SHETANI RUDISHA AKILI ZETU
MTUNZI: SINGANOJR
SEHEMU YA 76.
Baada ya kupandishwa kwenye gari walichukua uelekeo wa kurudi Mbagala na ndani ya dakika chache tu walikunja kushoto na kuingia katika kambi ya jeshi.
Eneo hilo licha ya kuhifadhia maghala makubwa ya siraha za kijeshi lakini vilevile lilikuwa na gereza la siri ambalo hufungia wafungwa maalumu.
Ndio gereza ambalo mara nyingi lilitumiwa na kitengo cha MALIBU na TISA kwa ajili ya kuhoji na kutesa kupata taarifa.
Hamza mara baada ya kutolewa kwenye gari ndani ya eneo hilo alipelekwa mpaka kwenye nyumba ambayo ilikuwa imejengwa kwa mawe, jengo hilo lilionekana kama ngome ambayo haina madirisha.
Mara baada ya kupitishwa kwenye mlango mpana wa chuma hatimae aliingizwa kwenye chumba maalumu cha mahojiano ambacho kilikuwa kama sero.
Chumba hicho kilikuwa kimezungukwa na vioo vigumu ambavyo havipitishi risasi na hata kuhimili mlipuko wa bomu la kawaida, kulikuwa na kila aina ya ufundi uliotumika eneo hilo kuhakikisha usalama na ilimshangaza Hamza huku akijiuliza kama kuna mtu ambae ashawahi kufikishwa ndani ya eneo hilo.
Hamza alikarishwa kwenye benchi na kujikuta akigeuza macho na kugundua kulikuwa na kila tahadhari zilichochukuliwa , ilikuwa ni kama vile waliomleta hapo walikuwa wakimhofia na kujikuta kutamani kucheka.
Lakini kitendo cha kuona namna ambavyo chumba hiki kimejengwa aliamini pengine Tanzania sio nchi ya Amani kama ambavyo alitarajia,pengine kuna mambo mengi yanaendelea chini chini.
Ikumbukwe kwamba kutengeneza chumba kwa vioo ambavyo vina uwezo wa kuzuia risasi na bomu gharama yake ni kama kutumia dhahabu, sasa kama nchi imeamua kutumia kiasi chote hiko cha hela kujenga eneo hilo aliona haiwezi kuwa bure.
Haikuchukua dakika nyingi wanajeshi kadhaa waliovalia kombati za jeshi waliingia , wakiongozwa na Afande Mdudu, mmoja kati yao alikuwa amevalia kombati za jeshi la polisi zenye cheo cha Kamishina.
Afande Mdudu alikuwa na tabasamu kama lote , kitendo cha kumwingiza Hamza kwenye eneo hilo alijiona mshindi na hakuwa na wasiwasi tena.
“Hamza huyu ni Kamanda Wazo mkuu wa kitengo cha Special Crimes,huyu mwingine ni mtaalamu wa mahojiano alietumwa kutoka makao makuu ya polisi , anaitwa Afande Maningi, Hawa ndio walikuwa bize kudili na kesi yako hivyo unapaswa kutoa ushirikiano kwa kuwajibu kila watakacho kuuliza bila kupindisha”Aliongea Mdudu.
Baada ya kuwatambulisha Afande Mdudu alivuta viti viwili na kuwapa ishara wale ma’afande kukaa .
Wote walionekana kuwa na vyeo vikubwa kuliko hata Afande Mdudu, hata ambae alikuwa na sare za jeshi la polisi alionekana pia ni mwenye cheo kikubwa kutokana na vyeo vilivyokuwa kwenye sare yake.
Afande Wazo aliwapa ishara ya kuondoka wanajeshi wote waliokuwa wamefuatana nao.
“Mnaweza kuondoka , huyu mfungwa yupo kwenye selo yenye ulinzi mkali hata kama ana uwezo mkubwa hawezi kufanya chochote”Aliongea Kamanda Wazo.
“Anachomaanisha kamanda mahojiano haya yanapaswa kuwa siri hivyo mtupe nafasi ya kufanya kazi yetu”Aliogea Afande Maningi na kufanya wale makomandoo na baadhi ya wanajeshi wengine kutoka ndani ya eneo hilo na kuwaacha.
“Hili gereza lenu ni la kisasa mno mnaliitaje?”Aliuliza Hamza huku akichezesha miguu chini.
“Ukisikia Dragon lair ndio hili gereza , hakuna mtu ambae ashawahi kuingizwa hapa akatoka kwa hiari yake hata kama ana uwezo namna gani , tunao uwezo wa kukufungia hapa mpaka ukafa”Aliongea Afande Mdudu huku akicheka.
“Kwa maelezo yako hata mimi naamini hili gereza ni la hatari”Aliongea Hamza huku akitabasamu.
“Hamza huna haja ya kuwa na wasiwasi , sababu kubwa ya kukuleta hapa ni kutaka majibu juu ya maswali yetu , kama huna kosa hatuwezi kukusingizia”Aliongea Kamishina.
“Oh , maswali gani hayo afande?”
“Kwa muda mrefu kidogo tulikuwa tukifanya uchunguzi juu ya maninja wanaojiita wawindaji kutoka Samar ambao walikutwa wameuwa wilaya ya Bagamoyo , baada ya uchunguzi wetu tulibaini wewe ndio muhusika, hawa watu wametokea nchi ya Ufilipino na sio rahisi kuja Tanzania na kuuwawa hivi hivi , siku ya jana tumeweza kukamata wengine wawili ambao walijaribu kuzamia hapa nchini kama watalii na baada ya kuwafanyia mahojiano ya kina wamesema kwamba wanafuatilia siri uliokuwa nayo juu ya kitu kinachoitwa Ankh”Aliongea Kamishina Maningi na kauli yake ilimfanya Hamza kukunja sura.
Hamza alijiambia inamaana wale wapuuzi hawakukata tamaa tu au walikuja kufuatilia kwanini wenzao hawakurudi, lakini hata hivyo aliona haiwezekani, mara nyingi wawindaji hao wa binadamu wakitumwa katika misheni kuna mmoja kazi yake ni kufuatilia kisirisiri maendeleo ya misheni hio , hivyo Hamza aliamini kwa onyo alilotoa lingefika kupitia huyo mwenzao.
“Hamza hawa bounty hunters inaonekana bado hawajakata tamaa na wamerudi tena nchini na kutaka hiki kitu kinachotwa Ankh, kwa taarifa yako hivi unajua kwasababu yako nchi imeingia katika hatari huko mipakani kutokana na ongezeko kubwa la wahalifu kutaka kuingia nchini?”
“Hilo kundi ni daraja B na kwa taarifa nilzokuwa nazo kitengo chenu cha MALIBU kinahesabika kama Daraja A kwa kuwa na wataalamu wengi wenye mbinu mbalimbali za kupambana mpaka na nguvu za giza , kinachowaogopesha nini juu ya hawa Wasamar?”Aliongea Hamza.
“Hili sio swala la sisi kuogopa ama kutokuogopa , tunachotaka kujua ni mzizi wa haya yote , mpaka sasa ma Ajenti wetu wanaendelea kuwahoji hawa Wasamar lakini hatujapata majibu , tunachotaka kujua kutoka kwako hiki kitu kinachoitwa Ankh ni nini?, kwa maelezo yao wanachosema Ankh ni kama dawa ya uzima wa milele , wengine wanasema Ankh ni kitabu cha ufunuo, sasa wewe tunataka utupe majawabu ya kipi ni kweli, pili sisi kama serikali utupatie hio Ankh ili tukutunzie , vinginevyo uwepo wako hapa nchini unaweka usalama wa nchi rehani”
“Si useme tu na wewe unachotaka ni Ankh, kwa bahati mbaya hicho kitu wanachozungumzia ni uzushi tu wa kinadharia ila hakuna kitu cha namna hio”Aliongea Hamza.
“Ongea ukweli wewe”Aliongea Afande Maningi huku akipiga kofi meza.
“Hawa wazamiaji wamesema kitu ulichokuwa nacho kimetoka kwa mwanasayansi nguli wa kihistoria maarufu kama kichwa cha Tembo au Dokta Genesha na ndani ya maabara yake aliacha anuani ya uelekeo wako na ndio maana wamekupata kirahisi hapa Tanzania. Kama ni kweli unafahamiana na Dokta Genesha basi wewe sio mtu wa kawaida, taarifa tulizokuwa nazo mpaka sasa haijulikani kama kweli Dokta Genesha amekufa ama yupo hai na hata mara ya mwisho alipozushiwa kifo chake iliaminika yupo hai baada ya kuwasiliana kwa siri na wewe, kwa mantiki hio lazima utakuwa na taarifa ya siri ambayo hutaki kuongea”
“Ushasema taarifa ambayo sitaki kuongea , kwanini nikuambie sasa Afande?”Aliongea Hamza.
“Kuwa na adabu , endelea kuongea dharau uone kitakacho kupata, unajua wewe ni nani hapa ndani? , wewe ni mfungwa na ukiendelea kuongea uongo usije kulaumu tukichukua hatua nyingne kali zaidi?”
“Elezea hizo hatua kali zaidi?”Aliuliza Hamza huku mwonekano wake ukibadilika palepale.
“Tuta..”Kabla hajaongea alizuiwa na Afande Maningi.
“Hamza huna haja ya kuwa mkali juu ya hili, sisi jukumu letu kama wanajeshi ni kuhakikisha usalama wa nchi unaendelea kudumu na kwakuwa wewe ni raia wa nchi yetu tunapaswa kujua hiki kitu kinachoitwa Ankh ni nini ili tupate namna ya kukulinda bila kuathiri usalama wa nchi , ukituambia kila kitu hatutafanya mambo kuwa magumu kwako , isitoshe tunajua wewe sio mtu wa kufanya vitu ambavyo vinaweza kuumiza usalama wa nchi”Aliongea na kumfanya Hamza kuwaangalia kwa zamu.
“Kwahio ni wewe unaetaka kujua hii siri ama ni serikali inayotaka kujua?”Aliuliza.
“Sisi kujua maana yake serikali imejua , wewe weka wazi Ankh ndio nini?”Aliongea Afande Wazo.
“Kama serikali ndio inayotakiwa kujua basi itifaki ya vyeo inapaswa kuzingatiwa?”Aliongea na kauli ile ilimfanya hata Mdudu kushangaa.
“Unataka kumaanisha nini Mr Hamza ?”
“Namaanisha kwamba taarifa unayotaka kujua ni nyeti mno na inaingia katika taarifa za juu za siri za nchi , hivyo kwa cheo chako hutoshi, itifaki hapa ifuatwe nataka kuonana na kiongozi wa juu wa jeshi Daraja S?”Aliongea na kauli ile iliwafanya wote kutoa macho.
Katika nchi yoyote licha ya Raisi kuwa na madaraka makubwa ya kujua siri nyingi za nchi haimaanishi kwamba anaweza kujua kila siri ambayo anataka kuifahamu
Itifaki ya clearence ya siri za nchi huanzia dajara E ambao hawa mara nyingi ni polisi au wanajeshi wa kawaida tu kama wa doria , siri ambazo hawa wanajua ni zile ambazo mara nyingi zinahusisha matukio ya eneo husika ambazo hazina athari kubwa za ki’usalama hata zikiwa wazi, mara nyingi maelekezo ya siri hizi hutolewa kwa mdomo tu kama onyo la kutoongea chochote.
Daraja D hili ni daraja ambalo huhusisha polisi au wanajeshi pia lakini wale polisi wa vyeo vikubwa ambao wengi wao wanafanya kazi mpaka kwenye vitengo vya usalama wa taifa , hawa wanakuwa daraja D kwasababu watu wa daraja E wote huwasilisha hizi taarifa kwao na kuamua ni siri gani iweke daraja lipi.
Daraja C hili linahusisha siri zinazoendelea katika vikosi maalumu kama vile tukio la Hamza kuua Wawindaji kutoka Samar , hio operesheni inasimamiwa na vitengo maalumu vya uchunguzi na mara nyingi hapa unaweza wakuta polisi au wanajeshi mfano wa Afande Mdudu na kuendelea.
Daraja linalofuatia sasa linakuja B halafu linafuatia daraja A , Daraja A hapa anazungumziwa raisi wa nchi , Amiri jeshi mkuu na baadhi ya viongozi wenzake wa juu, mara nyingi ikitokea siri ambayo inahitaji operesheni ndani ya eneo la tukio hapa wanahusishwa watu wa Daraja B.
Daraja B anaweza kuwa mwanajeshi yoyote anaweza kuwa hata na cheo cha Ukapteni lakini akawa na Clearence ya kujua siri zote zinazoendelea katika daraja B kwa kibali maalumu kulingana na kile anachofanyia uchunguzi.
Siri zote ambazo zinatokea katika Daraja A yaani ngazi ya raisi ambazo ni nyeti hupewa hadhi ya Top Secret na hizi watu wanaopewa Clearence ya kuziona ni Daraja S.
Sasa daraja S katika itifaki hio ni daraja ambalo lijategemea kabisa na hili ndio huwa na uwezo wa kujua siri kubwa za nchi(Top Secret) siri ambazo hata kama raisi azihitaji hapewi au kama akizitaka anapaswa kuomba ruhusa kwanza kwa watu wa hili daraja.
Raisi anaweza kujua siri za daraja S lakini ni baadhi na mara nyingi siri hizo zote huwa zinatokea katika kipindi chake cha uongozi , lakini ikitokea anahitaji siri ambazo zimetokea katika uongozi uliopita ambazo zipo chini ya Daraja S ni mpaka apate kibali ambacho kinaambatana na sababu maalumu na ikitokea akikataliwa hana cha kufanya kisheria.
Bila shaka kuna baadhi ya taarifa nyeti sana ambazo baadhi ya wanajeshi wanajua siri hizo wakati wa uchunguzi lakini hata kama walihusika kwenye uchunguzi wakitaka taarifa hio hawawezi kupewa ruhusa.
Hayo madaraja ni mfano tu ila kila taifa lina itifaki zake namna ya kutoa hizo Clearence lakini zinakuwa katika mtiririko huo katika kuhakikisha usalama wa nchi unazingatiwa.
Lakini pia kuna itifaki ambayo inahusisha kujuana nani anaclearence ya daraja lipi , kwa mfano asilimia nyingi ya wanausalama ambao wana Clearence ya daraja C hawajui nani ana Clearence(Uwezo wa kufungua) ya daraja S.
Kwa mfano kuna matukio ambayo yakawa yametokea katika uongozi wa kwanza wa serikali , matukio kama haya licha ya kwamba kuna uwezekano wa kuyafuta lakini serikali kama serikali haipaswi kuyafuta kutokana na kwamba kuna siku yanaweza yakahitajika hivyo hutunzwa katika jalada la siri nyeti za nchi.
Sasa Hamza alikuwa akitaka kutoa siri yake kwa mwanausalama ambae yupo daraja la juu kabisa ambalo ni S kitu ambacho kiliwafanya Mdudu na wenzake kumuona kama ana kichaa
“Unakichaa , wewe ni nani mpaka mpaka tukutie mtu wa cheo hicho?”Aliongea Afande Mdudu huku akionyesha kutoridhishwa na Hamza kabisa.
“Hamza unapaswa kutuambia ukweli , haina haja ya kupotezena muda la sivo tutatumia njia za mateso”Aliongea Afande Wazo.
“Mimi nimekuona kama mtu ambae una akili , lakini hapa unaonekana kama mtoto mwenye kiburi uliejaa sifa kiasi cha kutaka kuonana na kiongozi wa daraja la juu”
“Mnaongea sana , ila je kuna hata mwenye fununu kati yenu juu ya hicho kitu kinachoitwa Ankh?”Aliuliza Hamza
“Kimya , kama hutaki kuongea ukweli hatuwezi kuendelea kubembelea”
“Kwahio mpo tayari kutumia nguvu kwa ajili ya hili?, kama ni hivyo msije kwenda kinyume na maneno yenu”Aliongea Hamza kwa namna ya tahadhari
Mara baada ya kuona namna ambavyo Hamza alionekana kutokuwa na hofu , wote watatu walijikuta wakisaga meno yao kwa hasira.
Kwa yale matukio machache waliokwisha kuona walijua kabisa Hamza uwezo wake sio kichekesho , lakini bado walishangaa kama alikuwa kwenye Gereza lao la Pango kwanini bado auaonyesha ukiburi.
“Kama unataka kuonana na kiongozi ambae ana Clearence daraja S , tukuambie tu kwamba hata sisi hatuwajui hawa viongozi maana majina yao ni siri , pili hata kama tunamjua mmoja wapo ni watu ambao hatuwezi kuwaambia kiwepesi wepesi lazima hatua za maombi pamoja na sababu za kueleweka zitolewe , kwahio hili ombi ambalo unataka halina mantiki, hivyo hakuna namna tunaweza kulitimiza”Aliongea Afande Maningi.
“Kwa ulichoongea ni sahihi kabisa, kwa vyeo vyenu hapa sioni kama kuna amabe atakuwa anawajua hawa watu wa usalama wenye madaraja hayo ya Clearence , mnaonaje tukifanya hivi, kwa uelewa wangu katika kila idara ya ulinzi na usalama hapa nchini wapo wawili au watatu”Aliongea Hamza na kauli yake ilimfanya Afande Mdudu na Afande Wazo kuonyesha hali ya wasiwasi maana hawakujua Hamza imekuwaje akawa na taarifa hio maana yenyewe ni siri ya daraja C.
“Kuhusu mtu ambae nataka aje hapa kama sikosei cheo chake kitakuwa ni maarufu kama Mshauri wa jeshi”Aliongea Hamza kana kwamba anajaribu kukumbuka jina lakini kauli yake iliwafanya wale wanajeshi kushituka.
“Unafaamiana na Mshauri mkuu!!?”Aliuliza Afande Mdudu maana alikuwa akifahamu mshauri mkuu ndio huyo huyo mshauri mkuu wa jeshi.
“Mdudu anazungumzia mshauri yupi?”Aliuliza Afande Maningi , sio kama hakujua ni kwasababu kulikuwa na washauri wengi na wote walikuwa wanajeshi.
“Ni Generali, Afande Himidu Siwa , unaweza kumuita mkuu wa vitengo vyote, kwanzia kitengo cha TISA, Malibu na kuendelea, hana cheo maalumu ila anafahamika kwa jina la code kama Mshauri Mkuu, kwa muda mrefu watu wanajua mshauri mkuu wa jeshi ni mkuu wa majeshi lakini yeye ndio mshauri mkuu sasa , kwa mtu ambae upo nje ya jeshi huwezi kuelewa, Afande Himidu alipaswa kuwa mkuu wa Majeshi mara mbili mfululizo lakini alikosa kigezo cha umri na kuishia kutoa ushauri wa majina ya nani awe mkuu wa majeshi huku yeye akijipachika cheo cha ushauri mkuu”Aliongea Mdudu.
Viongozi wengi wakisiasa walikuwa wakimheshimu Afande Himidu kutokana na kwamba ndio ambae alikuwa na cheo kikubwa katika utunzaji wa siri za nchi , hivyo kwa lugha nyepesi alikuwa akijua siri nyingi mno.
Kwa namna ambavyo Hamza alikuwa akiongea ni kama Afande Himidu alikuwa akimjua na hatanii katika hilo na ndio maana iliwafanya Afande Mdudu na wenzake kuwa na wasiwasi wakijiuliza amemjuaje.
“Unatuthibitishia vipi kama Afande Himidu anakufahamu na kwanini akubali kuonana na wewe?”Aliuliza Afande Wazo.
“Akigoma kuja kwa jina la Hamza, mwambie Murphy anataka kuonana na wewe”Aliongea Hamza.
“Mafiii!?”
Afande Wazo , Afande Maningi na Mdudu hawakujua jina hilo lilikuwa linamaanga gani ila limekaa kwa kingereza.
“Fanyeni haraka maana najua yupo makao makuu ya nchi , mimi nitatumia huu muda kujipumzisha kidogo mpaka akija maana mmenichosha bure tu”Aliongea Hamza na palepale alipandisha miguu kwenye benchi na kujinyoosha akiwa amejiagamiza na kufumba macho.
Ilikuwa sawa kupumzika maana kama kweli Mshauri mkuu atatoka Dodoma mpaka kufika Dar basi inaweza kuchukua angalau masaa mawili mpaka kupanda ndege na kuanza safari.
Walikuwa hawajaridhika na maelezo ya Hamza lakini Afande Wazo alikuwa makini sana na cheo chake , hakutaka kukurupuka mpaka awasilishe ripoti kwanza kwa mkuu wa kitengo chake na kisha mkuu wa kitengo chake atoe taarifa kwenda kwa Mshauri mkuu.
“Nitawasiliana na Afande Msuya na atajua namna ya kumfikishia taarifa Afande Himidu, weka watu hapa wawe wanamwangalia”Aliongea Afande Wazo huku akitoka.
Kesi hio ya Hamza ilikuwa chini ya Mkuu wa kitengo msaidizi Afande Msuya na kwa kufuata itifaki hata kama Afande Wazo alikuwa na namba ya mshauri mkuu basi asingempigia simu moja kwa moja.
“Fanya hivyo afande , huyu haina haja hata ya kumuwekewa watu wa kuangalia , hii sehemu hawezi kutoka hata kama a na uwezo kiasi gani”Aliongea Afande Maningi na wote walikubaliana nae.
*****
Mji kuu wa kiserikali licha ya kuwa na vumbi la kuchafua pamoja na jua la saa tisa mchana kwenda saa kumi kuwa kali kwa watu wenye vyeo na matajiri hawakusumbuliwa na hali hio ya karaha ya mji.
Haikuwa nyumba kubwa sana wala ndogo sana , ilikuwa ya wastani lakini yenye mazingira ya kuvutia ambayo yaliwakilisha hadhi ya mtu anaeishi ndani ya hilo eneo katika mtaa maarufu wa Mji mpya.
Upande wa eneo la bustani ndani ya nyumba hio walionekana watu wawili mwanamke na mwanaume wakiwa wamekaa katika eneo la bustani la kupumzikia pembeni ya Swimming pool.
Mwanaume alikuwa amevalia tshirt ya rangi ya ugoro , jeans na American boot , alikuwa na kipara na muonekano wake ulikuwa wa kawaida lakini macho yake yalijaa umakini ulioonyesha utulivu wa akili..
Upande wa mwanamke aliekuwa nae alikuwa mrembo haswa alievaa akapendeza , nywele zake ambazo haikufahamika ni za bandia au asili zilikuwa ndefu na nyeusi zilizomfikia mgongoni , alikuwa amevalia kana kwamba ni mgeni ambae yupo ndani ya hilo eneo kwa ajili ya kumpagawisha mwanaume aliekuwa pembeni yake.
“Ni watu wachache sana ambao wanaweza kucheza mchezo wa Chess hapa nchiin na mmoja wapo ni wewe Sophia . ijapokuwa nakwenda kushinda hii mechi lakini niseme umezidi kuimarika tokea mara ya mwisho tulivyocheza pamoja , sio mbaya licha huwezi kunishinda pengine siku zijazo utafanikiwa ukiendelea na mwendo huu huu”Aliongea yule mwanaume kwa sauti nzito na kisha alichukua chupa ya maji na kunywa kidogo huku akimsubiria yule mwanamke mrembo kucheza.
Wawili hao walikuwa makini katika kucheza mchezo maarufu wa Chess.
Mwanamke yule mrembo alionekana kukodolea ubao ule wa kuchezea kwa macho yenye hali ya kutafakari kwa kina, upande wa mwanaume simu yake ya batani iliokuwa na mkonga mkubwa ilianza kuita na aliichukua na kuipokea.
“Ongea!”Alitikia akiwa sirasi , mara nyingi akipokea simu kupitia simu hio basi ni ya kikazi ndio maana anakuwa siriasi.
“Mshauri mkuu , jina langu ni Afande Msuya..”
“Hebu acha kuzunguka nishakufahamu , nenda moja kwa moje kwenye pointi”Aliongea kwa sauti ya amri kama mtu ambae hakupendezwa kupigiwa simu hio.
“Sawa afande , ipo hivi kuna operesheni maalumu ya ki uchunguzi ambayo inaendelea hapa kitengoni chini yangu , katika operesheni hii tumeweza kumkamata mtuhumiwa anaefahamika kwa jina la Hamza Mzee , nimepokea simu kutoka kwa wanausalama wakiwa wanamfanyia mahojiano na amekataa kutupa taarifa na anataka kuonana na wewe Afande”Aliongea .
“Hamza Mzee!!”Aliongea yule bwana huku akionekana kama vile anawaza wapi amesikia hilo hina lakini hakukumbuka.
“Simfahamu mtu wa jina hilo mimi , hili swala mnaweza kudili nalo wenyewe sidhani linahitaji ushauri wangu , sitaki ripoti za namna hii kuripotiwa kwangu”Aliongea na muda ule wakati akitaka kukata simu upande wa pili uliropoka.
“Anasema Murphy anakuita”Aliongea na jina lile lilimfanya yule bwana mwenye sura ya maji ya kunde kukunja sura kiasi cha kumfanya mwanamke mrembo aliekuwa pembeni yake kumwangalia kwa wasiwasi.
“Wewe.. umesemaje hebu rudia vizuri?”
“Amesema kama humtambui kwa jina la Hamza, nikuambie Mafi…. Murphy anakuita”Sauti upande wa pili ilirudia na kumfanya yule bwana kuvuta pumzi nyingi na kuzishusha.
“Waambie wanisubiri wasifanye chochote , narudia huyo mtu ambae umesema anaitwa Hamza asichokozwe , nitafika hapo ndani ya lisaa limoja au mawili yajayo kwa kutumia chopa ya jeshi”Aliongea kwa msisitizo.
“Mshauri ni kweli unafahamiana na huyu Hamza?”Upande wa pili uliuliza kwa namna ya mshangao.
“Hata mimi simjui ni nani mpaka nimuone mwenyewe”Aliongea na kisha palepale alikata simu.
“Sophia nataka kwenda Dar es salaam mara moja , nina haraka , vipi tuongozane wote?”
Mwanamke huyo mrembo alievalia nguo za rangi nyekundu aliishia kutingisha kichwa kukataa bila ya kusema neno.
“Naona kwa leo mechi yetu inaishia hapa , isitoshe sikuwezi na nakufanya usifurahie mchezo, nakuombea apatikane mtu wa kuendana na uwezo wako”Aliongea kwa namna ya kuvutia kana kwamba anamtega.
“Nadhani kuna kitu kingine tunaweza kupimana uwezo”Aliongea na kauli yake ilimfanya yule mrembo ukauzu kumvaa palepale na ghafla tu aliinua mkono wake wa kulia na kuanza kuchezesha vidole katika muundo wa ajabu na hazichukua sekunde vitu kama moshi moshi ulitawala vidole vyake.
“Upo sahihi , siku nyingine nitakuonyesha ufunuo niliopata kwenye kuvuna nishati za mbingu na ardhi”Aliongea .
“Naisubiri hio siku kwa hamu kubwa”Aliongea Afande Himidu na yule mwanamke alitingisha kichwa na kisha akasimama na kitendo cha kuinama kama mchawi alipotea palepale.
********
Masaa kama mawili mbele katika eneo la kambi ya jeshi walionekana Afande Mdudu na wenzake wakipiga saluti mbele ya Kamanda Himidu anaeshuka kwenye chopa huku wakijitahidi kupotezea wasiwasi wao na tabasamu la kulazimisha.
“Afande umetokea ghafla sana , tulikuwa tukipanga kuja kukupokea na escort”Aliongea Afande Wazo lakini upande wa Afande Himidu hakuwa na muda wa kuongea nao kwani baada ya kutoka kwenye chopa aliwapita.
“Huyo Hamza yupo wapi?”Aliuliza
“Yupo ndani ya Dragon Lair Afande”
“Nini!, yaani mmefungia ndani ya hilo gereza, vipi hakuwaletea ukinzani wowote?”Aliongea huku akionyesha mshangao kidogo.
“Afande hakuleta ukinzani pengine ameogopa wingi wetu , anaweza kutushindwa mmoja mmoja lakini kwa wingi wetu hawezi kufanya chochote”Aliongea Afande Wazo kwa majigambo.
“Una akili kweli wewe , unajua hata ninachomaanisha , nakuuliza je mpo salama?”Aliuliza lakini swali lake liliwachanganya.
“Afande unauliza nini kuhusu usalama?”Aliuliza lakini Afande Himidu hakutaka hata kuwaelezea kile anachoataka kumaanisha.
Afande huyo mara baada ya kuingia ndani na kumwangalia Hamza kupitia kioo kizito kilichokuwa mbele yake mshangao ulivaa palepale huku pumzi yake ikiwa nzito ni kama vile ameona mtu ambae hakutarajia kumuona.
“Mshauri yule ndio Hamza”Aliongea Afande Maningi.
“Nani alietoa wazo la kumfungia pale?”Aliuliza akiwa siriasi na kuwafanya Afande Wazo na Afande Maningi kuangaliana , wao sio ambao walikuwa wamemkamata Hamza Afande Mdudu ndio alifanikisha hilo na wao walipewa jukumu la kumhoji pekee.
SEHEMU YA 77.
Baada ya wote kumwangalia Afande Mdudu na Mshauri pia alimwangalia Mdudu akionekana anahitaji maelezo na kumfanya afande huyo sura yake kuzidi kuwa nyeusi.
“Afande naripoti kwako.. mimi ndio nimemkamata”
Afande Mdudu hakuona haja ya kujificha muda huo hivyo aliamua kuuvaa ujasiri na kusogea mbele.
Ukweli ni kwamba hata alipoomba ruhusa kwa mkuu wake wa misheni Afande Msuya alipewa maelekezo ikitokea ameshindwa kumkamata Hamza basi ajisalimishe kama alichukua maamuzi peke yake , ijapokuwa ilikuwa kweli Msuya alikuwa akitaka kumkamata Hamza lakini alipingana na wazo hilo kwa kuhofia kile ambacho anaweza kufanya lakini Mdudu alilazimisha.
“Afande nimemkata kwasababu mpaka sasa ameua watu wengi , tulikuwa na wasiwasi ataende…”
“Haina haja ya kuendelea kuongea”Aliongea Afande Himidu akimkatishia njiani .
"Mdudu kama niko sawa wewe ni mtoto wa pili wa Mkuu wa Majeshi aliepita Afande Mbwana?”
“Ndio afande , babu yangu pia ni waziri mkuu mstaafu”Aliongea kwa kujiamini.
“Huna haja ya kuendelea kuelezea vyeo vya wanafamilia yako , japo ni kweli familia unayotokea ni ya watu maarufu lakini haitoshi katika hali kama hii”Aliongea na kumfanya Afande Mdudu kuonyesha hali ya kuchanganyikiwa.
Ukweli alikuwa akijiamini katika sehemu nyingi , sifa za jina la familia yake lilikuwa likimtangulia katika maeneo mengi , sasa alijiuliza inakuwaje jina lake hapo lisitoshe au Afande anajaribu kuongea kitu gani.
“Afande umeulizia kuhusu familia yangu , hili swala lina uhusiano?”Aliuliza.
“Unaweza kufikiria unachoweza , ila itakuwa vizuri kama ukiongea na baba yako kwanza umwelezee kilichotokea leo, pengine inaweza kukusaidia”Aliiongea lakini kauli yake ilizidi kumchanganya Mdudu kwani hakuwa akijua ni kitu gani amekosea..
Hata upande wa Afande Wazo na Maningi hawakuelewa Mshauri anachojaribu kumaanisha.
“Acha kuonyesha dalili za kuchanganyikiwa , ninachomaanisha hapa fanya kila namna kuokoa maisha ako”Aliiongea.
“Lakini Afande baso sielewi , sijui kama kuna kosa lolote nimefanya kiasi cha kutaka kunipa adhabu”
“Una uwezo mdogo wa kufikiria na sijui aliekupatia uongozi wa hii kesi alikuwa akilenga nini , ninachomaanisha yule mtu akitoka unaweza usiwe salama na akiamua kukuua sitoweza kumzuia”Aliongea na mara baada ya kusikia maelezo hayo alijikuta akitetemeka.
“Lakini Afande huyu si mfungwa , kwani tunamuachia atoke?”
“Afande anachoongea ni sahihi , sidhani kuna haja ya kumuachia huru , ana siri juu ya kitu kinachoitwa Ankh na inaonekana ni siri ya thamani kubwa mno inayofuatiliwa na watu wengi kiasi cha kuhatarisha usalama wa nchi”
“Ndio Afande Hamza yupo pale na hakuna namna anaweza kutoka kwa hiari yake labda tumuachie bila ya kujali uhalifu wake”Alikazia Afande Mdudu.
Lakini Afande Himidu hakuwa akiwasikiliza kwa maneno yao, macho yake yalikuwa yamemkazia Hamza ambae alikuwa ashasimama tayari na kusogelea kioo huku akijivuta.
Japo kwa ndani ya chumba hicho ilikuwa ngumu kuona anaengalia nyuma ya kioo lakini muda ule ni kama Hamza alikuwa akiangaliana na Afande Himidu kwani alitoa tabasamu la ishara ya salamu na kumfanya hata Afande Himidu kutabasamu pia, huku macho yake yakionyesha ishara ya heshima kwa Hamza.
“Hebu fanyeni haraka , mfungulieni atoke”Aliongea kwa sauti kubwa iliojaa ubabe.
Kundi hilo la wanajeshi waliishia kusita kupokea maagizo hayo , hawakujua wamuachie Hamza au wasimauchie , isitoshe kwao walimuona kama mhalifu na Mshauri anataka kuvunja sheria.
Lakini sasa kilichotokea baada ya hapo kiliwafanya kuganda kama vile wamegeuka mawe ya barafu.
Hamza alikuwa akipiga piga kuta za eneo hilo la ndani kana kwamba anajaribu kuona ni wapi kuna udhaifu na uimara, baada ya kuonyesha kuridhika na kugonga gonga alisogelea kioo na kuweka kiganja cha mkono huku akionekana kufumba macho.
“Anajaribu kufanya nini , au amepatwa na uchizi wa ghafla?”Mmoja aliongea kwasababu waliamini kioo alichoshika Hamza kilikuwa ni kioo kigumu mno ambacho ni kipana kiasi kwamba hakiwezi kupitisha risasi wala kupasuka kwasababbu ya mlipuko.
Afande Maningi palepale wasiwasi ulimwingia na alibonyeza kitufe ambacho kinasafirisha sauti.
“Mr Hamza tunakuomba utulie tutakuachia muda si mrefu”Aliongea , alijua kama kweli Hamza anafahamiana na Afande Himidu basi kuna uwezekano asiwe wa kawaida.
Isitoshe walikuwa ni wanajeshi wa kitengo cha kupambana na nguvu za ziada na kupitia uzoefu na stori nyingi walizosikia juu ya mafunzo mbalimbali ya maajabu walipatwa na hisia za hatari wakiamini Hamza anaweza kuwa na hayo mafunzo ya nishati za mbingu na ardhi.
Hamza aliendelea kushikilia kile kioo kwa nguvu na alioekana kama mtu ambae anasali kwani midomo ilikuwa ikicheza kwa kuongea na kabla hata wale wanajeshi hawajachukua hatua ya kumfungulia eneo hilo lilianza kutetemeka kama vile ni mtikisiko wa ardhi.
Kitu kile kiliwafanya watoe macho washindwe kujua nini kinakwenda kutokea.
Wakati wakishangaa ghafla ule mtikisiko ulipotea lakini Hamza bado alikuwa ameshikilia kile kioo huku akiwa amefumba macho na kuendelea kuongea maneno.
Ghafla tu macho yaliwatoka mara baada ya kile kioo walichoamini hakiwezi kupasuka hata kwa nyundo kikianza kutengeneza nyufa taratibu kana kwamba kinapata kiwango cha juu cha moto ,hazikupita sekunde kumi kioo chote kama vile ni glasi imedondoshwa chini kwani kilipasuka vipande vipande.
Bahati ni kwamba kioo hakikuwa kimoja pekee kulikuwa na layers angalau tatu za vioo vinavyofanana.
“Afande wazo si umesema hivi vioo haviwezi kupasuka hata kama vipigwe na bomu?”Aliuliza Afande Mdudu huku akitetemeka.
“Inawezekana vipi kupasua kioo bila ya kutumia nguvu?”Afande Wazo aliekuwa kwenye bumbuwazi.
Ilikuwa ngumu kukubali maana walitumia kiasi kingi cha pesa kwa ajili ya ujenzi wa hilo eneo , lakini namna ambavyo Hamza alikuwa akividondosha sio uwezo wa kawaida.
Hamza kabla hajafikia kioo cha mwisho Afande Wazo alishikwa na hasira , alitaka kujihakikishia kama ni kweli vioo hivyo vilikuwa vigumu au kuna tatizo , hivyo mara baada ya kushika bunduki alianza kuvimiminia risasi. Lakini hakuna risasi hata moja ilioacha hata ufa kwani zilidunda tu na kudondoka chini.
“Hakuna haja ya kufanya majairibio , hakuna tatizo kabisa na ujenzi wa hili eneo, Shida ni kwamba ana uwezo mkubwa mno na wa ajabu”Aliongea Afande Himidu huku macho yake ni kama amefurahi kuona tukio kama hilo.
Hatimae vioo vyote vilipasuka chini bila ya kupigwa ngumi zaidi ya kuwekewa kiganja cha mkono tu.
“Kuna mwenye sigara kati yenu?”Aliuliza Hamza mara baada ya kutoka nje lakini kila mtu alikuwa amemkodolea macho kana kwamba wameona mnyama.
“Mnashangaa nini sasa , au hamhawahi kuona kioo kikipasuka?”Aliongea Hamza na Afande Himidu ndio aliekuwa wa kwanza kushituka.
‘”Inamaana hamjamsikia , hakuna mwenye sigara kati yenu?”Aiuliza na Afande Wazo kwa kutetemeka aliingiza mkono kwenye mfuko wake wa kombati na kuchomoka na sigara na kibiriti.
Upande wa Afande Himidu hakushangaa Hamza kuhitaji sigara , kwa mtu wa kawaida anaweza kuona Hamza hakutumia nguvu kupasua vioo hivyo lakini kwa uelewa wake alijua Hamza ametumia nguvu nyingi tu japo sio zote, kutengeneza resonance pacha kwenye kitu kigumu kama hicho haikuhitaji tu nguvu lakini matumizi makubwa ya ubongo ili kupatia hivyo hufanya akili kupata hali ambayo inaweza kuondolewa na sigara au kilevi.
“Kijana naona una mabadiliko makubwa mno , umepata mke nini?”Aliongea Hamza akimshika bega Afande Himidu huku wakiwa na tabasamu .
Kwa namna ambavyo Hamza alianzisha mazunguzo na afande wa heshima kama huyo iliwafanya Mdudu na wenzake kuzidi kushikwa na wasiwasi.
“Kama ningekuwa nimeshaoa wewe ungekuwa wa kwanza kujua , yaani nifunge ndoa bila ya kukualika mlevi kama wewe”Aliongea Afande Himidu huku akicheka,
“Haha……utaachaje kunialika na unavyopenda vitu vya mteremko , sidhani bila kutoa mchangao wangu utataka kuoa wewe”Aliongea na kumfanya Afande Himidu kujikuta akicheka mpaka mabega yanamtingishika.
Muda huo Hamza akipata muda wa kuangalia watu waliokuwa ndani ya eneo hilo na aliweza kuona kila mtu alikuwa akimwangalia kwa wasiwasi.
“Nyie watu haina haja ya kujenga upya hivyo vioo , ni kujitia hasara tu”Aliongea Hamza huku akiwa na tabasamu la kejeli lakini Afande Wazo na Afande Maningi walikuwa na wasiwasi mno.
“Ndio Afande tumekuelewa” Aliongea Afande Maningi huku hana uhakika kama kumuita Hamza afande ni sawa , alijaribu kubahatisha kwa namna yoyote ile ili kumtuliza asichukue hatua.
Muda ule Hamza macho yake yalitua kwa Afande Mdudu ambae alikuwa akijificha ficha kana kwamba anatamani kuikimbia hilo eneo.
“Afande Mdudu unajua umefanya kosa gani leo?”Aliongea Hamza na Afande Mdudu alijikuta akitetemeka kwa hofu.
“Sikupaswa kukukamata .. naomba msamaha wako”Aliongea
“Kunikamata halikuwa kosa kwasababu ulikuwa ukifuata sheria na ulikuwa na ushahidi , mtu kushurutisha watu kutii sheria sio kosa hata kidogo”
“Basi kosa langu itakuwa ni kutokukuheshimu?”Aliongea huku aking’ata meno kwa hasira , mpaka dakika hio ameshindwa kujua kabisa Hamza ni mtu wa aina gani mbona anatisha.
“Mimi sio mtu wa kukasirika kwa vitu vidogo vidogo kama hivyo , hata mimi nisingekuongelesha kwa upole, kosa lako kubwa ni ni kujaribu kunitengenezea udhaifu mbele ya mwanamke huku ukiwa na uhakika mimi ni mhalifu, umeshindwa kunikamata nikiwa Kijichi na kuniwekewa mtego njiani, mpango wako haukuwa kunikamata ila kujaribu kunidhalilisha”Aliongea Hamza huku akionyesha hali ya ukauzu na swala lile lilimfanya Afande Himidu kuingiwa na wasiwasi.
“Ni mtoto wa pili wa mkuu wa majeshi Afande Mbwana, babu yake pia alishawahi kuwa Waziri mkuu”Aliongea.
“Nishayajua hayo yote tokea muda tu , lakini kuwa mtoto wa nani haimaanishi ndio tiketi ya kuachwa afanye atakavvo”
“Unapanga kumuua?” Aliuliza. Afande Himidu akiwa na wasiwasi na Afande Mdudu kwa woga alipiga magoti mbele ya Hamza.
“Hamza naomba unisamehe , nilikosea kweli”Aliongea lakini Hamza ni kama hakuwa hata na hio hasira ya kumuua kama alivyoulizwa , alitaka kumtishia kidogo tu.
“Nikikuua mtu kama wewe nitaonekana kama mtu ambae naonea dhaifu, onyo langu kwako usije kumsumbua Yonesi tena”Aliongea Hamza na mara baada ya Mdudu kusikia kauli hio alijikuta akipatwa na ahueni huku akijiambia kwa muda huo ataacha kumsumbua Yonesi lakinin sio kama atamwacha kabisa.
“Asante sana Hamza” Aliongea huku akijifuta , licha ya kwamba alikuwa mwanajeshi lakini ukweli ni kwamba alilelewa kimayai sana kutokana na utajiri wa familia yao hivyo kumfanya kuwa mjivuni sana.
Sababu ya Hamza pia kutomfanya kitu chochote Afande Mdudu ni kwa ajili ya Afande Himidu, alikuwa ni rafiki yake hivyo hakutaka kumuingiza kwenye matatizo.
“Mnaweza kutoka nje sasa , nataka kuongea na Hamza, hakuna anaeruhusiwa kusogelea hapa”Aliongea Afande Himidu mara baada ya hali kutulia.
Wote baada ya kutoka nje Afande Himidu ghafla tu alipiga goti kwa mguu mmoja huku akiongea kwa unyenyekevu
“My Prince!!”
“Inatosha Bro , kwanini unafanya hivi kama watu wengine bwana , hatujaonana kwa zaidi ya miaka sita lakini naona bado hujasahau hizi itifaki, nakumbuka kipindi kile ukiwa kambini ulikuwa mjeuri mno lakini baada ya kuimarika ukawa humble”Aliongea Hamza.
“Hakuna mtu yoyote ndani ya Tanzania hii naweza kumpigia magoti , hata awe raisi , kwangu hii ni ishara ya kukuheshimu kama mwalimu wangu na bosi wangu”Aliongea Afande Himidu huku akiwa na tabasamu.
“Haha. Vizuri , lakini naona sasa hivi unaitwa Himidu Mshauri , jina lako la Murphy Stopphilius umelitelekeza , huwa na kukubali sana maana hubadiliki sio kama rafiki yako Mameni”Aliongea Hamza.
Kitu ambacho hawakukijua wakina Afande Wazo na wenzake ni kwamba Murphy halikuwa jina la Hamza bali ni la Afande Himidu.
“Ukweli miaka miwili iliopita niliposikia umestaafu mwanzoni sikuwaza ni wapi utaenda , lakini nikikumbuka kipindi kile ulivyokuwa ukinisumbua kufahamu kiswahili nilijua tu lazima utakuwa hapa nchini na hisia zangu zilikuwa kweli , nimefurahi kukuona sana bosi”Aliongea.
“Mwaka wa kwanza wakati nafika hapa nchini nilikuwa nikijiuliza nikutafute au nipotezee , isitoshe kati ya marafiki zangu wote wewe ndio ulikuwa mtanzania pekee, lakini mara baada ya kupata taarifa umejipenyeza kwenye jeshi la Tanzania niliona nisikusumbue , isitoshe mpango wangu ulikuwa ni kuishi maisha ya chini chini”
“Bosi hata usiwe na wasiwasi naelewa..”Aliongea huku akimwangalia Hamza kwa namna ya kumchunguza..
“Lakini bosi kwanini naona kama umebadilika sana , mbinu uliotumia kupasua vioo haifanani kabisa na ile niliokuzoea nayo?”Aliongea na kauli ile ilimfanya Hamza kucheka.
“Ndio sijatumia kabisa mbinu ya nishati za mbingu na ardhi maana nishaachana nazo?”
“Kama ni hivyo umetumia mbinu gani sasa?”Aliuliza huku akiwa anashangaa , ukweli ni kwamba hakujua kabisa ni kitu gani kinaendelea kuhusu Hamza.
“Usiwaze sana nimeachana na mbinu zote zilizozoeleka sasa hivi nipo kwenye kitu kingine kabisa”
“Boss kila siku unaonyesha wewe sio mtu wa kawaida , yaani umepata mbinu mpya na umeweza kujifunza ndani ya muda mfupi tu na sasa unaonekana kama mtu mwingine , yaani unatufanya sisi binadamu wa kawaida tukose kabisa hata tumaini”
“Hehe.. unawaza nini sasa, kama tungefanana unadhani ningekuwa bosi wenu wewe mshenzi, huna haja ya kuwaza sana labda kama unataka kunipindua”
“Hamna bosi bado najichukulia nipo chini ya himaya yako mpaka sasa. halafu sio kama nina cheo kikubwa tokea nirudi kuliko kule”
“Huko nako ndio kujihusha , ndani ya miaka saba uliorudi nchini umeweza kuingia ndani ya kitengo cha Malibu na baadae kuwa mshauri wa vitengo vyote vya usalama na ulinzi na kupanda cheo mpaka kuwa jenerali , sio kazi ndogo kulingana na umri wako”
“Mafanikio yangu ni kama kichekesho nikijaribu kulinganisha na yako , isitoshe kwa kujilinganisha na wenzangu niliowaacha sidhani napaswa kusema nina mafanikio ya juu”
Hamza aliona alichoongea kinaleta maana , isitoshe kwa kipindi kirefu walichokuwa chini yake, alikuwa kama kikwazo kwa mafanikio yao , lakini wengi baada ya kuwaachia na kurudi kwenye mataifa yao waliweza kupata mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi.
Walijikuta wakiongea kwa muda mrefu kidogo mpaka muda ambao Afande Himidu alikumbuka swala la Ankh.
“Bosi vipi kuhusu hili swala la Ankh , kwannini watu wanakufualitia nalo sana au ulikuwa mtego wa Genesha?”
“Genesha aliiniingia kwenye majaribu ni kama ananiambia hata kama nimekufa huwezi kuishi kwa amani , unadhani ni nani kajua kuhusu hii siri kama sio yeye alieisambaza , mtu ananipa kitu halafu anawapa watu taarifa ili waanze kuniwinda , huyu alichotaka ni kuona sipati amani.
Hivi unajua ndio alinirudisha hapa Tanzania , baada ya kunitumia ujumbe wa kila aina kwamba anakaribia kufa na yupo hapa hivyo nionane nae kwa mara ya mwisho , lakini sikujua kama aliacha anuani kwenye maabara yake ili ijulikane nipo Tanzania.
“Nini! , kwahio unamaanisha Dokta Genesha alifia hapa nchini, maiti yake..”
“Nilimtupia baharini , aliniambia mwenyewe niifunge maiti yake na jiwe zito na kisha nimtupe”Aliongea Hamza huku akiwasha kwa mara nyingine sigara na kuvuta moshi kidogo.
“Kama ni hivyo bosi , vipi kuhusu hii Ankh , ni siri gani , maana kwa ninavojua kama nipo sahihi Ankh maana yake ni alama ya msalaba ambayo ilikuwa ikiwakilisha uhai ndani ya Misri ya kale , si ndio?”
“Upo sahihi Ankh ni ishara ambayo alitengeneza Nekhbet mungu wa Misri ya kale kama ishara ya zawadi ya uhai kwenda kwa Farao, sababu ya dokta Genesha kuipa siri hii Ankh ni kwasababu ni siri ambayo inahusianisha na uhai wa binadamu, ushawahi kusikia mtu yoyote anasema simulizi ya njiwa juu ya mti wa Uzima?”Aliongea Hamza.
“Nakumbuka nilishawahi kusoma hiki kitu kwenye Deep web , nilichukulia kama uzushi lakini walisema kuna Dokta kagundua siri juu ya kwanini binadamu anakufa mapema?”
“Unadhani nimeanza kukuelezea juu ya Nekhbet ili ulichukulie hili swala kama hadithi za kale?”Aliuliza Hamza.
“Kwahio Bro unasema Ankh ni kitu cha enzi ya Farao au unamaanisha nini?”
“Kama nilivyokwisha kusema Ankh kama Ankh ni ishara tu ambayo imetumika kuficha siri juu ya hatua za uhai wa binadamu ulivyo , chukulia ni kama maandiko ya enzi hizo yameonekana sasa hivi kwa ligha ngumu isioweza kutafsirika”
“Kwahio bosi kama ulichoshikilia ni kanuni , si inamaanisha umeshika siri ya dunia , sidhani ni makundi ya kihalifu tu ambayo yanaweza kupigania, hata nchi zitajiingiza katika vita za kupata hiki kitu”
“Enzi ya kale watu walikuwa tayari kusafiri kwa kuvuka bahari kwa ajili ya kutafuta namna ya kurefusha maisha lakini sasa hivi sio kutafuta bali sayansi imeendelea na wanasayansi wanakaa tu maabara kufanya tafiti za kutengeneza madawa , lakini mtu yoyote ukimwambia kama kuna uwezekano maisha yakarefushwa na dawa atakuona kichaa tu”Aliongea Hamza na kumfanya Himidu kutingisha kichwa kukubaliana nae.
“Kwahio bosi kama ulichoshikiria ni kanuni juu ya siri ya uhai wa binadamu , je imewezwa kufanyiwa utafiti?”
“Hapana , Genesha alijaribu kufanyia utafiti ili kuweza kuitafsiri lakini alishindwa , kulingana na maelezo yake ana uhakika kabisa ni kitu ambacho kinaweza kubadilisha mtazamo wa binadamu juu ya uhai , lakini kutokana na msongo wa mawazo juu ya mke wake yalimshida hivyo aliniachia kila kitu na kisha akajiua , nadhani unajua nisingeweza kumzuia kama alitaka kujiua mwenyewe”
Afande Himidu alijikuta akivuta pumzi ya ahueni ,ukweli kulingana na mtazamo wake anaomba isiwe kweli , aliona kama kweli binadamu atajua namna ya kurefusha maisha , basi atakuwa kiumbe hatari zaidi kuliko hata siraha za nyuklia.
“Mimi kwangu naona hizi ni kama stori tu na uwezekano huo haupo?”Aliongea Himidu.
Hamza licha ya kuamua kumwambia ila hakutaka kumpa ukweli wote , isitoshe kuna misheni ilikuwa ikiendelea kuhusu yeye chini chini
“Ukweli ni kwamba Ankh ni ni nadharia ambayo wanasayansi wanayo tayari”Aliongea Hamza.
“Kivipi?”
“Kwanza unajua namna mwili unavyofanya kazi , mfano tu chukulia seli ambazo zinazunguka utumbo zinajigawa kila baada ya siku tatu mpaka tano na kuweka nyingine , sio hivyo tu kila baada ya miezi miwili seli za kibofu cha mkojo zinajiondoa na kuwa zingine , seli za damu zenyewe zinabadilika kila baada ya miezi minne , maana yake ni kwamba asilimia tisini na nane ya seli zote zilizopo ndani ya mwili wetu zinaondolewa na hewa na chakula kwa mwaka , kwa ligha nyepesi ni kwamba kila mwaka mmoja ukipita mwili wako umebadilika vitu vingi sana, sasa kadri mwili unavyoendelea kwa kasi kuzalisha seli mpya na kuhamisha zile zilizokufa huo mchakato unazuia mwili kuzeeka , , hivyo kama mchakato huu ni endelevu bila kupungua nyakati zote basi binadamu asingekufa mapema, ukichana na swala la kuugua na kupata ajali”
“Kama ni hivyo sasa kwanini sisi binadamu bado tunaendelea kuzeeka?”Aliuliza Afande.
“Kwasababu inafikia hatua ule mchakato wa seli kugawanyika ndani ya mwili na kutengeneza mpya hupungua kabisa , huu mchakato wote unadhibitiwa na DNA, Chukulia urefu wa uhai wako ni kama kamba ya kiatu, kadri unayotoka mwanzo wa kamba kueleleka mwisho wa kamba ndio namna unavyopunguza siku za uhai wako kutokana na seli za mwili kutojigawa na kutengeneza mpya , ukifika mwishoni mwa kamba unakutana na kile kichopoo ambacho kimeifunga kamba kuonyesha ndio mwisho, sasa pale ndio mwisho wa seli za mwili kujitengeneza upya , ukizungumzia kisayansi sasa DNA ina muundo kama wa kamba kwani mwishoni mwa urefu wake kumefungwa kitu kama kichopoo ambacho kisayansi kinaitwa Telomere.
Sasa chukulia kitendo cha kutaka kuongeza urefu wa kamba ndio kuongeza urefu wa maisha ya binadamu , utakachofanya ni kuondoa kile Kichopoo na kutafuta kamba inayofanana kwa asilimia mia moja na ulokuwa nayo kisha kutafuta namna ya kuunganisha ile kamba bila kubadili muundo wake na mwisho wa siku utafanikiwa kuiongezea urefu, ukichukulia huo mfano katika muundo wa DNA utakuwa umeongeza urefu wa maisha yako, hiki ndio kitu ambacho Genesha anaamini kipo katika siri ya Ankh”Aliongea Hamza.
Ijapokuwa hakuwa mwanabailojia lakini kwa kiasi kidogo alihisi kuelewa alichokuwa akitaka kumaanisha juu ya itu kinachoitwa Ankh.
“Inaonekana nadharia yake inaleta maana kwa kiasi flani , lakini kwasababu haikukamilika na kanunni imeshindikana kutafsirika kutokana na lugha yake si inamaanisha ni kitu ambacho hakitowezekana, kwanini akaamua kukupatia wewe hii siri ya Ankh?”
“Kwasababu anaamini kazi kubwa amekwisha ifanya , kwa maelezo yake anaamini kuna elementi moja ambayo haijagundulika bado na inaweza isigundulike kama tu kutakosekana tafsiri ya Kanuni ya Ankh , elementi hii ameitaja kama Elementi ya Nuru na kama ikipatikana basi kila kitu kitabadilika”
“Kwahio bosi Dokta Genesha anaamini fumbo la hii elementi litapatikana katika tafsiri ya kanuni hio ya Ankh?”
“Uwezekano huo upo ila sina uhakika , kuna uwezekano hii elementi isiwepo kabisa hapa duniani au hata angani katika sayari nyingine”
Ilikuwa ni siri nzito sana juu ya Ankh aliopata kuisikia Afande Himidu ,ijapokuwa aliona Hamza hakuwa ameielezea vizuri kueleweka lakini aliona pengine kuna sababu ya Dokta Genesha kumpatia Hamza, hata hivyo alijiuliza kwanini maana Hamza sio mwanasayansi.
“Bosi hiki kitu ni kama kiazi cha moto ni kheri ubakie nacho tu , sitouliza tena kuhusu hili , kuna kila sabababu ya Dokta Ganesha kutotaka tafiti zake zipotee , lakini hata hivyo swala hili likijulikana kwa watu wachache ni bora zaidi”
“Ndio maana nilitaka kuongea na wewe , ili uweze kutuliza shauku wanayoanza kuipata wanajeshi wenzio , siku zote watu wakinifuata niliishia kuwaambia simulizi ya njiwa juu ya mti wa uzima ni uzushi tu, nafanya hayo kwasababu nataka watu wasahau, vyovyote vile hata kama ikitokea kanuni yote nimeijua nitaenda nayo kaburini , sioni kama kuna faida ya binadamu kuishi muda mrefu, hivyo hakikisha uchunguzi wowote unaendelea kuhusu mimi uachwe mara moja , sio salama watu wengi kuanza kuulizia kuhusu Ankh , wakikusumbua wewe waonyeshee dole”Aliongea Hamza na kufanya Afande Himidu kucheka.
“Bosi usiwe na wasiwasi , hii ni siri yagu na wewe kwanzia sasa , hata taarifa azitake Mfalme Nyoka”
“Haha.. halafu huyu Mfalme Nyoka sijamuona kwa muda mrefu , unadhani atakuwa amenipita ki uwezo kwasasa?”
“Kama ni kipindi cha mwanzo ningeweza kusema unamuweza , lakini sasa hivi naona umeua nguvu zako zote za nishati , hivyo ni ngumu kutabiri chochote”
******
Waliongea mambo mengi mno mpaka juu ya Hamza kuoa, na Afande Himidu alitaka kujua imekuwaje kuwaje Hamza akaoa lakini Hamza alimwambia ni stori ndefu.
Alimwambia kama ni stori ndefu basi amtambulishe kwa shemeji, Hamza aliona sio mbaya kumtambulisha kwa Regina , hivyo alimwambia wakitoka hapo watafute sehemu kwa ajili ya chakula cha usiku na ampigie simu Regina kufika.
Afande Himidu alitoa maagizo kwa makamanda waachane na uchunguzi wote unaohusiana na Hamza kwanzia dakika hio na wiki inayofuatia atafika makao makuu kutoa maelekezo zaidi.
Kwasababu maneno yake ni sheria wote walikubali na kisha waliondoka huku bado wakiwa na maswali mengi , kati yao ambae hakuwa ameridhika kwa kiasi kikubwa alikuwa ni Afande Mdudu.
Baada ya Hamza kuingia kwenye V8 ya Afande Himidu ili kutafuta sehemu kwa ajili ya kupata chakua cha usiku , Hamza alitumia nafasi hio kumtafuta Regina na kumuuliza kama yupo free wakapate Dinner lakini Regina alisema yuko bize na kazi hivyo Hamza hakujishughulisha nae zaidi.
Japo Himidu alitaka kujua Hamza kashikika kwa nani lakini mara baada ya Hamza kumwambia haiwezekani kwa siku hio kukutana na shemaji yake aliamua kuridhika . Hamza hakumwambia kama ni Regina mmiliki wa makampuni ya Dosam , alitaka kuweka cheo chake pembeni na kutambulisha Regina kama Regina.
Hamza kwasababu alikataliwa na Regina kutoka wote Dinner aliona haina haja ya kwenda mjini kwa ajili ya chakula bali walichukua barabara ya kuelekea Kijichi kwa Dina.
Himidu alishangaa kuona Hamza alikuwa na mahusiano na Dina , alikuwa akimjua sana Dina kutokana na faili nyeti la mtandao wa Chatu alikuwa amekwisha kulisoma.
Kwa Hamza ilikuwa kama sherehe ya kukutana na rafiki yake na kwasababu ilikuwa wikiend walijiachia mgahawani kwa Dina na baadae wakabadilisha kijiwe na kwenda mjini zaidi.
Himidu aliamua kutumia pesa zake kuhakikisha Hamza anayafurahia maisha na Hamza hakuona shida.
Hamza upande wake hakusahau kumpigia simu Prisila na kumpa taarufa alishatoka , taarifa ambayo ilikuwa nuri kwa Prisila.
Hamza hakufanikiwa kurudi nyumbani kabisa siku hio na kuishia kulala nyumbani kwa Dina mpaka asubuhi na kulivyokucha aliendelea kukaa mpaka muda wa jioni ndio alivyoanza safari ya kurudi nyumbani.
Ilikuwa muda wa saa kumi na moja kama na nusu hivi ya jumapili ndio aliingia nyumbani na kitendo cha kuingia getini aliweza kuona gari ambayo sio ya Regina ikiwa katika maegesho ya muda mfupi.
Hamza palepale kwa kuichunguza tu hio gari aliikumbuka vizuri.
“Hii gari si ni ya Yulia hii, anafanya nini hapa nyumbani”Aliwaza Hamza huku hisia zikimwambia huyo mwanamke kamfuata mpaka hapo zikimvaa.
Unadhani Yulia kaenda nyumbani kwa Hamza kufanyaje ?
ITAENDELEA-Alhamisi
nicheki watsapp kupata mwendelezo namba ni 0687151346