo hapa mapema yote haya?”Aliuliza Eliza mara baada ya Hamza kuingia katika ofisi yake.
Hamza hakutaka kupoteza muda alimsogela mrembo huyo na kisha alimshika kiuno na kumbusu mdomoni.
“Nimekumisi sana siku nzima ya jana na leo , nimekuja kukukiss?”
“Unimisi wapi , najua kabisa mpango wako ni kwenda kula chakula cha mchana na Yonesi, Asha ameniambia imekuwa ratiba yenu , lazima mkae meza moja kila siku kwa ajili ya chakula”Aliongea Eliza huku akionyesha dalili ya wivu.
“Sio hivyo Eliza, nimemuona Kapteni akila peke yake ki’upweke ndio maana ninampa kampanni , unaonaje tukifanya nae urafiki na kumchangamsha mara kwa mara”
“Huwezi kunipata mchana , muda mwingi natoka hivyo ni mara chache sana kuniona katika mgahawa wa kampuni”
Hamza mara baada ya kusikia jibu hilo alijikuta akivuta pumzi ya ahueni , alijiambia kama akikaa meza ambayo kuna Yonesi na Eliza kuna tukio baya lazima lingetokea.
“Niambie , najua una sababu ya kuja ofisini kwangu?”Aliongea Eliza
“Daktari niliekuambia nitamwita kuja kumwangalia mama yako tayari yupo hapa Dar , jioni nitaenda kuonana nae wakati wa chakula cha usiku , tunapaswa kwenda pamoja”
“Dokta amefika! , mbona hukuniambia nikafanya maandalizi ya atakapofikia, napaswa kumpa heshima yake kama mgeni wangu”
“Usiwe na wasiwasi maandalizi yashafanyika , unachopaswa ni kutangulizana na mimi tu , nitaenda chuo nikitoka huko nitakutaarifu”Aliongea Hamza na Eliza alitingisha kichwa kumuelewa.
Kwasababu muda umeenda Hamza alielekea chuo moja kwa moja kwa kutumia mwendokasi.
Asilimia kubwa ya wanafunzi wa mwaka wa pili na wa tatu walikuwa wanaelekea Field , kwa wanafunzi wa mwaka wa tatu walikuwa wakimalizia field yao ya mwisho.
Ijapokuwa Regina alikuwa akijua kuchagua nguo lakini nguo ambazo Dina alimvalisha Hamza zilikaa ki ujana zaidi na kumfanya Hamza kuvutia mno na swala hili lilimfanya kuangaliwa na wanafunzi wengi ambao alipishana nao.
Macho yao ilikuwa ni kama pale ambapo unadharau kitu ambacho mwanzoni hukujua ni cha thamani na mara baada ya kuokotwa na mwingine unaanza kuona thamani yake , hayo ndio macho ya wanawake warembo aliopishana nao Hamza.
Siku kadhaa zilizopita Hamza alionekana kuwa wa kawaida sana , kitu pekee ambacho kilikuwa kikimfanya kuonekana ni muonekano wake pekee wa kuchanganya rangi lakini hakukuwa na dalili yoyote ya Hamza kuwa mtu mwenye hela.
Sio kama Hamza hakuwa na hizo dalili ni kwasababu alikuwa katika jamii ambayo ilikuwa ni ya daraja la chini kuliko yeye hivyo hawakuweza kuona dalili ambazo zimejificha kama ilivyokuwa kwa yule mzungu alivyoitambua hadhi ya Hamza kupitia mavazi.
Hivyo Hamza karibia siku zote aliweza kufika chuoni hapo akiwa na mavazi ya bei ghali mno lakini hakuna mwanafunzi hata mmoja aliewahi kutambua, yale mavazi ambayo yalikuwa na chapa za makampuni makubwa ndio yalionekana ya thamani.
Hamza sasa siku hio alikuwa amevaa mavazi ambayo yalikuwa na chapa ya kampuni kubwa zenye jina duniani ndio maana aliteka macho ya watu wengi , saa tu pekee ambayo alivalia ilimfanya asionekane kinyonge.
Hata yeye mwenyewe alijua kwanini watu walikuwa wakimwangalia hivyo ilimfanya kutokujali lakini kwa wakati mmoja kujisikia vizuri kwa kuonekana , ni tabia ya kila binadamu kupenda kuonekana zaidi katika kundi la watu.
Hamza aliingia chuoni lakini tofauti na siku zote ni kwamba hakuweza kuonana na watu ambao alikuwa amezoeana nao , alikuwa maarufu lakini hakuwa na mazoea ya watu wengi.
Wakati akitaka kuelekea upande wa maktaba simu yake ilianza kuita na alipoangalia jina aljikuta akishangaa kidodo , alikuwa ni CR(Class representative) wake ndio aliekuwa akipiga , alishangaa kwasababu ndio amefika chuo na CR anampigia simu.
“Madam!Kwema?”Alipokea Hamza.
“Kwema Genious, nimekuona ukiingia geti la chuo nikakumbuka kuna mtu alikuwa akikutafuta”Sauti ya kike iliongea.
“Nani alikuwa akinitafuta Winnie?”
“Profesa Singano, aliniambia nikutaarifu jana lakini mambo yalikuwa mengi nikasahau, nenda ofisini kwake nadhani atakuwepo”Aliongea na upande wa pili ulionekana kuwa na haraka maana simu ilikatwa mara moja.
Hamza aliishia kujikuna kichwa na kujiuliza Mr Bonus point anamtafutia nini , lakini hata hivyo hakutaka kufikiria sana , alitii wito na kuanza kutembea kuelekea upande jengo la utawala.
Baada ya kupanda lift sekunde chache tu alikuwa nje ya ofisi ya Mzee wa Bonus pointi , kilichomchosha Hamza ni uwepo wa watu wengi ndani ya eneo hilo, ambao ilionekana walikuwa kwenye foleni ya kwenda kuonana na Profesa Singano.
Ilileta maana hata hivyo maana Profesa alikuwa ni Cordinator wa wanafunzi hivyo huwa inakuwa kawaida kukuta watu wengi wakitaka kuingia katika ofisi yake.
Hamza alikagua sura zilizokuwa katika eneo hilo na karibia zote zilikuwa ni za wanafunzi wa mwaka wa pili na mwaka wa tatu kozi tofauti.
Kwasababu alikuwa akiujua utaratibu hakuaka kuuvunja hivyo alikaa kwenye viti mwisho kabisa akisubiria zamu yake , hata hivyo kwa haraka haraka aliona angekaa hapo muda mrefu mno.
Zilipita dakika chache tu mwanafunzi alitoka , Hamza hata hakuwa bize kuangalia nani anaingia au anatoka , alikuwa amekza macho kwenye simu yake akiperuza peruza kwenye mtandao wa Jamiiforum , ni tabia yake hio hivyo haikumpotea kirahisi.
“Hi!”
Kabla ya kusikia sauti tamu ikimsalimia alichoanza kuhisi ni marashi mazuri ya kuvutia na Hamza aliinua macho yake na kumwangalia aliempa salamu , alikuwa ni Anitha, mwanamke ambae Hamza alishawahi kumtokea na akampiga chini kwa kuambiwa hana hadhi , ilishangaza siku hio mrembo huyo kuanza salamu kwenda kwa Hamza maana alikuwa akimdharau mno.
“Nimekusalimia Hamza”
Aliongea Anitha mara baada ya kuona Hamza ana mwangalia tu bila kumjibu , alionekana kuwa na muonekano wa kirafiki .
“Oh! Mambo mrembo?, nimeshangaa kidogo maana sio kawaida hii?”
“Sio kawaida nini?”Aliongea Anitha.
Ki ufupi Anitha alikuwa mwanamke mrembo haswa , dosari yake pekee ni miguu tu , alikuwa na miguu miembamba, ilikuwa ikivutia lakini haikuendana na umbo lake.
“Sio kawaida kupokea salamu kutoka kwako?”Aliongea Hamza huku akitabasamu.
“Itakuwa kawaida kwanzia sasa na kuendelea?”Aliongea huku akitoa tabasamu , lakini pia hakuacha kumwangalia Hamza kuanzia juu mpaka chini na macho yake yalikuwa yakionyesha wazi kile ambacho anafikiria.
“Salamu yangu kwako ilikuwa kama tusi , ulinipiga tofali kila kona , nini kimekupata ndani ya siku hizi chache , unaumwa?”Aliongea Hamza.
Ukweli Hamza kama angekuwa muigizaji angekuwa na kipaji kikubwa sana , kwa jinsi ambavyo alikuwa akionekana mbele ya Anitha alikuwa ni kijana wa kawaida sana mpole.
Kauli ile ya Hamza kiasi flani ilimfanya Anitha kujisikia vibaya kwa kuona aibu.
“Uliyasababisha wewe, unaongea kama vile hujui?”Aliongea huku akikaa chini kwenye benchi.
“Nimeyasababisha nini?”
“Kipi kilikufanya kunitongoza mbele ya mpenzi wangu , tena kwa kupiga magoti mbele za watu na kila mtu anaona?”Aliongea Anitha na kauli ile ilimuacha Hamza na mshangao.
Na alijiambia inamaana siku ile alivyoziweka wazi hisia zake kwa Anitha mpenzi wake alikuwa kwenye kundi la wanafunzi , lakini mbona hakuwa na habari.
“Ile siku hukuwa ukinitongoza , ulikuwa ukinidhalilisha , ni jaribio ambalo umefanya nionekane sio mwaminifu”
“Kwahio unachomaanisha , siku ile mpenzi wako alikuwepo , mbona sikuwa na habari kama una mpenzi ndani ya chuo?”Aliongea Hamza na kumfanya Anitha kumwangalia Hamza kwa usiriasi.
“Mpenzi lazima awe wa chuo tu?”Aliuliza na Hamza aliishia kushika pua.
“Kama lilikuwa jaribio la kukudhalilisha , niliishia kujidhalilisha mwenyewe , lakini kwanini unaongea kama vile unanilaumu , yale yashapita na nilipotezea”Aliongea Hamza huku akianza kuonyesha dalili ya kukosa uvumilivu wa kuendelea kuongea na Anitha, siku zote wanawake hawakosi sababu , alihisi pengine anadanganywa na Anitha ili apata gia ya kurudisha muda nyuma , lakini Hamza alikuwa na Eliza tayari hivyo hakumhitaji Anitha.s
“Ulipotezea au umenipotezea?”
“Vyote”Aliijibu Hamza na kumfanya Anitha kuvuta mdomo.
“Kwasababu tayari ushafanikiwa kupata mpenzi na anakupendezesha?”Aliongea huku akiangalia mavazi ya Hamza.
“Unamaanisha nini?, umejuaje nimepata mpenzi mzuri zaidi yako?” Hamza aliona huyu mwanamke ashaanza kuleta dharau.
“Huna haja ya kumsifia mbele yangu , ninachojua tu hamuendani”Aliongea na kisha alisimama lakini Hamza alimzuia.
“Nani siendani nae?”Aliuliza Hamza akiwa siriasi kidogo .
“Eliza!”Aliongea na kisha bila hata ya Hamza kuuliza zaidi amemjuaje Eliza mwanamke huyo aliondoka mbele yake, akionekana kabisa hajafurahishwa na Hamza kuwa katika mahusiano.
Hamza hakujua acheke wala alie,lakini hata hivyo hakutaka kujali sana , hakuwa na mpango tena na Anitha , kwanza hata kumtongoza kwake kupitia njia ya ile mpaka kukataliwa alikuwa kwenye majaribio ya uanaume bwege, kwenye maisha yake hajawahi kutongoza, yeye ndio aliekuwa akishobokewa na warembo.
Anitha haikueleweka alikuwa amemuona wapi Hamza na Eliza , lakini ilionekana wazi aliamini mabadiliko ya Hamza yalitokana na gharama za mwanamke , ni kama hakuwa akiamini kama Hamza anao uwezo wa kujinunulia mavazi ya bei ghali.
Hamza aliendelea kusubiri zamu yake ifike lakini muda ulikuwa ukienda na taarifa zilitolewa ambao wamebakia kuonana na Profesa wafike siku inayofuata.
Hamza alichoka kwenye mambo ambayo yalikuwa yakimchoka kwenye maisha yake ni kupanga foleni, lakini hata hivyo alishukuru maana ilikuwa ni muda wa chakula cha mchana na mpango wake ilikuwa ni kwenda kula kazini.
Lakini sasa wakati akijiandaa kutoka Profesa Singano alitoka nje na alikuwa ametangulizana na mama mmoja ambae Hamza alimtambua ni Sekretari.
“Mr Hamza!”
Profesa Singano aliita , Hamza alikuwa akifahamika na karibia walimu wake wote , hio yote ni kutokana na uwezo wake darasani , alikuwa ndio kichwa tokea akiwa mwaka wa kwanza.
“Yes!, Good afternoon Professor!”Alisalimia Hamza, huwa ilikuwa ngumu sana kwake kusema shikamoo hivyo mara nyingi alikuwa akitumia salamu ya kingereza.
“Good afternoon ,I’ve been expecting you”Aliongea Profesa akimaanisha alikuwa akitarajia ujio wake baada ya kumuita.
“Niwie radhi profesa , nilichelewa kupata taarifa za wito wako”
“Hakuna shida , wanafunzi wengi hampo maeneo ya karibu ni kawaida kuchelewa kupokea taarifa, huu ni muda wa mchana , unaonaje ukiungana na mimi kwenda kupata chakula cha mchana ili nikuambie na dhumuni la kukuita?”Aliongea Profesa na Hamza alisita kidogo.
“Huna haja ya kuwa na wasiwasi bwana mdogo, gharama zitakuwa juu yangu”Aliongea Profesa na kumfanya Hamza kutoa tabasamu huku akitingisha kichwa kukubali.
Ukweli ni kwamba sio kama hakuwa na hela ya kulipa , ila kwasababu mpango wake ilikuwa ni kurudi kazini kula chakula cha bure aliona lazima ajihakikishie Profesa atalipia chakula chake.
Dakika kadhaa tu wote kwa pamoja walikuwa ndani ya mgahawa katika hoteli ya Peacock, ni sehemu ambayo maprofesa wengi walitumia kupata chakula maana ilikuwa mkabala na chuo , hata baadhi ya wanafunzi wa chuo waliingia ndani ya hoteli hio lakini ni wale ambao walikuwa na uwezo wa juu wa kifedha.
Hamza licha ya kujiuliza nini ambacho Profesa Singano anamtafutia , lakini alichowaza kwa dakika hio ni kuagiza chakula cha maana, sekretari ambae walitangulizana nae alionekana kwenda kuungana na wenzake.
“So, I’m sure you’re wondering why I called you?”Alianza maongezi mara baada ya oda zao kuchukuliwa.
“Ndio Profesa”
“Kwenye wiki hizi tatu nimepokea watu watatu tofauti tofauti waliofika chuo na kuulizia taarifa zako , ndio maana nimechukua uamuzi kukuita”
“Kweli!!, Ni wakina nani?”Aliuliza Hamza huku akionyesha mshangao.
“Sina uhakika sana , hawakuacha majina yao , ila kati yao kuna waliojitambulisha kutokea kampuni ya Zena”
“Zena!?”Aliuliza Hamza kwa mshangao kidogo na akili yake ilifanya kazi,hio ni kampuni ambayo ipo chini ya James.
“Ndio , unaifahamu?”
“Naisikia lakini sina mawasiliano na mfanyakazi yoyote wa Zena Profesa”Alijibu Hamza na kumfanya Profesa kumwangalia usoni kwa umakini.
“Haishangazi sana kufuatiliwa na watu wa kampuni ya Zena , wewe ni mwanafunzi namba moja katika kozi yako, walionyesha kuvutiwa pia na wewe na wamesema wanataka kukuingiza kwenye timu yao ya idara ya fedha”Aliongea Profesa na Hamza aliishia kujiwazia ndani kwa ndani, hakuna kitu kama hicho kampuni ya Zena kumtafuta kwa ajili ya kazi ni James huyo akihangaika kumchimba.
Ukweli ni kwamba haikuwa mara ya kwanza Hamza kufuatiliwa na watu wa makampuni , lakini yeye hakuwa na mpango wa kuajiriwa , kitendo cha kujiunga na chuo yalikuwa ni maagizo ya Mzee tu pekee, chuoni kwenyewe aliingia kimagumashi kwa kufoji vyeti vya elimu ya high school.
“Ni fursa kwangu hio Profesa , lakini kwasasa malengo yangu ni kufanya kazi ndani ya kampuni ya Dosam , napanga internship kuanzia huko moja kwa moja”
“Dosam ni kampuni nzuri , sio wazo baya”Aliongea na muda uleule wahudumu walichafua meza yao kwa vyakula na kumfanya Hamza kumeza mate kama vile chakula sio chake.
“Profesa kuhusu wengine waliokuja kunitafuta , hujawatambua wametokea wapi?”
“Wote walijitambulisha kwa namna inavyofanana , lakini kwa uzoefu wangu maswali waliouliza yalinifanya nione kuna la ziada”
“Kitu gani cha ziada?”
“Wameuliza sana taarifa zako za maisha ya chuo, na mambo mengi binafsi , kama ni waajiri haikuwa na haja ya kuuliza”Aliongea Profesa huku akionekana kumwangalia Hamza , ni kama kuna kitu ambacho alikuwa akitafuta.
“Unaonekana kutokuwa na wasiwasi?”
“Mimi kama raia mwema , nisiekuwa na ugomvi na mtu sidhani kama napaswa kuwa na wasiwasi”Aliongea Hamza huku akijiweka bize na chakula lakini upande wa Profesa aliona kabisa kuna kitu sio cha kawaida kutoka kwa Hamza.
Ukweli ni kwamba sio kwasababu ya Hamza kutafutwa na watu siku kadhaa bali ni tokea Hamza alivyojiunga chuo na matendo yake ya kila siku.
“Umejiandaaje na mtihani wako wa mwisho?”Aliuliza Profesa
“Ah , Nimejiandaa vizuri tu Profesa”Aliongea Hamza huku kidogo akijifanyisha kuona aibu za kizembe.
“Wakati unaanza chuo uliomba uongozi kutokukujumuisha na baadhi ya kazi za vikundi kwasababu ulikuwa ukijitafutia kipato , unaweza vipi kusoma na kufanya kazi kwa wakati mmoja na ukaendelea kushikilia namba moja ndani ya darasa?”.
“Profesa niseme tu sijawahi kusoma kabisa , uwezo wangu wa kutunza kumbukumbu ni mkubwa”Aliongea na kauli ile ilimfanya Profesa kushangaa kidogo lakini hata hivyo aliacha kuuliza maswali mara baada ya simu yake kuita.
Wakati wa kuongea na simu Hamza alijua nani alikuwa akiongea nae , ilionekana ni Prisila ndio anaongea na baba yake kwani mzee huyo alibadilika mara moja kutoka kuwa profesa na kuwa baba, ilionyesha ni dhahiri kiasi gani Prisila alikuwa na ukaribu na baba yake , Hamza hata hivyo hakujali sana maana hakuwa na ukaribu na Prisila ila alikumbuka alikuwa na deni na mrembo huyo.
Baada ya kumaliza kupata chakula aliachana na Profesa na aliamua kurudi maktaba ambako kama kawaida yake alipoteza muda kwa kufurahia AC na kuperuzi mitandaoni mpaka jioni ikamfikia ndani ya chuo.
Hamza mara baada ya kutoka alimpigia simu Eliza , miadi ya kukutana na Dokta Ronica ilikuwa ni saa kumi na mbili na nusu za jioni.
Kwasababu Hamza alikuwa mjini na Eliza nyumbani ilibidi amsubiri aje yeye wakutane njiani ndio waende.
Nusu saa mbele Hamza aliweza kukutana na Eliza na kuingia kwenye gari lake na walienda moja kwa moja kusimama mbele ya mgahawa wa McDonald’s kilomita chache kutoka ilipo Serena hotel.
“Sehemu ambayo tunakutana na huyo dokta ni ndani ya huu mgahawa?”Aliuliza Eliza kwa mshangao kidogo.
“Ndio , ni mpenzi wa mavyakula aina ya Hamburger na chipsi na kadri chakula kinavyokuwa cha bei rahisi ndio anaona ndio kitamu”
“Mh , chakula cha hapa ni cha bei rahisi?”
“Haha..Eliza uzunguni KFC na McDonalds ndio wanaunza chakula bei rahisi lakini chenye ubora , vyakula vya bei rahisi hapa Tanzania havina ubora wa kuzidi hii migawaha ya fastfood”
“Kwanini anafurahi kikiwa cha rahisi , ninachojua madaktari kutoka Ulaya na Amerika wengi wana kipato cha juu, kwanini rafiki yako anaonekana kama masikini?”Aliongea Eliza na kumfanya Hamza kucheka.
“Hey!, sio masikini kuna utofauti mkubwa wa kuzaliwa ukiwa tajiri na kuzaliwa masikini na kisha ukawa tajiri , yeye alizaliwa akiwa masikini lakini akaja kuwa tajiri , hivyo kuna radha ya vyakula vya bei rahisi havisahauliki na mara kwa mara lazima uvikumbuke , wengine sio kukumbuka tu ni kwasababu pia vinawakumbusha walikotoka”
“Nimelewa sasa yupo hapa sio kwa ajili ya kula chakula bali kwa ajili ya kujikumbushia mapambano yake?”
“Safi , hapo umepatia , wataalamu wa mauzo wengi mnajua kuelezea kitu kwa lugha rahisi na kueleweka , unakidhi kuwa meneja”Aliongea Hamza huku akishika shavu la Eliza.
“Wewe acha kunifanyia hivyo , tunangaliwa ujue”Aliongea Eliza huku akiona aibu za kike na Hamza alimuacha akiongoza njia.
Hamza mara baada ya kuingia ndani ya mgahawa huo aliweza kumuona mwanamke ambae ni mzungu mwenye nywele nyeupe(Blonde) na kavaa kofia ya chepelu , tisheti nyeupe na jeans.
Kwenye meza yake kulikuwa tayari na Baga(Burger) nne , soda ya Cocacola , glasi ya juisi na boksi mbili za chipsi.
Ukimwangalia ungesema ni mtu ambae alikuwa na njaa kwa muda mrefu maana mkononi tayari alikuwa ameshikilia Burger lakini kuna zingine ambazo hakuwa amegusa.
“Flora !!”Aliita Hamza huku akimshika mkono Eliza na kusogea nae upande wa alipo mwanamke huyo.
“Ugh!!”
Mwanamke huyo wa kizungu alishituka mara baada ya kuitwa jina hilo na kutokana na kubugia kiasi kikubwa cha baga aliishia kutoa chembechembe za mkate.
“Hamza why did you only just arrive?,I’ve been waiting for you guys for half an hour , I really can’t help but eat first.”Aliongea akimwambia Hamza kwanini ndio wanafika maana amesubiri kwa zaidi ya nusu saa na alikosa uvumilivu na kuanza kula.
“This burger with blu-thin mushroom is so delicious”Aliendelea kuongea.
“Unaongea nini wewe , mbona sijawahi kusikia Buga ya aina hio?”Ukweli ni kwamba Hamza hakuwa mpenzi wa mibaga hivyo hakuelewa alichokuwa akimaanisha Dr Flora Ronicas.
Hamza alimvuta mbele Eliza ambae alionekana kukaa kizembezembe na kumuweka mbele yake.
“Ngoja nikutambulishe , huyu ni Eliza niliekutajia , mama yake ndio mgonjwa unaekwenda kumtibia”Aliongea Hamza.
Upande wa Eliza alikuwa akimkagua mzungu huyo , kwa maelezo ya Hamza ni dokta kutoka Marekani lakini alivyokuwa akiongea ni tofauti kabisa na watu wa Marekani alionekana kuwa muingereza mwenye pua iliochongoka , kidevu chenye ncha na macho yenye kiini kilichopauka , alikuwa mwanamke mrembo wa kizungu ambae ungetamani kumwangalia mara mbilimbili na kwa uwezo wake wa kukadiria umri alijiambia pengine ana miaka ishirini hivi kwenda therathini.
“Hello , my name is Eliza Mlowe , Nice to meet you Dr Ronica”Aijitambulisha Eliza kwa kingereza , alikuwa ashamuuliza Hamza jina lake kabla ya kuingia.
Lakini mara baada ya kumuona daktari mwenyewe ambae alikuwa mrembo lakini vilevile anaekula sana , wasiwasi alikuwa nao kuamini kama huyo ndio daktari anaekwenda kumponyesha mama yake.
“Niite Flora tu , wewe ni mpenzi wa Hamza haina haja ya kuwa mpole kiasi hicho”Aliongea huku akiendelea kuwa bize na mkate wake.
Eliza masikio yalipata moto na kumwangalia Hamza , hakujua Hamza alikuwa ameenda mbali kumtambulisha kama mpenzi wake.
“Flora nimekuambia usijionyeshe sana lakini sio kujigeuza chokoraa , unadhani kula namna hio ndio kujificha?”
“Mimi mwenyewe nilikuwa sijui , ndio mara yangu ya kwanza kuja Tanzania na sikujua kama nina umaarufu , kufika tu simu zimeanza kuingia watu wanataka kuonana na mimi , sijui wamejuaje nipo Tanzania, lakini muda wa kuwajali sina , kama usingeniita ningekuwa zangu Rochester naendelea na utafiti”
Eliza mara baada ya kusikia hivyo alijiuta akishangaa na alimwangalia Hamza kwa maswali.
“Kwanini hukuniambia Dokta Flora ni maarufu hivyo , mimi nilijua ni daktari wa kawaida wa binadamu”
“Awe maarufu asiwe maarufu , wewe mchukulie kama rafiki yako , wewe ni wa kwetu kwanzia sasa haina haja ya kujiweka nae mbali”Aliongea Hamza na Eliza alifurahi kusikia hivyo.
“Dr Flora , umekwisha kupitia taarifa ya matibabu ya mama yangu , umeonaje?”
“Hali yake sio nzuri , lakini haimaanishi kwamba hana nafasi ya kupona , mpaka nitakapomfanyia uchunguzi ndio nitajua zaidi, taarifa ambayo mmenipatia haijazingatia vitu vingi hivyo ni ngumu kuwa na suluhisho, teknolojia ya tiba imeendelea ila kwa hapa Tanzania naona bado sana”
“Kwahio Dokta unamaanisha unaondoka na mama yangu kwenda Marekani moja kwa moja?”
“Ndio , mimi naondoka kesho kutwa , kuhusu mama yako utaratibu wa kusafirishwa utakamilika ndani ya wiki moja”Aliongea na Eliza baada ya kusikia hivyo alisita.
“Vipi kuhusu malipo ya gharama za matibabu na mahitaji mengine?”
“Kwasababu ya Hamza nitakutajia bei ya chini tu, unaonaje tukianza na Dollar milio…”
“Utalipia dollar elfu kumi ambazo ni sawa na milioni ishirini na tano za kitanzania”Aliongea Hamza akiingilia lakini kauli yake ilimfanya Dokta Flora mikono yake kutetemeka huku akimkazia macho Hamza.
“Milioni ishirini , kumbe rahisi hivyo?”Aliongea Eliza kwa mshangao , wakati anakuja hapo alikuwa akiwaza matibabu yatakuwa ni zaidi ya milioni mia moja kama mgonjwa wake atasafirishwa na alikuwa akiwaza kwenda kumpigia magoti bosi wake Regina ampatie mkopo.
Upande wa Hamza alimwangalia Dokta Ronica na tabasamu na kisha alibadilisha lugha na kuanza kuongea kiitaliano.
“Unathubutu vipi kupokea gharama za matibabu kumtibu mama mkwe wangu, Unataka niipige bomu Mayo clinic”
“Gharama ya chini ya matibabu ni bilioni ishirini na hapo sijajumlisha ya makato kwenda kwa Mwanafalme wa Saudi Arabia , utajiri wote huo uliokuwa nao unanilipa hela ya maji , huu ni uonevu , nimekuja Tanzania kwasababu ninaamini kuna mapato”
“Sikia Flora hela unazo za kutosha , huna haja ya hela wewe , isitoshe mimi saivi sina hela , pesa zangu zote zimepotelea nje ya nchi , hivyo usifikire kuona kama nitakulipa hela nyingi, bado najitafuta”Aliongea Hamza huku akiwa na usiriasi wa hali ya juu.
“Wewe na mshikaji wako wa Saudi Arabia mnaninyanyasa sana mkihitaji kitu kutoka kwangu , ila haina shida chukulia ninachofanya leo hii ni zawadi yangu kwako kama mdogo wako wakati wa ndoa yako na Eliza”
“Haha.. hayo ndio maneno sasa ..”Aliongea Hamza huku akicheka , huku akijiwazia huyu chizi kaja Tanzania akiwa na mawazo ya kumchuna hela zake lakini mpango wake umegeuka ndoto.
“Nyie mnaongea nini jamani , ni Milioni ishirini au kuna makosa?”Aliuliza Eliza ambae hakuwa akielewa Hamza na Dokta Flora wanaongea nini.
“Gharama ni hio hio, taasisi yetu imekuwa ikitibia watu wengi kwa bei rahisi ili kujua mbinu za kupunguza gharama za matibabu, hivyo usiwe na wasiwasi”Aliongea Flora.
“Kama ni hivyo mlikuwa mkitumia lugha gani , Hamza ulikuwa ukijadiliana nae kunipunguzia bei , nitajisikia vibaya ukifanya hivyo?”
“Ni lugha ya kirumi , nilikuwa nikiongea maongezi binafsi kuhusiana na mwalimu wake , hivyo tunaweza sasa kuongea kuhusu gharama , halafu udaktari ni swala la wito kutoka kwa Mungu haina haja ya kutanguliza malipo”Aliongea Hamza huku akicheka.
“Ndio Miss Eliza usiwe na wasiwasi sana kuhusu gharama”Aliongea Frola aliekuwa akilazimisha tabasamu lakini moyo wake ulikuwa ukiuma hatari kwa uonevu wa Hamza..
Eliza alikuwa msomi , kuna kitu alihisi lakini kwasababu dokta mwenyewe ndio amesema aliishia kukubali tu.
“Sikutarajia kama utakuwa unajua zaidi ya kuongea kifaransa , kingeereza na kitaliano , unaweza kuzungumza lugha ngapi?”Aliuliza Eliza , kila kitu kilikuwa kikimwambia Hamza ubini wake sio wa kawaida kabisa lakini pia kuwa na uwezo wa kufahamina na dokta kama huyo halikuwa swala la kawaida.
“Sijajua kuhesabu, halafu lugha ni kama zana tu , sawa kabisa na kanuni ya kushikilia spana au Screwdrivers kufungua nati tofauti tofauti , hakuna kitu cha ajabu kuongea lugha nyingi”
Eliza aliona kabisa Hamza anaongea pumba ili tu kukwepa kumwambia ukweli hivyo hakuuliza zaidi.
Lakini mara baada ya kuona Dokta huyo ndio anaekwenda kumtibia mama yake nje ya nchi , aliona kuna kila haja ya kumfahamu ki undani.
“Dokta Flora uaonekana kuwa mdogo mno , hakuna mtu ambae anaweza kuamini wewe ni daktari mkubwa, utakuwa ni moja ya madaktari vijana katika fani ya tiba”Aliongea Eliza na kauli ile ilimfanya Hamza kukohoa kwa kupaliwa, upande wa Flora alijisikia vizuri .
“Kama ni hivyo otea nitakuwa na umri gani?”Aliongea akiwa na tabasamu na kana kwamba anamrahisishia Eliza kujua umri wake alianza kuchezea nywele zake, isitoshe nywele ni kiashiria kikubwa cha umri .
“Umri wako utakuwa kati ya miaka ishirini na nane kwenda therathini”Aliongea na kumfanya Flora kucheka.
“Hamza, your girlfriend said that I am between 28 to 30 years old , she is really a cute little girl”Aliongea Flora na kumfanya Eliza kumwangalia Hamza.
“Hamza nimekosea wapi?” aliongea Eliza na kumfanya Hamza kukuna kichwa, ila hakumlaumu kabisa Eliza.
“Ana miaka sitini na sita huyo?”
“Nini!!?”
Eliza alijikuta akimaka kwa sauti kiasi kwamba kushitua watu waliokuwa ndani ya mgahawa huo.
Eliza aliona anachezewa akili kabisa na aliishia kuziba mdomo wake na kujiambia yaani hawa watu wanamuonaje kwa mfano , hakukuwa na uwezekano msichana mrembo namna hio kuwa na miaka sitini na sita.
“Usishangae sana Eliza nilichokuambia ni ukweli , hata wewe kama utakuwa mtaalamu wa maswala ya tiba na kuwa na mbinu za kuuboresha mwili unaweza kuwa kama yeye miaka arobaini ijayo , lakini unapaswa kuwa na pesa nyingi pia”Aliongea Hamza.
“My research is mainly focused on extending the life of humans , so it is not difficult for me to make myself look younger”Aliongea Dokta Flora akimaanisha kwamba tafiti zake anazo fanya ni kujua namna ya kurefusha maisha ya binadamu na yeye kama mtafiti sio ngumu kujitengeneza na kuwa kijana zaidi.
Ijapokuwa Flora alielezea kwa namna hio lakini ilikuwa ngumu bado kwa Eliza kuamini , lakini kwa namna moja ama nyingine alikuwa akionea wivu muonekano wa Flora.
Alikuwa akimwangalia Flora kwa macho ya uchunguzi , hakuwa akiamini kabisa kama mwanamke aliekuwa mbele yake alikuwa ni bibi yake , lakini kwasababu sayansi ilikuwa ni njia ya uwezekano mwingi aliona pengine yote ni kweli , isitoshe dunia imejaa siri nyingi.
Baada ya kumaliza kula waliagana , Dokta Ronicas alirudi hotelini kwake huku Eliza akiendesha gari.
Njjia nzima Eliza alikuwa akimwangalia Hamza kwa kuibia ibia , alionekana kama mwanamke mwenye maswali mengi.
“Ijapokuwa mimi mpenzi wako ni handsome sana , haina haja ya kuniangalia muda wote”Aliongea Hamza.
“Halafu lini nimekubali kuwa mpenzi wako?”
“Hata kama hujakubali , ni bure tu , kwa vyvoyote vile moyo wako umeshakubali”Aliongea Hamza kwa tabasamu la uchokozi.
Eliza aliishia kuinamisha kichwa chake chini kwa aibu za kike , na mara baada ya kufikiria kwa muda alimwangalia Hamza.
“Hamza .,,, Asante sana”
“Huna haja ya kunishukuru , wewe niambie ni lini utanipikia”Aliongea Hamza huku akimkonyeza.
“Unaonaje Wikiend ukija nyumbani , nitakupikia chakula kitamu sana”
“Dili, usije kubadilika”Aliongea Hamza kwa furaha , huku akijiwazia kwenda kwa Eliza kuna mambo mengi yanaweza kutokea , pengine ukaribu wao unaweza kuongezeka zaidi na zaidi.
Lakini Hamza alishangaa kidogo mara baada ya Eliza kupoteza tabasamu usoni mwake , alionekana kana kwamba alikuwa na wasiwasi.
“Eliza unafikiria nini , au bado hujakubaliana na mama yako kwenda kutibiwa nje ya nchi?”
“Hapana , Dokta Flora anaonekana sio daktari wa kawaida na ninaamini atamtibia mama vizuri … lakini. , wakati nilivyoona namna unavyoongea nae kiitaliano leo hii , ghafla tu nilihisi , siwezi kufiti kwenye ulimwengu wako”Aliongea Eliza.
Hamza alishangazwa na kauli hio , hakutegemea Eliza angekuwa na mawazo ya namna hio , lakini hata hivyo alielewa hisia zake.
“Kwamba huamini maisha yangu ya nyuma?”
“Sio kama siamini , ila najihisi kuna umbali mkubwa kati yetu”Aliongea na Hamza alitaka kumbembeleza kwa maneno lakini ghafla tu mwili wake ulimsisimka mara baada ya kunusa hatari ya kupata ajali.
SEHEMU YA 40.
Masaa kadhaa nyuma Kanali Dastani alikuwa ashaachiwa huru na kitengo cha MALIBU na sasa alikuwa akiingia ndani viunga vya Ikulu.
Katika kipindi chote akiwa amezuiwa hakuwa na wasiwasi kabisa , kutokana na kwamba alikuwa na ukaribu na Mheshimiwa Raisi lilikuwa swala la muda kutolewa ndio maana hata wakati wa mahojiano hakutaka kuongea chochote akijaribu kupoteza muda.
Amosi Undercover Agent wa kitengo cha MALIBU ambae alipewa jukumu la kumfanyia mahojiano Kanali Dastani alijikuta akiwa katika wakati mgumu.
Kosa kubwa ambalo lilimfanya Kanali Dastani kuwa kizuizini ni mara baada ya kumuingiza Amosi katika hatari kwa kumpeleka katika mikono ya Tresha Noah ninja kutoka kisiwa cha Binamu.
Dastani alimhadaa Amosi kwa kumwambia taarifa ambayo anaitaka juu ya uchunguzi wa kifo cha mwanamke aliehusishwa katika kesi ya radi atapata pa kuanzia kwa kupata faili kutoka katika moja ya mtu ambae anaabudu uchawi yaani Wiccan.
Lakini ule ulikuwa mtego ambao Dastani alimwekea Amosi na kwa bahati mbaya mtego wake haukunasa kama ambavyo alikuwa ametarajia , yalikuwa ni makosa upande wa Tresha na mwenzake kwa kushindwa kumdhiibiti Amosi kikamilifu.
Moja ya maagizo ambayo yalimfanya Amosi kusaga meno kwa hasira ni mara baada ya kuambiwa amuachie Kanali Dastani huru , na maagizo yametoka kwa mkuu wa nchi.
Amosi aliona kabisa kuna kitu ambacho Dastani anajua kuhusu kesi ya Radi lakini hakuwa tayari kuweka wazi , kilichomchanganya zaidi Amosi alishindwa kujua ni upande gani ambao Dastani yupo , hakuelewa kama Dastani alikuwa upande wa jamhuri au watu wa Binamu.
Ushahidi wa kumfungamanisha na upande wa Binadamu pia haukupatikana na kwasababu Afande Doswe mkuu wake alimpa masaa ishirini na nne pekee ya kumhoji Dastani, baada ya kupokea simu kumuachia huru , muda pia ulikuwa umeisha hivyo alijikuta akiwa hana jinsi na kufanya wakubwa zake wanachotaka kufanya.
“Kanali hili halijaisha , nilikuamini sana lakini ukautumia uaminifu wangu kwako vibaya , iwe sasa hivi au muda wowote nitakukamata na ushahidi na ikifika huo wakati ama zako ama zangu”Aliongea Amosi mara baada ya kuingia katika chumba cha mahojiano na kumruhusu Kanali kuondoka.
“Amosi najua wewe ni mtu ambae unafuata sheria , hili swala tushindane sisi wenyewe bila ya kutumia watu wetu wa karibu , ukinishinda nitakubali kushindwa nikikushinda kubali kushindwa pia”Aliongea Kanali Dastani mara baada ya kuwa huru.
“Taarifa za kuipeleka familia yako sehemu salama nimezisikia , lakini umenishusha hadhi yangu sana kudhania nitatumia familia yako ili kukubana, Mimi Amosi , licha ya kuonekana jambazi na mbwa wa vigogo, lakini mimi ni mzalendo wa kweli na mapemzi yangu kwa Taifa hili ndio kitu kinachonipa nguvu ya kushindana na watu mafisadi kama wewe”Aliongea Amosi kwa hasira na Dastanni alitoa tabasamu.
“Ni kama nilivyokuwazia Amosi , umeweza kuishi undercover kwa muda mrefu bila kugundulika , inaonyesha ni kwa kiasi gani una uwezo wa juu , lakini uwezo wako umeshindwa kuelewa kitu kimoja , mimi pia naipenda nchi yangu na kila ninachofanya ni kwa maslahi ya nchi hii , hakuna kingine njia zetu tu ndio zinatofautiana”Aliongea na baada ya hapo alitoka katika chumba hicho.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa baina ya Amosi Jasusi wa siri wa serikali na Kanali Dastani mfanyakazi wa upelelezi kitengo cha MALIBU.
Siku chache zilizopita Amosi alikuwa akiripoti operesheni zake zote za kiuchunguzi kwa Dastani , lakini baada ya Dastani kumuingiza katika mtego waligeuka kuwa mtu na bosi wake na sasa ni mahasamu ambao walikuwa wakijivunia kwa kuipenda nchi yao.
Ukweli ni kwamba haijalishi kati yao nani mkweli , Amosi alionekana kuipenda hela , huku Dastani akiwa na matendo ambayo yalimfanya kutokueleweka yupo upande gani.
Kwa muda mrefu sana iliaminika serikali ya Tanzania ilikuwa ikiongozwa kwa mkono wa watu wa kisiwa cha Binamu , licha ya kwamba ushahidi huo hakuwa wazi , lakini ni jambo la kuwezekana kwa taifa dogo kutawaliwa na watu wenye nguvu ya hali ya juu kutoka kisiwa cha Binamu.
Kanali Dastani hakujali ahadi ya Amosi zidi yake , kitendo cha kuiwa ikulu , ilimaanisha Mheshimiwa alikuwa na swala nyeti la kuzungumza nae na yeye kama jasusi mpelelezi alipenda changamoto.
Baada ya kukaguliwa na kutii itifaki zote za awali kabla ya kuingia katika ofisi ya Raisi , hatimae alipokewa na katibu Muhtasi Maulidi Bakari.
“Mheshimiwa anakusubiri Kanali”Aliongea Maulidi mara baada ya kutoa taarifa ujio wa Kanali.
Dastani hakuwa na mshangao sana , alikuwa amefika Ikulu mara nyingi mno na kama ni kuonana na raisi ameonana nae sana tu katika kazi mbalimbali ambazo aliaminiwa na mheshimiwa Samweli Eliasi Mbilu.
“Haina haja ya kukaa chini Kanali”Aliongea Mheshimiwa akimzuia Dastani asikae kwenye kiti.
“Nimeitikia wito mheshimiwa”Aliongea Dastani, kitendo cha kukatazwa kukaa chini moja kwa moja alijua Mheshimiwa hajaridhika na matokeo yake.
“Dastani kwanini umekosa umakini mpaka unaingia katika Rada za TISA?”Aliuliza .
“Mheshimiwa sikutegemea kama mpango wa kumuondoa Amosi kwenye kufatilia ungefeli?”
“Hata kama mpango wa kwanza ulifeli , ulipaswa kuwa na mpango B , kwanini umekuwa mzembe kwenye kitu kidogo namna hii , kitendo cha kufeli kumuua Amosi moja kwa moja mmempatia kinga”Aliongea na kumfanya Kanali kushangaa kidogo.
“Mheshimiwa unamaanisha nini kuhusu Kinga?”
“Huna clearence ya kujua kinachoendelea , ila kwanzia sasa Amosi hapaswi kuguswa tena , kuna watu wapo nyuma yake na sio Wabrazili wanaotaka uchunguzi wa kesi ya radi uendelee, kuna wenye nguvu zaidi , Wabrazili walikuwa ni kivuli tu”Aliongea na kauli hio ilimfanya Kanali paji lake la uso kutoa jasho.
“Mheshimiwa kipi ambacho natakiwa kufanya , sijawhai kudhania kuna watu wenye nguvu zaidi ya watu wa Binamu?”
“Binamu ni sehemu ya wavamizi tu na wanachojivunia ni teknolojia, unadhani wanaweza kuwa na nguvu kushinda nchi kubwa duniani, wao ili waendelee kuwepo wanahitaji sapoti kutoka kwao hivyo wakipewa oda wanatii mara moja bila ya maswali”
“Mheshimiwa napaswa kufanya nini juu ya hili?”
“Hutakiwi kufanya kitu Kanali , nimekuita kwa kazi nyingine kabisa, sijaridhika na matokeo yaliopita , ila kwenye hili la pili sitaki uzembe”Aliongea na kisha alitoa faili na kumpatia Amosi.
Amosi mara baada ya kushika faili hilo na kufungua ndani alikuta ni ripoti ambayo aliwasilisha kwa Brigedia Doswe kabla ya kuingia kizuizini kwa ajili ya mahojiano.
“Hio ripoti nadhani wewe ndio umeifanyia kazi , inakosa baadhi ya vitu lakini haihitaji kuongezewa kitu , unachopaswa ni kuondoka na jina moja tu la huyo Hamza Mzee na kish….”Aliongea Mheshimiwa na alimalizia kwa kuweka vidole shingoni akimaanisha Hamza auwawe na jambo lile lilimpa mushikeli Kanali.
“Mheshimiwa lakini uchunguzi haujakamilika na hakuna uhakika wa Hamza kuhusika”
“Unadhani nimekuagiza hivyo kwasababu ya watu waliokufa Zinga, sihitaji hata kujua kwanini walikufa , Hivi Dastani unanichukuliaje , unadhani kwasababu nastaaafu na akili imestaafu”
“Hapana mheshimiwa najaribu kuwa makini , ana uhusiano na bosi wa kampuni ya Dosam , ikitokea amekufa swala hili haliwezi kuwa rahisi kupita”
“Ndio maana unachotakiwa ni kuhakikisha kifo chake kinakuwa cha kawaida kabisa, ikishindikana kumuua kwa kifo cha kawaida , tumia mbinu yoyote ili mradi nisikie habari za msiba”Aliongea Mheshimiwa, kanali alitaka kupinga lakini mheshimiwa alimpa ishara ya kutoka ofisini kwake.
Baada ya Kanali Dastani kutoka palepale mheshimiwa alinyanyua simu yake na kuitafuta namba na kupiga.
“Gabusha , huna haja ya kuwa na wasiwasi tena , kazi nimempatia kijana ninaemuamini , amefanya kazi za namna hii kwa muda mrefu”Aliongea Mheshimiwa.
“Hahaha… Mbilu wewe ni rafiki yangu ,sikudhania ungenizingatia kwa muda mchache hivi”
“Huna haja ya kunishukuru katika hili Gabusha, wewe na Benjamini wote mnataka matokeo ya aina moja na natumia shida zenu kama matofali ya kujenga ngome yangu kabla ya kutoka Ikulu”Aliongea huku akiwa na tabasamu lililojaa kejeli usoni.
“Haha… kama unatumia shida zetu kama matofali ya kujenga ngome yako , vipi upande wako , mpango wako wa kuumiliki mtandao wa Chatu umekwama?”
“Hakuna utofauti kati yetu , nilichofanya ni kuazima kibiriti kuuwasha moto , huyu kijana anaonekana kuwa na maadui wengi na hakuna namna akipoteza maisha tukio lake linaweza kuunganishwa kwangu”Aliongea.
“Ni kweli na sidhani ana famili ya kuweza kutusumbua , hata mahusiano yake na Regina yanaonekana kutokuwa siriasi , kama ni hivyo asingejichanganya na kuingia kwa Eliza”Aliongea.
“Ukimzungumzia Eliza , najua kabisa hili swala linahusiana na maswala yako ya utajiri wa majini , Gabusha ninaemjua hawezi kuhangaikia mwanamke muda mrefu”
“Mbilu tusiende mbali, usiku ndio umeingia , nataka kuimaliza siku vizuri”Aliongea upande wa pili na kumfanya Raisi Mbilu kutoa tabasamu la kejeli.
“Wapuuzi nyie ,mpango wangu ukifanikiwa na ikatokea kuna makosa kila kitu nitawaangushia na baada ya hapa nitadili na Mstaafu lazima nimtoe kwenye ramani , anajikuta wa mjini ila hana lolote, Bilioni tisini kwa mwezi kila kitu kitakuwa changu haha..”Hayo ndio yalikuwa mawazo yake, alikuwa na miezi michache sana ya kumaliza muda wake , hakuwaza tena raia alikuwa akiwaza maisha baada ya kustaafu.
*******
Ilikuwa ni wakati ambao wanaingia katika makutano ya barabara inayoingia bandarini , licha ya kwamba magari ya upande wa kulia kwao yalikuwa yamesimamishwa kwa taa nyekundu ya kuongozea magari , lakini gari la mizigo lilikuwa katika spidi , ilikuwa ni kama vile gari yao ndio ilikuwa ikisubiriwa ingie katika makutano yale.
Hamza akili yake ilikuwa imecheza haraka na aliweza kujua sio kama dereva amekosea bali ni kitendo cha kukusudiwa.
“Eliza simamisha gari”Aliongea Hamza kwa nguvu na kumfanya Eliza ashituke.
“Simamisha gari pembeni usipite”Aliongea Hamza na sasa mara baada ya Eliza kuelewa alichokuwa akimaanisha Hamza alikuwa amechelewa kwani alikuwa tayari katika usawa wa gari lile kubwa na lilikuwa likisogea kwa spidi kubwa mno na kosa ni kwamba Eliza alisimamisha gari akiwa katikati ya barabara.
“Ahhhhh…!!”
Elliza alijikuta akifumba macho mara baada ya kukishuhudia kifo chake mwenyewe , lakini ndani ya sekunde tatu tu kabla ya gari ile ya Toyota hajafikiwa Hamza alikuwa ashamfungua Eliza mkanda tayari na kufungua mlango upande mwingine, kutokana Eliza alikuwa amekanyaga breki tayari Hamza alifanikiwa kuchoropoka akiwa amemshikilia Eliza na kwenda kutua pembeni ya barabara.
Dereva wa gari lile kubwa la mizigo mara baada ya kuona waliokuwa ndani ya gari wametoka upande mwingine haraka sana alizungusha usukani na kulikwepa na aliishia kuharibu mlango wa kulia wa gari.s
Licha ya kwamba eneo lile ilikuwa ni sehemu ya kuelekea upande wa bandarini na kulikuwa na giza lakini daladala ambayo ilikuwa ikishusha abiria pembeni yao waliweza kushuhudia lile tukio na wanawake walipiga makelele wakiamini vifo vya ajali vinakwenda kutokea..
Hamza mpaka anakwenda kumshusha Eliza chini , alikuwa ashapoteza fahamu tayari, ni kama alipoteza fahamu kabla hata ya kugongwa.
Upande wa Hamza hakuwa na hofu kabisa kwenye macho yake , na aliishia kumshikilia vizuri Eliza ambae alikuwa ni kama mtoto aliepakatwa.
Lakini cha ajabu ni kwamba mkono wake wa kushoto ulikuwa ukicheza kwa kulenga lile gari na ilikuwa ni kitendo cha haraka sana baada ya dereva kukwepesha kugongana na gari yao , lilipinduka lile gari na kulitokea mshindo mkubwa mno ambao ulimtoa Eliza katika usingizi.
Eliza alijikuta akishituka kwa nguvu na woga ulimvaa lakini Hamza alimtuliza.
“Usiwe na wasiwasi , hujaumia”Aliongea Hamza kumtuliza ,
Eliza alitamani kutoa kilio kwa nguvu , mwili wake ulianza kumtetemeka , lakini alishindwa kabisa kulia zaidi ya macho kuwa mekundu.
Sekunde chache zilizopita aliamini anakwenda kupoteza uhai moja kwa moja , lakini miujiza imetokea na amepona.
Muda uleule watu walikuwa washajazana kuzunguka eneo la tukio na walijikuta wakiwa katika bumbuwazi baada ya kugundua waliokuwa ndani ya gari washatoka nje , kila mtu alihisi ni kama anaona picha isio na uhalisia na kujiuliza wametokaje.
Hamza hakujali watu waliokuwa wakimuuliza maswali na alitembea mpaka kwenye gari lile kubwa na kisha alifungua mlango uliopondeka kwa juu na kutaka kumchoropoa yule dereva lakini mara baada ya kuangalia kwa umakini aligundua dereva yule hana uhai na cha kushangaza zaidi alikuwa ameshikilia bastora iliofungwa kiwambo cha kuzuia sauti , alionekana kujiua mwenyewe na palepale akili ya Hamza ilicheza , tukio hilo alithibitisha lilikuwa ni la kupangwa.
“Assassin…”Hamza alijikuta akimwemwesa midomo yake huku akijiuliza nani ambae alitaka kumuua.
Aliamini tukio hilo alilengwa yeye , kama ingekuwa Eliza basi angesubiriwa akiwa peke yake na ingekuwa rahisi zaidi.
“Bro upo sawa , huyu dereva anapaswa kunyongwa , anaendeshaje gari kwa ukichaa namna hii”
“Pigieni simu polisi, aisee hawa watu wanabahati mno , nilijua tunaokota maiti”Watu waliokuwa wamezunguka walianza kuongea wao kwa wao huku wakimwangalia Hamza na Eliza kwa macho ya mshangao , hawakuamini kama wamepona katika tukio hilo.
Upande wa Hamza hakujali swala la polisi kufika hapo, kwasababu hisia mbaya zilishamvaa , aliwaza kama mpango huo wa kuuwawa umepangwa na familia ya James basi Regina na yeye atakuwa kwenye matatizo.
Alikumbuka tukio la James kufika kwenye kampuni akiwa na yule mzee anaejua mapigano kwa kutumia vidole na kengele ya hatari ilizidi kugonga.
Haraka sana alichukua simu yake na kumpigia Regina lakini simu iliishia kuita bila kupokelewa , alijaribu mara ya pili ilikuwa vilevile simu haipokelewi.
Hamza hakuamini kama kumuacha Regina peke yake kwa siku moja tayari ashapatwa na matatizo , hakutaka kuchelewa aliamua kumpigia shangazi simu na hakuwa hata na salamu.
“Shangazi , Regina amerudi?”
“Alipiga simu muda wa saa kumi na moja na kusema atachelewa kurudi mpaka sasa hivi hajarudi bado”Aliongea shangazi na Hamza palepale alihisi hatari na alikata simu na kumsogelea Eliza ambae amezungukwa na watu.
“Eliza panda daladala urudi nyumbani kwanza , naenda makao makuu mara moja”Aliongea Hamza
Gari ya Eliza licha ya kwamba haikuharibika sana , lakini haikuwa ikiendesheka tena.
“Unamaanisha bosi…”Eliza alijikuta akipatwa na mshituko na Hamza alitingisha kichwa na bila ya kusema neno alitimua nduki kama kichaa na kufanya watu kumshangaa na wengine walihisi labda tukio limemchnganya.
Spidi ya Hamza kukimbia haikuwa ya kawaida kabisa , kilichoonekana ni kivuli, kwani alikuwa ni kama vile anaibukia sehemu na kupotea tena anaibukia sehemu nyingine na kupotea.
Ilimchukua dakika kumi tu kutoka makutano ya barabara ya kuingia bandarini mpaka mawasiliano yalipo makao makuu ya kampuni.
Mara baada ya kufika mbele ya geti la kampuni alikutana na mlinzi ambae alimzuia lakini mara baada ya kuona ni Hamza alishangaa kidogo.
“Mkurugenzi ashaondoka?”Aliuliza Hamza.
“Sidhani , sijamuona akitoka , wewe si msaidizi wake?”Aliuliza Jamali , alikuwa akimjua Hamza vizuri.
Hamza mara baada ya kusikia hakutaka kuhangaishana na maneno na mlinzi huyo na alifyatuka mbio kuingia ndani ya jengo hilo na mara baada ya kufika katika floor ya juu na kuingia kwenye korido aliweza kuona floor hio taa zilikuwa zikiwaka na alitembea kwa haraka na kuingia ndani na aliweza kumuona Regina.
Alikuwa ameshikilia karamu na alikuwa bize akifanya kazi , sasa mara baada ya kusikia mlango kufunguliwa kwa nguvu alijikuta akikunja ndita lakini mara baada ya kuona ni Hamza , ndita ziliongezeka zaidi.
“Umerudi kufanya nini tena?”
Hamza hakutaka hata kumsikiliza na alitembea mpaka kwenye meza yake na kuitafuta simu na mara baada ya kuangalia aliweza kuona Missed call zake.
“Kwanini hukupokea simu?”Aliuliza Hamza kibabe , sauti yake haikuwa ya kawaida kabisa , kwa Regina alihisi ni kama sio Hamza anaeongea na alikuwa akitoa msisimko ambao ulimuogopesha Regina.
“Sikuwa na sababu ya kupokea simu yako”Aliongea kwa jeuri.
“Kwahio unapokea simu ukiwa na sababu , kwanini unakuwa mjeuri hata kwenye mambo ya msingi?”
“Kama ulikuwa na cha kuongea ongea , kwani ni sheria kupokea simu yako kila ukinipigia?”
Kauli ile ilimkasirisha mno Hamza , kila akikumbuka alivyoruka viunzi mpaka kufika hapo ndio hasira zake zilimvaa na tabasamu la ajabu lilimvaa na kuanza kuzipiga hatua kuzunguka meza akimsogelea Regina.
Regina mara baada ya kuona namna ambavyo Hamza yupo siriasi alishindwa kujizuia na kuanza kujawa na hofu..
“Wewe unataka kufanya nini.. usinisogelee”Alipiga makelele lakini Hamza hakumjali tena na palepale alimbeba juu juu kumtoa kwenye kiti na kumlaza kifudifudi juu ya meza.
“Arghhh… wewe mshenzi niache , niache, mamaa..”Regina alikuwa akifurukuta kwa kurusha miguu lakini mbele ya Hamza hakuwa na nguvu za kumshinda.
“Pah!
Kilichosikika ni mtu kupigwa vibao vya makalio na jambo hilo lilimfanya Regina kujawa na hasira na aibu kwa wakati mmoja.
Kama Dokta Flora Ronicas ana miaka sitini na sita unadhani Hamza ana mingapi , kwanini tukio la radi liliuwa familia ya mwanamke kule Sumbawanga linafichwa sana , kuna siri gani.